Sura Ya Sita
Kufumbua Fumbo la Ule Mti Mkubwa
1. Ni nini lililompata Mfalme Nebukadreza, nalo lilizusha maswali gani?
YEHOVA alimruhusu Mfalme Nebukadreza awe mtawala wa ulimwengu. Akiwa mtawala wa Babiloni, alikuwa na mali nyingi, vyakula vingi vinono, na makao makubwa ya kifalme—vitu vyote vya kimwili alivyotamani. Lakini ghafula, akadhiliwa. Akiwa amerukwa na akili, Nebukadreza alitenda kama mnyama! Akiwa ameondoshwa kwenye meza yake ya kifalme na makao yake makuu, aliishi kondeni na kula nyasi kama ng’ombe. Ni nini kilichosababisha msiba huo? Na kwa nini twapaswa kupendezwa na jambo hilo?—Linganisha Ayubu 12:17-19; Mhubiri 6:1, 2.
MFALME AMTUKUZA ALIYE JUU
2, 3. Mfalme wa Babiloni aliwatakia raia zake nini, naye alimwonaje Mungu Aliye Juu?
2 Punde baada ya kurudiwa na akili timamu, Nebukadreza alipeleka kotekote katika milki yake ripoti yenye kutokeza ya mambo yaliyotokea. Yehova alimpulizia nabii Danieli ahifadhi rekodi sahihi ya matukio hayo. Yaanza kwa maneno haya: “Mfalme Nebukadreza, kwa watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wanaokaa katika dunia yote; Amani iongezeke kwenu. Mimi nimeona vema kutangaza habari za ishara na maajabu, aliyonitendea Mungu aliye juu. Ishara zake ni kubwa kama nini! na maajabu yake yana uweza kama nini! ufalme wake ni ufalme wa milele; na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi.”—Danieli 4:1-3.
3 Raia wa Nebukadreza walikuwa “wa[ki]kaa katika dunia yote”—milki yake ikitia ndani sehemu kubwa ya ulimwengu wa rekodi ya Biblia. Kuhusu Mungu wa Danieli, mfalme alisema hivi: “Ufalme wake ni ufalme wa milele.” Jinsi maneno hayo yalivyomtukuza Yehova kotekote katika Milki ya Babiloni! Isitoshe, hiyo ilikuwa mara ya pili ambayo Nebukadreza alikuwa ameonyeshwa kwamba Ufalme wa Mungu peke yake husimama “milele na milele.”—Danieli 2:44.
4. Kuhusu Nebukadreza, “ishara na maajabu” ya Yehova zilianzaje?
4 “Aliye juu” alifanya “ishara na maajabu” gani? Hizo zilianza kwa mambo ambayo mfalme mwenyewe alijionea, yanayosimuliwa katika maneno haya: “Mimi, Nebukadreza, nalikuwa nikistarehe katika nyumba yangu, nikisitawi katika nyumba yangu ya enzi. Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha.” (Danieli 4:4, 5) Mfalme wa Babiloni alifanya nini juu ya ndoto hiyo yenye kusumbua?
5. Nebukadreza alimwonaje Danieli, na kwa nini?
5 Nebukadreza aliwaita wenye hekima wa Babiloni na kuwaambia ndoto hiyo. Nao walishindwa kama nini! Hawakuweza kuifasiri hata kidogo. Rekodi yaongezea kusema hivi: “Hatimaye Danieli akaingia mbele yangu, ambaye jina lake ni Belteshaza, kwa kufuata jina la mungu wangu; tena ndani yake inakaa roho ya miungu watakatifu; nikamhadithia ile ndoto.” (Danieli 4:6-8) Kwenye makao ya mfalme, Danieli aliitwa Belteshaza, na huenda ikawa mungu asiye wa kweli ambaye mfalme alimwita “mungu wangu” alikuwa Bel au Nebo au Marduki. Kwa kuwa aliabudu miungu mingi, Nebukadreza alimwona Danieli kuwa mtu aliyekuwa na “roho ya miungu watakatifu.” Na kwa sababu ya cheo cha Danieli akiwa liwali juu ya watu wote wenye hekima wa Babiloni, mfalme alimwita “mkuu wa waganga.” (Danieli 2:48; 4:9; linganisha Danieli 1:20.) Bila shaka, Danieli mwaminifu hakuacha kamwe kumwabudu Yehova ili afanye uganga.—Mambo ya Walawi 19:26; Kumbukumbu la Torati 18:10-12.
MTI MKUBWA SANA
6, 7. Ungefafanuaje kile ambacho Nebukadreza aliona katika ndoto yake?
6 Ndoto iliyomfadhaisha mfalme wa Babiloni ilikuwa juu ya nini? “Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi,” akasema Nebukadreza, “naliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana. Mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia. Majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote; wanyama wa kondeni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake; kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake.” (Danieli 4:10-12) Yaripotiwa kwamba Nebukadreza alipenda sana mierezi mikubwa ya Lebanoni, alienda kuiona, hata akaleta mbao zake kadhaa Babiloni. Lakini hakuwa amepata kuona mti wowote ulio kama ule aliouona kwenye ndoto yake. Ulikuwa mahali penye kutokeza zaidi “katikati ya nchi,” ulionekana kote duniani, nao ulizaa sana hivi kwamba uliandalia kila kitu chenye mwili chakula.
7 Mengi zaidi yalihusika katika ndoto hiyo, kwa kuwa Nebukadreza aliongezea kusema hivi: “Nikaona katika njozi za kichwa changu kitandani mwangu, na tazama, mlinzi, naye ni mtakatifu, alishuka kutoka mbinguni. Akapaza sauti yake, akasema, Ukateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yapukusieni mbali majani yake, na kuyatawanya matunda yake, wanyama na waondoke hapo chini yake, na ndege katika matawi yake. Walakini kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikapate maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama katika majani ya nchi.”—Danieli 4:13-15.
8. “Mlinzi” alikuwa nani?
8 Wababiloni walikuwa na dhana yao wenyewe ya kidini juu ya viumbe wa kiroho walio wema na walio waovu. Lakini “mlinzi” huyo kutoka mbinguni alikuwa nani? Kwa kuwa alisemwa kuwa “mtakatifu,” alikuwa malaika mwadilifu aliyemwakilisha Mungu. (Linganisha Zaburi 103:20, 21.) Hebu wazia maswali ambayo lazima yalimsumbua Nebukadreza! Mbona mti huo ukatwe? Kisiki cha shina kilichozuiwa kisikue kwa kufungwa pingu ya chuma na shaba kina faida gani? Kwa kweli, kisiki hicho cha shina chatimiza kusudi gani?
9. Mlinzi alisema nini hasa, na ni maswali gani yanayozuka?
9 Lazima Nebukadreza alitatanishwa kabisa aliposikia maneno yafuatayo ya mlinzi: “Moyo wake ubadilike, usiwe moyo wa binadamu, na apewe moyo wa mnyama; nyakati saba zikapite juu yake. Hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge.” (Danieli 4:16, 17) Kisiki cha shina hakina moyo wa binadamu unaopigapiga ndani yake. Kwa sababu hiyo, kisiki cha shina chaweza kupewaje moyo wa mnyama? Zile “nyakati saba” ni nini? Na yote hayo yahusianaje na utawala katika “ufalme wa wanadamu”? Bila shaka Nebukadreza alitaka kujua.
MFALME APATA HABARI ZISIZOPENDEZA
10. (a) Kulingana na Maandiko, miti yaweza kufananisha nini? (b) Ni nini kinachowakilishwa na ule mti mkubwa?
10 Baada ya kuisikia ndoto, Danieli alishangazwa kwa muda, kisha akaogofywa. Akihimizwa na Nebukadreza aifafanue, nabii huyo alisema hivi: “Bwana wangu, ndoto hii iwapate wao wakuchukiao, na tafsiri yake iwapate adui zako. Ule mti uliouona, uliokua, ukawa na nguvu . . . ; ni wewe, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia.” (Danieli 4:18-22) Katika Maandiko, miti yaweza kufananisha watu, watawala, na falme. (Zaburi 1:3; Yeremia 17:7, 8; Ezekieli, sura ya 31) Kama ule mti mkubwa wa ndoto yake, Nebukadreza alikuwa ‘amekua na kupata nguvu’ akiwa mtawala wa serikali ya ulimwengu. Lakini ‘mamlaka yanayofika mpaka mwisho wa dunia,’ kutia ndani ufalme wote wa wanadamu, yawakilishwa na ule mti mkubwa. Kwa hiyo, mti huo wawakilisha enzi kuu ya Yehova ya ulimwengu wote, hasa uhusiano kati ya enzi hiyo na dunia.—Danieli 4:17.
11. Ndoto ya mfalme yaonyeshaje kwamba angepata badiliko lenye kumdhili?
11 Nebukadreza angepatwa na badiliko lenye kumdhili. Akieleza juu ya hilo, Danieli alisema hivi: “Kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake; tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme.” (Danieli 4:23, 24) Kwa hakika ujasiri ulihitajiwa ili kumpa mfalme huyo mwenye nguvu ujumbe huo!
12. Ni nini ambacho kingempata Nebukadreza?
12 Ni nini ambacho kingempata Nebukadreza? Wazia alivyotenda, Danieli alipoendelea kusema: “Utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng’ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote.” (Danieli 4:25) Yaonekana hata maofisa wa makao ya kifalme ya Nebukadreza ‘wangemfukuza mbali na wanadamu.’ Lakini je, angetunzwa na wachungaji wenye huruma? La, kwa kuwa Mungu alikuwa ameagiza kwamba Nebukadreza angekaa pamoja na “wanyama wa kondeni,” akila majani.
13. Ndoto ya mti ilionyesha cheo cha Nebukadreza akiwa mtawala wa ulimwengu kingepatwa na nini?
13 Kama vile mti huo ulivyokatwa, Nebukadreza angeondolewa asiwe mtawala wa ulimwengu—lakini kwa muda tu. Danieli alieleza hivi: “Kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.” (Danieli 4:26) Katika ndoto ya Nebukadreza kisiki cha shina cha mti ulioangushwa kiliachwa, ingawa kilifungwa kwa pingu kisikue. Vivyo hivyo, “kisiki cha shina” cha mfalme wa Babiloni kingeendelea kuwapo, ingawa kingefungwa pingu kisisitawi kwa “nyakati saba.” Cheo chake akiwa mtawala wa ulimwengu kingekuwa sawa na kile kisiki cha shina kilichofungwa pingu. Cheo hicho kingehifadhiwa hadi nyakati saba zipite. Yehova angehakikisha kwamba katika kipindi hicho hakuna mtu ambaye angekuwa mtawala wa pekee wa Babiloni akichukua mahali pa Nebukadreza, ingawa huenda ikawa mwana wake aitwaye Evil-merodaki aliendeleza utawala kwa niaba yake akiwa kama mtawala.
14. Danieli alimhimiza Nebukadreza afanye nini?
14 Kwa sababu ya yale yaliyosemwa kuhusu Nebukadreza, Danieli alihimiza hivi kwa ujasiri: “Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.” (Danieli 4:27) Ikiwa Nebukadreza angeacha mwenendo wake wenye dhambi wa uonevu na kiburi, huenda hilo lingebadili mambo yaliyompata. Kumbuka, karne mbili hivi mapema, Yehova alikuwa ameazimia kuwaharibu watu wa Ninewi, jiji kuu la Ashuru, lakini hakufanya hivyo kwa sababu mfalme wake na raia zake walitubu. (Yona 3:4, 10; Luka 11:32) Vipi Nebukadreza mwenye kiburi? Je, angebadili njia zake?
UTIMIZO WA KWANZA WA NDOTO
15. (a) Nebukadreza aliendelea kuonyesha mtazamo gani? (b) Maandishi yafunua nini juu ya utendaji mbalimbali wa Nebukadreza?
15 Nebukadreza aliendelea kuwa na kiburi. Akitembea huku na huku kwenye paa ya jumba la kifalme miezi 12 baada ya ndoto yake, alijivuna hivi: “Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?” (Danieli 4:28-30) Nimrodi alikuwa ameujenga Babiloni (Babeli), lakini Nebukadreza aliupa fahari. (Mwanzo 10:8-10) Katika mojawapo ya maandishi yake ya kikabari, ajisifu hivi: “Nebukadreza, Mfalme wa Babiloni, aliyejenga upya Esagila na Ezida, mwana wa Nabopolasa ndimi. . . . Ngome ya Esagila na ya Babiloni niliziimarisha na kuliweka jina la utawala wangu milele.” (Kichapo Archaeology and the Bible, kilichoandikwa na George A. Barton, 1949, ukurasa wa 478-479) Maandishi mengine hurejezea mahekalu yapatayo 20 ambayo alirekebisha au kujenga upya. “Chini ya utawala wa Nebukadreza,” chasema kichapo The World Book Encyclopedia, “Babiloni lilipata kuwa mojawapo ya majiji yenye fahari sana ya ulimwengu wa kale. Katika rekodi zake mwenyewe, alitaja utendaji wake wa kijeshi mara chache sana, lakini aliandika juu ya ujenzi wake mwingi na ibada yake kwa miungu ya Babilonia. Huenda Nebukadreza ndiye aliyejenga Bustani Zenye Kuning’inia za Babiloni, mojawapo ya Maajabu Saba ya Ulimwengu wa Kale.”
16. Nebukadreza alikuwa amekaribia kudhiliwaje?
16 Ingawa alijivuna, Nebukadreza mwenye kiburi alikuwa akikaribia kudhiliwa. Simulizi lililopuliziwa lasema hivi: “Neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.”—Danieli 4:31, 32.
17. Ni nini kilichompata Nebukadreza mwenye kiburi, na mara moja akajikuta katika hali gani?
17 Papo hapo Nebukadreza akarukwa na akili. Akafukuzwa mbali na wanadamu, na kula majani “kama ng’ombe.” Akiwa miongoni mwa wanyama wa kondeni, haielekei kwamba aliketi tu kwenye majani katika aina fulani ya paradiso, akifurahia kupunga hewa siku baada ya siku. Katika Iraki ya leo, yalipo magofu ya Babiloni, kiwango cha joto hupanda hadi digrii 50 Selsiasi katika miezi ya kiangazi na kushuka chini ya kiwango cha kuganda wakati wa majira ya baridi kali. Kwa kuwa hazikutunzwa na kwa sababu ya hali ya hewa, nywele ndefu za matimutimu za Nebukadreza zilifanana na manyoya ya tai nazo kucha zake ndefu za mikono na miguu zikawa kama kucha za ndege. (Danieli 4:33) Mtawala huyo wa ulimwengu mwenye kiburi alikuwa amedhiliwa kama nini!
18. Wakati wa zile nyakati saba, ni nini kilichotokea kwa kiti cha ufalme cha Babiloni?
18 Katika ndoto ya Nebukadreza, ule mti mkubwa uliangushwa na kisiki cha shina lake kikafungwa pingu kizuiwe kukua kwa nyakati saba. Vivyo hivyo, Nebukadreza “aliuzuliwa katika kiti chake cha enzi” Yehova alipompiga kwa kichaa. (Danieli 5:20) Hilo hasa lilibadili moyo wa mfalme uliokuwa wa binadamu ukawa wa ng’ombe. Hata hivyo, Mungu alimhifadhia Nebukadreza kiti cha ufalme hadi nyakati saba zilipoisha. Ingawa huenda Evil-merodaki alitawala kwa muda, Danieli alikuwa ‘mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli.’ Wale waandamani wake watatu waliendelea kushiriki katika kusimamia mambo ya wilaya hiyo. (Danieli 1:11-19; 2:48, 49; 3:30) Wahamishwa hao wanne walingojea kurudishwa kwa Nebukadreza kwenye kiti cha ufalme akiwa mfalme timamu ambaye amejifunza kwamba “Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.”
KURUDISHWA KWA NEBUKADREZA
19. Baada ya Yehova kumrudishia Nebukadreza fahamu, mfalme huyo wa Babiloni alitambua nini?
19 Yehova alirudisha utimamu wa Nebukadreza mwishoni mwa zile nyakati saba. Kisha akimkiri Mungu Aliye Juu, mfalme huyo alisema hivi: “Hata mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi; na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu; naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe?” (Danieli 4:34, 35) Naam, Nebukadreza alikuja kufahamu kwamba Aliye Juu ndiye kwa kweli Mtawala Mwenye Enzi Kuu katika ufalme wa wanadamu.
20, 21. (a) Kuondolewa kwa pingu ya metali iliyofunga kisiki cha shina kulilinganaje na yaliyompata Nebukadreza? (b) Nebukadreza alikiri nini, na je, kufanya hivyo kulimfanya awe mwabudu wa Yehova?
20 Nebukadreza aliporudi kwenye kiti chake cha ufalme, ilikuwa kana kwamba ile pingu ya metali iliyofunga kisiki cha shina la mti ulioonekana kwenye ndoto ilikuwa imeondolewa. Kuhusu kurudishwa kwake, alisema hivi: “Basi wakati uo huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu, enzi yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na madiwani wangu, wakaja kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu, nikaongezewa enzi kupita kiasi.” (Danieli 4:36) Ikiwa maofisa wowote walikuwa wamemdharau mfalme aliyerukwa na akili, sasa walikuwa ‘wakimtafuta’ ili kumsaidia.
21 Mungu Aliye Juu alikuwa amefanya “ishara na maajabu” kama nini! Si ajabu kwamba mfalme wa Babiloni aliyerudishwa alisema hivi: “Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa mbinguni, namtukuza na kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia zake ni za adili; na wale waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.” (Danieli 4:2, 37) Hata hivyo, kukiri huko hakukumfanya Nebukadreza awe mwabudu wa Yehova, asiye Myahudi.
JE, KUNA UTHIBITISHO WA KILIMWENGU?
22. Watu fulani wamesema kichaa cha Nebukadreza kilikuwa ugonjwa gani, lakini twapaswa kutambua nini kuhusu kisababishi cha kichaa hicho?
22 Watu fulani wamesema kwamba kichaa cha Nebukadreza kilikuwa ugonjwa uitwao lycanthropy. Kamusi moja ya kitiba yasema hivi: “LYCANTHROPY . . . latokana na [lyʹkos], lupus, mbwa-mwitu; [anʹthro·pos], homo, mwanadamu. Jina hilo lilipewa ugonjwa wa watu ambao wanaamini kwamba wamegeuka na kuwa mnyama, na ambao huiga sauti na milio, umbo au tabia za mnyama huyo. Kwa kawaida watu hao hujiwazia wamegeuka kuwa mbwa-mwitu, mbwa au paka; nyakati nyingine kuwa fahali [ng’ombe], kama katika kisa cha Nebukadreza.” (Dictionnaire des sciences médicales, par une société de médicins et de chirurgiens, Paris, 1818, Buku la 29, ukurasa wa 246) Dalili za ugonjwa huo zafanana na zile za kichaa cha Nebukadreza. Hata hivyo, kwa kuwa ugonjwa wake wa akili ulitokana na amri ya Mungu, hauwezi kutambulishwa waziwazi kuwa ugonjwa fulani ujulikanao.
23. Ni ushuhuda gani wa kilimwengu uliopo unaothibitisha kichaa cha Nebukadreza?
23 Msomi John E. Goldingay ataja mambo fulani yanayopatana na kichaa na kurudishwa kwa Nebukadreza. Kwa mfano, ataarifu hivi: “Yaonekana kipande fulani cha maandishi ya kikabari charejezea aina fulani ya ugonjwa wa akili wa Nebukadreza, na huenda kupuuza kwake Babiloni na kuiacha.” Goldingay ataja hati iitwayo “Yobu wa Babiloni” na kusema kwamba hiyo “yatoa ushuhuda juu ya kutiwa adabu na Mungu, ugonjwa, kudhiliwa, kutafuta fasiri ya ndoto yenye kuogofya, kutupwa kama mti, kuwekwa nje, kula majani, kupoteza uelewevu, kuwa kama fahali, kunyeshewa na Marduki, kucha kuharibika, nywele kukua, na kufungwa pingu, kisha kurudishwa ambako yuamsifia mungu.”
NYAKATI SABA ZINAZOTUATHIRI
24. (a) Ule mti mkubwa wa ndoto wawakilisha nini? (b) Ni nini kilichozuiwa kwa nyakati saba, na hilo lilitokeaje?
24 Kama alivyowakilishwa na ule mti mkubwa, Nebukadreza alifananisha utawala wa ulimwengu. Lakini kumbuka kwamba ule mti unawakilisha utawala na enzi kuu iliyo kubwa kuliko utawala wa mfalme wa Babiloni. Mti huo wafananisha enzi kuu ya ulimwengu wote ya Yehova, “Mfalme wa mbinguni,” hasa kuhusiana na dunia. Kabla ya Yerusalemu kuharibiwa na Wababiloni, ufalme uliokuwa katika jiji hilo, Daudi na warithi wake wakikalia “kiti cha enzi cha BWANA,” uliwakilisha enzi kuu ya Mungu kuhusiana na dunia. (1 Mambo ya Nyakati 29:23) Mungu mwenyewe alifanya enzi hiyo kuu ikatwe na kufungwa pingu mwaka wa 607 K.W.K. alipomtumia Nebukadreza kuharibu Yerusalemu. Utawala wa Mungu duniani kupitia ufalme wa nasaba ya Daudi ulizuiliwa kwa nyakati saba. Nyakati hizo saba zilikuwa na urefu gani? Zilianza lini, na ni nini kilichoonyesha mwisho wake?
25, 26. (a) Katika kisa cha Nebukadreza, “nyakati saba” zilikuwa na urefu gani, na kwa nini wajibu hivyo? (b) Katika utimizo mkubwa, zile “nyakati saba” zilianza lini na jinsi gani?
25 Wakati wa kichaa cha Nebukadreza, “nywele zake zi[li]kua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.” (Danieli 4:33) Hilo lilichukua muda uliozidi siku saba au majuma saba. Tafsiri mbalimbali husema “nyakati saba,” na badala ya kusema hivyo nyingine husema “nyakati zilizowekwa rasmi (dhahiri)” au “vipindi vya wakati.” (Danieli 4:16, 23, 25, 32) Tafsiri moja ya Kigiriki cha Kale (Septuagint) husema “miaka saba.” Yosefo, mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza, aliziona zile “nyakati saba” kuwa “miaka saba.” (Antiquities of the Jews, Kitabu cha 10, Sura ya 10, fungu la 6) Na wasomi fulani Waebrania waliziona “nyakati” hizo kuwa “miaka.” Tafsiri ya Biblia Habari Njema, An American Translation, Today’s English Version, na tafsiri ya James Moffatt husema “miaka saba.”
26 Ni dhahiri kwamba “nyakati saba” za Nebukadreza zilihusisha miaka saba. Katika unabii, mwaka mmoja una wastani wa siku 360, au miezi 12 yenye siku 30. (Linganisha Ufunuo 12:6, 14.) Kwa hiyo, “nyakati saba,” au miaka saba ya mfalme huyo, ilikuwa siku 360 mara 7, au siku 2,520. Lakini vipi juu ya utimizo mkubwa wa ndoto yake? Zile “nyakati saba” za kiunabii zilikuwa ndefu kuliko siku 2,520. Hilo lilionyeshwa na maneno ya Yesu: “Yerusalemu litakanyagwa-kanyagwa na mataifa, hadi nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa ziwe zimetimizwa.” (Luka 21:24) ‘Kukanyaga-kanyaga’ huko kulianza mwaka wa 607 K.W.K. wakati ambapo Yerusalemu liliharibiwa nao ufananisho wa ufalme wa Mungu ukakoma kutenda katika Yuda. Kukanyaga-kanyaga huko kungekoma lini? Kungekoma “nyakati za kurudishwa kwa mambo yote,” wakati ambapo enzi kuu ya Mungu ingedhihirishwa tena kwenye dunia kupitia Yerusalemu la ufananisho, Ufalme wa Mungu.—Matendo 3:21.
27. Kwa nini ungesema kwamba zile “nyakati saba” ambazo zilianza mwaka wa 607 K.W.K. hazikuisha siku 2,520 halisi baadaye?
27 Ikiwa tungehesabu siku halisi 2,520 kuanzia kuharibiwa kwa Yerusalemu mwaka wa 607 K.W.K., tungefikia mwaka wa 600 K.W.K., mwaka usio na maana yoyote ya Kimaandiko. Hata mwaka wa 537 K.W.K., wakati ambapo Wayahudi waliowekwa huru walirudi Yuda, enzi kuu ya Yehova haikuwa duniani. Na hiyo ni kweli kwa kuwa Zerubabeli, mrithi wa kiti cha Daudi, hakufanywa mfalme bali liwali tu wa Yuda, mkoa wa Uajemi.
28. (a) Ni kanuni gani ambayo lazima itumiwe kuhusu zile siku 2,520 za zile “nyakati saba” za kiunabii? (b) “Nyakati saba” za kiunabii zilikuwa na urefu gani, nazo zilianza na kuisha tarehe gani?
28 Kwa kuwa zile “nyakati saba” ni za kiunabii, lazima tutumie kanuni ya Kimaandiko kwenye zile siku 2,520: “Siku moja kwa mwaka mmoja.” Kanuni hiyo yatumika kwenye hali ya Babiloni kuzingira Yerusalemu. (Ezekieli 4:6, 7; linganisha Hesabu 14:34.) Kwa hiyo, zile “nyakati saba” za serikali za wasio Wayahudi kutawala dunia bila kuingiliwa na Ufalme wa Mungu zilikuwa na urefu wa miaka 2,520. Zilianza wakati ambapo Yuda na Yerusalemu zilifanywa ukiwa katika mwezi wa saba unaofuata kuandama kwa mwezi (Tishri 15) mwaka wa 607 K.W.K. (2 Wafalme 25:8, 9, 25, 26) Kuanzia wakati huo hadi mwaka wa 1 K.W.K. ni miaka 606. Ile miaka iliyosalia 1,914 yaanza kutoka wakati huo hadi mwaka wa 1914 W.K. Kwa hiyo, “nyakati saba,” au miaka 2,520, ziliisha kufikia Tishri 15, au Oktoba 4/5, 1914 W.K.
29. “Mnyonge” ni nani, na Yehova alifanya nini ili kumtawaza?
29 Mwaka huo “nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa” zilitimia, na Mungu akampa utawala “mnyonge”—Yesu Kristo—ambaye adui zake walimwona kuwa mnyonge sana hivi kwamba wakafanya atundikwe mtini. (Danieli 4:17) Ili kumtawaza Mfalme wa Kimesiya, Yehova alifungua pingu ya mfano ya chuma na shaba iliyofunga “kisiki cha shina” cha enzi kuu yake mwenyewe. Mungu Aliye Juu akaruhusu “chipukizi” la kifalme likue kutokana nacho ukiwa udhihirisho wa enzi kuu ya kimungu kwenye dunia kupitia Ufalme wa kimbingu mikononi mwa Mrithi mkuu zaidi wa Daudi, Yesu Kristo. (Isaya 11:1, 2; Ayubu 14:7-9; Ezekieli 21:27) Twamshukuru Yehova kama nini kwa ajili ya matokeo mazuri ya matukio na kwa sababu ya kufumbua fumbo la ule mti mkubwa!
UMEFAHAMU NINI?
• Mti mkubwa wa ndoto ya Nebukadreza ulifananisha nini?
• Ni nini kilichompata Nebukadreza katika utimizo wa kwanza wa ndoto ya mti?
• Baada ya ndoto yake kutimizwa, Nebukadreza alikiri nini?
• Katika utimizo mkubwa wa ndoto ya mti ya kiunabii, “nyakati saba” zilikuwa na urefu gani, nazo zilianza na kuisha lini?
[Picha katika ukurasa wa 83]
[Picha katika ukurasa wa 91]