Kitabu Cha Biblia Namba 1—Mwanzo
Mwandikaji: Musa
Mahali Kilipoandikiwa: Jangwani
Uandikaji Ulikamilishwa: 1513K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: “Katika mwanzo” mpaka 1657
1. Ni nini baadhi ya vichwa muhimu ambavyo vyazungumzwa katika Mwanzo?
WAZIA ukichukua kitabu chenye sura fupi 50 na kukuta ndani ya ukurasa wa kwanza au wa pili simulizi lililo sahihi peke yake la historia ya mapema zaidi ya binadamu na maandishi yanayoonyesha uhusiano wa binadamu kwa Mungu, Muumba wake, na pia kwa dunia pamoja na makumi ya maelfu ya viumbe vyayo! Katika kurasa hizo chache, pia, wapata muono-ndani wenye kina kirefu wa kusudi la Mungu la kuweka binadamu duniani. Usomapo mbele kidogo, wagundua ni kwa nini binadamu hufa na sababu ya hali ya sasa yenye msukosuko, nawe unapata maarifa kuhusu msingi halisi wa imani na wa tumaini, hata kuhusu kutambulisha chombo cha Mungu cha ukombozi—Mbegu (Uzao) ya ahadi. Kitabu cha kutokeza chenye mambo hayo yote ni Mwanzo, cha kwanza cha vile vitabu 66 vya Biblia.
2. Ni nini maana ya jina Mwanzo, na ni sehemu ya kwanza ya nini?
2 “Mwanzo” humaanisha “Asili; Uzawa,” jina hilo likiwa limetolewa kwa tafsiri ya Kigiriki ya Septuagint ya kitabu hicho. Katika hati za Kiebrania, kichwa hicho ni neno la utangulizi, Bere’·shithʹ, “katika mwanzo” (Kigiriki, en ar·kheiʹ). Mwanzo ndicho kitabu cha kwanza cha Pentateuki (neno la Kigiriki lililotoholewa kwa Kiswahili linalomaanisha “makunjo matano” au “buku lenye mijumlisho mitano”). Kwa wazi hapo awali kilikuwa kitabu kimoja kilichoitwa Tora (Sheria) au “kitabu cha torati ya Musa” lakini baadaye kikagawanywa kuwa makunjo matano ili iwe rahisi kukitumia.—Yos. 23:6; Ezra 6:18.
3. (a) Ni nani Mtungaji wa Mwanzo, lakini ni nani alikiandika? (b) Yawezekana Musa alipataje habari aliyotia ndani ya Mwanzo?
3 Yehova Mungu ndiye Mtungaji wa Biblia, lakini alimpulizia Musa aandike kitabu cha Mwanzo. Musa alipataje habari aliyoandika katika Mwanzo? Baadhi yayo yaweza kuwa ilipokewa moja kwa moja kupitia ufunuo wa kimungu na nyingine, chini ya mwelekezo wa roho takatifu, kupitia kupokezwa kwa kinywa. Yawezekana pia kwamba Musa alikuwa na hati zilizoandikwa ambazo zilihifadhiwa na mababu wake kuwa maandishi ya bei kubwa yenye thamani juu ya asili za ainabinadamu.a
4. (a) Ni wapi na ni wakati gani Musa alipokamilisha uandikaji wake? (b) Ni jinsi gani Musa angeweza kupata habari aliyotia katika kisehemu cha mwisho cha Mwanzo?
4 Yawezekana ilikuwa katika jangwa la Sinai mwaka 1513 K.W.K. ndiko Musa, chini ya upulizio wa Mungu, alikamilisha maandishi yake. (2 Tim. 3:16; Yn. 5:39, 46, 47) Musa alipata wapi habari ya sehemu ya mwisho ya Mwanzo? Kwa kuwa Lawi babu mkuu wake alikuwa ndugu nusu ya Yusufu, habari hizo za kindani zingejulikana kwa usahihi ndani ya familia yake mwenyewe. Hata huenda ikawa Lawi alikuwa angali hai wakati wa baba ya Musa, Amramu. Na zaidi, roho ya Yehova kwa mara nyingine ingehakikisha kuandikwa kwa usahihi kisehemu hiki cha Maandiko.—Kut. 6:16, 18, 20; Hes. 26:59.
5. Ni ushuhuda gani wa ndani ya Biblia unaothibitisha uandikaji wa Musa?
5 Hakuna shaka juu ya aliyeandika Mwanzo. “Kitabu cha torati ya Musa” na marejezo kama hilo kuhusu vitabu vitano vya kwanza vya Biblia, kimoja kikiwa ni Mwanzo, yanapatikana mara nyingi tangu wakati wa mwandamizi wa Musa, Yoshua, na kuendelea. Kwa kweli, kuna marejezo yapatayo 200 juu ya Musa katika vitabu 27 vya baadaye vya Biblia. Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo yanamtaja Musa mara nyingi kuwa mwandikaji wa “torati,” ushuhuda wa kutia tamati ukiwa ule wa Yesu Kristo. Musa aliandika kwa kuamriwa na Yehova moja kwa moja na chini ya upulizio Wake.—Kut. 17:14; 34:27; Yos. 8:31; Dan. 9:13; Luka 24:27, 44.
6. Ni nini kinachodokeza kwamba kuandika kulianza mapema katika historia ya kibinadamu?
6 Watia-shaka fulani wameuliza, Lakini Musa na waliomtangulia waliwezaje kuandika? Je! kuandika hakukuwa tukio la kibinadamu lililositawi baadaye? Kwa wazi mwanzo wa kuandika ulikuwa mapema katika historia ya kibinadamu, labda kabla ya Gharika ya siku za Nuhu, iliyotukia katika 2370 K.W.K. Je! kuna ushuhuda wowote kwamba binadamu aliweza kuandika mapema? Ingawa ni kweli kwamba waakiolojia (wabukuzi wa vitu vya kale) wamesema mabamba fulani ya matope ambayo wamechimbua ni ya tarehe za mapema zaidi kabla ya 2370 K.W.K., tarehe hizo ni za kukisia tu. Hata hivyo, yapasa kuangaliwa kwamba Biblia inaonyesha waziwazi kwamba ujenzi wa majiji, usitawi wa vyombo vya kimuziki, na ufuaji wa vyombo vya chuma ulianza mapema mno kabla ya Gharika. (Mwa. 4:17, 21, 22) Basi, ni jambo la akili wanadamu hawangeona ni vigumu sana kusitawisha mbinu fulani ya kuandika.
7. Ni ushuhuda gani wa ki-nchi uliopo wa gharika ya tufe lote na wa matawi matatu ya mbari ya kibinadamu, kama inavyosimuliwa katika simulizi la Biblia?
7 Katika mambo mengine mengi, Mwanzo kimethibitisha kuwa kinakubaliana kiajabu na mambo ya hakika yaliyothibitishwa. Ni Mwanzo pekee kinachotoa simulizi la kweli na la uhakika juu ya Furiko na waokokaji walo, ingawa masimulizi ya gharika fulani na kuokoka kwa binadamu (katika visa vingi likiwa ni tokeo la kuhifadhiwa ndani ya merikebu) yanapatikana katika hadithi za mapokeo ya matawi mengi ya familia za kibinadamu. Simulizi la Mwanzo vilevile laonyesha mianzo ya makao ya matawi tofauti-tofauti ya ainabinadamu, kutokana na wana watatu wa Nuhu—Shemu, Hamu, na Yafethi.b Asema hivi Dakt. Melvin G. Kyle, wa Seminari ya Kitheolojia ya Xenia, Missouri, U.S.A.: “Haikanushiki kwamba kutoka kitovu fulani, mahali fulani katika Mesopotamia, tawi la Hamu la mbari lilihamia kusini-magharibi, tawi la Yafethi hadi kaskazini-magharibi, na tawi la Shemu ‘upande wa mashariki’ kuelekea ‘bara la Shinari.’”c
8. Ni aina gani nyingine za ushuhuda zinazothibitisha uasilia wa Mwanzo?
8 Uasilia wa Mwanzo kuwa sehemu ya maandishi ya kimungu waonyeshwa pia na upatani wacho wa ndani, na pia ukubaliano wacho kamili pamoja na Maandiko yale mengine yaliyopuliziwa na Mungu. Ufichuzi wacho unaonyesha mwandikaji aliyemhofu Yehova na kupenda kweli na ambaye bila kusita aliandika juu ya dhambi za taifa na wale waliokuwa mashuhuri katika Israeli. Zaidi ya yote, usahihi usio na kigeugeu ambao unabii mbalimbali umekuja kutimizwa, kama itakavyoonyeshwa kuelekea mwisho wa sura hii, hutia alama Mwanzo kuwa kielelezo cha kutokeza cha maandishi yaliyopuliziwa na Yehova Mungu.—Mwa. 9:20-23; 37:18-35; Gal. 3:8, 16.
YALIYOMO KATIKA MWANZO
9. (a) Ni nini kinachosimuliwa katika sura ya ufunguzi ya Mwanzo kuhusu uumbaji wa Mungu? (b) Ni habari gani zaidi ambazo zatolewa na sura ya pili kuhusu binadamu?
9 Uumbaji wa mbingu na dunia, na kutayarishwa kwa dunia kuwa makao ya binadamu (1:1–2:25). Kwa wazi kikirudisha nyuma kwenye mabilioni ya miaka ya wakati, Mwanzo kinafungua kwa njia nyepesi yenye kuvutia: “Katika mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.” (NW) Ni jambo la maana kwamba sentensi hiyo ya kwanza inatambulisha kwamba Mungu ni Muumba na uumbaji wake uonekanao ni mbingu na dunia. Kwa maneno yenye fahari, yaliyochaguliwa vizuri, sura ya kwanza inaendelea kutoa simulizi la ujumla juu ya kazi ya kuumba inayohusiana na dunia. Hilo linatimizwa katika vipindi sita vya wakati vinavyoitwa siku, kila kimoja kikianza na jioni, wakati ambao kazi ya kuumba ya kipindi hicho haijatambulika wazi, na kumalizika katika uangavu wa asubuhi, huku utukufu wa kazi ya uumbaji ukiwa wazi zaidi. Katika “siku” za mfululizo nuru inatokea; mtandao wa halianga; bara na majani mabichi; vimulikaji vya kugawanya siku na usiku; samaki na nyuni; na wanyama wa bara na hatimaye binadamu. Hapa Mungu anajulisha sheria yake inayoongoza aina za vitu, kizuizi kisichopitika kinachofanya isiwezekane aina moja kugeuka kuwa nyingine. Akiisha kufanya binadamu katika mfano Wake mwenyewe, Mungu atangaza kusudi Lake lenye kufungamanisha matatu kwa binadamu duniani: kuijaza wazao waadilifu, kuitawala, na kutiisha uumbaji-wanyama. “Siku” ya saba yabarikiwa na kutangazwa kuwa takatifu na Yehova, ambaye sasa anachukua hatua ya ‘kustarehe kwa kazi yake yote aliyoifanya.’ Kisha simulizi hilo latoa muono wa karibu, au uliokuzwa, wa kazi ya uumbaji wa Mungu kuhusu binadamu. Laeleza juu ya bustani ya Edeni na mahali ilipokuwa, laeleza juu ya sheria ya Mungu ya mti uliokatazwa, laeleza juu ya Adamu kuita majina wanyama, na kisha latoa simulizi la Yehova kupanga ndoa ya kwanza kwa kufanya mke kutoka kwa mwili wa Adamu mwenyewe na kumleta kwa Adamu.
10. Mwanzo chaelezaje juu ya chanzo cha dhambi na kifo, na ni kusudi gani la maana lajulishwa hapa?
10 Dhambi na kifo vyaingia ulimwenguni; “mbegu” atabiriwa kuwa mwokozi (3:1–5:5). Mwanamke anakula tunda lililokatazwa na amshawishi mume wake ajiunge naye katika uasi, na kwa hiyo Edeni yanajisiwa kupitia kutokutii. Mungu ataja mara iyo hiyo njia ambayo kwayo kusudi lake litatimizwa: “Na Yehova Mungu akaendelea kunena kwa nyoka [Shetani, mchochezi wa uasi asiyeonekana]: ‘ . . . Na mimi nitaweka uadui kati ya wewe na mwanamke na kati ya mbegu yako na mbegu yake. Yeye atachubua wewe katika kichwa na wewe utachubua yeye katika kisigino.’” (3:14, 15, NW) Binadamu afukuzwa kutoka bustani, akaishi katika maumivu na kazi ya jasho miongoni mwa miiba na michongoma. Hatimaye, ni lazima afe na kurudi kwenye mavumbi alikokuwa ametolewa. Ni wazao wake tu wangeweza kutumaini katika Mbegu aliyeahidiwa.
11. Madhara ya dhambi yaliendeleaje nje ya Edeni?
11 Madhara ya dhambi yaendelea nje ya Edeni. Kaini, mtoto-mwanamume wa kwanza kuzaliwa, awa mwuaji wa nduguye Abeli, mtumishi mwaminifu wa Yehova. Yehova amwondosha Kaini aende kwenye bara la Makimbilio, ambako anazaa wazao waliofagiliwa mbali na Gharika baadaye. Adamu sasa ana mwana mwingine, Sethi, anayekuwa baba yake Enoshi; wakati huo watu waanza kuliitia jina la Yehova kwa unafiki. Adamu afa akiwa na umri wa miaka 930.
12. Dunia yapataje kuharibiwa katika siku za Nuhu?
12 Wanaume na malaika waovu waharibu dunia; Mungu aleta Gharika (5:6–11:9). Nasaba kupitia Sethi yatolewa hapa. Wa kutokeza kati ya wazao hao wa Sethi ni Henoko, ambaye atakasa jina la Yehova kwa “kutembea pamoja na Mungu wa kweli.” (5:22, NW) Mwanamume anayefuata wa imani ya kutokeza ni Nuhu kitukuu wa Henoko, ambaye azaliwa miaka 1,056 baada ya kuumbwa kwa Adamu. Katika wakati huo jambo fulani latokea la kuongeza jeuri katika dunia. Malaika wa Mungu waacha makao yao ya kimbingu ili waoe mabinti warembo wa wanadamu. Unyumba huo usioruhusiwa unatokeza jamii ya mbegu yenye nguvu ya majitu wanaoitwa Wanefili (maana yake “Waangushaji”), wanaofanya jina, si kwa ajili ya Mungu, bali kwa ajili yao wenyewe. Kwa hiyo Yehova atangazia Nuhu kwamba Yeye atafutilia mbali binadamu na wanyama kwa sababu ya ubaya wenye kuendelea wa ainabinadamu. Nuhu pekee ndiye anayepata upendeleo wa Yehova.
13. Yehova atakasaje jina lake sasa?
13 Nuhu awa baba ya Shemu, Hamu, na Yafethi. Jeuri na uharibifu vinapoendelea duniani, Yehova afunulia Nuhu kwamba Yeye yu karibu kutakasa jina Lake kupitia furiko kubwa, na Yeye amwamuru Nuhu ajenge safina ya kuhifadhi, akimpa ramani za ujenzi zenye maelezo marefu. Nuhu afanya hima kutii na kukusanya familia yake ya watu wanane, pamoja na wanyama na ndege; kisha, katika mwaka wa 600 wa maisha yake (2370 K.W.K.), Furiko laanza. Mvua kubwa hiyo yaendelea kwa siku 40, hadi milima yote mirefu inafunikwa kwa dhiraa zipatazo 15 (karibu meta 7) za maji. Wakati, baada ya mwaka mmoja, Nuhu awezapo hatimaye kuongoza familia yake kutoka kwenye safina, tendo lake la kwanza ni kutoa dhabihu kubwa ya shukrani kwa Yehova.
14. Sasa Yehova aamuru na kutoa agano gani, na ni matukio gani yanayojaza maisha ya Nuhu?
14 Yehova sasa ambariki Nuhu na familia yake na kuwaamuru waijaze dunia kwa wazao wao. Amri ya Mungu yaruhusu kula nyama lakini yataka damu iepukwe, ambayo ndiyo nafsi, au uhai, wa mnofu, na yataka mwuaji auawe. Agano la Mungu la kutoleta tena gharika juu ya dunia lathibitishwa na kutokea kwa upinde wa mvua mbinguni. Baadaye, Hamu aonyesha kukosa staha kwa nabii wa Yehova, Nuhu. Ajuapo hilo, Nuhu alaani mwana wa Hamu, Kanaani, lakini aongeza baraka fulani akionyesha kwamba Shemu atapendelewa kipekee na kwamba Yafethi pia atabarikiwa. Nuhu afa akiwa na umri wa miaka 950.
15. Wanadamu wajaribuje kujifanyia jina mashuhuri, na Yehova azuiaje madhumuni yao?
15 Wana watatu wa Nuhu watimiza amri ya Mungu ya kuongezeka, na kuzaa familia 70, wazaaji wa jamii ya kibinadamu ya wakati huu. Nimrodi, mjukuu wa Hamu, hatiwi ndani, kwa wazi kwa sababu awa “mwindaji hodari katika kupinga Yehova.” (10:9, NW) Asimamisha ufalme na kuanza kujenga majiji. Wakati huu dunia yote ina lugha moja. Badala ya kutawanyika juu ya dunia na kuijaza na kuilima, wanadamu wanaamua kujenga jiji na mnara wenye ncha ya kufika katika mbingu ili wajifanyie jina mashuhuri. Hata hivyo, Yehova anaharibu madhumuni yao kwa kuvuruga lugha yao, na kwa hiyo awatawanya. Jiji hilo laitwa Babeli (maana yake “Mvurugo”).
16. (a) Kwa nini nasaba ya Shemu ni ya maana? (b) Ni jinsi gani Abramu aja kuitwa ‘rafiki wa Yehova,’ naye anapokea baraka gani?
16 Shughuli za Mungu pamoja na Abrahamu (11:10–25:26). Mstari wa ukoo wa maana kutoka Shemu hadi kwa Abramu mwana wa Tera, unafuatishwa, hilo likitoa pia viunzi vya kronolojia (tarehe za matukio). Badala ya kujitafutia jina, Abramu azoea imani katika Mungu. Aondoka kwenye jiji la Ukaldayo la Uru kwa kuamriwa na Mungu na akiwa na miaka 75, auvuka Frati akielekea kwenye bara la Kanaani, akiliitia jina la Yehova. Kwa sababu ya imani na utii wake, aja kuitwa “rafiki [mpenzi] wa Yehova,” na Mungu asimamisha agano lake pamoja naye. (Yak. 2:23, NW; 2 Nya. 20:7; Isa. 41:8) Mungu alinda Abramu na mke wake wakati wa kukaa kwao kidogo katika Misri. Arudipo Kanaani, Abramu aonyesha ukarimu na kuwa kwake mwenye amani kwa kuruhusu mpwa wake na mwabudu mwenziye, Lutu, achague kisehemu bora zaidi cha bara. Baadaye, amwokoa Lutu kutoka kwa wafalme wanne ambao wamemteka nyara. Kisha, arejeapo kutoka kwenye pigano hilo, Abramu akutana na Melkizedeki, mfalme wa Salemu, ambaye akiwa kuhani wa Mungu ambariki Abramu, na Abramu ampa zaka.
17. Mungu akuzaje agano lake, na ni nini kinachofunuliwa kuhusu mbegu ya Abramu?
17 Baadaye Mungu atokea Abramu, akitangaza kwamba Yeye ni ngao ya Abramu na kukuza ahadi ya agano kwa kufunua kwamba mbegu ya Abramu itakuwa kama nyota za mbingu kwa hesabu. Abramu aambiwa kwamba mbegu yake itapata udhia (mateso) kwa miaka 400 lakini itaokolewa na Mungu, hukumu ikipitishwa juu ya taifa lenye kuleta udhia. Abramu awapo na miaka 85, Sarai mke wake, akiwa angali hana mtoto, ampa kijakazi wake Mmisri Hagari ili apate mtoto kupitia kwake. Ishmaeli azaliwa na aonwa kuwa yawezekana akawa ndiye mrithi. Hata hivyo, Yehova akusudia tofauti. Abramu awapo na miaka 99, Yehova abadili jina lake kuwa Abrahamu, abadili jina la Sarai kuwa Sara, na kuahidi kwamba Sara atazaa mwana. Abrahamu apewa agano la tohara, na bila kukawia atahiri watu wa nyumba yake.
18. Ni matukio gani makubwa ambayo yafikisha tamati ya maisha ya Lutu?
18 Sasa Mungu atangazia rafiki Yake Abrahamu azimio Lake la kuangamiza Sodoma na Gomora kwa sababu ya dhambi yao nzito. Malaika wa Yehova waonya Lutu na kumsaidia atoroke Sodoma pamoja na mke wake na mabinti wawili. Hata hivyo, mke wake, akijivuta-vuta atazame vitu vilivyo nyuma, awa nguzo ya chumvi. Ili wapate wazao, mabinti wa Lutu walewesha baba yao kwa divai, na kwa kufanya ngono naye, wazaa wana wawili, ambao wanakuwa baba za mataifa ya Moabu na Amoni.
19. Ni mtihani gani ambao Abrahamu afaulu kupita kuhusiana na Mbegu, na Yehova afunua nini zaidi katika kuthibitisha ahadi Yake?
19 Mungu alinda Sara asichafuliwe na Abimeleki wa Wafilisti. Mrithi aliyeahidiwa, Isaka, azaliwa wakati Abrahamu ana miaka 100 na Sara kama 90. Miaka mitano baada ya hilo, Ishmaeli mwenye miaka 19 afanyia Isaka mzaha, yule mrithi, tokeo likiwa ni kufukuzwa kwa Hagari na Ishmaeli, kwa kibali cha Mungu. Miaka kadhaa baadaye, Mungu ampa Abrahamu mtihani kwa kumwamuru atoe dhabihu mwana wake Isaka juu ya mmoja wa milima ya Moria. Imani kubwa ya Abrahamu katika Yehova haitikisiki. Yeye afanya jaribio la kumtoa mwana na mrithi wake lakini asimamishwa na Yehova, ambaye amtoa kondoo-ndume kuwa dhabihu iliyo badala. Kwa mara nyingine Yehova athibitisha ahadi Yake kwa Abrahamu, akisema kwamba Yeye ataongeza mbegu ya Abrahamu kama nyota za mbinguni na punje za mchanga zilizoko pwani ya bahari. Aonyesha kwamba mbegu hiyo itatwaa lango la maadui wake na kwamba mataifa yote ya dunia yatajibarikia hakika kupitia ile Mbegu.
20. Abrahamu afanya uangalifu gani katika kumpatia Isaka mke, na Isaka afanywaje kuwa mrithi pekee?
20 Sara afa akiwa na miaka 127 na kuzikwa katika konde ambalo Abrahamu anunua kutoka kwa wana wa Hethi. Abrahamu sasa atuma mtumishi mkuu wa nyumba yake akalete mke kwa ajili ya Isaka kutoka nchi ya watu wa ukoo wake. Yehova aongoza mtumishi huyo kwa familia ya Bethueli mwana wa Nahori, na mipango yafanywa Rebeka arudi naye. Rebeka aenda kwa kupenda, akiwa na baraka ya familia yake, na kuwa bibi-arusi wa Isaka. Abrahamu, kwa upande wake, atwaa mke mwingine, Ketura, anayemzalia wana sita. Hata hivyo, awapa zawadi na kuwaondosha na kufanya Isaka awe mrithi wake pekee. Halafu, akiwa na miaka 175, Abrahamu afa.
21. Isaka na Rebeka wapataje kuwa na wana mapacha?
21 Kama Yehova alivyokuwa ametabiri, Ishmaeli ndugu nusu wa Isaka awa kichwa cha taifa kubwa, lililowekewa msingi na wana-majumbe wake 12. Kwa miaka 20 Rebeka abaki tasa, lakini Isaka aendelea kumsihi Yehova, naye azaa mapacha, Esau na Yakobo, ambao Yehova alikuwa amemwambia mkubwa angemtumikia mdogo. Isaka sasa ana miaka 60.
22. Esau na Yakobo wana maoni gani kuelekea lile agano lililofanywa pamoja na Abrahamu, na matokeo yawa nini?
22 Yakobo na wana wake 12 (25:27–37:1). Esau awa mpenda kuwinda. Kwa kushindwa kuthamini agano pamoja na Abrahamu, arejea kutoka mawindo siku moja na kuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa kwa kigugumio kimoja tu cha mchuzi. Pia aoa wanawake Wahiti wawili (na baadaye Mwishmaeli), ambao wanakuwa chanzo cha uchungu wa moyo kwa wazazi wake. Kwa usaidizi wa mama yake, Yakobo ajisingizia kuwa Esau kusudi apate baraka ya mzaliwa wa kwanza. Esau, ambaye hakuwa amefunulia Isaka kwamba alikuwa ameuza haki yake ya kuzaliwa, sasa apanga kumwua Yakobo anapojua aliyofanya Yakobo, kwa hiyo Rebeka amshauri Yakobo atoroke kwenda Harani kwa ndugu yake Labani. Kabla Yakobo hajaondoka, Isaka ambariki tena na kumwagiza atwae mke, si mpagani, bali mtu fulani kutoka kwa nyumba ya mama yake. Kule Betheli, akiwa njiani kwenda Harani, katika ndoto aona Yehova, ambaye anamtuliza na kumthibitishia ahadi ya agano.
23. (a) Yakobo apataje kuwa na wana 12? (b) Reubeni apotezaje haki yake ya kuzaliwa?
23 Kule Harani, Yakobo afanyia kazi Labani, na kuoa mabinti wake wawili, Lea na Raheli. Ingawa yeye atwikwa ndoa yake hii ya wake wengi kwa ujanja wa Labani, Mungu aibariki kwa kumpa Yakobo wana 12 na binti mmoja kupitia wake hao na wajakazi wao wawili, Zilpa na Bilha. Mungu ahakikisha kwamba mifugo wa Yakobo waongezeka sana na kumwagiza arudi kwenye nchi ya mababu wake. Afuatiwa na Labani, lakini wao wafanya agano mahali paitwapo Galeedi na Mnara wa Mlinzi (Kiebrania, ham·Mits·pahʹ). Akianza tena safari yake, Yakobo apewa uhakikisho upya na malaika na kushindana usiku kucha na malaika mmoja, ambaye hatimaye ambariki na kubadili jina lake Yakobo kuwa Israeli. Yakobo afanya makubaliano ya amani ya kukutana na Esau na kusafiri hadi Shekemu. Hapa bintiye, Dina, anajisiwa na mwana wa jumbe Mhivi. Ndugu zake, Simeoni na Lawi walipa kisasi kwa kuchinja wanaume wa Shekemu. Hilo lamchukiza Yakobo kwa sababu akiwa mwakilishi wa Yehova lampa jina baya katika bara. Mungu amwambia aende Betheli akafanye madhabahu huko. Katika safari ya kutoka Betheli, Raheli afa akimzalia Yakobo mwana wake wa 12, Benyamini. Reubeni amnajisi Bilha mjakazi wa Raheli, mama ya wana wawili wa Yakobo, na kwa sababu ya hilo apoteza haki yake ya kuzaliwa. Upesi baada ya hapo Isaka afa, akiwa na miaka 180, na Esau na Yakobo wamzika.
24. Kwa nini Esau na nyumba yake wahamia mkoa wa milima-milima wa Seiri?
24 Esau na nyumba yake wahama hadi mkoa wa milima-milima wa Seiri, mali iliyokusanywa ya Esau na Yakobo ikiwa ni kubwa mno kutoruhusu waendelee kukaa pamoja. Orodha za wazao wa Esau na pia mashehe na wafalme wa Edomu zimetolewa. Yakobo aendelea kukaa katika Kanaani.
25. Ni matukio gani yaongoza kwenye Yusufu kuwa mtumwa katika Misri?
25 Kwenda Misri ili kuhifadhi uhai (37:2–50:26). Kwa sababu ya kibali cha Yehova na ndoto fulani ambazo asababisha Yusufu awe nazo, ndugu zake waja kumchukia Yusufu. Watunga hila ya kumwua lakini badala yake wamwuza kwa wafanya-biashara fulani Waishmaeli wanaopita. Kwa kuchovya joho lenye milia la Yusufu ndani ya damu ya mbuzi, walipeleka hilo kwa Yakobo kuwa ushuhuda wa kwamba mvulana huyo wa miaka 17 ameuawa na wanyama-mwitu. Yusufu apelekwa Misri na kuuzwa kwa Potifa, mkuu wa walinzi wa Farao.
26. Kwa nini simulizi la kuzaliwa kwa Perezi ni la maana?
26 Sura ya 38 yaondoka kando kidogo itoe simulizi la kuzaliwa kwa Perezi na Tamari, ambaye, kwa werevu, amfanya Yuda baba-mkwe wake afanye ndoa iliyo haki yake ambayo ingalipasa kuwa imefanywa na mwana wake. Simulizi hilo kwa mara nyingine lakazia uangalifu mkubwa ambao kwao Maandiko yana maandishi ya kila hatua inayoongoza kwenye kutokezwa kwa Mbegu ya ahadi. Mwana wa Yuda, Perezi awa mmoja wa mababu wa Yesu.—Luka 3:23, 33.
27. Yusufu awaje waziri mkuu wa Misri?
27 Wakati uo huo, Yehova abariki Yusufu katika Misri, na Yusufu awa mkuu katika nyumba ya Potifa. Hata hivyo, tatizo lamfuata akataapo kusuta jina la Mungu kwa uasherati na mke wa Potifa, kwa hiyo ashtakiwa kiubandia na kutupwa gerezani. Humo atumiwa na Yehova katika kufasiri ndoto za wafungwa-wenzi wawili, mnyweshaji wa Farao na muokaji-mkate wake. Baadaye, Farao aotapo ndoto ambayo yamhangaisha sana, ajulishwa uweza wa Yusufu, hivi kwamba aletwa upesi kwa Farao kutoka shimo lake la gereza. Akimpa Mungu sifa, Yusufu afasiri ndoto hiyo kuwa utabiri wa miaka saba ya utele, ikifuatwa na miaka saba ya njaa kubwa. Farao atambua “roho ya Mungu” juu ya Yusufu na kumweka kuwa waziri mkuu wa kushughulikia hali hiyo. (Mwa. 41:38) Sasa akiwa na miaka 30, Yusufu asimamia kwa hekima kwa kuweka akibani vyakula wakati wa miaka saba ya utele. Halafu wakati wa njaa kubwa ya ulimwenguni pote inayofuata, awauzia nafaka watu wa Misri na wa nchi nyinginezo wanaokuja Misri kwa ajili ya chakula.
28. Ni matukio gani yazunguka kuhamia Misri kwa nyumba ya Yakobo?
28 Hatimaye Yakobo atuma wana wake kumi wenye umri mkubwa waende Misri kuleta nafaka. Yusufu awatambua, lakini wao hawamtambui. Akimkamata Simeoni kuwa rehani, adai kwamba waje na ndugu yao mchanga kabisa wakati wa safari itakayofuata ya kupata nafaka. Wana tisa warejeapo wakiwa na Benyamini, Yusufu ajifunua, atoa msamaha kuelekea wale kumi wenye hatia, na kuwaagiza wakamlete Yakobo na kuhamia Misri kwa ajili ya hali njema yao wakati wa ile njaa kubwa. Kwa hiyo, Yakobo, na 66 wa wazao wake, ahamia Misri. Farao awapa bara lililo bora zaidi, bara la Gosheni, wakae humo.
29. Ni mfululizo wa unabii gani mbalimbali ambao Yakobo atoa kitandani alimofia?
29 Yakobo akaribiapo kufa, abariki Efraimu na Manase, wana wa Yusufu, na kisha awaita wana wake mwenyewe 12 pamoja awaambie yatakayowapata “siku za mwisho.” (49:1) Sasa atoa mfululizo wa unabii wenye maelezo mengi, na wote umekuja kutimizwa kiajabu tangu wakati huo.d Hapo atabiri kwamba fimbo ya utawala itabaki katika kabila la Yuda hadi kuja kwa Shilo (maana yake “Yeye Ambaye Ni Yake; Yeye Ambaye Ni Mali Yake”), Mbegu aliyeahidiwa. Baada ya kubariki hivyo vichwa vya makabila 12 na kutoa amri zinazohusu maziko yake mwenyewe ya wakati ujao katika Bara la Ahadi, Yakobo afa akiwa na miaka 147. Yusufu aendelea kutunza ndugu zake na nyumba zao hadi kifo chake mwenyewe akiwa na miaka 110, ambapo aonyesha imani yake kwamba Mungu atarejeza Israeli katika bara lao na aomba mifupa yake pia ipelekwe kwenye hilo Bara la Ahadi.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
30. (a) Mwanzo chatoa msingi gani wa kuelewa vitabu vya baadaye vya Biblia? (b) Mwanzo chaelekeza kwenye shabaha gani inayofaa?
30 Kikiwa mwanzo wa Neno la Mungu lililopuliziwa, Mwanzo kina mafaa yasiyokadirika katika kutanguliza makusudi matukufu ya Yehova Mungu. Jinsi kinavyotoa msingi wa kuelewa vitabu vya Biblia vya baadaye! Katika upana wacho, kinaeleza mwanzo na mwisho wa ulimwengu mwadilifu katika Edeni, kusitawi na kufagiliwa kwa ulimwengu wa kwanza wa wasiomcha Mungu, na kutokea kwa ulimwengu mwovu wa sasa. Kwa njia yenye kutokeza, chaanzisha vizuri kichwa kikuu cha Biblia yote, yaani, kutetewa kwa Yehova kupitia Ufalme ambao mtawala wao ni “mbegu” (NW) iliyoahidiwa. Kinaonyesha ni kwa nini binadamu hufa. Tangu Mwanzo 3:15 kuendelea—na hasa katika maandishi ya shughuli za Mungu pamoja na Abrahamu, Isaka, na Yakobo—chatoa tumaini la uhai katika ulimwengu mpya chini ya Ufalme wa Mbegu. Ni chenye mafaa katika kuonyesha madhumuni yanayofaa kwa ainabinadamu yote—kuwa washika ukamilifu na watakasaji wa jina la Yehova.—Rum. 5:12, 18; Ebr. 11:3-22, 39, 40; 12:1; Mt. 22:31, 32.
31. Kwa kurejezea chati iliyoambata, onyesha kwamba Mwanzo kina (a) unabii mbalimbali wenye maana na (b) kanuni zenye thamani.
31 Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo hurejezea kwenye kila tukio na mtu maarufu aliyeandikwa katika kitabu cha Mwanzo. Kuongezea hayo, kama ionyeshwavyo kotekote katika Maandiko, unabii mbalimbali ulioandikwa katika Mwanzo umetimizwa bila kukosea. Mmojawapo, ile “miaka mia nne” ya kuteswa kwa mbegu ya Abrahamu, ulianza wakati Ishmaeli alipomfanyia mzaha Isaka katika 1913 K.W.K. na ukaisha kwa kukombolewa Misri katika 1513 K.W.K.e (Mwa. 15:13) Vielelezo vya unabii mwingine mbalimbali wenye maana na utimizo wao vyaonyeshwa katika chati inayoambata. Pia zenye mafaa makubwa katika kujenga imani na kuelewa ni kanuni za kimungu zilizoelezwa kwanza katika Mwanzo. Manabii wa kale, na pia Yesu na wanafunzi wake, mara nyingi walirejezea na kuonyesha matumizi ya vifungu kutoka kitabu cha Mwanzo. Tutafanya vema kufuata kielelezo chao, na kuchunguza chati inayoambata kwapasa kusaidia katika hilo.
32. Ni habari gani ya maana iliyo katika Mwanzo juu ya ndoa, nasaba, na kuhesabu wakati?
32 Mwanzo chafunua wazi sana mapenzi na kusudi la Mungu kuhusu ndoa, uhusiano ufaao wa mume na mke, na kanuni za ukichwa na mazoezi ya familia. Yesu mwenyewe alitumia habari hiyo, akinukuu sura ya kwanza na ya pili ya Mwanzo katika ile taarifa moja yake: “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?” (Mt. 19:4, 5; Mwa. 1:27; 2:24) Maandishi katika Mwanzo ni muhimu katika kuonyesha nasaba ya familia ya kibinadamu na pia katika kupiga hesabu ya wakati ambao binadamu amekuwa katika dunia hii.—Mwa., sura 5, 7, 10, 11
33. Taja kanuni na mazoea fulani ya jumuiya ya wazee wa ukoo yaliyo ya maana katika kuielewa Biblia.
33 Pia lenye mafaa halisi kwa mwanafunzi wa Maandiko ni kuchunguza jumuiya ya wazee wa ukoo ambayo Mwanzo hueleza. Jumuiya ya wazee wa ukoo ilikuwa namna ya ujamii wa serikali ya familia iliyokuwako miongoni mwa watu wa Mungu tangu siku ya Nuhu hadi kutolewa kwa Sheria kwenye Mlima Sinai. Mengi ya maelezo yaliyotiwa ndani ya agano la Sheria yalikuwa tayari yakizoewa katika jumuiya ya wazee wa ukoo. Kanuni kama ustahili wa kijumuiya (18:32), daraka la kijumuiya (19:15), adhabu ya kifo na pia utakatifu wa damu na wa uhai (9:4-6), na chuki ya Mungu juu ya kutukuzwa kwa wanadamu (11:4-8) yamekuwa na matokeo juu ya ainabinadamu katika historia yote. Mazoea na semi nyingi za kisheria zinaangaza juu ya matukio ya baadaye, hata kufikia siku za Yesu. Sheria ya wazee wa ukoo inayaosimamia kutunza watu na mali (Mwa. 31:38, 39; 37:29-33; Yn. 10:11, 15; 17:12; 18:9) na jinsi ya kupokeza mali (Mwa. 23:3-18), na pia sheria inayoongoza urithi wa mtu aliyepokea haki ya mzaliwa wa kwanza (48:22), lazima ijulikane ikiwa tutakuwa na msingi unaohitajiwa ili kuelewa wazi Biblia. Mazoea mengine ya jumuiya ya wazee wa ukoo yaliyotiwa katika Sheria yalikuwa dhabihu, tohara (aliyopewa Abrahamu kwanza), ufanyaji wa maagano, ndoa ya ndugu-mkwe (38:8, 11, 26), na utumizi wa viapo ili kuthibitisha jambo.—22:16; 24:3.f
34. Ni masomo gani, yaliyo na thamani kwa Wakristo, yaweza kuwa funzo kupitia uchunguzi wa Mwanzo?
34 Mwanzo, kitabu cha kufungua cha Biblia, hutoa masomo mengi katika ukamilifu, imani, uaminifu, utii, staha, adabu nzuri, na moyo mkuu. Hapa pana vielelezo vichache: Imani ya Henoko na moyo mkuu katika kutembea pamoja na Mungu akikabiliana na maadui wenye jeuri; uadilifu wa Nuhu, kutokuwa na kosa, na utii kamili; imani ya Abrahamu, azimio lake lenye nguvu, na uvumilivu wake, kuchukua kwake daraka akiwa kichwa cha familia na mwalimu wa amri za Mungu kwa watoto wake, ukarimu wake, na upendo wake; ujitiishaji wa Sara kwa mume-kichwa wake na bidii yake ya kazi; upole wa roho wa Yakobo na kuhangaikia kwake ahadi ya Mungu; utii wa Yusufu kwa baba yake, unyofu wake wa kiadili, moyo mkuu wake, mwenendo wake mzuri gerezani, staha yake kwa mamlaka zilizo kubwa, unyenyekevu wake katika kumpa Mungu utukufu, na msamaha wake wenye rehema kwa ndugu zake; tamaa kubwa yenye kuwala watu hao wote ya kutakasa jina la Yehova. Tabia hizo zilizo kielelezo kizuri zatokeza wazi katika maisha za wale waliotembea pamoja na Mungu wakati wa kile kipindi kirefu cha miaka 2,369 tangu kuumbwa kwa Adamu hadi kifo cha Yusufu, kama yazungumzwavyo katika kitabu cha Mwanzo.
35. Katika kujenga imani, Mwanzo chaelekeza kwenye nini?
35 Kweli kweli, simulizi katika Mwanzo lina mafaa katika kujenga imani, likisimulia vielelezo vizuri ajabu vya imani, ile sifa ya imani iliyowekwa kwenye mtihani ambayo hujitahidi kufikia jiji lililojengwa na kuumbwa na Mungu, serikali yake ya Ufalme ambayo alianza kutayarisha zamani za kale kupitia Mbegu yake ya ahadi, yule mtakasaji mwenye kuongoza wa jina kubwa la Yehova.—Ebr. 11:8, 10, 16.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 919-20; Buku 2, ukurasa 1212.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 328-9
c Biblical History in the Light of Archaeological Discovery,1934, D. E.Hart-Davies, ukurasa 5.
d Mnara wa Mlinzi (Kiingereza), 1962, kurasa 360-74, 392-408.
e Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 460-1, 776.
f Mnara wa Mlinzi (Kiingereza), 1952, kurasa 432-45.
[Chati katika ukurasa wa 18]
MWANZO—KIMEPULIZIWA NA MUNGU NA NI CHENYE MAFAA
Mwanzo Kanuni Marejezo Kutoka
Waandikaji Wengine
wa kifungo cha ndoa Mt. 19:4, 5
2:7 Mwanadamu ni nafsi 1 Kor. 15:45
2:22, 23 Ukichwa 1 Tim. 2:13; 1 Kor. 11:8
9:4 Utakatifu wa damu Mdo. 15:20, 29
24:3; 28:1-8 Oa mwamini tu 1 Kor. 7:39
Unabii Mbalimbali Uliotimizwa na Vilingani vya Kiunabii
12:1-3; 22:15-18 Kitambulisho cha Mbegu
ya Abrahamu Gal. 3:16, 29
14:18 Melkizedeki afananisha Kristo Ebr. 7:13-15
16:1-4, 15 Maana ya ki-picha ya Sara, Hagari,
Ishmaeli, Isaka Gal. 4:21-31
17:11 Maana ya ki-picha ya tohara Rum. 2:29
49:1-28 Baraka ya Yakobo
juu ya makabila 12 Yos. 14:1–21:45
49:9 Simba aliye wa kabila la Yuda Ufu. 5:5
Maandishi Mengine Yaliyotumiwa na Manabii, Yesu, na Wanafunzi—Kuwa Kielezi, Katika Maana ya Utumizi, au Kuwa Kielelezo—Yakithibitisha Zaidi Uasilia wa Mwanzo
1:1 Mungu aliumba mbingu na dunia Isa. 45:18; Ufu. 10:6
1:26 Mwanadamu alifanywa katika
mfano wa Mungu 1 Kor. 11:7
2:2 Mungu alistarehe siku ya saba Ebr. 4:4
3:1-6 Nyoka alidanganya Hawa 2 Kor. 11:3
3:20 Ainabinadamu yote ilitoka
kwa watu wawili wa kwanza Mdo. 17:26
4:8 Kaini aliua Abeli Yuda 11; 1 Yn. 3:12
4:9, 10 Damu ya Abeli Mt. 23:35
Sura 5, 10, 11 Nasaba Luka, sura 3
5:29 Nuhu Eze. 14:14; Mt. 24:37
6:13, 17-20 Furiko Isa. 54:9; 2 Pet. 2:5
12:1-3, 7 Agano la Kiabrahamu Gal. 3:15-17
15:6 Imani ya Abrahamu Rum. 4:3; Yak. 2:23
15:13, 14 Safari kwenda Misri Mdo. 7:1-7
18:1-5 Ukaribishaji-wageni Ebr. 13:2
19:24, 25 Sodoma na Gomora zaharibiwa 2 Pet. 2:6; Yuda 7
19:26 Mke wa Lutu Luka 17:32
20:7 Abrahamu ni nabii Zab. 105:9, 15
21:9 Ishmaeli amdhihaki vikali Isaka Gal. 4:29
22:10 Abrahamu ajaribu kutoa
Isaka Ebr. 11:17
25:23 Yakobo na Esau Rum. 9:10-13; Mal. 1:2, 3
25:32-34 Esau auza haki ya uzaliwa Ebr. 12:16, 17
37:28 Yusufu auzwa Misri Zab. 105:17
41:40 Yusufu afanywa waziri mkuu Zab. 105:20, 21