Ashuru Yenye Ukatili Ile Serikali Kubwa ya Pili ya Ulimwengu
Magunduzi ya wachimbuzi wa vitu vya kale kuhusu majumba ya wafalme wa kale Waashuri yanaweza kuongeza uhakika wako katika usahihi wa historia ya Biblia. Magunduzi hayo yanaonyesha nini juu ya historia ya Kibiblia, na yanapasa kumaanisha nini kwako wewe?
WAASHURI walikuwa jamii ya watu wa kivita wenye jeuri. Wao walikuza milki kubwa sana yenye ukorofi ambayo ilienea kutoka nchi ya kwao nyumbani katika ule mwisho wa kaskazini wa utambarare wa Mesopotamia. Wao wanarejezelewa nyakati nyingi katika Biblia, wakiwa adui za Yuda na Israeli.
Kwa uhakika kujua mengi zaidi juu ya jamii hiyo ya watu wa kale kutatusaidia sisi kuelewa mambo ambayo Biblia inasema. Hata maandishi ya kumbukumbu za Ashuru yenyewe yanahakikisha ukweli wa historia na unabii wa Biblia. Lakini Waashuri walipata wapi asili yao?
Jamii hiyo ya watu imara, ambao walijichora wenyewe picha zenye kuwaonyesha wakiwa na vinywele vingi vya juu ya macho, na ndevu nyingi, walikuwa wazao wa Ashuru, mwana-mjukuu wa Noa. Kwa kweli, neno hilo hilo moja la Kiebrania linamaanisha yote mawili, “Ashuru” na “(Mu)A-siria.” Nimrodi, ambaye anajulishwa katika Biblia kuwa “mwindaji hodari katika upinzani kwa Yehova,” ndiye aliweka misingi ya miji ya Ninawi na Kala. Miji hiyo miwili, pamoja na Ashuru na Khorsabadi, ilikuja baadaye kuwa miji mikuu ya Ashuru.—Mwanzo 10:8-12, 22, NW.
Kitabu cha Nahumu kinafunguka kwa maneno haya: “Lile tamko rasmi dhidi ya Ninawi,” ule mji mkuu wa Ashuru. Kwa sababu gani? Kwa sababu, kama vile nabii Nahumu anavyosimulia baadaye, Ninawi ulikuwa mji wa umwagaji-damu . .. wote ukiwa umejaa udanganyifu na unyang’anyi.” (Nahumu 1:1; 3:1, NW) Je! yeye alikuwa akitia chumvi? Hata kidogo!
Waashuri walikuwa na sifa ya unyaa usiotangulia kuwa na ulinganifu. Mapambo katika majumba yao wenyewe ya kifalme yaliyokuwa na fahari yanawaonyesha wakipora vitu, wakivichoma kwa moto, na kuviangamiza katika nchi moja baada ya nyingine. Ashurnasirpali mfalme wao anajisifu juu ya kufunika nguzo moja kwa ngozi za miili ya adui zake. Yeye anasema: “Watekwa wengi kutoka miongoni mwao mimi nilichoma kwa moto . . . Kutoka kwa watu fulani mimi nilikata na kutoa pua zao, masikio yao na vidole vyao, kutoka kwa wengi mimi niliyang’oa macho. Mimi nilifanya nguzo moja ya walio hai na nyingine ya vichwa.”
Mavutano ya Kidini
Hata hivyo, watu hao walikuwa wa kidini sana. Imesemwa kuhusu wale Waashuri wa kale: “Kupigana kulikuwa ndiyo shughuli ya lile taifa, na makuhani walikuwa wachochea-vita wa wakati wote. Sana-sana wao walipewa riziki yao kutokana na nyara za ushindi. . . Jamii hiyo ya wateka-nyara ilikuwa ya kidini mno.”—Ancient Cities, W. B. Wright, ukurasa 25.
Waashuri walirithi dini yao kutoka Babuloni. Inasema The Illustrated Bible Dictionary: “Katika pande zilizo nyingi dini ya Kiashuri ilitofautiana kidogo tu na ile ya Babulonia, ambako ndiko ilikuwa imetolewa.” Muhuri mmoja wa Kiashuri, ambao sasa umewekwa katika wonyesho wa Jumba la Hifadhi ya Vitu vya Kihistoria kule London, unaonyesha Ashuru mungu wao m kitaifa akiwa na vichwa vitatu. Ile itikadi ya mafungu matatu-matatu ya miungu ilikuwa ya kawaida katika ibada yao. Kwa hiyo, pamoja na kumbukumbu yao ya matendo ya ukatili na jeuri, si ajabu sana kwamba Nahumu nabii wa Biblia aliandika kwamba yule Mungu mmoja wa kweli, Yehova, “analipiza kisasi na ana uelekevu wa hasira-kali” kuelekea Waashuri.—Nahumu 1:2, NW.
Wakati Ninawi ulipoanguka, uangamivu wao ulikuwa kamili sana hivi kwamba kwa muda wa karne nyingi hata mahali mji huo ulipokuwa palisahauliwa. Wachambuzi fulani walidhihaki Biblia, wakisema mji huo haukupata kamwe kuwako. Lakini ulipata kuwako! Huo uligunduliwa upya, na habari ambazo wachimbuzi wa vitu vya kale walipata huko zilikuwa za kusisimua kweli kweli!
Majumba ya Kifalme Yenye Fahari Yagunduliwa
Katika 1843 mwakilishi wa nchi ya Ufaransa, Paul-Emile Botta, alichimba kule Khorsabadi, akitumaini kwamba hapo ndipo ungekuwa Ninawi wa kale. Badala ya hivyo, yeye aligundua lile jumba lenye fahari la “Sargoni mfalme wa Ashuru,” ambaye anatajwa kwa jina katika Biblia kwenye Isaya 20:1. Wachambuzi walikuwa wamedai kwamba Biblia ilikosea kwa sababu ilikuwa ndiyo hati moja tu ya kale iliyotaja mfalme huyo. Lakini Sargoni alikuwako, kwa maana wachimbuzi wa vitu vya kale walifukua jumba lake la kifalme lenye vyumba 200, na pia hazina nzuri sana ya michoro na vitu vingine. Hiyo ni kutia ndani habari za kila mwaka za Sargoni ambazo zinahakikisha, kulingana na maoni ya Kiashuri, matukio ambayo yametajwa katika Biblia. Tangu katikati ya ile karne ya 19, Sargoni amekuwa mmoja wa Wafalme wanaojulikana vizuri zaidi wa Kiashuri, ingawa bado kuna maelezo mengi madogo-madogo yanayomhusu ambayo si kamili.
Ndipo, katika 1847, Austin Henry Layard akagundua jumba la kifalme la Senakeribu kule Ninawi, zapata kilometa 19 kusini-magharibi mwa Khorsabadi. Huyo ndiye Senakeribu yule yule ambaye alipinga Yerusalemu kwa jeuri na ambaye anatajwa kwa jina mara 13 katika Biblia. Layard alichunguza vyumba 71 vya hilo jumba la kifalme. Lilikuwa limepambwa sana na tamasha za mapigano, vipindi vya ushindi, na sherehe za kidini.
Jambo la kustaajabisha hata zaidi, wachimbuzi wa vitu vya kale walipata ripoti za Senakeribu mwenyewe juu ya matukio ya kila mwaka, ambazo ziliandikwa juu ya mizinga ya udongo, au prizimu. Moja imewekwa kwenye Taasisi ya Nchi za Mashariki ya Chuo Kikuu cha Chicago, huku nyingine, ile Prizimu ya Taylor, ikiwa katika Jumba la Uingereza la Hifadhi ya Vitu vya Kihistoria.
Magunduzi hayo yalionyesha nini? Kwamba mambo ambayo Biblia inasema juu ya watu hawa na matukio ambayo walihusika nayo ni ya kweli kabisa—hata kufikia kuyataja majina ya watawala Waashuri!
Wale Wafalme Waashuri
Majina ya wafalme hao wa kale huenda yakasikika ya kigeni kwako, hata hivyo ni vizuri kuzoelea angalau saba kati yayo, kwa kuwa yanashirikishwa kwa ukaribu pamoja na matukio yanayosimuliwa katika Biblia.
Shalmaneseri wa 3 alifuata Ashurnasirpali baba yake katika kiti cha ufalme. Ile Nguzo Nyeusi yake inayojulikana sana, ambayo ilipatikana kule Nimrudi (Kala) na kutiwa katika wonyesho wa Jumba la Uingereza la Hifadhi ya Vitu vya Kihistoria, ina mchoro wa kuchongelewa ambao unaonyesha Mfalme Yehu wa Israeli akimlipa yeye zawadi za heshima, labda kupitia mjumbe fulani.—Linganisha hali zinazotajwa kwenye 2 Wafalme 10:31-33.
Baadaye karne iyo hiyo, wakati fulani karibu na mwaka 844 K.W.K., nabii Yona alitumwa kuonya Ninawi juu ya uharibifu uliokuwa unakuja.a Mji huo ulitubu na kuachiliwa. Ingawa sisi hatujui vizuri kabisa ni nani aliyekuwa mfalme katika Ninawi wakati jambo hilo lilipotukia, inapendeza kuangalia kwamba katika kipindi hicho ushambulizi wa Kiashuri ulikuwa umepungua.
Tiglathi-pileseri wa 3 (anayeitwa Puli pia) ndiye mfalme wa kwanza wa Kiashuri kutajwa kwa jina katika Biblia. Yeye alisonga mbele akaingia katika ufalme wa kaskazini wa Israeli wakati wa utawala wa Menahemu (791-780 K.W.K.). Biblia inasema Menahemu alimlipa yeye talanta elfu moja za fedha ili aondoke humo.—2 Wafalme 15:19, 20.
Katika habari zake mwenyewe za matukio ya kila mwaka, ambazo zilipatikana kule Kala, Tiglathi-pileseri anathibitisha uhakika huo wa Kibiblia, akisema: “Mimi nilipokea zawadi ya heshima kutoka kwa . . . Menahemu wa Samaria.”
Samaria Waanguka
Hata hivyo, Samaria na ufalme wa Israeli wa kaskazini wenye makabila kumi walikuwa matatani, si pamoja na Waashuri tu, bali pia pamoja na Muumba wa mbingu na dunia, Yehova Mungu. Wao walikuwa wamegeuka kutoka ibada yake kwenda kwenye ibada ya Baali iliyo yenye fujo-fujo na ulevi-ulevi. (Hosea 2:13) Ingawa walipokea onyo jingi kupitia manabii wa Yehova, wao walikataa kugeuka. Kwa hiyo nabii Hosea alivuviwa na Mungu kuandika: “Kwa uhakika Samaria na mfalme wao utafanywa uwe kimya, kama kitawi ambacho kimekonyolewa kilicho juu ya uso wa mafungu-mafungu ya maji.” (Hosea 10:7; 2 Wafalme 17:7, 12-18, NW) Biblia inasema kwamba Waashuri walitenda Israeli jambo hilo—na ndivyo maandishi ya kumbukumbu za Waashuri wenyewe yanavyosema, kama vile sisi tutaona.
Shalmaneseri wa 5, ambaye alifuata Tiglathi-pileseri katika cheo, alivamia ufalme wa kaskazini wa Israeli wenye makabila kumi na akalaza mazingiwa katika Samaria mji wao mkuu wenye ngome imara. Baada ya mazingiwa ya miaka mitatu, Samaria ulianguka (katika 740 K.W.K.), kama vile manabii wa Yehova walikuwa wamesema.—Mika 1:1, 6; 2 Wafalme 17:5.
Sargoni wa 2 alifuata Shalmaneseri katika cheo, na huenda akawa ndiye alikamilisha ushinde wa Samaria, kwa kuwa mwanzo wa utawala wake unasemwa ulisadifiana na mwaka ambao mji huo ulianguka. Biblia inasema kwamba baada ya Samaria kuanguka, mfalme wa Ashuru “aliongoza Israeli kuingia ndani ya uhamisho katika Ashuru.” (2 Wafalme 17:6, NW) Mchoro mmoja wa maandishi ya Kiashuri, ambao ulipatwa kule Khorsabadi, unathibitisha jambo hilo. Juu ya huo, Sargoni anataarifu hivi: “Mimi nilifanya mazingiwa na kushinda Samaria, nikapeleka wakaaji wao 27,290 wakiwa mateka.”
Biblia inazidi kusema kwamba baada ya Waisraeli hao kuhamishwa humo, mfalme wa Ashuru alileta watu kutoka majimbo mengine “na alifanya wakae katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; na wao wakaanza kumiliki Samaria na kukaa katika miji yao.”—2 Wafalme 17:24, NW.
Je! maandishi ya kumbukumbu za Ashuru yanathibitisha hilo pia? Ndiyo, habari za matukio ya kila mwaka za Sargoni mwenyewe, ambazo zimeandikwa juu ya ile Prizimu ya Nimrudi, zinasema: “Mimi nilirudisha mji wa Samaria kama ulivyokuwa . . . Mimi nilileta ndani ya huo watu kutoka zile nchi ambazo zilishindwa na mikono yangu mwenyewe.”—Illustrations of Old Testament History, R. D. Barnett, ukurasa 52.
Yerusalemu Waokolewa
Senakeribu, mwana wa Sargoni aliyemfuata katika cheo, anajulikana sana kwa wanafunzi wa Biblia. Katika 732 K.W.K. mfalme huyo mpenda-vita alileta songamano hodari la kivita dhidi ya ufalme wa kusini wa Yuda.
Biblia inasema kwamba “Senakeribu mfalme wa Ashuru alikuja akapanda dhidi ya miji yote ya Yuda yenye ngome na kuibamba.” Kwa kuogopeshwa sana na tisho hilo, Mfalme Hezekia wa Yerusalemu ‘alituma ujumbe kwa mfalme wa Ashuru kule Lakishi’ na akajitolea kununua mwondoko wa mfalme huyo kwa kumpa zawadi nyingi sana za heshima.—2 Wafalme 18:13, 14, NW.
Je! Senakeribu anathibitisha kwamba yeye alikuwa kule Lakishi? Ni wazi! Yeye alionyesha tamasha za mazingiwa hayo juu ya mabapa-laini makubwa katika jumba lake kubwa sana ambalo wachimbuzi wa vitu vya kale walichunguza kule Ninawi. Hayo mabapa-laini yaliyo na maelezo mengi, ambayo yamo katika Jumba la Uingereza la Hifadhi ya Vitu vya Kihistoria, yanaonyesha Lakishi ukishambuliwa. Wakaaji wanamiminika nje kwa kusalimu amri. Mateka wanapelekwa. Watu fulani wametundikwa juu ya vigingi. Wengine wanainamia Senakeribu mwenyewe kumpa heshima zao, mtu yule yule ambaye ametajwa katika ule usimulizi wa Kibiblia. Maandishi mamoja yaliyochorwa kwa maneno yenye umbo la kabari yanasema: “Senakeribu, mfalme wa ulimwengu, mfalme wa Ashuru, aliketi juu ya kiti-nimedu cha ufalme na kupitisha mbele yake wale mateka (waliochukuliwa) kutoka Lakishi ili awakague.”
Biblia inasema kwamba Hezekia alilipa zawadi za heshima za “talanta mia tatu za fedha na talanta thelathini za dhahabu.” (2 Wafalme 18:14, 15, NW) Lipo hilo linathibitishwa katika habari za matukio ya kila mwaka za Senakeribu, ingawa yeye anadai alipokea “talanta 800 za fedha.”
Ijapokuwa lipo hilo lilitolewa, wale wajumbe wa mfalme Mwashuri walisimama nje ya kuta za Yerusalemu, wakamfanyia mzaha Yehova Mungu, na kutisha mji mtakatifu wake. Kupitia Isaya, ambaye alikuwa ndani ya Yerusalemu, Yehova alisema hivi juu ya Senakeribu: “Yeye hatakuja ndani ya mji huu wala yeye hatarusha mshale humo wala kuukabili kwa ngao wala kukupusha juu boma la mazingiwa dhidi yao. Kwa njia ambayo yeye alikuja, yeye atarudi, na ndani ya mji huu yeye hatakuja.”—2 Wafalme 18:17–19:8, 32, 33, NW.
Je! Yehova alikomesha Senakeribu, kama ilivyoahidiwa? Usiku uo huo Waashuri 185,000 waliuawa kupitia malaika wa Mungu! Senakeribu aling’oa kituo chake na kurudi Ninawi, na baadaye akauawa na wawili wa wana wake mwenyewe alipokuwa akiinama chini kwa Nisroki mungu wake.—2 Wafalme 19:35-37.
Bila shaka, Senakeribu mwenye moyo uliotukuka hangetazamiwa kujisifu juu ya hasara hiyo ya vikosi vyake. Lakini jambo ambalo yeye anasema ni la kupendeza. Habari zake za matukio ya kila mwaka, ambazo zimeandikwa katika ile Prizimu ya Taasisi ya Nchi za Mashariki na pia ile Prizimu ya Taylor, zinasema: “Kwa habari ya Hezekia Myahudi, yeye hakujiweka chini ya nira yangu, Mimi nililaza mazingiwa kwa 46 ya miji yake imara, ngome za ukuta na kwa vijiji vidogo visivyohesabika katika ujirani wao, na kushinda (hivyo) . . . Yeye mwenyewe mimi nilifanya mfungwa-gereza katika Yerusalemu, kao lake la kifalme, kama ndege katika kizimba chake.” Senakeribu anasema kwamba “ile fahari yenye kutia hofu nyingi ya ubwana wangu” ililemea Hezekia. Hata hivyo, yeye hasemi aliteka Hezekia au alishinda Yerusalemu, kama alivyokuwa amesema juu ya ile ‘miji imara’ na “vijiji vidogo.” Kwa sababu gani sivyo? Kama vile Biblia inavyoonyesha, ile sehemu bora kabisa ya vikosi ambavyo Senakeribu alikuwa amepeleka vikafanye hivyo ilikuwa imeangamizwa!
Esari-hadoni, mwana wa umri mdogo zaidi ambaye pia alifuata Senakeribu katika cheo anatajwa mara tatu katika Biblia—katika Kitabu cha Pili cha Wafalme, Ezra, na Isaya. Biblia inaandika katika Kumbukumbu kwamba Waashuri waliteka Manase mfalme wa Yuda. Wachimbuzi wa vitu vya kale wamepata orodha ya Kiashuri ambayo inatia ndani “Manase mfalme wa Yuda” miongoni mwa wale ambao walilipa zawadi za heshima kwa Esari-hadoni.—2 Nya kati 33:11, NW.
Ashurbanipali, mwana wa Esari-hadoni, anafikiriwa ndiye “yule Asenapari mkuu na mwenye kuheshimika” ambaye anatajwa kwenye Ezra 4:10, NW. Yeye alipanua milki ya Kiashuri ikafikia kadiri iliyo kubwa zaidi.
Mwisho wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu
Kwa sababu ya uovu wa Ashuru, uangamivu wayo ulikuwa umeamuliwa. Nahumu nabii wa Yehova alikuwa ameandika kwamba Ninawi mji mkuu wa serikali hiyo ungetobolewa tundu kwenye “milango ya ile mito . . . na kwa kweli jumba la kifalme lenyewe [linge]yeyushwa.” Kungekuwa na uporaji wa fedha na dhahabu, ule mji ungeachwa utupu, na watu wangesema: “Ninawi umetekwa nyara! Nani atauhurumia?”—Nahumu 2:6-10; 3:7, NW.
Je! jambo hilo lilitukia pia? Acha wenye kushinda Ninawi wajibu. Katika 632 K.W.K. Wababuloni na Wamedi walitekeleza kisasi kwa ukali mwingi juu ya mji mkuu huo wa Kiashuri Orodha za matukio ya Babuloni zinaripoti: “Wao walienda na ile nyara kubwa ya mji na hekalu na [wakageuza] mji huo kuwa rundiko la magofu.”
Sasa marundiko makubwa mawili ya ardhi ndiyo yaliyo katika mahali hapo ulipokuwapo mji mkuu huo wenye kiburi. Hayo ni ushuhuda ulio kimya wa uhakika wa kwamba hakuna taifa —wala hata Ashuru yenye kiburi na jeuri—linaloweza kuzuia utimizo hakika wa maunabii ya Yehova.
[Maelezo ya Chini]
a ‘Kwa habari ya tarehe, sisi tunakubali ile orodha ya tarehe inayoonyeshwa na Biblia, ambayo inatofautiana na tarehe za kale zinazotegemea vyanzo vya kilimwengu visivyotegemeka kwa kadiri hiyo. Kwa zungumzo lenye maelezo marefu juu ya orodha ya tarehe za Kibiblia, ona Aid to Bible Understanding, kurasa 322-48 hasa kile kisehemu juu ya Ashuru, kurasa 325-6.
[Ramani katika ukurasa wa 24]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ASHURU
Ninawi
Babuloni
Damascus
Samaria
Lakishi
Yerusalemu
ARABIA
Misri
Bahari Kuu
[Credit Line]
Based on a map copyrighted by Pictorial Archive (Near Eastern History) Est. and Survey of Israel
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mfalme Ashurbanipali anamimina toleo la divai juu ya simba waliouawa. Je! hiyo inakukumbusha wewe juu ya Nimrodi?
[Credit Line]
Courtesy of the British Museum, London
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mchoro wa kuchongelewa wa Kiashuri ukionyesha lile shambulizi, huku mtambo wa mazingiwa ukiwa dhidi ya Lakishi ule mji wa Kiyudea wenye ngome
[Credit Line]
Kwa ruhusa ya Jumba la Uingereza la Hifadhi ya Vitu vya Kihistoria, London
Tell Lakishi. Mahali hapa pa maana pa kushikia doria nje-nje ya nchi katika kusini-magharibi palilinda eneo la Yudea lenye vilima-vilima mpaka Waashuri walipolaza mazingiwa Lakishi na kushinda mji huo
[Credit Line]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Picha katika ukurasa wa 27]
Mchoro wa kuchongelewa wa Sargoni 2 (kushoto) akielekeana na afisa mmoja Mwashuri ambaye huenda akawa ni Senakeribu yule Mwana-Mfalme mwenye kurithi ufalme
[Credit Line]
Kwa ruhusa ya Jumba la Uingereza la Hifadhi ya Vitu vya Kihistoria, London