Abrahamu—Kielelezo cha Imani
“[Abrahamu alikuwa] baba ya wote wale walio na imani.”—WAROMA 4:11.
1, 2. (a) Wakristo wa kweli leo wanamkumbuka Abrahamu kwa sababu ya mambo gani? (b) Kwa nini Abrahamu anaitwa “baba ya wote wale walio na imani”?
ALIKUWA babu wa taifa lenye nguvu, nabii, mfanyabiashara, na kiongozi. Hata hivyo, leo yeye anakumbukwa sana miongoni mwa Wakristo kwa sababu ya sifa iliyofanya Yehova Mungu amwone kuwa rafiki—imani yake thabiti. (Isaya 41:8; Yakobo 2:23) Jina lake ni Abrahamu, nayo Biblia humwita “baba ya wote wale walio na imani.”—Waroma 4:11.
2 Je, wanaume walioishi kabla ya Abrahamu kama vile Abeli, Enoki, na Noa, hawakuonyesha imani? Ndiyo, lakini agano la kubariki mataifa yote ya dunia lilifanywa pamoja na Abrahamu. (Mwanzo 22:18) Hivyo akawa baba kwa njia ya mfano kwa wote ambao hudhihirisha imani katika Mbegu aliyeahidiwa. (Wagalatia 3:8, 9) Kwa kadiri fulani, Abrahamu anaweza kuonwa kuwa baba yetu, kwa kuwa imani yake ni kielelezo cha kuigwa. Maisha yake yote yanaweza kuonwa kuwa udhihirisho wa imani, kwa kuwa yalikuwa na majaribu mengi sana. Naam, muda mrefu kabla ya Abrahamu kukabili lile linaloweza kuitwa jaribu kubwa zaidi la imani yake—amri ya kumtoa dhabihu mwana wake Isaka—Abrahamu alidhihirisha imani yake katika majaribu mengi madogo-madogo. (Mwanzo 22:1,2) Acheni sasa tuchunguze baadhi ya majaribu haya ya imani yaliyotokea mapema na kuona tunaweza kujifunza nini kutokana nayo.
Amri ya Kuondoka Uru
3. Biblia inatuambia nini kuhusu malezi ya Abramu?
3 Biblia inamtaja Abramu (ambaye baadaye aliitwa Abrahamu) kwa mara ya kwanza kwenye andiko la Mwanzo 11:26, ambalo lasema: “Tera akaishi miaka sabini, akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani.” Abramu alikuwa mzawa wa Shemu aliyemcha Mungu. (Mwanzo 11:10-24) Kulingana na Mwanzo 11:31, Abramu aliishi na familia yake katika mji wenye ufanisi wa “Uru wa Wakaldayo,” ambao wakati mmoja ulikuwa mashariki ya Mto Eufrati.a Hivyo, hakukua akiwa mhamaji mwenye kuishi mahemani bali alikuwa mkazi wa mji wenye anasa nyingi. Bidhaa kutoka nchi za nje zingeweza kununuliwa kwenye masoko ya Uru. Mitaa ya Uru ilikuwa na nyumba kubwa zilizopakwa chokaa ambazo zilikuwa na maji ya mfereji.
4. (a) Ni magumu gani ambayo waabudu wa Mungu wa kweli walipata huko Uru? (b) Abramu alikuja kudhihirishaje imani katika Yehova?
4 Mbali na manufaa za kimwili, maisha katika mji wa Uru yalifanya hali iwe ngumu sana kwa mtu yeyote aliyetaka kumtumikia Mungu wa kweli. Mji huo ulikolea ibada ya sanamu na ushirikina. Naam, jengo lililokuwa kubwa zaidi mjini humo ni hekalu refu lililomtukuza mungu-mwezi aitwaye Nanna. Yaelekea Abramu alishinikizwa sana, hata na watu fulani wa jamaa yake ashiriki ibada hiyo iliyopotoka. Kulingana na mapokeo fulani ya Wayahudi, Tera babake Abramu alikuwa mtengeneza sanamu. (Yoshua 24:2, 14, 15) Kwa vyovyote vile, Abramu hakushiriki ibada isiyo ya kweli na iliyopotoka. Babu yake Shemu aliyekuwa mzee alikuwa bado hai na yaelekea alimwambia Abramu kuhusu Mungu wa kweli. Kwa sababu hiyo, Abramu alidhihirisha imani katika Yehova badala ya Nanna!—Wagalatia 3:6.
Imani Yajaribiwa
5. Mungu alimpa Abramu amri na ahadi gani alipokuwa Uru?
5 Imani ya Abramu ingejaribiwa. Mungu alimtokea na kumwamuru hivi: “Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”—Mwanzo 12:1-3; Matendo 7:2, 3.
6. Kwa nini Abramu alihitaji kuwa na imani ya kweli ili kuondoka Uru?
6 Abramu alikuwa mzee na hakuwa na mtoto. Angewezaje kufanywa “kuwa taifa kubwa”? Nayo nchi aliyoamriwa aende ilikuwa wapi? Mungu hakumwambia. Kwa hiyo Abramu alihitaji kuwa na imani ya kweli ili kuondoka mji wa Uru wenye ufanisi na anasa. Kitabu kiitwacho Family, Love and the Bible chasema hivi kuhusu nyakati za kale: “Adhabu kali zaidi ambayo ingeweza kutolewa kwa mshiriki wa familia mwenye hatia ya kufanya uhalifu mbaya ni kumfukuza, kumnyima haki ya kuwa ‘mshiriki’ wa familia. . . . Hivyo kwa njia ya pekee Abrahamu alionyesha utii kamili na tumaini alipoitikia amri ya Mungu na kuacha nchi yake na watu wake.”
7. Huenda Wakristo leo wakakabiliwaje na majaribu kama yale yaliyomkabili Abramu?
7 Huenda Wakristo leo wakakabiliwa na majaribu kama hayo. Kama Abramu, huenda tukahisi tunashinikizwa kutanguliza mambo ya kimwili badala ya mambo yanayohusiana na ibada ya kweli. (1 Yohana 2:16) Huenda tukapingwa na watu wa familia wasioamini, kutia ndani watu wa ukoo waliotengwa, ambao huenda wakajaribu kutushawishi tushirikiane nao isivyofaa. (Mathayo 10:34-36; 1 Wakorintho 5:11-13; 15:33) Hivyo, Abramu alituwekea kielelezo kizuri. Aliweka uhusiano wake na Yehova mbele ya kitu kingine chochote—hata uhusiano wa kifamilia. Hakujua hasa ni lini, ni wapi, na ni jinsi gani ahadi za Mungu zingetimizwa. Hata hivyo, alikuwa tayari kutegemeza maisha yake juu ya imani aliyokuwa nayo katika ahadi hizo. Ni kitia moyo kizuri kama nini kwamba tutangulize Ufalme katika maisha yetu leo!—Mathayo 6:33.
8. Imani ya Abramu ilikuwa na matokeo gani kwa washiriki wa karibu wa familia yake, nao Wakristo wanaweza kujifunza nini kutokana na jambo hilo?
8 Vipi washiriki wa karibu wa familia ya Abramu? Yaelekea imani na usadikisho wa Abramu ulikuwa na matokeo yenye kutokeza kwa familia yake, kwa kuwa Sarai mke wake na mpwa wake Loti, aliyekuwa yatima, walichochewa kutii amri ya Mungu ya kuondoka Uru. Nahori, nduguye Abramu, na baadhi ya wazao wake waliondoka Uru baadaye, wakawa wakazi wa Harani ambako walimwabudu Yehova. (Mwanzo 24:1-4, 10, 31; 27:43; 29:4, 5) Hata Tera babake Abramu alikubali kuondoka pamoja na mwanawe! Hivyo, Biblia inasema kwamba Tera, akiwa kichwa cha familia, ndiye aliyechukua hatua ya kuhamisha familia yake kwenda Kanaani. (Mwanzo 11:31) Sisi pia tunaweza kufurahia mafanikio ya kadiri fulani tukiwatolea jamaa zetu ushahidi kwa busara.
9. Ilimpasa Abramu afanye matayarisho gani kwa ajili ya safari yake, na kwa nini huenda matayarisho hayo yalitia ndani kujidhabihu?
9 Kabla ya kuanza safari yake, Abramu alikuwa na shughuli nyingi. Ilimpasa kuuza mali na bidhaa na kununua mahema, ngamia, chakula, na vifaa alivyohitaji. Huenda Abramu alipata hasara kwa sababu ya matayarisho hayo ya harakaharaka, lakini alifurahia kumtii Yehova. Ilikuwa siku muhimu kama nini wakati alipomaliza matayarisho hayo na msafara wake ukasimama nje ya kuta za Uru, ukiwa tayari kusafiri! Msafara huo ulisafiri kuelekea kaskazini-magharibi, kandokando ya sehemu iliyojipinda ya Mto Eufrati. Baada ya kusafiri umbali upatao kilometa 1,000 kwa majuma kadhaa, msafara huo ulifika kwenye mji uliokuwa kaskazini mwa Mesopotamia uitwao Harani, kituo kikuu cha misafara.
10, 11. (a) Yaelekea ni kwa nini Abramu alikaa Harani kwa muda fulani? (b) Wakristo wanaowatunza wazazi wao wazee wanapewa kitia moyo gani?
10 Yaelekea Abramu alikaa Harani kwa sababu ya babake Tera, aliyekuwa mzee. (Mambo ya Walawi 19:32) Vivyo hivyo Wakristo wengi leo wana pendeleo la kutunza wazazi wao wazee au wagonjwa, wengi hata wakifanya marekebisho fulani ili kufanya hivyo. Inapokuwa lazima kuwatunza wazazi, watu hao wanaweza kuwa na hakika kwamba kujidhabihu kwao kwa upendo ‘kunakubalika machoni pa Mungu.’—1 Timotheo 5:4.
11 Muda ulipita na “siku za Tera zilikuwa miaka mia mbili na mitano; Tera akafa katika Harani.” Bila shaka Abramu alihuzunishwa sana na kifo hicho, lakini kipindi cha kuomboleza kilipomalizika, aliondoka mara moja. “Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani. Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu [“Loti,” NW] mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani.”—Mwanzo 11:32; 12:4, 5.
12. Abramu alifanya nini alipokuwa huko Harani?
12 Inapendeza kuona kwamba Abramu ‘alijipatia vitu’ alipokuwa Harani. Japo alikuwa ameacha vitu vya kimwili alipoondoka Uru, Abramu aliondoka Harani akiwa tajiri. Bila shaka jambo hilo lilitokana na baraka za Mungu. (Mhubiri 5:19) Ingawa Mungu haahidi watu wake wote utajiri leo, yeye hutimiza ahadi yake ya kutosheleza mahitaji ya wale ambao ‘wameacha nyumba, ndugu, au dada’ kwa ajili ya Ufalme. (Marko 10:29, 30) Abramu pia ‘alijipatia watu,’ yaani watumishi wengi. Maandishi yaitwayo The Jerusalem Targum na Chaldee Paraphrase yanasema kwamba Abramu ‘alibadili watu imani.’ (Mwanzo 18:19) Je, imani yako inakuchochea kuzungumza na majirani, wafanyakazi wenzako, au wanashule wenzako? Badala ya kukaa tu huko Harani na kusahau amri ya Mungu, Abramu alitumia wakati wake huko kwa matokeo. Lakini wakati wa kukaa huko sasa ulikuwa umeisha. “Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru.”—Mwanzo 12:4.
Ng’ambo ya Eufrati
13. Abramu alivuka Mto Eufrati lini, na kuvuka huko kulimaanisha nini?
13 Ilimbidi Abramu asafiri tena. Aliondoka Harani na kusafiri umbali upatao kilometa 90 kuelekea magharibi. Huenda ikawa kwamba Abramu alikaa kwa muda katika eneo fulani kwenye Eufrati, ng’ambo ya kituo cha kale cha biashara cha Karkemishi. Kituo hicho kilikuwa muhimu kwa misafara iliyovuka kwenda ng’ambo ya pili.b Msafara wa Abramu ulivuka mto huo lini? Biblia inaonyesha kwamba ulivuka miaka 430 kabla ya kule Kutoka kwa Wayahudi nchini Misri mwezi wa Nisani 14, 1513 K.W.K. Andiko la Kutoka 12:41 lasema: “Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya BWANA yalitoka nchi ya Misri.” (Italiki ni zetu.) Basi inaelekea kwamba lile agano la Kiabrahamu lilianza kufanya kazi Nisani 14, 1943 K.W.K., wakati ambapo kwa utii Abramu alivuka Eufrati.
14. (a) Abramu angeweza kuona nini kwa macho yake ya imani? (b) Ni katika maana gani watu wa Mungu leo wamebarikiwa zaidi kuliko Abramu?
14 Abramu alikuwa ameacha mji wenye ufanisi. Lakini sasa angeweza kuona kimbele “jiji lililo na misingi halisi,” serikali ya uadilifu itakayotawala wanadamu. (Waebrania 11:10) Naam, japo Abramu alikuwa na ujuzi kidogo sana, alikuwa ameanza kupata ufahamu wa juujuu tu kuhusu kusudi la Mungu la kukomboa wanadamu wenye kufa. Leo, tumebarikiwa kuwa na ujuzi mwingi zaidi wa makusudi ya Mungu kuliko Abramu. (Mithali 4:18) Sasa “jiji,” au utawala wa Ufalme, ambao Abramu alitumaini unatawala, na ulisimamishwa tangu mwaka wa 1914. Kwa hiyo, je, hatupaswi kuchochewa kutenda mambo yanayoonyesha imani na tumaini katika Yehova?
Kukaa Katika Bara Lililoahidiwa Kwaanza
15, 16. (a) Kwa nini Abramu alihitaji kuwa na ujasiri ili kumjengea Yehova madhabahu? (b) Wakristo leo wanawezaje kuwa na ujasiri kama Abramu?
15 Andiko la Mwanzo 12:5, 6 latuambia: “[Mwishowe] wakaingia katika nchi ya Kanaani. Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa shekemu; mpaka mwaloni wa More.” Shekemu ulikuwa umbali wa kilometa 50 kaskazini ya Yerusalemu kwenye bonde lenye rutuba ambalo limeelezwa kuwa “paradiso ya bara takatifu.” Hata hivyo, “Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.” Kwa kuwa maadili ya Wakaanani yalikuwa yamepotoka, ilimbidi Abramu ajitahidi kulinda familia yake na uvutano wao wenye kupotosha.—Kutoka 34:11-16.
16 Kwa mara nyingine, “BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao [“mbegu,” NW] wako nitawapa nchi hii.” Ni jambo lenye kusisimua kama nini! Bila shaka, Abramu alihitaji kuwa na imani ili kufurahia jambo ambalo lingenufaisha tu uzao wake wakati ujao. Hata hivyo, Abramu aliitikia kwa ‘kumjengea madhabahu BWANA aliyemtokea.’ (Mwanzo 12:7) Msomi mmoja wa Biblia adokeza: “Kujengwa [kwa] madhabahu nchini humo kulikuwa hasa njia ya kuimiliki nchi hiyo kirasmi kwa kutegemea haki ambayo Abramu alipata kutokana na imani yake.” Pia ujenzi wa madhabahu hiyo ulikuwa tendo la ujasiri. Yaelekea kwamba madhabahu hiyo ilikuwa kama ile ambayo imeelezwa katika agano la Sheria, ambayo ilijengwa kwa mawe ya asili (yasiyochongwa). (Kutoka 20:24, 25) Ingekuwa tofauti kabisa na madhabahu zilizotumiwa na Wakanaani. Kwa hiyo Abramu alichukua msimamo wa kijasiri akiwa mwabudu wa Mungu wa kweli, Yehova, jambo ambalo lingeweza kufanya achukiwe na hata kuhatarisha maisha yake. Namna gani sisi leo? Je, baadhi yetu—hasa wachanga—tunasita kuwajulisha majirani au wanashule wenzetu kwamba tunamwabudu Yehova? Acheni kielelezo cha ujasiri cha Abramu kituchochee sote kujivunia kuwa watumishi wa Yehova!
17. Abramu alijithibitishaje kuwa mhubiri wa jina la Mungu, na jambo hilo linawakumbusha nini Wakristo leo?
17 Sikuzote Abramu aliiona ibada ya Yehova kuwa muhimu kokote alikokwenda. “Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea BWANA madhabahu huko, akaliita jina la BWANA.” (Mwanzo 12:8) Maneno ya Kiebrania ‘kuliitia jina’ pia yanamaanisha “kulitangaza (kulihubiri) jina hilo.” Yaelekea Abramu alilitangaza jina la Yehova kwa ujasiri miongoni mwa majirani wake Wakaanani. (Mwanzo 14:22-24) Jambo hilo linatukumbusha jukumu letu la kushiriki kadiri tuwezavyo “kulifanyia jina lake tangazo la hadharani” leo.—Waebrania 13:15; Waroma 10:10.
18. Abramu alikuwa na uhusiano wa aina gani na wakazi wa Kanaani?
18 Abramu hakukaa sana katika maeneo hayo. “Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu”—eneo kavu upande wa kusini wa milima ya Yuda. (Mwanzo 12:9, Biblia Habari Njema) Kwa kuendelea kuhamahama na kujithibitisha kuwa mwabudu wa Yehova katika kila eneo jipya, Abramu na jamaa yake ‘walitangaza hadharani kwamba wao walikuwa watu wasiojulikana na wakaaji wa muda katika nchi.’ (Waebrania 11:13) Sikuzote waliepuka kuwa na ukaribu sana na majirani wao wapagani. Vivyo hivyo leo, Wakristo hawapaswi kuwa “sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:16) Japo sisi huwaonyesha fadhili na heshima majirani wetu na wafanyakazi wenzetu, tunakuwa waangalifu tusijiingize katika mwenendo unaoonyesha roho ya ulimwengu uliojitenga na Mungu.—Waefeso 2:2, 3.
19. (a) Kwa nini maisha ya kuhamahama yalikuwa magumu kwa Abramu na Sarai? (b) Ni magumu gani zaidi yaliyokuwa karibu kumpata Abramu?
19 Na tusisahau kwamba haikuwa rahisi kwa Abramu na Sarai kuzoea maisha magumu ya kuhamahama. Walipata chakula kutokana na mifugo yao badala ya kukinunua kwenye mojawapo ya masoko ya Uru yaliyojaa bidhaa; waliishi mahemani badala ya kuishi katika nyumba iliyojengwa vizuri. (Waebrania 11:9) Abramu alikuwa na shughuli nyingi katika maisha yake; alikuwa na kazi nyingi ya kusimamia mifugo yake na watumishi wake. Yaelekea Sarai alifanya kazi ambazo kidesturi zilifanywa na wanawake wa utamaduni huo: kukanda unga, kuoka mikate, kusokota sufu, na kushona nguo. (Mwanzo 18:6, 7; 2 Wafalme 23:7; Mithali 31:19; Ezekieli 13:18) Hata hivyo, majaribu zaidi yalikuwa karibu. Muda si muda Abramu na jamaa yake wangekabili hali ambayo ingehatarisha maisha yao! Je, imani ya Abramu ingekuwa yenye nguvu za kukabili hali hiyo ngumu?
[Maelezo ya Chini]
a Japo sasa Mto Eufrati uko umbali wa kilometa 16 mashariki ya mahali ambapo mji wa zamani wa Uru ulikuwa, kuna uthibitisho unaoonyesha kwamba nyakati za kale mto huo ulikuwa magharibi ya mji huo. Hivyo, baadaye ingeweza kusemwa kwamba Abramu alitoka “ng’ambo ya Mto [Eufrati].”—Yoshua 24:3.
b Karne kadhaa baadaye, Mfalme Ashurnasirpal wa Pili wa Ashuru alitumia vyelezo kuvuka Eufrati karibu na Karkemishi. Biblia haisemi iwapo Abramu na msafara wake walitumia vyelezo au hawakuvitumia kuvuka mto huo.
Je, Umefahamu?
• Kwa nini Abramu anaitwa “baba ya wote wale walio na imani”?
• Kwa nini Abramu alihitaji kuwa na imani ili kuondoka Uru wa Wakaldayo?
• Abramu alionyeshaje kwamba aliiona ibada ya Yehova kuwa muhimu?
[Ramani katika ukurasa wa 16]
SAFARI YA ABRAMU
Uru
Harani
Karkemishi
KANAANI
Bahari Kuu
[Hisani]
Based on a map copyrighted by Pictorial Archive (Near Eastern History) Est. and Survey of Israel
[Picha katika ukurasa wa 15]
Abramu alihitaji kuwa na imani ili kuacha maisha ya starehe huko Uru
[Picha katika ukurasa wa 18]
Kwa kuishi katika mahema, Abramu na jamaa yake ‘walitangaza hadharani kwamba wao walikuwa watu wasiojulikana na wakaaji wa muda’