Watoto—Ni Faida au Ni Hasara?
SUALA la kupanga uzazi mara nyingi linahusianishwa kwa ukaribu na ukuzi wa kasi sana wa idadi ya watu. Muda mwingi wa historia ya ainabinadamu, ukuzi wa idadi ya watu ulikuwa wa polepole kwa kulinganisha; idadi ya waliokuwa wakifa ilikuwa karibu sawa na idadi ya waliokuwa wakizaliwa. Hatimaye, wapata mwaka 1830, idadi ya watu wa ulimwengu ikafika watu bilioni moja.
Ndipo yakaja maendeleo ya kitiba na ya kisayansi yaliyopunguza vifo kutokana na maradhi, hasa maradhi ya utotoni. Kufikia wapata 1930, idadi ya watu wa ulimwengu ikawa watu bilioni mbili. Kufikia 1960, bilioni nyingine moja ikawa imeongezwa. Kufikia 1975, bilioni nyingine moja. Kufikia 1987, idadi ya watu wa ulimwengu ikafikia bilioni tano.
Kutazama hali hiyo kwa njia nyingine, idadi ya watu duniani kwa wakati wa sasa inaongezeka kwa watu wapata 170 kila dakika. Hiyo hujumlika kuwa watu wapatao 250,000 kila siku, wa kutosha jiji moja kubwa. Vilevile, hiyo yamaanisha kwamba kila mwaka huleta ongezeko la idadi ya watu zaidi ya milioni 90, sawa na mara tatu za idadi ya watu wa Kanada au sawa na idadi ya watu wa Meksiko. Zaidi ya asilimia 90 ya ukuzi huo inatukia katika nchi zinazositawi, ambako tayari asilimia 75 ya idadi ya watu wa ulimwengu huishi.
Serikali Zenye Kuhangaika
Lakini kwa nini serikali zinataka kupunguza ukuzi wa idadi ya watu kupitia njia ya kupanga uzazi? Dakt. Babs Sagoe, Ofisa wa Programu ya Taifa kwa ajili ya Hazina ya Idadi ya Watu ya UM, ajibu swali hilo kwa kutumia kielezi rahisi ambacho, yeye hutahadharisha kwamba chaelekea kurahisisha mno hali ngumu na yenye kubishaniwa. Yeye aeleza hivi:
‘Tuseme mkulima ana hekta 4 za ardhi. Ikiwa ana watoto kumi na agawanya ardhi hiyo sawasawa miongoni mwao, kila mtoto atakuwa na nusu hekta. Ikiwa kila mmoja wa watoto hao ana watoto kumi na agawanya ardhi hiyo hivyohivyo, kila mmoja wa watoto wao atakuwa na hekta 0.04. Kwa wazi, watoto hao hawatakuwa nafuu kama babu yao, aliyekuwa na hekta 4 za ardhi.’
Kielezi hicho chakazia uhusiano uliopo kati ya idadi ya watu yenye kukua na dunia ambayo maliasili yayo ina kikomo. Kadiri idadi ya watu inavyokua, nchi nyingi zinazositawi hujitahidi kuwezana na idadi ya watu ya sasa. Fikiria baadhi ya matatizo.
Maliasili. Kadiri idadi ya watu inavyoongezeka, misitu, udongo wenye rutuba, ardhi ya mazao, na maji safi hutumiwa zaidi. Matokeo ni nini? Gazeti Populi laomboleza hivi: “Nchi zinazositawi . . . mara nyingi hushurutishwa kutumia kupita kiasi maliasili ya taifa ambayo ukuzi wa wakati ujao waitegemea.”
Muundo wa msingi. Kadiri idadi ya watu ikuavyo, serikali huona ugumu unaozidi kuandaa makao, shule, vifaa vya usafi, barabara, na utumishi wa afya wa kutosha. Zikiwa zinalemewa na mzigo maradufu wa deni kubwa na maliasili inayopungua, mataifa yanayositawi yanasongwa sana katika kutunza mahitaji ya idadi hata ya sasa, achia mbali idadi kubwa zaidi.
Kazi za kuajiliwa. Kichapo Population and the Environment: The Challenges Ahead cha Hazina ya Idadi ya Watu ya UM chataarifu kwamba katika nchi nyingi zinazositawi, tayari asilimia 40 ya watu wanaoweza kufanya kazi hawana kazi. Kotekote katika nchi zinazositawi, zaidi ya watu nusu bilioni ama hawana kazi ama wana kazi isiyotosha, tarakimu inayokaribia kuwa sawa na wafanyakazi wote katika mataifa ya ulimwengu yenye usitawi wa viwanda.
Ili kuzuia mwendo huu usiwe mbaya zaidi, nchi zinazositawi lazima zitokeze zaidi ya nafasi za kazi milioni 30, kila mwaka. Watu ambao watahitaji kazi hizo wako hai leo—ni watoto wa leo. Wastadi hukisia kwamba ukosefu mkubwa mno wa kazi za kuajiriwa huenda ukaongoza kwenye fujo ya kiraia, umaskini unaozidi kuwa mbaya, na uharibifu zaidi wa maliasili.
Si ajabu kwamba mataifa yanayositawi ambayo yanazidi kuongezeka yanajitahidi kuendeleza njia za kupanga uzazi. Ikitoa elezo juu ya kilicho mbele, tahariri moja ya Lancet jarida la kitiba la Uingereza lilitaarifu hivi: “Msongo wa ongezeko [la idadi ya watu], sana-sana ukiwa katika nchi maskini zaidi za ulimwengu, huongeza mno jukumu zinalokabili. . . . Mamilioni watatumia maisha zao bila kuelimishwa, bila kuajiriwa kazi, bila makao ya kutosha na bila kupata utumishi mbalimbali wa afya ya msingi, wa misaada ya umma na wa usafi, na ongezeko lisilozuiwa la idadi ya watu ni kisababishi kikubwa cha tatizo hilo.”
Familia Zenye Kuhangaika
Ni rahisi kuweka miradi na kuanzisha programu za kupanga uzazi katika taifa zima lakini ni vigumu kusadikisha umma. Katika jamii nyingi maoni ya kimapokeo yenye kupendelea familia kubwa yangali yenye nguvu. Kwa mfano, mama mmoja Mnaijeria aliitikia kitia-moyo cha serikali yake cha kupunguza uzazi kwa kusema: “Mimi ni wa mwisho kati ya watoto 26 wa baba yangu. Wakubwa wangu wote, kutia wa kiume na wa kike, wana watoto kati ya 8 na 12. Hivyo, je, ni mimi nitakuwa na watoto wachache?”
Hata hivyo, maoni hayo si ya kawaida sana kama yalivyokuwa wakati mmoja, hata katika Naijeria, ambako mwanamke wa wastani huzaa watoto sita. Wakikabiliwa na bei zenye kupanda, mamilioni ya watu wanasongwa sana katika kulisha kuvisha familia zao. Wengi wamejifunza kupitia mambo yaliyowapata ukweli wa mithali ya Kiyoruba: “Ọmọ bẹẹrẹ, òsì bẹẹrẹ (wingi wa watoto, ni wingi wa umaskini).
Waume na wake wengi wanaelewa manufaa za kupanga uzazi, hata hivyo hawapangi uzazi. Matokeo ni nini? Kichapo The State of World’s Children 1992, ambacho huchapishwa na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, kilisema kwamba karibu mimba 1 kati ya 3 katika nchi zinazositawi mwakani haingekuwa tu isiyopangwa bali pia isiyotakwa.
Kupanga Uzazi Huokoa Maisha
Kando na magumu ya kiuchumi, sababu kubwa ya kufikiria kupanga uzazi ni afya ya mama na watoto wake. “Mimba ni mchezo wa kamari na kuzaa ni mng’ang’anio wa kufa na kupona,” yasema mithali moja ya Afrika Magharibi. Kila mwaka katika nchi zinazositawi, wanawake nusu milioni hufa wakati wa mimba au wa kuzaa, watoto milioni moja huachwa bila mama, na wanawake wengine milioni tano hadi milioni saba hulemazwa au kuwa viwete kutokana na madhara ya kiafya yanayohusiana na uzazi.
Si wanawake wote katika nchi zinazositawi ambao huhatirishwa kadiri hiyohiyo. Kama vile kisanduku kinachoambatana kionyeshavyo, wale walio hatarini ni wanawake ambao huzaa watoto wengi mno mapema mno, mara nyingi mno, au kwa kuchelewa mno. Vyanzo vya UM hukadiria kwamba kupanga uzazi kungeweza kuzuia kuanzia robo moja hadi theluthi moja ya vifo hivyo na kungeweza kuzuia mamilioni ya visa vya ulemavu.
Lakini je, kuokoa mamilioni ya maisha hakungetumikia tu kuongeza ukuzi wa idadi ya watu? Kwa kushangaza, wastadi wengi husema la. “Ingedhaniwa,” chataarifu kichapo Human Development Report 1991, “kwamba, watoto zaidi wakiokoka, matatizo ya idadi ya watu yangekuwa mabaya zaidi. Kinyume kabisa. Kima cha uzazi huelekea kushuka wazazi wanapokuwa na uhakika zaidi kwamba watoto wao wataokoka.”
Hata hivyo, mamilioni ya wanawake, hasa katika jamii maskini, huendelea kuzaa mara nyingi. Kwa nini? Kwa sababu jamii yao hutarajia hilo kutoka kwao, kwa sababu kuwa na watoto wengi huongeza uwezekano kwamba baadhi yao wataokoka, na kwa sababu huenda wasijue juu ya au wasiweze kupata utumishi mbalimbali wa kupanga uzazi.
Hata hivyo, wanawake wengi walio na familia kubwa hawangetaka iwe vingine. Wao humuona kila mtoto kuwa baraka kutoka kwa Mungu.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Mimba Zenye Hatari Kubwa Katika Nchi Zinazositawi
Mapema Mno: Hatari ya kifo wakati wa mimba na wa uzazi miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19 ni kufikia mara tatu juu zaidi ya miongoni mwa wanawake wa kuanzia umri wa miaka 20 hadi 24. Watoto wanaozaliwa na wanawake matineja wana uelekeo zaidi wa kufa, kuzaliwa mapema mno, au kuwa na uzito mdogo mno wakati wa kuzaliwa.
Karibu-Karibu Mno: Urefu wa pindi kati ya uzazi huathiri sana hali ya kuokoka kwa mtoto. Mtoto anayezaliwa chini ya miaka miwili baada ya mtoto aliyetangulia wa mama huwa na mwelekeo mkubwa zaidi wa asilimia 66 wa kufa wakati wa utotoni. Watoto hao wakiokoka, ukuzi wao utaelekea zaidi kudumaa na ukuzi wao wa akili uelekee zaidi kupungukiwa. Chapata kifo 1 kati ya vifo 5 vya watoto kingeweza kuzuiwa kupitia uzazi uliotenganishwa ifaavyo. Vipindi vya miaka mitatu au zaidi kati ya uzazi huwa na hatari ndogo zaidi.
Wengi Mno: Kuzaa watoto zaidi ya wanne huongeza hatari za mimba na uzazi, hasa ikiwa watoto waliotangulia hawakutenganishwa kwa zaidi ya miaka miwili. Baada ya mimba nne, akina mama huelekea zaidi kupatwa na ukosefu wa damu na kuelekea zaidi kuvuja damu, na watoto wao huwa katika hatari kubwa zaidi ya kuzaliwa wakiwa na ulemavu mbalimbali.
Kwa Kuchelewa Mno: Wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 35 wana uelekeo mara tano wa kufa wakati wa mimba au uzazi zaidi ya wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 20 hadi 24. Watoto wanaozaliwa na wanawake wenye umri mkubwa zaidi wana uelekeo zaidi wa kufa.
Vyanzo: Shirika la Afya Ulimwenguni, Hazina ya Watoto ya UM, na Hazina ya Idadi ya Watu ya UM.