Wengi Hudai Kuwa na Imani
“YESU ni mwema! Yeye ni wa kustaajabisha sana!” akasema kwa mkazo mwanamke mmoja wa kidini huko Brazili. Kwa kweli, hakuna shaka kwamba jina la Yesu ni lenye nguvu. Katika historia yote, watu wamekuwa tayari kuteseka na kufa kwa ajili yake.
Mtume Petro na Yohana walihubiri “juu ya msingi wa jina la Yesu” katika Yerusalemu. Kwa kufanya hivyo, walikamatwa na kuchapwa viboko. Hata hivyo, “[wali]shika njia yao kwenda kutoka mbele ya Sanhedrini, wakishangilia kwa sababu walikuwa wamehesabiwa wenye kustahili kuvunjiwa heshima kwa ajili ya jina lake.”—Matendo 5:28, 41.
Mkristo mwingine wa karne ya kwanza aliyestahi jina la Yesu alikuwa Antipasi. Katika kitabu cha mwisho cha Biblia cha Ufunuo, Yesu alimrejezea kuwa “shahidi wangu, aliye mwaminifu, aliyeuawa kando yenu, mahali anapokaa Shetani.” (Ufunuo 2:13) Pamoja na Wakristo wengine wa Pergamamu, Antipasi alikataa kukana imani katika Kristo. Antipasi alidumisha imani thabiti katika jina la Yesu hata ilipomgharimu uhai wake mwenyewe!
Katika 155 W.K., nusu karne hivi baadaye, mtu aitwaye Polycarp aliyekiri kuwa Mkristo alikabili jaribu sawa na hilo alipoamriwa amtukane Kristo. Itikio lake lilikuwa: “Nimemtumikia kwa miaka 86, Yeye hakunikosea. Ninawezaje kukufuru Mfalme wangu ambaye ameniokoa?” Kwa sababu ya kukataa kumkana Kristo, Polycarp alichomwa kwenye mti.
Mitume, Antipasi, na wengineo walikuwa tayari kuimarisha ushahidi wao kuhusu Kristo kwa kifo! Vipi watu leo?
Jina la Yesu Leo
Jina la Yesu laendelea kuchochea hisia-moyo zenye nguvu. Katika Amerika ya Latini, kiwango cha ongezeko la makanisa ambayo hudai kumwamini Yesu kimefikia kilele katika miongo ya hivi majuzi. Hata vijiji vidogo zaidi vina kanisa la Pentekoste. Wakati huohuo, uvutano wa kisiasa wa makanisa hayo unaongezeka. Kwa kielelezo, katika Bunge na Baraza Kuu la Brazili, viti 31 vimeshikiliwa na washiriki wa makanisa hayo.
Yesu pia ndiye kiini cha harakati mpya ya kidini huko Marekani. Wafuasi wa hiyo harakati hujiita Promise Keepers (Watimiza Ahadi). Gazeti la Time liliripoti katika mwaka wa 1997 kwamba hudhurio kwenye mikutano yao liliongezeka kutoka watu 4,200 mwaka wa 1991 hadi watu milioni 1.1 mwaka wa 1996. Mmoja wa nyimbo zake huimbwa hivi: “Ee ushindi katika Yesu, Mwokozi wangu milele.”
Hata hivyo, si hisia zote ambazo zimechochewa na jina la Yesu zimekuwa nzuri. Mara nyingi vita vimepiganwa katika jina la Yesu. Wayahudi wameuawa, wapagani wakachinjwa, wabishi wakateswa, wakakatwakatwa, na kuchomwa kwenye mti—yote hayo yakifanywa katika jina la Yesu. Na hivi karibuni zaidi, kueneza evanjeli ili kujinufaisha kifedha kumekuwa jambo lenye kuleta sifa mbaya. Hayo yote ni matumizi yaliyopotoka na yenye kuchukiza ya jina la Yesu, na kile kimaanishwacho na jina hilo!
Isitoshe, mambo hayo huzusha maswali ya maana: Ni nini kinachohitajiwa katika kuweka imani katika jina la Yesu? Mashahidi wa Yehova wana maoni gani kuhusu habari hiyo? Makala inayofuata itajibu maswali hayo.