Utawala wa Kibinadamu Wapimwa Katika Mizani
Sehemu 4: “Sisi Watu”
Demokrasi: Serikali kupitia watu, inayotawala ama moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa.
“SISI WATU wa United States . . . twafanya uteuzi na kusimamisha Katiba hii.” Maneno hayo ya ufunguzi ya kitangulizi cha Katiba ya U.S. yafaa, kwa kuwa waanzilishi walikusudia United States iwe demokrasi. Neno hili lenye asili ya Kigiriki, “demokrasi” humaanisha “utawala wa watu,” au kama Abraham Linclon, yule rais wa 16 wa United States, alivyolifafanua: “serikali ya watu, kupitia watu, kwa ajili ya watu.”
Ugikiri ya kale, ambayo mara nyingi iliitwa kitovu cha demokrasi, hujivunia kwamba demokrasi ilifuatwa katika mikoa yayo ya majiji, hasa katika Athene, mapema mno katika karne ya tano K.W.K. Lakini demokrasi ya wakati huo haikuwa kama ilivyo leo. Tofauti moja ni kwamba raia Wagiriki walihusika kwa njia ya moja kwa moja zaidi katika utaratibu wa utawala. Kila raia wa kiume alikuwa mshiriki wa baraza fulani lililokutanika mwaka wote ili kuzungumza juu ya matatizo ya karibuni. Lakini ni kwa kura tu ya wengi, kwamba baraza hilo liliamua siasa za mkoa wa jiji, au polis.
Hata hivyo, wanawake, watumwa, na wakazi wa kigeni hawakuhusishwa wafurahie haki za kisiasa. Kwa hivyo, demokrasi ya Athene ilikuwa demokrasi ya namna ya aristocracy (serikali ya masharifu) kwa ajili ya wachache tu wenye kufanikiwa.
Hata hivyo, mpango huo ulihimiza uhuru wa uneni, kwa kuwa raia wenye kupiga kura walipewa haki ya kusema maoni yao kabla ya maamuzi kufanywa. Cheo cha kisiasa kilikuwa wazi kwa kila raia wa kiume, wala hakikuwa kwa ajili ya wachache wenye kufanikiwa. Mfumo wa vizuizi ulibuniwa ili kuzuia watu mmoja mmoja au vikundi visitumie vibaya mamlaka.
“Waathene wenyewe walikuwa wanajivunia demokrasi yao,” asema mwanahistoria D.B. Heater. “Wao waliamini hiyo ilikuwa hatua iliyokaribia maisha kamili na makamilifu zaidi ya utawala wa mtu mmoja au watawala wa masharifu.” Kwa wazi demokrasi ilikuwa imeanzwa vizuri.
Demokrasi Imevuka Kitovu Chayo
Isipokuwa inayozoewa kwa kadiri ndogo katika New England, U.S.A., mikutano ya mji na kwa kadiri ndogo katika tarafa fulani za Uswisi, demokrasi ya moja kwa moja, au isiyochanganywa na kingine chochote haipo tena. Tukifikiria hali kubwa mno ya mataifa ya ki-siku-hizi na mamilioni ya raia zayo, kutawala kwa njia hiyo kungekuwa hakuwezekani kihalisi. Isitoshe, ni raia wangapi katika ulimwengu wenye shughuli mno wa leo wangekuwa na wakati unaotakwa ili wajitoe kwa saa nyingi za mjadala wa kisiasa?
Demokrasi imekua ikapevuka kuwa yenye ubishi—yenye nyuso kadha wa kadha. Kama gazeti Time lilivyoeleza: “Haiwezekani kugawanya ulimwengu kuwa makundi yaliyo tofauti kabisa ya demokrasi na yasiyo ya demokrasi. Ndani ya zile ziitwazo demokrasi, kuna hatua mbalimbali za uhuru wa mtu binafsi, vyama vingi na haki za kibinadamu, kama vile kulivyo viwango vyenye kutofautiana vya ugandamizaji katika tawala za kiimla.” Hata hivyo, watu walio wengi hutazamia kuona mambo fulani ya msingi katika serikali za kidemokrasi, mambo kama vile uhuru wa kibinafsi, usawa, heshima kwa haki za kibinadamu, na haki kupitia sheria.
Demokrasi ya moja kwa moja ya wakati uliopita imekuwa demokrasi ya wawakilishi iliyopo wakati huu. Mabaraza ya kutunga sheria, ama yenye halmashauri moja, au yenye mbili, yana washiriki mmoja mmoja waliochaguliwa na watu—au wakateuliwa kwa njia nyingine—wawawakilishe na kufanyiza sheria, zinazodhaniwa ni kwa faida yao.
Mtindo huo wa kuelekea demokrasi za kuwakilishwa ulianza katika Enzi za Kati. Kufikia karne za 17 na 18, matengenezo ya karne ya 13, kama vile Magna Charta na Bunge katika Uingereza, pamoja na mawazo ya kisiasa juu ya usawa wa watu, yalikuwa yakifikia kuwa na maana kubwa zaidi.
Kufikia nusu ya pili ya karne ya 18, usemi “demokrasi” ulikuwa umeanza kutumiwa kwa ujumla, ingawa ulitiliwa shaka na wengine. The New Encyclopædia Britannica chasema hivi: “Hata watungaji wa Katiba ya United States katika 1787 walikuwa na wasiwasi juu ya kuhusisha watu kwa ujumla katika utaratibu huo wa kisiasa. Mmoja wao, Elbridge Gerry, aliiita demokrasi ‘uovu wa kisiasa ulio mbaya zaidi ya wote.’” Kwa hiyo, watu kama Mwingereza John Locke waliendelea kubisha kwamba serikali yategemea ukubali wa watu, ambayo haki zao za asili hazipasi kuvunjwa.
Jamhuri
Demokrasi nyingi ni jamhuri, yaani hiyo ni kusema serikali zenye kiongozi wa taifa asiye mfalme, kwa kawaida sasa akiwa ni rais. Mojawapo jamhuri za kwanza za ulimwengu ilikuwa Roma ya kale, ijapokuwa kwa kweli demokrasi yayo ilikuwa yenye mipaka. Hata hivyo, jamhuri hiyo ambayo kwa sehemu ilikuwa demokrasi iliendelea kwa miaka zaidi ya 400 kabla ya kuachia nafasi utawala wa wafalme (mornachy) na Milki ya Roma.
Wakati huu jamhuri ndizo zilizo aina ya serikali inayopendwa zaidi sana na wengi. Kati ya zile serikali na matengenezo ya kimataifa 219 yaliyoorodheshwa katika kitabu cha marejezo cha 1989, 127 zaorodheshwa kuwa jamhuri, ijapokuwa si zote zilizo demokrasi za wawakilishi. Kwa kweli, kuna namna nyingi sana za serikali za jamhuri.
Jamhuri fulani ni mifumo inayoongozwa na serikali moja kuu yenye nguvu. Nyingine ni mifumo ya federal, ikimaanisha kwamba kuna mgawanyo wa kuongoza kati ya viwango viwili vya serikali. Kama inavyoonyeshwa na jina layo, United States ya Amerika ina aina hiyo ya mwisho ya mfumo unaojulikana kuwa federalism. Serikali ya kitaifa hutunza masilahi ya taifa lote kwa ujumla, ambapo serikali za mkoa hushughulika na mahitaji ya mitaa. Bila shaka, katika ujumla huo, kuna utofautiano-tofautiano mwingi.
Jamhuri fulani hufanya uchaguzi unaohusisha wote. Raia zazo waweza pia kupewa wingi wa vyama vya kisiasa na wingi wa wagombea uchaguzi wa kuchagua kati yao. Jamhuri nyingine huona uchaguzi wenye kuhusisha wote kuwa si wa lazima, zikibisha kwamba takwa la kidemokrasi la watu laweza kutekelezwa kwa njia nyinginezo, kama vile kuhimiza uenyeji wa kijamaa wa uzalishaji. Ugikiri ya kale ni kitangulizi, kwa kuwa uchaguzi wa kuhusisha wote haukuwako huko. Wasimamizi walichaguliwa kwa kura na kwa ujumla waliruhusiwa kutumikia kwa vipindi vya mwaka mmoja au miwili. Aristotle alipinga uchaguzi, akisema kwamba ulitokeza kile kiasili cha aristocracy cha kuteua “watu bora zaidi.” Hata hivyo, demokrasi ilipaswa kuwa serikali ya watu wote, si ya “walio bora” tu.
Ni Bora Zaidi Kwa Kulinganisha Tu?
Hata katika Athene ya kale, utawala wa kidemokrasi ulileta ubishi. Plato alikuwa na shaka. Utawala wa kidemokrasi ulionwa kuwa dhaifu kwa sababu ulikuwa mikononi mwa watu mmoja mmoja wasio na maarifa ambao wangeweza kupotoshwa na maneno yenye kusisimua ya watawala wachochezi. Socrates alidokeza kwamba demokrasi ilikuwa tu utawala wa kundi la watu wenye fujo. Na Aristotle, wa tatu wa wanafalsafa Wagiriki hao watatu waliokuwa maarufu, alibisha, chasema kitabu A History of Political Theory, kwamba “kwa kadiri ambavyo demokrasi inavyokuwa ya kidemokrasi, ndivyo inavyoelekea kutawalwa na kundi lenye fujo, . . . ikizorota kuwa utawala wa mabavu.”
Wengine wameonyesha shaka hizo. Jawaharlal Nehru, aliyekuwa zamani waziri mkuu wa India, aliita demokrasi kuwa njema, lakini akaongeza maneno haya yenye kufafanua: “Nasema hivyo kwa sababu mifumo mingine ni mibaya zaidi.” Na William Ralph Inge, kasisi na mwandishi Mwingereza, aliandika hivi wakati mmoja: “Demokrasi ni namna ya serikali ambayo kwa usawaziko yaweza kutetewa, kuwa si ni nzuri, bali kuwa si mbaya sana kama nyinginezo.”
Demokrasi ina udhaifu mbalimbali. Kwanza, ili ifanikiwe, watu mmoja mmoja lazima wawe na nia ya kutanguliza faida za walio wengi mbele ya masilahi yao. Huenda hilo likamaanisha kutegemeza hatua za kodi au sheria nyingine ambazo huenda zikawa hazikubaliki kibinafsi lakini zilizo za lazima kwa ajili ya wema wa taifa lote. Ni vigumu kuona upendezi huo usio na ubinafsi, hata katika mataifa ya kidemokrasi yaliyo ya “Kikristo.”
Udhaifu mwingine ulionwa na Plato. Kulingana na A History of Political Theory, yeye alishambulia “ukosefu wa maarifa na kutostahili kwa wanasiasa, ambako ni laana ya pekee ya demokrasi.” Wanasiasa wengi wenye ujuzi hujuta juu ya tatizo la kupata watu wanaostahili na wenye kipawa watumikie katika serikali. Hata maofisa waliochaguliwa waweza kuwa ni wanagenzi (wanafunzi) tu wa kisiasa. Na katika kipindi hiki cha televisheni, sura nzuri au haiba ya mgombea uchaguzi yaweza kumshindia kura ambazo uwezo wake wa usimamizi usingeweza kamwe.
Jambo jingine lisilofaa lililo wazi kuhusu demokrasi ni kwamba hizo husonga polepole. Mtawala wa imla hunena, na mambo hutendeka! Mwendo wa maendeleo katika demokrasi waweza kupunguzwa na mijadala isiyo na mwisho. Bila shaka, kuzungumza kikamilifu masuala yenye ubishi kuna faida zilizo wazi. Lakini, kama Clement Attlee, aliyekuwa zamani waziri mkuu wa Uingereza, alivyoonelea wakati mmoja: “Demokrasi humaanisha serikali kwa njia ya mazungumzo lakini huwa yenye matokeo wakati tu unapoweza kusimamisha watu wasiongee.”
Hata baada ya maongezi kusimamishwa, kadiri ambayo maamuzi hayo yanawakilisha kikweli yale ambayo “watu” wanataka ni jambo la kubishaniwa. Je! wawakilishi hupigia kura masadikisho ya wengi ambao wanawawakilisha au, mara nyingi, ni yale yao wenyewe? Au je! wao huidhinisha tu mwongozo rasmi wa chama chao?
Kanuni ya kidemokrasi ya kuwa na mfumo wa vikwazo na vizuizi ili kuzuia ufisadi huonwa kuwa wazo zuri lakini haufanikiwi sana. Gazeti Time la 1989 lilinena juu ya “ufisadi wa kiserikali katika viwango vyote,” likiita serikali moja ya kidemokrasi yenye kuongoza kuwa “jitu lililonona, lisilotimiza lolote, lililo hoi.” Mwenyekiti wa tume ya uchunguzi iliyowekwa katika miaka ya katikati ya 1980 kuchunguza ufujaji (utumizi mbaya wa mali) katika serikali nyingine alisukumwa kusema hivi kwa huzuni: “Serikali inaendeshwa vibaya sana.”
Kwa ajili ya sababu hizo na nyingine nyingi, demokrasi haziwezi kuwa serikali yenye kufaa. Kweli ya wazi, kama ilivyotajwa na John Dryden, mshairi wa karne ya 17, ni kwamba “walio wengi waweza kukosea sana kama vile walio wachache.” Henry Miller, mwandikaji Mwamerika, alitoboa mambo, lakini kwa usahihi, aliposema hivi: “Vipofu wanaongoza vipofu. Hiyo ndiyo njia ya kidemokrasi.”
Yaelekea Mwisho Wayo?
Utawala wa kidemokrasi umekubalika zaidi katika karne hii kuliko katika wakati mwingine wowote uliotangulia. Misukosuko ya hivi majuzi katika Ulaya ya Mashariki yathibitisha hilo. Hata hivyo, “demokrasi yenye kutoa uhuru mkubwa imo matatani makubwa sasa katika ulimwengu,” aliandika mwandikaji wa magazeti James Reston miaka kadhaa iliyopita. Daniel Moyniham alionya kwamba “demokrasi yenye kutoa uhuru mkubwa si mwongozo wa kisiasa ulio bora” na kwamba “yaelekea demokrasi zinakwisha.” Mwanahistoria Mwingereza Alexander Tyler alisema kwamba serikali ya kidemokrasi haiwezi kudumu kwa wakati usiojulikana kwa sababu “sikuzote huangushwa na mwongozo wa matumizi ya fedha ya kupita kiasi.” Bila shaka, maoni yake ni yenye kubishaniwa.
Kwa vyovyote, demokrasi ni mwendelezo ulio wazi wa mtindo ulioanza katika Edeni, wakati binadamu walipoamua kufanya mambo kivyao, kuliko kuyafanya katika njia ya Mungu. Hiyo ndiyo upeo wa utawala wa binadamu, kwa kuwa hujitahidi kuhusisha kila mmoja, angalau kama inavyowaziwa, katika utaratibu wa kutawala. Lakini ule usemi wa Kilatini Vox populi, vox Dei, “sauti ya watu ndiyo sauti ya Mungu,” si kweli. Kwa hiyo, wale wanaounga mkono utawala wa kidemokrasi wa binadamu lazima wawe tayari kushiriki malawama kwa ajili ya matendo yao.—Linganisha 1 Timotheo 5:22.
Uhakika huo umekuwa na maana kubwa zaidi tangu 1914. Katika mwaka huo wenye matukio makubwa, utawala wa kimungu ulianza kutenda katika njia ya ajabu. Ufalme wa Mungu wa Kimesiya sasa umesimama tayari kutwaa uongozi kamili wa mambo ya ulimwengu. Namna zote za utawala wa kibinadamu—kutia ndani namna za kidemokrasi—zinapimwa katika mizani. Kwa kadiri ambayo sisi mmoja mmoja tunazitetea, ndivyo tunavyopimwa pamoja nazo.—Danieli 2:44; Ufunuo 19:11-21.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
“Kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.”—Yeremia 10:23
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Wale wanaotegemeza utawala wa kidemokrasi wa binadamu lazima wawe tayari kushiriki malawama kwa ajili ya matendo yao
[Picha katika ukurasa wa 23]
“Kuna njia ionekanayo kuwa nyoofu kwa mwanadamu, lakini mwishoni hiyo huongoza kwenye kifo.”—Mithali 14:12, “New International Version”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]
U.S. National Archives photo