Ahadi ya Ulimwengu Usio na Ufisadi
UFISADI umepenya ndani ya kila tabaka la jamii. Iwe ni katika serikali, sayansi, michezo, dini, au biashara, ufisadi unaonekana kama hauwezi kudhibitiwa.
Ulimwenguni kote, habari zenye kushusha moyo za kashfa za ufisadi hutangazwa katika vyombo vya habari. Wengi waliokubali kutumikia masilahi ya watu hufichuliwa kuwa wenye kutumikia masilahi yao wenyewe kwa kupokea hongo na viinuamgongo. Ule uitwao uhalifu usio wa mabavu umeongezeka. Idadi inayoongezeka ya watu mashuhuri kijamii au kiuchumi wana hatia mbaya ya kiadili katika kazi zao za kawaida.
Kuna hangaiko linaloongezeka juu ya kile ambacho gazeti la Ulaya lakifafanua kuwa “‘ufisadi mkubwa sana’—zoea la maafisa wa ngazi za juu, mawaziri na mara nyingi sana wakuu wa serikali kutaka hongo na viinuamgongo kabla ya kutia sahihi kibali cha ununuzi mkubwa wa vitu na miradi.” Katika nchi moja “miaka miwili ya uchunguzi wa polisi na kushikwa [kwa watu] karibu kila siku bado hakujazuia wafisadi wenye kupotoka,” lasema gazeti la Uingereza The Economist.
Kwa sababu ya ufisadi wenye kuenea hivyo, wengi leo huhisi kwamba hakuna mtu wawezaye kutumaini. Wao husema maneno ya mwandikaji wa Biblia Daudi aliposema: “Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja [“wote vilevile ni wenye ufisadi,” New World Translation], hakuna atendaye mema, la! hata mmoja.”—Zaburi 14:3.
Wewe hukabilije uhalisi wa ufisadi wenye kuenea? Watu wengi zaidi leo huupuuza. Lakini hata ukiupuuza ufisadi, bado utakuumiza. Jinsi gani?
Ufisadi Hukuathiri Wewe
Ufisadi wa hali ya juu na vilevile wa hali ya chini huongeza gharama ya maisha, hupunguza thamani ya vitu, na hutokeza upungufu wa kazi na mishahara ya chini. Kwa kielelezo, inakadiriwa kwamba uhalifu kama vile wizi wa fedha za amana na udanganyifu unagharimu karibu mara kumi zaidi ya jumla ya hasara ya uporaji, unyang’anyi, na wizi. The New Encyclopædia Britannica (1992) husema kwamba “hasara ya uhalifu wa makampuni makubwa katika Marekani imekadiriwa kuwa dola 200,000,000,000 kila mwaka—ikishinda kwa mara tatu hasara ya uhalifu wa vikundi vya magenge.” Kitabu hiki kinaeleza kwamba matokeo yajapokosa kugunduliwa mara moja, “uhalifu kama huo unatisha sana usalama wa wafanyakazi, wanunuzi, na mazingira.”
Matokeo yenye kusikitisha ya ufisadi hutukumbusha juu ya maneno ya Mfalme Sulemani: “Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.”—Mhubiri 4:1.
Basi, je, sasa tuachilie tu ufisadi? Je, hauepukiki? Je, ulimwengu usio na ufisadi hauwezekani kuwapo? Kwa furaha, jibu ni la! Biblia yatufundisha kwamba karibuni ukosefu wa haki na uvunjaji wa sheria vitaondolewa.
Yale Biblia Hutuambia
Biblia hutuambia kwamba ufisadi ulianza wakati malaika mwenye nguvu nyingi alipoasi dhidi ya Mungu na kuwashawishi wenzi wa ndoa wa kwanza wa kibinadamu wamuunge mkono. (Mwanzo 3:1-6) Hakuna kitu kizuri kilicholetwa na mwendo wao wa dhambi. Badala ya hilo, tangu siku ile Adamu na Hawa walifanya dhambi dhidi ya Yehova Mungu, walianza kuumizwa na matokeo mabaya ya ufisadi. Miili yao ikaanza hatua ya polepole ya kudhoofika, ikiongoza kwenye kifo kisichoepukika. (Mwanzo 3:16-19) Tangu hapo, historia imejaa vielelezo vya hongo, hila na udanganyifu. Hata hivyo, wengi wanaotenda hayo huonekana wakiyafanya bila kuadhibiwa.
Tofauti na wahalifu wa kawaida, wakurugenzi na wanasiasa wafisadi mara chache sana hufungwa gerezani au kurudisha vitu walivyopata kwa njia isiyo halali. Kwa sababu ya hongo, viinuamgongo, na malipo yasiyo halali ambayo hufanywa kisiri, mara nyingi ni vigumu kufunua ufisadi wa hali ya juu. Lakini hili halimaanishi kwamba ulimwengu usio na ufisadi hauwezekani kuwapo.
Ukombozi kutokana na ufisadi utakuja kutoka kwa Muumba wa mwanadamu, Yehova Mungu. Kuingilia mambo kimungu ndilo suluhisho pekee. Kwa nini? Kwa sababu adui wa binadamu asiyeonekana, Shetani Ibilisi, anaendelea kupotosha wanadamu. Kama tusomavyo kwenye 1 Yohana 5:19, “dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.” Ni nini kingine kingeweza kueleza kuongezeka kwa ufisadi—wingi wao bila adhabu?
Hakuna jitihada yoyote ya kibinadamu iwezayo kushinda Shetani na mashetani wake. Ni kuingilia mambo kimungu pekee kunakoweza kuhakikishia wanadamu wenye utii “uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.” (Warumi 8:21) Yehova anaahidi kwamba karibuni Shetani atazuiwa ili asiweze kudanganya wanadamu tena. (Ufunuo 20:3) Tungojapo wakati huo, ikiwa tunatamani kuishi katika ulimwengu mpya wa Mungu usio na ufisadi, ni lazima sisi tukatae njia zilizopotoka za ulimwengu huu.
Watu Wanaweza Kubadilika
Katika siku za Yesu Kristo, kulikuwa na wale waliotumia uwezo wao vibaya na kuwadhulumu wanadamu wenzao. Kwa mfano, watoza-ushuru walikuwa na sifa mbaya ya matendo ya ufisadi. Jambo hili lilikuwa hivyo ijapokuwa sheria ya Mungu ilisema wazi hivi: “Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.” (Kutoka 23:8) Zakayo, aliyekuwa mtoza-kodi mkubwa, alikiri kwamba alikuwa akitoza pesa kwa mashtaka ya bandia. Lakini badala ya kuanzisha marekebisho ya kijamii kila mahali, Yesu alisihi mtu mmoja-mmoja kutubu na kuacha njia zao za ufisadi. Kama tokeo, watoza-ushuru wenye sifa mbaya kama vile Mathayo na Zakayo waliacha mtindo-maisha wao wa awali.—Mathayo 4:17; 9:9-13; Luka 19:1-10.
Wale wanaohusika katika mazoea yasiyo ya ufuatiaji haki leo wanaweza vilevile kukataa ufisadi kwa kuvaa “utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.” (Waefeso 4:24) Huenda isiwe rahisi kulipa kodi kwa kufuata haki au kuacha kushiriki katika mipango yenye kutilika shaka. Lakini, manufaa zipatikanazo zastahili jitihada zote.
Kwa sababu hawafuati tena ulimwengu huu wenye ufisadi, wale wanaojali hali njema ya wengine hufurahia amani ya ndani. Hawana woga wa kushikwa wakifanya mambo mabaya. Badala ya hilo, wao hufurahi kuwa na dhamiri safi. Wao huiga kielelezo cha Biblia cha nabii Danieli. Simulizi la Biblia lasema kwamba sikuzote wakuu wa serikali walikuwa wakitafuta udhuru dhidi ya Danieli. “Lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa [“ufisadi,” NW]; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia [“ufisadi,” NW] ndani yake.”—Danieli 6:4.
Ahadi ya Yehova
Yehova anaahidi kwamba “ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake; walakini haitakuwa heri kwa mwovu, wala hatazidisha siku zake, zilizo kama kivuli; kwa sababu hana kicho mbele za Mungu.”—Mhubiri 8:12, 13.
Ni faraja iliyoje wakati ufisadi hauleti tena hali ya kukosa furaha! Ni baraka iliyoje kuishi milele katika ulimwengu usio na ufisadi! Hili litawezekana. Biblia huzungumza juu ya “tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele.” (Tito 1:2) Ikiwa unachukia ufisadi na unapenda uadilifu, huenda utaona utimizo wa ahadi ya Mungu ya ulimwengu usio na ufisadi.
[Picha katika ukurasa wa4]
Ufisadi umejaa katika serikali na nyanja za biashara
[Picha katika ukurasa wa5]
Mara nyingi ufisadi huathiri shughuli na maofisa wa umma