Kuzaliwa Kunakokumbukwa
‘Leo amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.’—Luka 2:11, “Union Version.”
MIAKA elfu mbili hivi iliyopita, mwanamke mmoja katika mji wa Bethlehemu alijifungua mtoto wa kiume. Wakaaji wachache tu ndio waliotambua umuhimu wa kuzaliwa huko. Lakini wachungaji fulani ambao walikuwa wakichunga makundi yao usiku mashambani, waliona umati wa malaika, nao waliwasikia wakiimba: “Utukufu katika vilele vilivyo juu kwa Mungu, na juu ya dunia amani kati ya watu wa nia njema.”—Luka 2:8-14.
Kisha, wachungaji hao wakampata Maria na mume wake, Yosefu, katika kibanda cha mifugo, kama vile tu malaika walivyowaeleza. Maria ambaye alimwita mtoto huyo Yesu, alikuwa amemlaza ndani ya hori, katika kibanda. (Luka 1:31; 2:12) Sasa, miaka elfu mbili baadaye, yapata sehemu moja ya tatu ya wanadamu hudai kwamba wanamfuata Yesu Kristo. Na yaelekea matukio yanayohusiana na kuzaliwa kwake ndiyo chanzo cha hadithi ambayo huenda imesimuliwa mara nyingi kuliko hadithi nyingine katika historia ya binadamu.
Hispania, nchi ambayo hufuata sana mapokeo ya Kikatoliki na ambayo ina ustadi wa kutayarisha sherehe hizo, imebuni njia nyingi za kusherehekea usiku huo wa pekee huko Bethlehemu.
Jinsi Krismasi Husherehekewa Huko Hispania
Tangu karne ya 13, mandhari ya kuzaliwa kwa Yesu imekuwa mojawapo ya mambo yanayojulikana sana katika sherehe za Kihispania. Familia nyingi hutengeneza mfano wa hori ndogo ambako Yesu alilazwa. Sanamu za udongo hufananisha wachungaji na Mamajusi (au “wafalme watatu”), na vilevile Yosefu, Maria, na Yesu. Mara nyingi mandhari kubwa zaidi zenye sanamu kubwa huwekwa karibu na makao makuu ya halmashauri ya miji wakati wa Krismasi. Yaonekana Francis wa Assisi alianzisha desturi hiyo huko Italia ili kuelekeza fikira za watu kwenye masimulizi ya Injili ya kuzaliwa kwa Yesu. Baadaye, watawa wa kiume wa Mtakatifu Francis walifanya desturi hiyo iwe maarufu huko Hispania na katika nchi nyingine nyingi.
Mamajusi hutimiza sehemu muhimu katika Sherehe za Krismasi huko Hispania, kama vile Baba Krismasi katika nchi nyingine. Huko Hispania, inaaminika kwamba watoto hupokea zawadi zao kutoka kwa Mamajusi Januari 6, Día de Reyes (Siku ya Wafalme), kama vile Mamajusi, kulingana na maoni ya wengi, walivyoleta zawadi kwa Yesu aliyetoka kuzaliwa. Hata hivyo, ni watu wachache wanaojua kwamba masimulizi ya Injili hayataji ni Mamajusi wangapi waliomtembelea Yesu. Badala ya kuwa wafalme, wao wanajulikana kwa usahihi zaidi kuwa wanajimu.a Isitoshe, baada ya ziara ya Mamajusi, Herode aliwaua watoto wote wa kiume huko Bethlehemu “kuanzia umri wa miaka miwili kwenda chini,” akijaribu kumuua Yesu. Hilo linaonyesha kwamba ziara yao ilifanyika muda fulani baada ya kuzaliwa kwa Yesu.—Mathayo 2:11, 16.
Tangu karne ya 12, miji fulani ya Hispania imekuwa na michezo ya kuigiza ya kuzaliwa kwa Yesu, kutia ndani ziara ya wachungaji huko Bethlehemu na baadaye ile ya Mamajusi. Siku hizi, majiji mengi ya Hispania huwa na cabalgata, au msafara kila Januari 5, ambapo “wafalme watatu” hupitishwa katikati ya mji kwa magari yaliyopambwa na ambayo yana jukwaa, huku wakiwapa watazamaji peremende. Mapambo yanayotumiwa wakati wa Krismasi na villancicos (nyimbo) hufanya sherehe hizo ziwe zenye kuchangamsha.
Familia nyingi za Hispania hupenda kula mlo wa jioni wa pekee Usiku wa Kuamkia Krismasi (Desemba 24). Chakula kinacholiwa wakati huo hutia ndani turrón (peremende zilizotengenezwa kwa lozi na asali), keki ya unga wa mlozi na sukari, matunda yaliyokaushwa, nyama ya kuchomwa ya kondoo, na chakula kinachotoka baharini. Huenda washiriki wa familia, hata wale wanaoishi mbali, wakafanya jitihada ya pekee kukutana kwa ajili ya pindi hiyo. Wakati wa chakula kingine ambacho huliwa Januari 6, familia hula roscón de reyes, keki ya mviringo ya “Wafalme” ambayo ina sorpresa (sanamu ndogo) iliyofichwa ndani yake. Desturi kama hiyo katika siku za Waroma ilimwezesha mtumwa aliyepata kipande cha keki chenye sanamu iliyofichwa awe “mfalme” kwa siku moja.
“Wakati Wenye Furaha na Shughuli Zaidi Katika Mwaka”
Sasa Krismasi imekuwa sherehe kuu ulimwenguni pote bila kujali desturi za mahali. Kitabu The World Book Encyclopedia kinaeleza Krismasi kuwa “wakati wenye furaha na shughuli zaidi katika mwaka kwa mamilioni ya Wakristo na wale wasio Wakristo ulimwenguni pote.” Je, sherehe hiyo ina faida yoyote?
Ni wazi kwamba kuzaliwa kwa Kristo kulikuwa tukio muhimu. Kwa kuwa malaika walitangaza kuzaliwa huko kuwa dalili ya “amani kati ya watu wa nia njema,” hilo linaonyesha waziwazi umuhimu wake.
Hata hivyo, “katika siku za mapema za Ukristo, hakukuwa na sherehe zenye Mandhari ya Kuzaliwa kwa Yesu,” asema mwandishi-habari Mhispania Juan Arias. Ikiwa ndivyo ilivyo, basi sherehe ya Krismasi ilitoka wapi? Ni njia gani iliyo bora zaidi ya kukumbuka kuzaliwa na maisha ya Yesu? Utapata majibu kwa maswali hayo katika makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Kitabu La Sagrada Escritura—Texto y comentario por profesores de la Compañía de Jesús (Maandiko Matakatifu—Maandishi na Maelezo ya Maprofesa wa Shirika la Yesu) yanasema kwamba “kati ya Waajemi, Wamedi, na Wakaldayo, Mamajusi walifanyiza jamii ya ukuhani ambayo iliendeleza mambo ya uchawi, unajimu, na uganga.” Hata hivyo, kufikia Enzi za Kati, Mamajusi ambao walienda kumwona mvulana Yesu walitangazwa kuwa watakatifu na kupewa majina Melchior, Gaspar, na Balthasar. Na inadaiwa kwamba mabaki yao yamehifadhiwa katika kanisa kuu la Cologne, Ujerumani.