Maoni ya Biblia
Je, Sayansi na Biblia Zaafikiana?
KUANZIA ndege na mabomu ya atomu hadi chembe zilizobadilishwa kijeni na kuumbwa kwa kondoo bila njia ya kujamiiana, karne yetu ya 20 imekuwa muhula uliotawalwa na sayansi. Wanasayansi wamewezesha watu watue mwezini, wamemaliza ndui, wamebadilisha kilimo, na kuletea mabilioni mawasiliano ya papo hapo ulimwenguni pote. Kwa hiyo, si ajabu kwamba watu hukubali chochote wasemacho wanasayansi. Lakini wanasayansi wana nini cha kusema, ikiwa kipo, kuhusu Biblia? Biblia nayo hutueleza nini kuhusu sayansi?
Je, Miujiza Si ya Kisayansi?
“Watu wenye mawazo ya kisayansi huitikadi katika uhusiano wa ‘kisababishi na matokeo.’ Wanahisi kwamba kuna elezo la kiasili kabisa kwa kila kitu,” yaeleza ensaiklopedia ya kisasa. Wanafunzi wa Biblia pia wakubali kanuni zilizothibitishwa za sayansi. Hata hivyo, wanatambua kwamba Biblia mara nyingi huzungumza juu ya matukio ya kimuujiza ambayo haiwezi kuelezwa kisayansi kulingana na ujuzi wa wakati huu. Vielelezo ni kusimama tuli kwa jua katika siku ya Yoshua na kutembea kwa Yesu juu ya maji. (Yoshua 10:12, 13; Mathayo 14:23-34) Hata hivyo, miujiza hii huelezwa kuwa ilitokana na nguvu za Mungu zikitenda katika njia inayozidi ile ya kibinadamu.
Hoja hii ni ya maana. Ikiwa Biblia ilidai kwamba watu wanaweza kutembea juu ya maji bila msaada wa kimungu au kwamba mwendo uonekanao kuwa wa kawaida wa jua kuvuka anga waweza kukatizwa bila sababu yoyote, hiyo ingeonekana kuwa yapinga mambo hakika ya sayansi. Hata hivyo, Biblia inapopatia sifa nguvu za Mungu kwa matukio hayo, haipingi sayansi bali masimulizi hayo huongoza kwenye uwanja wa kitaaluma ambao sayansi bado haina ufahamu.
Je, Biblia Hupinga Sayansi?
Kwa upande ule mwingine, namna gani kuhusu visa ambapo Biblia huzungumza juu ya matukio ya kawaida katika maisha za watu au kutaja mimea, wanyama, au mambo ya kiasili? Kwa kupendeza, hakuna kielelezo kilichothibitishwa cha Biblia ikipinga mambo hakika ya sayansi yajulikanayo katika visa kama hivyo wakati muktadha wa maelezo hayo ufikiriwapo.
Kwa kielelezo, Biblia mara nyingi hutumia lugha ya kishairi ambayo huonyesha mawazo ya watu walioishi maelfu ya miaka iliyopita. Kitabu cha Ayubu kisemapo kuhusu Yehova akifua au kufanyiza anga “ambazo zina nguvu kama kioo cha kuyeyushwa,” hicho hufafanua kwa kufaa sana anga kuwa kama kioo cha chuma ambacho hutoa mwakiso mwangavu. (Ayubu 37:18) Hakuna haja ya kuchukua kielelezo hicho kihalisi, kama vile tu hungechukua kihalisi kielelezo cha dunia ikiwa na “misingi” au “jiwe la pembeni.”—Ayubu 38:4-7.
Hilo ni la maana kwa sababu waelezaji wengi wamechukua vielelezo kama hivyo kihalisi. (Ona 2 Samweli 22:8; Zaburi 78:23, 24.) Wamefikia mkataa kwamba Biblia hufunza jambo kama lifuatalo, lililonukuliwa kutoka The Anchor Bible Dictionary.
“Dunia ambayo juu yayo wanadamu hukaa yafikiriwa kuwa ya mviringo, kitu kigumu, labda chenye umbo la kisahani, ikielea juu ya maji mengi yasiyo na mipaka. Yenye kuenea sambamba ni maji mengine, pia yasiyo na mipaka, yakiwa juu angani, ambayo kutoka kwake maji hushuka kwa namna ya mvua kupitia mashimo na mifereji inayotoboa hifadhi ya maji ya kimbingu. Mwezi, jua, na vimulikaji vinginevyo haviwezi kusonga vikiwa katika muundo wa tao ambao hujipinda juu ya dunia. Muundo huu ni ‘mbingu’ (rāqîa‛) za ufafanuzi wa kikuhani.”
Kwa wazi, ufafanuzi huu hupingana na sayansi ya kisasa. Lakini je, huo ni ukadiriaji wa haki wa mafundisho ya Biblia kuhusu mbingu? Sivyo hata kidogo. The International Standard Bible Encyclopaedia hutaarifu kwamba ufafanuzi kama huo wa ulimwengu wote mzima wa Waebrania “kwa uhalisi unategemea zaidi mawazo yaliyoenea Ulaya wakati wa Enzi za Giza kuliko taarifa zozote hakika katika A[gano] la K[ale].” Mawazo hayo ya enzi za kati yalitoka wapi? Kama David C. Lindberg aelezavyo katika kitabu The Beginnings of Western Science, yalitegemea kwa sehemu kubwa kosmolojia ya mwanafalsafa wa kale Mgiriki Aristotle, ambaye maandishi yake yalikuwa msingi wa mafunzo mengi ya enzi za kati.
Lingekuwa jambo lisilo na maana na lenye kutatiza kwa Mungu kuelezea Biblia kwa lugha ambayo ingevutia mwanasayansi wa karne ya 20. Badala ya kuwa na fomyula za kisayansi, Biblia imejaa vielezi dhahiri vilivyotolewa katika maisha ya kila siku ya watu ambao waliviandika kwanza—ufafanuzi wa wazi sana ambao umekuwa na uvutano usio na mwisho hadi leo hii.—Ayubu 38:8-38; Isaya 40:12-23.
Ujuzi Kutoka Chanzo cha Juu Zaidi
Hata hivyo, kwa kupendeza, marejezo fulani ya Biblia huelekea kuonyesha ujuzi wa kisayansi ambao haukupatikana kwa watu walioishi wakati huo. Ayubu amfafanua Mungu kuwa “hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, na kuutundika ulimwengu pasipo kitu.” (Ayubu 26:7) Wazo la dunia kuwa imetundikwa “pasipo kitu” lilikuwa tofauti sana na ngano za watu wengi wa kale, ambao walifikiri imewekwa juu ya tembo au kasa wa baharini. Sheria ya Kimusa ina matakwa ya usafi ya hali ya juu sana kuliko ujuzi wa kitiba uliopatikana wakati huo. Maagizo ya kutenga kando watu walioshukiwa kuwa na ukoma na makatazo dhidi ya kugusa wafu bila shaka yaliokoa maisha ya Waisraeli wengi. (Mambo ya Walawi 13; Hesabu 19:11-16) Kinyume sana na hilo, mazoea ya kitiba ya Waashuri hufafanuliwa kuwa “mchanganyiko wa dini, uaguzi, na itikadi katika roho waovu” na yalihusisha kutibiwa na kinyesi cha mbwa na mkojo wa binadamu.
Kama vile mtu awezavyo kutarajia kutoka kitabu kilichopuliziwa na Muumba, Biblia ina habari sahihi sana kisayansi ambayo kwa wazi imeendelea sana kuliko wakati wayo, ingawa haikazii sana maelezo ya kisayansi ambayo hayangekuwa na maana au yangewatatanisha watu wa kale. Biblia haina chochote ambacho hupinga mambo hakika ya kisayansi yajulikanayo. Kwa upande ule mwingine, Biblia ina mengi ambayo hupingana na nadharia zisizothibitishwa, kama vile nadharia ya mageuzi.
[Blabu katika ukurasa wa 27]
Maelezo ya Ayubu kwamba dunia ‘imetundikwa pasipo kitu’ huonyesha ujuzi ambao haukupatikana kwa watu wa wakati wake
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
NASA