Kujua Yaliyo Katika Habari
“Wanawake Wakiozwa”
Si kwamba tu kuna ongezeko la kufunga ndoa katika United States—ongezeko la asimilia 16 kutoka miaka kumi iliyopita—bali pia gharama ya kufunga ndoa imeongezeka. Wastani wa matumizi ya pesa kuhusu arusi na karamu ya arusi imeongezeka sana kupita dola 6,000 na arusi nyingine zimekuwa za anasa sana zikawa na matumizi ya dola zaidi ya 50,000. Je! ni ajabu kwamba gharama za arusi mwaka jana zilikuwa dola elfu 20 milioni—ongezeko la asimilia 152 tangu mwaka 1975? Pesa hizo zilitumiwa kuhusu nini? Kuhusu karibu vitu vya kila namna “kuanzia pete na maua mpaka kwenye muziki, magari ya bei kubwa sana, na safari za kwenda malikizo ya arusi,” inaripoti gazeti Fortune.
Arusi zinapasa kuwa pindi zenye furaha. Hata hivyo, Yesu Kristo alionyesha upande mmoja wa ndoa kuwa ungeonyesha tabia ya kizazi ambacho kingeishi wakati wa ‘kuwapo kwake na umalizio wa mfumo huu mbovu wa mambo.’ (Mathayo 24:3, 34,NW) Yeye alisema: “Kama vile siku za Noa zilivyokuwa, vivyo ndivyo kuwapo kwa Mwana wa mtu kutakavyokuwa. Kwa maana kama walivyokuwa katika siku hizo kabla ya gharika, wakila na kunywa, wanaume wakioa na wanawake wakiozwa, mpaka siku ile Noa aliyoingia ndani ya safina; nao hawakujali mpaka gharika ikaja na kuwafagia mbali wote, vivyo ndivyo kuwapo kwa Mwana wa mtu kutakavyokuwa,” (Mathayo 24:37-39, NW) Yesu hakumaanisha kwamba ni kosa kwa watu wanaoishi katika “siku za mwisho” kufunga ndoa. (2 Timotheo 3:1) Bali, yeye alionya kwamba wengi wangejihusisha sana katika ndoa, jambo ambalo sasa limekuja kutia ndani arusi zenye mapambo na gharama nyingi kupita kiasi, mpaka waupuuze uharaka wa nyakati hizi.
“Ni Nani Aliyevificha Vitabu vya Kukunjwa vya Bahari ya Chumvi?”
Chini ya kichwa hicho, katika kichapo Biblical Archaeologist, Norman Golb, profesa wa Uchunguzi wa Kiebrania na Kiyuda na Kiarabu kwenye Chuo Kikuu cha Chicago anajikaza afunue ni nani kwa kweli aliyevificha Vitabu vya Kukunjwa vya Bahari ya Chumvi. Wakati ule ule, yeye anajaribu kukanusha nadharia ambayo imekuwapo kwa makumi zaidi ya matatu. Katika masika ya mwaka 1947, vitabu vya kukunjwa vya kale vya Maandiko ya Kiebrania na maandishi yasio ya Kibiblia viligunduliwa katika mapango kando kando ya pwani ya magharibi kaskazini ya Bahari ya Chumvi. Ugunduzi huo ulishangiliwa kuwa “pato lililo kubwa zaidi ambalo limeweza kufanywa katika shughuli ya kuchimbua vitu vya kale vya kibiblia.” Vitabu hivi vya kukunjwa ni kutia ndani hati zinazojulikana zilizo za zamani zaidi za vitabu vyo vyote vya Biblia, navyo ni vya kurudi nyuma kwenye karne ya pili K. W. K.
Mpaka sasa, wanachuo wamewahesabia Waessene, madhehebu ya kidini ya Wayahudi, kuwa ndio waliokuwa kwanza na hati hizo. Lakini Golb anaamini kwamba magunduzi ya baadaye ya maandishi zaidi ya kale ya Kiebrania ya Masada, Jeriko, na kwingineko katika jangwa la Yudea yanaonyesha kwamba Yerusalemu ndipo mahali ambapo vitabu vile vya kukunjwa vilitoka mara ya kwanza. Si Waessene, bali ni Wayahudi wenye kuyakimbia majeshi ya Waroma kati ya mwaka 66 na 70 W. K. “walivileta vifurushi au magunia yaliyojazwa maandishi kutoka mji mkuu kuyaleta kwenye mapango ya jangwa ili wayafiche,” anashikilia Golb.
Bila kujali ni ushuhuda gani zaidi unaoweza kuchimbuliwa, vitabu vya kukunjwa vya Kibiblia vilivyopatikana kwenye mapango hayo vinakazia usafi wa maandishi ya Biblia na uwezo wa Yehova kuhifadhi Neno lake. “Miili yote ni kama majani, na utukufu wake wote ni kama kuchanua kwa maua ya majani; majani hunyauka, nayo maua huanguka, lakini usemi wa Yehova wadumu milele,” linasema andiko la 1 Petro 1:24, 25, NW.
Je! Ni Hekima ya Kimungu kwa Viongozi wa Ulimwengu?
Inapoendelea kuwa vigumu zaidi kupata amani ya ulimwengu, tisho linaloendelea kuwapo daima la kutokea vita linatawala akili za viongozi wa ulimwengu. Gazeti Time liliripoti kwamba kiongozi wa chama cha Urusi Mikhail S. Gorbachev aliomboleza hivi: “Kwa hakika, Mungu kule juu hakukataa kutupa hekima inayotosha ya kupata njia ya kuleta maendeleo . .. katika uhusiano kati ya yale mataifa mawili makubwa duniani, ambayo ndiyo yenye kuamua matokeo ya mwisho wa ustaarabu wa nchi zile nyingine.” Vivyo hivyo, alipokuwa akimalizia hotuba yake yenye ubishi katika Durban, siku ya Agosti 15, Rais wa Afrika ya Kusini P. W. Botha alisema hivi kwa kuhangaikia amani ya taifa lake: “Sisi tumechukua hatua kufanya yote ambayo mwanadamu anaweza kufanya. . . . Mimi nasali kwamba Mungu Mwenyezi atupe hekima na nguvu za kutafuta kutimiza mapenzi Yake.”
Inapendeza kwamba viongozi mashuhuri wa kiserikali wanaongea juu ya uhitaji wa hekima ya kimungu kuhusiana na jitihada zao za kuleta amani. Lakini, kulingana na Biblia, amani na usalama wa duniani pote utapatikana kupitia Ufalme wa Mungu tu. (Danieli 2:44; linganisha Isaya 9:6, 7) Hivyo, ni wale tu wanaojipanga upande wa Ufalme huo wa kimbingu wanaoweza kutumaini kupata amani yenye kudumu.