“Nyumba ya Daudi”—Jambo la Hakika au Hadithi Yenye Kubuniwa?
DAUDI—yule mvulana mchungaji mchanga, aliyekuja kuwa mwanamuziki, mshairi, askari-jeshi, nabii, na mfalme—hutokeza katika Biblia katika fahari kubwa. Jina lake linatajwa mara 1,138; usemi “Nyumba ya Daudi”—mara nyingi ukirejezea nasaba ya Daudi—watumiwa mara 25. (1 Samweli 20:16) Je, Mfalme Daudi na nasaba yake walikuwa hadithi yenye kubuniwa tu? Akiolojia hufunua nini? Uvumbuzi wenye kutazamisha wa juzijuzi mahali pa akiolojia huko Tel Dan kaskazini mwa Galilaya wasemwa kuwa hutegemeza usahihi wa kihistoria wa Daudi na nasaba yake.
Katika kiangazi cha 1993, kikundi cha waakiolojia, kikiongozwa na Profesa Avraham Biran, kilifyeka eneo nje ya lango la nje zaidi la Dan la kale. Kiligundua eneo wazi lililosakifiwa. Jiwe jeusi la basalti lenye kutokeza ardhini liliondolewa kwa urahisi. Hilo jiwe lilipogeuzwa kuelekea jua la alasiri, herufi zikaonekana waziwazi. “Mungu wangu, tumepata maandishi!” Profesa Biran akasema kwa sauti.
Profesa Biran na mfanyakazi mwenzake, Profesa Joseph Naveh wa Chuo Kikuu cha Kiebrania katika Yerusalemu, upesi waliandika ripoti ya kisayansi juu ya maandishi hayo. Kwa kutegemea ripoti hiyo, makala katika gazeti Biblical Archaeology Review, la Machi/Aprili 1994, yasomwa hivi: “Si kawaida kwa uvumbuzi wa kiakiolojia kuwa kichwa kikuu cha gazeti New York Times (licha ya kupatikana katika gazeti Time). Lakini hilo ndilo lililotukia kiangazi kilichopita kufuatia uvumbuzi katika Tel Dan, kilima kizuri kaskazini mwa Galilaya, chini ya Mlm. Hermoni kando ya mojapo vyanzo vya Mto Yordani.
“Huko Avraham Biran na kikundi chake cha waakiolojia walipata maandishi yenye kutazamisha ya karne ya tisa K.W.K. ambayo hurejezea ‘Nyumba ya Daudi’ na ‘Mfalme wa Israeli.’ Hiyo ndiyo mara ya kwanza ambayo jina Daudi limepatikana katika maandishi yoyote ya kale nje ya Biblia. Jambo la kwamba maandishi hayo hayarejezei mtu fulani aitwaye ‘Daudi’ tu bali yanarejezea Nyumba ya Daudi, nasaba ya yule mfalme mkubwa wa Israeli, ni jambo lenye kutazamisha hata zaidi.
“‘Mfalme wa Israeli’ ni mtajo upatikanao mara nyingi katika Biblia, hasa katika Kitabu cha Wafalme. Hata hivyo, uvumbuzi huo huenda ukawa ndio rejezo la nje ya Biblia la zamani zaidi kwenye Israeli katika maandishi ya Kisemiti. Ikiwa maandishi hayo yanathibitisha chochote, zaidi ya yote, yanaonyesha kwamba Israeli pamoja na Yuda, kinyume cha madai ya wasomi walio wahakiki wa Biblia, zilikuwa falme za maana wakati huo.”
Kuwekea tarehe kwategemea jinsi herufi zilivyo, uchanganuzi wa vyombo vya udongo vilivyopatikana karibu na hilo pande la jiwe, na yaliyomo katika hayo maandishi. Njia zote tatu huelekeza kwenye kipindi kilekile cha wakati, karne ya tisa K.W.K., miaka zaidi ya mia moja hivi baada ya Mfalme Daudi. Wasomi huamini kwamba hayo maandishi yalikuwa sehemu ya nguzo ya ukumbusho ya ushindi iliyojengwa katika Dan na maadui Waaramaea wa “Mfalme wa Israeli” na pia “[Mfalme wa] Nyumba ya Daudi.” Waaramaea, walioabudu Hadadi, mungu-dhoruba aliyekuwa maarufu, waliishi mashariki ya Israeli.
Wakati wa kiangazi cha 1994, mapande mengine mawili ya nguzo hiyo ya ukumbusho yalipatikana. Profesa Biram aripoti hivi: “Katika mapande hayo mawili kuna jina la mungu wa Aramea, Hadadi, pamoja na rejezo kwenye vita kati ya Waisraeli na Waaramea.”
Pande kuu lililopatikana katika 1993 lilikuwa na mistari 13 yenye kuonekana nusu-nusu iliyoandikwa katika maandishi ya Kiebrania cha zamani. Wakati huo, nukta zilitumiwa zikiwa vigawanya-neno ili kutenganisha maneno katika maandishi. Hata hivyo, “Nyumba ya Daudi” limeandikwa likiwa neno moja kwa herufi “bytdwd” (zilizotoholewa katika herufi za kiroma) badala ya “byt” (nyumba), nukta, na kisha “dwd” (Daudi). Kwa kueleweka, maswali yamezushwa kuhusu ufasiri wa “bytdwd.”
Mtaalamu wa lugha Profesa Anson Rainey aeleza hivi: “Joseph Naveh na Avraham Biran hawakueleza maandishi hayo kwa kina, labda kwa kuwa walidhani kuwa wasomaji wangejua kwamba mara nyingi kigawanya-neno kati ya vitengo viwili katika umbo la aina hiyo huachwa, hasa ikiwa muungano ni jina pekee lililothibitishwa. ‘Nyumba ya Daudi’ bila shaka lilikuwa jina la pekee la kisiasa na kijiografia katikati ya karne ya tisa K.W.K.”
Ushuhuda Mwingine wa Kiakiolojia
Baada ya uvumbuzi huo, mtaalamu wa nguzo ya ukumbusho ya Mesha (pia iitwayo Jiwe la Moabu), Profesa André Lemaire, aliripoti kwamba hilo hurejezea pia “Nyumba ya Daudi.”a Ile nguzo ya ukumbusho ya Mesha, iliyovumbuliwa katika 1868, yafanana sana na ile nguzo ya ukumbusho ya Tel Dan. Zote mbili zina tarehe ya karne ya tisa K.W.K., ni zenye maunzi yaleyale, zatoshana kwa ukubwa, nazo zimeandikwa kwa maandishi ya Kisemiti yanayokaribia kufanana.
Kwa habari ya kuundwa upya kwa mstari wa maandishi ulioharibika kwenye nguzo ya ukumbusho ya Mesha, Profesa Lemaire aliandika hivi: “Karibu miaka miwili kabla ya uvumbuzi huo wa pande la Tel Dan, nilifikia mkataa kuwa nguzo ya ukumbusho ya Mesha ilikuwa na rejezo kwenye ‘Nyumba ya Daudi.’ . . . Sababu ya kutoonekana kamwe kwa rejezo hilo kwenye ‘Nyumba ya Daudi’ kabla ya wakati huo huenda ikawa kwa sababu ya lile jambo la hakika la kwamba nguzo ya ukumbusho ya Mesha haijapata kamwe kuwa na editio princeps [toleo la kwanza]. Toleo hilo ndilo ninalotayarisha, miaka 125 baada ya uvumbuzi wa nguzo ya ukumbusho ya Mesha.”
Habari ya kiakiolojia kama hiyo ni yenye kupendeza kwa sababu malaika, Yesu mwenyewe, wanafunzi wake, na watu kwa ujumla walishuhudia usahihi wa kihistoria wa Daudi. (Mathayo 1:1; 12:3; 21:9; Luka 1:32; Matendo 2:29) Mavumbuzi ya kiakiolojia kwa hakika yakubali kwamba yeye na nasaba yake, ile “Nyumba ya Daudi,” ni mambo ya hakika, wala si hadithi yenye kubuniwa.
[Maelezo ya Chini]
a Nguzo ya ukumbusho ya Mesha yajulikana kwa wasomaji wa fasihi za Watch Tower Society. (Ona Mnara wa Mlinzi, Aprili 15, 1990, kurasa 30-31.) Imewekwa katika Louvre Museum, Paris ili ionwe na watu.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Pande la Tel Dan,* lililovumbuliwa katika 1993 kwenye jiji la Dan, kaskazini mwa Galilaya
*Mchoro wategemea picha ipatikanayo katika Israel Exploration Journal.