“Bibi Mwenye Nywele Nyeusi wa Jangwa la Siria”
RANGI ya uso wake ilikuwa nyeusi, meno yake meupe kama lulu, macho yake meusi na maangavu. Alielimishwa vema naye alikuwa bingwa wa lugha kadha wa kadha. Malkia huyu mpambanaji alisemwa kuwa bora katika taaluma kuliko malkia Kleopatra na labda alikuwa mrembo kama yeye. Kwa kuwa alijasiria kukabili serikali ya ulimwengu yenye nguvu ya siku yake, yeye alitimiza fungu la kiunabii katika tamthiliya ya Kimaandiko. Muda mrefu baada ya kifo chake, waandishi walimsifu, nao wachoraji walimchora akiwa mrembo zaidi ya alivyokuwa. Mshairi wa karne ya 19 alimfafanua kuwa “bibi mwenye nywele nyeusi wa jangwa la Siria.” Mwanamke huyu mwenye kusifiwa sana alikuwa Zenobia—malkia wa jiji la Palmyra la Siria.
Zenobia alipataje umashuhuri? Ni hali gani ya kisiasa iliyomwongoza kupata mamlaka? Ni nini kiwezacho kusemwa kuhusu sifa yake? Naye malkia huyu alitimiza fungu gani la kiunabii? Kwanza chunguza hali ya kijiografia ambamo tamthiliya hiyo yajitokeza.
Jiji Ukingoni mwa Jangwa
Jiji la Zenobia, Palmyra, lilikuwa karibu kilometa 210 upande wa kaskazini-mashariki mwa Damasko, kwenye ukingo wa kaskazini mwa Jangwa la Siria ambapo milima ya Anti-Lebanon ipo ukingoni pa uwanda. Jiji hili la oasisi lilikuwa katikati ya Bahari ya Mediterania upande wa magharibi na Mto Frati upande wa mashariki. Huenda ikawa Mfalme Solomoni alilijua kuwa Tadmori, mahali ambapo palikuwa muhimu kwa usitawi wa ufalme wake, kwa sababu mbili: ngome kwa ajili ya kukinga mpaka wa kaskazini na, kiunganishi muhimu sana kati ya miji ya misafara iliyofuatana. Kwa hiyo, Solomoni “akaujenga [upya] Tadmori wa nyikani.”—2 Mambo ya Nyakati 8:4.
Historia ya miaka elfu baada ya utawala wa Mfalme Solomoni haitaji jambo lolote kuhusu Tadmori. Ikiwa kwa usahihi jiji hilo latambuliwa kuwa Palmyra, kuinuka kwake kufikia umashuhuri kulianza baada ya Siria kuwa mkoa wa mpakani wa Milki ya Roma katika 64 K.W.K. “Palmyra lilikuwa jiji la maana kwa Roma katika sehemu mbili, kiuchumi na kijeshi,” asema Richard Stoneman katika kitabu chake Palmyra and Its Empire—Zenobia’s Revolt Against Rome. Kwa kuwa jiji hili la michikichi lilikuwa kwenye njia kuu ya biashara iliyounganisha Roma na Mesopotamia na vilevile Mashariki, utajiri wa kibiashara wa ulimwengu wa kale ulipitia humo—viungo kutoka East Indies, hariri kutoka China, na bidhaa nyinginezo kutoka Uajemi, Mesopotamia ya Chini, na nchi za Mediterania. Roma ilitegemea kuingizwa kwa bidhaa hizi.
Kijeshi, mkoa wa Siria ulitumika ukiwa eneo la amani kati ya serikali zenye kushindana za Roma na Uajemi. Mto Frati uligawanya Roma na ujirani wake wa mashariki wakati wa miaka 250 ya kwanza ya Wakati Wetu wa Kawaida. Palmyra lilikuwa tu ng’ambo ile nyingine ya jangwa, magharibi mwa jiji la Dura-Europos kwenye Frati. Wakitambua cheo cha maana cha jiji hilo, maliki hao Waroma kama vile Hadrian na Valerian walizuru Palmyra. Hadrian aliongezea fahari ya usanifuujenzi wa jiji hilo, naye akatoa michango mingi ya ukarimu. Valerian alimthawabisha mheshimiwa wa Palmyra aliyeitwa Odaenathus—mume wa Zenobia—kwa kumkweza, katika 258 W.K., hadi kufikia cheo cha balozi mdogo wa Roma kwa sababu alikuwa amefanikiwa kupiga kampeni dhidi ya Uajemi na kupanua mpaka wa Milki ya Roma hadi Mesopotamia. Zenobia alitimiza fungu la maana katika kupata mamlaka kwa mume wake. Mwanahistoria Edward Gibbon aliandika: “Mafanikio ya Odaenathus kwa kiwango kikubwa yalikuwa kwa sababu ya busara na ushupavu wake [Zenobia].”
Wakati huohuo, Mfalme Sapor wa Uajemi aliamua kutoa mwito wa ushindani kwa mamlaka ya juu ya Roma na kuonyesha mamlaka yake juu ya mikoa yote ya zamani ya Uajemi. Akiwa na jeshi lenye kuogofya, alisafiri kwenda upande wa magharibi, akateka miji iliyokuwa ngome ya Nisibis na Karrhae (Harani), kisha akaharibu eneo la kaskazini mwa Siria na Kilikia. Maliki Valerian alikuja binafsi kuongoza majeshi yake dhidi ya washambulizi lakini alishindwa na kutekwa na Waajemi.
Odaenathus aliona kuwa inafaa kutuma zawadi ghali na ujumbe wa amani kwa maliki wa Uajemi. Mfalme Sapor aliamuru kwa kiburi kwamba zawadi hizo zitupwe katika Frati na kwamba Odaenathus afike mbele zake akiomba kuachiliwa kwa mateka. Katika kujibu, Wapalmyra walikusanya jeshi la wahamaji wa jangwani na mabaki ya majeshi ya Roma nao wakaanza kuwashambulia Waajemi waliokuwa sasa wakikimbia. Majeshi ya Sapor—yakiwa yamechoka kupambana kijeshi na pia kulemewa na nyara—hayangeweza kujihami dhidi ya mbinu za kushambulia na kukimbia za wapiganaji wa jangwani, nayo yalilazimika kukimbia.
Akitambua ushindi wake juu ya Sapor, mwana wa Valerian na mwandamizi wake, Gallienus, walimpa Odaenathus cheo cha corrector totius Orientis (gavana wa Mashariki yote). Baada ya muda, Odaenathus alijipatia mwenyewe cheo cha “mfalme wa wafalme.”
Zenobia Ajaribu Kuunda Milki
Katika 267 W.K., akiwa katika upeo wa kazi-maisha yake, Odaenathus na mrithi wake waliuawa, labda na mpwa wa kiume mwenye kulipiza kisasi. Zenobia alichukua cheo cha mume wake, kwa kuwa mwana wake alikuwa mchanga mno. Akiwa mrembo, mwenye kutaka makuu, mwenye uwezo wa kuwa msimamizi, aliyezoea kupiga kampeni pamoja na hayati mume wake, na mwenye ufasaha wa lugha kadhaa, aliweza kujipatia staha na utegemezo kutoka kwa raia zake—utimizo wenye kutokeza miongoni mwa Wabedui. Zenobia alipenda sana kujifunza naye alikuwa na wasomi wengi. Mmojawapo wa washauri wake alikuwa mwanafalsafa na mwenye elimu ya usemi Sashio Longinusi—aliyesemwa kuwa “maktaba iliyo hai na nyumba ya hazina ya ujuzi.” Mwandishi Stoneman ataja hivi: “Wakati wa miaka mitano baada ya kifo cha Odaenathus . . . Zenobia alikuwa amejithibitisha katika akili za watu wake kuwa bibi wa Mashariki.”
Kwenye upande mmoja wa utawala wa Zenobia kulikuwako Uajemi, ambao yeye na mume wake walikuwa wameudhoofisha, na kwenye upande ule mwingine kulikuwako Roma iliyokuwa ikiporomoka. Kuhusu hali zilizokuwa katika Milki ya Roma wakati huo, mwanahistoria J. M. Roberts asema: “Karne ya tatu ilikuwa . . . wakati mbaya sana kwa Roma katika mipaka ya Mashariki na vilevile Magharibi, ilhali nyumbani kipindi kipya cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na mashindano ya kurithi mamlaka yalikuwa yameanza. Maliki 22 (bila kuhesabu wenye kujisingizia) walikuja nao wakaenda.” Kwa upande ule mwingine, bibi wa Siria, alikuwa amethibitika kabisa kuwa mtawala mkuu katika milki yake. “Akiwa anadhibiti usawaziko wa miliki mbili [ya Uajemi na ya Roma],” Stoneman atoa maoni, “yeye angejaribu kuunda milki ya tatu ambayo ingezitawala hizo mbili.”
Fursa ya Zenobia ya kupanua mamlaka yake ya kifalme ilikuja katika 269 W.K., wakati msingiziaji mmoja aliyekuwa akishindania utawala wa Roma alipotokea katika Misri. Jeshi la Zenobia liliingia Misri mara moja, likamaliza mwasi huyo, nalo likatwaa nchi hiyo. Akijitangaza mwenyewe kuwa malkia wa Misri, alipiga chapa sarafu kwa jina lake. Sasa ufalme wake ulienea kutoka mto Naili hadi mto Frati. Kufikia hatua hii maishani mwake, alikuja kuwa “mfalme wa kusini” anayesemwa katika unabii wa Biblia wa Danieli, kwa kuwa ufalme wake huo ulitawala eneo la kusini la nchi ya nyumbani ya Danieli. (Danieli 11:25, 26) Pia alishinda sehemu kubwa zaidi ya Asia Ndogo.
Zenobia aliimarisha na kupamba jiji lake kuu, Palmyra, hivi kwamba lililingana na majiji makubwa ya ulimwengu wa Roma. Lilikuwa na idadi ya watu waliokadiriwa kuwa zaidi ya 150,000. Majengo maridadi ya umma, mahekalu, bustani, nguzo, na nguzo za ukumbusho zilijaa jijini, zikizungukwa na kuta ambazo zilisemwa kuwa na mzingo upatao kilometa 21. Safu za nguzo zilizofanyizwa kwa nguzo za ujenzi wa Kigiriki zenye urefu wa meta 15—1,500—zikiwa kwenye barabara kuu. Sanamuumbo na sanamu za kichwa na mabega za watu mashuhuri na wafadhili wenye mali zilijaa jijini humo. Katika 271 W.K., Zenobia alisimamisha nguzo mbili za sanamuumbo yake mwenyewe na ya hayati mume wake. Ukingoni mwa jangwa, Palmyra lilimetameta kama kito.
Hekalu la Jua lilikuwa mojawapo ya majengo yaliyo bora zaidi katika Palmyra na hapana shaka yalitawala mandhari ya kidini katika jiji hilo. Yaelekea kwamba, Zenobia pia aliabudu mungu aliyehusiana na mungu-jua. Hata hivyo, Siria ya karne ya tatu, ilikuwa nchi ya dini nyingi. Katika utawala wa Zenobia kulikuwako Wakristo wa kujidai tu, Wayahudi, wanajimu, na waabudu wa jua na mwezi. Alikuwa na mtazamo gani kuelekea njia tofauti-tofauti za ibada katika milki yake? Mwandishi Stoneman atoa maoni haya: ‘Mtawala mwenye hekima hatapuuza desturi zozote zinazoonekana kuwa zenye kufaa kwa watu wake. Ilitumainiwa kwamba, miungu hiyo, ililetwa pamoja na kupangwa upande wa Palmyra.’ Ni dhahiri, Zenobia alikuwa mwenye kuvumilia dini. Lakini je, kwa kweli miungu ilikuwa “imeletwa na kupangwa upande wa Palmyra”? Ni nini kilichoelekea kutokea karibuni kwa Palmyra na “mtawala [wake] mwenye hekima”?
Maliki ‘Achochea Moyo Wake’ Dhidi ya Zenobia
Katika 270 W.K., Aurelian akawa maliki wa Roma. Majeshi yake yalishinda kwa mafanikio na kutia nidhamu wakatili wa kaskazini. Katika 271 W.K.—sasa akiwakilisha “mfalme wa kaskazini” wa unabii wa Danieli—Aurelian ‘alichochea mamlaka yake na moyo wake dhidi ya mfalme wa kusini,’ aliyewakilishwa na Zenobia. (Danieli 11:25a) Aurelian alituma baadhi ya majeshi yake moja kwa moja hadi Misri na kuongoza jeshi lake kuu kuelekea mashariki kupitia Asia Ndogo.
Mfalme wa kusini—chombo cha utawala kilichoongozwa na Zenobia—‘alijichochea’ afanye vita dhidi ya Aurelian “kwa jeshi kubwa mno na lenye nguvu nyingi” chini ya majenerali wawili, Zabdas na Zabbai. (Danieli 11:25b) Lakini Aurelian alitwaa Misri kisha akaanzisha safari ya uvumbuzi katika Asia Ndogo na Siria. Zenobia alishindiwa huko Emesa (sasa ni Homs), naye akakimbia kurudi Palmyra.
Aurelian alipolizingira Palmyra, Zenobia akitumaini kupata msaada, alitoroka na mwana wake kuelekea Uajemi, lakini alishikwa na Waroma kwenye Mto Frati. Wapalmyra walisalimisha jiji lao katika 272 W.K. Aurelian aliwatendea wakazi wa hapo kwa ukarimu, akapora vitu vingi sana, kutia ndani sanamu iliyokuwa katika Hekalu la Jua, na kuondoka kwenda Roma. Maliki Mroma hakumuua Zenobia, bali alimfanya awe kivutio kikuu katika mwandamano wake wa shangwe ya ushindi katika Roma mwaka wa 274 W.K. Huko alibaki akiwa mwanamke mkomavu mwenye daraja la kuheshimiwa wa Roma katika maisha yake yote.
Jiji la Jangwani Laharibiwa
Miezi kadhaa baada ya Aurelian kutwaa Palmyra, Wapalmyra waliwaua askari walinzi wa Roma ambao alikuwa amewaacha. Habari ya uasi huu ilipofikia Aurelian, mara moja Aurelian aliamuru askari wake warudi huko tena, na wakati huu walilipiza kisasi kwa kiwango kikubwa dhidi ya wakazi wote wa huko. Wale walionusurika kutokana na machinjo hayo yasiyo na huruma walipelekwa utumwani. Jiji hilo lenye fahari liliporwa na kuharibiwa kiasi cha kwamba halingeweza kurekebishwa. Hivyo, jiji hilo kubwa lenye shughuli nyingi lilirudia tena hali yake ya zamani—“Tadmori wa nyikani.”
Wakati Zenobia alipojasiria kukabili Roma, pasipo kujua yeye na Maliki Aurelian walitimiza mafungu yao wakiwa “mfalme wa kusini” na “mfalme wa kaskazini,” wakitimiza sehemu ya unabii uliorekodiwa kwa kina zaidi na nabii wa Yehova miaka 800 hivi mapema. (Danieli, sura ya 11) Akiwa mwenye utu wake wenye kutokeza, Zenobia alipendwa na watu wengi. Hata hivyo, la maana zaidi, lilikuwa fungu lake katika kuwakilisha chombo cha kisiasa kilichotabiriwa katika unabii wa Danieli. Utawala wake haukudumu kwa zaidi ya miaka mitano. Palmyra, jiji kuu la ufalme wa Zenobia, leo ni kijiji tu. Hata Milki yenye uwezo ya Roma tangu wakati huo imefifia na kuziachia nafasi falme za kisasa. Wakati ujao wa mamlaka hizi utakuwaje? Hali yao ya baadaye pia inaamuliwa na utimizo wa unabii wa Biblia.—Danieli 2:44.
[Sanduku katika ukurasa wa 29]
Urithi wa Zenobia
Aliporudi Roma baada ya kumshinda Zenobia, malkia wa Palmyra, Maliki Aurelian alijenga hekalu kwa ajili ya jua. Ndani yake aliweka sanamuumbo za mungu-jua alizoleta kutoka jiji la Zenobia. Likieleza juu ya mavumbuzi zaidi, gazeti History Today lasema: “Mojawapo ya matendo ya Aurelian yenye kudumu zaidi labda ni kuanzishwa, katika AD 274, kwa sherehe ya kila mwaka ya kutokea kwa jua wakati wa majira ya baridi kali ya kikomo cha jua, Desemba 25. Milki hiyo ilipopata kuwa ya Kikristo kuzaliwa kwa Kristo kulihamishwa hadi tarehe hiyo ili kufanya dini mpya ikubalike kwa wale waliofurahia sherehe za zamani. Ni kioja kwamba, hatimaye ni kwa sababu ya Malkia Zenobia kwamba . . . [watu] wanasherehekea Krismasi yetu.”
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 28, 29]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BAHARI YA MEDITERANIA
SIRIA
Antiokia
Emesa (Homs)
PALMYRA
Damasko
MESOPOTAMIA
Frati
Karrhae (Harani)
Nisibis
Dura-Europos
[Hisani]
Ramani: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
Safu ya Nguzo: Michael Nicholson/Corbis
[Picha katika ukurasa wa 29]
Sarafu ya Roma yawezekana inayoonyesha Aurelian
[Picha katika ukurasa wa 30]
Hekalu la jua huko Palmyra
[Hisani]
The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck
[Picha katika ukurasa wa 31]
Malkia Zenobia akihutubia askari-jeshi wake
[Hisani]
Giovanni Battista Tieupolo, Queen Zenobia Addressing Her Soldiers, Samuel H. Kress Collection, Photograph © Board of Trustees, National Gallery of Art, Washington
[Picha katika ukurasa wa 28 zimeandaliwa na 28]
Habari kuhusu: Giovanni Battista Tiepolo, Queen Zenobia Addressing Her Soldiers, Samuel H. Kress Collection, Photograph © Board of Trustees, National Gallery of Art, Washington