Christophe Plantin Mtangulizi wa Uchapishaji wa Biblia
JOHANNES GUTENBERG (karibu 1397-1468) anajulikana sana kwa kutokeza Biblia ya kwanza iliyochapwa kwa kutumia mashini ya kuchapishia yenye herufi zinazopangwa. Lakini watu wengi hawamjui Christophe Plantin. Alikuwa mtangulizi wa uchapishaji ambaye alifanya kazi muhimu ya kuwawezesha watu ulimwenguni pote kupata vitabu na Biblia katika miaka ya 1500.
Christophe Plantin alizaliwa mwaka wa 1520 hivi huko Saint-Avertin, Ufaransa. Akipendelea eneo ambalo lilikuwa na watu ambao walikubali imani mbalimbali za kidini na ambalo lilikuwa na nafasi nyingi za kujiendeleza kiuchumi kuliko Ufaransa, Plantin, akiwa na umri wa miaka 28 hivi, alihamia Antwerp katika Nchi za Chini.a
Mwanzoni, Plantin alifanya kazi ya kutia vitabu jalada na kutengeneza bidhaa za ngozi. Bidhaa zake maridadi za ngozi zilipendwa sana na matajiri. Hata hivyo, jambo fulani lililotukia mwaka wa 1555 lilimfanya Plantin abadili kazi yake. Akiwa njiani kupeleka mkoba wa ngozi ulioagizwa na mtawala wa Nchi za Chini, Mfalme Philip wa Pili wa Hispania, Plantin alishambuliwa barabarani huko Antwerp. Walevi fulani walimdunga kwa upanga kwenye bega. Ingawa alipona jeraha hilo, Plantin hangeweza kufanya kazi ya mikono na hivyo akalazimika kuacha kazi yake. Akitegemezwa kifedha na Hendrik Niclaes, aliyekuwa kiongozi wa kikundi fulani cha Waanabaptisti, Plantin alianza kazi ya uchapishaji.
“Kazi na Subira”
Plantin alikiita kiwanda chake De Gulden Passer (Bikari ya Dhahabu). Alama ya kiwanda hicho ilikuwa bikari mbili za dhahabu zenye maneno “Labore et Constantia,” yaani, “Kazi na Subira.” Ilionekana kwamba alama hiyo ilimfaa sana mtu huyo mwenye bidii.
Akiishi nyakati zenye mabadiliko makubwa ya kidini na kisiasa huko Ulaya, Plantin alijaribu kuepuka matatizo. Kazi ya kuchapisha ilikuwa muhimu sana kwake kuliko jambo lolote lile. Ingawa alipendelea Marekebisho ya Kiprotestanti, yeye “hakujihusisha sana na suala la dini,” asema mtungaji wa vitabu Maurits Sabbe. Kwa sababu hiyo, uvumi ulienea kwamba Plantin alichapisha vitabu vya uasi wa kidini. Hivyo, katika mwaka wa 1562, alilazimika kukimbilia Paris kwa zaidi ya mwaka.
Plantin aliporudi Antwerp mnamo 1563, alishirikiana na wafanya-biashara matajiri, ambao baadhi yao walijulikana kwa sababu ya kufuata mafundisho ya Calvin. Katika miaka mitano ya kushirikiana nao, kiwanda cha Plantin kilichapisha vichapo mbalimbali 260. Vilitia ndani tafsiri ya Biblia ya Kiebrania, Kigiriki, na Kilatini na vilevile tafsiri maridadi ya Kiholanzi ya Biblia ya Kikatoliki ya Louvain.
“Kazi Muhimu Zaidi ya Uchapishaji”
Mnamo mwaka wa 1567, upinzani kwa utawala wa Hispania ulipokuwa ukiongezeka katika Nchi za Chini, Mfalme Philip wa Pili wa Hispania alimtuma Mtawala wa jimbo la Alba ili awe gavana huko. Akiwa na mamlaka kamili aliyopewa na mfalme, mtawala huyo alijaribu kukomesha upinzani wa Waprotestanti uliokuwa ukiongezeka. Kwa hiyo, Plantin alianzisha mradi mkubwa ambao alitumaini ungewafanya watu waache kumshuku kuwa mwasi wa kidini. Alitamani sana kuchapisha tafsiri ya wasomi ya maandishi ya Biblia katika lugha za awali. Ili kuichapisha, Plantin alifaulu kupata msaada wa Philip wa Pili. Mfalme huyo aliahidi kumpa msaada wa kifedha na kumtuma mteteaji maarufu wa haki za kibinadamu Arias Montano ili asimamie mradi huo.
Montano alikuwa na kipawa cha lugha, naye alifanya kazi kwa saa 11 kila siku. Alisaidiwa na wataalamu wa lugha wa Hispania, Ubelgiji, na Ufaransa. Kusudi lao lilikuwa kutayarisha tafsiri mpya ya Biblia maarufu ya Complutensian Polyglot.b Mbali na Vulgate ya Kilatini, Septuajinti ya Kigiriki, na maandishi ya awali ya Kiebrania, Biblia mpya ya Polyglot ya Plantin ilikuwa na Targumi ya Kiaramu, Peshitta ya Kisiria, na tafsiri nyingine za Kilatini za neno kwa neno zinazotambuliwa.
Kazi ya uchapishaji ilianza mwaka wa 1568. Kazi hiyo kubwa ilifanywa haraka sana na kukamilishwa mwaka wa 1572. Montano alisema hivi katika barua aliyomwandikia Mfalme Philip wa Pili: “Kazi kubwa inafanywa hapa kwa mwezi mmoja kuliko ile inayofanywa Roma kwa mwaka mmoja.” Plantin alichapisha nakala 1,213 za Biblia mpya ya Polyglot. Kila nakala ilikuwa na mabuku manane makubwa. Kwenye ukurasa wa kwanza wa Biblia hiyo, kulikuwa na picha ya simba, ng’ombe-dume, mbwa-mwitu, na mwana-kondoo wakila pamoja kwa amani katika chombo kimoja, kama inavyoonyeshwa katika Isaya 65:25. Bei ya mabuku ambayo hayakuwa yameunganishwa ilikuwa gilda 70 (pesa za Uholanzi). Ilikuwa bei ghali kwa sababu wakati huo familia ya kawaida ilipata mshahara wa gilda 50 hivi kwa mwaka. Baadaye, Biblia yenye jalada iliitwa Antwerp Polyglot. Pia, iliitwa Biblia Regia (Biblia ya Kifalme) kwa sababu Mfalme Philip wa Pili ndiye aliyeutegemeza kifedha mradi huo.
Hata ingawa Papa Gregory wa 13 alikubali Biblia hiyo, Arias Montano alishutumiwa vikali kwa sababu ya kazi yake. Sababu moja ni kwamba Montano aliona maandishi ya awali ya Kiebrania kuwa bora kuliko Vulgate ya Kilatini. Mpinzani wake mkuu alikuwa León de Castro, mwanatheolojia Mhispania ambaye aliiona Vulgate ya Kilatini kuwa yenye mamlaka kamili. De Castro alimshutumu Montano kwamba aliivuruga Biblia kwa kuingiza falsafa zinazopinga Utatu. Kwa mfano, de Castro alidai kwamba Peshitta ya Kisiria haikuwa na sehemu ifuatayo iliyoongezwa kwa uwongo kwenye andiko la 1 Yohana 5:7: “Mbinguni, Baba, Neno, na Roho Mtakatifu: na watatu hawa ni mmoja.” (King James Version) Hata hivyo, Baraza la Kihispania la Kuwahukumu Waasi wa Kidini, halikumpata Montano na hatia ya uasi. Tafsiri ya Antwerp Polyglot huonwa na watu fulani kuwa “kazi muhimu zaidi ya uchapishaji iliyofanywa na mchapishaji mmoja katika karne ya 16.”
Faida Yenye Kudumu
Viwanda vingi vya uchapishaji vilikuwa na mashini mbili au tatu tu. Hata hivyo, katika kilele cha kazi yake, inaelekea Plantin alikuwa na mashini 22 za kuchapisha na wafanyakazi 160. Katika nchi zote zinazotumia lugha ya Kihispania, alijulikana kuwa mchapishaji maarufu zaidi.
Wakati huohuo, upinzani kwa utawala wa Hispania ulikuwa ukiongezeka katika Nchi za Chini. Jiji la Antwerp lilijikuta katika mzozo huo. Katika mwaka wa 1576, askari wa kukodishwa wa Hispania ambao hawakuwa wamelipwa mshahara waliasi na kulipora jiji hilo. Zaidi ya nyumba 600 ziliteketezwa, na maelfu ya wakaaji wa Antwerp wakauawa. Wafanya-biashara walikimbia jiji hilo. Kwa sababu hiyo, Plantin alipata hasara kubwa ya kifedha. Isitoshe, alilazimika kulipa askari hao waasi kodi kubwa sana.
Mnamo mwaka wa 1583, Plantin alihamia Leiden, jiji ambalo lilikuwa kilometa 100 kaskazini ya Antwerp. Akiwa huko alianzisha kiwanda cha uchapishaji na akachaguliwa kuwa mchapishaji wa Chuo Kikuu cha Leiden, taasisi iliyoanzishwa na Waprotestanti waliokuwa wafuasi wa Calvin. Shutuma za awali kwamba aliasi Kanisa Katoliki zikatokea tena. Hivyo, Plantin akarudi Antwerp mwishoni mwa mwaka wa 1585, muda mfupi baada ya jiji hilo kuanza kutawaliwa na Hispania. Kufikia wakati huo, alikuwa na umri wa miaka 60 na kitu, na kiwanda chake cha uchapishaji kilikuwa na wafanyakazi wanne tu walioendesha mashini moja. Plantin alianza kukijenga upya kiwanda chake. Hata hivyo, hakikurudia kabisa hali yake ya kwanza, naye Plantin akafa tarehe 1, Julai (Mwezi wa 7) 1589.
Katika muda wa miaka 34, Christophe Plantin alichapisha matoleo mbalimbali 1,863 ya vitabu, yaani, wastani wa matoleo 55 hivi kila mwaka. Hata leo, hiyo ingekuwa kazi kubwa sana kufanywa na mchapishaji mmoja tu! Ingawa Plantin mwenyewe aliepuka kuchukua msimamo imara wa kidini, jitihada zake hazikuendeleza tu kazi na ufundi wa uchapishaji, lakini pia ziliwasaidia watu kujifunza Maandiko yaliyoongozwa kwa roho ya Mungu. (2 Timotheo 3:16) Bila shaka, Plantin na wachapishaji wenzake walisaidia sana kuwawezesha watu wa kawaida waipate Biblia.
[Maelezo ya Chini]
a Maneno “Nchi za Chini” yanarejelea eneo la pwani kati ya Ujerumani na Ufaransa, ambalo sasa ni nchi ya Ubelgiji, Uholanzi, na Luxembourg.
b Biblia hiyo ya lugha kadhaa iliyochapishwa mnamo 1517, ilikuwa na maandishi ya Kiebrania, Kigiriki, Kilatini, na visehemu vya Kiaramu. Ona makala “Tafsiri ya Complutensian Polyglot—Ni Kifaa Muhimu Katika Utafsiri,” katika gazeti Mnara wa Mlinzi la Aprili 15, 2004, ukurasa wa 28-31.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]
JUMBA LA MAKUMBUSHO LA PLANTIN-MORETUS
Mnamo mwaka wa 1877, jengo lililo jijini Antwerp, ambako Plantin na wazao wake waliishi na kufanyia kazi lilifunguliwa kwa ajili ya watu wote likiwa jumba la makumbusho. Hakuna kiwanda kingine chochote kilichojengwa wakati huo ambacho kipo katika hali nzuri leo. Mashini tano za kuchapishia zilizotumiwa katika karne ya 17 na 18 ziko katika jumba hilo. Mashini nyingine mbili ambazo zinaonwa kuwa za zamani zaidi ulimwenguni, zilitengenezwa nyakati za Plantin. Jumba hilo la makumbusho lina vyombo 15,000 hivi vya kuyeyushia madini ili kutengeneza herufi, mihuri 15,000 ya mbao, na mabamba 3,000 ya shaba. Maktaba ya jumba hilo la makumbusho ina hati 638 za kuanzia karne ya 9 hadi ya 16, na pia vitabu 154 vilivyochapishwa kabla ya mwaka wa 1501. Hivyo vinatia ndani Biblia ya kwanza ya Gutenberg ambayo ilichapishwa kabla ya mwaka wa 1461, na vilevile nakala moja ya Biblia maarufu ya Plantin iliyoitwa Antwerp Polyglot.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Arias Montano
[Picha katika ukurasa wa 16]
Biblia ya “Antwerp Polyglot” ina maandishi ya Kiebrania, “Vulgate” ya Kilatini, “Septuajinti” ya Kigiriki, “Peshitta” ya Kisiria, na Targumi ya Kiaramu pamoja na tafsiri zake za Kilatini
[Picha zimeandalia na]
By courtesy of Museum Plantin-Moretus/Stedelijk Prentenkabinet Antwerpen
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Both images: By courtesy of Museum Plantin-Moretus/Stedelijk Prentenkabinet Antwerpen