Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
MFALME Sulemani alikuwa mmoja wa watu wenye hekima zaidi waliopata kuishi. Aliutaja ukweli huu: “Nimejipatia hekima nyingi kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; naam, moyo wangu umeona kwa wingi hekima na maarifa.” (Mhu. 1:16) Aliposema kwamba ‘moyo wake umeona kwa wingi hekima na maarifa,’ Sulemani alikuwa na maana ya kwamba ubongo wake haukujawa na habari nyingi tu. Bali hekima na maarifa yalikuwa yameugusa moyo wake, yakawa ndani yake kabisa. Alithamini ubora wayo, kisha akataka kuyatumia maarifa hayo na hekima hiyo.
Sulemani alitafuta hekima kwa kuchunguza pande zote za mambo. Anaeleza hivi: “Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu. . . . Nikatia moyo wangu ili kuijua hekima, na kujua wazimu na upumbavu” (Mhu. 1:13, 17) Sulemani alichochewa awe mwenye bidii na kujitahidi kwa moyo wote aifahamu sana hekima. Yeye hakuchunguza amri za hekima tu, bali alipeleleza wazimu na upumbavu pia. Alichunguza kwa uangalifu jinsi wanadamu wengine walivyofuata wazimu na upumbavu. Sulemani alikata maneno kwa njia nzuri juu ya jinsi ya kuepuka matatizo, akitegemea mambo aliyoona.
Alijifunza nini kutokana na uchunguzi wake mwingi wa pande zote za maarifa na hekima ya kilimwengu? “Hayo yote nayo ni kujilisha upepo. Yaani, katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni; naye aongezaye maarifa huongeza masikitiko.”—Mhu. 1:17,18.
Kama alivyoonyesha Sulemani, sababu kubwa ya mambo kuwa hivyo ni hii: “Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, wala yasiyokuwapo hayahesabiki.” (Mhu. 1:15) Mtu anayeongeza maarifa ya kilimwengu anapata masikitiko ya kujua kwamba mambo mengi “yaliyopotoka” katika taratibu hii isiyo kamilifu hayawezi kunyoshwa. Wakati wala hali haziruhusu yasahihishwe. Kwa kweli, mambo mengi ya kibinadamu yana kasoro hivi kwamba hayawezi hata kuhesabiwa. Basi, kadiri mtu azidivyo kuwa na maarifa na hekima, ndivyo azidivyo kujua jinsi alivyo na nafasi chache za kubadili mambo yawe bora. Maisha mafupi na hali zisizopendeza katika jamii ya kibinadamu isiyo kamilifu zinamtatiza. Basi anaudhika na kuvurugika akili.
Walakini, hekima ya kimungu haileti matokeo hayo mabaya, bali inaongeza tumaini, imani na uhakika. Hekima hiyo inaelezwa katika Maandiko kama hivi: “Hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.” (Yak. 3:17) Wewe unakaza fikira nyingi zaidi juu ya hekima ya aina gani—juu ya ile inayovuruga akili au juu ya hekima ya kimungu, aina ambayo inaweza kukusaidia upate faida zote za maisha hata sasa?