Kuutazama Ulimwengu
VISA VYA KUJIUA CHINA
Kujiua kumekuwa kisababishi chenye kuongoza cha kifo kisicho cha kawaida katika China, na wenye mamlaka Wachina wahangaika. Kulingana na China Daily, “karibu watu 140,000 wanajiua” kila mwaka, huku wanawake wakiwa karibu 98,000 kati ya hesabu hiyo. Kwa nini wanawake wengi hivyo hutwaa uhai wao? Jambo kubwa lililotajwa ni kushindwa kwa waume kutimiza “mahitaji ya kimawazo na kihisia-moyo” ya wake zao. Mtafiti Shan Guangnai alisema hivi: “Takwimu huonyesha kwamba nusu ya wanawake wenye kujiua walikufa kwa sababu ya magomvi na ukosefu wa mafanikio katika ndoa.” Jambo jingine lililotajwa lilikuwa maendeleo ya viwandani, ambayo, kwa kufanya maisha yaende haraka zaidi, yameleta “hitilafiano kati ya kanuni za zamani na mpya za kijamii na viwango vya kiadili.” Guangnai apendekeza kwamba msaada wa kuzuia kujiua ni maisha ya jamaa yenye uchangamfu na upendo pamoja na mahusiano yenye upatano.
USHINDI WA HANDAKI
Handaki la reli la Mount Macdonald lililomalizwa hivi majuzi katika Safu ya Milima Roki ya Kanada, lenye urefu wa kilometa 14.6, ndilo handaki refu zaidi katika Amerika Kaskazini. Ilichukua miezi 54 kwa timu mbili za wafanya kazi 500 kulimaliza. Kulingana na Ron Tanaka, mhandisi mkuu wa ujenzi wa reli, timu za wafanya kazi zilianza kila upande wa mlima na zikakutana katikati, kwa kukosana kwa futi moja tu. Handaki hilo ni sehemu ya mradi wa dola milioni 500 ambalo pia hutia ndani handaki la kilometa 1.8 chini ya Mlima Shaughnessy, madaraja matano makubwa, na daraja-mapao la meta 1,229. Uhandisi wa mradi huo ulifanywa ili mwinuko wa kupitia Bonde la Beaver upungue kutoka asilimia 2.2 uwe asilimia 1, hivyo kuondoa uhitaji wa kuongezea vichwa vya usukumaji kwenye hesabu ya magari-moshi ya uchukuzi yenye kuelekea magharibi. Hapo zamani vichwa sita vyenye nguvu-farasi 3,000 ndivyo vilivyohitajiwa ili kusukuma magari-moshi ya mizigo yavuke kipito cha Rogers Pass kuingia Bonde la Beaver.
FARU ASIYE NA PEMBE
Katika jitihada ya kufa au kupona ya kupinza wawindaji haramu, maofisa wenye kuangalia wanyama-mwitu wa Namibia wameanza kutumia msumeno kukata pembe za faru ili kuwafanya wasiwe wa thamani yoyote kwa wawindaji haramu. Wahifadhi wanyama hudai kwamba kufanya hivyo ni jambo lisilo na maumivu sawasawa na kukata kucha za vidole vya mtu, kwa maana pembe hizo ni vichipuko tu vyenye kutokana na nywele zilizofinyana sana, navyo havina milango yoyote ya fahamu. Ingawa faru asiye na pembe hana kinga dhidi ya wanyama wanyemeleaji na dhidi ya faru wengine, hatua hiyo ya mwisho kabisa yaonekana yahitajiwa ili kukomesha machinjo ya faru mweusi wa Afrika, ambayo ni namna moja ya mnyama aliyehatarishwa. Katika muda unaopungua mwongo mmoja, faru mweusi wa Kiafrika wamepunguzwa kutoka 15,000 wakawa 3,500, ndivyo lilivyoripoti gazeti African Wildlife. Na katika Namibia, ambako ni faru karibu 100 tu waliofikiriwa kuwa wamebaki, angalau 16 wameangushwa na wawindaji haramu katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu. Pembe za faru mweusi, ambazo huthaminiwa sana kwa kudhaniwa kuwa zaweza kutumiwa kama dawa ya utibabu, kwa sasa huuzwa kimagendo kwa kiasi kinachofikia dola 50,000 kwa kila jozi moja.
WITO MPYA WA KUOMBA MSAADA WA HARAKA
“Morse code” yenye kutumika kupeleka ishara za kuomba msaada wa haraka, ambayo imekuwa ikitumiwa tangu zile siku za mwanzo-mwanzo wa mawasiliano ya simu, imo katika hatari ya kutoweka kabisa—angalau kuhusiana na usafiri-meli. Kuanzia 1993, meli zitakuwa na kifaa cha bikoni-redio yenye mlio wa kusononesha ambayo “hupeleka ishara ya msononeko [kupitia setilaiti] wakati kibonyezo fulani kifinywapo,” yaripoti International Herald Tribune. Karibuni kutakuwa na sharti la kutumia mfumo mpya huu ulimwenguni pote baada ya 1999, nao utaruhusu walinda-pwani wasome katika mitambo ya kompyuta zao jina la meli iliyohatarika na mahali ilipo hasa. Hata hivyo, “Morse code” ingali ina matumizi. “Wakati tetemeko la dunia la Jiji la Meksiko 1985 lilipozima kadiri kubwa ya nguvu za umeme,” lasema gazeti hilo, “waendeshi wa muda wa redio walitumia telegrafu ya Morse kupiga simu ya msaada. Ishara za ‘Morse code’ zaweza kupita kwa sababu huhitaji nguvu chache za utangazaji kuzipeleka kuliko zile ambazo zingehitajiwa ili kupeleka jumbe za sauti, na haivurugiki hata ikipotoka kidogo katika upelekaji.”
KULIPIA SALA
Wasiwasi mkubwa wa Wajapani wengi wenye umri mkubwa ambao watu wao wa ukoo ni wachache au hawana wowote ni kwamba wakiisha kufa, hakutakuwa na mtu wa kutoa sala kwa ajili yao wala wa kutunza makaburi yao. Hata hivyo, mahekalu ya Kibuddha yanaanza kuitikia kufanya hivyo—kwa malipo. Hekalu moja la Tokyo lajitolea kuchimbua masalio ya mfu kwenye sikukuu zote kubwa-kubwa na kutoa sala kwa ajili ya mfu huyo, kwa muda wote ambao hekalu hilo litakuwapo. Malipo ni ¥500,000 (dola 3,500 za United States). Ua wa makaburi katika Wilaya ya Saitama iliyo karibu hutoa uhakikishio kamili wa kutoa sala na kutunza kaburi kwa miaka 50 kwa malipo ya ¥700,000 (dola 4,800 za United States). Tayari maombi yanaingia kutoka kwa watu mmoja mmoja wanaotafuta huduma ya ‘malipo ya sala.’
KUNYWA AU KUTOKUNYWA
Je! kweli kiasi “cha kawaida” cha kunywa pombe kila siku hutokeza tisho kwa afya? Ndiyo, adai H. H. Kornhuber wa Hospitali ya Ugonjwa wa Neva kwenye Chuo Kikuu cha Ulm, Jamhuri ya Muungano ya Ujeremani. Kunywa pombe kila siku huharibu utaratibu wa ini wa kuyeyusha shahamu (mafuta) na huongoza kwenye unene wa kupita kiasi. Athari nyingine za kando ni kupanda kwa mpigo wa damu na mkazo wa damu na ongezeko la kiasi cha kolesteroli. Uchunguzi mbalimbali waonyesha “waziwazi kwamba mpaka wenye kutofautisha—mahali ambapo tisho kwa afya huanzia—haupo kati ya wanywaji wa pombe kidogo na wanywaji wa pombe nyingi bali kati ya wanywaji wa pombe ya kiasi na wale wasiokunywa yoyote,” lasema gazeti la Kijeremani Frankfurter Allgemeine Zeitung.
MATOKEO BAADA YA MVUJO WA CHERNOBYL
Katika Aprili 1986 mlipuko wa Chernobyl wa kiwanda cha nguvu za nyukilia ulitoa vijipande vya redioaktivu juu ya sehemu kubwa ya uso wa dunia. Sasa mipotoko ya maumbile ya kiurithi inatokea katika mimea na wanyama katika ukanda uliochafuliwa kuzunguka kiwanda hicho, yaripoti International Herald Tribune. Kulingana na Tribune, gazeti la Urusi Leninskoye Znamya husema kwamba misunobari yenye ukubwa usio wa kawaida inakua katika eneo hilo, na pia mipopla yenye majani ya upana wa karibu sentimeta 18, ukubwa ulio karibu mara tatu za ule wa kawaida. Kuongezea visa zaidi vya kansa yenye kusababishwa na redioaktivu katika wanadamu, sasa wanasayansi wahofu kwamba kwa sababu ya nusu-maisha marefu (kufikia miaka 33) ya aisotopu fulani zilizoponyoka katika msiba huo, ongezeko la magonjwa ya kurithi, maumbo ya mwili yenye sura mbaya, visa vya kutoka kwa mimba, na vya kuzaa watoto wasiokomaa litasumbua kwa muda wa vizazi vingi vijavyo.
VIJITI HATARI VYA KUCHOKORA MENO
Kila mwaka katika United States, wastani wa majeraha 8,176 yanayohusiana na vijiti vya kuchokora meno huripotiwa, yasema The New York Post. Kwa kielelezo, gazeti hilo lilitaja kisa cha mwanamume wa miaka 28 aliyeuawa na kimoja. Alikuwa ametafuta utibabu kwa ajili ya homa, mizizimo, na kutoka damu. Madaktari walifanya upasuaji wa dharura wakagundua kijiti cha kuchokora meno kilichokuwa kimetoboa mshipa wa tumboni. Mgonjwa alikuwa amemeza hicho kijiti cha kuchokora meno miezi sita mapema na kukisahau. Vijiti vya kuchokora meno vimesababisha vifo kwa kukaba pumzi na kutoboa matumbo ya mgonjwa, au sehemu pana ya kuelekea ukunduni. Madaktari wakazia “uhitaji wa kupata utibabu wa kutosha mara tu baada ya kumeza kitu cha jinsi hiyo.”
TAKATAKA ZA ANGANI
Tangu Sputnik, setilaiti ya kwanza ya Urusi, iliporushwa angani siku ya Oktoba 4, 1957, jumla ya vitu 19,287 vyenye kufanyizwa na mwanadamu vimepelekwa viwe vikipita-pita katika njia za mizunguko yavyo, hasa kuzunguka dunia. NASA (shirika la usimamizi wa vyombo vya kitaifa vya safari za angani) liliripoti kwamba kufikia Juni 30, 1988, kungali kuna 7,184 vilivyobaki. Vingi vyavyo vilikuwa takataka zilizotokana na roketi zilizokwisha kazi. Hata hivyo, gazeti la Uingereza Spaceflight News laripoti kwamba ingawa kungali kuna vyombo 1,777 ambavyo vingali vinazunguka angani, ni asilimia 5 tu kati yazo ambazo zaendelea kufanya kazi.
UVUTANO UNAOFIFIA
Uchunguzi wa maoni ya watu ulipofanywa kwa wanafunzi wa koleji katika United States, karibu asilimia 80 walisema kwamba dini ina sehemu ya maana katika maisha zao, lakini asilimia 69 hawaoni kosa la kufanya ngono kabla ya ndoa. Kulingana na The Atlanta Journal and Constitution, mhariri mmoja wa shirika la utangazaji la Christian Broadcasting Network, ambalo liliagiza uchunguzi huo, alisema hivi: “Sisi tulitamauka kuona kwamba hata ingawa wao huamini katika Mungu, imani yao haionekani kuwa na matokeo mengi juu ya maisha na tabia zao za kibinafsi, maoni na mazoea yao kuhusu ngono.”
MAUZO YA SILAHA
United States na Urusi zinashindana: Nani awezaye kuuza silaha zilizo nyingi zaidi kwenye nchi zinazositawi? Mauzo ya Amerika yalipanda kwa asilimia 66 katika 1988 yakawa dola milioni elfu 9.2, karibu kulingana na kiwango cha Urusi cha dola milioni elfu 9.9—anguko la asilimia 47 katika kipindi kile kile. Yakiwa yote pamoja, yanafanya karibu theluthi mbili za mauzo yote ya silaha kwenye nchi zinazositawi. Zinazofuata ni Ufaransa na China, zote mbili zikipeleka kila mwaka karibu dola milioni elfu 3.1 za silaha kwenye nchi zinazositawi. Mashariki ya Kati imekuwa ndiyo soko kubwa zaidi. Theluthi mbili za silaha zote zilizouzwa katika miaka minne iliyopita zilipelekwa huko.