“Uzishike Amri Zangu Ukaishi”
ALIKUWA kijana, mwenye akili, “mtu mzuri na mwenye uso mzuri.” Mke wa mwajiri wake alikuwa mwenye ashiki tena mshupavu. Alivutiwa na kijana huyo kiasi cha kwamba alishindwa kujizuia, hivyo akajaribu kumshawishi kila siku. “Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami.” Lakini Yosefu, mwana wa mzee wa ukoo Yakobo, aliiacha nguo yake na kumkimbia mke wa Potifa.—Mwanzo 39:1-12.
Bila shaka, si kila mtu ambaye hukwepa hali yenye kushawishi. Kwa mfano, fikiria kijana ambaye Mfalme Solomoni wa Israeli la kale alimwona barabarani usiku. Baada ya kutongozwa na mwanamke mpotovu, “akafuatana naye mara hiyo, kama vile ng’ombe aendavyo machinjoni.”—Mithali 7:21, 22.
Wakristo wanashauriwa ‘waukimbie uasherati.’ (1 Wakorintho 6:18) Paulo alimwandikia hivi Timotheo, mwanafunzi mchanga Mkristo: “Kimbia tamaa zenye kutukia ujanani.” (2 Timotheo 2:22) Tunapokabili hali zinazotushawishi kufanya uasherati, uzinzi, au makosa mengine ya kiadili, lazima sisi pia tuazimie kukimbia kama vile Yosefu alivyomkimbia mke wa Potifa. Ni nini kitakachotusaidia kuazimia kufanya hivyo? Katika sura ya 7 ya kitabu cha Biblia cha Mithali, Solomoni atutolea shauri lenye thamani sana. Mbali na kuzungumzia mafundisho ambayo hutulinda na hila za watu wasio na maadili, Solomoni pia anafunua njia wanazotumia kwa kueleza waziwazi tukio ambapo kijana atongozwa na mwanamke mpotovu.
‘Funga Amri Zangu Katika Vidole Vyako’
Mfalme aanza na shauri hili lililo kama la baba: “Mwanangu, yashike maneno yangu, na kuziweka amri zangu akiba kwako. Uzishike amri zangu ukaishi, na sheria yangu kama mboni ya jicho lako.”—Mithali 7:1, 2.
Wazazi, hasa akina baba, wana daraka walilopewa na Mungu la kufundisha watoto wao viwango vya Mungu vya mema na mabaya. Musa aliwahimiza akina baba hivi: “Maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.” (Kumbukumbu la Torati 6:6, 7) Naye mtume Paulo aliandika hivi: “Nanyi, akina baba, msiwe mkiwasumbua watoto wenu, bali endeleeni kuwalea katika nidhamu na rekebisho la akilini la Yehova.” (Waefeso 6:4) Kwa hiyo, maagizo ya mzazi yanayopasa kuthaminiwa sana, bila shaka yatia ndani, vikumbusha, amri, na sheria zilizo katika Neno la Mungu, Biblia.
Mafundisho ya mzazi yaweza kutia ndani pia kanuni nyinginezo—sheria za familia. Hizo ni za kuwafaidi washiriki wa familia. Ni kweli kwamba ikitegemea mahitaji, sheria zaweza kutofautiana kati ya familia mbalimbali. Hata hivyo, wazazi wana wajibu wa kuamua ni nini kinachofaa zaidi familia yao. Na kwa kawaida sheria wanazoweka hudhihirisha upendo na hangaiko lao la kweli. Vijana wanashauriwa kufuata kanuni hizo pamoja na mafundisho ya Maandiko wanayopokea kutoka kwa wazazi wao. Naam, kuna uhitaji wa kuona maagizo hayo “kama mboni ya jicho lako”—kuyalinda kadiri uwezavyo. Hiyo ndiyo njia ya kuepuka matokeo yenye kuleta kifo ya kupuuza viwango vya Yehova—na hivyo “kuishi.”
“Zifunge [amri zangu] katika vidole vyako,” Solomoni aendelea kusema, “ziandike juu ya kibao cha moyo wako.” (Mithali 7:3) Kama vile vidole, ambavyo sisi huviona daima na ambavyo ni vya maana katika kutekeleza makusudi yetu, ndivyo na masomo tuliyojifunza tangu utotoni kutoka kwa Maandiko au kupitia ujuzi wa Biblia yapasavyo kutukumbusha na kutuongoza daima katika yote tufanyayo. Twapaswa kuyaandika katika bamba la moyo wetu, na kuyafanya kuwa sehemu yetu.
Mfalme akazia umuhimu wa hekima na ufahamu kwa kuhimiza hivi: “Mwambie hekima, Wewe ndiwe umbu langu; mwite ufahamu jamaa yako mwanamke.” (Mithali 7:4) Hekima ni uwezo wa kutumia ujuzi tuliopewa na Mungu kwa njia ifaayo. Twapaswa kuipenda hekima kama dada anayependwa sana. Uelewevu ni nini? Ni uwezo wa kuchunguza jambo na kupata maana yake kwa kuelewa jinsi ambavyo sehemu zake mbalimbali zinahusiana na jambo lote zima. Yatupasa kupenda uelewevu kama vile tupendavyo rafiki wa karibu.
Kwa nini tushikamane sana na mafundisho ya Kimaandiko na kupenda hekima na uelewevu? Ili ‘tujilinde wenyewe na malaya, na mgeni atubembelezaye kwa maneno yake.’ (Mithali 7:5) Naam, kufanya hivyo kutatulinda na njia zenye udanganyi na ushawishi za mgeni—mtu asiye na maadili.a
Kijana Akutana na ‘Mwanamke Mwerevu’
Baada ya hapo mfalme wa Israeli aeleza hali ambayo amejionea mwenyewe: “Maana katika dirisha la nyumba yangu nalichungulia katika shubaka yake; nikaona katikati ya wajinga, nikamtambua miongoni mwa vijana, kijana mmoja asiyekuwa na akili, akipita njiani karibu na pembe yake, akiishika njia iendayo nyumbani kwake, wakati wa magharibi, wakati wa jioni, usiku wa manane, gizani.”—Mithali 7:6-9.
Solomoni alichungulia kutoka kwenye dirisha lililokuwa na kiunzi cha fito—labda muundo wenye fito zilizokingamana na michongo iliyonakshiwa sana. Utusitusi unapotoweka, barabara zaanza kuwa na giza. Aona kijana anayeweza kudhuriwa kwa urahisi. Hana akili kwa sababu amekosa ufahamu au busara. Yaelekea anajua ujirani huo ukoje na kile kinachoweza kumpata akiwa mle. Kijana huyo yuaja karibu na “pembe yake,” iliyo njiani kuelekea nyumbani kwa mwanamke. Mwanamke huyo ni nani? Anakusudia kufanya nini?
Mfalme mwenye uelekevu aendelea kusema: “Tazama, mwanamke akamkuta, ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; ana kelele [“machachari,” “NW”], na ukaidi; miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, naye huotea kwenye pembe za kila njia.”—Mithali 7:10-12.
Mvao wa mwanamke huyu waonyesha waziwazi yeye ni mwanamke wa aina gani. (Mwanzo 38:14, 15) Amevalia bila kiasi kama kahaba. Zaidi ya hayo, ni mwerevu wa moyo—ana akili “yenye hila na makusudio ya ujanja.” Ni machachari tena mkaidi, mzungumzaji tena mshupavu, mwenye kelele tena mgumu, mjasiri tena mfidhuli. Badala ya kukaa nyumbani, anapendelea kutembea mahali pa umma mara nyingi, akiotea pembeni mwa barabara ili kunasa windo lake. Anangojea mtu fulani kama yule kijana.
‘Ushawishi Mwingi’
Hivyo kijana akutana na mwanamke mpotovu mwenye mpango wa hila. Lazima Solomoni awe alizingatia jambo hilo kwa makini kama nini! Asema hivi: “Akamshika, akambusu, akamwambia kwa uso usio na haya, kwangu ziko sadaka za amani; leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; ndiyo maana nikatoka nikulaki, nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona.”—Mithali 7:13-15.
Midomo ya mwanamke huyu ni laini. Akiwa na uso usio na haya, asema maneno yake kwa uhakika. Maneno yote anayosema yamefikiriwa vizuri ili kumshawishi kijana huyo. Kwa kusema kwamba ametoa sadaka za amani siku hiyohiyo na kulipa nadhiri zake, anajionyesha kuwa mwadilifu, akidokeza kwamba hali yake ya kiroho si mbaya. Sadaka za amani kwenye hekalu katika Yerusalemu zilitia ndani nyama, unga, mafuta, na divai. (Mambo ya Walawi 19:5, 6; 22:21; Hesabu 15:8-10) Kwa kuwa mwenye kutoa sadaka angeweza kuchukua sehemu fulani ya sadaka za amani kwa ajili yake na familia yake, anadokeza kwamba ana chakula na vinywaji vya kutosha nyumbani. Dokezo hilo ni wazi: Kijana huyo angejifurahisha huko. Ametoka nyumbani mwake kwa kusudi la kumtafuta yeye hasa. Inasikitisha kama nini—ikiwa yeyote angeweza kuamini maneno hayo. “Ni kweli kwamba alikuwa akimtafuta mtu fulani,” asema msomi mmoja wa Biblia, “lakini je, kwa kweli alikuwa amekuja kumtafuta kijana huyuhuyu hasa? Ni mpumbavu tu—labda kijana huyu—ndiye ambaye angemwamini.”
Baada ya kujipamba ili avutie kwa mavazi yake, kwa maneno yake ya kurairai, kwa kumbatio, na kwa busu, mwanamke huyo mwenye utongozi atumia manukato. Asema hivi: “Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. Nimetia kitanda changu manukato, manemane na udi na mdalasini.” (Mithali 7:16, 17) Amerembesha kitanda chake kwa kutumia matandiko mazuri kutoka Misri na kukitia manukato mazuri ya manemane, udi, na mdalasini.
“Haya, na tushibe upendo hata asubuhi,” aendelea kusema, “tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.” Hamwaliki tu kula mlo mkuu wa siku ulio mtamu wakiwa wawili. Amwahidi kufurahia uhusiano wa kingono. Ombi hilo lamsisimua kijana huyo na analiona kuwa jambo la kujasiria! Anamchochea zaidi kwa kuongezea hivi: “Maana mume wangu hayumo nyumbani, amekwenda safari ya mbali; amechukua mfuko wa fedha mkononi; atarudi wakati wa mwezi mpevu.” (Mithali 7:18-20) Amhakikishia kwamba atakuwa salama kabisa, kwa kuwa mume wake ameenda safari ya kibiashara na hatarajii arudi karibuni. Jinsi alivyo na kipawa cha kumdanganya kwa werevu kijana! “Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.” (Mithali 7:21) Ingehitaji mtu awe na nguvu za kiadili kama Yosefu ili kukinza mwaliko huo wa utongozi. (Mwanzo 39:9, 12) Je, kijana huyu ana nguvu za kiadili zinazohitajika?
‘Kama Ng’ombe Aendaye Machinjoni’
“Huyo akafuatana naye mara hiyo,” aripoti Solomoni, “kama vile ng’ombe aendavyo machinjoni; au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu; hata mshale umchome maini; kama ndege aendaye haraka mtegoni; wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.”—Mithali 7:22, 23.
Kijana huyo ashindwa kukataa mwaliko huo. Huku akipuuza busara, anamfuata ‘kama ng’ombe aendaye machinjoni.’ Kama vile mtu aliyefungwa pingu miguuni asivyoweza kutoroka adhabu yake, ndivyo kijana huyo anavyovutwa kwenye dhambi. Haoni hatari yote iliyopo mpaka “mshale umchome maini,” yaani mpaka apate kidonda kinachoweza kumwua. Kifo hicho chaweza kuwa cha asili katika maana ya kwamba anaweza kupatwa na maradhi yanayoambukizwa kingono ambayo huua.b Kidonda hicho chaweza pia kuharibu kabisa hali yake ya kiroho; ‘chahusisha nafsi yake mwenyewe.’ Yeye mwenyewe na maisha yake yameathiriwa sana, na amemkosea sana Mungu. Hivyo anakimbia katika kifo kama ndege aendaye mtegoni!
‘Usizielekee Njia Zake’
Kwa kujifunza kutokana na yale aliyoona, mfalme mwenye hekima ahimiza hivi: “Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, mkayaangalie maneno ya kinywa changu. Moyo wako usizielekee njia zake, wala usipotee katika mapito yake. Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, naam, jumla ya waliouawa naye ni jeshi kubwa. Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, hushuka mpaka vyumba vya mauti.”—Mithali 7:24-27.
Kwa wazi, Solomoni atushauri tuepuke njia zenye kuleta kifo za mtu asiye na adili na ‘kuendelea kuishi.’ (Mithali 7:2) Shauri hilo linafaa wakati wetu kama nini! Kwa hakika kuna uhitaji wa kuepuka sehemu ambazo hutembelewa mara kwa mara na watu wanaootea ili kunasa wengine. Kwa nini unaswe na mbinu zao kwa kwenda mahali kama hapo? Kwa kweli, kwa nini uwe mmoja wa ‘wasio na akili’ na kutangatanga katika njia za “mgeni”?
“Mgeni” ambaye mfalme aliona alimtongoza kijana kwa kumwalika ‘wajifurahishe nafsi zao kwa mahaba.’ Je, vijana wengi—hasa wasichana—hawajadanganywa kwa njia kama hiyo? Lakini fikiria jambo hili: Mtu fulani anapojaribu kukutongoza ujihusishe na mwenendo usiofaa kingono, je, huo ni upendo halisi au ni uchu wa kibinafsi? Kwa nini mwanamume anayempenda mwanamke kikweli amsonge kukiuka dhamiri yake na mafunzo ya Kikristo aliyopata? ‘Moyo wako usizielekee’ njia hizo, ashauri Solomoni.
Kwa kawaida maneno ya mwanamke mwenye utongozi huwa laini na yaliyofikiriwa vizuri. Kuwa na busara na uelewevu kutatusaidia kuelewa ujanja wake. Kutosahau kamwe yale ambayo Yehova ametuamuru kutatulinda. Kwa hiyo, sikuzote na tujitahidi ‘kufuliza kushika amri za Mungu na kuendelea kuishi,’ hata milele.—1 Yohana 2:17.
[Maelezo ya Chini]
a Neno “mgeni” lilitumika kwa watu waliojitenga na Yehova kwa kutoshika Sheria. Hivyo, mwanamke asiye na maadili, kama vile kahaba, anaitwa “mgeni.”
b Maradhi fulani yanayoambukizwa kingono huharibu ini. Kwa mfano, kaswende inapokomaa, hufanya ini lilemewe na bakteria. Navyo vijidudu vinavyosababisha kisonono vyaweza kufanya ini livimbe.
[Picha katika ukurasa wa 29]
Unaonaje sheria za wazazi?
[Picha katika ukurasa wa 31]
Kushika amri za Mungu kwamaanisha uhai