Yesu Alifananaje?
USHUHUDA wa historia ya kilimwengu kuhusu jinsi Yesu alivyofanana unaathiriwa sana na mambo kadhaa. Mambo haya huchanganua tofauti kubwakubwa zilizoko katika picha za Yesu.
Mambo mawili ni utamaduni wa nchi hiyo na wakati picha ilipochorwa. Kwa kuongezea, itikadi za kidini za wachoraji na wale waliowaagiza ziliathiri jinsi ambavyo Yesu alichorwa.
Kwa karne nyingi, wachoraji mashuhuri, kama vile Michelangelo, Rembrandt, na Rubens, walikazia uangalifu sana sura ya Kristo. Mara nyingi picha zao zikiwa za ishara na mafumbo, zimeathiri sana maoni ya ujumla juu ya jinsi Yesu alivyofanana. Lakini fasiri zao zilitegemea nini?
Isemavyo Historia ya Kilimwengu
Picha zenye tarehe zinazotangulia Maliki Mroma Konstantino, aliyeishi wapata mwaka wa 280 hadi 337 W.K., mara nyingi zilimwonyesha Yesu akiwa kijana “Mchungaji Mwema” akiwa ama na nywele fupi ama nywele ndefu, zenye kujikunja-kunja. Lakini kuhusu hili kitabu Art Through the Ages chasema: “Mchungaji Mwema aweza kuonekana katika sanaa za [wapagani] Wagiriki wa Kale hadi sanaa za Wamisri, lakini hapa anafananisha mlinzi mwaminifu wa kundi la Kikristo.”
Baada ya muda, uvutano huu wa kipagani ukawa dhahiri hata zaidi. Kitabu hicho chaongezea hivi “Yesu angeweza kwa urahisi kuonwa kuwa sawa na miungu iliyojulikana katika eneo la Mediterania, hasa Helios (Apollo), mungu jua [ambaye duara inayomzunguka baadaye ilipewa Yesu na kisha “watakatifu”], au jinsi alivyofanywa kuwa wa Kiroma katika mashariki, Sol Invictus (Jua Lisiloweza Kushindwa).” Kwa kweli katika kaburi kubwa lililogunduliwa chini ya St. Peter, Roma, Yesu anaonyeshwa akiwa Apollo “akiendesha farasi wa gari-vita la jua kupitia mbingu.”
Hata hivyo, umbo hili linaloashiria ujana zaidi halikudumu kwa muda mrefu. Katika kitabu chake Christian Iconography, Adolphe Didron asema kilichotukia: “Umbo la Kristo, ambalo hapo kwanza liliashiria ujana, lazidi kuzeeka kutokea karne moja hadi nyingine . . . kadiri umri wa Ukristo unavyozidi kuendelea.”
Maandishi ya karne ya 13 yanayodai kuwa barua ya mtu fulani anayeitwa Publius Lentulus kwa Baraza la Roma yafafanua sura ya Yesu, ikisema kwamba alikuwa na “nywele za rangi ya kikahawia hafifu zilizokuwa laini na karibu kufikia masikio yake, lakini kutoka kwenye masikio ana vishungi ambavyo ni vyeusi kwa kiasi fulani na vyenye kung’aa zaidi, vikijipinda juu ya mabega yake; na nywele zake zimegawanyika katikati ya kichwa chake . . . , ana madevu yenye rangi kama nywele zake, ambayo si marefu, lakini yamegawanyika kwenye kidevu; . . . ana macho ya rangi ya kijivu . . . na maangavu.” Baadaye ufafanuzi huu bandia uliathiri wachoraji wengi. “Kila kipindi,” yasema New Catholic Encyclopedia “kilitokeza Kristo waliyetaka.”
Katika njia hiyohiyo, Kristo alionyeshwa kwa njia tofauti-tofauti na jamii na dini mbalimbali. Picha za kidini kutoka mabara ya wamishonari ya Afrika, Amerika, na Asia huonyesha picha ya Kristo wa Magharibi akiwa na nywele ndefu; lakini nyakati nyingine sura yake imeongezwa “maumbile ya wenyeji,” yasema hiyo ensaiklopedia.
Waprotestanti pia wamekuwa na wachoraji wao, na hawa wamefasiri sura ya Kristo kwa namna yao. Katika kitabu chake Christ and the Apostles—The Changing Forms of Religious Imagery, F. M. Godfrey asema: “Picha ya Rembrandt ya Kristo mwenye huzuni yatokana na maoni ya Waprotestanti, yenye mtu wa majonzi, mnyonge, mwenye maadili kali, . . . mtu wa Kiprotestanti mwenye kujinyima.” Asema picha hiyo yaonyeshwa na “wembamba Wake wenye kupita kiasi, kujinyima kwa mwili, ‘hali ya chini, ya kusikitikiwa na yenye uzito’ ambayo [Rembrandt] alitunga kuwa ngano ya Kikristo.”
Hata hivyo, kama tutakavyoona sasa, Kristo dhaifu, mwenye kuzungukwa na duara, mwenye hali za kike, mwenye huzuni, na nywele ndefu, ambaye mara nyingi hutokea katika picha za Jumuiya ya Wakristo, si sahihi. Kwa kweli, picha hiyo yatofautiana kabisa na Yesu anayetajwa katika Biblia.
Biblia na Sura ya Yesu
Akiwa “Mwana-Kondoo wa Mungu,” Yesu hakuwa na kasoro, kwa hiyo bila shaka alikuwa mwanamume mwenye sura nzuri. (Yohana 1:29; Waebrania 7:26) Na kwa hakika hangekuwa na sura yenye huzuni kama aonyeshwavyo katika michoro inayopendwa. Ni kweli kwamba alipatwa na mambo mengi yenye kutaabisha maishani mwake, lakini katika mwelekeo wake wa ujumla, alifanana na Baba yake kikamilifu, “Mungu mwenye furaha.”—1 Timotheo 1:11; Luka 10:21; Waebrania 1:3.
Je, Yesu alikuwa na nywele ndefu? Ni Wanadhiri peke yao ambao hawakutakiwa kunyoa nywele zao au kunywa divai, na Yesu hakuwa Mnadhiri. Hivyo huenda nywele zake zilinyolewa vizuri kama za mwanamume yeyote Myahudi. (Hesabu 6:2-7) Pia alifurahia divai kwa kiasi aliposhirikiana na wengine, na hii hukazia wazo la kwamba alikuwa mtu mchangamfu. (Luka 7:34) Hata alitengeneza divai kwa kufanya muujiza kwenye karamu moja ya arusi katika Kana ya Galilaya. (Yohana 2:1-11) Na inaonekana alikuwa na ndevu, jambo linalothibitishwa na unabii unaohusu kuteseka kwake.—Isaya 50:6.
Vipi juu ya rangi na maumbile ya Yesu? Yaelekea alifanana na Wayahudi. Angerithi maumbile haya kutoka kwa mama yake, Maria, aliyekuwa Myahudi. Wazazi wake wa kale walikuwa Wayahudi, wa nasaba ya Waebrania. Hivyo, labda Yesu angekuwa na rangi na maumbile yanayofanana na ya Wayahudi.
Hata akiwa miongoni mwa mitume wake, yaonekana Yesu hakuwa tofauti sana kimwili na wengine, kwa kuwa Yudasi alihitaji kumsaliti kwa maadui wake kwa kumbusu ili kumtambulisha. Hivyo, Yesu angeweza kuchangamana kwa urahisi na umati. Na alifanya hivyo, kwa kuwa katika pindi moja, alisafiri bila kujulikana kutoka Galilaya hadi Yerusalemu.—Marko 14:44; Yohana 7:10, 11.
Hata hivyo, wengine wanafikia mkataa wa kwamba Yesu alikuwa dhaifu. Kwa nini wanasema hivyo? Sababu moja ni kwamba alihitaji kusaidiwa kubeba mti wake wa mateso. Pia alikuwa wa kwanza kufa akiwa kati ya watu watatu waliotundikwa mtini.—Luka 23:26; Yohana 19:17, 32, 33.
Yesu Hakuwa Dhaifu
Kinyume cha mapokeo, Biblia haimfafanui Yesu kuwa dhaifu au mwenye sifa za kike. Badala ya hivyo, inasema kwamba hata alipokuwa kijana, ‘alifuliza kufanya maendeleo katika hekima na ukuzi wa kimwili na katika upendeleo pamoja na Mungu na wanadamu.’ (Luka 2:52) Alikuwa seremala kwa karibu miaka 30. Hiyo haionekani kuwa kazi ya mtu ambaye ni dhaifu kimwili, hasa katika enzi hiyo ambapo hakukuwa na mashine za kisasa za kurahisisha kazi. (Marko 6:3) Pia, Yesu aliwafukuza ng’ombe, kondoo, na wabadili-fedha kutoka hekaluni, na kuzipindua meza za wabadili-fedha. (Yohana 2:14, 15) Jambo hili pia huonyesha kwamba Yesu alikuwa mwanamume mwenye nguvu.
Katika miaka yake mitatu na nusu ya mwisho duniani, Yesu alitembea mamia ya kilometa katika safari zake za kuhubiri. Na bado, mitume wake hawakumdokezea kamwe “apumzike kidogo.” Badala ya hivyo, Yesu aliwaambia, baadhi yao wakiwa wavuvi wenye nguvu: “Njoni, nyinyi wenyewe, kwa faragha mwingie katika mahali pa upweke mpumzike kidogo.”—Marko 6:31.
Kwa kweli, “simulizi lote la kievanjeli,” yasema Cyclopædia ya M’Clintock na Strong “laonyesha [Yesu alikuwa na] afya timamu na yenye nguvu kimwili.” Basi kwa nini alihitaji msaada wa kubeba mti wake wa mateso, na kwa nini alikufa kabla ya wale wengine waliotundikwa mtini pamoja naye?
Jambo moja kubwa ni taabu ya kupita kiasi. Wakati wa kuuawa kwa Yesu ulipokaribia, alisema: “Kwa kweli, nina ubatizo wa kubatizwa kwao, na jinsi ninavyotaabishwa mpaka umalizike!” (Luka 12:50) Taabu hiyo ikawa “maumivu makali,” kwenye usiku wake wa mwisho: “Akiingia katika maumivu makali akaendelea kusali kwa bidii zaidi; na jasho lake likawa kama matone ya damu yakianguka kwenye ardhi.” (Luka 22:44) Yesu alijua kwamba matazamio ya wanadamu ya kupata uhai wa milele yalitegemea kushika kwake ukamilifu mpaka kifo. Jinsi ulivyokuwa mzigo mzito kubeba! (Mathayo 20:18, 19, 28) Pia alijua kwamba angeuawa kama mhalifu ‘aliyelaaniwa’ na watu wa Mungu wenyewe. Hivyo, alisumbuka kwamba jambo hili lingeleta suto kwa Baba yake.—Wagalatia 3:13; Zaburi 40:6, 7; Matendo 8:32.
Baada ya kusalitiwa, alitendwa kwa ukatili sana. Katika jaribio lenye dhihaka lililofanywa baada ya usiku wa manane, maofisa waliokuwa na nyadhifa kubwa zaidi katika nchi walimdhihaki, wakamtemea mate, na kumpiga kwa makonde. Ili kutolea udhuru uhalali wa jaribio la usiku, kulikuwa na jaribio jingine asubuhi iliyofuata. Hapo Yesu alihojiwa na Pilato; kisha Herode, ambaye pamoja na askari wake, walimdhihaki; halafu akadhihakiwa tena na Pilato. Hatimaye, Pilato alifanya apigwe mijeledi. Na hayo hayakuwa mapigo ya kawaida. Kichapo The Journal of the American Medical Association kilisema hivi kuhusu zoea la Waroma la kupiga mijeledi:
“Kifaa cha kawaida kilikuwa mjeledi mfupi . . . wenye mikanda ya ngozi iliyosokotwa yenye urefu mbalimbali, ambapo mipira midogo ya chuma au vipande vyenye ncha kali vya mifupa ya kondoo vilifungiwa mikanda mbalimbali. . . . Askari Waroma walipomcharaza mtu mgongoni kwa nguvu zote, mipira hiyo ya chuma ingemfanya mtu avimbe, na mikanda ya ngozi na mifupa ya kondoo ingekata ndani ya ngozi kutia na tishu zilizo chini ya ngozi. Kisha, kupigwa viboko kulipoendelea, majeraha hayo yangefikia misuli ya mifupa na kutokeza nyuzinyuzi za nyama zenye kuvuja damu.”
Kwa wazi, ni lazima nguvu za Yesu zingekuwa zikidhoofika muda mrefu kabla hajadidimia akiwa amebeba mti wa mateso uliokuwa mzito. Kwa kweli, The Journal of the American Medical Association kilisema: “Kutendwa vibaya kimwili na kiakili na Wayahudi na Waroma, vilevile kukosa chakula, maji, na usingizi, pia kulichangia hali yake dhaifu kwa ujumla. Kwa hiyo, kabla hata ya kusulubiwa kwenyewe, hali ya kimwili ya Yesu angalau ilikuwa mbaya na labda hatarini.”
Je, Sura Yake Ni ya Maana?
Kutoka picha bandia ya Lentulus hadi michoro ya wasanii mashuhuri hadi madirisha ya sasa yenye vioo vilivyotiwa rangi, yaonekana Jumuiya ya Wakristo inapendezwa na picha zinazovutia macho. “Nguvu zenye kuamsha hisia zisizo na kifani za sanamu ya Yesu Kristo zapasa kudumishwa,” akasema askofu mkuu wa Turin, mtunzi wa Sanda ya Turin.
Na bado, Neno la Mungu hukosa kutaja kimakusudi mambo hayo yenye “kuamsha hisia” juu ya sura ya Yesu. Kwa nini? Yaelekea yangepotosha fikira za watu kuelekea kinachomaanishwa na uhai wa milele—ujuzi wa Biblia. (Yohana 17:3) Yesu mwenyewe—aliye kigezo chetu—‘hatazami,’ au kuona “kuonekana kwa mtu kwa nje,” kuwa kwa maana. (Mathayo 22:16; linganisha Wagalatia 2:6.) Kukazia sura ya Yesu ambayo haitajwi kamwe katika Gospeli zenye pumzi ya Mungu ni kupinga makusudio yake. Kwa kweli, kama tutakavyoona katika makala inayofuata, Yesu hata hafanani tena na umbo la kibinadamu.a
[Maelezo ya Chini]
a Bila shaka, katika funzo la Biblia, si kosa kutumia picha zinazotia ndani Yesu. Mara nyingi picha hizi hutokea katika vichapo vya Watch Tower Society. Hata hivyo, hakuna jaribio lolote ambalo hufanywa kusababisha mambo ya kifumbo, kumtia kicho mtazamaji, au kuendeleza dhana, ishara, au utukuzo usiokuwa wa Kimaandiko.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kristo dhaifu, mgonjwa-mgonjwa kama achorwavyo na wasanii wa Jumuiya ya Wakristo kwa kutofautishwa na picha ya Yesu inayotegemea masimulizi ya Biblia
[Hisani]
Jesus Preaching at the Sea of Galilee by Gustave Doré