Kitabu Cha Biblia Namba 22—Wimbo Ulio Bora
Mwandikaji: Sulemani
Mahali Kilipoandikiwa: Yerusalemu
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 1020 K.W.K.
1. Ni katika njia gani huu ni “Wimbo wa nyimbo”?
“ULIMWENGU wote haukustahiki siku ambayo katika hiyo Wimbo bora huu ulipopewa kwa Israeli.” Ndivyo “rabbi” wa Kiyahudi Akiba, aliyeishi katika karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida, alivyoeleza uthamini wake wa Wimbo Ulio Bora.a Kichwa cha kitabu hicho ni ufupizo wa maneno ya ufunguzi “Wimbo ulio bora, wa Sulemani.” Kulingana na maandishi ya neno kwa neno ya Kiebrania, ndio “Wimbo wa nyimbo,” kuonyesha upeo wa uzuri, sawa na usemi “mbingu za mbingu,” kumaanisha mbingu za juu zaidi. (Kum. 10:14) Huu si mkusanyo wa nyimbo bali wimbo mmoja, “wimbo wa ukamilisho kabisa, mojapo bora zaidi zilizopata kuwapo, au zilizopata kuandikwa.”b
2. (a) Ni nani aliyekuwa mwandikaji wa Wimbo Ulio Bora, sifa zake zilikuwa nini, na ni kwa nini kitabu hicho kingeweza kuitwa wimbo wa upendo usiofaulu? (b) Kitabu hicho kiliandikiwa wapi, na lini?
2 Mfalme Sulemani wa Yerusalemu ndiye aliyekuwa mwandikaji wa wimbo huu, kama inavyoonyeshwa na utangulizi wacho. Yeye alistahili sana kukiandika kielelezo hiki cha ushairi wa Kiebrania chenye uzuri wa juu zaidi. (1 Fal. 4:32) Hili ni shairi la hadithi lenye kujaa maana na lenye kupendeza sana katika usimulizi walo wa uzuri. Msomaji awezaye kuwazia kikao cha Nchi za Mashariki atathamini hilo hata zaidi. (Wim. 4:11, 13; 5:11; 7:4) Pindi ya kuliandika ilikuwa ya pekee sana. Mfalme mkuu Sulemani, aliyetukuka katika hekima, hodari wa nguvu, na mwenye kustaajabisha katika mng’ao wa utajiri wake wa kimwili, jambo lililovutia hata malkia wa Sheba, alishindwa kuvutia msichana wa kawaida wa mashambani ambaye alimwonea mapenzi. Kwa sababu ya udumifu wa upendo wake kwa ajili ya mvulana mchungaji, mfalme alishindwa. Kwa hiyo, kitabu hiki, kwa kufaa kingeweza kuitwa Wimbo wa Sulemani wa Upendo Usiofaulu. Yehova Mungu alimpulizia atunge wimbo huu kwa ajili ya mafaa ya wasomaji wa Biblia wa vizazi vya baadaye. Aliuandika katika Yerusalemu. Labda hiyo ilikuwa karibu 1020 K.W.K., miaka kadhaa baada ya hekalu kukamilika. Kufikia wakati alioandika wimbo huu, Sulemani alikuwa “na malkia sitini, na masuria themanini,” ikilinganishwa “na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu,” mwishoni mwa utawala wake.—Wim. 6:8; 1 Fal. 11:3.
3. Kuna uthibitisho gani juu ya Wimbo Ulio Bora kuwa sehemu ya maandiko?
3 Kukubaliwa kwa Wimbo Ulio Bora hakukubishwa hata katika nyakati za mapema. Kilionwa kuwa kisehemu halisi na kilichopuliziwa na Mungu cha maandiko ya Kiebrania muda mrefu kabla ya Wakati wa Kawaida. Kilitiwa ndani ya Septuagint ya Kigiriki. Yosefo alikitia katika orodha ya vitabu vitakatifu. Kwa hiyo, kina uthibitisho ule ule wa kukubaliwa kama unaokuwapo kwa kawaida kwa kitabu kinginecho chote cha Maandiko ya Kiebrania.
4. (a) Je! kutokuwapo kwa neno “Mungu” kunapinga kukubaliwa kwa kwa Wimbo Ulio Bora? (b) Ni nini kinachokitofautisha kiwe na mahali pacho pa pekee katika maandiko ya Biblia?
4 Hata hivyo, wengine wametilia shaka kukubaliwa kwa kitabu hicho kwa msingi wa kwamba hakuna rejezo kwa Mungu ndani yacho. Kutokuwapo kwa mtajo wowote wa Mungu hakungefanya kitabu hiki kisistahili kama vile kule kuwapo tu kwa neno “Mungu” kusingekifanya kikubaliwe. Jina la Mungu laonekana kwa namna ya ufupizo kwenye sura ya 8, mstari wa 6, ambapo upendo wasemekana kuwa “miali ya Yahu.” Bila shaka kitabu hiki chafanyiza sehemu ya maandishi yale ambayo Yesu Kristo alirejezea kwa kibali aliposema: “Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna [mtapata, NW] uzima wa milele.” (Yn. 5:39) Zaidi ya hayo, picha (wazo) yacho yenye nguvu ya sifa kamili ya upendo wa watu wawili, kama ule uliopo, kwa maana ya kiroho, baina ya Kristo na “Bibi-arusi” wake, hutofautisha Wimbo Ulio Bora kiwe na mahali pacho pa pekee katika maandiko ya Biblia yanayokubaliwa.—Ufu. 19:7, 8; 21:9.
YALIYOMO KATIKA WIMBO ULIO BORA
5. (a) Wahusika katika drama hii watambulishwaje? (b) Ni habari gani yenye kugusa inayoelezwa?
5 Habari iliyomo katika kitabu hiki imetolewa kupitia mfululizo wa mazungumzo. Daima kuna badiliko la wanenaji. Watu wenye sehemu za kunena ni Sulemani mfalme wa Yerusalemu, mchungaji, Mshulami wake mpendwa, ndugu zake, mabibi wa baraza (“binti za Yerusalemu”), na wanawake wa Yerusalemu (“binti za Sayuni”). (Wim. 1:5-7; 3:5, 11) Wanatambulishwa na yale wanayosema juu yao wenyewe au kwa yale yanayosemwa juu yao. Drama yaanza karibu na Shunemu, au Shulemu, ambako Sulemani amepiga kambi pamoja na msafara wake wa baraza. Yaonyesha habari yenye kugusa moyo—upendo wa msichana wa mashambani wa kijiji cha Shunemu kwa mwenzi wake mchungaji.
6. Ni mazungumzo gani yanayoendelea kati ya mwanamwali na mabibi wa baraza wa kambi ya Sulemani?
6 Mwanamwali Mshulami katika kambi ya Sulemani (1:1-14). Mwanamwali huyo atokea katika mahema ya kifalme ambako mfalme amemleta, lakini yeye ahangaikia tu kuona mpenzi wake mchungaji. Akitamani mpendwa wake, anena kama kwamba yupo. Mabibi wa baraza wanaomhudumia mfalme, “binti za Yerusalemu,” wamtazama Mshulami kiajabu-ajabu kwa sababu ya ngozi yake nyeusi-nyeusi. Aeleza kwamba yeye amechomwa na jua kwa sababu ya kutunza mashamba ya mizabibu ya nduguze. Kisha anena kwa mpenzi wake kama kwamba yuko huru na kuuliza ni wapi angempata. Mabibi wa baraza wamhimiza aende na kulisha kundi lake la wanyama kando ya mahema ya wachungaji.
7. Ni utongozi gani anaofanya Sulemani, lakini kukiwa na tokeo gani?
7 Sulemani ajitokeza. Hana nia ya kumruhusu aende. Asifu urembo wake na kuahidi kumpamba kwa “mashada ya dhahabu” na “vifungo vya fedha.” Mshulami akinza utongozi wake na kumjulisha kwamba upendo pekee anaoweza kuona ni kwa ajili ya mpendwa wake.—1:11.
8. Mpenzi wa mwanamwali huyo amtiaje moyo? Mshulami atamani nini?
8 Mpenzi mchungaji atokea (1:15–2:2). Mpenzi wa Mshulami aingia ndani ya kambi ya Sulemani na kumtia moyo. Amhakikishia Mshulami upendo wake. Mshulami atamani ukaribu wa mpenzi wake na raha tu ya kukaa pamoja naye makondeni na maporini.
9. Ni jinsi gani msichana huyo na mpenzi wake wanavyokadiri urembo wake?
9 Mshulami ni msichana mwenye kiasi. “Mimi ni ua la uwandani,” asema. Mpenzi wake mchungaji afikiri kuwa yeye hana kifani, akisema: “Kama nyinyoro kati ya miiba, kadhalika mpenzi wangu kati ya binti.”—2:1, 2.
10. Mwanamwali huyo akumbuka nini kuhusu upendo wake?
10 Mwanamwali atamani mchungaji wake (2:3–3:5). Akiwa ametenganishwa tena na mpenzi wake, Mshulami aonyesha jinsi anavyomstahi zaidi ya wengine wote, na awaambia mabinti wa Yerusalemu kwamba wako chini ya kiapo cha kutojaribu kuamsha ndani yake upendo usiotakwa kwa ajili ya mwingine. Mshulami akumbuka wakati mchungaji wake alipojibu wito wake na kumwalika kwenye vilima wakati wa vuli. Amwona akikwea juu ya milima, akishangilia. Amsikia akimwita: “Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako.” Hata hivyo, ndugu zake, ambao hawakuwa na uhakika juu ya uimara wake, wakakasirika na kumpa kazi ya kulinda mashamba ya mizabibu. Mshulami ajulisha rasmi, “Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake,” na amsihi aharakishe kuja kando yake.—2:13, 16.
11. Mshulami akumbusha tena mabinti wa Yerusalemu juu ya kiapo gani?
11 Mshulami aeleza kuzuiwa kwake katika kambi ya Sulemani. Usiku akiwa kitandani, atamani mchungaji wake. Kwa mara nyingine akumbusha mabinti wa Yerusalemu kwamba wako chini ya kiapo cha kutoamsha upendo usiotakwa ndani yake.
12. Mpenzi wake atoa kitia-moyo gani zaidi wakati mwanamwali huyo apelekwapo kwa Sulemani kule Yerusalemu?
12 Mshulami katika Yerusalemu (3:6–5:1). Sulemani arejea Yerusalemu kwa uzuri wa kifalme, na watu wastaajabia msafara wake. Katika saa hii ya maana sana, mchungaji mpenzi hamwachi Mshulami. Amfuata msichana mwenziye, ambaye amewekwa shela, na awasiliana naye. Amtia nguvu mpendwa wake kwa semi changamfu za kipenzi. Mshulami amwambia ataka kuwa huru na kuondoka kwenye jiji hilo, na kisha mchungaji amimina maneno ya furaha tele ya upendo: “Mpenzi wangu, u mzuri pia pia.” (4:7) Kumtupia jicho Mshulami tu kwafanya moyo wake udunde haraka zaidi. Semi za kipenzi za Mshulami ni bora zaidi ya divai, harufu yake ni kama ile ya Lebanoni, na ngozi yake ni kama paradiso ya makomamanga. Mwanamwali huyo amwalika mpenzi wake aingie “bustanini mwake,” naye akubali. Wanawake wenye urafiki wa Yerusalemu wawatia moyo: “Kaleni, rafiki zangu, kanyweni, naam, nyweni sana, [semi za kipenzi, NW] wapendwa wangu.”—4:16; 5:1.
13. Ni ndoto gani anayoota mwanamwali, naye aelezaje juu ya mpenzi wake kwa mabibi wa baraza?
13 Ndoto ya mwanamwali (5:2–6:3). Mshulami aambia mabibi wa baraza juu ya ndoto, ambayo katika hiyo asikia mbisho. Mpenzi wake yuko nje, akisihi amruhusu aingie. Lakini yuko kitandani. Hatimaye ainukapo akafungue mlango, ametokomea usiku. Amfuata, lakini haonekani. Walinzi wamtendea vibaya. Awaambia mabibi wa baraza kwamba kama wakimwona mpenzi wake, wana wajibu wa kumwambia kwamba yeye Mshulami ni mgonjwa mapenzi. Wao wamwuliza ni nini kinachofanya mchungaji awe maalumu hivyo. Aeleza juu yake kwa maneno mengi, akisema yeye “ni mweupe, tena mwekundu, mashuhuri miongoni mwa elfu kumi.” (5:10) Wanawake hao wa baraza wamwuliza mahali aliko mchungaji. Mshulami asema ameenda kuchunga miongoni mwa mabustani.
14. Ijapokuwa ufundi wake wote, Sulemani ashindwaje katika jaribio lake?
14 Utongozi wa mwisho wa Sulemani (6:4–8:4). Mfalme Sulemani amkaribia Mshulami. Kwa mara nyingine amwambia jinsi alivyo mrembo, mwenye kupendeza zaidi ya “malkia sitini, na masuria themanini,” lakini Mshulami amkataa. (6:8) Yuko hapo tu kwa sababu shughuli ya kutumwa ilikuwa imemleta karibu na kambi yake. ‘Kwani wanitazama?’ auliza. Sulemani afanya werevu wa kutumia swali la Mshulami lenye nia safi ili kumwambia juu ya urembo wake, tangu nyayo za miguu yake hadi kipaji cha kichwa chake, lakini mwanamwali huyo apinga ujanja wake wote. Kwa moyo mkuu ajulisha rasmi ujitoaji wake kwa mchungaji wake, akimpaazia sauti. Kwa mara ya tatu, akumbusha mabinti wa Yerusalemu kwamba wako chini ya kiapo cha kutoamsha upendo ndani yake bila ya yeye kutaka hivyo. Sulemani amruhusu aende nyumbani. Ameshindwa katika jitihada yake ya kupata upendo wa Mshulami.
15. (a) Mwanamwali huyo arejea kwa ndugu zake akiwa na ombi gani? (b) Ujitoaji kamili umeshindaje?
15 Mshulami arejea (8:5-14). Ndugu zake wamwona akikaribia, lakini hayuko peke yake, ‘amtegemea mpendwa wake.’ Mshulami akumbuka alikutana na mpenzi wake chini ya mtofaa na kujulisha rasmi upendo wake usiovunjika kwa ajili ya mchungaji. Baadhi ya maelezo ya mapema ya ndugu zake juu ya hangaiko lao kumhusu alipokuwa “umbu mdogo” yatajwa, lakini yeye ajulisha rasmi amejithibitisha kuwa mwanamke mkomavu na imara. (8:8) Sasa ndugu zake na wakubali ndoa yake. Mfalme Sulemani akae na utajiri wake! Yeye ameridhika na shamba lake moja la mizabibu, kwa maana apenda mmoja ambaye ni mpenzi kwake peke yake. Katika kisa chake upendo huo ni wenye nguvu kama kifo na miako yake kama “mwali wa Yah.” Msisitizo juu ya ujitoaji kamili “usioachilia kama Sheoli” umeshinda na kuongoza kwenye vilele vitukufu vya muungano pamoja na mpenzi wake mchungaji.—8:5, 6, NW.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
16. Ni masomo gani yenye thamani yanayofundishwa katika wimbo huu?
16 Ni masomo gani yanayofundishwa katika wimbo huu wa upendo yanayoweza kunufaisha mtu leo? Uaminifu, uaminifu-mshikamanifu, na ukamilifu kwa kanuni za kimungu vyaonyeshwa waziwazi. Wimbo huo wafundisha urembo wa wema na nia safi katika mpenzi wa kweli. Wafundisha kwamba upendo halisi hubaki ukiwa usioweza kushindika, usioweza kuzimika, usioweza kununulika. Wanaume na wanawake vijana Wakristo na pia waume na wake waweza kunufaika na kielelezo hiki cha kufaa cha ukamilifu wakati majaribu yatokeapo na vishawishi kujitokeza.
17. (a) Paulo aonyeshaje wimbo huu uliandikwa kwa ajili ya kuagiza kundi la Kikristo? (b) Ni kwa nini yawezekana Paulo alikuwa akiufikiria katika kuandikia Wakorintho na Waefeso? (c) Ni ulinganishi gani mbalimbali wenye kupendeza unaoweza kufanywa pamoja na maandishi yaliyopuliziwa na Mungu ya Yohana?
17 Lakini wimbo huu uliopuliziwa na Mungu ni wenye mafaa kabisa pia kwa ajili ya kundi la Kikristo kwa ujumla. Ulitambuliwa kuwa sehemu ya Maandiko yenye pumzi ya Mungu na Wakristo wa karne ya kwanza, ambao mmoja wao aliandika hivi: “Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini.” (Rum. 15:4) Mwandikaji uyo huyo aliyepuliziwa na Mungu, Paulo, angeweza kuwa alikuwa anafikiria upendo kamili wa msichana Mshulami kwa mchungaji wake alipoandikia hivi kundi la Kikristo: “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.” Paulo pia aliandika juu ya upendo wa Kristo kwa ajili ya kundi kama ule wa mume kwa mke. (2 Kor. 11:2; Efe. 5:23-27) Si kwamba tu Yesu Kristo ndiye Mchungaji Mwema wao bali pia ndiye Mfalme wao anayewatolea wafuasi wake wapakwa mafuta shangwe isiyoelezeka ya “ndoa” pamoja naye katika mbingu.—Ufu. 19:9, NW; Yn. 10:11.
18. Ni katika njia gani wafuasi wapakwa mafuta wa Kristo Yesu waweza kunufaika na kielelezo cha msichana Mshulami?
18 Hakika wafuasi wapakwa mafuta hawa wa Kristo Yesu waweza kunufaika sana na kielelezo cha msichana Mshulami. Pia lazima wawe waaminifu-washikamanifu katika upendo wao, wasinaswe na mmeremeto wa mali za ulimwengu, wakidumisha usawaziko katika ukamilifu wao hadi wafikie thawabu yao. Wamekaza akili zao kwenye mambo yaliyo juu na ‘hutafuta kwanza Ufalme.’ Wakaribisha mapenzi ya upendo ya Mchungaji wao, Yesu Kristo. Wanaona shangwe kubwa kwa kujua mpendwa huyu, ingawa haonekani, yuko karibu kando yao, akiwatolea wito wajipe moyo mkuu na kuushinda ulimwengu. Wakiwa na upendo huo usiozimika, wenye nguvu kama “miali ya Yahu,” kwa ajili ya Mfalme Mchungaji wao, bila shaka watashinda na kuungana naye wakiwa warithi wenzi katika Ufalme mtukufu wa mbingu. Hivyo jina la Yah litatakaswa!—Mt. 6:33, NW; Yn. 16:33.
[Maelezo ya Chini]
b Commentary cha Clarke, Buku 3, ukurasa 841.