Kukabiliana na Mishiko ya Hofu ya Ghafula
Robert alikuwa ameketi akiwa amestarehe katika ofisi yake. Kwa ghafula moyo wake ukaanza kupiga upesi-upesi. Akaketi wima mara moja huku jasho likimtoka kwenye kipaji cha uso. Robert alikuwa na hakika kuwa alikuwa anapatwa na mshiko wa moyo! Akachukua simu aombe msaada. “Jambo baya linanipata,” alisema akivuta pumzi kwa nguvu. “Nahisi kana kwamba nitazimia!”
HIYO ilikuwa mara ya kwanza kwa Robert kushikwa na hofu ya ghafula. Kwa kuhuzunisha, haikuwa mara ya mwisho. Hisia iyo hiyo ilimpata baadaye kwenye mkahawa na madukani. Hiyo hofu ya ghafula ilimpata tena alipokuwa akitembelea marafiki. Upesi, mahali “salama” pekee kwa Robert palikuwa nyumbani. Hatua kwa hatua, akashuka moyo. “Hata nilikuwa nimefikiria kujiua,” akiri.
Miezi sita baadaye Robert akapata makala ya gazeti juu ya mishiko ya hofu ya ghafula na hofu ya hofu (agoraphobia). Aliyojifunza yaliokoa uhai wake.
Mbona Uhofu Ghafula?
Hofu ya ghafula ni itikio la kawaida la mwili ukabilipo hatari. Jiwazie ukivuka barabara kuu. Kwa ghafula unaona gari likija mbio kukuelekea. Mabadiliko ya papo hapo ya kimwili na kikemikali mwilini mwako hukuwezesha kukimbilia usalama.
Lakini sasa wazia hisia iyo hiyo ya hofu ya ghafula bila sababu yoyote ya wazi. Dakt. R. Reid Wilson asema: “Mishiko ya hofu ya ghafula hutokea wakati hofu ya ghafula iudanganyapo ubongo ufikiri kuna hatari inayokaribia. Wazia kuwa umesimama kwenye kijia cha duka kubwa, bila kusumbua mtu yeyote. Flip. Swichi ya dharura yawaka. ‘Kaa chonjo! Mifumo yote ya mwili iwe tayari kwa vita!’”
Ni wale tu ambao wamepatwa na mishiko kama hiyo wawezao kuelewa uzito wayo. Gazeti American Health hufasili woga huo kuwa “kusukasuka kwa adrenalini ambako huuhofisha mwili kwa dakika tano au saa moja au siku moja na kisha kuondoka upesi kama tu vile kulivyoanza bila kueleweka, ikikuacha ukiwa umedhoofika na kuchoshwa huku ukihofu shambulio litakalofuata.”
Chanzo cha Hofu ya Ghafula
Mishiko ya hofu ya ghafula mara nyingi huanza mtu aanzapo kuwa mtu mzima nayo huathiri wanawake zaidi ya wanaume. Ni nini huyasababisha? Hakuna jibu lililo wazi. Watu fulani husema kuwa wanaokumbwa nayo wana mwelekeo huo kibiolojia kwa sababu ya kasoro katika mfumo wa hisia na uchochezi wa ubongo. Watu wengi huhisi kuwa hali hiyo yaweza kurithiwa, na wengine hudai kwamba kemikali za ubongo hubadilishwa na mambo yachocheayo mkazo.
Katika visa fulani mishiko huchochewa na kumbukumbu za mambo yenye kufadhaisha waliyojionea, kama vile vita, kulalwa kinguvu, au kutendwa vibaya wakiwa watoto. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba wahasiriwa wa ngono ya maharimu waliokuwa na tatizo la hofu ya ghafula walikuwa asilimia 13 zaidi ya wale ambao hawakuwa wahasiriwa wa ngono ya maharimu. Kwa kweli, ingawa mishiko ya hofu ya ghafula na magonjwa mengineyo ni matatizo kivyao, yaweza pia kuwa kile mwandikaji E. Sue Blume hukiita “ngono ya maharimu ikiwa habu ya njukuti.”
Bila shaka, si mishiko yote ya hofu ya ghafula ichochewayo na madhara. Lakini Dakt. Wayne Kritsberg atahadharisha kwamba iwapo hivyo “kutibu mishiko ya hofu ya ghafula—badala ya kutibu madhara ya awali—hakutasuluhisha hilo tatizo kabisa. Ni kama kutumia dawa ya homa kutibu kichomi.”
Je, Yaweza Kuponywa?
Mishiko ya hofu ya ghafula yaweza kudhibitiwa. Wengi ambao kuhofu kwao hofu ya ghafula huwafanya wakae nyumbani wamesaidiwa na matibabu ya kukabili hali waliyohofu. Katika matibabu hayo mgonjwa huwekwa katika hali anayohofu naye husaidiwa kubaki hapo hadi hofu yake ya ghafula iishe. Walio na matatizo ya moyo, ugonjwa wa pumu, vidonda vya tumbo, mchochota wa colon, na magonjwa mengine kama hayo wapaswa wamwone daktari kabla ya kujaribu matibabu hayo.
Njia mbalimbali za kupumzika zaweza kutumiwa ili kupunguza ongezeko la mahangaiko.a Baadhi yazo zimezungumziwa katika kisanduku kinachoandamana na makala hii “Stadi za Kutuliza.” Lakini usisubiri upatwe na hofu ya ghafula. Mtu aweza kujizoeza stadi hizo kwa matokeo zaidi wakati hana mahangaiko mengi. Zikishazoewa, zaweza kupunguza au hata kuzuia mishiko ya wakati ujao.
Hofu ya ghafula husitawi mtu atazamiapo sana ukamilifu na akosapo kujistahi. “Nilipokuwa nikishambuliwa na mahangaiko, Bw. Hisia Hasi alitawala maisha yangu,” asema mhasiriwa mmoja. “Niliwaza kwamba kwa kuwa nilikuwa na mahangaiko, nilikuwa wa hali ya chini kwa kulinganishwa na wengine na hivyo asiyependeka.” Kubadili mitazamo kama hiyo kwaweza kupunguza mahangaiko yatokezayo hofu ya ghafula.b
Kuna faida kubwa katika kumwambia rafiki umtumainiye mahangaiko yako. Kuzungumza juu yayo kwaweza kusaidia mhasiriwa atofautishe matatizo ambayo lazima yavumiliwe na yale yawezayo kusuluhishwa. Lisilopaswa kupuuzwa ni sala. Zaburi 55:22 husema: “Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza. Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.”
Badala ya tatizo moja kubwa, mara nyingi ni mrundamano wa ionekanayo kuwa mishuko moyo midogo-midogo usababishao hofu ya ghafula—sawa tu na vile kutumia vyombo vingi sana vya stima katika soketi ileile kuwezavyo kuunguza fyuzi. Suluhisho moja ni kuandika kila tatizo katika kadi zilizopangwa kialfabeti na uzipange kuanzia tatizo rahisi kabisa hadi lile gumu kabisa. Uyashughulikie moja baada ya jingine. Kuandika mifadhaiko yako hubadili hali yayo kutoka hali ya kuogofya hadi kuwa jambo uwezalo kukabili na kusuluhisha.
Wengine husaidiwa kwa kutumia dawa za kutuliza au za kuzuia mshuko wa moyo walizopendekezewa na daktari. Hata hivyo, kutahadhari kwafaa. “Siamini kwamba dawa pekee ndiyo suluhisho,” asema mshauri Melvin Green. “Yapaswa kutumiwa kama kibadala huku njia za kusuluhisha tatizo zikitafutwa. . . . Huenda dawa zikakuruhusu kufanya mambo ya kawaida ya maisha, na hiyo yaweza kukupa fursa ya kutafuta msaada wa kushughulika na visababishi vya hofu ya hofu na kufanyia kazi kupona kwako.”
Tatizo la Kiroho?
“Nilidhani kwamba Wakristo hawakupaswa kupatwa na mahangaiko,” asema Brenda, “kwa kuwa Yesu alisema ‘usisumbuke.’ Nilifikia mkataa kwamba sikuwa nikimtegemea Mungu vya kutosha.” Lakini muktadha wa maneno ya Yesu katika Mathayo 6:34 huonyesha kwamba hakuwa akizungumza juu ya kasoro za hofu ya ghafula. Badala ya hivyo alikuwa akikazia hatari ya kuhangaikia sana mahitaji ya kimwili kuliko yale ya kiroho.
Kwelikweli, hata wale watangulizao mahitaji ya kiroho waweza kupatwa na kasoro hii, kama vile jambo lililoonwa la mwanamke mmoja kutoka Finland lionyeshavyo.
“Mwenzangu nami, sote tukiwa Mashahidi wa Yehova, tulikuwa katika kazi ya kuhubiri mlango hadi mlango. Ghafula, nikaanza kuhisi kizunguzungu. Mawazo yangu yakazuiwa. Hakuna kitu chochote kilichoonekana kuwa halisi, na niliogopa kuwa ningeanguka. Katika mlango uliofuata, sikuweza kabisa kufuata mazungumzo.
“Jambo hilo la kuogofya lilitukia 1970. Lilikuwa la kwanza katika mfululizo wa vipindi vya mkazo wa akili na mwili ambao ulinisumbua kwa miongo miwili iliyofuata. Kwa kurudiarudia, nilijikuta nikiwa nimetatanika, nisiweze kufikiri vizuri. Nilipatwa na kizunguzungu, nao moyo wangu ulipiga kwa nguvu. Nilikatizakatiza maneno yangu au hata kuyasahau.
“Nilikuwa mchanga, mwenye nguvu, na mhudumu wa wakati wote mwenye furaha wa Mashahidi wa Yehova. Jinsi nilivyopenda kuwasaidia wengine kuifahamu Biblia! Lakini mishiko hiyo ilikuwa mateso ya kudumu kwangu. Nilijiuliza, ‘Nina kasoro gani?’ Daktari wa neva alichunguza hali yangu na kusema kwamba ilikuwa kifafa-hafifu. Kwa miaka kumi iliyofuata, nilitumia dawa alizopendekeza. Na bado, nilijiuliza ni kwa nini hazikuwa na matokeo. Nilikuja kukubali hali yangu kuwa kitu ambacho nililazimika kuvumilia tu.
“Baada ya muda nikatambua kuwa ugonjwa wangu haukuwa kifafa, na dawa nilizotumia hazikuwa zikifanya kazi. Hata kutembea sehemu nilizojua kulikuwa vigumu sana. Nilihofu sana kukutana na mtu yeyote njiani. Nilitumia nguvu zangu zote kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Mara nyingi niliketi nikitokwa jasho na nikiwa na kizunguzungu mikono yangu ikiwa kwenye kipaji cha uso wangu, moyo wangu ukipiga kwa nguvu, na akili yangu ikiwa tupu. Nyakati fulani mwili wangu wote ulikuwa umekazika na misuli ikiwa imepindana. Wakati mmoja nilikuwa na hakika kuwa ningekufa.
“Huduma yangu ilisaidia kunitegemeza, ingawa ulikuwa muujiza kwelikweli kwamba niliweza kuendelea. Kuongoza funzo la Biblia nyakati nyingine kulinishinda kabisa hivi kwamba mwandamani wangu alilazimika kuliongoza. Kwa kweli, kuhubiri kwetu ni jitihada za timu, na mwishowe ni Mungu akuzaye. (1 Wakorintho 3:6, 7) Wenye mfano wa kondoo husikia na kuitikia licha ya mapungukio ya mwalimu.
“Siku moja katika Machi 1991, mume wangu alinionyesha kijitabu juu ya kasoro ya hofu ya ghafula. Dalili zilizoelezwa zilikuwa tu kama zangu! Nilisoma mengi zaidi juu ya hiyo habari, nikahudhuria mihadhara, na kupanga kumwona daktari. Baada ya miongo miwili, tatizo langu hatimaye lilitambuliwa. Nilikuwa nikielekea kupona!
“Wengi wa wale wenye kasoro ya hofu ya ghafula waweza kusaidiwa kwa kupata matibabu yafaayo. Marafiki waweza kuwa utegemezo mkubwa wakiwa wenye hisia-mwenzi. Badala ya kumfanya mhasiriwa ahisi kuwa na hatia kwa sababu ya kutoshirikiana na wengine, mwandamani mwenye utambuzi atatambua kuwa mtu aliye na hofu ya ghafula hakatai kushirikiana na wengine kwa kupenda kwake.—Linganisha 1 Wathesalonike 5:14.
“Nifikiriapo miaka 20 ambayo imepita, nashukuru kwamba wakati wa miaka hiyo yote nimeweza kubaki katika huduma ya wakati wote. Imekuwa baraka istahiliyo kupiganiwa. Wakati huohuo, natambua kwamba, kama Epafrodito, wengine lazima waache mapendeleo ya utumishi kwa sababu ya afya mbaya. Yehova hatamaushwi na watu kama hao. Hatarajii mengi zaidi kuliko awezayo kutoa mtu.
“Kuishi na kasoro hii kumenifundisha kutojichukua kwa uzito sana. Kumeniwezesha kuwa na hisia-mwenzi kwa wengine waliopungukiwa. Lakini zaidi ya yote, kumenisaidia kumkaribia Yehova. Wakati wote wa masaibu yangu nimeendelea kumwona kuwa chanzo cha kweli cha nguvu na faraja.”
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari juu ya kubadili mawazo hasi, ona Amkeni!, Oktoba 8, 1992, kurasa 3-9, na Oktoba 8, 1988, kurasa 7-16.
b Wakristo huepuka njia zinazotia ndani uzugaji au kujizuga. Hata hivyo, kuna mazoezi ya macho na ya kutafakari ambayo kwa wazi hayahusishi kuondoa kila kitu katika akili au kuiacha iongozwe na mtu mwingine. Kukubali au kukataa matibabu hayo ni uamuzi wa kibinafsi.—Wagalatia 6:5.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Stadi za Kutuliza
Kupumua kwa utulivu. Mishiko ya hofu ya ghafula kwa kawaida hufuatwa na kupumua sana isivyo kawaida. Ili kutuliza kupumua kwako, jaribu zoezi hili: Lala kifudifudi. Hesabu moja hadi sita uvutapo pumzi; hesabu moja hadi sita utoapo pumzi. Kisha, jaribu kupumua kwa kina vivyo hivyo uketipo chini. Halafu, jaribu hilo ukiwa umesimama. Pumua kwa kina kutoka kwenye kiwambo, na ujizoeze hilo kila siku hata iwe kawaida. Watu wengine hufaidika kwa kuwazia mazingira yenye kupendeza wafanyapo zoezi hilo.
Kufikiri kwa utulivu. ‘Namna gani nikizimia?’ ‘Namna gani ikiwa hakuna mtu wa kunisaidia?’ ‘Namna gani moyo wangu ukiacha kupiga?’ Mawazo mabaya huchochea hofu ya ghafula. Kwa kuwa mawazo hayo kwa kawaida huwa ya misiba ya wakati ujao au mishiko ya wakati uliopita, jaribu kukazia fikira hali ya wakati uliopo. “Kukazia fikira wakati uliopo hutuliza mara moja,” asema Dakt. Alan Goldstein. Wengine hudokeza uvae mpira kiwikoni. Mawazo mabaya yatokeapo, uvute mpira na kuuachilia na ujiambie: “Acha!” Katiza mahangaiko kabla hayajapata fursa ya kugeuka na kuwa hofu ya ghafula.
Maitikio matulivu. Hofu ya ghafula ikikupata, usishindane nayo. Ni hisia tu, na hisia hazipaswi kukudhuru. Wazia kwamba uko katika bahari-kuu ukitazama mawimbi. Yainuka, na kufikia kilele, na kisha kupotea. Hofu ya ghafula hutokea kwa njia iyo hiyo. Badala ya kushindana na hilo wimbi, safiri pamoja nalo. Hisia hiyo itapita. Iishapo, usiirejelee au kuichanganua kupita kiasi. Imepita, kama vile kupiga chafya au kuumwa kichwa.
Hofu ya ghafula ni kama mchokozi. Mkasirishe, naye atakushambulia; usimkasirishe, naye aweza kuondoka. Dakt. R. Reid Wilson aeleza kwamba stadi za kutuliza “hazijafanyizwa ili uweze ‘kushindana’ vizuri zaidi na hofu ya ghafula au ‘kuiondolea mbali’ wakati huo. Badala ya hilo, zione kuwa njia za kupitisha wakati huku hofu ya ghafula ijaribupo kukuchokoza.”
[Sanduku katika ukurasa wa23]
Hofu ya Hofu
Wengi ambao hupatwa na hofu ya ghafula hukuza hofu ya hofu. Ingawa imefasiliwa kuwa hofu ya kuwa sehemu za hadharani, hiyo kwa kweli ni hofu ya hofu. Wenye hofu ya hofu huhofu sana hofu ya ghafula hivi kwamba wao huepuka sehemu zote ambapo hofu ya ghafula iliwapata. Upesi, ni mahali pamoja tu pabakio “salama”—kwa kawaida nyumbani.
“Wazia kuwa unatoka katika nyumba yako,” asema mwandikaji Melvin Green. “Kwa ghafula, atokea mtu ambaye hujui alikotoka, aonekana kuwa mtu mkubwa zaidi ambaye umepata kuona. Ana kibao cha besiboli na, bila sababu yoyote, akugonga kichwani. Unajikokota kurudi nyumbani, ukiwa umeshangazwa na yaliyotoka kutokea. Uhisipo afadhali, unachungulia mlangoni na mambo yote yaonekana kuwa shwari. Waanza tena kuelekea hicho kijia. Kwa ghafula yupo pale, na kwa mara ya pili anakugonga. Unarudi nyumbani ambapo u salama. Unatazama kupitia mlango wa nyuma . . . Yuko huko. Unatazama kupitia madirisha . . . Yuko huko. Unajua kwamba ukiondoka kwenye usalama wa nyumba yako, utagongwa tena. Swali ni: Je, ungeondoka?”
Wengi wenye hofu ya hofu hufananisha hisia zao na kielezi hicho nao huhisi kwamba hali yao haina tumaini. Lakini Dakt. Alan Goldstein atoa uhakikisho huu: “Ninyi si tofauti, si ninyi peke yenu. . . . Mwaweza kujisaidia.”