Maisha Katika Nyakati za Biblia Mvuvi
“Alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya [Yesu] aliona ndugu wawili, Simoni anayeitwa Petro na Andrea ndugu yake, wakishusha wavu wa kuvulia samaki ndani ya bahari, kwa maana walikuwa wavuvi. Naye akawaambia: ‘Nifuateni, nami nitawafanya ninyi kuwa wavuvi wa watu.’”—MATHAYO 4:18, 19.
SAMAKI, uvuvi, na wavuvi ni mambo yanayotajwa mara kwa mara katika masimulizi ya Injili. Hata Yesu alitumia mifano mingi inayohusu uvuvi. Na hilo si jambo la ajabu kwa sababu alitumia muda mwingi akifundisha karibu au kando ya Bahari ya Galilaya. (Mathayo 4:13; 13:1, 2; Marko 3:7, 8) Ziwa hilo maridadi lenye maji safi lina urefu wa kilomita 21 hivi na upana wa kilomita 11 hivi. Huenda mitume saba wa Yesu—Petro, Andrea, Yakobo, Yohana, Filipo, Tomasi, na Nathanaeli—walikuwa wavuvi.—Yohana 21:2, 3.
Maisha ya mvuvi yalikuwaje katika siku za Yesu? Tunakuomba ujifunze mengi kuhusu wanaume hao na kazi yao. Utawathamini zaidi mitume hao na kuelewa vizuri matendo na mifano ya Yesu. Kwanza, fikiria jinsi mambo yalivyokuwa wavuvi walipofanya kazi kwenye Bahari ya Galilaya.
“Msukosuko Mkubwa Ukatokea Katika Bahari”
Bahari ya Galilaya iko katika bonde la ufa, na eneo hilo liko karibu mita 210 chini ya usawa wa bahari. Kando ya ziwa hilo kuna miteremko yenye miamba, na upande wa kaskazini, kuna Mlima mrefu wa Hermoni wenye kilele kinachofika mawinguni. Katika majira ya baridi kali, nyakati nyingine upepo baridi husababisha mawimbi. Wakati wa majira ya joto, hewa yenye joto hufunika maji ya bahari hiyo. Bila kuonekana, upepo mkali huvuma kutoka juu ya milima iliyo karibu na kusababisha dhoruba inayowavuruga mabaharia wanaosafiri katika bahari hiyo. Yesu na wanafunzi wake walikabiliana na dhoruba kama hiyo.—Mathayo 8:23-27.
Wavuvi walitumia mashua zilizotengenezwa kwa mbao ambazo zilikuwa na urefu wa mita 8 hivi na upana wa karibu mita 2. Nyingi kati ya mashua hizo zilikuwa na mlingoti na chumba kidogo kilichokuwa katika tezi. (Marko 4:35-41) Mashua hizo zenye nguvu zilikabili mkazo wa upepo ambao ulisukuma tanga na mlingoti upande mmoja, huku uzito wa wavu ukiivuta mashua hiyo upande mwingine.
Wanaume waliendesha mashua hizo kwa kutumia makasia yaliyokuwa kwenye pande zote mbili za mashua hizo. Huenda kikundi cha wavuvi kilikuwa na wanaume sita au zaidi. (Marko 1:20) Kwa kuongezea, inaelekea mashua hizo zilibeba vifaa mbalimbali, kama vile tanga iliyotengenezwa kwa kitani (1), kamba (2), makasia (3), nanga iliyotengenezwa kwa jiwe (4), mavazi yaliyokauka na yenye joto (5), vyakula (Marko 8:14) (6), vikapu (7), mto (Marko 4:38) (8), na wavu (9). Huenda pia walibeba maboya ya ziada (10), na vilevile uzani wa kuzamisha wavu (11), vifaa vya kurekebisha (12), na mienge (13).
“Wakakusanya Samaki Wengi Sana”
Leo, kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza, maeneo yenye samaki wengi katika Bahari ya Galilaya yako karibu na milango ya vijito na mito inayoleta maji katika bahari hiyo. Katika maeneo hayo, mimea huingia baharini na kuwavutia samaki. Ili kushika mawindo yao, mara nyingi wavuvi katika nyakati za Yesu walifanya kazi usiku, wakitumia mienge. Pindi moja, wanafunzi fulani wa Yesu walijaribu kuvua samaki usiku kucha na hawakupata chochote. Lakini siku iliyofuata, baada ya kuagizwa na Yesu, walishusha nyavu zao tena na wakavua samaki wengi sana hivi kwamba mashua zao zilikuwa karibu kuzama.—Luka 5:6, 7.
Nyakati fulani wavuvi walivua katika maeneo yaliyokuwa na maji yenye kina kirefu. Walitumia mashua mbili walipokuwa wakivua. Wanaume hao walitandaza wavu katikati ya mashua hizo na wakaziendesha kwenda pande tofauti, huku wakishusha wavu na kuwazingira samaki. Mashua hizo zilizunguka katika mwendo wa duara, na kuwanasa samaki waliokuwa katikati. Kisha, wavuvi walivuta kamba zilizofungwa kwenye ncha za wavu, na kuwainua samaki mpaka ndani ya mashua. Huenda wavu huo ulikuwa na urefu unaozidi mita 30 na kina cha mita mbili hivi, ukubwa uliotosha kushika kundi zima la samaki. Sehemu ya juu ya wavu huo iliinuliwa na maboya, na upande wa chini ulikuwa umefungiliwa vitu vizito. Wavuvi walitega wavu tena, kisha kuukokota tena na tena, kwa saa nyingi.
Katika maji yasiyo na kina kirefu, kikundi cha wavuvi kilitumia mbinu tofauti. Mashua ilivuta upande mmoja wa wavu kutoka kwenye ufuo na kuingia baharini na kisha kuzunguka na kurudi ufuoni, na hivyo kuwanasa samaki. Kisha, wanaume waliokuwa kando ya bahari walikokota wavu ili kuwaleta samaki ufuoni na kuwachagua. Waliwaweka samaki wazuri ndani ya mitungi. Wengine wao waliuzwa katika eneo hilo kabla hawajakaushwa. Wengi wao walikaushwa na kutiwa chumvi au siki, kisha wakahifadhiwa ndani ya mitungi iliyotengenezwa kwa udongo na kusafirishwa hadi Yerusalemu au nchi nyinginezo. Viumbe wasio na magamba na mapezi, kama vile mikunga, walionwa kuwa wasio safi na walitupwa. (Mambo ya Walawi 11:9-12) Yesu alirejezea mbinu hiyo ya uvuvi alipolinganisha “ufalme wa mbinguni” na wavu wa kukokotwa. Pia, alilinganisha aina mbalimbali ya samaki na watu wazuri na wabaya.—Mathayo 13:47-50.
Huenda mvuvi mmoja alitumia uzi wenye ndoano ili kuvua. Au angetumia wavu mdogo. Ili kutumia wavu huo, angetembea na kuingia ndani ya bahari, angeshika wavu kwa mikono yake, na kuurusha juu na mbali kutoka kwenye mwili wake. Wavu huo uliokuwa na umbo la kuba ungefunguka, ungeanguka juu ya maji, na kisha kuzama. Ikiwa mvuvi angetupa wavu mahali penye samaki, angenasa samaki wachache na kuvuta wavu kwa kutumia kamba iliyofungwa katikati ya wavu huo.
Nyavu ziliuzwa kwa bei ya juu na zilihitaji kazi nyingi ili kurekebishwa, hivyo wanaume hao walizitumia kwa uangalifu. Mvuvi alitumia wakati wake mwingi akirekebisha, kuosha, na kukausha nyavu, na alifanya kazi hizo baada ya kurudi kutoka kwenye kila safari ya uvuvi. (Luka 5:2) Mtume Yakobo na ndugu yake Yohana walikuwa wameketi katika mashua yao wakitengeneza nyavu zao Yesu alipowaomba wamfuate.—Marko 1:19.
Kati ya samaki waliotafutwa na wavuvi wa karne ya kwanza ni samaki wanaopatikana kwa wingi wanaoitwa tilapia. Samaki hao waliliwa kwa ukawaida na watu wengi huko Galilaya, na inaelekea Yesu alikula samaki hao wenye ladha tamu. Huenda alitumia tilapia waliokaushwa na kutiwa chumvi alipofanya muujiza wa kulisha maelfu ya watu kwa kutumia samaki wawili. (Mathayo 14:16, 17; Luka 24:41-43) Mara nyingi samaki hao huogelea wakiwa wamebeba samaki wadogo kinywani. Hata hivyo, ikiwa hawabebi samaki wadogo, yaelekea wanabeba jiwe dogo, au huenda wakaokota sarafu inayong’aa iliyolala chini ya bahari.—Mathayo 17:27.
Katika karne ya kwanza wavuvi wenye mafanikio walikuwa na subira, bidii, na walikuwa tayari kuvumilia hali ngumu walipokuwa wakitafuta kitu chenye thamani. Wale waliokubali mwaliko wa Yesu wa kujiunga naye katika kazi ya kufanya wanafunzi pia walihitaji sifa kama hizo ili wafanikiwe kuwa “wavuvi wa watu.”—Mathayo 28:19, 20.
[Picha katika ukurasa wa 19]
(Tazama chapisho)