Walsingham—Patakatifu pa Uingereza Penye Kubishaniwa
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
WALSINGHAM, kijiji cha kuvutia katika Kata ya Norfolk, Uingereza, hupokea kufikia wasafiri wa kidini 100,000 wazuruo sehemu takatifu za Bibi Mheshimiwa Wetu wa Walsingham.[3] Sehemu moja hudhaminiwa na Wakatoliki wa Roma, na ile nyingine hudhaminiwa na Kanisa la Uingereza. Hiyo imetokeza hali ya kubishaniwa.
“Usafiri wa Kidini Taifani wa Kwenda Walsingham umekuwa tukio lenye maumivu katika miaka ya hivi majuzi,” ndivyo alivyoandika kasisi mmoja wa Kanisa la Uingereza katika Church Times. “Andamano la wasafiri wa kidini . . . hukabiliwa na makelele ya hasira ya . . . umati wenye kuzidi kuwa mkubwa wa wateti waliojiandaa vyema.”[1]
Kwa nini watete? “Kile kinachofanywa hapa kwa jina la Ukristo ni upagani mtupu,” wakapiga mbiu wateti hao dhidi ya patakatifu pa Kanisa la Uingereza, “kuiaibisha Kweli waziwazi, chukizo kubwa machoni pa Mungu na kutusi vibaya kabisa urithi wetu wa kiprotestanti.”[2]
Katika Uingereza, ni mara chache dini iamshapo hasira za jinsi hiyo. Kuna nini kule Walsingham cha kuchochea hisia kali jinsi hiyo? Pitio la historia ya sehemu takatifu hiyo litakusaidia kuelewa.
Kabiliano Baina ya Uprotestanti na Ukatoliki
Kabla ya yale Marekebisho ya Kidini ya karne ya 16, Uingereza ilikuwa ya Katoliki ya Roma na ilijivunia kuwa na sehemu nyingi takatifu.[5] Kati ya sehemu zilizo za zamani zaidi ilikuwako Walsingham, ambayo ndiyo sehemu kuu takatifu ya Bikira Maria katika nchi hiyo.[6] Ilianza katika mwaka 1061 wakati bibi mheshimiwa wa kikabaila alipojenga nyumba katika kijiji hicho. Kulingana na ngano ya mapokeo, maelezo marefu juu ya kujengwa kwacho yalitolewa katika njozi, kwa sababu mahali hapo palisemekana kuwa kifanano halisi cha ile nyumba katika Nazareti ambamo Maria, mama ya Yesu, alikuwa ameishi.[7] Katika zile Enzi za Kati, mahali hapa palipofanywa patakatifu kwa ajili ya Maria palipata umaana wa kimataifa na kupendwa na watu wengi zaidi.[8]
Wafalme na akina yahe pia walimiminika Walsingham.[8a] Ni nini kilichowavutia? Mbali na ule mfano wa mbao wa Maria akiwa na kitoto kichanga Yesu juu ya goti lake, masamaha na masalio yalipatikana kwa urahisi kwa kuuzwa, na magonjwa yaliripotiwa kuwa yaliponywa huko.[9] Wasafiri wa kidini wangeweza pia kuuangalia “muujiza” wa Walsingham, kichupa kilichosifika kuwa na matone machache yaliyoganda ya maziwa ya Maria. Wageni fulani walisadiki kwamba ni chokaa tu au risasi nyeupe iliyokuwa katika kichupa hicho,[10] hali Erasmus, yule mwanachuo wa Biblia, alitia shaka juu ya uasilia wa salio hilo, ambalo watu fulani waliliona kuwa kama chokaa iliyopondwapondwa kwa kuchanganywa na ute wa yai.[11]
Kwa nini mwanamarekebisho maarufu kama Erasmus akafunga safari ya kidini kwenda Walsingham? Labda ilikuwa ni kutimiza nadhiri fulani. Ingawa alieleza kwa marefu juu ya mahali hapo patakatifu, “maneno yake ya kudhihaki sherehe zote za kidini ni makali ajabu,” yasema The Catholic Encyclopedia.[12] Erasmus aliandika “kwa hali ya akili ya kudhihaki na kutoamini,” aeleza mwanahistoria Frederic Seebohm, akiongezea kwamba hakuna uthibitisho wa “kwamba yeye mwenyewe alimwabudu Bikira au aliamini kuna faida ya kufunga safari za kidini kwenda mahali pake patakatifu.”[13]
Wakati wa yale Marekebisho ya Kidini lile Kanisa la Uingereza lililokuwa limetoka sasa tu kuundwa liliuzulu dini ya Katoliki ya Roma. Katika mwaka 1538, hapo mahali patakatifu pa yule “Mchawi wa Kike wa Walsingham,”[14] kama alivyokuwa amekuja kujulikana, paliharibiwa kwa agizo la Mfalme Henry 8, kichwa cha kanisa hilo lililovunja uhusiano, na uwanja ukauzwa.[15] Ile sanamu, ikiwa ni mfano wenye kuchukiwa wa ibada ya sanamu, ilipelekwa kilometa mia moja sitini hadi Chelsea katika London na kuchomwa huko hadharani.[16]
Waprotestanti Waiga Wakatoliki
Hata hivyo, mapema katika karne hii Kanisa la Uingereza lilirudisha Bibi Mheshimiwa Wetu wa Walsingham—kuwa mahali patakatifu pa Kiprotestanti! Katika 1921 salio lililochongwa la ile sanamu ya awali lilisimamishwa katika kanisa la eneo la Walsingham, na wasafiri wa kidini wa kwanza wa ki-siku-hizi wakawasili mwaka mmoja baadaye.[17] Kwa kadiri ambavyo mahali hapo patakatifu pamezidi kuwa maarufu, ndivyo pia hasira ya washiriki fulani wa kanisa imeongezeka. Katika Mei wa kila mwaka, wakati ile sanamu ibebwapo kupitishwa katika barabara za mji wakati wa andamano la dakika 30, wao huteta kwa kupinga vikali hiyo ibada ya sanamu.[18]
Katika 1934, Wakatoliki wa Roma walisimamisha katika Walsingham Sanamu Takatifu ya Kitaifa yao ya Bibi Mheshimiwa Wetu. Sanamu hii takatifu ni chapa ya pili ya ile sanamu ya awali ya mama na mtoto nayo iko katika kile Kikanisa cha Slipper cha zamani. Hapa ndipo mahali ambapo wasafiri wa kidini walikuwa wakiacha viatu vyao kutembea miguu mitupu hadi ile sanamu ya awali ya kijijini.[19] Kwa kupendeza, wale wateti wanateta juu ya Kanisa la Uingereza tu, ambalo wanashikilia kwamba linaendeleza ibada ya Maria na kuukataa kabisa urithi wa Uprotestanti ambao kanisa limepata.[19a]
Lakini je, kuna sababu nyingine ya upinzani mkali wa wateti hao? Wengi huamini kunayo. Hayo “mateto yamezidi hivi majuzi kuwa yenye hofu juu ya wagoni-jinsia-moja,” laripoti gazeti The Independent, “yakielekezwa hasa kwa wagoni-jinsia-moja.”[20] Hii yarejezea kikundi cha wanaume wa Kanisa la Uingereza, sana-sana makasisi, ambao kwa muda wa miaka michache iliyopita wamekuwa wakienda Walsingham mahali pa kukusanyikia kila mwaka. [21] Kwa nini wao huja? Msafiri wa kidini aliye wa kawaida alieleza hivi: “Hili si tukio la watu kuzoea ngono za kawaida.”[22]
Ni wazi kwamba tukio ambalo limetia mizizi katika ibada ya sanamu kwa kadiri hiyo na ambalo sasa linahusika kwa njia fulani na ugoni-jinsia-moja, lapasa kuepukwa na Wakristo wa kweli.—1 Wakorintho 6:9; 10:14; 1 Yohana 5:21.