Dhahabu Ingali Inavutia
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA
KATIKA kichaka cha Australia, mtu anayetafuta madini anatembea katika mto uliokauka. Jua la mchana linaunguza mgongo wake. Jasho linapenya shati yake yenye vumbi. Bila kukata tamaa, anashika chuma kirefu ambacho katika sehemu ya chini kina kifaa kinachotoshana na sahani na anakisogeza huku na huku juu ya ardhi. Kifaa hicho cha hali ya juu hutumiwa kutambua vyuma nacho kinaweza kutambua chuma kilicho meta moja chini ya ardhi yenye mawemawe. Vifaa alivyovaa masikioni vinanasa ishara kutoka kwenye kifaa hicho na kutokeza sauti ya juu iliyo kama mbinja.
Ghafula, anasisimuka kwani sauti hiyo kama mbinja inapungua na kuanza kukatika-katika hiyo ikiwa ishara kwamba kifaa chake kimegundua chuma kilichozikwa. Anapiga magoti na kuanza kuchimba. Anachimba kwa bidii ardhi ngumu akitumia sururu yake ndogo. Huenda chuma hicho ni msumari tu wenye kutu. Labda ni sarafu iliyochakaa. Lakini anapozidi kuchimba, anakodoa macho yake kuona kama kuna dhahabu.
Harakati za Kutafuta Dhahabu Zinaendelea
Huenda ikawa mbinu za kutafuta dhahabu zimebadilika, lakini katika historia yote mwanadamu ametafuta kwa bidii metali hiyo ya manjano inayometameta. Kwa kweli, kulingana na Shirika la Dhahabu Ulimwenguni, kwa zaidi ya miaka 6,000 iliyopita, zaidi ya tani 125,000 za dhahabu zimechimbwa.a Ingawa nchi zilizostaarabika za zamani kama Misri, Ofiri, na Amerika Kusini zilikuwa mashuhuri kwa sababu ya utajiri uliotokana na dhahabu, zaidi ya asilimia 90 ya dhahabu yote ambayo imewahi kuchimbwa, imechimbwa katika miaka 150 iliyopita.—1 Wafalme 9:28.
Harakati za kutafuta dhahabu zilianza mnamo 1848 wakati dhahabu ilipopatikana huko Sutter’s Mill, kwenye Mto America, California, Marekani. Ugunduzi huo uliwachochea watu wengi waliotaka kupata dhahabu wahamie huko. Wote waliohama waliwaza kwamba watapata hazina yao katika udongo wa California. Wengi hawakufanikiwa, lakini wengine walipata mafanikio makubwa. Mnamo 1851 pekee, tani 77 zilichimbwa katika migodi ya dhahabu ya California pekee.
Karibu wakati huohuo, dhahabu iligunduliwa upande mwingine wa dunia, katika koloni mpya ya Australia. Edward Hargraves, ambaye alijifunza kuchimba dhahabu katika migodi ya California, alielekea Australia na kupata dhahabu katika kijito karibu na mji mdogo wa Bathurst, huko New South Wales. Mnamo 1851, maeneo yenye dhahabu nyingi yalipatikana huko Ballarat na Bendigo, katika jimbo la Victoria. Habari za ugunduzi huo zilipoenea, harakati nyingine ikaanza. Baadhi ya watu waliokuja walikuwa wachimbaji stadi. Hata hivyo, wengi walikuwa wafanyakazi wa shambani au wa ofisini ambao hawakuwa wamewahi kutumia sururu ya wachimba migodi. Likieleza jinsi hali ilivyokuwa katika mji mmoja ambako wanaharakati walikuwa wakiishi, gazeti moja la eneo hilo lilisema hivi wakati huo: “Mji wa Bathurst umepatwa na kichaa tena. Kichaa cha kutafuta dhahabu kimerudi kwa kishindo. Wanaume hukutana, hutazamana kijinga, huzungumza upuuzi usioeleweka, na kushangaa ni nini kitakachotokea.”
Ni nini kilichotokea? Idadi ya watu iliongezeka haraka. Miaka kumi baada ya 1851, idadi ya watu nchini Australia iliongezeka maradufu, huku watu kutoka pembe zote za ulimwengu waliokuwa wakitafuta madini wakikutana katika nchi hiyo. Dhahabu iligunduliwa katika viwango mbalimbali barani humo. Harakati moja ilipopungua, nyingine ilianza. Mnamo 1856 pekee, Waaustralia ambao hutafuta madini walichimba tani 95 za dhahabu. Kisha, mnamo 1893, wachimbaji walianza kuchimba dhahabu karibu na Kalgoorlie-Boulder, Australia Magharibi. Tangu wakati huo, zaidi ya tani 1,300 zimechimbwa katika eneo ambalo limetajwa kuwa “sehemu yenye ukubwa wa kilometa 2.5 za mraba yenye dhahabu nyingi zaidi ulimwenguni.” Bado eneo hilo hutokeza dhahabu na sasa mgodi huo ni mojawapo ya migodi ya dhahabu yenye kina kirefu zaidi ulimwenguni, kwani umekuwa bonde lenye upana wa kilometa mbili hivi, urefu wa kilometa tatu hivi, na kina kinachofikia meta 400!
Leo, Australia ndiyo nchi ya tatu inayotokeza dhahabu kwa wingi ulimwenguni. Watu 60,000 wameajiriwa katika kazi hiyo, nayo hutokeza tani 300 hivi za dhahabu, au dhahabu yenye thamani ya dola bilioni tano (za Australia) kila mwaka. Marekani ndiyo nchi ya pili inayotokeza dhahabu kwa wingi ulimwenguni. Hata hivyo, kwa miaka zaidi ya mia moja, Afrika Kusini ndiyo imekuwa ikitokeza dhahabu kwa wingi zaidi ulimwenguni. Karibu asilimia 40 ya dhahabu yote ambayo imewahi kuchimbwa imetoka katika nchi hiyo. Ulimwenguni pote zaidi ya tani 2,000 huchimbwa kila mwaka. Metali hiyo yote yenye thamani hutumiwa katika njia zipi?
Utajiri na Urembo
Bado kuna sarafu zinazotengenezwa kwa dhahabu. Kiwanda cha kutengeneza pesa cha Perth, huko Australia Magharibi, ni mojawapo ya viwanda vikuu ulimwenguni vinavyotokeza sarafu hizo. Sarafu hizo hazitumiwi bali zimehifadhiwa na watu wanaokusanya vitu. Isitoshe, karibu robo ya dhahabu yote ambayo imewahi kuchimbwa imegeuzwa kuwa vipande vya dhahabu na kufungiwa katika vyumba vya benki. Ulimwenguni pote, Marekani ndiyo nchi yenye vipande vingi zaidi vya dhahabu kwenye benki zake.
Siku hizi, karibu asilimia 80 ya dhahabu inayochimbwa kila mwaka, yaani, tani 1,600 hivi, hutumiwa kutengeneza vito. Huenda Marekani ikawa na dhahabu nyingi zaidi katika benki zake, lakini vito vinapotiwa ndani, India ndiyo nchi yenye dhahabu nyingi zaidi. Mbali na kuwa yenye thamani na maridadi, metali hiyo laini inaweza kutumiwa katika njia nyingi sana.
Metali ya Zamani Inayotumiwa Katika Njia Mbalimbali
Yaelekea Farao wa Misri ya kale walijua kwamba dhahabu haiwezi kushikwa na kutu na hivyo waliitumia kutengeneza vinyago ambavyo vingetumiwa kuwazika walipokufa. Ili kuthibitisha uwezo wa kudumu wa dhahabu, waakiolojia walipochimbua kaburi la Farao Tutankhameni maelfu ya miaka baada ya kifo chake, walipata kinyago cha mfalme huyo mchanga kikiwa bila dhara lolote na bado kikiwa na rangi ya manjano inayometameta.
Dhahabu huendelea kung’aa kwa sababu haiathiriwi na maji na hewa, vitu ambavyo huharibu metali nyingine kama vile chuma. Dhahabu inafaa kutengeneza vitu vya elektroni kwa sababu haishiki kutu na pia inaweza kupitisha umeme. Kila mwaka, karibu tani 200 za dhahabu hutumiwa kutengeneza televisheni, mashini za video, simu za mkononi, na kompyuta milioni 50 hivi. Kwa kuongezea, diski za hali ya juu zina tabaka nyembamba ya dhahabu inayodumu ili kuhakikisha kwamba zinahifadhi habari kwa muda mrefu.
Tepe nyembamba za dhahabu hufanya kazi kwa njia isiyo ya kawaida. Fikiria jinsi metali hiyo hupatana na nuru. Tepe nyembamba sana za dhahabu hupitisha nuru. Tepe hizo nyembamba hupitisha mawimbi ya nuru ya kijani kibichi lakini huakisi miale ya nuru isiyoonekana. Madirisha yaliyopakwa dhahabu hupitisha nuru lakini si joto. Kwa hiyo, madirisha ya chumba cha rubani katika ndege za kisasa yamepakwa dhahabu, na pia madirisha ya ofisi nyingi mpya. Pia, vifaa fulani vya vyombo vya angani vinavyoweza kutokeza hatari vinapoharibika hufungwa kwa tepe za dhahabu zisizopenya nuru na hivyo kuzuia mnururisho na joto jingi.
Pia dhahabu haiwezi kuathiriwa na bakteria kwa urahisi. Kwa hiyo, madaktari wa meno huitumia kurekebisha meno yaliyoharibika au yaliyooza. Katika miaka ya karibuni, dhahabu imetumiwa kutengeneza vitu ambavyo hupandikizwa ndani ya mwili wa mwanadamu, kama vile vifaa vya kupanua mishipa ya damu iliyoziba.
Kwa kuwa dhahabu ina matumizi mengi, ni yenye thamani, na ni maridadi, bila shaka watu wanaotafuta madini wataendelea kuchimba dunia ili kupata metali hiyo inayovutia.
[Maelezo ya Chini]
a Dhahabu ni metali nzito sana hivi kwamba kipande chenye ukubwa wa sentimeta 37 tu kila upande, kinaweza kuwa na uzito wa tani moja hivi.
[Sanduku katika ukurasa wa 25]
Dhahabu Hupatikana Wapi?
◼ Miamba: Dhahabu hupatikana kwa kiasi kidogo katika miamba yote iliyoyeyuka. Miamba katika sehemu fulani za dunia huwa na kiasi kikubwa sana cha dhahabu hivi kwamba kampuni fulani huwa tayari kutumia pesa nyingi kuichimba, kuivunja-vunja, na kutumia kemikali kuitenganisha na mawe. Tani moja ya mawe yenye madini mengi ina gramu 30 tu za dhahabu.
◼ Kati ya Kwazi: Ni mara chache sana dhahabu hupatikana kati ya mabamba ya kwazi.
◼ Mito: Baada ya muda, mabamba ya kwazi yaliyo na dhahabu ambayo hupigwa na jua, upepo, na kunyeshewa, huvunjika na kutoa dhahabu iliyokuwa imebanwa, ambayo hujikusanya kwenye vijito na mito ikiwa vipande vidogo sana.
◼ Juu ya Ardhi: Vibamba vya dhahabu vyenye maumbo yasiyo ya kawaida hutokea juu ya ardhi. Nyakati nyingine vibamba hivyo vinaweza kuwa vikubwa ajabu. Bamba kubwa zaidi la dhahabu ambalo limewahi kupatikana liliitwa The Welcome Stranger, nacho kilikuwa na uzito wa kilogramu 70 hivi! Kilipatikana mnamo 1869 katika jimbo la Victoria, Australia. Australia ndiyo nchi yenye vibamba vikubwa zaidi vya dhahabu kwani vibamba 23 kati ya 25 vikubwa zaidi vilipatikana nchini humo. Leo ni rahisi zaidi kupata almasi bora kuliko kupata vibamba vya dhahabu vyenye ukubwa wa kiberiti.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]
Kifaa cha Kutambua Chuma Hufanyaje Kazi?
Kwa kawaida sehemu muhimu katika kifaa cha kutambua chuma ni nyaya mbili za mviringo. Umeme hupitishwa katika waya moja na kutokeza sumaku. Kifaa hicho kikipita juu ya chuma kama vile dhahabu, sumaku hiyo huathiriwa na chuma hicho. Waya ya pili hutambua uvutano ulitokea na kumpelekea ishara mtu anayetumia kifaa hicho kwa kuwasha taa, kutoa sauti, au kupitia kwenye geji.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Harakati ya kutafuta dhahabu katikati ya miaka ya 1800:
1. Sutter’s Mill, California, Marekani;
2. Bendigo, Victoria, Australia
3. Golden Point, Ballarat, Victoria, Australia
[Hisani]
1: Library of Congress; 2: Gold Museum, Ballarat; 3: La Trobe Picture Collection, State Library of Victoria
[Picha katika ukurasa wa 26]
Jinsi Dhahabu Inavyotumiwa Leo
Diski za hali ya juu zina tabaka nyembamba ya dhahabu
Tepe za dhahabu hutumiwa katika vyombo vya angani
Dhahabu hutumiwa kutengeneza vidude vya kupitisha umeme
Nyaya zenye dhahabu zina uwezo mkubwa sana wa kupitisha umeme
[Hisani]
NASA photo
Carita Stubbe
Courtesy Tanaka Denshi Kogyo
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mgodi wa dhahabu wenye kina kirefu zaidi ulimwenguni, huko Kalgoorlie—Boulder, Australia Magharibi
[Hisani]
Courtesy Newmont Mining Corporation
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Brasil Gemas, Ouro Preto, MG