Sura ya 19
Yehova Aharibu Kiburi cha Tiro
1, 2. (a) Tiro la kale lilikuwa jiji la aina gani? (b) Isaya alitoa unabii gani juu ya Tiro?
ALIKUWA “mkamilifu katika uzuri” naye alijaa “utajiri wa kila aina.” (Ezekieli 27:4, 12, linganisha An American Translation.) Kundi lake kubwa la meli lilisafiri baharini kuelekea sehemu za mbali. Akawa “mtukufu sana, katika moyo wa bahari,” naye ‘akawatajirisha wafalme wa dunia kwa wingi wa mali zake.’ (Ezekieli 27:25, 33) Katika karne ya saba K.W.K., ndivyo Tiro lilivyokuwa—jiji la Foinike kwenye sehemu ya mwisho ya mashariki ya Mediterania.
2 Ingawa hivyo, uharibifu wa Tiro ulikuwa ukikaribia. Miaka ipatayo 100 kabla ya Ezekieli kulifafanua, nabii Isaya alitabiri kuanguka kwa ngome hiyo ya Foinike na maombolezo ya wale wanaoitegemea. Isaya pia alitabiri kwamba baada ya muda fulani Mungu angeligeukia jiji hilo na kulipa ufanisi mpya. Maneno ya nabii yalitimizwaje? Nasi twaweza kujifunza nini kutokana na yale yaliyotendeka kwa Tiro? Kuelewa vema mambo yaliyolikumba jiji hilo na sababu ya kufanyika kwa mambo hayo kutaimarisha imani yetu katika Yehova na katika ahadi zake.
“Toeni Sauti za Uchungu, Enyi Merikebu za Tarshishi”!
3, 4. (a) Tarshishi ilikuwa wapi, na kulikuwako uhusiano gani baina ya Tiro na Tarshishi? (b) Kwa nini mabaharia wanaofanya biashara na Tarshishi ‘watatoa sauti za uchungu’?
3 Chini ya kichwa, “Ufunuo juu ya Tiro,” Isaya atangaza: “Toeni sauti za uchungu, enyi merikebu za Tarshishi, kwa maana umeharibika kabisa, hata hapana nyumba, hapana mahali pa kuingia.” (Isaya 23:1a) Yaaminika kwamba Tarshishi ilikuwa sehemu ya Hispania, mbali sana kutoka Tiro iliyo upande wa Mediterania ya mashariki.a Licha ya hayo, Wafoinike walikuwa mabaharia hodari, na meli zao zilikuwa kubwa na bora. Wanahistoria fulani huamini kwamba Wafoinike walikuwa wa kwanza kutambua uhusiano uliopo baina ya mwezi na kujaa na kupwa kwa maji baharini na pia wa kwanza kutumia astronomia iwaongoze katika safari ya baharini. Basi safari ndefu toka Tiro hadi Tarshishi haikuwa kuzuizi kwao.
4 Katika siku ya Isaya, Tarshishi ya mbali ni soko muhimu kwa Tiro, labda chanzo kikuu cha mali yake wakati fulani wa historia yake. Hispania ina migodi yenye kujaa fedha, chuma, bati, na madini mengineyo. (Linganisha Yeremia 10:9; Ezekieli 27:12.) “Merikebu za Tarshishi,” ambazo labda ni meli za Tiro zinazofanya biashara na Tarshishi, zitakuwa na sababu nzuri ya ‘kutoa sauti za uchungu,’ zikiombolezea kuharibiwa kwa bandari ya kwao.
5. Mabaharia wanaokuja kutoka Tarshishi watapata wapi habari za kuanguka kwa Tiro?
5 Mabaharia walio baharini watapataje habari za kuanguka kwa Tiro? Isaya ajibu: “Toka nchi ya Kitimu wamefunuliwa habari.” (Isaya 23:1b) Labda “nchi ya Kitimu” hurejezea kisiwa cha Saiprasi, kilichoko karibu kilometa 100 magharibi mwa pwani ya Foinike. Hicho ndicho kituo cha mwisho kwa meli zinazoelekea mashariki kutoka Tarshishi kabla hazijafika Tiro. Kwa hiyo, mabaharia watapokea habari za kupinduliwa kwa bandari yao waipendayo watuapo huko Saiprasi. Watashtuka kwelikweli! Kwa huzuni, ‘watatoa sauti za uchungu’ kwa kuvunjika moyo.
6. Eleza uhusiano uliopo baina ya Tiro na Sidoni.
6 Watu wa pwani ya Foinike pia watavunjika moyo. Nabii asema: “Tulieni, enyi mkaao kisiwani [“pwani,” “NW”]; wewe ambaye wafanya biashara wa Sidoni, wavukao bahari, walikujaza. Vitu vilivyopandwa, vya Shihori, mavuno ya Nile, yaliyokuja juu ya maji mengi, ndiyo pato lake, naye alikuwa soko la mataifa.” (Isaya 23:2, 3) ‘Wakazi wa pwani’—jirani za Tiro—watakaa kimya wakishangaa sana juu ya maafa ya kuanguka kwa Tiro. “Wafanya biashara wa Sidoni” ambao ‘wamewajaza’ wakazi hao, wakiwafanya matajiri, ni kina nani? Hapo awali Tiro lilikuwa koloni la jiji la pwani liitwalo Sidoni, ambalo lilikuwa kilometa 35 tu upande wa kaskazini. Kwenye sarafu zake, Sidoni lajiita mama ya Tiro. Ingawa mali za Tiro zimeshinda za Sidoni, hilo lingali “binti wa Sidoni,” na wakazi wake wangali wajiita Wasidoni. (Isaya 23:12) Kwa hiyo, yaelekea usemi “wafanya biashara wa Sidoni” wawarejezea wafanya-biashara wakazi wa Tiro.
7. Wafanya-biashara wa Sidoni wamesambazaje mali?
7 Wafanya-biashara matajiri wa Sidoni wavuka Bahari ya Mediterania katika shughuli zao za biashara. Wasafirisha mbegu, au nafaka, ya Shihori, ambao ni mfereji wa mashariki kabisa wa Mto Nile kwenye eneo la delta la Misri. (Linganisha Yeremia 2:18.) “Mavuno ya Nile” yatia ndani pia mazao mengine ya Misri. Kuuza na kununua na pia kubadilishana bidhaa hizo huleta faida kubwa kwa wafanya-biashara hao wa baharini na vilevile kwa mataifa wanayofanya biashara nayo. Wafanya-biashara wa Sidoni wajaza mapato Tiro. Watahuzunika kwelikweli Tiro litakapoanguka!
8. Kuharibiwa kwa Tiro kutaathirije Sidoni?
8 Kisha Isaya asema na Sidoni maneno haya: “Tahayari, Ee Sidoni; kwa maana bahari imenena, hiyo ngome ya bahari ilisema, Sikuona utungu, wala sikuzaa, wala sikulea vijana, wala sikulea wanawali.” (Isaya 23:4) Baada ya kuharibiwa kwa Tiro, pwani ambako jiji hilo lilikuwa hapo awali itaonekana kame na ukiwa. Bahari itaonekana kana kwamba inapaza kilio chenye maumivu makali, kama mama aliyefiwa na watoto na kufadhaika sana hivi kwamba asema hakuzaa watoto wowote. Sidoni ataaibikia jambo linalompata bintiye.
9. Huzuni ya watu baada ya kuanguka kwa Tiro itafanana na hofu kuu baada ya matukio gani mengine?
9 Naam, habari za kuharibiwa kwa Tiro zitasababisha huzuni kotekote. Isaya asema: “Habari itakapofika Misri [“kama vile ilivyo kwa habari ihusuyo Misri,” “NW”] wataona uchungu sana kwa sababu ya habari ya Tiro.” (Isaya 23:5) Uchungu wa waombolezaji utafanana na ule unaosababishwa na habari ihusuyo Misri. Nabii amaanisha habari gani? Labda amaanisha utimizo wa “ufunuo [wake wa mapema] juu ya Misri.”b (Isaya 19:1-25) Au labda nabii amaanisha habari za kuharibiwa kwa jeshi la Farao katika siku ya Musa, kulikosababisha hofu kuu kotekote. (Kutoka 15:4, 5, 14-16; Yoshua 2:9-11) Kwa vyovyote, wale wanaosikia habari za kuharibiwa kwa Tiro watapata maumivu makali. Waelezwa wakimbilie mbali huko Tarshishi ili kupata usalama nao waamriwa wapige kelele ya huzuni yao: “Piteni mpaka Tarshishi, enyi mkaao kisiwani, toeni sauti ya uchungu.”—Isaya 23:6.
Furaha “Tangu Siku za Kale”
10, 12. Toa maelezo kuhusu mali, mambo ya kale, na uvutano wa Tiro.
10 Tiro ni jiji la kale, kama vile Isaya anavyotukumbusha aulizapo: “Je! huu ndio mji wenu wa furaha, ambao mwanzo wake ulikuwako tangu siku za kale?” (Isaya 23:7a) Historia ya ufanisi wa Tiro yarudi nyuma angalau hadi wakati wa Yoshua. (Yoshua 19:29) Miaka ipitapo, Tiro limepata kuwa mtengenezaji maarufu wa vyombo vya chuma, vya kioo, na rangi ya zambarau. Kanzu za zambarau ya Tiro ni ghali sana, na watu wenye vyeo wavitafuta sana vitambaa vyenye thamani vya Tiro. (Linganisha Ezekieli 27:7, 24.) Pia, Tiro ni kituo cha biashara, inayofanywa na wasafiri kwenye nchi kavu hali kadhalika cha kuuza na kununua mali katika nchi za nje.
11 Isitoshe, jiji hilo lina nguvu kijeshi. L. Sprague de Camp aandika: “Ijapokuwa hawakupenda vita sana—walikuwa wafanya-biashara, sio wanajeshi—Wafoinike waliyalinda majiji yao kwa ujasiri na ukaidi mkubwa. Sifa hizo, na vilevile jeshi lao lenye nguvu la wanamaji, ziliwawezesha Watiro kukabiliana na jeshi la Ashuru, lililokuwa lenye nguvu zaidi wakati huo.”
12 Kwa kweli, Tiro laacha alama yake kwenye ulimwengu wa Mediterania. “Miguu yake ilimchukua akae mbali sana.” (Isaya 23:7b) Wafoinike wasafiri nchi za mbali, wakianzisha vituo vya biashara na bandari, ambavyo vingine vyageuka kuwa makoloni. Kwa kielelezo, Carthage, iliyoko pwani ya kaskazini mwa Afrika, ni koloni la Tiro. Baada ya muda, itapita Tiro na kushindana na Roma kwa habari ya uvutano katika ulimwengu wa Mediterania.
Kiburi Chake Kitaharibiwa
13. Kwa nini swali lazuka kuhusu yule anayethubutu kutangaza hukumu dhidi ya Tiro?
13 Kwa kuzingatia mambo ya kale na mali za Tiro, swali lifuatalo lafaa: “Ni nani aliyefanya shauri hili juu ya Tiro, uliotia watu taji, ambao wafanya biashara wake walikuwa wana wa wafalme, na wachuuzi wake ni watu wakuu wa dunia?” (Isaya 23:8) Ni nani anayethubutu kusema dhidi ya jiji ambalo limeteua watu wenye nguvu kwenye vyeo vya mamlaka ya juu katika makoloni yake na kwingineko—hivyo likiwa ‘mwenye kutia watu taji’? Ni nani anayethubutu kusema dhidi ya jiji ambalo wafanya-biashara wake ni wana wa wafalme na wachuuzi wake ni watu wakuu? Maurice Chehab, aliyekuwa mkurugenzi wa mambo ya kale kwenye Jumba la Makumbusho ya Taifa la Beirut, Lebanon, alisema: “Tangu karne ya tisa hadi ya sita K.K., jiji la Tiro lilikuwa na umaarufu kama ule wa jiji la London mwanzoni mwa karne ya ishirini.” Basi, ni nani anayethubutu kusema dhidi ya jiji hilo?
14. Ni nani anayetangaza hukumu dhidi ya Tiro, na kwa nini?
14 Jibu lililopuliziwa litasababisha wasiwasi jijini Tiro. Isaya asema: “BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi ndiye aliyefanya shauri hili, ili kuharibu kiburi cha utukufu wote, na kuwaaibisha watu wa duniani wote pia.” (Isaya 23:9) Kwa nini Yehova atangaza hukumu dhidi ya jiji hilo la kale lenye mali? Je, ni kwa sababu wakazi wake ni waabudu wa Baali, mungu asiye wa kweli? Je, ni kwa sababu ya uhusiano wa Tiro na Yezebeli—binti ya Mfalme Ethbaali wa Sidoni, kutia ndani Tiro—aliyeolewa na Mfalme Ahabu wa Israeli, naye akawaua manabii wa Yehova? (1 Wafalme 16:29, 31; 18:4, 13, 19) Jibu kwa maswali hayo mawili ni la. Tiro lahukumiwa kwa sababu ya kiburi chake chenye majigambo—limejitajirisha kwa kutia watu wengine hasara, kutia ndani Waisraeli. Katika karne ya tisa K.W.K., Yehova aliliambia Tiro na majiji mengine kupitia nabii Yoeli: “Watoto wa Yuda na watoto wa Yerusalemu mmewauzia Wayunani, mpate kuwahamisha mbali na mipaka yao.” (Yoeli 3:6) Je, Mungu aweza kupuuza vile Tiro linawatenda watu wake wa agano kama bidhaa tu za uchuuzi?
15. Tiro litatendaje Yerusalemu liangukapo mikononi mwa Nebukadreza?
15 Tiro halitabadilika baada ya miaka mia moja kupita. Jeshi la Mfalme Nebukadreza wa Babiloni liharibupo Yerusalemu mwaka wa 607 K.W.K., Tiro litashangilia: “Aha! yeye [Yerusalemu] amevunjika aliyekuwa lango la kabila za watu; amenigeukia; nitajazwa kwa kuwa sasa ameharibika.” (Ezekieli 26:2) Tiro litashangilia, likitarajia kunufaika kutokana na kuharibiwa kwa Yerusalemu. Kwa kuwa jiji kuu la Yuda halishindani tena, Tiro litatarajia kujipatia biashara zaidi. Yehova atawaaibisha wale wanaojiita ‘wakuu wa dunia,’ wanaosimama kwa kiburi na adui za watu wake.
16, 17. Ni nini kitakachowapata wakazi wa Tiro jiji hilo liangukapo? (Ona kielezi-chini.)
16 Isaya aendelea na hukumu ya Yehova juu ya Tiro: “Pita katika nchi yako, kama [Mto] Nile, Ee binti wa Tarshishi, hapana tena mshipi wa kukuzuia. Amenyosha mkono wake juu ya bahari, amezitikisa falme; Bwana ametoa amri katika habari za Kanaani, kuziangamiza ngome zake. Naye akasema, Usizidi kufurahi, ewe bikira uliyeaibishwa, binti wa Sidoni, haya, ondoka, uende hata Kitimu; huko nako hutapata raha.”—Isaya 23:10-12.
17 Kwa nini Tiro laitwa “binti wa Tarshishi”? Labda kwa sababu baada ya kushindwa kwa Tiro, Tarshishi litaendelea kuwa na nguvu zaidi kati ya majiji hayo mawili.c Wakazi wa Tiro lililoharibiwa watatawanyika kama mto uliofurika, kingo zake zimevunjika na maji yake yakifurika kuingia kwenye nyanda zote jirani. Ujumbe wa Isaya kwa “binti wa Tarshishi” wakazia ukali wa yale yatakayolikumba Tiro. Yehova mwenyewe anyosha mkono wake na kutoa amri. Hakuna awezaye kubadilisha matokeo.
18. Kwa nini Tiro laitwa “bikira . . . binti wa Sidoni,” na hali yake itabadilikaje?
18 Isaya pia asema juu ya Tiro kuwa “bikira . . . binti wa Sidoni,” kuonyesha kwamba washindi wa kigeni hawajaliteka na kulipora jiji hilo hapo awali nalo bado lafurahia hali ya kutoshindwa. (Linganisha 2 Wafalme 19:21; Isaya 47:1; Yeremia 46:11.) Lakini sasa litaharibiwa, na baadhi ya wakazi wake, sawa na wakimbizi, watavuka hadi Kitimu, koloni la Foinike. Hata hivyo, kwa kuwa wamepoteza nguvu zao za kiuchumi, hawatapata raha huko.
Wakaldayo Watamfanya Ukiwa
19, 20. Ni nani anayetabiriwa kuwa atashinda Tiro, na unabii huo watimizwaje?
19 Ni serikali gani itakayotekeleza hukumu ya Yehova juu ya Tiro? Isaya atangaza: “Tazama, nchi ya Wakaldayo; watu hao hawako tena; Mwashuri ameiweka tayari kwa hayawani wa jangwani; wamesimamisha buruji zao za vita, wameyaharibu majumba yake ya enzi, akaufanya kuwa uharibifu. Pigeni yowe, enyi merikebu za Tarshishi; maana ngome yenu imefanywa ukiwa.” (Isaya 23:13, 14) Wakaldayo—wala sio Waashuri—ndio watakaoshinda Tiro. Watasimamisha buruji zao za mazingiwa, wayaharibu majumba ya enzi ya Tiro, na kuifanya hiyo ngome ya meli za Tarshishi kuwa magofu yanayobomoka.
20 Kwa utimizo wa unabii huo, muda mfupi baada ya kuanguka kwa Yerusalemu, Tiro laasi dhidi ya Babiloni, na Nebukadreza azingia jiji hilo. Tiro lakabili mazingiwa hayo, likiamini kwamba haliwezi kushindwa. Mazingiwa yaendeleapo, wakuu wa majeshi ya Babiloni watiwa ‘upaa vichwani’ kutokana na mkwaruzo wa kofia zao za chuma na mabega yao ‘yaambuliwa ngozi’ kutokana na kubeba vifaa vinavyotumiwa katika ujenzi wa mazingiwa. (Ezekieli 29:18) Mazingiwa hayo yamgharimu sana Nebukadreza. Jiji la Tiro barani laharibiwa, ingawa Nebukadreza haiteki nyara yake. Hazina nyingi za Tiro zimehamishiwa kwenye kisiwa kidogo kilichoko karibu meta 800 kutoka pwani. Kwa kuwa hana kundi la meli, mfalme huyo wa Wakaldayo ashindwa kuteka kisiwa hicho. Tiro lasalimu amri baada ya miaka 13, ingawa litasalia na lione utimizo wa unabii mwingine mbalimbali.
“Atarudi Apate Ujira Wake”
21. Tiro ‘limesahauliwaje,’ na kwa muda gani?
21 Isaya aendelea kutoa unabii: “Itakuwa katika siku ile, Tiro utasahauliwa miaka sabini, kadiri ya siku za mfalme mmoja.” (Isaya 23:15a) Baada ya Wababiloni kuliharibu jiji la barani, jiji la kisiwani la Tiro ‘litasahauliwa.’ Sawasawa kabisa na unabii huo, kwa muda wa “mfalme mmoja”—Milki ya Babiloni—jiji la kisiwani la Tiro halitakuwa kitovu muhimu kiuchumi. Yehova, kupitia Yeremia, aweka Tiro kati ya mataifa yatakayotengwa ili yanywe divai ya hasira Yake kali. Asema: “Mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.” (Yeremia 25:8-17, 22, 27) Ni kweli kwamba jiji la kisiwani la Tiro haliwi chini ya Babiloni kwa miaka 70 kamili, kwa vile Milki ya Babiloni yaanguka mwaka wa 539 K.W.K. Yaonekana kwamba miaka 70 huwakilisha kipindi cha utawala mkuu wa Babiloni ambapo nasaba ya wafalme ya Babiloni yajisifu kuwa imeinua kiti chake cha ufalme hata juu ya “nyota za Mungu.” (Isaya 14:13) Mataifa mbalimbali yaja chini ya utawala huo nyakati mbalimbali. Lakini mwishoni mwa miaka 70, utawala huo utaanguka. Ni nini kitakacholipata Tiro wakati huo?
22, 23. Ni nini kitakachotendeka kwa Tiro litokapo chini ya utawala wa Babiloni?
22 Isaya aendelea: “Hata mwisho wa miaka sabini, Tiro utakuwa kama vile ulivyo wimbo wa kahaba. Twaa kinubi, tembea mjini, Ewe kahaba uliyesahauliwa; piga vizuri, imba nyimbo nyingi, upate kukumbukwa tena. Hata itakuwa mwisho wa miaka sabini, BWANA ataizuru nchi ya Tiro, naye atarudi apate ujira wake, atafanya ukahaba pamoja na falme zote za ulimwengu juu ya uso wa dunia.”—Isaya 23:15b-17.
23 Baada ya kuanguka kwa Babiloni mwaka wa 539 K.W.K., Foinike yawa koloni la Milki ya Umedi na Uajemi. Mtawala Mwajemi, Koreshi Mkuu, ni mtawala anayetoa uhuru zaidi. Chini ya utawala wake mpya, Tiro litaanza tena utendaji wake wa awali na kujitahidi sana kupata umaarufu wake wa kuwa kituo cha kibiashara—kama vile kahaba ambaye amesahauliwa na kupoteza wateja wake atafutavyo kuvutia wateja wapya kwa kutembea jijini, akipiga kinubi chake na kuimba nyimbo zake. Je, Tiro litafanikiwa? Ndiyo, Yehova atalipatia mafanikio. Baada ya muda, jiji hilo la kisiwani litapata ufanisi mwingi sana hivi kwamba mwishoni mwa karne ya sita K.W.K., nabii Zekaria atasema: “Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu.”—Zekaria 9:3.
‘Faida Yake Itakuwa Wakfu’
24, 25. (a) Faida ya Tiro yawaje wakfu kwa Yehova? (b) Licha ya msaada wa Tiro kwa watu wa Mungu, ni unabii gani mwingine anaopulizia Yehova juu ya jiji hilo?
24 Maneno ya unabii yanayofuata yanavutia kama nini! “Biashara [“faida,” “NW”] yake na ujira wake utakuwa wakfu kwa BWANA, hautawekwa hazinani wala hautawekwa akiba; bali mapato ya biashara yake yatakuwa mali zao wakaao mbele za BWANA, wapate kula na kushiba, na kuvaa mavazi ya fahari.” (Isaya 23:18) Faida ya mali ya Tiro yapataje kuwa wakfu? Yehova aongoza mambo ili itumiwe kulingana na mapenzi yake—ili watu wake wapate kula na kushiba na kuvaa. Hayo yatokea baada ya kurudi kwa Waisraeli kutoka uhamishoni Babiloni. Watu wa Tiro wawasaidia kwa kuleta mbao za mierezi kwa kujenga hekalu upya. Pia waanza tena kufanya biashara na jiji la Yerusalemu.—Ezra 3:7; Nehemia 13:16.
25 Licha ya hayo, Yehova apulizia ufunuo mwingine dhidi ya Tiro. Zekaria atoa unabii juu ya jiji la kisiwani ambalo sasa lina mali nyingi: “Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto.” (Zekaria 9:4) Hayo yatimizwa Julai 332 K.W.K. wakati Aleksanda Mkuu abomoapo jiji hilo maarufu la baharini.
Epuka Ufuatiaji wa Vitu vya Kimwili na Kiburi
26. Kwa nini Mungu alihukumu Tiro?
26 Yehova alihukumu Tiro kwa sababu ya kiburi chake, tabia ambayo yeye huikataa. “Macho ya kiburi” yameorodheshwa kwanza miongoni mwa vitu saba anavyovichukia Yehova. (Mithali 6:16-19) Paulo alihusianisha kiburi na Shetani Ibilisi, na maelezo ya Ezekieli juu ya Tiro lenye kiburi yana mambo yanayomfafanua Shetani mwenyewe. (Ezekieli 28:13-15; 1 Timotheo 3:6) Kwa nini Tiro lilikuwa na kiburi? Ezekieli, akizungumza na Tiro, asema: “Moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako.” (Ezekieli 28:5) Jiji hilo lilijitolea kwa biashara na ukusanyaji wa pesa. Mafanikio ya Tiro kwa mambo hayo yalifanya lijiinue mno. Kupitia Ezekieli, Yehova alimwambia “mkuu wa Tiro”: “Moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu.”—Ezekieli 28:2.
27, 28. Wanadamu waweza kuangukia mtego gani, na Yesu alitoaje kielezi cha jambo hilo?
27 Mataifa na pia watu mmoja-mmoja waweza kushindwa na kiburi na mtazamo usiofaa kuhusu mali. Yesu alitoa mfano ulioonyesha jinsi mtego huo uwezavyo kuwa wenye hila. Alinena kuhusu mtu fulani tajiri ambaye mashamba yake yalizaa vema sana. Akiwa amejawa furaha, mtu huyo akapanga kujenga ghala kubwa zaidi kwa ajili ya mazao yake naye akatazamia kwa furaha maisha marefu yenye starehe. Lakini haikutukia hivyo. Mungu alimwambia: “Wewe mwenye kukosa akili, usiku huu wanadai nafsi yako kutoka kwako. Ni nani, basi, atakayepaswa kuwa na vitu ulivyoviweka akiba?” Naam, mtu huyo akafa, na mali yake haikumfaa chochote.—Luka 12:16-20.
28 Yesu alimalizia mfano huo, akisema: “Hivyo ndivyo huwa kwa mtu ajilimbikiaye hazina mwenyewe lakini si tajiri kuelekea Mungu.” (Luka 12:21) Halikuwa kosa kuwa na mali, wala haikuwa dhambi kupata mavuno mema. Kosa la mtu huyo lilikuwa kufanya vitu hivyo kuwa mambo muhimu zaidi maishani mwake. Aliweka matumaini yake yote katika utajiri wake. Alipokuwa akitazamia wakati ujao, hakumzingatia Yehova Mungu.
29, 30. Yakobo alitoaje onyo juu ya kujitegemea?
29 Yakobo alikazia sana jambo hilohilo. Alisema: “Haya, basi, nyinyi msemao: ‘Leo au kesho hakika sisi tutafunga safari kwenda kwenye jiji hili na hakika tutamaliza mwaka huko, nasi hakika tutajitia katika biashara na kuzipata faida,’ kwa kuwa hamjui uhai wenu utakuwa nini kesho. Kwa maana nyinyi ni ukungu unaotokea kwa muda kidogo na kisha kutoweka. Badala ya hivyo, mwapaswa kusema: ‘Yehova akipenda, tutaishi na pia kufanya hili au lile.’” (Yakobo 4:13-15) Kisha Yakobo akaonyesha uhusiano uliopo baina ya mali na kiburi alipoendelea, akisema: “Lakini sasa mwaonea fahari kujigamba kwenu kwa kujitanguliza. Kuona fahari kote kwa namna hiyo ni kuovu.”—Yakobo 4:16.
30 Kwa kurudia tena, si dhambi kufanya biashara. Dhambi ni kile kiburi, kujigamba, kujitumaini, mambo ambayo kupata mali kwaweza kutokeza. Kwa hekima, mithali ya kale ilisema: “Usinipe umaskini wala utajiri.” Umaskini waweza kufanya maisha yawe machungu sana. Lakini utajiri waweza kufanya mtu ‘amkane Mungu, akisema, Yehova ni nani?’—Mithali 30:8, 9, NW.
31. Yafaa Mkristo ajiulize maswali gani?
31 Twaishi katika ulimwengu ambamo wengi wametumbukia katika pupa na ubinafsi. Kwa sababu ya hali ya kibiashara iliyopo, mkazo mwingi huwekwa juu ya mali. Basi, yafaa Mkristo ajichunguze ili kuhakikisha kwamba haangukii mtego uleule uliolinasa jiji la kibiashara la Tiro. Je, anatumia wakati wake mwingi mno na nguvu zake nyingi mno akifuatia vitu vya kimwili, hivi kwamba ageuka kuwa mtumwa wa utajiri? (Mathayo 6:24) Je, anahusudu watu fulani ambao huenda wana mali nyingi au bora zaidi kushinda zake? (Wagalatia 5:26) Ikiwa ana mali, je, aona kwa kiburi kwamba astahili ufikirio au mapendeleo zaidi ya wengine? (Linganisha Yakobo 2:1-9.) Ikiwa yeye si tajiri, je, ‘ameazimia kuwa tajiri,’ kwa vyovyote vile? (1 Timotheo 6:9) Je, anajishughulisha sana na mambo ya kibiashara hivi kwamba aacha sehemu ndogo tu ya maisha yake kwa ajili ya utumishi wa Mungu? (2 Timotheo 2:4) Je, anajishughulisha mno na ufuatiaji wa mali hivi kwamba apuuza kanuni za Kikristo katika shughuli zake za kibiashara?—1 Timotheo 6:10.
32. Yohana alitoa onyo gani, nasi twaweza kulitumiaje?
32 Haidhuru hali yetu ya kiuchumi, Ufalme wapaswa kutangulizwa nyakati zote maishani mwetu. Ni muhimu kwamba tusiyasahau kamwe maneno ya mtume Yohana: “Msiwe mkipenda ama ulimwengu ama vitu vilivyo katika ulimwengu. Ikiwa yeyote aupenda ulimwengu, kumpenda Baba hakumo katika yeye.” (1 Yohana 2:15) Ni kweli kwamba twalazimika kutumia mipango ya kiuchumi ya ulimwengu ili kujiruzuku. (2 Wathesalonike 3:10) Basi, ‘twautumia ulimwengu’—lakini hatuutumii “kwa ukamili.” (1 Wakorintho 7:31) Ikiwa twavipenda mno vitu vya kimwili—vitu vilivyo ulimwenguni—hatumpendi tena Yehova. Kufuatia “tamaa ya mwili na tamaa ya macho na wonyesho wa mtu wa kujivunia njia yake ya kutegemeza maisha” hakupatani na kufanya mapenzi ya Mungu.d Na kufanya mapenzi ya Mungu ndiko kuongozapo kwenye uhai wa milele.—1 Yohana 2:16, 17.
33. Wakristo wawezaje kuepuka mtego ulionasa Tiro?
33 Mtego wa kutanguliza ufuatiaji wa vitu vya kimwili zaidi ya mambo mengine yote ulinasa Tiro la kale. Jiji hilo lilifanikiwa kwa vitu vya kimwili, likawa na kiburi, nalo likaadhibiwa kwa kiburi chake. Kielelezo chake ni onyo kwa mataifa na watu mmoja-mmoja leo. Ni afadhali kama nini kufuata shauri la mtume Paulo! Awasihi Wakristo “wasiwe wenye kunia ya juu, na waweke tumaini lao, si juu ya mali zisizo hakika, bali juu ya Mungu, ambaye hututolea sisi vitu vyote kwa utajiri kwa ajili ya ufurahio wetu.”—1 Timotheo 6:17.
[Maelezo ya Chini]
a Wasomi fulani huhusianisha Tarshishi na Sardinia, kisiwa kilichoko Mediterania ya magharibi. Kisiwa cha Sardinia pia kilikuwa mbali kutoka Tiro.
b Ona Sura ya 15, ukurasa wa 200-207, wa kitabu hiki.
c Au, usemi “binti wa Tarshishi” huenda ukawarejezea wakazi wa Tarshishi. Kitabu kimoja cha marejezo chasema: “Wenyeji wa Tarshishi sasa wako huru kusafiri na kufanya biashara kwa uhuru kama vile Nile ufurikapo pande zote.” Ijapokuwa hivyo, mkazo wawekwa juu ya matokeo mabaya ya kuanguka kwa Tiro.
d “Wonyesho . . . wa kujivunia” ni usemi uliotumiwa kutafsiri neno la Kigiriki a·la·zo·niʹa, linalofafanuliwa kuwa “maoni yasiyo na heshima na ya bure tu yanayomfanya mtu aweke tumaini katika uthabiti wa vitu vya duniani.”—The New Thayer’s Greek-English Lexicon.
[Ramani katika ukurasa wa 256]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ULAYA
HISPANIA (Labda TARSHISHI ilikuwa hapa)
BAHARI YA MEDITERANIA
SARDINIA
SAIPRASI
ASIA
SIDONI
TIRO
AFRIKA
MISRI
[Picha katika ukurasa wa 250]
Tiro lingejitiisha kwa Babiloni, wala sio kwa Ashuru
[Picha katika ukurasa wa 256]
Sarafu ikionyesha Melkart, mungu mkuu wa Tiro
[Picha katika ukurasa wa 256]
Mfano wa meli ya Foinike