Wale Mapilgrimu na Kupigania Kwao Uhuru
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UHOLANZI
MNAMO 1620, kikundi kimoja cha Wapiuriti (Puritans) Waingereza ambacho kilikuwa kimeabiri kutoka Delfshaven, karibu na Rotterdam, Uholanzi, kilianzisha makao ya kwanza ya kudumu ya watu wa Ulaya katika New England—ile Koloni ya Plymouth—ambayo sasa ni sehemu ya kusini-mashariki mwa Massachusetts. Ni nini kilichowafanya watu hawa wenye kufuatia dini sana kujihatarisha katika safari ndefu ngumu kuvuka Bahari-Kuu ya Atlantiki iliyo hatari katika meli ndogo iitwayo Mayflower? Na walikuwa wakifanya nini Uholanzi? Kwa nini walitoka huko?
Hali ya Kidini Katika Uingereza
Katika miaka ya 1500, Kanisa la Katoliki ya Kiroma lilidhoofishwa na Warekebishaji. Makanisa ya Kiprotestanti yakaja kuwapo kotekote Ulaya, kutia ndani na Uingereza. Katika kisa cha Uingereza, mgawanyiko wa mwisho na Roma ulitokea baada ya papa kukataa ombi la Mfalme Henry 8 la kutaka ndoa yake ya kwanza ivunjwe. Kanisa la Uingereza likajitenganisha na Roma, na katika 1534 Bunge la Uingereza likamtambua rasmi Henry kuwa “Mkuu Kuliko Wote wa Kanisa la Uingereza hapa duniani, akiwa wa pili tu kwa Mungu.” Bintiye Elizabeth, aliyezaliwa 1533, alilelewa akiwa Mprotestanti, na baada ya kuwa Malkia Elizabeth 1, alifanya Kanisa la Kianglikana kuwa la Kiprotestanti kwelikweli. Hata hivyo, kulikuwa na vikundi vidogo vya Kiprotestanti ambavyo havikukubaliana na Kanisa la Kianglikana lililo kuu. Vingi vya vikundi hivyo vikaja kuitwa Wapiuriti kwa sababu wao walitaka kutakasa Kanisa la Kianglikana kutokana na masalio yoyote ya Ukatoliki wa Roma. Kikundi kimoja cha Kipiuriti kilionwa kuwa chenye ubishi kwelikweli, kwa kuwa kilikataa kanisa lisisimamiwe na maaskofu na makasisi. Wao waliona kutaniko lao kuwa huru kabisa, likitawalwa na wazee wao wenyewe.
Malkia Elizabeth alihofu kwamba angeshindwa kudhibiti watu Wapiuriti wasipozuiwa. Basi akatunga sheria kali dhidi yao. Japo hilo, vikundi kadhaa vya Wapiuriti viliendelea kukutana, lakini kisiri, katika nyumba za watu binafsi. Wapiuriti pia waligawanya karatasi nyingi za kidini wakifafanua itikadi zao. Wapiuriti wa London waliweka rasmi baraza lao la wazee, wengi wao wakiwa wale waliokuwa wahudumu wa Anglikana waliokuwa wamesimamishwa kwa muda. Vikundi ambavyo viliacha kufanya marekebisho katika Kanisa la Kianglikana na kuondoka kwalo viliitwa Separatists.
Mfalme James 1, aliyemwandama Malkia Elizabeth, alifuata sera zake za kidini, akitisha “kuondosha [Wapiuriti] kutoka nchi hiyo.” Na kwa wakati uo huo, akaagiza tafsiri mpya ya Kiingereza ya Biblia ifanywe—King James Version, iliyomalizika katika 1611. Tafsiri hii mpya ilichochea watu wengi kuchunguza Biblia. Tokeo likawa nini? Watu wengi hata zaidi wakaanza kutofautiana na kanisa la Serikali. Ungalifanya nini kama ungaliishi siku hizo? Je, unafikiri kwamba ungalirekebisha itikadi zako za kidini ukitishwa kunyanyaswa? Je, ungalishikilia kabisa itikadi zako, hata jambo jipi litokee? Wapiuriti wengi walishikilia itikadi zao wakakataa kuridhiana.
Kutorokea Uholanzi
Kikundi kimoja cha Separatists ambacho hakikuridhiana kilikuwa katika mji mdogo wa Scrooby katika Uingereza. Huko walikutanika kisiri katika nyumba ya mkuu wa posta William Brewster, “Mzee [wao] Atawalaye.” John Robinson, aliyekuwa hapo awali kasisi wa Anglikana alishirikiana nao pia. Zaidi ya kupendekeza kanisa lisimamiwe na wazee badala ya makasisi na maaskofu, kikundi kilichokuwapo Scrooby kilikataa mavazi ya kikasisi na desturi nyingi za ibada ya Kanisa la Kianglikana, ingawa mambo hayo yalikuwa ya lazima chini ya sheria.
Mkazo ulipozidi, kikundi hiki kidogo kiliamua kutorokea Uholanzi, wakati huo ikiwa mahali pekee ambapo mawazo na mazoea yao yangekubalika katika Ulaya. Lakini ilikuwa kinyume cha sheria kuhama. Basi, kwa usiri kabisa, wao waliuza nyumba zao na kila kitu kinginecho ambacho hawangeweza kubeba, na katika 1608 walienda Amsterdam kwa meli. Ilikuwa huko Uholanzi kwamba Separatists walianza kujifikiria kuwa mapilgrimu.
Mapilgrimu walihamia Leiden mwaka mmoja baada ya kufika, mwaka uleule ambao mkataba wa amani ulikatisha vita ambayo ilikuwa imewaka kati ya Hispania na Uholanzi. Mkataba huo ulitokeza hali tulivu zaidi kwa Mapilgrimu. Polepole, watoro wengine wakafika kutoka Uingereza, na kikundi hicho kilikua kufikia watu wapatao 300. Hatimaye, walinunua nyumba kubwa, ambamo John Robinson na familia yake iliishi na ambamo waliweza kufanya mikutano yao.
Baada ya kukaa Leiden kwa karibu miaka kumi, hao Mapilgrimu wakaanza kuwa na wasiwasi. Ule mkataba wa amani na Hispania ulikuwa karibu kuisha, nao walihofu kwamba iwapo Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi ya Hispania yatapata kudhibiti Uholanzi, wangekuwa katika hali mbaya zaidi kuliko walivyokuwa chini ya Mfalme James. Isitoshe, hawakukubaliana kimafundisho na majirani wao Waholanzi wenye kukubali mambo mengi, nao walikuwa na wasiwasi juu ya ushirika wa watoto wao pamoja na vijana Waholanzi, ambao hao waliwaona kuwa watovu wa maadili. Wafanye nini? Wakafikiria kuhamia mbali tena—wakati huu kwenda Marekani!
Meli Mayflower Yaabiri!
Tatizo kubwa zaidi lilikuwa kugharamia kifedha safari ndefu hivyo. Tatizo jingine kubwa sana lilikuwa kwamba kibali cha safari kama hiyo kilipaswa kutoka kwa mfalme wa Uingereza—mfalme yuleyule ambaye walimtoroka walipotorokea Uholanzi! Mapilgrimu hao walimshinda Mfalme James kwa maombi yao mengi, mpaka mwishowe akawapa kibali. Hatimaye, kikundi cha wafanyabiashara wa London kikadhamini kifedha safari hiyo.
Hatimaye, wakati ukafika wa kuondoka! Wale wa Kanisa la Pilgrimu katika Leiden walioamua kuhama walipanda meli Speedwell na mnamo Julai 22, 1620, wakaondoka Delfshaven kuelekea Uingereza ili wajiunge na washiriki wengine zaidi huko. Hao Mapilgrimu walipanda meli mbili, Speedwell na Mayflower. Hata hivyo, mivujo mibaya katika Speedwell ililazimisha meli hizo zirudi Uingereza, ambako Mayflower ikachukua abiria na maandalio kutoka kwa Speedwell. Hatimaye, mnamo Septemba 6, meli hiyo ndogo ya Mayflower, yenye meta 27, ikaanza safari kutoka Plymouth, Uingereza, peke yayo, ikiwa imebeba familia 24—jumla ya abiria 102—na wafanyakazi 25. Hilo lilihitaji ujasiri kama nini kwa wasafiri hao wasio na ujuzi kujaribu safari ya bahari-kuu ya kilometa 5,000! Meli hiyo ilijaa kupita kiasi nayo ililazimika kukabiliana na halihewa mbaya ya Atlantiki ya Kaskazini. Ebu wazia hisia za wale waliokuwa ndani wakati walipoona bara baada ya majuma tisa marefu katika bahari-kuu!
Kuanzisha Koloni
Kabla ya Mapilgrimu kwenda barani, walifanya mapatano, au agano, kuhusu serikali ya wakati ujao ya koloni mpya. Kwa mapatano hayo, yaliyotiwa sahihi na wanaume 41 ambao walikuwa katika kikundi hicho, Mapilgrimu walijifanyizia “Serikali Moja” nao wakatwaa madaraka ya kutunga na kuishi kulingana na sheria za kuongoza mambo yao yote. Ingawa wanahistoria fulani wameita hati hiyo katiba ya kwanza ya Marekani, Grote Winkler Prins Encyclopedie yasema kwamba Mapilgrimu waliokuwa wameifanyiza “walifikiria kuanzisha mamlaka ya aina ya kidini.” Kusudi layo lilikuwa kufanya washiriki wote wa koloni kubaki pamoja, kihalisi na kidini.
Baada ya kuchunguza pwani na bara, katika Desemba yenye baridi kikundi hicho kikakaa mahali walipopaita New Plymouth, baadaye pakaitwa Koloni ya Plymouth. Walipata mashamba ambayo yalikuwa yamelimwa na Wahindi. Lakini ile idadi kubwa ya Wahindi ambayo ilikuwa imeonwa na wavumbuzi miaka michache tu iliyokuwa imepita ilikuwa imepunguzwa sana na maradhi ya wavumbuzi—kutia ndani ndui na surua. La sivyo, Wahindi wangalikinza jitihada za Mapilgrimu kuanzisha koloni.
Mapilgrimu walianza kwa kujenga nyumba ya kijumuiya na nyumba kadhaa za binafsi. Ulikuwa mwanzo mgumu, kwa kuwa walifika wakati wa kipupwe nao hawakuwa na chakula kingi kilichosalia katika maandalio ya meli. Katika kipupwe hicho cha kwanza, watu 52 walikufa kutokana na maradhi, kutia ndani waume 13 kati ya 24 na wake 14 kati ya wale 18. Miongoni mwa wale waliokufa alikuwa gavana wao wa kwanza, John Carver. Lakini wale waliookoka waliazimia kubaki katika New Plymouth. Gavana aliyefuata, William Bradford mwenye shauku, aliandika rekodi ya mambo mengi ya historia ya koloni hiyo changa na hivyo ameonwa kuwa mwanahistoria wa kwanza wa Marekani.
Mapilgrimu na Wahindi
Mapilgrimu wa kwanza kufika New Plymouth walifanya mapatano ya amani na Massasoit, chifu mkuu wa kabila la Wahindi la Wawampanoag wa huko. Katika mapatano hayo Mapilgrimu na Wawampanoag waliahidi kwamba hawatafanyiana madhara, nao waliahidi kulindana iwapo kuna vita na watu wa nje. Bila urafiki wa Massasoit, haielekei kwamba yeyote kati ya Mapilgrimu hao angeokoka. Wahindi hao waliwapa masetla hao mahindi ya kienyeji ya kula na kupanda, na kwa kushirikiana nao kulifanya Mapilgrimu wasiuawe na makabila mengine.
Katika siku za mapema, wakoloni hao walipokea msaada sana kutoka kwa Wahindi. Kwa maneno ya Gavana William Bradford, Mhindi mmoja aitwaye Tisquantum aliwafundisha wakoloni “jinsi ya kupanda mahindi, mahali pa kuvua samaki, na jinsi ya kupata bidhaa nyinginezo, na ni yeye aliyekuwa kiongozi wao aliyewapeleka sehemu ambazo hawakuzijua kwa manufaa yao.” Mavuno ya kwanza ya mahindi ya Wahindi yalikuwa mazuri, nao Mapilgrimu wakapata mafanikio katika kuwinda ndege. Walimshukuru Mungu nao wakaamua kufanya sherehe ya siku tatu ya mavuno. Massasoit na mashujaa wake 90 wakaja, wakileta dia watano kwa kuongezea karamu.
Kama ile koloni yenyewe, sherehe hiyo ilikuwa na mambo mengi ya kidini. Ingawa Mapilgrimu hawakufanya sherehe hiyo mwaka uliofuata kwa sababu ya kutopata mazao mazuri, Sikukuu ya Kushukuru baadaye ilikuja kuwa sikukuu ya kila mwaka ya kitaifa na kidini Marekani, Kanada na nchi nyinginezo chache. Leo, Sikukuu ya Kushukuru katika Amerika ya Kaskazini ni pindi halisi ya mlo wa familia ya kula bata-mzinga, mchuzi wa cranberry, na pai ya boga—lakini hasa, hiyo inabaki kuwa “wakati wa kufikiria kwa uzito kidini, ibada za kanisa, na sala.”—The World Book Encyclopedia, 1994.a
Maendeleo ya Baadaye
Katika 1622 Mapilgrimu wengi wakaja kutoka Leiden na Uingereza. Baadaye, meli zaidi zilifika zikibeba waamini wenzao kutoka Ulaya. Katika 1630 kikundi cha mwisho cha Mapilgrimu kutoka Leiden kilijiunga na koloni hiyo, jambo lililofanya wafikie 300 hivi. Hatimaye koloni hiyo ilijiunga na Koloni ya Massachusetts Bay iliyokuwa kubwa zaidi na ambayo haikuwa mbali upande wa kaskazini. Koloni hizo pia zilikuwa na itikadi za Kipiuriti. Hata hivyo, kwa wakati huo, uhasama ulikuwa ukikua kati ya wakoloni na majirani wao Wahindi. Wapiuriti, ambao waliamini kwamba Mungu alikuwa amewapangia kimbele kudhibiti hilo bara jipya, wakazidi kuonyesha madharau. Wakiona hilo, Wahindi wakaja kuwachukia zaidi na zaidi. Kwa kusikitisha, miaka 55 tu baada ya kufanya mapatano na Wawampanoag, hiyo koloni ya Plymouth, ikishirikiana na koloni nyinginezo tatu za Uingereza pamoja na Wahindi wengine, walipiga vita dhidi ya mwana wa Massasoit. Huyo na wanaume, wanawake, na watoto Wahindi wapatao elfu tatu waliuawa, na Wapiuriti wakauza mamia mengine utumwani. Kabila la Wawampanoag likatokomea.
Urithi wa Mapilgrimu
Katika Uholanzi bado waweza kuzuru sehemu ya Leiden ambako Mapilgrimu waliishi, na vilevile Delfshaven, ile bandari waliyotumia walipoondoka kwenda Marekani. Katika mji wa sasa wa Plymouth, Massachusetts, unaweza kuona Plymouth Plantation, mfanyizo upya wa kijiji cha awali kilichojengwa na Mapilgrimu, pamoja na jumba la kuhifadhi vitu vya kale la Mapilgrimu, na mfano mdogo wa Mayflower. Katika hicho kijiji, waigizaji huigiza wakazi wa awali. Wao watakuambia kwamba jina la Mungu ni Yehova na kwamba “kanisa” si jengo la mawe bali limefanyizwa kwa watu. Kwa kujibu swali, “Kuna wazee wangapi katika kanisa lenu?” wao hujibu: “Wengi kwa kadiri wanaotimiza matakwa ya Biblia.”
Mapilgrimu walijaribu kufanya jamii yao “kuwa kama makabila kumi na mawili ya Israeli chini ya Musa kwa kadiri iwezekanavyo,” kulingana na kitabu The Puritan Heritage—America’s Roots in the Bible. Hata hivyo, nyakati nyingine Wapiuriti walikuwa wenye kupita kiasi. Kwa kielelezo, sifa yao ya kuwa wafanya kazi wenye bidii ilitokana kwa kadiri fulani na itikadi yao kwamba ufanisi wa kimwili ulionyesha upendeleo wa Mungu. Ingawa kwa kweli wao walipenda watoto wao, Wapiuriti wengi wa mapema waliamini kwamba wao walipaswa “kuficha . . . shauku inayopita kiasi.” Hivyo, neno “puritanical” limehusianishwa na hali ya kujinyima, ugumu, na ukali kupita kiasi. Hata hivyo, wajapokuwa watu wasiokamilika, Mapilgrimu walikuwa na kadiri fulani ya maadili, walikuwa wachaji, nao walijitahidi kuishi kulingana na Biblia. Kwa wazi, sifa hizo ziliwaunganisha Wapiuriti na kuwadumisha kupitia majaribu yao mengi.
[Maelezo ya Chini]
a Wakristo wa kweli hawahitaji sikukuu hususa ili kumshukuru Mungu. Kwa habari zaidi, tafadhali ona toleo la Amkeni! la Novemba 22, 1976, kurasa 9-13, la Kiingereza.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Wahindi Wawampanoag walisaidia Mapilgrimu
[Hisani]
Harper’s Encyclopædia of United States History
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Juu: Model van de Mayflower