Linda Jina Lako
MWANAMUME anayesanii majengo mazuri hujifanyia jina la kuwa msanifu-ujenzi stadi. Mwanamke mchanga anayepita mitihani shuleni husifika kuwa mwanafunzi mwerevu. Hata mtu asiyefanya chochote aweza kujifanyia jina la kuwa mvivu. Ikikazia ubora wa kujifanyia jina jema, Biblia yasema hivi: “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; na neema [“sifa njema,” NW] kuliko fedha na dhahabu.”—Mithali 22:1.
Mtu hujifanyia jina jema kupitia matendo mengi madogo madogo kwa muda fulani. Ingawa hivyo, huharibiwa kwa tendo moja tu la kipumbavu. Kwa mfano, tendo moja tu la ukosefu wa adili katika ngono, laweza kuharibu sifa njema. Katika sura ya 6 ya kitabu cha Biblia cha Mithali, Mfalme Solomoni wa Israeli ya kale aonya dhidi ya mitazamo na matendo yanayoweza kuharibu sifa yetu na pia kuharibu uhusiano wetu na Yehova Mungu. Baadhi ya hayo ni ahadi za kipumbavu, uvivu, udanganyifu, na ukosefu wa adili katika ngono—mambo ambayo hasa Yehova huchukia. Kutii ushauri huo kutatusaidia kulinda jina letu jema.
Jiondoe Katika Ahadi za Kipumbavu
Sura ya 6 ya Mithali yaanza kwa maneno haya: “Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako, ikiwa wewe na mgeni mmepana mikono, basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe, kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako; Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako.”—Mithali 6:1-3.
Mithali hiyo yaonya dhidi ya kujiingiza katika shughuli za kibiashara za wengine, hasa za wageni. Naam, Waisraeli walipaswa ‘kumsaidia ndugu yao ambaye amekuwa maskini na mkono wake umelegea.’ (Mambo ya Walawi 25:35-38) Lakini Waisraeli fulani wenye kujasiria walijiingiza katika shughuli hatari za kibiashara na kupata mikopo kwa kuwasadikisha wengine ‘wawadhamini,’ hivyo wakiwaachia daraka la deni hilo. Hali kama hizo zaweza kutokea leo. Kwa mfano, huenda mashirika ya fedha yakataka mtiaji-sahihi wa pili kabla ya kuidhinisha mkopo ambao yanaona ni hatari. Ni ukosefu wa busara kama nini kujifunga wajibu huo haraka-haraka kwa niaba ya wengine! Kwani, hilo laweza kutudhuru kifedha, na hata kutuharibia jina katika mabenki na kwa wakopeshaji wengine!
Vipi tukijikuta kwamba tumechukua hatua fulani iliyoonekana yenye hekima mwanzoni lakini baada ya kuichunguza kwa makini twaona ni ya kipumbavu? Ushauri tunaopewa ni kutupilia mbali kiburi na “kumsihi jirani yako”—kwa kutoa ombi tena na tena. Sharti tufanye yote tuwezayo ili kunyoosha mambo. Kichapo kimoja cha marejezo chasema hivi: “Jaribu kila njia hadi ukubaliane na adui yako na kusuluhisha jambo hilo, ili dhamana yako isikudhuru wewe wala familia yako.” Hatua hiyo ichukuliwe pasipo kukawia, kwa maana mfalme aongeza hivi: “Usiache macho yako kupata usingizi, wala kope za macho yako kusinzia. Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, na kama ndege katika mkono wa mtega mitego.” (Mithali 6:4, 5) Ni afadhali kujitoa katika wajibu usiofaa inapowezekana kuliko kunaswa nao.
Uwe na Bidii Kama Chungu
“Ewe mvivu, mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima,” ashauri Solomoni. Twaweza kupata hekima gani kwa njia za chungu mdogo? Mfalme atoa jawabu hili: “Kwa maana yeye hana akida, wala msimamizi, wala mkuu, lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.”—Mithali 6:6-8.
Chungu wana utaratibu wa ajabu na hushirikiana kwa njia yenye kutokeza. Wao hukusanya akiba ya chakula ya wakati ujao pasipo kuamriwa. Wao ‘hawana akida, wala msimamizi, wala mkuu.’ Ni kweli kwamba kuna chungu malkia, lakini umalkia wake ni wa kutaga mayai tu na yeye ndiye mama wa kundi. Yeye hatoi amri zozote. Hata pasipo mnyapara wa kuwaongoza au msimamizi wa kuwaangalia, chungu huendelea kufanya kazi pasipo kuchoka.
Je, sisi nasi hatupaswi kuwa na bidii kama chungu? Kufanya kazi kwa bidii na kujitahidi kuboresha kazi yetu ni jambo zuri kwetu, iwe tunaangaliwa au la. Naam, tuwe shuleni, kazini, na tunaposhiriki utendaji mbalimbali wa kiroho, twapaswa kufanya kadiri ya uwezo wetu. Kama vile chungu apatavyo faida kutokana na bidii yake, ndivyo Mungu atakavyo sisi ‘tujiburudishe kwa mema katika kazi yetu yote.’ (Mhubiri 3:13, 22; 5:18) Dhamiri safi na kuridhika ndizo thawabu za kazi ya bidii.—Mhubiri 5:12.
Akitumia maswali mawili yasiyodai majibu, Solomoni ajaribu kumwamsha mvivu kutoka katika uzembe wake: “Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?” Akisimulia matendo ya mzembe, mfalme aongeza hivi: “Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang’anyi, na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.” (Mithali 6:9-11) Mvivu akiwa usingizini, umaskini humjia upesi kama mnyang’anyi, na uhitaji humshambulia kama mtu mwenye silaha. Mashamba ya mvivu upesi hujaa miiba na viwavi. (Mithali 24:30, 31) Biashara yake hufilisika haraka. Mwajiri atamvumilia mzembe hata lini? Na je, mwanafunzi aliye mvivu kadiri ya kutoweza kujifunza aweza kutarajia kufanikiwa shuleni?
Fuata Haki
Akitoa muhtasari wa tabia nyingine inayoharibu sifa ya mtu katika jumuiya na uhusiano wake na Mungu, Solomoni aendelea kusema hivi: “Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu; huenda njiani mwenye kinywa cha upotofu. Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu, huwaashiria watu kwa vidole vyake. Mna upotofu moyoni mwake, hutunga uovu daima, hupanda mbegu za magomvi.”—Mithali 6:12-14.
Ufafanuzi huo wamhusu mdanganyifu. Kwa kawaida mwongo hujaribu kuficha uwongo wake. Vipi? Si kwa “kinywa cha upotofu” tu bali pia kwa ishara za mwili. Msomi mmoja ataja hivi: “Ishara, sauti, na hata ishara za uso ni mbinu zilizotungwa za udanganyifu; nyuma ya uso unaojifanya kuwa mnyoofu kuna akili potofu na roho ya ugomvi.” Mtu huyo asiyefaa kitu hutunga uovu na husababisha ugomvi nyakati zote. Mambo yatakuwaje kwake?
“Basi msiba utampata kwa ghafula,” ajibu mfalme huyo wa Israeli. “Ghafula atavunjika, bila njia ya kupona.” (Mithali 6:15) Sifa ya mwongo huharibika mara anapofichuliwa. Ni nani atakayemwamini tena? Hatima yake ni mbaya kabisa, kwa maana “waongo wote” wameorodheshwa miongoni mwa wale watakaokumbwa na kifo cha milele. (Ufunuo 21:8) Kwa vyovyote vile, na ‘tujiendeshe wenyewe kwa kufuata haki katika mambo yote.’—Waebrania 13:18.
Chukia Mambo Anayochukia Yehova
Kuchukia mabaya—hicho ni kizuizi kilichoje dhidi ya kufanya matendo yawezayo kuharibu sifa yetu! Basi, je, hatupaswi kusitawisha chuki kwa yaliyo mabaya? Lakini ni mambo gani hasa tunayopaswa kuchukia? Solomoni ataarifu hivi: “Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; moyo uwazao mawazo mabaya; miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; shahidi wa uongo asemaye uongo; naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”—Mithali 6:16-19.
Mambo saba ambayo mithali hii inataja ni ya msingi nayo hujumuisha karibu kila aina ya mabaya. “Macho ya kiburi” na “moyo uwazao mawazo mabaya” ni dhambi zinazofanywa kimawazo. “Ulimi wa uongo” na “shahidi wa uongo asemaye uongo” ni maneno maovu. “Mikono imwagayo damu isiyo na hatia” na “miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu” ni matendo maovu. Yehova huchukia kabisa mtu anayefurahia sana kuchochea ugomvi kati ya watu ambao, pasipo uchochezi huo, wangeishi pamoja kwa amani. Kuongezwa kwa idadi kutoka sita hadi saba hudokeza kuwa orodha hiyo haikusudiwi kuwa kamili, kwa maana wanadamu sikuzote huendelea kuzidisha matendo yao maovu.
Kwa kweli, twahitaji kusitawisha chuki kubwa kwa mambo ambayo Mungu huchukia. Kwa mfano, ni lazima tuepuke “macho ya kiburi” au wonyesho mwingine wowote wa kiburi. Na ni sharti kuepuka porojo yenye kudhuru, kwa sababu inaweza kwa urahisi kuleta “fitina kati ya ndugu.” Kwa kusambaza uvumi mbaya, uchambuzi usio na msingi, au uwongo, huenda tukawa ‘hatumwagi damu isiyo na hatia,’ lakini kwa hakika twaweza kuharibu sifa nzuri ya mtu mwingine.
“Usiutamani Uzuri Wake”
Solomoni aanza sehemu inayofuata ya ushauri wake kwa kusema hivi: “Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, wala usiiache sheria ya mama yako. Yafunge hayo katika moyo wako daima; jivike hayo shingoni mwako.” Sababu gani? “Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, na uamkapo yatazungumza nawe.”—Mithali 6:20-22.
Je, kweli malezi ya Kimaandiko yaweza kutulinda kutokana na mtego wa ukosefu wa adili katika ngono? Ndiyo, yaweza kutulinda. Twathibitishiwa hivi: “Maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, na kukuponya na ubembelezi wa mgeni.” (Mithali 6:23, 24) Kuukumbuka ushauri wa Neno la Mungu na kuutumia kama ‘taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu’ kutatusaidia tukinze utongozaji laini wa mwanamke mbaya, au ule wa mwanamume mbaya.—Zaburi 119:105.
“Usiutamani uzuri wake moyoni mwako,” ashauri mfalme huyo mwenye hekima, “wala usikubali akunase kwa kope za macho yake.” Kwa nini? “Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; na kahaba [“mke wa mwanamume mwingine,” “NW”] humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani.”—Mithali 6:25, 26.
Je, Solomoni amtaja mke mzinzi kuwa kahaba? Labda. Au labda atofautisha matokeo ya kufanya uasherati na kahaba na yale ya kuzini na mke wa mwanamume mwingine. Mtu anayefanya mapenzi na malaya aweza kukumbwa na uhitaji wa “kipande cha mkate”—umaskini hohehahe. Huenda hata akashikwa na magonjwa yanayoambukizwa kingono, yenye maumivu na yenye kudhoofisha, ukiwemo UKIMWI unaoua. Kwa upande mwingine, yule anayetafuta kuzini na mwenzi wa ndoa wa mtu mwingine angekuwa katika hatari kubwa ya papo hapo chini ya Sheria. Mke mzinzi huhatarisha ‘nafsi iliyo na thamani’ ya mwenzi wake wa haramu. “Kuna maana zaidi inayodokezwa . . . kuliko tu kudhoofu kunakofupisha maisha,” kichapo kimoja cha marejezo chasema. “Mtenda-dhambi huyo astahili adhabu ya kifo.” (Mambo ya Walawi 20:10; Kumbukumbu la Torati 22:22) Kwa vyovyote vile, licha ya urembo wake, mwanamke huyo hapasi kutamaniwa.
‘Usiweke Moto Kifuani Pako’
Ili kukazia zaidi hatari ya uzinzi, Solomoni auliza hivi: “Je! mtu aweza kuua [“kuweka,” “Biblia Habari Njema”] moto kifuani pake, na nguo zake zisiteketezwe? Je! mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, na nyayo zake zisiungue?” Akifafanua maana ya kielezi hicho, yeye asema hivi: “Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia.” (Mithali 6:27-29) Mtenda-dhambi huyo sharti ataadhibiwa.
“Watu hawamdharau mwivi, akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa,” twakumbushwa. Ijapokuwa hivyo, “akipatikana, atalipa mara saba; atatoa mali yote ya nyumba yake.” (Mithali 6:30, 31) Katika Israeli ya kale, mwizi alihitajika kulipa, hata kama ingemgharimu mali yake yote.a Basi mzinzi angestahili adhabu kali zaidi, kwa kuwa hana kisingizio cha kutenda hivyo!
“Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa,” asema Solomoni. Mtu asiye na akili hana uamuzi mzuri, kwa kuwa ‘aiangamiza nafsi yake.’ (Mithali 6:32) Huenda akaonekana mwenye sifa nzuri kwa nje, lakini kwa ndani hana kabisa ukomavu unaofaa.
Mzinzi huvuna matunda zaidi ya hayo. “Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; wala fedheha yake haitafutika. Maana wivu ni ghadhabu ya mtu; wala hatahurumia siku ya kujilipiza kisasi. Hatakubali ukombozi uwao wote; wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi.”—Mithali 6:33-35.
Mwizi aweza kulipia alichoiba, lakini mzinzi hawezi kutoa malipo. Ni malipo gani awezayo kumpa mume mwenye hasira? Sihi zozote zile haziwezi kufanya mtenda-dhambi huyo ahurumiwe. Mzinzi huyo hawezi kwa vyovyote kutoa malipo yawezayo kufunika dhambi yake. Suto na aibu inayolikumba jina lake mwenyewe hubaki. Isitoshe, hawezi kwa vyovyote kujitolea fidia au kujiweka huru na adhabu anayostahili.
Ni jambo la hekima kama nini kuepukana kabisa na uzinzi na vilevile mienendo na mitazamo mingine inayoliharibia sifa jina letu jema na inayoweza kumwaibisha Mungu! Basi, na tujihadhari tusifanye ahadi za kipumbavu. Acheni bidii na ukweli zipambe sifa yetu. Na tunapojitahidi kuchukia mambo anayochukia Yehova, na tujifanyie jina jema pamoja naye na vilevile na wanadamu wenzetu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa mujibu wa Sheria ya Kimusa, mwizi alihitajika kulipa mara mbili, mara nne, au mara tano. (Kutoka 22:1-4) Usemi “mara saba” labda wamaanisha kipimo kamili cha adhabu, ambacho kingeweza kuwa mara kadhaa ya kile alichoiba.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Tahadhari kuhusu kuwa mtiaji-sahihi wa pili wa mkopo
[Picha katika ukurasa wa 26]
Uwe na bidii kama chungu
[Picha katika ukurasa wa 27]
Jilinde dhidi ya porojo yenye kudhuru