Sura ya 22
Sehemu ya 1—Kuwa Mashahidi Hadi Sehemu ya Mbali Zaidi Sana ya Dunia
Hiki ni cha kwanza kati ya visehemu vitano katika sura ambayo huripoti jinsi utendaji wa Mashahidi wa Yehova umefika duniani pote. Sehemu ya 1, inayozungumza juu ya enzi ya kutoka miaka ya 1870 hadi 1914, imo katika kurasa 404 hadi 422. Jamii ya kibinadamu haijapata nafuu kutokana na misukosuko iliyosababishwa na Vita ya Ulimwengu 1, iliyoanza katika 1914. Huo ndio mwaka ambao Wanafunzi wa Biblia walikuwa wameutambulisha kwa muda mrefu kuwa waonyesha mwisho wa Nyakati za Mataifa.
KABLA ya kupaa mbinguni, Yesu Kristo aliwapa mitume wake utume, akisema: “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu . . . hadi sehemu ya mbali zaidi sana ya dunia.” (Mdo. 1:8, NW) Pia alikuwa ametabiri kwamba “habari njema hii ya ufalme itahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa kwa ajili ya kuwa ushahidi kwa mataifa yote.” (Mt. 24:14, NW) Kazi hiyo haikukamilishwa katika karne ya kwanza. Sehemu kubwa yayo imefanywa katika nyakati za kisasa. Na rekodi ya kukamilishwa kwayo tokea miaka ya 1870 hadi sasa ni yenye kusisimua kwelikweli.
Ijapokuwa Charles Taze Russell alipata kujulikana sana kwa sababu ya hotuba zake za Biblia zilizotangazwa sana, kupendezwa kwake hakukuwa tu katika wasikilizaji wengi lakini katika watu. Hivyo, muda mfupi baada ya kuanza kutangaza Watch Tower katika 1879, alianza safari ndefu ili kutembelea vikundi vidogo vya wasomaji wa gazeti hilo na kuzungumza Maandiko pamoja nao.
C. T. Russell alihimiza wale walioamini ahadi zenye thamani za Neno la Mungu wazishiriki pamoja na wengine. Wale ambao mioyo yao ilichochewa sana na yale waliyojifunza walionyesha bidii halisi katika kufanya hilohilo. Ili kusaidia kazi, habari iliyochapwa ilitolewa. Mapema katika 1881, idadi fulani ya trakti zilitokea. Kisha habari kutoka hizo iliunganishwa na habari zaidi ili kufanyiza kijitabu Food for Thinking Christians chenye habari nyingi zaidi, na nakala 1,200,000 zilitayarishwa ili zigawanywe. Lakini kikundi kidogo cha Wanafunzi wa Biblia (labda 100 wakati ule) kingewezaje kugawanya nakala hizo zote?
Kufikia Waenda-Kanisani
Baadhi yazo zilipewa watu wa ukoo na marafiki. Idadi fulani ya magazeti ya habari yalikubali kupeleka nakala moja kwa kila mmoja wa waandikishaji wayo. (Mkazo wa pekee ulitiwa kwenye magazeti ya kila juma na ya kila mwezi ili kwamba Food for Thinking Christians kiweze kufikia watu wengi walioishi katika maeneo ya mashambani.) Lakini ugawanyaji mwingi ulifanywa katika Jumapili kadhaa mfululizo mbele ya makanisa katika Marekani na Uingereza. Hakukuwa na Wanafunzi wa Biblia wa kutosha kufanya kazi yote wao binafsi, hivyo waliwalipa wengine ili wasaidie.
Ndugu Russell alituma washirika wawili, J. C. Sunderlin na J. J. Bender, Uingereza ili kusimamia kazi ya kugawanya nakala 300,000 huko. Ndugu Sunderlin alienda London, hali Ndugu Bender alisafiri kwenda kaskazini katika Scotland na kisha akafanya kazi akielekea kusini. Majiji makubwa ndiyo yaliyokaziwa fikira zaidi. Kwa njia ya matangazo ya magazeti ya habari, watu wenye uwezo walipatikana, na mikataba ilifanywa pamoja nao wapate wasaidizi wa kutosha kugawanya mafungu yao ya nakala. Wagawanyaji karibu 500 waliajiriwa kazi katika London pekee. Kazi ilifanywa haraka, katika Jumapili mbili mfululizo.
Mwaka huohuo, mipango ilifanywa ili Wanafunzi wa Biblia ambao wangeweza kutumia nusu au zaidi ya wakati wao katika kazi ya Bwana tu, wawe makolpota, wakigawanya fasihi kwa ajili ya funzo la Biblia. Watangulizi hao wa wale wanaojulikana leo kuwa mapainia walifikia ugawanyaji wenye kutokeza kikweli wa habari njema.
Wakati wa mwongo uliofuata, Ndugu Russell alitayarisha trakti mbalimbali ambazo zingeweza kutumiwa kwa urahisi kueneza baadhi ya zile kweli za Biblia zenye kutokeza walizokuwa wamejifunza. Pia aliandika mabuku kadhaa ya Millenial Dawn (baadaye yaliitwa Studies in the Scriptures). Kisha akaanza kusafiri kwenye nchi nyinginezo ili aeneze evanjeli kibinafsi.
Russell Asafiri Ng’ambo
Katika 1891 alizuru Kanada, ambako kupendezwa kwa kutosha kulikuwa kumechochewa tangu 1880 hivi kwamba kusanyiko lililohudhuriwa na 700 lingeweza kufanywa sasa katika Toronto. Pia alisafiri Ulaya katika 1891 ili kuona ni jambo gani lingeweza kufanywa ili kusogeza mbele kuenezwa kwa kweli huko. Safari hiyo ilimpeleka Ireland, Scotland, Uingereza, nyingi za nchi za bara la Ulaya, Urusi (lile eneo liitwalo sasa Moldova), na Mashariki ya Kati.
Alifikia mkataa gani baada ya kuwasiliana na watu katika safari hiyo? “Sisi hatukuona kufunguka au utayari kwa ajili ya kweli katika Urusi . . . Hatukuona jambo lolote la kututia moyo tutumainie vuno lolote katika Italia au Uturuki au Austria au Ujerumani,” akaripoti. “Lakini Norway, Sweden, Denmark, Uswisi, na hasa Uingereza, Ireland, na Scotland, ni mashamba yaliyo tayari na yanangojea kuvunwa. Mashamba hayo yaonekana yakilia, Njooni huku mtusaidie!” Hiyo ilikuwa ile enzi ambayo Kanisa Katoliki lilikuwa lingali likikataza usomaji wa Biblia, wakati Waprotestanti wengi walikuwa wakiacha makanisa yao, na wengi, wakikatishwa tamaa na makanisa, walikuwa wakikataa Biblia kabisa.
Ili kusaidia wale watu waliokuwa na njaa kiroho, baada ya safari ya Ndugu Russell katika 1891, jitihada zilizoongezwa zilifanywa kutafsiri fasihi katika lugha za Ulaya. Pia, mipango ilifanywa ili kuchapa na kuweka akiba ya fasihi katika London ili fasihi hizo ziweze kupatikana kwa urahisi kwa matumizi katika Uingereza. Shamba la Uingereza, lilithibitika kwelikweli kuwa tayari kuvunwa. Kufikia 1900, tayari kulikuwa makutaniko tisa na jumla ya Wanafunzi wa Biblia 138—miongoni mwao makolpota fulani wenye bidii. Wakati Ndugu Russell alipotembelea Uingereza tena katika 1903, watu elfu moja walikusanyika katika Glasgow ili kumsikia akihutubu juu ya “Matumaini na Matarajio ya Mileani,” 800 walihudhuria katika London, na wasikilizaji 500 kufikia 600 katika miji mingine.
Hata hivyo, katika kuthibitisha maoni ya Ndugu Russell, baada ya ziara yake miaka 17 ilipita kabla ya kutaniko la kwanza la Wanafunzi wa Biblia kuundwa katika Italia, katika Pinerolo. Vipi Uturuki? Wakati wa miaka ya mwisho-mwisho ya 1880, Basil Stephanoff alikuwa amehubiri katika Makedonia, katika ile iliyoitwa wakati ule Uturuki ya Ulaya. Ijapokuwa wengine walionekana kuonyesha kupendezwa, wengine kutoka katika wale waliodai kuwa ndugu walitoa ripoti za uwongo, zilizomfanya atiwe gerezani. Haikuwa mpaka 1909 kwamba barua kutoka kwa Mgiriki katika Smirna (sasa Izmir), Uturuki, iliripoti kwamba kikundi huko kilikuwa kikijifunza kwa uthamini vichapo vya Watch Tower. Kwa habari ya Austria, Ndugu Russell mwenyewe alirudi katika 1911 ili kutoa hotuba katika Vienna, ikawa tu kwamba mkutano ulikatizwa na wafanyaghasia. Katika Ujerumani pia, itikio lenye uthamini lilikuja hatua kwa hatua. Lakini Waskandinevia walionyesha kujua zaidi uhitaji wao wa kiroho.
Waskandinevia Washiriki Pamoja na Wengine
Wasweden wengi walikuwa wakiishi katika Amerika. Katika 1883 sampuli ya nakala ya Watch Tower iliyotafsiriwa katika Kisweden ilitolewa ili kugawanywa miongoni mwao. Upesi nakala hizo zikafikia kwa njia ya barua watu wa ukoo na marafiki katika Sweden. Bado hakukuwa na fasihi zilizokuwa zimetolewa katika Kinorway. Hata hivyo, katika 1892, mwaka baada ya safari ya Ndugu Russell kwenda Ulaya, Knud Pederson Hammer, Mnorway aliyekuwa amejifunza kweli katika Amerika, alirudi Norway yeye binafsi ili kutolea watu wake wa ukoo ushahidi.
Halafu, katika 1894, wakati fasihi zilipoanza kutangazwa katika lugha ya mchanganyiko ya Kidenmark na Kinorway, Sophus Winter, Mdenmark-Mwamerika mwenye umri wa miaka 25, alitumwa Denmark akiwa na ugavi wa kugawanya. Kufikia masika yaliyofuata, alikuwa ameangusha mabuku 500 ya Millennial Dawn. Katika muda mfupi, wengine wachache waliosoma vichapo hivyo walishiriki katika kazi pamoja naye. Kwa kuhuzunisha, baadaye aliacha kuona thamani ya pendeleo lake lenye thamani alilokuwa nalo; lakini wengine waliendelea kuacha nuru iangaze.
Hata hivyo, kabla ya kuacha utumishi, Winter alifanya kazi fulani ya kolpota katika Sweden. Muda mfupi baada ya hapo, nyumbani mwa rafiki katika kisiwa cha Sturkö, August Lundborg, kijana kapteni wa Jeshi la Wokovu, aliona mabuku mawili ya Millennial Dawn. Aliyaazima, akayasoma kwa hamu, akaacha kanisa, na kuanza kushiriki pamoja na wengine yale aliyokuwa amejifunza. Macho ya kijana mwingine, P. J. Johansson, yalifunguliwa kama tokeo la kusoma trakti aliyookota juu ya benchi la bustanini.
Kikundi cha Wasweden kilipoanza kukua, baadhi yao walienda Norway ili kugawanya fasihi za Biblia. Hata kabla ya jambo hilo, fasihi zilikuwa zimewasili katika Norway kwa njia ya posta kutoka kwa watu wa ukoo katika Amerika. Ni kwa njia hiyo kwamba Rasmus Blindheim alianza utumishi wa Yehova. Miongoni mwa wengine katika Norway, Theodor Simonsen, mhubiri wa kanisa la Free Mission, alipokea kweli wakati wa miaka hiyo ya mapema. Alianza kukanusha fundisho la moto wa helo katika hotuba zake katika kanisa la Free Mission. Wasikilizaji wake waliinuka juu kwa kusisimuliwa na habari hiyo ya ajabu; lakini ilipojulikana kwamba alikuwa amekuwa akiwasiliana na “Millennial Dawn,” alifukuzwa kutoka kanisa. Hata hivyo, yeye aliendelea tu kuongea juu ya mambo mema aliyokuwa amejifunza. Kijana mwingine aliyepokea baadhi ya fasihi alikuwa Andreas Øiseth. Mara aliposadikishwa kwamba alikuwa amepata kweli, aliondoka kwenye shamba la familia akaanza kazi ya kolpota. Alifanya kazi kwa utaratibu kuelekea kaskazini, kisha kusini kuelekea zile ghuba ndogo, bila kupita kijiji chochote. Wakati wa kipupwe alichukua ugavi wake—chakula, mavazi, na fasihi—katika kigari cha kujisukuma kwa mguu juu ya theluji, nao watu wenye ukaribishaji-wageni walimwandalia mahali pa kulala. Katika safari ya miaka minane, alieneza habari njema katika karibu nchi nzima.
Ebba, mke wa August Lundborg, alitoka Sweden akaenda Finland kufanya kazi ya kolpota katika 1906. Karibu wakati uo huo, watu waliokuwa wakirudi kutoka Marekani walikuja na fasihi za Watch Tower na kuanza kushiriki yale waliyokuwa wakijifunza. Hivyo katika muda wa miaka michache, Emil Österman, aliyekuwa akitafuta kitu bora zaidi ya kilichokuwa kikitolewa na makanisa, alipata The Divine Plan of the Ages. Alikishiriki pamoja na rafiki yake Kaarlo Harteva, aliyekuwa akitafuta pia. Akitambua thamani ya walichokuwa nacho, Harteva alikitafsiri katika Kifinland na, kwa msaada wa kifedha wa Österman, akapanga kitangazwe. Pamoja walianza kukigawanya. Wakionyesha roho ya kweli ya kueneza evanjeli, waliongea na watu hadharani, wakafanya ziara nyumba hadi nyumba, na kutoa hotuba katika majumba makubwa yaliyokuwa yanajaa kabisa. Katika Helsinki, baada ya kufunua mafundisho bandia ya Jumuiya ya Wakristo, Ndugu Harteva aliwaalika wasikilizaji watumie Biblia ili kutetea imani katika nafsi isiyoweza kufa, wakiweza. Macho yote yalielekezwa kwa makasisi waliokuwapo. Hakuna mtu aliyesema; hakuna mtu angeweza kukanusha taarifa iliyo wazi ipatikanayo kwenye Ezekieli 18:4. Baadhi ya wasikilizaji walisema kwamba ilikuwa vigumu kulala usiku huo baada ya yale waliyosikia.
Mtunza-Bustani Mnyenyekevu Awa Mweneza-Evanjeli Katika Ulaya
Wakati huohuo, Adolf Weber, akitiwa moyo na rafiki Mwanabaptisti mwenye umri mkubwa, aliondoka Uswisi kwenda Marekani akatafute uelewevu kamili zaidi wa Maandiko. Huko, ili kujibu tangazo, akawa mtunza-bustani wa Ndugu Russell. Kwa msaada wa The Divine Plan of the Ages (wakati huo kikipatikana kwa Kijerumani) na mikutano iliyoongozwa na Ndugu Russell, Adolf alipata ule ujuzi wa Biblia aliokuwa akitafuta, naye alibatizwa katika 1890. ‘Macho ya moyo wake yalitiwa nuru,’ hivi kwamba alithamini kikweli ile fursa bora sana iliyokuwa imefunguka mbele yake. (Efe. 1:18) Baada ya kutoa ushahidi kwa bidii kwa muda fulani katika Marekani, alirudi katika nchi alimozaliwa akaanze kazi “katika shamba la mizabibu la Bwana” huko. Hivyo, kufikia miaka ya katikati ya 1890, alikuwa amerudi Uswisi akishiriki kweli za Biblia pamoja na wale waliokuwa na mioyo yenye kuitikia.
Adolf alipata riziki yake akiwa mtunza-bustani na mtunza-misitu, lakini lililompendeza zaidi ni kueneza evanjeli. Alitolea ushahidi wale aliofanya kazi nao, pamoja na watu katika miji na vijiji vya karibu vya Uswisi. Yeye alijua lugha kadhaa, naye alitumia ujuzi huo kutafsiri vichapo vya Sosaiti katika Kifaransa. Wakati wa kipupwe alikuwa akipakia fasihi za Biblia katika mfuko wake na kwenda Ufaransa kwa miguu, na nyakati nyingine alisafiri kaskazini-magharibi kwenda Ubelgiji na kusini kwenda Italia.
Ili kufikia watu ambao huenda yeye binafsi asiweze kuonana nao, alitia matangazo katika magazeti na majarida akivuta fikira zao kwenye fasihi zilizopatikana kwa ajili ya funzo la Biblia. Elie Thérond, kutoka katikati mwa Ufaransa, alijibu mojayapo matangazo hayo, akitambua kweli katika jambo alilosoma, upesi alianza kueneza ujumbe huo yeye mwenyewe. Katika Ubelgiji, Jean-Baptiste Tilmant, Sr., aliona pia mojayapo matangazo hayo katika 1901 na kupata mabuku mawili ya Millennial Dawn. Ulikuwa msisimuko kama nini kuona kweli ya Biblia ikiwa imetolewa kwa njia yenye kueleweka jinsi hiyo! Angewezaje kujizuia kuwaambia marafiki wake! Kufikia mwaka uliofuata, kikundi cha funzo kilikuwa kikikutana kwa ukawaida katika kao lake. Upesi baada ya hapo utendaji wa kikundi hicho kidogo ulikuwa ukizaa tunda hata katika kaskazini mwa Ufaransa. Ndugu Weber aliendelea kuwasiliana nao, akitembelea pindi kwa pindi vikundi hivyo mbalimbali vilivyokuwa vimesitawi, akivijenga kiroho na kutoa maagizo juu ya jinsi ya kushiriki habari njema na wengine.
Wakati Habari Njema Zilipofika Ujerumani
Muda mfupi baada ya baadhi ya vichapo hivyo kuanza kutokea katika Kijerumani, katika miaka ya katikati ya 1880, Wajerumani-Waamerika waliovithamini walianza kupeleka nakala kwa watu wao wa ukoo katika nchi walimozaliwa. Mwuguzi mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika hospitali moja ya Hamburg alishiriki nakala za Millennial Dawn na wengine katika hospitali. Katika 1896, Adolf Weber, katika Uswisi, alikuwa akitia matangazo katika magazeti ya lugha ya Kijerumani na kupeleka trakti Ujerumani kwa posta. Mwaka uliofuata depo ya fasihi ilifunguliwa katika Ujerumani ili kurahisisha ugawanyaji wa chapa ya Kijerumani ya Watch Tower, lakini matokeo yalikuja hatua kwa hatua. Hata hivyo, katika 1902, Margarethe Demut, aliyekuwa amejifunzia kweli katika Uswisi, alihamia Tailfingen, mashariki mwa Black Forest. Bidii yake ya kutoa ushahidi kibinafsi iliweka msingi wa mojawapo vikundi vya mapema vya Wanafunzi wa Biblia katika Ujerumani. Samuel Lauper, kutoka Uswisi, alihamia Bergisches Land, kaskazini-mashariki mwa Cologne, ili kueneza habari njema katika eneo hilo. Kufikia 1904, mikutano ilikuwa ikifanywa huko katika Wermelskirchen. Miongoni mwa waliokuwapo alikuwa mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 80, Gottlieb Paas, aliyekuwa akitafuta kweli. Akiwa kitandani mwake wakati wa kufa, muda mfupi baada ya mikutano hiyo kuanza, Paas aliinua Watch Tower na kusema: “Hii ndiyo kweli; shikamaneni nayo.”
Idadi ya waliokuwa wakipendezwa katika kweli hizo za Biblia iliongezeka hatua kwa hatua. Ijapokuwa ilikuwa ghali, mipango ilifanywa kutia nakala sampuli za Watch Tower magazetini nchini Ujerumani. Ripoti iliyotangazwa katika 1905 ilisema kwamba zaidi ya nakala 1,500,000 za sampuli hizo za Watch Tower zilikuwa zimegawanywa. Hiyo ilikuwa kazi kubwa iliyotimizwa na kikundi hicho kidogo.
Wanafunzi wa Biblia wote hawakuhisi kwamba kwa kufikia watu karibu na nyumbani walikuwa wamefanya yote yaliyohitajiwa. Mapema sana kama 1907, Ndugu Erler, kutoka Ujerumani, alifunga safari nyingi kwenda Bohemia katika ile iliyokuwa wakati huo Austria na Hungaria (baadaye sehemu ya Chekoslovakia). Aligawanya fasihi zilizoonya juu ya Har–Magedoni na kuwaambia juu ya baraka ambazo zingekuja kwa wanadamu baada yayo. Kufikia 1912 Mwanafunzi wa Biblia mwingine alikuwa amegawanya fasihi za Biblia katika eneo la Memel, katika ile ambayo sasa ni Lithuania. Wengi waliitikia ujumbe huo kwa idili, na upesi vikundi kadhaa vikubwa kidogo vya Wanafunzi wa Biblia vilifanyizwa huko. Hata hivyo, wakati walipojifunza kwamba Wakristo wa kweli lazima pia wawe mashahidi, idadi yao ilianza kupungua. Hata hivyo, wachache walijithibitisha wenyewe kuwa waigaji wa kweli wa Kristo, “shahidi mwaminifu na wa kweli.”—Ufu. 3:14, NW.
Wakati Nikolaus von Tornow, kabaila Mjerumani mwenye mali nyingi katika Urusi, alipokuwa katika Uswisi kama mwaka 1907, alipewa mojayapo trakti za Watch Tower Society. Miaka miwili baadaye alitokea kwenye Kutaniko la Berlin, katika Ujerumani, akiwa amevalia mavazi yake yaliyo bora zaidi huku mtumishi wake wa kibinafsi akiambatana naye. Ilichukua muda ndipo athamini kwa nini Mungu angeaminisha kweli hizo za thamani nyingi sana kwa watu wanyenyekevu, lakini yale aliyosoma kwenye 1 Wakorintho 1:26-29 yalimsaidia: “Mwatazama wito wake kwenu, akina ndugu, kwamba si wengi wenye hekima katika njia ya kimwili walioitwa, si wengi wenye nguvu, si wengi wa uzawa wa kikabaila . . . , ili mwili wowote usipate kujisifu machoni pa Mungu.” Akisadiki kwamba alikuwa amepata kweli, von Tornow aliuza mali zake katika Urusi akajitoa mwenyewe na mali zake kusogeza mbele masilahi ya ibada safi.
Katika 1911, wakati wenzi wawili Wajerumani, akina Herkendell, walipofunga ndoa, bibi-arusi aliomba baba yake, ikiwa mahari, pesa kwa ajili ya fungate isiyo ya kawaida. Yeye na mume wake walifikiria kufunga safari ngumu ambayo ingechukua miezi mingi. Fungate yao ilikuwa safari ya kwenda kuhubiri katika Urusi ili kufikia watu wasemao Kijerumani huko. Hivyo kwa njia nyingi watu wa aina zote walikuwa wakishiriki na wengine yale waliyokuwa wamejifunza juu ya kusudi la Mungu lenye upendo.
Ukuzi Katika Shamba la Uingereza
Baada ya ule ugawanyaji wa bidii wa fasihi katika Uingereza katika 1881, baadhi ya waenda-kanisani waliona uhitaji wa kutenda juu ya yale waliyokuwa wamejifunza. Tom Hart wa Islington, London, alikuwa mmoja wa wale waliovutiwa na shauri la Kimaandiko la Watch Tower, “Tokeni kwake, watu wangu”—yaani, tokeni katika makanisa ya Kibabiloni ya Jumuiya ya Wakristo na kufuata mafundisho ya Biblia. (Ufu. 18:4, NW) Aliacha kanisa katika 1884, akifuatwa na hesabu fulani ya wengine.
Wengi walioshirikiana na vikundi vya funzo walisitawi wakawa waeneza-evanjeli wenye matokeo. Baadhi yao walitoa fasihi za Biblia katika bustani za London na sehemu nyingine ambako watu walikuwa wakistarehe. Wengine walikazia fikira sehemu za biashara. Hata hivyo, ile njia ya kawaida zaidi ilikuwa kufanya ziara za nyumba hadi nyumba.
Sarah Ferrie, mwandikishaji wa Watch Tower, aliandikia ndugu Russell akisema kwamba yeye na marafiki wachache katika Glasgow wangetaka kujitolea kushiriki katika kugawanya trakti. Ulikuwa mshangao kama nini wakati lori lilipowasili mlangoni pake likiwa na trakti 30,000, zote za kugawanywa bila malipo! Wakaanza kutenda mara hiyo. Minnie Greenlees, pamoja na wavulana wake watatu, akiwa na kigari chenye kukokotwa na farasi kikiwa usafiri, alijitahidi kugawanya fasihi za Biblia katika sehemu za mashambani za Scotland. Baadaye, Alfred Greenlees na Alexander MacGillivray, wakisafiri kwa baiskeli, waligawanya trakti katika sehemu iliyo kubwa zaidi ya Scotland. Badala ya kulipa wengine wagawanye fasihi, wenye kujitolea walio wakfu walikuwa sasa wakifanya kazi hiyo wao wenyewe.
Mioyo Yao Iliwasukuma
Katika mmojapo mifano yake, Yesu alikuwa amesema kwamba watu ‘waliosikia neno la Mungu kwa moyo mzuri’ wangezaa tunda. Uthamini wa moyo mweupe wa maandalizi ya Mungu yenye upendo ungewasukuma kushiriki pamoja na wengine habari njema juu ya Ufalme wa Mungu. (Luka 8:8, 11, 15) Bila kujali hali zao, wangepata njia ya kufanya hivyo.
Hivyo ilikuwa ni kutoka kwa baharia Mwitalia kwamba msafiri Mwargentina alipata kisehemu cha ile trakti Food for Thinking Christians. Alipokuwa bandarini katika Peru, msafiri huyo aliandika apate habari zaidi, na akiwa na kupendezwa kulikoongezeka akaandika tena kutoka Argentina katika 1885, kwa mhariri wa Watch Tower aombe fasihi. Mwaka huohuo mshiriki wa Jeshi la Manowari la Uingereza, aliyetumwa pamoja na kikosi chake cha silaha, kwenda Singapore, alichukua Watch Tower. Alifurahia aliyojifunza kutoka kwa gazeti hilo na akalitumia sana kujulisha maoni ya Biblia juu ya habari zilizokuwa mazungumzo ya umma. Katika 1910 meli ambamo wanawake wawili Wakristo walikuwa wakisafiria ilitua kwenye bandari katika Colombo, Ceylon (sasa Sri Lanka). Walichukua fursa hiyo kumtolea ushahidi Bw. Van Twest, ofisa-msimamizi wa bandari. Walisema naye kwa moyo wa bidii juu ya mambo mema waliyokuwa wamejifunza kutoka kitabu The Divine Plan of the Ages. Kama tokeo, Bw. Van Twest akawa Mwanafunzi wa Biblia, na kazi ya kuhubiri habari njema ikaanza katika Sri Lanka.
Hata wale ambao hawangeweza kusafiri walitafuta njia za kushiriki kweli za Biblia zenye kuchangamsha moyo pamoja na watu katika nchi nyinginezo. Kama ilivyofunuliwa na barua ya shukrani iliyochapwa katika 1905, mtu fulani katika Marekani alikuwa amepeleka kitabu The Divine Plan of the Ages kwa mwanamume mmoja katika St. Thomas, katika ile iliyokuwa wakati huo Indies Magharibi ya Denmark. Baada ya kukisoma, mpokeaji alipiga magoti na kueleza tamaa yake ya kutaka kutumiwa na Mungu katika kufanya mapenzi yake. Katika 1911, Bellona Ferguson katika Brazili alitaja kisa chake kuwa “uthibitisho hakika ulio hai kwamba hakuna walio mbali mno wasiweze kufikiwa” na maji ya kweli. Yaonekana alikuwa amekuwa akipokea vichapo vya Sosaiti kwa posta tangu 1899. Wakati fulani kabla ya Vita ya Ulimwengu 1, mhamiaji Mjerumani katika Paraguai alipata mojayapo trakti za Sosaiti katika sanduku lake la posta. Aliagiza fasihi zaidi na upesi akaacha kushirikiana na makanisa ya Jumuiya ya Wakristo. Hapakuwa na mwingine nchini wa kuwabatiza, hivyo yeye na shemeji yake wakaamua wabatizane. Kwelikweli, ushahidi ulikuwa ukitolewa katika sehemu za mbali za dunia nao ulikuwa ukizaa tunda.
Bado wengine kati ya Wanafunzi wa Biblia walihisi wakisukumwa wasafiri hadi mahali ambapo wao au wazazi wao walizaliwa ili kuwaambia marafiki na watu wa ukoo juu ya kusudi la ajabu la Yehova na jinsi wao wangelishiriki. Hivyo, katika 1895, Ndugu Oleszynski alirudi Poland akiwa na habari njema juu ya “fidia, kufanywa upya kwa vitu vyote na ule mwito wa juu”; ingawa, kwa kusikitisha, yeye hakuendelea katika utumishi huo. Katika 1898 mmoja aliyekuwa profesa, Mhungaria, aliondoka Kanada ili kueneza ujumbe wa Biblia wenye uharaka katika nchi yake ya kuzaliwa. Katika 1905 mtu aliyekuwa amekuwa Mwanafunzi wa Biblia katika Amerika alirudi Ugiriki ili kutoa ushahidi. Na katika 1913 kijana mmoja alichukua mbegu za kweli ya Biblia kutoka New York hadi mji wa nyumbani mwa familia yao, Ramallah, si mbali na Yerusalemu.
Kufungua Kazi Katika Eneo la Karibea
Wakati idadi ya waeneza-evanjeli ilipokuwa ikikua katika Marekani, Kanada, na Ulaya, kweli ya Biblia ilikuwa inaanza kutia mizizi pia katika Panama, Kosta Rika, Guiana ya Uholanzi (sasa ni Suriname), na Guiana ya Uingereza (sasa ni Guyana). Joseph Brathwaite, aliyekuwa katika Guiana ya Uingereza wakati aliposaidiwa kuelewa kusudi la Mungu, aliondoka kwenda Barbados katika 1905 ili kutumia wakati wake wote katika kufundisha watu huko. Louis Facey na H. P. Clarke, waliosikia habari njema wakati walipokuwa wakifanya kazi katika Kosta Rika, walirudi Jamaika katika 1897 ili kushiriki imani yao mpya waliyoipata miongoni mwa watu wao wenyewe. Wale waliokubali kweli huko walikuwa wafanyakazi wenye bidii. Katika 1906 pekee, kikundi hicho katika Jamaika kiligawanya trakti zipatazo 1,200,000 na vipande vingine vya fasihi. Mfanyakazi mwingine mhamaji, aliyejifunza kweli katika Panama, alipeleka ujumbe wa tumaini katika Grenada.
Mapinduzi katika Mexico katika 1910-1911 yalikuwa jambo jingine lililosaidia katika kuletea watu wenye njaa ya kweli ujumbe wa Ufalme wa Mungu. Watu wengi walikimbilia kaskazini wakaingia Marekani. Huko baadhi yao walionana na Wanafunzi wa Biblia, wakajifunza juu ya kusudi la Mungu la kuletea wanadamu amani ya kudumu, nao wakapeleka fasihi walikotoka Mexico. Hata hivyo, hiyo haikuwa ndiyo mara ya kwanza kwamba Mexico ilipata kufikiwa na ujumbe huo. Mapema sana kama 1893, Watch Tower lilichapisha barua kutoka kwa F. de P. Stephenson, wa Mexico, aliyekuwa amesoma baadhi ya vichapo vya Watch Tower Society naye alitaka zaidi ili avishiriki pamoja na marafiki wake katika Mexico na katika Ulaya pia.
Ili kufungua nchi zaidi za Karibea kwa kazi ya kuhubiri kweli ya Biblia na kupanga mikutano ya ukawaida kwa ajili ya funzo, Ndugu Russell alituma E. J. Coward kwenda Panama katika 1911 na kisha kwenye visiwa. Ndugu Coward alikuwa msemaji mwenye mkazo na mwenye kupendeza, na wasikilizaji ambao mara nyingi walifikia idadi ya mamia walisongamana kusikia hotuba zake zenye kukanusha fundisho la moto wa helo na kutokufa kwa nafsi ya kibinadamu, pia akisimulia juu ya wakati ujao mtukufu kwa ajili ya dunia. Alisonga toka mji mmoja kwenda ufuatao, na toka kisiwa kimoja hadi kingine—St. Lucia, Dominika, St. Kitts, Barbados, Grenada, na Trinidad—akifikia watu wengi iwezekanavyo. Pia alitoa hotuba katika Guiana ya Uingereza. Alipokuwa Panama, alikutana na W. R. Brown, ndugu kijana Mjamaika mwenye bidii sana, ambaye baada ya hapo alitumika pamoja na Ndugu Coward katika visiwa kadhaa vya Karibea. Baadaye Ndugu Brown alisaidia kufungua kazi katika mashamba mengine.
Katika 1913, Ndugu Russell mwenyewe alitoa hotuba katika Panama, Kuba, na Jamaika. Majumba mawili yalijaa pomoni kwa ajili ya hotuba ya watu wote aliyotoa katika Kingston, Jamaika, na bado watu 2,000 hawakuruhusiwa kuingia kwa kutokuwa na nafasi. Vyombo vya habari vilitaja uhakika wa kwamba msemaji hakusema lolote juu ya pesa na michango haikukusanywa.
Nuru ya Kweli Yafika Afrika
Afrika vilevile ilikuwa ikipenywa na nuru ya kweli wakati wa pindi hiyo. Barua moja iliyopelekwa kutoka Liberia katika 1884 ilifunua kwamba msomaji wa Biblia huko alikuwa amepata nakala moja ya Food for Thinking Christians naye alitaka vichapo zaidi ili kushiriki pamoja na wengine. Miaka michache baada ya hapo, iliripotiwa kwamba kasisi mmoja katika Liberia alikuwa ameacha cheo chake cha kasisi ili awe huru kufundisha wengine kweli za Biblia alizokuwa amejifunza kwa msaada wa Watch Tower na kwamba mikutano ya ukawaida ilikuwa ikifanywa huko na kikundi cha Wanafunzi wa Biblia.
Mhudumu wa Dutch Reformed Church kutoka Uholanzi alichukua baadhi ya vichapo vya C. T. Russell akaenda navyo alipotumwa Afrika Kusini katika 1902. Ijapokuwa yeye hakunufaishwa navyo kwa njia yenye kudumu, Frans Ebersohn na Stoffel Fourie, walioziona fasihi hizo katika maktaba yake, walinufaika. Miaka michache baadaye, idadi katika sehemu hiyo ya shamba iliimarishwa wakati Wanafunzi wa Biblia wawili wenye bidii kutoka Scotland walipohamia Durban, Afrika Kusini.
Kwa kuhuzunisha, miongoni mwa wale waliopata fasihi zilizoandikwa na Ndugu Russell na kisha wakatumia baadhi yazo kufundisha wengine, kulikuwa wachache, kama vile Joseph Booth na Elliott Kamwana, waliochanganya mawazo yao wenyewe, yaliyokusudiwa kuchochea mabadiliko ya kijamii. Kwa baadhi ya watazamaji katika Afrika Kusini na Nyasaland (baadaye ikawa Malawi), jambo hilo lilielekea kuvuruga utambulisho wa Wanafunzi wa Biblia wa kweli. Hata hivyo, wengi walikuwa wakisikia na kuthamini ujumbe uliovuta uangalifu kwenye Ufalme wa Mungu ukiwa suluhisho kwa matatizo ya wanadamu.
Hata hivyo, kwa habari ya kazi ya kuhubiri yenye kuenea barani Afrika, hiyo ilikuwa bado ni ya wakati ujao.
Kwenda Nchi za Mashariki na Visiwa vya Pasifiki
Muda mfupi baada ya vichapo vya Biblia vilivyotayarishwa na C. T. Russell kugawanywa mara ya kwanza katika Uingereza, vilifika nchi za Mashariki pia. Katika 1883, Bi. C. B. Downing, mishonari Mpresbiteri katika Chefoo (Yantai), China, alipokea nakala moja ya Watch Tower. Alithamini yale aliyojifunza juu ya kufanywa upya kwa vitu vyote naye alishiriki fasihi hizo na wamishonari wengine, kutia na Horace Randle, aliyeshirikiana na Baraza la Misheni ya Kibaptisti. Baadaye, kupendezwa kwake kulichochewa zaidi na tangazo juu ya Millennial Dawn lililotokea katika gazeti Times la London, nalo lilifuatwa na nakala za vitabu vyenyewe—kimoja kutoka kwa Bi. Downing na kingine kilichopelekwa na mama yake aliyeishi Uingereza. Mwanzoni, alishtushwa na yale aliyosoma. Lakini mara alipopata kusadikishwa kwamba Utatu si fundisho la Biblia, aliacha Kanisa la Baptisti na akaendelea kushiriki na wamishonari wengine yale aliyokuwa amejifunza. Katika 1900 yeye aliripoti kwamba alikuwa amepeleka barua 2,324 na trakti zipatazo 5,000 kwa wamishonari katika China, Japani, Korea, na Siam (Thailand). Wakati ule ushahidi ulikuwa ukitolewa sanasana kwa wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo katika nchi za Mashariki.
Katika pindi iyo hiyo ya wakati, mbegu za kweli zilipandwa pia katika Australia na New Zealand. “Mbegu” za kwanza kati ya hizo zilizowasili katika Australia huenda zikawa zilipelekwa huko katika 1884 au muda mfupi baada ya hapo na mtu aliyefikiwa kwanza na Mwanafunzi wa Biblia katika bustani nchini Uingereza. “Mbegu” nyinginezo zilikuja kwa barua kutoka kwa marafiki na watu wa ukoo kutoka ng’ambo.
Katika muda wa miaka michache baada ya kufanyizwa kwa Jumuiya ya Mikoa ya Australia katika 1901, mamia ya watu huko walikuwa waandikishaji wa Watch Tower. Kama tokeo la utendaji wa wale walioona pendeleo la kushiriki kweli na wengine, maelfu ya trakti zilipelekewa watu ambao majina yao yalikuwa katika orodha ya wenye kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura. Trakti zaidi ziligawanywa kwa watu barabarani, na wafanyakazi na wenye nyumba waliokuwa peke yao katika sehemu za mbali zilizokuwa kandokando ya njia za reli walirushiwa vifurushi vya trakti kutoka katika madirisha ya garimoshi. Watu walikuwa wakijulishwa juu ya mwisho uliokuwa ukikaribia wa Nyakati za Mataifa katika 1914. Arthur Williams, Sr., aliongea juu ya jambo hilo na wateja wote katika duka lake katika Magharibi mwa Australia na akawaalika wenye kupendezwa nyumbani kwake kwa mazungumzo zaidi.
Haijulikani sasa ni nani aliyefika New Zealand kwanza akiwa na kweli ya Biblia. Lakini kufikia 1898, Andrew Anderson, mkazi wa New Zealand, alikuwa amesoma vichapo vya Watch Tower vya kutosha kusukumwa kueneza kweli huko akiwa kolpota. Jitihada zake ziliimarishwa katika 1904 na makolpota wengine waliokuja kutoka Amerika na kutoka ofisi ya tawi ya Sosaiti iliyoanzishwa mwaka huohuo katika Australia. Bi. Thomas Barry, katika Christchurch, alikubali mabuku sita ya Studies in the Scriptures kutoka kwa mmojawapo makolpota. Mwana wake Bill alivisoma katika 1909 wakati wa safari ya majuma sita ya kwenda Uingereza kwa merikebu naye akatambua ukweli wa yaliyokuwamo. Miaka mingi baadaye mwanae Lloyd alipata kuwa mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova.
Miongoni mwa wafanyakazi wenye bidii katika siku hizo za mapema alikuwa Ed Nelson, ambaye, ijapokuwa hakuwa mwenye busara sana, alitumia wakati wake wote kwa miaka 50 akieneza ujumbe wa Ufalme toka ncha ya kaskazini ya New Zealand hadi kusini. Baada ya miaka michache, Frank Grove ambaye alisitawisha kumbukumbu lake ili kusaidia hali yake ya kutoweza kuona vizuri, na ambaye pia alipainia kwa miaka zaidi ya 50 mpaka kifo chake, alijiunga naye.
Safari ya Ulimwengu ili Kuendeleza Kuhubiriwa kwa Habari Njema
Jitihada nyingine kubwa ilifanywa katika 1911-1912 ili kusaidia watu wa nchi za Mashariki. International Bible Students Association lilituma halmashauri ya wanaume saba, ikiongozwa na C. T. Russell, ili wao binafsi wakadirie hali huko. Kokote walikoenda walisema juu ya kusudi la Mungu la kuletea wanadamu baraka kwa njia ya Ufalme wa Kimesiya. Nyakati nyingine wasikilizaji wao walikuwa wachache, lakini katika Filipino na India, kulikuwa maelfu. Wao hawakuunga mkono kampeni iliyopendwa na wengi wakati huo katika Jumuiya ya Wakristo ya kukusanya pesa kwa ajili ya wongofu wa ulimwengu. Waliona kwamba jitihada iliyo nyingi ya wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo ilitumiwa katika kuendeleza elimu ya kilimwengu. Lakini Ndugu Russell alisadiki kwamba walichohitaji watu kilikuwa “ile Gospeli ya uandalizi wa upendo wa Mungu wa Ufalme ujao wa Mesiya.” Badala ya kutarajia kuongoa ulimwengu, Wanafunzi wa Biblia walielewa kutoka kwa Maandiko kwamba jambo lililopasa kufanywa wakati huo lilikuwa kutoa ushahidi na kwamba hilo lingetumikia kusudi la kukusanya “wachaguliwa wachache kutoka kwa mataifa yote, jamaa, kabila na lugha ili kushiriki katika jamii ya Bibi-arusi wa [Kristo]—ili kukaa pamoja Naye katika kiti Chake cha ufalme wakati wa miaka elfu, wakishirikiana kuinua jamii nzima ya kibinadamu.”a—Ufu. 5:9, 10; 14:1-5.
Baada ya kutumia wakati katika Japani, China, na Filipino, na kwingineko, hao washiriki wa halmashauri hiyo waliongeza kilometa 6,400 zaidi za safari katika India. Watu fulani mmoja-mmoja waliokuwa wakiishi India walikuwa wamesoma fasihi za Sosaiti nao walikuwa wameandika barua kuonyesha uthamini wao kwa ajili yayo mapema sana kama 1887. Kazi ya kutoa ushahidi kwa bidii ilikuwa imefanywa pia miongoni mwa watu wenye kusema lugha ya Tamil tangu 1905 na kijana mmoja mwanamume ambaye, akiwa mwanafunzi katika Amerika, alikuwa amekutana na Ndugu Russell naye akajifunza kweli. Mwanamume huyo kijana alisaidia kuanzisha vikundi vya funzo la Biblia vipatavyo 40 kusini mwa India. Lakini, baada ya kuhubiria wengine, yeye mwenyewe alipata kupoteza kibali kwa kuacha kufuata viwango vya Kikristo.—Linganisha 1 Wakorintho 9:26, 27.
Hata hivyo, karibu na wakati huohuo, A. J. Joseph, wa Travancore (Kerala), katika kujibiwa ulizo alilokuwa amemuuliza kwa barua Mwadventisti mashuhuri, alipelekewa buku la Studies in the Scriptures. Humo alipata majibu ya Kimaandiko yenye kuridhisha kwa maswali yake juu ya Utatu. Upesi yeye na washiriki wa familia yake walitoka kwenda kwenye mashamba ya mpunga na minazi ya kusini mwa India wakishiriki imani zao mpya walizozipata. Baada ya ziara ya Ndugu Russell katika 1912, Ndugu Joseph alianza utumishi wa wakati wote. Kwa njia ya reli, mkokoteni wenye kukokotwa na ng’ombe, mashua, na kwa miguu, alisafiri kugawanya fasihi za Biblia. Alipokuwa akitoa hotuba za watu wote, mara nyingi zilikatizwa na makasisi na wafuasi wao. Katika Kundara, wakati kasisi “Mkristo” alipokuwa akitumia wafuasi wake kukatiza mkutano kama huo na kumtupia Ndugu Joseph kinyesi, mwanamume muungwana mashuhuri Mhindu alikuja kuona kelele zilikuwa za nini. Alimwuliza kasisi huyo hivi: ‘Je, hicho ndicho kielelezo kilichowekwa na Kristo cha kufuatwa na Wakristo, au je, yale unayofanya ni kama mwenendo wa Mafarisayo wa wakati wa Yesu?’ Kasisi huyo akaondoka.
Kabla ya ile safari ya miezi minne ya ulimwengu ya halmashauri ya IBSA haijakamilishwa, Ndugu Russell alikuwa amepangia R. R. Hollister kuwa mwakilishi wa Sosaiti katika nchi za Mashariki na kuhakikisha kwamba kazi inafanywa ya kueneza kwa vikundi vya watu ujumbe wa uandalizi wa upendo wa Mungu wa Ufalme wa Kimesiya. Trakti za pekee zilitayarishwa katika lugha kumi, na mamilioni yazo yalienezwa kotekote katika India, China, Japani, na Korea na waenezaji wenyeji. Kisha vitabu vilitafsiriwa katika lugha nne kati ya hizo ili kuandaa chakula zaidi cha kiroho kwa wale walioonyesha kupendezwa. Hapa palikuwa na shamba kubwa, na mengi bado yalihitaji kufanywa. Hata hivyo, yale yaliyokuwa yametimizwa kufikia hapo yalikuwa yenye kustaajabisha kwelikweli.
Ushahidi Wenye Kutokeza Ulitolewa
Kabla uharibifu wa vita ya kwanza ya ulimwengu haujaanzishwa, ushahidi wa bidii ulikuwa umetolewa ulimwenguni pote. Ndugu Russell alikuwa amesafiri kutoa hotuba katika mamia ya majiji katika Marekani na Kanada, alikuwa amesafiri mara kadhaa kwenda Ulaya, alikuwa ametoa hotuba katika Panama, Jamaika, na Kuba, pamoja na majiji makuu ya nchi za Mashariki. Makumi ya maelfu ya watu walikuwa wamesikia hotuba zake za Biblia zenye kusisimua na walikuwa wameona akijibu hadharani kutoka kwa Maandiko maswali yaliyozushwa na marafiki na maadui pia. Kupendezwa kwingi kulikuwa kumechochewa kwa njia hiyo, na maelfu ya magazeti katika Amerika, Ulaya, Afrika Kusini, na Australia yalikuwa yakichapisha kwa ukawaida mahubiri ya Ndugu Russell. Mamilioni ya vitabu, pamoja na mamia ya mamilioni ya trakti na fasihi nyinginezo katika lugha 35, vilikuwa vimegawanywa na Wanafunzi wa Biblia.
Ingawa fungu lake lilikuwa lenye kutokeza, si Ndugu Russell pekee aliyekuwa akihubiri. Wengine vilevile, waliotawanyika kotekote duniani, walikuwa wakiunganisha sauti zao wakiwa mashahidi wa Yehova na Mwana wake, Yesu Kristo. Wale walioshiriki hawakuwa wote watoaji wa hotuba za watu wote. Walikuwa watu wa kila aina, nao walitumia kila njia iliyofaa waliyokuwa nayo ili kueneza habari njema.
Katika Januari 1914, mwisho wa Nyakati za Mataifa ukiwa umbali unaopungua mwaka mmoja, ushahidi mwingine wa bidii ulianzishwa. Huo ulikuwa ni ile “Photo-Drama of Creation,” iliyokazia kwa njia mpya kusudi la Mungu kwa dunia. Ilifanya hivyo kwa njia ya slaidi nzuri zenye rangi zilizochorwa kwa mkono na sinema, zilizoambatana na sauti. Vyombo vya habari vya umma katika Marekani viliripoti kwamba kotekote nchini mamia ya maelfu ya watazamaji walikuwa wakizitazama kila juma. Kufikia mwisho wa mwaka wa kwanza, jumla ya hudhurio katika Marekani na Kanada ilikuwa imefika karibu milioni nane. Katika London, Uingereza, kulikuwa umati uliojaa na ukazidi kwenye majumba Opera House na Royal Albert Hall ili kuona wonyesho huo wa picha uliokuwa wa sehemu nne za saa 2 kila moja. Katika muda wa nusu mwaka, zaidi ya watu 1,226,000 walikuwa wamehudhuria katika majiji 98 katika Visiwa Uingereza. Vikundi vya umati katika Ujerumani na Uswisi vilijaza kabisa majumba yaliyokuwa yanapatikana. Pia ilionwa na watazamaji wengi katika nchi za Skandinevia na visiwa vya Pasifiki Kusini.
Lo! ulikuwa ushahidi wa bidii wenye kutokeza kama nini wa duniani pote uliotolewa katika miongo hiyo ya mapema ya historia ya kisasa ya Mashahidi wa Yehova! Lakini, kwa kweli, kazi ilikuwa ndiyo tu inaanza.
Ni mamia wachache tu waliokuwa wameshiriki kwa bidii katika kueneza kweli ya Biblia wakati wa miaka ya mapema ya 1880. Kufikia 1914, kulingana na ripoti zipatikanazo, kulikuwa kama 5,100 walioshiriki katika kazi. Wengine huenda wakawa waligawanya trakti pindi kwa pindi. Wafanyakazi walikuwa wachache.
Kikosi hiki kidogo cha waeneza-evanjeli kilikuwa, kwa njia mbalimbali, tayari kimeeneza kazi yao ya kupiga mbiu ya Ufalme wa Mungu kuingia katika nchi 68 kufikia nusu ya pili ya 1914. Na kazi yao wakiwa wahubiri na walimu wa Neno la Mungu ilikuwa imeimarishwa kwa msingi uliokuwa imara vya kutosha katika nchi 30 kati ya hizo.
Mamilioni ya vitabu na mamia ya mamilioni ya trakti yalikuwa yamegawanywa kabla ya mwisho wa Nyakati za Mataifa. Kwa kuongezea hayo, kufikia 1913 magazeti ya habari mengi kama 2,000 yalikuwa yakitangaza kwa ukawaida mahubiri yaliyotayarishwa na C. T. Russell, na katika mwaka 1914 wasikilizaji wanaojumlika kuwa zaidi ya 9,000,000 katika mabara matatu waliona ile “Photo-Drama of Creation.”
Kwelikweli, ushahidi wenye kushangaza ulikuwa umetolewa! Lakini mengi zaidi yangekuja.
[Maelezo ya Chini]
a Ripoti kamili juu ya safari hiyo ya ulimwengu huonekana katika The Watch Tower la Aprili 15, 1912.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 405]
C. T. Russell binafsi alitoa hotuba za Biblia katika majiji zaidi ya 300 (katika maeneo yanayoonyeshwa kwa alama) katika Amerika Kaskazini na Karibea—katika mengi yayo mara 10 au 15
[Ramani]
(See publication)
[Ramani katika ukurasa wa 407]
(See publication)
Safari za Russell za kwenda kuhubiri Ulaya, kwa kawaida kupitia Uingereza
1891
1903
1908
1909
1910 (mara mbili)
1911 (mara mbili)
1912 (mara mbili)
1913
1914
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 408]
Aliposadiki kwamba alikuwa amepata kweli, Andreas Øiseth aligawanya kwa bidii fasihi za Biblia katika karibu kila sehemu ya Norway
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
NORWAY
Mzingo Aktiki
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 409]
Adolf Weber, mtunza-bustani mnyenyekevu, alieneza habari njema kutoka Uswisi hadi kwenye nchi nyinginezo katika Ulaya
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UBELGIJI
UJERUMANI
USWISI
ITALIA
UFARANSA
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 413]
Bellona Ferguson, katika Brazili—“hakuna walio mbali mno wasiweze kufikiwa”
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BRAZILI
[Ramani katika ukurasa wa 415]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ALASKA
KANADA
GREENLAND
ST. PIERRE NA MIQUELON
MAREKANI
BERMUDA
BAHAMAS
VISIWA VYA TURKS NA CAICOS
KUBA
MEXICO
BELIZE
JAMAIKA
HAITI
JAMHURI YA DOMINIKA
PUERTO RIKO
VISIWA VYA CAYMAN
GUATEMALA
EL SALVADOR
HONDURAS
NIKARAGUA
KOSTA RIKA
PANAMA
VENEZUELA
GUYANA
SURINAME
GUIANA YA UFARANSA
KOLOMBIA
EKUADO
PERU
BRAZILI
BOLIVIA
PARAGUAI
CHILE
ARGENTINA
URUGUAI
VISIWA VYA FALKLAND
VISIWA VYA VIRGIN (MAREKANI)
VISIWA VYA VIRGIN (UINGEREZA)
ANGUILLA
ST. MAARTEN
SABA
ST. EUSTATIUS
ST. KITTS
NEVIS
ANTIGUA
MONTSERRAT
GUADELOUPE
DOMINIKA
MARTINIQUE
ST. LUCIA
ST. VINCENT
BARBADOS
GRENADA
TRINIDAD
ARUBA
BONAIRE
KURASAO
BAHARI YA ATLANTIKI
BAHARI YA KARIBEA
BAHARI YA PASIFIKI
[Ramani katika ukurasaw wa 416, 417]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
GREENLAND
SWEDEN
ICELAND
NORWAY
VISIWA VYA FAEROE
FINLAND
URUSI
ESTONIA
LATVIA
LITHUANIA
BELARUS
UKRAINIA
MOLDOVA
GEORGIA
ARMENIA
AZERBAIJAN
TURKMENISTAN
UZBEKISTAN
KAZAKHSTAN
TAJIKISTAN
KYRGYZSTAN
POLAND
UJERUMANI
UHOLANZI
DENMARK
UINGEREZA
IRELAND
UBELGIJI
LUXEMBOURG
LIECHTENSTEIN
USWISI
CHEKOSLOVAKIA
AUSTRIA
HUNGARIA
RUMANIA
YUGOSLAVIA
SLOVENIA
KROATIA
BOSNIA NA HERZEGOVINA
BULGARIA
ALBANIA
ITALIA
GIBRALTAR
HISPANIA
URENO
MADEIRA
MOROKO
SAHARA MAGHARIBI
SENEGAL
ALGERIA
LIBYA
MISRI
LEBANONI
ISRAELI
SAIPRASI
SIRIA
UTURUKI
IRAKI
IRAN
BAHRAIN
KUWAIT
YORDANI
SAUDI ARABIA
KATAR
MUUNGANO WA FALME ZA KIARABU
OMANI
YEMENI
JIBUTI
SOMALIA
ETHIOPIA
SUDAN
CHAD
NIGER
MALI
MAURITANIA
GAMBIA
GUINEA-BISSAU
SIERRA LEONE
LIBERIA
CÔTE D’IVOIRE
GHANA
TOGO
BENIN
GUINEA YA IKWETA
ST. HELENA
GUINEA
BURKINA FASO
NIGERIA
JAMHURI YA AFRIKA YA KATI
KAMERUN
SÃO TOMÉ
KONGO
GABON
ZAIRE
ANGOLA
ZAMBIA
NAMIBIA
BOTSWANA
AFRIKA KUSINI
LESOTHO
SWAZILAND
MSUMBIJI
MADAGASKA
RÉUNION
MAURITIUS
RODRIGUES
ZIMBABWE
MAYOTTE
KOMORO
SHELISHELI
MALAWI
TANZANIA
BURUNDI
RWANDA
UGANDA
UFARANSA
PAKISTAN
AFGHANISTAN
NEPAL
BHUTAN
MYANMAR
BANGLADESH
INDIA
SRI LANKA
UGIRIKI
MALTA
TUNISIA
KENYA
BAHARI YA ATLANTIKI
BAHARI YA HINDI
ALASKA
MONGOLIA
JAMHURI YA KIDEMOKRASI YA WATU WA KOREA
JAPANI
JAMHURI YA KOREA
CHINA
MACAO
TAIWAN
HONG KONG
LAOS
THAILAND
VIETNAM
KAMBODIA
FILIPINO
BRUNEI
MALASIA
SINGAPORE
INDONESIA
SAIPAN
ROTA
GUAM
YAP
BELAU
CHUUK
POHNPEI
KOSRAE
VISIWA VYA MARSHALL
NAURU
PAPUA NEW GUINEA
AUSTRALIA
NEW ZEALAND
KISIWA CHA NORFOLK
NEW CALEDONIA
VISIWA VYA WALLIS NA FUTUNA
VANUATU
TUVALU
FIJI
KIRIBATI
TOKELAU
HAWAII
SAMOA MAGHARIBI
SAMOA YA MAREKANI
NIUE
TONGA
VISIWA VYA COOK
TAHITI
VISIWA VYA SOLOMON
BAHARI YA PASIFIKI
BAHARI YA HINDI
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 421]
A. J. Joseph, wa India, pamoja na binti yake Gracie, aliyetumikia akiwa mishonari aliyezoezwa Gileadi
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
INDIA
[Picha katika ukurasa wa 411]
Hermann Herkendell, pamoja na bibi-arusi wake, walifunga safari ya miezi mingi wakati wa fungate yao wakahubirie wasemao Kijerumani katika Urusi
[Picha katika ukurasa wa 412]
Makolpota katika Uingereza na Scotland walijitahidi kumpa kila mtu fursa ya kupokea ushahidi; hata watoto wao walisaidia kugawanya trakti
[Picha katika ukurasa wa 414]
E. J. Coward alieneza kwa bidii kweli ya Biblia katika eneo la Karibea
[Picha katika ukurasa wa 418]
Frank Grove (kushoto) na Ed Nelson (waonekanao hapa wakiwa na wake zao) kila mmoja alitumia zaidi ya miaka 50 kueneza ujumbe wa Ufalme wakati wote kotekote katika New Zealand
[Picha katika ukurasa wa 420]
C. T. Russell na washirika sita walifunga safari ya ulimwenguni pote katika 1911-1912 ili kuendeleza kazi ya kuhubiri habari njema