Maji Halisi na ya Kiroho Ni Muhimu kwa Uhai
ZAIDI ya miaka 2,000 iliyopita, jiji moja mashuhuri lenye wakazi 30,000 lilisitawi katika Jangwa la Arabia. Ijapokuwa jiji hilo la Petra lilikuwa na ukame, na kwa wastani lilipata mvua yenye kipimo cha milimeta 150 kwa mwaka, wakazi wake walizoea kuishi bila maji ya kutosha. Jiji la Petra lilisitawi sana na kuwa na ufanisi.
Wakazi wa Petra (Wanabatea) hawakuwa na mashine za umeme za kupiga maji. Hawakujenga mabwawa makubwa ya maji. Hata hivyo, walijua jinsi ya kuvuta na kuhifadhi maji. Walisambaza maji jijini na kwenye mashamba yao madogo kwa mifereji, mabwawa, na matangi ya kuhifadhia maji. Walihifadhi maji kwa udi na uvumba. Walijenga visima na matangi yao kwa njia nzuri sana hivi kwamba Wabedui wa kisasa bado huyatumia.
“Mfumo wa maji wa Petra unavutia ajabu,” asema mtaalamu mmoja wa maji kwa mshangao. ‘Wakazi wa Petra walikuwa na akili na uwezo usio wa kawaida.’ Hivi karibuni, wataalamu wa Israeli wamejaribu kuiga ustadi wa wakazi hao wa Petra. Wakazi hao walikuza mimea katika Negebu, ambako mvua isiyozidi milimeta 100 hunyesha kila mwaka. Wataalamu wa kilimo wamechunguza maelfu ya mashamba madogo yaliyosalia ya wakazi hao. Wakazi hao walikusanya maji ya mvua kwa ustadi kupitia mifereji na kuyaelekeza kwenye mashamba yao.
Tayari wakulima wanaoishi kwenye nchi zenye ukame katika jangwa la Sahel barani Afrika wanatumia mbinu za wakazi wa Petra. Hata hivyo, mbinu za kisasa za kuhifadhi maji zina matokeo pia. Katika Lanzarote, kimojawapo cha Visiwa vya Canary, kilicho karibu na pwani ya Afrika, wakulima wamejifunza kukuza zabibu na tini kwenye maeneo yasiyopata mvua kabisa. Wao hupanda mizabibu au mitini ndani ya mashimo halafu hutia majivu ya volkano juu ya udongo ili kuzuia maji yasiwe mvuke. Umande wa kutosha hutiririka mizizini na hivyo wanavuna kwa wingi.
Utatuzi kwa Kutumia Mbinu Sahili
Kotekote ulimwenguni watu fulani wamefaulu kuishi kwenye maeneo yenye ukame—kutia ndani Wabishnoi, wanaoishi kwenye Jangwa la Thar huko India; wanawake Waturkana wanaoishi Kenya; na Wahindi wa Navajo wanaoishi Arizona, Marekani. Mbinu wanazotumia kukusanya maji ya mvua, ambazo wamejifunza kwa karne nyingi, zinawasaidia kujiruzuku kupitia kilimo kuliko mbinu za kisasa za tekinolojia.
Mabwawa mengi yalijengwa katika karne ya 20. Watu walitumia maji ya mito mikubwa, na mifumo mikubwa ya umwagiliaji-maji mashamba ilibuniwa. Mwanasayansi mmoja akadiria kwamba asilimia 60 ya mito na vijito vyote ulimwenguni vimedhibitiwa kwa njia fulani. Ijapokuwa miradi hiyo ilileta manufaa fulani, wataalamu wa mazingira na viumbe wanaeleza jinsi ambavyo mazingira yameharibiwa na jinsi ambavyo mamilioni ya watu wameathiriwa baada ya kupoteza makao yao.
Isitoshe, wakulima wanaohitaji maji sana hawafaidiki kutokana na miradi hiyo iliyoanzishwa kwa makusudi mazuri. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa India Rajiv Gandhi alisema hivi kuhusiana na miradi ya umwagiliaji-maji mashamba nchini humo: “Kwa miaka 16 tumetumia pesa nyingi. Watu hawajafaidika kwa vyovyote, mashamba hayamwagiliwi maji, hakuna maji, uzalishaji haujaongezeka, maisha ya watu yangali magumu.”
Kwa upande mwingine, mbinu sahili za kilimo ziliboresha hali na hazikuharibu mazingira. Vidimbwi vidogo na mabwawa milioni sita yaliyojengwa na jumuiya yamewasaidia sana watu nchini China. Nchini Israel, watu wamegundua kwamba maji yaliyotumiwa nyumbani yanaweza kutumiwa tena katika kilimo cha umwagiliaji-maji mashamba.
Mbinu nyingine inayofanya kazi ni kudondosha matone ya maji mashambani (drip irrigation). Mbinu hiyo huhifadhi udongo na hutumia asilimia 5 tu ya maji yanayotumiwa katika mbinu za kawaida za kumwagilia maji mashamba. Kutumia maji kwa hekima kwamaanisha pia kupanda mazao ambayo yanasitawi katika maeneo yenye ukame, kama vile mawele au mtama, badala ya mazao yanayohitaji maji mengi, kama vile miwa au mahindi.
Wale walio nyumbani na viwandani wanaweza kujitahidi kupunguza kiasi cha maji wanachotumia. Kwa mfano, kilogramu moja ya karatasi inaweza kutengenezwa kwa lita moja hivi ya maji ikiwa kiwanda kinasafisha na kutumia maji yaleyale—na hivyo kuhifadhi zaidi ya asilimia 99 ya maji. Jiji la Mexico City limeacha kutumia vyoo vya kawaida na badala yake linatumia vyoo vinavyotumia theluthi ya maji waliyotumia mbeleni. Jiji hilo pia lilifadhili kampeni ya kuelimisha watu ili kupunguza matumizi ya maji.
Utatuzi Unategemea Nini?
Utatuzi wa matatizo ya maji—na matatizo mengi ya mazingira—unategemea kubadili mitazamo. Watu wanahitaji kushirikiana badala ya kuwa na ubinafsi, kujidhabihu iwezekanapo, na kuazimia kutunza dunia kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kuhusiana na hilo Sandra Postel, aeleza hivi katika kitabu chake Last Oasis—Facing Water Scarcity: “Tunahitaji kuwa na kanuni za maji—ili kutusaidia kutenda ifaavyo tunapokabili maamuzi magumu kuhusu mifumo ya asili ambayo hatuelewi na tusiyoweza kuelewa kikamili.”
Bila shaka, ni lazima hizo “kanuni za maji” zimhusu kila mtu. Nchi zinahitaji kushirikiana na nchi jirani, kwa kuwa mito hutiririka katika nchi mbalimbali. Ismail Serageldin asema hivi katika ripoti yake Beating the Water Crisis (Kutatua Tatizo la Maji): “Sasa ni lazima mahangaiko kuhusu kiasi na hali ya maji—mambo ambayo hapo awali yalionwa kuwa hayahusiani—yaonwe kuwa matatizo yanayoathiri ulimwengu wote.”
Lakini Katibu-Mkuu wa UM Kofi Annan akiri kwamba kuunganisha mataifa ili yashughulikie matatizo yanayoathiri ulimwengu wote si kazi rahisi. Asema hivi: “Mbinu zilizopo leo za kutatua tatizo la maji ulimwenguni pote ni za hali ya chini sana. Huu ndio wakati ufaao wa kuzingatia kwa uzito wazo la ‘jamii ya kimataifa.’”
Kwa wazi, kuwa na afya bora na maisha yenye furaha hakutegemei kuwa na maji safi ya kutosha peke yake—japo maji ni muhimu. Ni lazima wanadamu watambue wajibu wao kwa Yule aliye chanzo cha maji na uhai. (Zaburi 36:9; 100:3) Na badala ya kutumia vibaya dunia na rasilimali zake, wanahitaji ‘kuilima na kuitunza,’ kama Muumba wetu alivyowaagiza wazazi wetu wa kwanza.—Mwanzo 2:8, 15; Zaburi 115:16.
Maji Bora Zaidi
Kwa kuwa maji ni muhimu sana, si ajabu kwamba Biblia huyatumia kwa njia ya mfano. Kwa kweli, ili kufurahia maisha kama ilivyokusudiwa, ni lazima tutambue chanzo cha maji hayo ya mfano. Ni lazima tujifunze pia kuwa na mtazamo kama ule wa mwanamke aliyeishi katika karne ya kwanza aliyemwomba hivi Yesu Kristo: “Bwana, nipe maji hayo.” (Yohana 4:15) Fikiria jambo lililotukia.
Yesu alisimama penye kisima chenye kina kirefu karibu na mji wa kisasa wa Nablus. Mara nyingi watu kutoka kote ulimwenguni hutembelea kisima hicho hata leo. Wakati huo, mwanamke Msamaria alifika pia kisimani. Kama wanawake wengi walioishi karne ya kwanza, bila shaka alienda mara nyingi kuteka maji kisimani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Lakini Yesu alimwambia kwamba angempa “maji yaliyo hai”—maji ambayo yatabubujika milele.—Yohana 4:10, 13, 14.
Kwa wazi, mwanamke huyo alipendezwa na habari hiyo. Lakini, bila shaka, “maji yaliyo hai” ambayo Yesu alirejezea hayakuwa maji halisi. Yesu alikuwa akizungumzia maandalizi ya kiroho ambayo yatawawezesha watu kuishi milele. Hata hivyo, kuna uhusiano kati ya maji halisi na maji ya mfano—tunahitaji yote ili kufurahia maisha kikamilifu.
Pindi kwa pindi, Mungu aliwapa watu wake maji halisi kulipokuwa na ukosefu wa maji. Kwa mwujiza aliuandalia umati mkubwa wa Waisraeli wakimbizi maji walipokuwa wakivuka jangwa la Sinai kuelekea Bara Lililoahidiwa. (Kutoka 17:1-6; Hesabu 20:2-11) Elisha, nabii wa Mungu, alikitakasa kisima cha Yeriko kilichokuwa na maji machafu. (2 Wafalme 2:19-22) Na mabaki ya Waisraeli wenye kutubu waliporejea nyumbani kutoka Babiloni, Mungu aliwapa “maji jangwani.”—Isaya 43:14, 19-21.
Dunia inahitaji kwa haraka ugavi usiokwisha wa maji leo. Kwa kuwa Muumba wetu, Yehova Mungu, alitatua matatizo ya maji hapo kale, je, hatafanya hivyo wakati ujao? Biblia inatuhakikishia kwamba atafanya hivyo. Mungu aeleza hivi kuhusu hali zitakazoletwa na Ufalme ambao ameahidi: “Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji, . . . ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa BWANA ndio uliofanya jambo hilo.”—Isaya 41:18, 20.
Biblia inatuahidi kwamba wakati huo, watu “hawataona njaa, wala hawataona kiu.” (Isaya 49:10) Utawala mpya wa dunia utatatua kabisa tatizo la maji. Utawala huo—Ufalme, ambao Yesu alitufundisha kusali juu yake—utategemezwa “kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele.” (Isaya 9:6, 7; Mathayo 6:9, 10) Tokeo ni kwamba mwishowe watu wote duniani watakuwa jamii ya kimataifa ya kweli.—Zaburi 72:5, 7, 8.
Tukitafuta maji ya kiroho sasa, tutakuwa na tumaini la kuishi wakati ambapo kila mtu atakuwa na maji ya kutosha kabisa.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Juu: Wakazi wa kale wa Petra walijua kuhifadhi maji
Chini: Mfereji wa maji uliojengwa na Wanabatea huko Petra
[Hisani]
Garo Nalbandian
[Picha katika ukurasa wa 10]
Wakulima kwenye kimojawapo cha Visiwa vya Canary wamejifunza kukuza mimea kwenye maeneo yasiyopata mvua kabisa
[Picha katika ukurasa wa 13]
Yesu alimaanisha nini alipoahidi kumpa huyo mwanamke “maji yaliyo hai”?