Kuutazama Ulimwengu
Jeuri Yazama Katika Adili Mbaya Zaidi
Kwa wale wanaohisi kwamba michezo kama vile michuano ya ndondi au mashindano ya mbinu za kujikinga si yenye jeuri vya kutosha, wadhamini katika Marekani wametokeza kibadala kipya kiitwacho “upiganaji wa kupita kiasi,” au “upiganaji wa kiwango cha juu zaidi.” Kulingana na ripoti moja katika The New York Times, dhana ya upiganaji wa kupita kiasi ni sahili: “Wanaume wawili wanatwangana hadi mmoja wao asalimu amri au kupigwa hadi azirai.” Hawavai glovu zozote za kupunguza uzito wa masumbwi yao; hakuna raundi au mapumziko; kuna sheria chache mbali na makatazo dhidi ya kuuma au kung’oa macho. Washindani hutumia mbinu za ndondi, judo, karate, mieleka, au mapigano ya mitaani—mara nyingi kukiwa na matokeo yenye umwagikaji mwingi wa damu. Hayo mashindano hufanywa mbele ya umati wa mashabiki wenye kushangilia kwa kelele nyingi, ambao hulipa tikiti za kufikia dola 200; mapigano hayo yanapendwa na wengi pia kwenye televisheni na katika kaseti za vidio zilizokodiwa. Ingawa hivyo, majimbo mengi tayari yamepiga marufuku michezo hii.
Kazi ya Ziada kwa Wanawake
Je, wanaume na wanawake hushiriki kazi kwa usawa nyumbani? Si kulingana na uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Serikali ya Takwimu ya Ujerumani. Wataalamu wa uchumi Norbert Schwarz na Dieter Schäfer waliomba makao 7,200 yachanganue na kurekodi kiwango cha wakati kilichotumiwa kufanya kazi nyumbani. Uchunguzi huo ulitia ndani kazi kama vile kuosha vyombo, kufanya ununuzi, kutunza watu wa ukoo walio wagonjwa, na urekebishaji wa gari. “Licha ya kama wana kazi ya kimwili au la, wanawake walitumia wakati mwingi wakifanya kazi isiyolipwa mara mbili kuliko wanaume,” laripoti gazeti Süddeutsche Zeitung.
Dini Katika “Ulimwengu wa Kompyuta”
Wale wanaotumia kompyuta kuvinjari “ulimwengu wa kompyuta,” mifumo ya mikusanyo ya data iliyounganishwa, wana machaguo ya kidini mengi zaidi siku hizi. Mfumo uitwao World Wide Web sasa una The Mary Page, ambapo mdadisi aweza kupata majibu kwa maswali kumi yaulizwayo sana kuhusu Bikira Mariamu, kama vile kwa nini sikuzote yeye huonyeshwa akiwa amevalia buluu hafifu. Waamishi, ambao huepuka tekinolojia kama vile nguvu za umeme, wanawakilishwa na sehemu iitwayo Ask the Amish. Wanapelekewa ukurasa wa maswali kwenye kiwambo, wanajibu kirefu, na majibu yanapitishwa na kompyuta—kupitia mtu mwingine. Gazeti The Christian Century hutaja kwamba sasa kuna “mkusanyo wa data kuhusu habari moja” kwenye Internet uitwao Confession Booth, ambapo kifanano cha padre huuliza, “Na ni nini ambacho wataka kuungama?” Mstari ufuatao kiwamboni ni jibu lenye machaguo kadhaa. “Nilitenda dhambi ifuatayo: (Uuaji-kimakusudi) (Uzinzi) (Sikuwa Mtendaji Kiroho) (Uchu) (Tamaa ya Kupita Kiasi ya Utajiri) (Udanganyaji) (Ulafi) (Kiburi) (Hasira) (Pupa) (Vipaumbele Visivyofaa).”
Ua Kubwa Mno, Lenye Kunuka Mno
Ua kubwa kuliko yote ulimwenguni ni uumbaji wa ajabu kwelikweli. Likiitwa raflesia, lina ukubwa ukadiriwao kuwa sawa na wa gurudumu la basi nalo huchukua muda mrefu sawa na achukuao mwanadamu kukua tangu kutungwa mimba hadi kuzaliwa. Na ukubwa si sababu pekee ya kufanya ua hili kutofaa kuchaguliwa kwa ajili ya shada la maua. Hilo hunuka. Ili kuvutia nzi wa kulichavusha, raflesia hunuka kama mnofu unaooza. Hapo zamani wanakijiji wa Malasia ambao huishi katika misitu ambamo raflesia hukua wamelibandika jina bakuli la ibilisi na wamekuwa wakilikata mara wanapoliona tu. Hata hivyo, kulingana na South China Morning Post, hifadhi ya serikali ya Malasia ya Kinabalu imechukua hatua kulinda ua hilo lililo nadra kupatikana ili kwamba wanasayansi wapate kulichunguza zaidi. Wanakijiji wenyeji sasa huchuma fedha zaidi kwa kuongoza watalii msituni ili kupiga picha raflesia. Bila shaka, wengi hukaa mbali.
Mji wa Lourdes wa Kiitalia?
Katika jiji la Italia la Civitavecchia, sanamu ya Bikira Mariamu hivi majuzi ilisemekana kwamba ililia machozi ya damu, hili likitokeza wingi wa maelfu ya watazamaji wadadisi na mapilgrimu. Kwa sababu hii meya, Pietro Tidei, ambaye hujiita asiyeamini, alisafiri hadi Ufaransa akiwa na mkuu fulani wa Katoliki. Walizuru mji ujulikanao sana wa Lourdes, ulio mashuhuri sana kwa madhabahu yao ya Kikatoliki ambamo “miujiza” yapaswa kutokea. Ziara hiyo haikuwa upilgrimu. Badala ya hivyo, lengo layo lilikuwa kuchunguza “muujiza wa kiuchumi” wa Lourdes, bila shaka kupata maoni juu ya jinsi ya kupanga na kusimamia Civitavecchia likiwa kama Mecca lenye mapato mengi kutoka kwa watalii na mapilgrimu.
“Vita Takatifu” ya Brazili
Padre mmoja Mpentekoste katika Brazili alianzisha kile ambacho waandishi wa habari wa taifa hilo walikibandika jina vita takatifu. Kwenye kipindi cha televisheni ya kitaifa, padre huyo, Sergio von Helde, alishutumu hadharani ibada ya sanamu ya Kanisa Katoliki. Ili kukazia hoja hii, alionyesha sanamu ya Our Lady of Aparecida, mwigizo mweusi wa Bikira Mariamu, ambao hutumika kuwa mtakatifu mfadhili kwa Wakatoliki 110,000,000 wa Brazili. Von Helde aliiita sanamu hiyo “mwanasesere mwenye kuchukiza, na mwenye kufadhaisha” huku akiichapa makofi na kuipiga mateke kwa kurudia-rudia. Maelfu ya Wakatoliki wameandamana, wakibeba sanamu za mtakatifu mfadhili wakipita barabarani. Umati wenye kupiga kelele, na kutupa mawe umezingira makanisa fulani ya farakano hilo la Pentekoste la Von Helde, liitwalo Universal Church of the Kingdom of God. Von Helde, ambaye tangu wakati huo ameondoshwa kwa muda na mkuu wa kanisa hili kutoka cheo chake rasmi, alaumu vyombo vya habari kwa kuonyesha kwenye televisheni kwa kurudia-rudia filamu ya ushambulizi wake. “TV Globo [mfumo mkubwa zaidi wa televisheni wa taifa hilo] ilifanya niwe dubwana,” padre huyo adai.
Mauaji ya Vikundi vya Kuzima Uhalifu
Katika Afrika Kusini kikundi kilichoshukiwa kuwa watekaji-nyara magari kilichukuliwa kutoka nyumbani mwao na umati uliokasirika, wakakatwa-katwa hadi kifo, na kufunikwa kwa rangi. Gazeti la habari Saturday Star lilisema kwamba ongezeko la matukio hayo ni “dalili ya jamii ambayo imepoteza imani katika polisi wayo na ambayo imesumbuliwa kupita kiasi na imesumbuliwa sana na uhalifu.” Ingawa hawakubali mwenendo huo, wataalamu wa uhalifu huona tendo la kupaka rangi wahasiriwa baada ya kifo chao kuwa jambo lenye umaana. Hili hunuiwa kuwa onyo kwa watu wengine waelekeao kuwa wahalifu. Mtaalamu mmoja wa uhalifu alisema: “Ishara zote zinaonyesha kwamba hali hiyo haiwezi kudhibitiwa hata kidogo na kwamba umma umepoteza udhibiti juu ya uwezo wao wenyewe wa kushughulikia wazo la kwamba hawawezi tena kukabili wahalifu kwa mafanikio.”
Taabu na Kondo Wabalehe
Kondo wa California—ndege mkubwa mno wenye kula mizoga ambaye karibu ametoweka katika karne hii—anatokeza ugumu wa kipekee kwa wahifadhi wanaojaribu kuachilia huru kondo waliozaliwa kifungoni ili waende porini. Ndege hao, walioachiliwa huru wakiwa wabalehe, wako katika “hatua yao ya utineja ya uvinjari na kudadisi kila kitu,” asema mhifadhi mmoja aliyenukuliwa katika gazeti New Scientist. Kutokuwa na hofu ya mwanadamu au waya za umeme kumewagharimu kadhaa ama uhai ama uhuru. Hivyo wahifadhi wamebuni mbinu mpya ya kulea vifaranga vya kondo. Wao hutumia mishtuo midogo ya umeme ili kufunza ndege huyo kuepuka waya za umeme. Ili kufunza kuepuka watu, wanahakikisha kondo hawawaoni isipokuwa tu, katika pindi fulani, ambapo watu kadhaa wanamkimbilia ndege kwa ghafula, kumshika, na kumweka chini akiwa chali. “Kondo huchukia hili,” lataja gazeti New Scientist, na kwa sababu hiyo wanajifunza kuepuka watu. Kufikia wakati huu mbinu hiyo imepata mafanikio kadiri fulani.
Nadhariatete ya Fumbo la Handaki
Waakiolojia wamejiuliza kwa muda mrefu kwa nini handaki la Hezekia, lililochimbuliwa katika karne ya nane K.W.K ili kuhakikisha Yerusalemu lapata maji wakati wa kuzingirwa na jeshi la Ashuru, lilifuata mkondo huo usio na utaratibu, wenye kupinda-pinda. Njia iliyonyooka ifaayo zaidi ingehitaji uchimbaji wa meta 320, badala ya meta 533 ambazo handaki hilo lilichukua. Maandishi, yaliyoandikwa kwa Kiebrania cha kale, yalipatikana kwenye ukuta wa hilo handaki katika 1880. Yalieleza jinsi vikundi viwili vya wafanyakazi vilivyoanza kwenye miisho tofauti ya handaki hilo lililochimbwa katika mwamba na kukutana katikati. Hili lilizusha swali la ziada la jinsi walivyofaulu kufanya hivyo, ukifikiria njia yenye kupinda-pinda ya handaki hilo. Wanajiolojia sasa wahisi kwamba wana jibu. Kulingana na Dan Gill wa Uchunguzi wa Kijiolojia wa Israeli, wafanyakazi walifuata na kupanua vipito vya asili vilivyofanyizwa na maji yaliyopitia mwambani ambamo mianya ilitokea chini ya mikazano ya tetemeko la dunia au mahali ambapo tabaka tofauti za mwamba zilipokutana. Baada ya kipindi cha wakati, vipito hivi vingekuwa vipana zaidi katika mahali fulani, jambo ambalo huenda likaeleza kwa nini kimo cha hilo handaki hutofautiana kuanzia meta 1.7 hadi kufikia meta 5 na pia jinsi wafanyakazi hao wakitumia taa za mafuta, waliweza kupata hewa ya kutosha. Wafanyakazi hao walikuwa wenye ustadi vilevile, kwa kuwa mafanikio ya handaki hilo yalitegemea kuwa na mwinamo wenye kushuka kidogo—sentimeta 31.75 tu kwa mkondo wote.