Biashara Yako Itakugharimu Nini?
MKE wa rais wa nchi moja ya Amerika Kusini alishtakiwa kumimina maelfu ya mamia ya dola katika mikataba iliyofanywa na kampuni bandia zilizoanzishwa na washiriki wa familia yake. Mfanya-biashara mmoja wa hisa mwenye umri wa miaka 38 katika India alishikwa na kunyang’anywa nyumba yake yenye starehe nyingi na magari yake 29 kwa sababu ya madai ya kuhusika katika kashfa ya dola bilioni 1.6 iliyohusu benki na soko la hisa. Katika Filipino, maelfu ya wakazi wa kisiwa kimoja hupata riziki yao kwa kutengeneza bunduki kinyume cha sheria. Na ili waendelee na biashara hii yenye mapato mazuri, yaripotiwa kwamba kwa kawaida wao huwahonga maofisa ili wasiingilie.
Ndiyo, kutofuatia haki na upunjaji katika biashara kumeenea kotekote ulimwenguni. Na mara nyingi kunagharimu watu waliohusika cheo chao na sifa yao, na pesa vilevile.
Vipi wewe? Je, unafanya biashara? Au unafikiria kuanzisha biashara? Itakugharimu nini? Bila shaka, kuwa katika biashara kutakugharimu jambo fulani. Hiyo si mbaya hasa. Hata hivyo ni jambo la hekima kuhesabu gharama kabla ya kuanzisha biashara au kufanya maamuzi kuhusu biashara ambayo tayari imeanzishwa. (Luka 14:28) Sanduku lililo katika ukurasa 31 laonyesha gharama fulani ambazo utafanya vema kufikiria.
Kwa wazi, si rahisi kuwa katika biashara. Kwa Mkristo, kuna matakwa ya kiroho na ya kimaadili ya kufikiriwa. Je, unaweza kulipa gharama na kudumisha usawaziko wa kiroho? Je, gharama nyinginezo ni zile usizoweza kukubali kimaadili? Ni zipi baadhi ya kanuni zitakazokuwezesha kuamua ni gharama zipi zinazokubalika na zipi hazikubaliki?
Usitukuze Pesa Isivyofaa
Pesa huhitajika katika kuendesha biashara, na inatumainiwa kwamba biashara italeta fedha za kutosha kugharimia familia ya mtu. Hata hivyo, ni rahisi sana kupotoshwa na miradi inayohusu pesa. Pupa yaweza kuwa sababu kuu. Kwa watu wengi, kila kitu kingine huwekwa kando mahali pesa inahusika. Lakini, mwandikaji mmoja wa kitabu cha Biblia cha Mithali, Aguru, alionyesha maoni yenye usawaziko aliposema: “Usinipe umaskini wala utajiri; unilishe chakula kilicho kadiri yangu.” (Mithali 30:8) Yeye alitambua thamani ya kuridhika na riziki ya kutosha—yeye hakutaka “ufanisi mkubwa,” kama ambavyo watu wengine husema katika biashara.
Hata hivyo, pupa yaweza kufanya mtu asahau kanuni hii wakati ile iitwayo fursa bora itokeapo. Mhudumu mmoja asafiriye wa Mashahidi wa Yehova katika nchi moja inayositawi aliripoti juu ya kisa kama hicho. Kampuni moja iliyohitaji rasilimali ya mtaji ilitokeza mtazamo wa kwamba washiriki wayo wangeongeza pesa zao maradufu, labda kwa miezi michache tu. Toleo hilo la kupata pesa nyingi kwa urahisi lilifanya wengi waweke fedha zao katika kampuni hiyo. Mhudumu huyo asafiriye asema hivi: “Wengine walitamani sana kujiingiza. Wao hawakuwa wakiuliza maswali mengi ya kutosha, nao walikopa pesa [ili waweke katika kampuni hiyo].”
Wakifanya tofauti, watu wawili walienda kuchunguza katika ofisi za kampuni hiyo kabla ya kuweka fedha zao. Ombi lao la kuona vifaa vya kutengeneza vitu lilikataliwa. Jambo hilo liliwafanya washuku sifa ya kampuni hiyo. Hilo likawa ulinzi kwao, kwa kuwa kwa majuma machache tu, hila iliyoonekana kuwa ya kupunja pesa iligunduliwa, na watu walishikwa. Ebu wazia hilo liligharimu nini wale ambao hawakuwa wamefanya uchunguzi kwanza. Wao walipoteza si pesa zao tu bali labda hata marafiki waliowakopesha na ambao sasa hawawezi kulipwa ule mpango ulipoharibika. Kwa habari za pesa, ni jambo la hekima kama nini kutumia kanuni ya Mithali 22:3: “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; bali wajinga huendelea mbele wakaumia”!
Shikilia Neno Lako
Vipi ikiwa biashara yabadilika kuwa mbaya? Zaburi 15:4 lapongeza mtu anayeshikilia mapatano yake hata kama hafaidiki kwa kufanya hivyo: “Ingawa ameapa kwa hasara yake, hayabadili maneno yake.” Ni rahisi kushikilia neno lako mambo yanapoenda vizuri. Lakini kunakuwa mtihani wa uaminifu wa maadili ukiwa unapata hasara ya kifedha.
Kumbuka kielelezo cha Biblia cha wakati wa Yoshua. Wagibeoni walifanya hila ili wakuu wa Israeli wafanye agano pamoja nao wasije wakaharibiwa. Kwa kweli wao walikuwa sehemu ya taifa lililoonwa kuwa tisho kwa Israeli. Hila hiyo ilipogunduliwa, “wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa BWANA.” (Yoshua 9:18) Hata ingawa kikundi hiki kilikuwa kimetoka katika eneo la adui, wakuu waliona kuwa muhimu kushikilia neno lao. Na matokeo yaliyofuata yaonyesha kwamba jambo hilo lilimpendeza Yehova.—Yoshua 10:6-11.
Je, wewe pia utashika mapatano na mikataba yako ya kibiashara mambo yasipoenda kama ulivyotazamia?a Kufanya hivyo kutakufanya uwe zaidi kama Yehova, ambaye sikuzote hushikilia neno lake.—Isaya 55:11.
Uwe Mwenye Kufuatia Haki
Ufuatiaji haki hupatikana mara chache sana au haupo kabisa katika ulimwengu wa biashara wa leo. Wengine wenye biashara kama yako waweza kutumia njia zisizo za haki ili kuongeza mapato yao. Wao waweza kukosa kufuatia haki katika matangazo yao ya biashara. Wanaweza kuiba jina la kampuni nyingine na kuliweka katika vitu wanavyotengeneza. Au wanaweza kutokeza vitu vyenye hali ya chini kuwa vya hali ya juu. Hizo zote ni namna za kutofuatia haki. Wale wafanyao hivyo ni kama “waovu” ambao, kulingana na Asafu, “wameongeza mapato yao,” yaonekana kwa njia ya upunjaji.—Zaburi 73:12.
Je, wewe, ukiwa Mkristo, utatumia njia zisizo halali? Au ni afadhali uongozwe na kanuni za Biblia, kama vile: “Hatukumdhulumu mtu ye yote, wala kumharibu mtu, wala kumkaramkia mtu”; “tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila”; “vipimo mbalimbali ni chukizo kwa BWANA; tena mizani ya hila si njema”? (2 Wakorintho 4:2; 7:2; Mithali 20:23) Kumbuka kwamba mwanzilishi wa kutofuatia haki si mwingine ila Shetani Ibilisi, ‘baba wa uongo.’—Yohana 8:44.
Huenda wengine wakapinga wakisema: ‘Ni vigumu kudumu katika biashara mpaka mtu atumie njia zisizo za haki kama wengine wanavyofanya.’ Hapa ndipo Mkristo aweza kuonyesha imani yake kwa Yehova. Ufuatiaji haki hutahiniwa unapogharimu kitu. Kusema kwamba mtu hawezi kuishi akiwa anafuatia haki ni kama kusema Mungu hajali wale wanaompenda. Mtu aliye na imani ya kweli kwa Yehova ajua kwamba Mungu anaweza kuandalia watumishi wake katika nchi yoyote na katika hali yoyote. (Waebrania 13:5) Ni kweli kwamba huenda mtu akalazimika kuridhika na mapato kidogo kuliko wawezavyo kupata wasiofuatia haki, lakini je, hiyo si gharama inayofaa kulipwa ili kupata baraka za Mungu?
Kumbuka kwamba kutofuatia haki ni kama bumerang’i ambayo, ikitupwa, humrudia yeye aliyeitupa. Mfanya-biashara akipatikana kuwa asiyefuatia haki, wateja na watu wa kumletea vitu watamwacha. Huenda akawadanganya mara moja, lakini huenda hiyo ikawa ya mwisho. Kwa upande mwingine, mfanya-biashara mwenye kufuatia haki mara nyingi hustahiwa na wengine. Uwe mwangalifu usishawishwe na kusababu kwa uwongo, ‘Kila mtu anafanya hivyo, kwa hiyo ni sawa.’ Kanuni ya Biblia ni, “Usiandamane na mkutano kutenda uovu.”—Kutoka 23:2.
Namna gani ikiwa mshiriki wako wa biashara wa muda mrefu si Mkristo mwenzako na sikuzote hashikilii kanuni za Biblia. Je, lafaa kutumia hilo kuwa udhuru wa kukwepa daraka lako mwenyewe jambo fulani lisilo la Kimaandiko linapofanywa? Kumbuka vielelezo kama Adamu na Sauli. Badala ya kuepuka dhambi, walishindwa na mikazo kutoka kwa wengine na kisha kulaumu wenzao. Walilipa gharama kubwa kama nini!—Mwanzo 3:12, 17-19; 1 Samweli 15:20-26.
Shughulika Ifaavyo na Waamini Wenzako
Je, kuna gharama za kufikiria unapoingia katika shughuli za biashara pamoja na waabudu wenzako wa Yehova? Nabii Yeremia aliponunua shamba fulani katika mji wa kwao wa Anathothi kutoka kwa binamu yake, yeye hakumpa tu pesa na kumsalimu. Badala ya hivyo, alisema hivi: “Nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani.” (Yeremia 32:10) Kuandika mapatano kama hayo kwaweza kuepusha kukosa kuelewana kunakoweza kutokea baadaye hali zikibadilika.
Lakini namna gani ikiwa ndugu Mkristo aonekana kama amekutendea isivyo haki katika biashara? Je, umpeleke mahakamani? Biblia yasema wazi juu ya jambo hili. “Je! mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu?” Paulo akauliza. Namna gani ikiwa tatizo hilo halisuluhishwi vizuri mara hiyo? Paulo aliongezea: “Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang’anywa mali zenu?” Ebu fikiria tu doa jeusi ambalo hilo lingetia katika tengenezo la Kikristo ikiwa watu wa nje wangesikia Wakristo wa kweli wakizozania mahakamani! Je, yaweza kuwa kwamba katika visa hivyo upendo wa pesa umezidi upendo kwa ndugu? Au yaweza kuwa kwamba heshima ya mtu imeharibiwa naye anafikiria tu kulipiza kisasi? Shauri la Paulo laonyesha kwamba katika visa hivyo ingekuwa afadhali kupata upotezo kuliko kwenda mahakamani.—1 Wakorintho 6:1, 7; Warumi 12:17-21.
Bila shaka, kuna njia ya Kimaandiko ya kushughulikia mizozo kama hiyo katika kutaniko. (Mathayo 5:37; 18:15-17) Katika kusaidia ndugu wanaohusika kufuata hatua zinazopendekezwa, waangalizi Wakristo huenda wakatoa shauri fulani lenye kusaidia kwa wote wahusikao. Yaweza kuonekana ikiwa rahisi katika mazungumzo hayo kukubali kanuni za Biblia, lakini baadaye, je, utaonyesha kwamba umesikiliza kwa kutumia shauri lililotolewa? Upendo kwa Mungu na kwa Wakristo wenzetu ungetusukuma kufanya hivyo.
Bila shaka, kufanya biashara kutakugharimu jambo. Inatumainiwa utalipa gharama ifaayo. Unapokabili maamuzi au hali yenye kutilika shaka, kumbuka kwamba kuna mambo mengi maishani yaliyo na thamani sana kuliko pesa. Kwa kutotukuza pesa isivyofaa, kushikilia neno lako, kuwa mwenye kufuatia haki, na kushughulika na washiriki wa biashara katika njia ya Kikristo, twaweza kuhakikisha kwamba biashara haigharimu wakati mwingi zaidi na pesa nyingi zaidi kuliko inavyohitajika, na wakati uo huo, twaweza kuhifadhi urafiki, dhamiri njema, na uhusiano mzuri pamoja na Yehova.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kupata kielelezo cha kisasa cha kushikilia neno lako katika biashara, ona makala “Neno Langu Kifungo Changu” katika Amkeni! la Mei 8, 1988, kurasa 11-13, (Kiingereza).
[Sanduku katika ukurasa wa 31]
Mambo Ambayo Biashara Yako Huenda Ikakugharimu
Wakati: Kujiendeshea biashara sikuzote huchukua karibu muda zaidi kuliko kufanya kazi ya kuajiriwa katika kampuni. Je, itavuruga ratiba yako, ikikuachia muda mdogo kwa utendaji muhimu wa kiroho? Kwa upande mzuri, je, utaweza kupanga mambo yako kutumia muda mwingi zaidi kufanya mapenzi ya Mungu? Ikiwa ndivyo, sawa. Lakini uwe mwangalifu! Si rahisi kufanya hivyo.
Pesa: Pesa huhitajika kutengeneza pesa. Ni rasilimali gani inayohitajika katika biashara yako? Je, tayari una fedha? Au utalazimika kukopa? Je, uko tayari kupoteza pesa kiasi fulani? Au gharama itapita uwezo wako mambo yasipoenda kama ulivyotazamia?
Marafiki: Kwa sababu ya matatizo yanayotokea katika utendaji wa kila siku, biashara za watu binafsi zimewafanya wapoteze marafiki. Ingawa kuna uwezekano wa kupata marafiki, uwezekano wa kuharibu mahusiano ni mkubwa mno. Namna gani ikiwa marafiki hawa ni ndugu zetu Wakristo?
Dhamiri Njema: Mtazamo wa kawaida kwa biashara katika ulimwengu wa leo ni “Mashindano makali” au “Nitafaidikaje?” Zaidi ya asilimia 70 ya wanafunzi katika uchunguzi mmoja wa Ulaya walisisitiza kwamba maadili yana fungu dogo sana au hayana kabisa katika maisha ya biashara. Si ajabu kwamba upunjaji, kutofuatia haki, na biashara zenye kutilika shaka zimekuwa za kawaida. Je, utashawishika kufanya kama wengine?
Uhusiano Wako Pamoja na Yehova: Tendo lolote katika biashara lililo kinyume cha sheria na kanuni za Mungu, hata kama ni la kawaida sana katika mambo ya kibiashara, lingeharibu uhusiano wa mtu pamoja na Mfanyi wake. Hilo laweza kumgharimu matazamio yake ya kupata uhai wa milele. Je, kwa wazi, hili halingekuwa gharama ya juu mno kwa Mkristo mwaminifu mshikamanifu kulipa, hata kama anafaidikaje kimwili?
[Picha katika ukurasa wa 31]
Ni ipi itakayoepusha kutoelewana baadaye? Kusikilizana tu au mkataba ulioandikwa?