Maoni ya Biblia
Uhai Huanza Wakati Gani?
SEPTEMBA 21, 1989, ilikuwa siku isiyo ya kawaida kwa Mahakama ya Tano ya Wilaya ya Tarafa ya Tennessee, U.S.A. Siku hiyo mahakama ndogo ilitoa maoni juu ya ni nani angechukua viinitete saba vya kibinadamu vilivyogandishwa kwa barafu. Mahakama hiyo ilipaswa kuamua ni yupi wa wazazi hao wenye kutalikana aliyekuwa na haki ya kuvichukua. Lakini, kwanza suala jingine lilipasa kusuluhishwa: Je! viinitete vyapasa kuonwa kuwa mali au binadamu?
Profesa Jerome Lejeune wa Paris, mtaalamu wa jenitiki mwenye kujulikana ulimwenguni pote, alitoa ushahidi mbele ya mahakama hiyo kwamba kila binadamu ana mwanzo maalumu, ambao huanza wakati ule mimba inapotungwa na kwamba “mara tu mimba ikiisha kutungwa, mwanadamu ni mwanadamu.” Kwa maneno mengine, kuanzia na ile hatua ya chembe tatu (zygote), viinitete ni “binadamu wadogo mno,” kama alivyoiambia mahakama hiyo.—Italiki ni zetu.
Alipoulizwa kama alikuwa akishuhudia kwamba zygote yapasa kupewa haki zile zile kama mtu mzima, Dakt. Lejeune alijibu hivi: “Mimi siwaambii hivyo kwa sababu sina uwezo wa kujua hilo. Mimi nawaambia, yeye ni binadamu, na kisha Hakimu ndiye atakayewaambia kama binadamu huyo ana haki zile zile kama wengine. . . . Lakini nikiwa mtaalamu wa jenitiki kama mkiniuliza je! binadamu huyo ni mwanadamu, mimi ningewaambia kwamba kwa sababu yeye yupo na akiwa binadamu, yeye ni mwanadamu.”
Kwa kutegemea hasa ushahidi usiokanushika wa Dakt. Lejeune, mitatu kati ya mikataa yenye kutokeza ya mahakama hizo ni hii:
◻ “Kuanzia mrutubisho, chembe za kiinitete cha binadamu hutofautishwa, zikiwa maalumu na za kipekee kwa kiwango cha juu zaidi cha utofautiano.”
◻ “Viinitete vya binadamu si mali.”
◻ “Uhai wa binadamu huanza mimba inapotungwa.”
Je! hilo lakubaliana na yale ambayo Biblia husema juu ya mwanzo wa uhai wa kibinadamu?
Uhai Huanza Mimba Inapotungwa
Yehova Mungu ndiye “chemchemi ya uzima” na “kwa yeye tuna uhai na tunatembea na kuwapo.” (Zaburi 36:9; Matendo 17:28, NW) Muumba asema uhai huanza lini? Yeye huona uhai wa mtoto kuwa wenye thamani hata wakati wa hatua za mapema sana za ukuzi baada ya mimba kutungwa. Miaka zaidi ya 3,000 kabla ya uamuzi huo ulio juu wa mahakama, yeye alipulizia Daudi, nabii wake, aandike hivi:
“Kwa maana wewe mwenyewe ulifanyiza figo zangu; uliendelea kunificha katika tumbo la mama yangu. Nitakusifu wewe kwa sababu kwa njia yenye kutia hofu mimi nimeumbwa kiajabu. Kazi zako ni za ajabu, kama nafsi yangu inavyojua sana. Mifupa yangu hukufichwa wewe wakati mimi niliumbwa kwa siri [ndani ya nyumba ya uzazi], wakati nilifumwa [ufananishi wa vena na ateri, ambazo zimefumwa mwilini mwote kama nyuzi za kitani zenye rangi] katika sehemu za chini za dunia [usimulizi wa kishairi wa giza katika nyumba ya uzazi]. Macho yako yaliona hata kiinitete cha mimi, na katika kitabu chako sehemu zake zote zilikuwa zimewekwa katika mwandiko, kwa habari za siku zile zilipofanywa na bado kulikuwa hakuna moja miongoni mwazo.”—Zaburi 139:13-16, NW.
Kuanzia ile dakika ya mimba kutungwa, uhai unaokua hufuata kiolezo fulani kama kwamba unatii maagizo yaliyoandikwa katika kitabu fulani, kitabu kikubwa mno. “Kiwango cha habari zilizomo ndani ya zygote,” asema Dakt. Lejeune, “kama zingeandikwa na kuwekwa ndani ya kompyuta zingeiambia kompyuta jinsi ya kujua kile kitakachotukia kufuatia, kiwango hicho cha habari ni kikubwa mno hivi kwamba hakuna mtu anayeweza kukipima.”
Uhai wa Asiyezaliwa Ni Wenye Thamani
Kwa hiyo, mtoto ambaye hajazaliwa bado, anayekua ndani ya nyumba ya uzazi ni kitu cha maana zaidi ya kuwa fundo la mnofu. Ana thamani kubwa, na kwa sababu hiyo, Mungu amesema kwamba mtu angetozwa hesabu kwa kujeruhi mtoto ambaye hajazaliwa. Sheria yake kwenye Kutoka 21:22, 23 yaonya hivi: “Watu waume wakiteta pamoja, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi [msiba wenye kuua, NW]; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke; atalipa kama hao waamuzi watakavyosema. Lakini kwamba pana madhara zaidi [msiba wenye kuua, NW], ndipo utatoza uhai kwa uhai.”
Biblia fulani hutafsiri mistari hiyo iliyo juu kwa njia yenye kuonyesha linalompata mwanamke huyo ndilo jambo kuu linaloelekezewa na sheria hiyo. Hata hivyo, maandishi ya awali ya Kiebrania yaelekeza uangalifu kwenye msiba wenye kuua ama kwa mama au kwa mtoto.a Kwa hiyo, kutoa mimba kimakusudi ili kuepuka tu kuzaa mtoto asiyetakwa ni kuua binadamu makusudi.
Watu fulani huenda wakabisha kwamba kiinitete cha kibinadamu si uhai wa kibinadamu kwa sababu hakiwezi kujiendeleza kikiwa nje ya nyumba ya uzazi. Huko ni kufikiri kwa kijuu-juu. Hakuna mtu anayetia shaka kwamba mtoto aliyetoka kuzaliwa—wa umri wa dakika chache tu—kuwa ni binadamu. Hata hivyo, kama mtoto huyo angewekwa akiwa uchi nje kondeni, mtoto huyo angeendelea kuwa hai kwa muda gani? Yeye ni hoi kabisa na, kama vile kiinitete, hana uwezo wa kujiendeleza. Mtoto aliyetoka kuzaliwa ahitaji makao, joto, na chakula—utegemezo, msaada, na usaidizi ambao ni mtu mzima tu, kama vile mama, aweza kutoa.
Kwa hiyo, uamuzi wa kisheria uliotangulia kutajwa wakubaliana na maoni ya Biblia kwamba uhai wa kibinadamu huanza mimba inapotungwa. Uhai wa mtoto ambaye hajazaliwa si jambo dogo la kupuuziwa mbali kimakusudi kuwa kitu cha kigeni chenye kusumbua. Uhai wa kibinadamu ni mtakatifu si baada tu ya kutoka kwenye nyumba ya uzazi bali pia unapokuwa ndani ya nyumba ya uzazi.
[Maelezo ya Chini]
a Nomino “msiba wenye kuua” (Kiebrania ’a·sohnʹ) haihusu moja kwa moja “mwanamke mwenye mimba”; kwa hiyo, msiba wenye kuua hauhusu tu mwanamke huyo bali kwa kufaa ungetia ndani pia “watoto wake” katika nyumba ya uzazi.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Windsor Castle, Royal Library. © 1970 Her Majesty The Queen