Dhahabu—Uvutio Wake
Dhahabu—tangu zamani za kale, metali hii nyororo ya manjano yenye kung’aa imethaminiwa sana kwa sababu ya sifa zake za kipekee. Rangi yake, mng’aro wake, kufulika kwake, na uwezo wake wa kudumu ni wa kipekee sana miongoni mwa metali. Kwa sababu ya thamani yake kulingana na wale ambao wameitafuta, dhahabu ina historia iliyo tofauti na metali nyinginezo.
“DHAHABU! Ni dhahabu, hakika hii ni dhahabu! Dhahabu!” Uvumbuzi wa dhahabu umedundisha mioyo, ukafanya mioyo ipige kwa kasi, na kutokeza ndoto za ufanisi. Imetafutwa ardhini, mitoni, na katika vijito, na hata katika mashimo yenye vina vya maelfu ya meta chini ya ardhi.
Ikiwa kito chenye thamani, dhahabu imepamba wafalme na malkia. Imepamba viti vya ufalme na kuta za makao ya kifalme. Sanamu za dhahabu, zinazowakilisha samaki, ndege, wanyama, na vitu vingine, zimeabudiwa kama miungu. Dhahabu imetafutwa kwa udi na uvumba, kwa jinsi ambavyo nayo imeathiri ustaarabu.
Dhahabu na Historia
Katika Misri ya kale, farao waliwatuma wafanya-biashara na majeshi katika nchi za mbali wakatafute dhahabu, ambayo ilionwa kuwa mali ya miungu ya Misri na ya farao pekee. Kaburi la Tutankhamen, lililogunduliwa mwaka wa 1922, lilijaa hazina zenye thamani kubwa sana za dhahabu. Jeneza lake lenyewe lilifanyizwa kwa dhahabu tupu.
Kulingana na wanahistoria fulani, Aleksanda Mkuu “alivutiwa awali kwenda Asia kwa sababu ya hadithi za hazina za dhahabu za Uajemi.” Inaripotiwa kwamba maelfu ya wanyama wa kubebea mizigo walitumiwa na jeshi lake kubebea dhahabu aliyotwaa huko Uajemi akaipeleke Ugiriki. Tokeo likawa kwamba Ugiriki ikawa taifa tajiri kwa dhahabu.
Mwanahistoria mmoja aripoti kwamba “maliki wa Roma walitumia dhahabu kwa wingi ili watiishe maofisa wao na vilevile kushawishi wakuu wa nchi nyinginezo. Wao walivutia na hata kutisha watu wao kwa utajiri wao, ambao ulijulikana kwa urahisi kwa mbwembwe zao za kuonyesha vitu vya dhahabu.” Waroma walipata dhahabu nyingi kutokana na ushindi wao dhidi ya Hispania na kutwaa kwao machimbo ya dhahabu ya Kihispania, chasema kitabu kimoja.
Lakini, hadithi ya dhahabu haiwezi kukamilika bila kuingilia kwa kina historia yake katili. Ni hadithi ya ushindi, unyama, utumwa, na kifo.
Historia Iliyojaa Umwagaji wa Damu
Ustaarabu ulipoendelea, meli kubwa zaidi na zenye nguvu zaidi ziliondoka ili kuvumbua nchi mpya, kuanzisha koloni mpya, na kutafuta dhahabu. Wavumbuzi wengi wakawa na tamaa kubwa ya kupata dhahabu, kutia ndani mvumbuzi jasiri Christopher Columbus (1451-1506).
Uhai wa wenyeji haukuwa kitu mbele ya Columbus alipokuwa akitafuta dhahabu. Akiwasimulia mfalme na malkia wa Hispania, ambao walikuwa wamedhamini safari zake kifedha, mambo yaliyompata katika kisiwa kimoja, Columbus aliandika hivi katika kitabu chake cha kumbukumbu: “Ili kutawala hapa, mtu ahitaji tu kutulia na kupiga ubwana juu ya hao wenyeji, ambao watatekeleza chochote wanachoagizwa. . . . Hawa Wahindi . . . wako uchi na hawana kinga, hivyo wako tayari kuamriwa na kutumikishwa.” Columbus aliamini kwamba ana baraka za Mungu. Hazina hizo za dhahabu zingesaidia Hispania kugharamia vita vyake vitakatifu. ‘Kwa rehema yake, Mungu anisaidie kupata dhahabu,’ alisema hivyo pindi moja baada ya kupokea kisetiri-uso kimoja cha dhahabu.
Watekaji wa Hispania, walioabiri wakitafuta dhahabu baada ya Columbus, waliamriwa na Mfalme Ferdinand wa Hispania: “Mniletee dhahabu! Ikiwezekana mwipate bila ukatili. Lakini mwilete, hata kama mnaipataje.” Wavumbuzi hao wakatili waliua maelfu ya wenyeji ambao waliwapata huko Mexico na Amerika ya Kati na ya Kusini. Dhahabu zilizopelekwa Hispania na watekaji hao ni kana kwamba zilikuwa zikitiririka damu nyingi.
Kisha wakaja maharamia ambao hawakuwakilisha taifa lolote. Huko baharini, walipora meli za Hispania zilizojaa dhahabu na hazina nyinginezo. Kwa sababu mara nyingi meli hizo hazikuwa na uwezo mkubwa wa kupigana na pia zilikuwa na watu wachache tu, hazikufua dafu mbele ya maharamia wenye silaha kali zaidi. Katika karne za 17 na 18, uharamia ukatanda kotekote baharini, hasa katika Visiwa vya West Indies na pwani ya Marekani.
Mbio za Kupata Dhahabu Katika Karne ya 19
Mnamo mwaka wa 1848 dhahabu nyingi ziligunduliwa katika Bonde la Sacramento, California. Punde si punde habari ikaenea, watu wakaanza kumiminikia sehemu hiyo wakitwaa maeneo ya dhahabu. Kufikia mwaka uliofuata, California ikafurika kwa makumi ya maelfu ya wale walioitwa forty-niners—watafutaji wa utajiri ambao walitoka sehemu zote za ulimwengu. Idadi ya watu wa California ikaongezeka kutoka watu wapatao 26,000 mnamo 1848 hadi wapatao 380,000 mwaka wa 1860. Wakulima waliacha mashamba yao, mabaharia wakaacha ubaharia, wanajeshi wakatoroka jeshi—ili tu wasafiri kutafuta dhahabu. Wengine walitajwa kuwa “majangili hayawani.” Kwa mchanganyiko huo wa watu, kukaja pia uhalifu na ujeuri mwingi. Wale walioshikwa na tamaa ya dhahabu lakini ambao hawakuwa tayari kuitolea jasho waligeukia unyang’anyi, wakipora magari na magarimoshi.
Mnamo 1851, kufuatia tu kukuru-kakara za kung’ang’ania dhahabu za California, ikaja habari ya kwamba dhahabu nyingi zilikuwa zinagunduliwa Australia. “Kwa kweli kuna dhahabu tele” ripoti hiyo ikasema. Kwa muda mfupi, Australia ikawa mtokezaji mkuu wa dhahabu ulimwenguni. Baadhi ya watu ambao walikuwa wamehamia California wakafunga virago vyao haraka na kuelekea Australia. Idadi ya watu Australia ikaongezeka haraka sana—tokea watu 400,000 mnamo 1850 hadi zaidi ya 1,100,000 katika 1860. Ukulima na kazi nyinginezo zikaachwa kabisa kwa kuwa wengi walikimbilia dhahabu.
Kuelekea mwishoni mwa karne ya 19, mbio hizo za kufa na kupona za kutafuta dhahabu zikaelekea Yukon na Alaska, kufuatia ugunduzi wa dhahabu katika maeneo hayo. Maelfu ya watu walienda Kaskazini ya Mbali, katika eneo la Klondike na Alaska, wakivumilia baridi kali ili watwae maeneo yenye dhahabu nyingi.
Hazina Zilizozama
Katika karne ya 20, kwa sababu ya maendeleo ya kupiga-mbizi ndani sana baharini, watafuta dhahabu wameelekeza uangalifu wao kwenye sakafu za bahari. Huko walitafuta meli zilizozama ikiwa zina hazina—vito vya dhahabu na vitu vingine vilivyotengenezwa karne nyingi zilizopita.
Mnamo Septemba 20, 1638, meli ya Hispania Concepción ilizama katika Bahari ya Pasifiki, karibu na pwani ya Saipan, baada ya kusukumwa kwenye mawe na hali mbaya ya hewa. Ilikuwa imebeba dhahabu na hazina nyinginezo ambazo leo zina thamani ya makumi ya mamilioni ya dola. Wengi kati ya watu 400 waliokuwa wameipanda walikufa. Wapiga-mbizi wamepata katika meli hiyo mikufu 32 ya dhahabu, kila mmoja ukiwa na urefu wa futi tano na uzito wa kilogramu kadhaa. Kwa ujumla, wapiga-mbizi wametoa vipande 1,300 vya vito vya dhahabu—mikufu, misalaba, vifungo, bruchi, pete, na bizimu.
Meli nyinginezo zilizozama zimegunduliwa pia. Mnamo 1980, wapiga-mbizi waliokuwa katika pwani ya Florida, Marekani, walipata mabaki ya meli ya Hispania iliyoitwa Santa Margarita, ambayo ilizama katika karne ya 17. Kufikia mwisho wa mwaka uliofuata, wapiga-mbizi walipata zaidi ya kilogramu 44 za dhahabu, pamoja na vitu vingine vya kale vya dhahabu.
Dhahabu Zilizoporwa Wakati wa Vita
Baada ya serikali ya Ujerumani kusalimu amri mwaka wa 1945, majeshi ya mataifa ya Muungano yalifanya ugunduzi wenye kushangaza sana katika machimbo ya chumvi ya Kaiseroda katika Thuringia, Ujerumani. Kulingana na The Atlanta Journal, “machimbo hayo yalitoa dhahabu, michoro, fedha na vyeti vya umilikaji zenye thamani ya dola bilioni 2.1.” Pia mifuko iliyojaa meno ya dhahabu na fedha, mengine yakiwa tayari yameyeyushwa, ambayo yaling’olewa kutoka kwa watu waliouawa katika Yale Maangamizi Makubwa. Dhahabu hizo chungu nzima ziliwasaidia mababe wa vita wa Nazi wagharamie vita hivyo ambavyo vilienea sana. Imekadiriwa kwamba dhahabu zenye thamani ya dola bilioni 2.5 zimerudishiwa nchi kumi hivi ambazo zilitwaliwa na Hitler, laripoti Journal. Kwa sababu inaaminiwa na watu wengi kwamba bado dhahabu zote zilizofichwa na Nazi hazijapatikana, utafutaji waendelea.
Kwa kweli, dhahabu ina thamani. Lakini, Biblia inasema kwamba dhahabu, kama ilivyo na mali nyinginezo, haiwezi kuwapa wale waitafutao uhai. (Zaburi 49:6-8; Sefania 1:18) Mithali moja ya Biblia yasema: “Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu?” (Mithali 16:16) Hekima ya kweli hutokana na Muumba, Yehova Mungu, na inapatikana katika Neno lake, Biblia. Kwa kujifunza Neno la Mungu, mtafutaji wa hekima aweza kujifunza sheria, kanuni, na mashauri ya Mungu, kisha azitumie maishani. Hekima inayopatikana hivyo ni yenye kutamanika zaidi kuliko dhahabu zote ambazo zimepata kugunduliwa na mwanadamu. Hekima kama hiyo inaweza kumaanisha maisha bora sasa na uhai wa milele katika wakati ujao.—Mithali 3:13-18.
[Sanduku katika ukurasa wa 27]
Mambo Fulani Kuhusu Dhahabu
• Dhahabu hufulika na kunyumbulika kuliko metali zote. Inaweza kulainishwa iwe nyembamba mara milioni nne kuliko inchi moja. Dhahabu ya gramu 28 inaweza kupigwa-pigwa ienee meta 17 hivi za mraba. Dhahabu ya gramu 28 inaweza kuvutwa kufikia urefu wa kilometa 70.
• Kwa sababu dhahabu safi ni nyororo, mara nyingi hiyo huchanganywa na metali nyinginezo ili kuongezea ugumu wake inapotumiwa kutengeneza vito na vitu vingine vya dhahabu. Kiasi cha dhahabu iliyochanganywa na metali nyinginezo hutajwa kwa vipimo vya 24, vinavyoitwa karati; kwa hiyo, kitu chenye karati 12 ya dhahabu inamaanisha nusu yake ni dhahabu, karati 18 ya dhahabu inamaanisha robo tatu ni dhahabu, na karati 24 ni dhahabu safi.
• Mataifa yanayoongoza katika kutokeza dhahabu ni Afrika Kusini na Marekani.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Aleksanda Mkuu: The Walters Art Gallery, Baltimore
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mchoro unaoonyesha kufika kwa Christopher Columbus kule Bahamas mwaka wa 1492 akitafuta hazina za dhahabu
[Hisani]
Courtesy of the Museo Naval, Madrid (Spain), and with the kind permission of Don Manuel González López