Ile Serikali Kubwa ya Sita ya Ulimwengu Roma!
Milki ya Kiroma ilitawala wakati ambapo Ukristo ulianza. Maarifa bora ya kujua juu ya Roma ya kale yatakusaidia wewe uelewe hali ambazo chini yazo Yesu alihubiri na mazingira yaliyokuwa yameenea sana wakati wafuasi wake wa mapema walipokuwa wakieneza Ukristo katika sehemu zote za ulimwengu uliojulikana wakati huo.
ROMA, ile serikali kubwa ya sita ya ulimwengu ya historia ya Biblia, ilikuwa inatawala wakati Yesu alipozaliwa na wakati mitume wake walipohubiri. Ugiriki, serikali kubwa ya ulimwengu iliyotangulia, ilikuwa imeandaa lugha ya kimataifa ambayo kwayo fundisho la Kikristo lingeweza kuendelezwa katika maeneo yote ya sehemu hiyo ya ulimwengu—ile Koine, au Kigiriki cha kawaida. Sasa Roma iliandaa hali na barabara zilizosaidia katika mwenezo wa haraka sana wa ukweli wa Kikristo.
Roma, ambayo wakati mmoja ilikuwa jiji dogo katika Latium, Italia, ilikua sana mpaka ikawa ndiyo milki kubwa zaidi ya zote za ulimwengu wa nyakati za kale za Biblia. Kwanza, ilipanuka ili kudhibiti peninsula ya Italia. Ilishinda Carthage yenye uweza katika pwani ya kaskazini mwa Afrika. Hispania, Makedonia na Ugiriki zikaja chini ya udhibiti wayo. Ndipo ilipoteka Yerusalemu katika 63 K.W.K. na kufanya Misri iwe mkoa wa Kiroma katika 30 K.W.K. Ilipofikia kilele chayo, milki hii yenye uweza ilitandaa kuanzia Uingereza kuja chini mpaka Misri na kutoka Ureno kwenda mwendo wote ule mpaka Mesopotamia, lile bara la Babuloni wa kale. Ilizunguka kabisa Mediterania ambayo iliiita Mare Nostrum (Bahari Yetu).
Magofu mengi ya Kiroma yangali yanaweza kufanyiwa ziara katika sehemu zote za eneo la milki hiyo iliyoenea mpaka mbali. Unaweza kuona Ukuta wa Hadriani katika Uingereza, ule mtaro mkubwa wa maji ulio na fahari sana kule Segovia katika Hispania, uwanja wa tamasha za Kiroma kule Orange, na uwanja wa mapigano ya nduli katika Arles (zote hizo mbili zikiwa katika Ufaransa ya kusini). Unaweza kutembea kupita magofu manyamavu ya Ostia Antica, karibu na Roma, na kustaajabia Pompeii ya kale, kusini mwa Naples. Katika Roma unaweza kuwazia misongamano ya watu wenye msisimuko katika ile Kolosiamu na kuona Tao la Tito linalotoa ukumbusho wa uharibifu wake wa Yerusalemu na hekalu lao katika 70 W.K., uliotabiriwa na Yesu zaidi ya miaka 35 mapema.
Katika Roma ya kale matajiri walikuwa na jamaa kubwa-kubwa, wakiwa na watumishi na watumwa ambao nyakati fulani walifikia mamia. Maskini walisongamana ndani ya vijumba vyenye ghorofa nyingi vilivyofuatana msururu katika barabara chafu, zenye kwenda kombo-kombo. Ni wachache sana ambao wangeweza kuitwa kuwa wa tabaka la katikati. Serikali iliandaa bila malipo alawansi fulani ya nafaka na kitumbuizo ili kuzuia maskini wasifanye ghasia. Kodi zilizoamrishwa katika mikoa ndizo zilizolipia gharama hizi.
Jeshi la Kiroma
Lile jeshi la Kiroma lenye sifa kubwa lilifanyizwa na hesabu fulani ya lejioni. Kila lejioni, ambayo ilikuwa na wanaume 4,500 mpaka 7,000, ilikuwa jeshi kamili yenyewe. Daraka la amiri la kujibu jinsi alivyoendesha kazi yake lilikuwa kwa mmaliki peke yake. Lejioni iligawanywa katika senchari 60, ambayo kwa kawaida yalikuwa ya wanaume mia moja kila moja. Senchari ilikuwa chini ya uongozi wa msenchari, ambaye anaitwa “afisa wa jeshi” katika Biblia ya New World Translation. Msenchari ndiye aliyekuwa msimamizi wa wale askari wanne walioua Yesu na ambao, walipoona hali na ajabu za kimuujiza zilizozunguka kifo chake, walisema: “Kwa uhakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” (Mathayo 27:54; Yohana 19:23, NW) Ni msenchari pia, Kornelio, aliyekuwa mtu wa kwanza asiye Myahudi mtahiriwa kuwa Mkristo.—Matendo 10:22.
Lejioni zilikuwa na nembo, yaonekana ni mifano au vifananisho vilivyofanywa kwa miti au metali, ambazo zilitumikia kusudi linalofanana na lile linalotumikiwa na bendera za ki-siku-hizi. Zikiwa zinaonwa kuwa takatifu, zilipewa ulinzi kwa hasara ya uhai wa kibinadamu. Encyclopædia Britannica inasema: “Nembo za Kiroma zililindwa kwa staha nyingi mno ya kidini katika mahekalu ya Roma. Halikuwa jambo lisilo la kawaida kwa jemadari kuagiza nembo itupwe katikati ya maadui, ili kuongeza juhudi ya kuchochea askari zake wawarukie ili kurudisha kile ambacho kwa maoni yao labda kilikuwa ndicho kitu kitakatifu zaidi kilichopata kuwa duniani.”
Barabara na Mitajo ya Vyeo vya Kiroma
Roma ilifanyiza mataifa yaliyokuwa chini yake yakawa milki ya ulimwengu. Iliandaa barabara kufanya sehemu zote za milki hii ziweze kufikiwa. Na watu walisafiri we! Wewe tazama tu ile orodha ya mahali-mahali walikokuwa wametoka watu waliokuja Yerusalemu kwa ajili ya ile Sikukuu ya Pentekoste 33 W.K. Wao walikuwa wa kutoka Umedi kule mbali kaskazini-mashariki, kutoka Roma na Afrika Kusini kule mbali magharibi, na kutoka mahali pengi pa humo katikati.—Matendo 2:9-11.
Nyingi za njia zilizotandazwa na wajenga-barabara Waroma zingali zinatumiwa leo. Kusini mwa Roma, unaweza kuendesha kando-kando ya ile Njia ya Appia ya kale, ambayo mtume Paulo mwenyewe alipandia kuingia Roma. (Matendo 28:15, 16) Imesemwa kwamba barabara za Kiroma “ziliandaa nafasi za usafiri wa barani ambao haukupitwa na mwingine mpaka ilipokuja reli.”—The Westminster Historical Atlas to the Bible.
Katika kusimamia milki yao iliyoenea mpaka mbali, mara nyingi Waroma walidumisha desturi za mahali penyewe. Hivyo, wenye mamlaka katika maeneo tofauti-tofauti walijulikana kwa majina mengi au mitajo ya vyeo iliyo tofauti. Katika Modern Discovery and the Bible, A. Rendle Short anasema kwamba hata “wanahistoria Waroma waliotambuliwa” walikuwa hawajaribu ‘kuwataja watu hao wenye madaraja kwa mitajo yao sahihi.’ Na bado, yeye anasema kwamba Luka mwandikaji wa Biblia “anamudu sikuzote kuwa na usahihi mkamilifu” katika jambo hili. Mathalani, Luka anamwita Herode kuwa ni “tetraki,” Herode Agrippa kuwa ni “mfalme,” wanaafisi Wathesalonike kuwa ni “wapolitarki,” na Sergio Paulusi, gavana wa Saiprasi, kuwa ni “prokonsoli.” (Luka 3:1; Matendo 25:13; Matendo 17:6; Matendo 13:7, ona New World Translation Reference Bible, maelezo ya chini.) Nyakati fulani ni sarafu moja tu yenye kupatikana hapa au andishi la kuchongelewa pale lililothibitisha kwamba mwandikaji huyu wa Biblia alitumia mtajo unaofaa katika wakati unaofaa. Uangalifu na usahihi kama huo ni ithibati ya ziada juu ya ukweli ambao kwao Biblia inaandika mambo ya uhakika wa kihistoria juu ya maisha na nyakati za Yesu Kristo.a
Milki na Ukristo
Kundi la Kikristo lenye kusitawi lilikuwa katika Roma. Inaelekea kwamba lilifanyizwa na wale waliorudi Roma baada ya kukubali Ukristo katika Yerusalemu siku ya Pentekoste 33 W.K. (Matendo 2:10) Kitabu cha Biblia cha Waroma kiliandikwa kwa kundi hili wapata mwaka 56 W.K. Baadaye, Paulo alikuja Roma akiwa mfungwa-gereza, na kwa miaka miwili akatoa ushuhuda wa kikamilifu kwa watu waliozuru nyumba yake ya uzuizi. Hivyo, washiriki wa Walinzi wa Praetoria ya mmaliki walipata habari juu ya ujumbe wa Ufalme, na hata washiriki wa “watu wa nyumba ya Kaisari” wakawa Wakristo.—Wafilipi 1:12, 13; 4:22, NW.
Mara nyingi desturi, sheria, na virekebi-rekebi vya Milki ya Kiroma vinatajwa katika Biblia. Amri ya Augusto ilifanya Yusufu na Mariamu waende Bethlehemu, ambako Yesu alizaliwa. Yesu alitilia nguvu ufaaji wa kulipa kodi ambayo Kaisari alidai. Makuhani Wayahudi walijifanya kuwa washikamanifu kwa Kaisari ili wafanye Yesu auawe. Na chini ya sheria ya Kiroma, mtume Mkristo Paulo aliomba kwa Kaisari rufani ya kesi yake.—Luka 2:1-6; 20:22-25; Yohana 19:12, 15; Matendo 25:11, 12.
Vao la kisilaha la askari Mroma—kofia yake ya kichwani, dirii ya kifuani, ngao, miguu iliyovikwa, na upanga—lilitumiwa kuwa kielezi cha thamani ya ukweli, tumaini la wokovu, uadilifu, imani, kuzihubiri habari njema, na Neno la Mungu kuwa ndizo kinga zinazotusaidia kusimama kwa uthabiti dhidi ya mashambulizi ya Shetani. (Waefeso 6:10-18; 1 Wathesalonike 5:8, NW) Ni kielelezo cha askari Mroma mwenye nidhamu nzuri ambaye Paulo alirejezea wakati alipoambia Timotheo awe “askari mzuri sana wa Kristo Yesu.” (2 Timotheo 2:3, 4, NW) Hata hivyo, vita ya Mkristo ilikuwa ya kiroho, si ya kimnofu. Hivyo, Wakristo wa mapema walikataa kutumikia katika jeshi la Kiroma. Justin Martyr (110 mpaka 165 W.K.) alisema kwamba Ukristo “ulibadili silaha zetu za kivita,—panga zetu zikawa vipanga vya kuplau, na mikuki yetu ikawa vifaa vya kulimia.” Wakristo wengi walipoteza uhai wao kwa kukataa utumishi wa kijeshi.
Wale Makaisari
Roma ilifikia kileleta cha utukufu wayo ikiwa chini ya Makaisari. Ingekuwa vema kupitia mambo makubwa-makubwa ya uhakika kuhusu wachache wao, kwa kuwa walihusika katika historia ya Biblia.
Katika mwaka 44 K.W.K., Yulio Kaisari aliuawa. Mwishowe Oktaviani akawa ndiye mtawala wa peke yake. Katika 30 K.W.K., Oktaviani alitiisha Misri, akileta mwisho wa ufalme wa Kigiriki wa Kiptolemai huko. Hiyo ilileta mwisho-hatima wa ile Serikali Kubwa ya Ulimwengu ya Ugiriki iliyokuwa imekuwako tangu wakati wa Aleksanda Mkuu, miaka 300 mapema.b
Katika mwaka 27 K.W.K., Oktaviani akawa mmaliki. Yeye alijitwalia mtajo wa cheo “Augusto,” wenye kumaanisha “mkwezwa, mtakatifu.” Aliita upya mwezi mmoja kwa ajili yake mwenyewe na akaazima siku moja kutoka Februari ili Agosti uwe na siku nyingi kama mwezi ule ulioitwa kulingana na jina la Yulo Kaisari. Augusto alikuwa mmaliki wakati Yesu alipozaliwa, na alitawala mpaka mwaka 14 W.K.—Luka 2:1.
Tiberio, mrithi wa cheo cha Augusto, alitawala kutoka 14 mpaka 37 W.K. Katika mwaka wa 15 wa utawala wa Tiberio, Yohana Mbatizaji alianza kuhubiri. Pia ni katika utawala wake kwamba Yesu alibatizwa, akafanya huduma yake ya kidunia ya miaka mitatu na nusu, na kutoa uhai wake uwe dhabihu. Bado huyo alikuwa akitawala wakati wafuasi wa Yesu walipoanza kueneza Ukristo katika sehemu zote za ulimwengu uliojulikana wakati huo.—Luka 3:1-3, 23.
Gayo, ambaye alibandikwa jina Caligula, alitawala kutoka 37 mpaka 41 W.K. Klaudio (41 mpaka 54 W.K.) alimrithi cheo na akafukuza Wayahudi watoke Roma, kama inavyotaarifiwa katika Matendo 18:1, 2. Baadaye yeye alitiliwa sumu na mke wake, na Nero mwana mchanga wa mwanamke huyo akaja kwenye kiti cha ufalme. Moto mkubwa ulipita Roma ukiikumba katika Julai 64 W.K., ukiharibu yapata robo moja ya jiji hilo. Tasito mwanahistoria anasema kwamba, ili ajiondolee tuhuma ya jambo hilo, Nero alilaumu moto huo juu ya Wakristo, ambao wakati huo walikuwa ‘wakiraruliwa na mbwa na kutoweka’ na ‘kuachiwa kwenye miali ya moto na kuchomwa, ili watumikie wakiwa kama mmuliko wa kila usiku, wakati mchana ulipokuwa umepita. Nero alitoa bustani zake zitumiwe kwa tamasha hiyo.’ Wakati wa mnyanyaso huu, Paulo, aliyekuwa amehubiri kutoka Yerusalemu mpaka Roma na labda hata kufika Hispania, alifungwa gerezani kwa mara ya pili. Inaelekea kwamba yeye aliuawa na Nero wapata 66 W.K.
Wamaliki wengine Waroma wanaotufanya tupendezwe kujua habari zao ni kutia ndani Vespasiani (69 mpaka 79 W.K.) ambaye chini ya utawala wake Tito aliharibu Yerusalemu, Tito mwenyewe (79 mpaka 81 W.K.), na Domitiani ndugu ya Tito (81 mpaka 96 W.K.), ambaye alianzisha upya mnyanyaso rasmi wa Wakristo. Kulingana na mapokeo, ni wakati wa mnyanyaso huu kwamba Yohana mtume aliyezeeka alihamishwa kupelekwa kwenye kisiwa cha Patmo cha kupokelea adhabu. Kule alipewa njozi ya kusisimua juu ya umalizio wa mifumo hii mibovu ya mambo ya kibinadamu na kuchukuliwa kwa mahali payo na Ufalme wa kimbingu wenye uadilifu wa Mungu, ambayo Yohana aliandika katika kitabu cha Biblia cha Ufunuo. (Ufunuo 1:9) Inaonekana Yohana aliachiliwa wakati wa utawala wa mmaliki aliyefuata, Nerva, 96 mpaka 98 W.K., na Injili yake na barua tatu zilikamilishwa baada ya Trajani (98 mpaka 100 W.K.) kuanza kutawala.
Kuzorota kwa Milki ya Kiroma
Katika karne ya nne, Mmaliki Konstantino aliamua kuwaunganisha watu chini ya dini moja ‘ya Kikatoliki,’ au ya ulimwengu wote mzima. Desturi na sherehe za kipagani zilipewa majina ‘ya Kikristo,’ lakini ufisadi ule ule za zamani uliendelea. Katika mwaka 325 K.W.K., Konstantino alisimamia baraza la kanisa kule Nikaya na kuamua kwa kupendelea fundisho la Utatu. Akiwa mbali na kuwa Mkristo wa kweli, baada ya muda mfupi Konstantino alipata sababu ya kuua Krispo, mwanaye wa umri mkubwa zaidi, na Fausta, mke wake mwenyewe.
Konstantino alihamisha serikali yake kuipeleka Byzantium, na jiji hilo akaliita Roma Mpya na baadaye Konstantinopo (Jiji la Konstantino). Jiji hili lilio katika Bosporus, ambako Ulaya na Esia zinakutana, lilibaki likiwa ndilo mji mkuu wa Milki ya Kiroma upande wa mashariki kwa karne 11, mpaka lilipoanguka mikononi mwa Waturuki wa Ottoman katika 1453.
Kule nyuma Roma, ubapa wa magharibi wa Milki ya Kiroma ulianguka katika 476 W.K., wakati mmaliki alipoondolewa cheoni na Mfalme Odoacer, jemadari mmoja wa uzaliwa wa Kijeremani, na kiti cha ufalme kikaachwa bila mtu. Baadaye Charlemagne alijaribu kurudisha milki ya magharibi, na katika mwaka 800 W.K. alivikwa taji la ufalme na Papa Leo wa 3. Halafu, katika 926 W.K. Papa John wa 12 akamvika taji Otto wa 1 awe mmaliki wa Milki Takatifu ya Kiroma ya taifa la Kijeremani—cheo ambacho kilikataliwa rasmi hivi majuzi tu katika mwaka 1806.
Hata hivyo, kufikia wakati huo serikali kubwa ya saba na ya hatima ya ulimwengu katika historia ya Biblia ilikuwa inaibuka. Kama ilivyosemwa katika unabii, hiyo pia ingepitilia mbali, na mahali payo pachukuliwe na serikali yenye kudumu, Ufalme wa kimbingu wa Mungu.—Ufunuo 17:10; Danieli 2:44.
[Maelezo ya Chini]
a Ona “All Scripture Is Inspired of God and Beneficial,” kurasa 340-1.
b Hivyo, wakati wa utawala wa Roma malaika angeweza kusema hivi juu ya hizi serikali kubwa za ulimwengu: “Na kuna wafalme saba: watano wameanguka [Misri, Ashuri, Babuloni, Umedi-Uajemi, na Ugiriki], mmoja yuko [Roma], yule mwingine [Uingereza-Amerika] hajawasili bado.”—Ufunuo 17:10, NW.
[Ramani katika ukurasa wa 26]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mweneo wa Milki ya Roma
Bahari Kuu ya Atlantiki
BRITANNIA
GAUL
HISPANIA
ITALIA
Roma
UGIRIKI
Bahari ya Mediterania
Bahari Nyeusi
Bahari Kaspiani
MISRI
Yerusalemu
Tigri
Eufrati
[Picha katika ukurasa wa 28]
Njia ya Appia ambayo Paulo alisafiria akielekea Roma