Kuutazama Ulimwengu
Misiba Siku za Jumatatu
Utafiti uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Flinders katika Australia umefunua kwamba Jumatatu yaonekana kuwa siku ya juma ambayo wanaume wanaelekea zaidi kujiua. Kama ilivyoripotiwa katika The Sydney Morning Herald, watu 19,425 walijiua katika Australia kati ya mwaka 1981 na 1990. Kiwango cha kujiua kwa wanawake kilibaki kikiwa sawa katika muda wote wa juma, lakini miongoni mwa wanaume, kiwango chao kilielekea kupanda sana katika siku za Jumatatu. Kisha kiwango hicho kilipungua polepole kadiri juma lilivyoendelea kupita. Ilitajwa kwamba sababu kubwa ilikuwa ni kurudi kazini. Katika Jumatatu ambazo zilikuwa sikukuu, idadi ya wanaojiua ilikuwa ikipungua, lakini zilipanda tena siku iliyofuata, Jumanne. Uchunguzi mwingine mbalimbali waonyesha kwamba kujiua kwingi hutokea katika pindi za alasiri, wakati ambapo watu huhangaika zaidi na watu wengi sana kupatwa na mafadhaiko mengi. Jumatatu pia ndiyo siku ya kupata maradhi ya moyo zaidi. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kati ya maradhi ya moyo 6,000, asilimia 18 zilitokea katika siku za Jumatatu zikilinganishwa na asilimia 12 katika siku za Jumapili. Watu wengi zaidi hukosa kwenda kazi katika siku za Jumatatu.
Kifua Kikuu Chaongezeka
Kifua-kikuu ni maradhi hatari zaidi ulimwenguni wakati huu, laripoti gazeti la kila siku la Sweden Dagens Nyheter. Katika 1992, zaidi ya watu 3,000,000 walikufa kutokana na maradhi hayo—kushinda kwa mbali wale waliokufa kutokana na UKIMWI, kipindupindu, na malaria. Katika jitihada za kuzuia mweneo wa kifua-kikuu, Shirika la Afya Ulimwenguni hivi karibuni lilikuwa na mkutano katika London. Ilitangazwa kwamba maradhi hayo yalienea sana ulimwenguni, yakikumba vibaya zaidi nchi ambazo hazijaendelea. Lakini yaendelea kusitawi pia katika nchi zilizoendelea kwa sababu ya kuongezeka kwa kusafiri na uhamiaji. Ile aina ya kawaida zaidi ya kifua-kikuu yaweza kutibiwa kwa asilimia 95 ya visa hivyo, lakini ile aina mpya na yenye ukinzani zaidi yaweza kutibiwa kwa asilimia inayopungua 40 ya visa hivyo.
Vifaru Wamo Hatarini
Karibu miaka 20 iliyopita, vifaru wapatao 65,000 walikuwa wakizurura-zurura katika nyanda na misitu ya Afrika. Lakini idadi hiyo imepunguzwa na kuwa 2,500 pekee leo, na wawindaji-haramu ndio wasababishi wakubwa. Katika Zimbabwe pekee idadi ya vifaru imepungua kutoka kuwa zaidi ya 2,000 katika 1990 hadi kuwa chini ya 500. “Hakuna mnyama yeyote mkubwa ulimwenguni anayechinjwa zaidi kwa kadiri hiyo, wala anayeelekea kuangamizwa kwa haraka hivyo [kuliko kifaru],” lasema gazeti Our Planet. Ni nini kinachosababisha machinjo hayo makubwa? Ni pembe za vifaru. Pembe mbili zilizokatwa kutoka kwenye pua ya kifaru zimeuzwa kufikia dola 50,000 (za U.S.) kimagendo. Pembe nyinginezo husagwa kuwa matumizi ya dawa za Mashariki. Pembe nyinginezo hutengenezwa kuwa vishikio maridadi vya jambia. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba pembe za vifaru—namna yake ya kipekee ya kujilinda—zimesababisha waangamizwe.
Muuaji Mkubwa Zaidi wa Kanada
Nchini Kanada, maradhi ya moyo husababisha vifo vya watu wapatao 75,000 kila mwaka. Idadi hiyo “inashinda idadi iliyojumlishwa [ya vifo] vya kansa, UKIMWI, na aksidenti,” chaeleza The Edmonton Journal. Kulingana na Shirika la Moyo na Maradhi ya Ghafula la Kanada, “maisha ya kukaa tu kitako sasa yaonwa kuwa yanahatarisha sana kama vile kuvuta sigareti kunavyohatarisha, msongo mkubwa wa damu na kuwapo kwa kolesteroli nyingi katika damu.” Mazoezi ya kawaida huonwa kuwa njia ya kuzuia maradhi ya moyo. Lakini kama Anthony Graham, ambaye ni mkuu wa mambo ya moyo katika Hospitali ya Wellesley ya Toronto alivyosema, ‘hufikiriwa kwamba mazoezi mazuri ni lazima yatie ndani mazoezi makali.’ Hata hivyo, aliongezea hivi: “Waweza kupata manufaa kidogo-kidogo kwa kufanya mazoezi yasiyo makali zaidi.” Jarida Journal liliripoti kwamba “sayansi imethibitisha manufaa za mazoezi yasiyo makali kama kutembea, kufanya kazi katika bustani ya nyumba, kazi za nyumba na kucheza dansi katika kuzuia maradhi ya moyo.”
Wanawake wa Asia Huishi Muda Mrefu Zaidi
Muda wa kuishi wa wanawake katika Hong Kong umeongezeka kwa utaratibu kuliko miaka 20 iliyopita, kulingana na gazeti China Today. Katika 1971 muda wa kuishi wa wanawake wa Hong Kong ulikuwa miaka 75.3. Katika 1981 muda huo uliongezeka kuwa miaka 78.5. Na katika 1991 ulifika kilele cha miaka 80.6. Lishe bora zaidi na huduma za afya zilizo bora zaidi zasemwa kuwa zilisababisha maendeleo hayo. Kwa ujumla yaonekana kwamba wanawake wa Asia hufurahia kuishi maisha yapitayo muda wa kuishi wa wastani. Wanawake katika Taiwan waweza kutazamia kuishi miaka ipatayo 77. Katika Singapore muda wa kuishi wa wanawake ni karibu miaka 76, na katika Jamhuri ya Watu wa Uchina, ni miaka 71. Gazeti China Today lasema kwamba “Wanawake wa Japani wangali wanaongoza ulimwenguni wakiishi kwa miaka 83.”
Michezo Yenye Jeuri
Michezo mipya yenye jeuri ya vidio inaanza kupendwa zaidi miongoni mwa vijana leo. Kulingana na gazeti Entertainment Weekly, mchezo mmoja watia ndani mandhari ambamo “mwanamke aliyevalia mavazi machache ya kulala ashikwa shingoni ili kuondolewa damu inayofanyizwa kuwa divai.” Katika mchezo mwingine, wachezaji “wapiga watu sana katika shindano la ulimwenguni la mapigano ya barabarani,” lasema gazeti Daily News la New York. Na mchezo mwingine tena wasimuliwa katika Daily News kuwa “wenye kuchukiza sana.” Gazeti hilo laendelea kusema hivi: “Mapigo ya mwili hufuatana na mibubujiko ya damu; mtu mbaya anaposhinda mara nyingi yeye hukata kichwa cha shujaa, na nyakati nyingine hubeba kichwa chake kwa ushindi, huku uti wa mgongo ukiwa ungali unaning’inia. Washiriki wengine wanaoshindwa wanaweza kutundikwa mtini au kuchomwa moto.”
Je! Wana Mizio ya Chakula?
Uchunguzi mmoja wa mizio katika Afrika Kusini ulifunua kwamba miongoni mwa watoto wenye ugonjwa wa pumu ambao walifanyiwa uchunguzi, asilimia 43 “waliathiriwa vibaya sana na dioksidi sulfuri,” laripoti gazeti The Star la Johannesburg. Dioksidi sulfuri hutumiwa sana ikiwa kihifadhi chakula katika Afrika Kusini. Mathalani, sulfiti na dioksidi sulfuri hunyunyizwa kwa mboga na matunda yaliyotoka tu shambani katika hoteli zenye kuandaa saladi na katika baadhi ya maduka ili kuzuia zisigeuke rangi. Sulfiti na dioksidi sulfuri hutumiwa pia katika vyakula vingine, kama vile unga uliokandwa, soda, mvinyo, na pombe. Uchunguzi huo umetokeza msongo mkubwa zaidi wa kuwa na sheria kali zaidi za vibandiko vya chakula.
UKIMWI Katika Japani
Kati ya wakazi milioni 124 wa Japani, watu wanaopungua 3,000 wamepatikana kuwa na virusi ya UKIMWI, kulingana na tarakimu rasmi. “Ingawa hivyo, wengi wa wafanyakazi wa afya wenyewe, baadhi yao wakiwa wameajiriwa na wizara ya afya, waamini kwamba Japani ina watu zaidi wanaougua kuliko idadi ionyeshwayo na tarakimu rasmi,” lasema gazeti The Economist. Mstadi mmoja akadiria idadi halisi kuwa mara kumi kuliko idadi ionyeshwayo rasmi. Gazeti hilo lilionyesha kwamba “zaidi ya nusu ya watu wenye matatizo ya kuvuja damu katika Japani waaminiwa kuwa wenye virusi HIV, na yadaiwa kwamba sababu moja ya hiyo ni kwamba walipewa sehemu fulani ya damu iitwayo Factor 8 iliyokuwa na virusi.” Katika Japani, watu wengi huepuka kuzungumza juu ya fungu la ugoni wa jinsia-moja katika kueneza UKIMWI. Lakini Yuichi Shiokawa, mkuu wa Kamati ya Kuchunguza UKIMWI ya Japani, asema kwamba “ugoni wa jinsia-moja umeenea sana, hasa miongoni mwa makasisi na wanajeshi.”
Wazee-Wazee Wanaotendwa Vibaya
Gazeti la Kanada The Vancouver Sun lilisema karibuni kwamba “watoto na matineja wapaswa kuwa shabaha ya programu zinazokusudiwa kuendeleza hali ya kuthamini wakazi wazee-wazee.” Kwa nini? Kwa sababu inakadiriwa kwamba katika Kanada “zaidi ya watu 315,000 wenye umri zaidi ya miaka 65 hutendwa vibaya kila mwaka,” laripoti gazeti Sun. Laongezea kwamba “wastadi wengi huamini kwamba tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa sababu mara nyingi kutenda wazee-wazee vibaya hufichwa na familia.” Walio wazee-wazee huona ugumu wa kukiri kwamba wanatendwa vibaya kimwili, kiakili, kupuuzwa, na fedha zao na mali yao kutumiwa vibaya. Matumizi mabaya ya fedha na mali na watoto ambao wana idhini ya kisheria ya kutenda kwa niaba ya mzazi katika hali fulani mara nyingi hufanya wazazi wanaozeeka waogope na kuwa shabaha ya kutendwa vibaya.
Ni Uchovu wa Kuendesha Gari?
Kulingana na The Star la Johannesburg, Afrika Kusini, kufikia theluthi moja kati ya magongano ya magari katika nchi hiyo husababishwa na uchovu wa madereva. Hilo laweza kuwa hatari kama vile kuendesha ukiwa mlevi au kuendesha kwa mwendo wa kupita kiasi. Baadhi ya ishara za uchovu wa kuendesha ni macho yenye kuwasha au yaliyo mazito, kuota ndoto za mchana, na kuvuka mistari inayogawanyisha barabara. Hatari ya kuchoka unapoendesha ni kwamba huenda madereva wasitambue hali zao mpaka kuwe kumechelewa mno. Muziki, kahawa, au hewa safi huenda hasa zisirekebishe tatizo hilo. Kwa kweli, kujaribu kupambana na uchovu huenda kukapunguza tu uwezo wa dereva wa kukaza akili. Msemaji wa Usimamizi wa Usalama wa Barabarani ashauri hivi: “Kuna jambo moja tu la kufanya uhisipo umechoka ukiwa unaendesha—pumzika mara hiyo. Ondoa gari kabisa kutoka barabarani ama uiegeshe katika mahali pa mapumziko na kisha uendelee na safari yako baada tu ya kupumzika kabisa.”
Muuaji Katika Chakula
Kila mwaka watu wapatao milioni 80 katika United States huugua kutokana na chakula chenye sumu, kulingana na karatasi ya habari ya Chuo Kikuu cha Tufts. “Tatizo hilo halitambuliwi mara nyingi kwa sababu ishara zalo—baridi, homa, kuchafuka moyo, kiharusi, kuhara, kutapika—zaweza kufanana na zile za homa kali,” ikasema karatasi hiyo ya habari. Katika hali nyinginezo maradhi hayo yenye kutokezwa na chakula huua. Katika United States pekee, karibu watu 9,000 hufa kila mwaka kutokana na chakula chenye sumu. Tufts University Diet & Nutrition Letter yasema kwamba “Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi vimekadiria kwamba asilimia 85 ya ugonjwa wote utokanao na chakula chenye sumu waweza kuepukwa watu wakichukua hatua zifaazo za tahadhari katika makao yao.” Miongoni mwa tahadhari zilizoorodheshwa zilikuwa kuweka vyakula vyote vilivyopikwa baada ya muda wa saa mbili katika friji na kuosha mboga zote na matunda kabla ya kuyala.