Ehudi—Mwanamume wa Imani na Moyo Mkuu
MIAKA mingi ilikuwa imepita tangu Waisraeli waingie Bara Lililoahidiwa kwa mara ya kwanza. Musa na mwandamizi wake, Yoshua, walikuwa wamekufa zamani. Kwa sababu ya kutokuwapo kwa wanaume kama hao wa imani, uthamini kwa ibada safi ulipungua sana. Waisraeli walikuwa hata wameanza kutumikia Baali na nguzo takatifu.a Likiwa tokeo, Yehova aliwakabidhi watu wake mikononi mwa Wasiria kwa miaka minane. Ndipo Waisraeli walipomlilia Mungu ili wapate msaada. Kwa rehema, aliwasikiliza. Yehova aliinua mwamuzi, Othnieli, ili kuwakomboa watu Wake.—Waamuzi 3:7-11.
Matukio hayo yalipasa kuwafundisha Waisraeli kweli ya msingi kwamba—utii kwa Yehova huleta baraka, hali kutokutii hutokeza laana. (Kumbukumbu la Torati 11:26-28) Hata hivyo, watu wa Israeli walishindwa kujifunza somo hilo. Baada ya kipindi cha miaka 40 cha amani, waliacha tena ibada safi.—Waamuzi 3:12.
Washindwa na Wamoabi
Wakati huo Yehova aliwaacha watu wake watumbukie mikononi mwa Mfalme Egloni wa Moabu. Biblia yamfafanua kuwa “mtu aliyewanda sana.” Kwa msaada wa Ammoni na Ameleki, Egloni alishambulia Israeli na kusimamisha jumba lake la mfalme katika Yeriko, “mji wa mitende.” Jinsi ilivyokuwa kinyume kwamba jiji la kwanza la Wakanaani lililoshindwa na Waisraeli sasa lilikuwa makao makuu ya mmoja aliyeabudu mungu asiye wa kweli Kemoshi!b—Waamuzi 3:12, 13, 17.
Egloni aliwaonea Waisraeli kwa miaka 18 iliyofuata, pasipo shaka akidai kwao ushuru wenye kulemeza. Kwa kutoza ushuru kila baada ya muda fulani, Moabu iliimarisha hali yayo ya kiuchumi, huku ikikumba mali za Israeli. Kwa kueleweka, watu wa Mungu walimlilia ili wapate kitulizo, na kwa mara nyingine tena Yehova akasikiliza. Aliwainulia mwokozi mwingine—wakati huo alikuwa Mbenyamini aliyeitwa Ehudi. Ili kumaliza uonevu wa Egloni juu ya Israeli, Ehudi alipanga kuchukua hatua siku ya ulipaji wa ushuru uliofuata.—Waamuzi 3:14, 15.
Ili kujitayarisha kwa ajili ya tendo lake lenye moyo mkuu, Ehudi alitengeneza upanga wenye makali kuwili wenye urefu wa dhiraa moja. Ikiwa hiyo ilikuwa ni dhiraa fupi, silaha hiyo ilikuwa kama sentimeta 38. Wengine wangeufikiria kuwa jisu. Kwa wazi hakukuwa na kijiti kilichokingamana katikati ya upanga na mpini. Kwa hiyo, Ehudi aliweza kuficha upanga wake mdogo katika makunjo ya vazi lake. Zaidi ya hayo, kwa kuwa Ehudi alikuwa mwenye kutumia mkono wa kushoto, aliweza kuufunga upanga wake upande wake wa kulia—si mahali pa kawaida pa silaha.—Waamuzi 3:15, 16.
Mkakati wa Ehudi ulikuwa wenye hatari. Kwa kielezo, namna gani ikiwa mahadimu wa mfalme walimpekua Ehudi wakitafuta silaha? Hata ikiwa hawakufanya hivyo, kwa hakika hawangemwacha mfalme wao peke yake pamoja na Mwisraeli! Lakini ikiwa wangefanya hivyo na Egloni hangeweza kuuawa, Ehudi angeponyokaje? Angeweza kukimbia umbali gani kabla ya mahadimu wa Egloni kugundua yaliyokuwa yametendeka?
Bila shaka Ehudi alifikiria kwa uzito habari hizo zote, labda akiwazia matokeo kadhaa yenye msiba. Hata hivyo, aliendelea na mpango wake, akionyesha moyo mkuu na kudhihirisha imani katika Yehova.
Ehudi Akutana na Egloni
Siku ya kutoa ushuru uliofuata ilifika. Ehudi na wanaume wake waliingia jumba la mfalme. Kabla ya muda mrefu, walikuwa wakisimama mbele ya Mfalme Egloni mwenyewe. Lakini wakati ulikuwa haujafika bado kwa Ehudi kushambulia. Baada ya utoaji wa ushuru, Ehudi aliwaagiza hao wachukuaji wa ushuru kwenda zao.—Waamuzi 3:17, 18.
Kwa nini Ehudi alikawia kumshambulia Egloni? Je, alishindwa na hofu? La hasha! Ili kutekeleza mpango wake, Ehudi alihitaji asikizwe faraghani na mfalme—jambo ambalo hakukubaliwa mara hiyo ya kwanza walipokutana. Zaidi ya hilo, Ehudi angehitaji kutoroka upesi. Kuponyoka kungekuwa rahisi zaidi kwa mtu mmoja kuliko kwa msafara wote wa wachukuaji wa ushuru. Kwa hiyo, Ehudi alingojea wakati ufaao. Hiyo ziara fupi pamoja na Egloni ilimsaidia kujua namna hilo jumba la mfalme lilivyokuwa limejengwa na kupata kujua mfalme alikuwa na usalama wa kadiri gani.
Baada ya kufika “kwenye sanamu zilizokuwa karibu na Gilgali,” Ehudi aliwaacha wanaume wake na kusafiri kurudi kwenye jumba la mfalme la Egloni. Huko kutembea kwa karibu kilometa mbili kulimpa Ehudi wakati kidogo wa kufikiria utume wake na kusali kupata baraka za Yehova.—Waamuzi 3:19.
Ehudi Arudi
Yaonekana Ehudi alikaribishwa tena ndani ya jumba la mfalme. Labda kile kiasi kikubwa cha ushuru alichotoa mapema kilimweka Egloni katika hali ya akili yenye kupendeza. Yawezekana kwamba ijapokuwa ziara ya kwanza ilikuwa fupi, ilimpatia Ehudi fursa ya kutosha ya kuweka imara uhusiano wenye upatano pamoja na mfalme. Hata hivyo, Ehudi alikuwa amerudi mbele ya Egloni.
“Mimi nina ujumbe wa siri kwako wewe, Ee mfalme,” Ehudi akasema. Uhakika wa kwamba alikuwa amefikia hatua hiyo, ulikuwa ni wonyesho wa kwamba Yehova alikuwa akimwongoza. Hata hivyo, kulikuwa na tatizo. Huo “ujumbe wa siri” aliokuwa nao Ehudi haungeweza kusemwa mbele ya mahadimu wa mfalme. Ikiwa Yehova alitarajiwa kuingilia mambo, Ehudi alihitaji msaada huo mara moja. “Nyamazeni kimya,” mfalme akaamuru. Kwa kuwa Egloni hakutaka yeyote atukie kusikia ‘ujumbe huo wa siri,’ aliwafukuza mahadimu wake. Ebu wazia kitulizo alichopata Ehudi!—Waamuzi 3:19.
Egloni alikuwa ameketi katika chumba chake cha paa wakati Ehudi alipomwendea na kusema hivi: “Mimi nina ujumbe utokao kwa Mungu kwako wewe.” Kwa kutaja neno “Mungu,” je, Ehudi alikuwa akimrejezea Kemoshi? Huenda Egloni alifikiria hivyo. Kwa sababu ya kupendezwa, Egloni aliinuka toka kiti chake cha ufalme na kusimama akiwa mwenye matarajio. Ehudi alimkaribia, yamkini akijongea kwa uangalifu ili mfalme asishuku kuwa yu ashambuliwa. Ndipo, kwa mwendo wa haraka, ‘Ehudi aliunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake [Egloni]; hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma.’—Waamuzi 3:20-22.
Wakiwa wanakaa karibu na hapo, mahadimu wa mfalme hawakushtuka. Lakini Ehudi alikuwa bado hatarini. Katika wakati wowote watumishi wa Egloni wangeweza kuingia kwa haraka na kugundua maiti ya mfalme wao aliyeanguka. Ehudi alihitaji kuondoka hapo haraka! Baada ya kufunga milango kwa kufuli, aliponyoka kupitia tundu la hewa la hicho chumba cha paa.—Waamuzi 3:23, 24a.
Ugunduzi na Ushinde
Upesi watumishi wa Egloni walikuwa na udadisi. Hata hivyo, hawakuthubutu kumwudhi mfalme kwa kukatiza mkutano wake wa faragha. Ndipo walipong’amua kwamba milango ya hicho chumba cha paa ilikuwa imefungwa kufuli. “Hapana budi amejifunika miguu yake ndani ya chumba cha baridi,” wao wakasababu. Hata hivyo, kadiri muda ulivyopita, hangaiko jingi lilichukua mahali pa udadisi tu. Mahadimu wa Egloni hawakuweza kungoja zaidi. “Basi wakatwaa ufunguo, na kuifungua [milango ya chumba cha paa]; na tazama, bwana wao alikuwa ameanguka nchi, naye amekufa!”—Waamuzi 3:24b, 25.
Wakati uleule, Ehudi alikuwa ameponyoka. Alipita sanamu katika Gilgali na hatimaye akafika Seira, mahali katika mkoa wenye milima wa Efraimu. Ehudi aliwakusanya wanaume wa Israeli pamoja, akawaongoza katika shambulizi lenye muungano juu ya Wamoabi. Hilo simulizi lasimulia kwamba ‘walipiga katika Wamoabi watu waume wapata kama elfu kumi, ambao wote walikuwa wanene, na wote mashujaa; hakupona hata mtu mmoja.’ Moabu ikiwa imetiishwa, nchi ya Israeli ilikuwa bila vurugu zaidi kwa miaka 80.—Waamuzi 3:26-30.
Kujifunza Kutokana na Kielelezo cha Ehudi
Imani katika Mungu ilimchochea Ehudi. Waebrania sura ya 11 haimtaji hususani kuwa mmoja wa wale “ambao kupitia imani walishinda falme katika pambano, . . . wakawa mashujaa katika vita, wakatimsha majeshi ya watoka-ugenini.” (Waebrania 11:33, 34) Hata hivyo, Yehova alimtegemeza Ehudi kwa kuwa alitenda kwa imani, akaokoa Israeli kutoka kwa mamlaka yenye uonevu ya Mfalme Egloni.
Moyo mkuu ulikuwa mojawapo ya sifa za Ehudi. Alihitaji kuwa na moyo mkuu ili kutumia upanga halisi kwa matokeo. Tukiwa watumishi wa Mungu wa siku hizi, hatuchukui upanga kama huo. (Isaya 2:4; Mathayo 26:52) Hata hivyo, sisi hutumia “upanga wa roho,” Neno la Mungu. (Waefeso 6:17) Ehudi alikuwa hodari katika kutumia silaha yake. Sisi pia twahitaji kuwa stadi katika kutumia Neno la Mungu tuhubiripo habari njema ya Ufalme. (Mathayo 24:14) Funzo la kibinafsi la Biblia, kuwapo kwa ukawaida kwenye mikutano ya Kikristo, kushiriki kwa bidii katika huduma, na kumtegemea kwa sala Baba yetu wa kimbingu kutatusaidia kuiga sifa zilizoonyeshwa na Ehudi, mtu wa imani na moyo mkuu kwa kweli.
[Maelezo ya Chini]
a Nguzo takatifu yamkini zilikuwa mifano ya uume. Zilishirikishwa na karamu za ngono zenye ukosefu mzito wa adili.—1 Wafalme 14:22-24.
b Kemoshi alikuwa mungu mkuu wa Wamoabi. (Hesabu 21:29; Yeremia 48:46) Katika angalau visa kadhaa, huenda watoto walitolewa wakiwa dhabihu kwa mungu huyo asiye wa kweli mwenye kuchukiza sana.—2 Wafalme 3:26, 27.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Ehudi na wanaume wake walimtolea Mfalme Egloni ushuru
[Hisani]
Imetokezwa tena kutokana na Illustrirte Pracht - Bibel/Heilige Schrift des Alten und Neuen Testaments, nach der deutschen Uebersetzung D. Martin Luther’s