Maoni ya Biblia
Je, Ni Wafalme Watatu Waliomzuru Yesu Huko Bethlehemu?
BAADA ya Yesu kuzaliwa, watu mashuhuri kutoka Mashariki walifika Bethlehemu ili kumsujudia akiwa mfalme wa Wayahudi. Watu wengi wanaosherehekea Krismasi ulimwenguni pote hukumbuka ziara hiyo hadi leo.
Katika maeneo fulani watu hujenga mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu zinazoonyesha wale wageni wa kutoka Mashariki wakiwa wafalme na wakimkaribia Yesu aliyezaliwa karibuni wakiwa na zawadi. Katika nchi nyingine, watoto hutembea mitaani wakiwa na mavazi ya “Wafalme Watakatifu.” Hata baada ya karne 20 kupita, watu kila mahali wangali wanakumbuka wageni hao wasio wa kawaida. Lakini walikuwa nani?
Je, Walikuwa Wafalme?
Rekodi ya historia ya tukio hilo iko katika kitabu cha Biblia cha Mathayo. Hapo twasoma hivi: “Baada ya kuzaliwa kwa Yesu . . . wanajimu kutoka mashariki walifika siku moja Yerusalemu wakauliza, ‘Yuko wapi mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa? Tuliiona nyota yake ilipotokea nasi tumekuja kumsujudia.’” (Mathayo 2:1, 2, New American Bible) Kwa nini tafsiri hii ya Biblia inawaita wageni hao kutoka mashariki wanajimu wala si wafalme?
Maandiko hapa yanatumia wingi wa neno la Kigiriki maʹgos. Tafsiri mbalimbali za Biblia hulifasiri kuwa “wanaume wenye hekima,” “wanajimu,” au “wataalamu wa nyota” au hulinukuu tu kuwa “magi.” Neno hilo hurejezea wale wanaotoa shauri na kutabiri kwa kutegemea mwendo wa nyota na sayari. Kwa hiyo, Biblia huwataja wageni waliozuru Bethlehemu kuwa waaguzi, waliozoea mambo ya kimafumbo yaliyokatazwa na Mungu.—Kumbukumbu la Torati 18:10-12.
Je, walikuwa wafalme pia? Iwapo walikuwa, ni jambo la kiakili kutarajia kwamba Biblia ingewataja kuwa wafalme. Andiko la Mathayo 2:1-12 hutumia neno “mfalme” mara nne, mara moja likimrejezea Yesu na mara tatu likimrejezea Herode. Lakini haliwaiti wale Magi wafalme hata mara moja. Kuhusiana na jambo hilo kichapo The Catholic Encyclopedia chataarifu: “Hakuna Mwanzilishi wa Kanisa aliyewaona Magi hao kuwa wafalme.” Wala Biblia haiwaoni hivyo.
Je, Walikuwa Watatu?
Idadi ya Magi hao haitajwi na rekodi ya Biblia. Hata hivyo, mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu na nyimbo za Krismasi hutetea pokeo la kawaida la kwamba walikuwa watatu. Kwa wazi pokeo hilo latokana na wazo la kwamba kulikuwa na zawadi za aina tatu. Biblia hutaarifu hivi kuhusu zawadi hizo: “Pia wakafungua hazina zao na kumtolea [Yesu] zawadi, dhahabu na ubani na manemane.”—Mathayo 2:11.
Je, ni jambo la kiakili kukata kauli kwamba kwa kuwa zawadi zilizotolewa na hao Magi zilikuwa za aina tatu, lazima wawe walikuwa Magi watatu? Acheni tuchunguze simulizi la mgeni mwingine mashuhuri aliyezuru Israeli. Wakati mmoja malkia wa Sheba alimzuru Mfalme Solomoni akamtolea “manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani.” (1 Wafalme 10:2) Ijapokuwa zawadi za aina tatu zinatajwa, mtu pekee anayetajwa kuwa alizitoa ni malkia wa Sheba. Idadi ya zawadi alizotoa haionyeshi kwamba watu watatu walimzuru Solomoni katika pindi hiyo. Vivyo hivyo, zawadi tatu alizopewa Yesu hazionyeshi idadi ya watu waliozileta.
Kichapo cha The Catholic Encyclopedia chasema: “Simulizi la Gospeli halitaji idadi ya Magi, wala pokeo fulani hususa kuhusu idadi yao. Baadhi ya Waanzilishi wa Kanisa hutaja Magi watatu; yaelekea sana kwamba wanategemea idadi ya zawadi.” Chaendelea kusema kwamba michoro fulani ya sanaa huonyesha wawili, watatu, wanne, na hata wanane wakimzuru Yesu. Mapokeo fulani hutaja 12. Kwa kweli hakuna njia ya kuthibitisha idadi ya hao Magi.
Simulizi Linalopendwa Sana Lisilo Sahihi
Kinyume cha itikadi ya kawaida, Magi hao walifika kwanza Yerusalemu wala si Bethlehemu baada ya Yesu kuzaliwa. Hawakuwapo Yesu alipozaliwa. Baadaye, walipoenda Bethlehemu, Biblia husema kwamba “walipoenda ndani ya ile nyumba wakaona huyo mtoto mchanga.” (Mathayo 2:1, 11) Kwa hiyo, ni wazi kwamba Magi hao walipomzuru Yesu, familia yake ilikuwa tayari imeshahamia nyumba ya kawaida. Hawakumkuta akiwa amelala kwenye hori.
Kupatana na Maandiko, lile simulizi linalopendwa sana na wengi la wafalme watatu wakimheshimu Yesu alipozaliwa si sahihi. Kama ilivyotajwa juu, Biblia hufundisha kwamba Magi waliomzuru Yesu hawakuwa wafalme bali wanajimu waliozoea mambo ya mafumbo. Maandiko hayasemi walikuwa wangapi. Pia, hawakumzuru Yesu punde baada ya kuzaliwa, alipolazwa horini, badala yake, walimzuru baadaye, familia yake ilipokuwa inaishi katika nyumba.
Simulizi linalopendwa sana na wengi la wafalme watatu na masimulizi mengine ya kidesturi ya Krismasi, kwa kawaida huonwa kuwa hadithi tu zisizodhuru za sikukuu ingawa hazipatani na Maandiko. Hata hivyo, Wakristo hustahi sana namna ya ibada isiyohusisha uwongo. Hivi ndivyo Yesu mwenyewe alivyohisi. Pindi moja alisema hivi katika sala kwa Baba yake: “Neno lako ni kweli.” (Yohana 17:17) Alisema kwamba ‘waabudu wa kweli watamwabudu Baba kwa roho na kweli, kwa maana, kwa kweli, Baba anawatafuta wa namna hiyo wamwabudu yeye.’—Yohana 4:23.
[Picha katika ukurasa wa 15]
“Magi wamsujudia”y