Ah, Angalau Hewa Safi!
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
UNAPOPUMUA, je, wewe hupumua hewa safi? Uchafuzi wa hewa wa siku hizi ni “adui mkubwa kuliko uvutaji sigareti,” adai daktari mmoja aliyenukuliwa katika The Times la London. Katika Uingereza na Wales, hewa ilivyochafuliwa huua watu wakadiriwao kuwa 10,000 kila mwaka. Ulimwenguni pote, hasa katika majiji makubwa, hali ni mbaya zaidi.
Wengi hulaumu kiwanda cha magari kwa kuchafua angahewa. Ili kupunguza mchemuo hatari, magari mapya katika nchi nyingi sasa yanakuja yakiwa yamewekwa vifaa vya kugeuza mchemuo wa gari kutodhuru, ambavyo hupunguza uchafuzi. Viwango vya hidrokaboni katika gesi za mchemuo vimeshuka hadi asilimia 12 za viwango vya 1970, kukiwa na upunguo kama huo katika oksidi za nitrojeni na kaboni monoksidi. Vitoto vibebwavyo katika vigari vya kubebea vitoto ndivyo hasa viwezavyo kudhuriwa kwa urahisi kwa sababu hivyo hubebwa kwa kiwango ambacho magari yachemua ufukizo. Lakini uchafuzi wa hewa hutisha walio ndani ya magari vilevile. Imeripotiwa kwamba uchafuzi ni wa juu mara tatu zaidi ndani ya magari kuliko nje. Madhara mengine zaidi huja kutokana na kupumua ufukizo wa benzeni kutoka fueli unapojaza tangi la mafuta la gari lako.
Sasa namna iliyoenea zaidi ya uchafuzi wa hewa ulimwenguni pote ni “Mata Ndogo Mno Inayoelea,” yasema ripoti ya habari za kimazingira ya 1993-1994 ya Umoja wa Mataifa. Yaelekea kwamba, vipande vidogo mno vya masizi, au mata ndogo mno, zina uwezo wa kupenya ndani sana ya mapafu na kuacha hapo kemikali zenye kudhuru.
Kumalizwa kwa tabaka la ozoni juu sana tufeni huvutia maelezo mengi ya vyombo vya habari. Hata hivyo, kwenye kiwango cha ardhi nuru ya jua huathiri oksidi za nitrojeni na elementi nyinginezo ziwezazo kuvukizwa kwa urahisi na kutokeza viwango vya juu vya ozoni. Viwango hivi vimerudufika katika Uingereza katika karne hii. Gesi hizi huharibu rangi na vifaa vingine vya ujenzi, husababisha maradhi katika miti, mimea, na mazao, na yaonekana huanzisha matatizo ya kupumua katika watu fulani. Ingawa mwingi wa uchafuzi wa ozoni hutukia mijini, kwa kushangaza ni maeneo ya mashambani ambayo hupatwa na athari mbaya zaidi. Katika maeneo ya mijini, oksidi za nitrojeni hufyonza ozoni ya ziada, lakini mahali ambapo oksidi hizi ni chache, ozoni ina uhuru wa kusababisha uharibifu.
Kwa kuongezea, uchafuzi wa hewa ni “mara 70 juu zaidi ndani ya nyumba kuliko nje,” laripoti The Times. Hapa ufukizo kutoka visafisha hewa, vizuia-nondo, na hata nguo zilizosafishwa kwa kemikali huchafua hewa. Moshi wa sigareti vilevile huongeza hatari za afya ndani ya nyumba.
Basi, waweza kufanya nini ili ulinde familia yako? Gazeti The Times la London liliandaa madokezo yafuatayo.
• Punguza utumizi wako wa gari. Ikiwezekana, safiri pamoja na wengine. Endesha kwa wanana. Ukizuiwa katika msongamano wa magari au kusimama kwa zaidi ya dakika chache, zima injini. Ikiwezekana, katika siku zenye joto egesha gari lako kivulini ili kupunguza uchafuzi unaotokezwa na kuvukizwa kwa fueli.
• Chagua kufanya mazoezi ya mwili mapema asubuhi wakati ambapo kwa kawaida viwango vya ozoni nje viko chini.
• Piga marufuku uvutaji sigareti nyumbani.
• Fungua kidogo madirisha ya chumba cha kulala wakati wa usiku ili kupunguza unyevu na kutoa nje vitu visababishavyo mizio.
Bila shaka wakubali: Ah, angalau hewa safi!