Wenye Muungamano Chini ya Beramu ya Upendo
Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana.—1 PETRO 4:8.
1. Tunaona upendo wa aina gani miongoni mwa watu wa Mungu leo, na Wakristo wapakwa-mafuta wamekuwa wakipiga mbiu ya jambo gani tangu 1922?
JE! SISI tunaona upendo wa aina hiyo miongoni mwa watu wa Mungu leo? Kwa uhakika tunaona! Huo ni upendo unaotegemea hasa kutambua na kuunga mkono enzi kuu ya Yehova, sawa na vile Daudi alivyoiunga mkono. Hasa ni tangu mwaka 1922 kwamba, ndugu wapakwa-mafuta wa Yesu Kristo, “Mwana wa Daudi,” wamekuwa wakipiga mbiu duniani pote ya kuwa Ufalme wa Mungu u karibu na kwamba watetezi wa utawala mwonevu wa Shetani wanakabiliana na hatua ya kuuawa na Hakimu mwekwa-rasmi wa Mungu, Yesu Kristo.—Mathayo 21:15, 42-44; Ufunuo 19:11, 19-21.
2. Kwa nini Daudi angeweza kuitwa ‘mtu aupendezaye moyo wa Yehova’?
2 Daudi alikuwa ‘mtu aupendezaye moyo wa Yehova.’ Hiyo ilionekana katika upendo wake kwa Yehova na uadilifu Wake—hivyo vikiwa ni vitabia ambavyo hata Mfalme Sauli mwoga-mwoga alikiri vilikuwa katika Daudi—ndiyo, katika sifa yake ya kutokuwa na hofu, ya kufuata Yehova kwa bidii ya moyo mzima, ya uongozi, na ya kujitiisha kwenye utaratibu wa kitheokrasi kwa unyenyekevu. —1 Samweli 13:14; 16:7, 11-13; 17:33-36; 24:9, 10, 17.
3. Mwelekeo wa Yonathani ulikuwa nini kuhusu Daudi, na kwa nini?
3 Baada ya shangwe yake ya kumshinda Goliathi, Daudi alirudi kumpa ripoti Sauli. Hapo ndipo mpenzi mwingine wa uadilifu alipojitokeza mbele. Huyo alikuwa Yonathani, mwana mkubwa zaidi wa Mfalme Sauli. “Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho [nafsi, NW] ya Yonathani, ikaambatana na roho [nafsi, NW] ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho [nafsi, NW] yake mwenyewe.” (1 Samweli 18:1) Kilichovutia Yonathani ampende Daudi kwa hisia za moyoni kilikuwa bidii yake yenye kuwaka moto ili aondolee jina la Mungu suto, kutokuwa kwake na ubinafsi, na utegemeo wake kamili juu ya Yehova, wala si uhodari wa kimnofu wala umahiri wake wa kutumia kombeo.—Linganisha Zaburi 8:1, 9; 9:1, 2.
4. Yonathani alifanya nini kwa kutambua kwamba Daudi ndiye aliyepakwa mafuta kuwa mfalme?
4 Ingawa Yonathani alimzidi Daudi umri kwa miaka kama 30, yeye aliungamana na kijana huyu shujaa wa vita katika kifungo cha urafiki wa daima. “Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake.” (1 Samweli 18:3, 4) Lo, Yonathani alionyesha utambuzi wenye kutokeza wazi kama nini! Yonathani angalikuwa ndiye mrithi wa Sauli kama ilivyo kawaida. Hata hivyo yeye alionyesha Daudi upendo mchangamfu wenye kuongozwa na kanuni, akajitiisha kwake kwa kuwa ndiye aliyepakwa mafuta kuwa mfalme, aliyekaza nia kuliko wengine wote ili ategemeze jina na enzi kuu ya Yehova.—2 Samweli 7:18-24; 1 Mambo ya Nyakati 29:10-13.
5. Yonathani alitambua nini wakati vita ya kitheokrasi ilipohusika?
5 Yonathani mwenyewe alikuwa pia mpigania uadilifu. Yeye alikuwa ametangaza kwamba “hakuna la kumzuia Bwana [Yehova, NW] asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache.” Kwa nini? Kwa sababu Yonathani alitambua kwamba siku-zote kuna uhitaji wa kutafuta mwongozo wa kimungu ili kupata ushindi katika vita ya kitheokrasi. Yonathani alipotenda kosa bila kujua na Sauli akamhukumia kufa kwa sababu hiyo, yeye alikubali hukumu hiyo kwa unyenyekevu. La kufurahisha ni kwamba, watu walimkomboa.—1 Samweli 14:6, 9, 10, 24, 27, 43-45.
Kuonyesha Upendo Mshikamanifu
6. Upendo mshikamanifu wa Yonathani uliokoaje Daudi?
6 Sauli akaona wivu juu ya sifa kubwa ya Daudi kwamba ni shujaa wa vita, naye akatafuta kumwua, lakini upendo mshikamanifu wa Yonathani ukamwokoa! Usimulizi unasomwa hivi: “Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha.” Katika pindi hiyo, Yonathani alimtuliza Sauli, basi Daudi akaachiliwa. Lakini mafanikio zaidi ya Daudi katika ‘kupigana na Wafilisti na kuwaua kwa uuaji mkuu’ yaliamsha tena uhasama wa Sauli. Hapo tena akapiga moyo konde kumwua Daudi, basi Daudi akakimbia.—1 Samweli 19:2-10.
7. Yonathani alipokutana na Daudi mtoro, wao waliambiana nini kwa kuimarisha tena agano fulani?
7 Baada ya muda, Daudi mtoro alikutana tena na Yonathani, aliyetangaza hivi: “Kadiri roho yako itakavyo, nitakutendea.” Hao wawili wakaimarisha tena agano mbele za Yehova, na Daudi akaahidi kwamba hangekatiza kamwe fadhili-upendo kutoka kwa watu wa nyumba ya Yonathani—hiyo ikiwa ni ahadi aliyoitimiza kwa uaminifu. “Naye Yonathani akamwapisha Daudi mara ya pili, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake; kwa maana alimpenda kama alivyoipenda roho [nafsi, NW] yake mwenyewe.”—1 Samweli 20:4-17; 2 Samweli 21:7.
8. Kwa nini Yonathani na Daudi walikutana kwa siri katika uwanja, na ni jambo gani lililotukia katika pindi hiyo?
8 Mfalme Sauli alishikilia sana azimio lake la kumuua Daudi. Kwani, Sauli hata alivurumisha mkuki kuelekea Yonathani mwana wake mwenyewe wakati huyo alipotoa sauti ya kumtetea Daudi! Kwa hiyo Yonathani akakutana na Daudi kwa siri katika uwanja fulani. “Daudi . . . akaanguka kifudifudi, akajiinama mara tatu; nao wakabusiana, wakaliliana, hata Daudi akazidi. Naye Yonathani akamwambia Daudi, Enenda kwa amani; kwa maana sisi sote wawili tumeapiana kwa jina la Bwana [Yehova, NW] ya kwamba, Bwana [Yehova, NW] atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele.” Kwa hiyo wakaachana, na Daudi akawa mtoro katika nyika ya Sifu.—1 Samweli 20:41, 42.
9, 10. (a) Ni jinsi gani Yonathani alivyomtia Daudi moyo kwenye ule ambao labda ulikuwa ndio mkutano wa mwisho kati yao wawili? (b) Yonathani na Sauli walipochinjwa na Wafilisti, Daudi alitunga wimbo gani wa maombolezo, na aliufikishaje kwenye upeo?
9 Kwa upendo, Yonathani aliendelea kumtia moyo Daudi. Kama vile maandishi yanavyotaarifu: “Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka, akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. Na hao wawili wakafanya agano mbele za Bwana [Yehova, NW].”—1 Samweli 23:15-18.
10 Inaonekana kwamba huo ulikuwa ndio mkutano wa mwisho kati ya Daudi na mwandamani wake mshikamanifu, Yonathani. Baadaye, wote wawili Yonathani na Sauli walipochinjwa katika vita pamoja na Wafilisti, Daudi alitunga wimbo wa maombolezo, “Ule Upinde.” (NW) Katika huo alionyesha staha kwa Sauli kuwa mpakwa-mafuta wa Yehova lakini akafikisha wimbo wake kwenye upeo kwa maneno haya: “Ee Yonathani, wewe umeuawa juu ya mahali pako palipoinuka! Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, ulikuwa ukinipendeza sana; upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, kupita upendo wa wanawake [unaotoka kwa wanawake, NW]. Jinsi mashujaa walivyoanguka, na silaha za vita zilivyoangamia!” (2 Samweli 1:18, 21, 25-27) Ndipo Daudi akapakwa mafuta mara ya pili, kuwa mfalme juu ya Yuda.
Ulinganifu Mbalimbali wa Ki-Siku-Hizi
11, 12. (a) Daudi na Yonathani waliweka kielelezo cha upendo wa aina gani? (b) Ule upendo wa juhudi nyingi sana kati ya Daudi na Yonathani ulitangulia kuwa kivuli cha jambo gani?
11 Kwa kuwa “andiko lote limevuviwa na Mungu na ni lenye manufaa kwa kufundisha,” tunajifunza nini kutokana na usimulizi unaohusu Daudi na Yonathani? (2 Timotheo 3:16, NW) Tunaona kwamba kuna upendo fulani ‘ulio wa ajabu kupita upendo unaotoka kwa wanawake.’ Ni kweli, ‘upendo unaotoka kwa wanawake’ unaweza kufurahisha na kuridhisha wakati sheria za Yehova kuhusu ndoa zinapoheshimiwa. (Mathayo 19:6, 9; Waebrania 13:4) Lakini Daudi na Yonathani waliweka kielelezo cha upande bora zaidi wa upendo, kupatana na amri hii: “Sikiliza, O Israeli: Yehova Mungu wetu ni Yehova mmoja. Na wewe lazima upende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na nafsi yako yote na nguvu zote za uhai ulizo nazo.”—Kumbukumbu 6:4, 5, NW.
12 Daudi na Yonathani walikuwa na muungamano katika kuonyesha upendo huo walipokuwa wakipigania kuondolea jina la Yehova suto lote ambalo adui Zake walitupa juu yalo. Kwa kufanya hivyo, pia walisitawisha kuwa na juhudi nyingi katika kupendana.’ (1 Petro 4:8) Uandamani waliofurahia katika jambo hilo hata ulizidi ile amri iliyo kwenye Walawi 19:18, NW: “Lazima upende mwenzako kama wewe mwenyewe.” Kweli kweli, uandamani huo ulitangulia kuwa kivuli cha upendo wa aina iliyoonyeshwa katika ‘amri mpya ya Yesu kwamba, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.’ Upendo wa Yesu ulikuwa wa kujidhabihu mwenyewe si kwa kujitiisha kikamili tu kwenye penzi la Yehova, bali pia kwa nia yake ya hata ‘kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.’—Yohana 13:34; 15:13.
“Kundi” Moja Lenye Muungamano
13. Ni kikundi gani cha wapiga mbiu ya Ufalme ambacho kimetokea kuanzia 1935 hasa, na Wakristo wapakwa-mafuta wana muungamano gani pamoja nao?
13 Wakristo wapakwa-mafuta wa “kundi dogo” ndio wanaohimili uzito mwingi zaidi wa vita katika kushindana na Goliathi wa ki-siku-hizi. Hata hivyo, tangu 1935 wameungwa na wapiga mbiu ya Ufalme walio wa “zizi” jingine, tena lililo kubwa zaidi. Hao “kondoo wengine” wamekuwa na muungamano pamoja na “kondoo” wapakwa-mafuta waliobaki na kuwa “kundi moja” chini ya “mchungaji mmoja,” “Mwana wa Daudi,” wakiwa katika kifungo cha muungamano wenye upendo, kilicho bora kuliko vyote—kama kile kilichokuwa kati ya Yonathani na Daudi.—Luka 12:32; Yohana 10:16; Ezekieli 37:24.
14. Ni jambo gani lililokuwa ulinganifu wa majaribio ya Sauli kumuua Daudi, na upendo wa Yonathani wa kujitambulisha kuwa mwenye uhusiano na Daudi?
14 Wakati ule ule kikundi hicho cha Yonathani kilipokuwa kikianza kuzidika kuwa umati mkubwa, Vita ya Ulimwengu 2 ilifoka, hivi kwamba wapakwa-mafuta na waandamani wao wakatahiniwa vikali Hiyo ilikuwa miaka ya mnyanyaso mbaya sana, ambao mara nyingi ulichochewa na makasisi. Hiyo ililingana na majaribio ya Sauli kumchinja Daudi mpakwa-mafuta na, baadaye, Yonathani wakati ambapo huyu wa pili alijitambulisha kwa upendo kuwa pamoja na Daudi. Jamii za Daudi na Yonathani zilionyeshana upendo wa juhudi nyingi kama nini katika kipindi hicho! Mara nyingi kielezi cha Yesu kwenye Mathayo 25:35-40 kilikuwa na utimizo halisi.a
15. (a) Ni mwendo gani uliofuatwa na Mashahidi ambao unatofautiana na ule uliofuatwa na jamii ya Sauli wa ki-siku-hizi? (b) Katika siku yetu ni nini huenda kikalingana na ile “roho mbaya kutoka kwa Bwana [Yehova, 7VW]” iliyoogofya-ogofya Mfalme Sauli?
15 Lo, kushika ukamilifu kwa Mashahidi wa Yehova kunatofautiana kama nini na mwendo wa jamii ya Sauli wa ki-siku-hizi! Mashahidi, ambao “si sehemu ya ulimwengu,” wametii amri ya Yesu ‘kupendana’ katika tufe lote. (Yohana 15:17-19) Kwa upande ule mwingine, katika vile vita vya ulimwengu viwili makasisi wa Jumuiya ya Ukristo wa pande zote mbili walisali kwa “mungu” wao kuomba ushindi, huku mamilioni ya askari wakichinjwa na wanadini wenzao wa mataifa mengine. Ile “roho mbaya kutoka kwa Bwana [Yehova, NW]” ambayo iliogofya-ogofya Sauli ingeweza kulingana vizuri na linalotokea wakati wale malaika wanapomwaga tauni za Ufunuo sura ya 8. Kuna ithibati ya kwamba makasisi wa Jumuiya ya Wakristo hawana roho takatifu ya Yehova. —1 Samweli 16:14; 18:10-12; 19:10; 20:32-34.
16. (a) Makasisi walitumiaje vita vya ulimwengu viwili kuonea watu wa Mungu? (b) Katika miaka ya majuzi, kwa nini inaweza kusemwa kwamba Sauli wa ki-siku-hizi amedumu katika kuwinda watu wa Mungu?
16 Katika 1918 makasisi walitumia mgogoro wa vita kubembeleza mamlaka za kisiasa katika United States zichukue hatua dhidi ya maofisa wenye madaraka wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi na mwishowe zikawafunga gerezani. (Baadaye hao wanafunzi wa Biblia waliondolewa kabisa mashtaka yao.) Wakati wa vita ya ulimwengu ya pili, Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku katika milki ya serikali za Mataifa-Mhimili na katika nchi zilizo nyingi za Jumuiya ya Madola ya Uingereza, mara nyingi hiyo ikitokana na fitina ya dini. Mathalani, angalia nakala asilia ya barua iliyo juu ambayo Askofu Mkuu wa Sydney (aliyekuwa kardinali baadaye) aliiandika kabla tu ya Mashahidi wa Yehova kupigwa marufuku katika Australia. Utetezi ulipofanywa katika Mahakama Kuu ya Australia kupinga marufuku katika nchi hiyo, hakimu mwenye kuchunguza kesi, Bw. Justice Starke, aliieleza kuwa “isiyofuata kanuni, yenye ugeugeu na uonevu.” Marufuku hiyo iliondolewa siku ya Juni 14, 1943, na serikali ikafanyiwa makadirio ya hasara ilizosababisha. Katika miaka ya hivi majuzi, fitina ambayo dini imetilia serikali kadhaa katika Afrika na Esia imefanya Mashahidi wa Yehova waonewe bila huruma. Hivyo Sauli wa ki-siku-hizi—makasisi wa Jumuiya ya Wakristo—amedumu katika kuwinda watu wa Mungu.
17. (a) Mashahidi wa Yehova wamekabilianaje na mibano ya kisiasa na kidini inayoendelea kuwapata? (b) Ni nini kinachoonyeshwa na hali ya ulimwenguni pote ya muungamaniko wa Mashahidi?
17 Katika miaka ya 1980, Mashahidi wa Yehova wamekabilianaje na mibano ya kisiasa na kidini inayoendelea kuwapata? Ni kwa jinsi ile ile tu ambayo Daudi alikabiliana na Goliathi, na jinsi Daudi na Yonathani walivyokabiliana na Mfalme Sauli! Wao hawana hofu na wamepiga moyo konde kushika ukamilifu kuhusiana na lile suala la enzi kuu, kwa maana wanajua kwamba Ufalme wa Mungu utapata shangwe ya ushindi. (Danieli 2:44) Wanapokabiliwa na mnyanyaso, wao wanajitokeza mbele kwa muungamano, wakitiana moyo katika kifungo cha kimataifa cha upendo ambao ulimwengu haujapata kuuona. Kwa kuwa wasiokuwamo wakati wa vita, wao hawamwagi damu ya waitikadi wenzao katika mataifa mengine. (Mika 4:3, 5) Hivyo wanaonyesha kwamba wao ndicho kikundi kile ambacho Yesu alirejezea aliposema hivi: “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:35) Wakiwa udugu wa tufe lote, Mashahidi wa Yehova ‘wamejivika upendo, ulio kifungo cha ukamilifu,’ kifungo kinachopita sana vipingamizi vyote vya rangi ya ngozi, vya kikabila na kitaifa.—Wakolosai 3:14.
Kuonyesha ‘Juhudi ya Kupendana’
18. (a) Kuna ulinganifu gani leo katika upendo wa Yonathani kwa Daudi, na ithibati ya jambo hilo inaonyeshwaje? (b) Msimamo wa jamii ya Daudi umetokeza nini ulimwenguni pote?
18 Kumbuka kwamba ‘nafsi ya Yonathani iliambatana na nafsi ya Daudi, na Yonathani akampenda kama nafsi yake mwenyewe.’ Katika hizi “siku za mwisho” kumekuwa na ulinganifu mzuri ajabu wa jambo hilo! (2 Timotheo 3:1, 14) Katika muda wote ule wa kuwako msukosuko wa kijinga katika kipindi hiki chenye jeuri, kumekuwa na kikundi kimoja, Mashahidi wa Yehova, ambacho kimedumisha muungamano wenye upendo katika tufe lote. Wakiwa ni Wakristo wasiokuwamo, wao wameheshimu Muumba wao kuwa Bwana Mwenye Enzi Kuu wa aina ya binadamu yote. (Zaburi 100:3) Oh, Warefaimu wa ki-siku-hizi—wanasiasa wenye ujamaa mmoja na “Goliathi”—huenda wakaendelea kudhihaki vikali Israeli wa kiroho. (2 Samweli 21:21, 22) Naye Sauli wa ki-siku-hizi—makasisi wa Jumuiya ya Wakristo—huenda akaendelea kufanyiza matata kwa jamii za Daudi na Yonathani. (1 Samweli 20:32, 33) Lakini “vita ni vya Bwana [Yehova, NW].” Akiwa ndiye Bwana Mwenye Enzi Kuu, yeye atapatia watumishi wake washikamanifu ushindi wa mwisho. Kwa kuona msimamo ambao jamii ya Daudi inashikilia bila kuuacha, mamilioni ya watu—katika mabara yote—walio wa kikundi cha Yonathani, hata kutia na waliokuwa wanyanyasi hapo kwanza, wamejiunga nao chini ya ‘beramu ya upendo’ ya Kristo.b—1 Samweli 17:47; Wimbo wa Sulemani 2:4.
19, 20. (a) Ni nini baadhi ya mambo makuu ya utendaji wa Mashahidi kama unavyoonyeshwa na orodha katika kurasa 4-7? (b) Ukuzi wa Mashahidi katika mwongo wa 1979-88 ulikuwa wa kadiri gani? (c) Kwa nini inaweza kusemwa kwamba kwa kweli Mashahidi wana muungamano ulimwenguni pote, na kwa hiyo ni swali gani linalotokea?
19 Unaweza kuupitia utendaji unaopanuka wa mamilioni hayo ya Mashahidi kwa kutazama orodha iliyo katika kurasa 4-7 za gazeti hili. Katika mwongo wa 1979-88, hesabu ya wahubiri wa habari njema za Ufalme wa Mungu uliosimamishwa imeongezeka kutoka 2,186,075 ikawa 3,592,654, huo ukiwa ni ukuzi wa asilimia 64.3. Ulimwenguni pote, hao ni watu ambao wameungamana kikweli katika kushiriki itikadi moja ya ujumla, katika kumpa Mungu utumishi mmoja wa ujumla, na bidii moja ya kufuata kanuni za maadili ya Biblia bila ugeugeu. Ni kuhusu kikundi hicho cha kimataifa kilichoshikamana kwa ukaribu kwamba maneno ya Yesu yanatumika leo: “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.”—Yohana 15:10; linganisha 1 Wakorintho 1:10.
20 Ingawa wao wanahubiri katika ndimi tofauti-tofauti zaidi ya 200, mashahidi hao wa Yehova wananena “lugha yenye utakato” iliyo ya ukweli wanapotumikia Mungu “bega kwa bega.” Kwa kufanya hivyo, wanaiga kielelezo chenye upendo cha Daudi na Yonathani. (Sefania 3:9; 1 Samweli 20:17; Mithali 18:24) Ikiwa hujaungamana pamoja na watu wa Mungu, je! wewe hungependa kuwa sehemu ya jamii ya Yonathani wa ki-siku-hizi? Unaweza kufanya huo uwe mradi wako, na Mashahidi wa Yehova wataonyesha upendo wenye juhudi nyingi sana katika kukusaidia ufikie mradi huo.
[Maelezo ya Chini]
a Kielelezo bora cha jambo bili kimesimuliwa katika 1972 Yearbook of Jehovah’s Witnesses, kuanzia ukurasa 216, fungu la 3, hadi ukurasa 217, fungu la 3.
b Ona Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova cha 1989, kurasa 150-4.
Maswali kwa Kupitia
◻ Yonathani alimwonyeshaje Daudi upendo mshikamanifu?
◻ Ni upendo wa aina gani uliotangulia kuwekewa kivuli na upendo kati ya Daudi na Yonathani?
◻ Makasisi wa Jumuiya ya Wakristo wametendaje kama Mfalme Sauli wakati alipomwinda Daudi?
◻ Ni nini leo kinacholinganika na upendo wa Yonathani kwa Daudi?
◻ Hali ya ulimwenguni pote ya muungamaniko wa Mashahidi inaonyesha nini?
[Sanduku katika ukurasa wa 27]
St. Mary’s Cathedral
Sydney
August 20, 1940.
The Rt. Hon. W. M. Hughes, M.H.R.,K.C.,
Attorney General,
CANBERRA.
Dear Mr. Hughes:
(TAFSIRI YA BARUA)
Nakushukuru kwa barua yako ya tarehe 9 mwezi huu kuhusu mwakilisho uliyopolekewa na Bw. Jennings, M.P.
Bila shaka, inathaminiwa kwamba ni lazima wewe utumie uangalifu mwingi sana katika jambo hilo linalohitaji ujalifu mwingi sana lililotajwa na mawakilisho hayo.
Hata hivyo, ikiwa shaka lako la pekee linatokana na uhakika wa kwamba watu hawa wanadai kuwa wanaeneza mafundisho ya Ukristo, mimi ningedokeza kwa staha nyingi sana kwamba uamuzi wako juu ya kama wanafanya hivyo ufanywe kwa kutegemea mambo ya uhakika, wala si vile wao wanavyodai. Ili kupata mambo ya uhakika, nimi nakutolea vichapo vyao wenyewe na maneno na matendo yao wenyewe, yaliyoshuhudizwa na Polisi wa New South Wales. Ingekuwa vigumu kuwazia jambo jingine lililo kinyume zaidi cha Ukristo.
Kamishna wa Polisi katika N.S.W. ameeleza ana tumaini kwamba wenye mamlaka wa Jumuiya ya Madola watatangaza sosaiti inayohusika kuwa kundi haramu kisheria ili Polisi wawe wanaweza kulichukulia hatua yenye matokeo makubwa zaidi.
With every good wish, I remain,
Yours faithfully,
ARCHBISHOP OF SYDNEY