Sura ya 14
Yehova Anyenyekeza Jiji Lenye Kujigamba
1. Kitabu cha Isaya sasa chaeleza kadiri gani mambo yatakayotukia?
KITABU cha unabii cha Isaya kiliandikwa katika karne ya nane K.W.K., Ashuru ilipokuwa ikivamia Bara Lililoahidiwa. Kama tulivyoona katika sura zilizotangulia za kitabu chake, Isaya atabiri kwa usahihi kabisa jinsi mambo yatakavyotukia. Hata hivyo, kitabu hicho chaeleza mambo yanayotukia hata baada ya wakati wa mamlaka ya Ashuru. Chatabiri juu ya kurudi kwa watu wa agano wa Yehova kutoka uhamishoni katika nchi nyingi, kutia ndani Shinari, lilipo jiji la Babiloni. (Isaya 11:11) Katika Isaya sura ya 13, mna unabii maarufu ambao, utakapotimizwa, utawezesha kurudi huko. Unabii huo waanza kwa maneno haya: “Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi.”—Isaya 13:1.
‘Nitashusha Kiburi’
2. (a) Hezekia aja kushirikianaje na Babiloni? (b) “Bendera” itakayoinuliwa ni nini?
2 Yuda yaanza kushirikiana na Babiloni wakati wa maisha ya Isaya. Mfalme Hezekia awa mgonjwa sana kisha apona. Mabalozi kutoka Babiloni waja ili wampongeze baada ya kupata nafuu, labda wakiwa na lengo la kisiri la kutafuta kuungwa mkono na Hezekia katika vita vyao dhidi ya Ashuru. Mfalme Hezekia awaonyesha hazina zake zote, jambo ambalo si la busara. Kwa sababu hiyo Isaya amwambia Hezekia kuwa baada ya kifo cha mfalme huyo, mali hizo zote zitachukuliwa mpaka Babiloni. (Isaya 39:1-7) Hilo latimizwa mwaka wa 607 K.W.K., Yerusalemu liharibiwapo na taifa hilo kupelekwa uhamishoni. Hata hivyo, watu wa Mungu waliochaguliwa hawataishi Babiloni milele. Yehova atabiri jinsi atakavyowafungulia njia ya kurudi nyumbani. Aanza hivi: “Haya! juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu.” (Isaya 13:2) “Bendera” ni serikali ya ulimwengu inayoinuka ambayo itapindua Babiloni kutoka mahali pake palipoinuka. Itainuliwa “juu ya mlima usio na miti”—mahali paonekanapo waziwazi kutoka mbali. Huku ikiwa imeitwa ije ishambulie Babiloni, serikali hiyo mpya ya ulimwengu itaingia kwa nguvu katika “malango ya wakuu,” malango ya jiji hilo kubwa, nayo italishinda.
3. (a) Ni nani “waliowekwa wakfu” ambao Yehova atainua? (b) Majeshi ya kipagani ‘yamewekwaje wakfu’?
3 Sasa Yehova asema: “Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kutakabari. Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; BWANA wa majeshi anapanga jeshi kwa vita.” (Isaya 13:3, 4) Ni nani hao “waliowekwa wakfu” ambao wameteuliwa kuangusha jiji la Babiloni lenye kiburi? Ni majeshi ya mataifa yaliyoungana, “mataifa waliokutana pamoja.” Wanashuka dhidi ya Babiloni kutoka nchi ya milima-milima. “Watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu.” (Isaya 13:5) Wamewekwaje wakfu? Pasipo shaka si katika maana ya kuwa watakatifu. Hayo ni majeshi ya kipagani ambayo hayapendi hata kidogo kumtumikia Yehova. Hata hivyo, katika Maandiko ya Kiebrania, usemi “-liowekwa wakfu” humaanisha “-liotengwa ili kutumiwa na Mungu.” Yehova aweza kuweka wakfu majeshi ya mataifa na kutumia tamaa yao ya kujitakia makuu ili kudhihirisha hasira yake. Aliitumia Ashuru kwa njia hiyo. Ataitumia milki ya Babiloni vivyo hivyo. (Isaya 10:5; Yeremia 25:9) Naye atayatumia mataifa mengine kuadhibu Babiloni.
4, 5. (a) Yehova atabiri nini kuhusu Babiloni? (b) Wale wanaoshambulia Babiloni watalazimika kukabiliana na nini?
4 Babiloni bado haijawa serikali kubwa ya ulimwengu. Ingawa hivyo, akimtumia Isaya kutangaza, Yehova aona kimbele wakati ambapo Babiloni itakuwa serikali ya ulimwengu, naye atabiri kuanguka kwake. Asema: “Pigeni kelele za hofu; maana siku ya BWANA [“Yehova,” “NW”] i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu.” (Isaya 13:6) Naam, majisifu ya Babiloni yatakwisha na yageuke kuwa kilio cha maumivu makali. Kwa nini? Kwa sababu ya ‘siku ya Yehova,’ siku ambayo Yehova atamhukumu.
5 Ingawa hivyo, itawezekanaje jiji la Babiloni liangamizwe? Wakati wa Yehova wa kutekeleza jambo hilo ufikapo, jiji hilo litaonekana kuwa salama. Majeshi yanayovamia yatakabiliana kwanza na kinga za asili za Mto Frati, unaopita katikati ya jiji na kutumiwa kujaza handaki la maji na kuleta maji ya kunywa jijini. Kisha yatakabiliana na kuta kubwa mno za Babiloni zenye sehemu mbili, zinazoonekana kuwa zisizoweza kupenywa. Zaidi ya hayo, jiji hilo litakuwa na akiba ya chakula cha kutosha. Kitabu cha Daily Bible Illustrations chasema kuwa Nabonido—mfalme wa mwisho wa Babiloni—“alikuwa amejizatiti kuweka akiba ya vyakula mjini humo, na ilisemekana kuwa mji huo ulikuwa na [chakula] cha kutosha kulisha wakazi wake kwa miaka ishirini.”
6. Ni nini kitakachotendeka bila kutarajiwa wakati shambulio lililotabiriwa dhidi ya Babiloni litukiapo?
6 Hata hivyo, sura yaweza kupotosha. Isaya asema: “Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto.” (Isaya 13:7, 8) Majeshi yenye kushinda yavamiapo jiji hilo, starehe ya wakazi wake itageuka kuwa utungu wa ghafula kama ule wa mwanamke anayezaa. Mioyo yao itayeyuka kwa hofu. Mikono yao italegea, huku imelemazwa, isiweze kuwakinga. Nyuso zao zitakuwa za “moto,” zenye kujaa hofu na maumivu makali. Watakodoleana macho kwa mshangao, wakistaajabia kuanguka kwa jiji lao kubwa.
7. ‘Siku ya Yehova’ inayokuja ni gani, na matokeo yatakuwaje kwa Babiloni?
7 Hata hivyo, lazima Babiloni litaanguka. Babiloni litakabili siku ya kulipa makosa, ‘siku ya Yehova,’ itakayokuwa yenye maumivu makali kwelikweli. Hakimu mkuu atadhihirisha hasira yake na kuwapasha hukumu ipasayo wakazi wenye dhambi wa Babiloni. Unabii huo wasema: “Tazama, siku ya BWANA [“Yehova,” “NW”] inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.” (Isaya 13:9) Matazamio ya Babiloni yako gizani. Ni kana kwamba jua, mwezi, na nyota zote zimekoma kutoa nuru. “Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.”—Isaya 13:10.
8. Kwa nini Yehova aamuru kuanguka kwa Babiloni?
8 Mbona msiba huo ulifike jiji hilo lenye kiburi? Yehova asema: “Nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali.” (Isaya 13:11) Kumwagwa kwa hasira ya kisasi ya Yehova kutakuwa adhabu kwa sababu ya ukatili wa Babiloni juu ya watu wa Mungu. Nchi yote itateseka kwa sababu ya ubaya wa Wababiloni. Wakali hao wenye kiburi hawatamkaidi Yehova tena waziwazi!
9. Ni nini kinachongojea Babiloni katika siku ya hukumu ya Yehova?
9 Yehova asema: “Nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.” (Isaya 13:12) Naam, watu wa jiji hilo wataangamizwa, jiji libaki ukiwa. Yehova aendelea: “Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali.” (Isaya 13:13) “Mbingu” za Babiloni, yaani miungu yake mingi, zitatetemeshwa, hazitaweza kulisaidia jiji hilo wakati wa dhiki. “Dunia,” ambayo ni Milki ya Babiloni, itatikiswa itoke katika mahali pake, iwe kitu cha kukumbukwa tu kama milki iliyoangamia. “Itakuwa kama vile paa aliyetishwa, na kama kondoo wasio na mtu wa kuwakusanya; kila mtu atageukia watu wake; nao watakimbia, kila mtu aende nchi yake mwenyewe.” (Isaya 13:14) Watu wote wa kigeni wanaounga Babiloni mkono wataiacha na kukimbia, wakitumaini kuanzisha uhusiano mpya pamoja na serikali ya ulimwengu yenye kushinda. Hatimaye Babiloni litapata maumivu ya kuwa jiji lililoshindwa, maumivu ambayo liliwatia watu wengine wengi sana katika siku za utukufu wake: “Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga. Na watoto wao wachanga watavunjwa-vunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watatendwa jeuri.”—Isaya 13:15, 16.
Chombo cha Mungu cha Kuharibu
10. Yehova atatumia nani ili kulishinda Babiloni?
10 Yehova atatumia serikali gani ili kuangusha Babiloni? Miaka ipatayo 200 mapema, Yehova afunua jibu: “Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu. Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto. Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza.” (Isaya 13:17-19) Yehova atatumia majeshi kutoka nchi ya mbali, yenye milima-milima ya Umedi, ili kuangusha Babiloni lenye utukufu.a Hatimaye, Babiloni litabaki ukiwa kama majiji ya Sodoma na Gomora yenye utovu mkubwa wa adili.—Mwanzo 13:13; 19:13, 24.
11, 12. (a) Umedi yawaje serikali ya ulimwengu? (b) Unabii huo wataja tabia gani isiyo ya kawaida kuhusu majeshi ya Umedi?
11 Katika siku ya Isaya, Umedi na Babiloni vilevile zatawaliwa na Ashuru. Karne moja hivi baadaye, mwaka wa 632 K.W.K., Umedi na Babiloni zaungana na kupindua Ninawi, jiji kuu la Ashuru. Hatua hiyo yaiwezesha Babiloni kuwa serikali kubwa ya ulimwengu. Yeye hatambui hata kidogo kwamba karibu miaka 100 baadaye, Umedi itamharibu! Ni nani mwingine isipokuwa Yehova Mungu, awezaye kutabiri kwa uhakika hivyo?
12 Akitambulishapo chombo chake alichokichagua cha kuharibu, Yehova asema kuwa majeshi ya Wamedi “hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu.” Ni tabia yenye kushangaza kama nini kwa wanajeshi waliozoea vita! Msomi wa Biblia Albert Barnes asema: “Ni majeshi machache sana yenye kuvamia ambayo hayakuvutiwa na tumaini la kupata nyara.” Je, majeshi ya Umedi yathibitisha kuwa Yehova alisema kweli kwa habari hiyo? Ndiyo. Fikiria maelezo haya yaliyo katika kichapo cha The Bible-Work, kilichoandikwa na J. Glentworth Butler: “Tofauti na mataifa yaliyo mengi ambayo yalipigana vita, Wamedi, na hasa Waajemi, hawakuzingatia sana dhahabu kuliko kupata ushindi na utukufu.”b Kwa hiyo, haishangazi kuwa Koreshi mtawala Mwajemi awaachiliapo Waisraeli kutoka katika uhamisho Babiloni, awarudishia maelfu ya vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadreza alipora kutoka katika hekalu la Yerusalemu.—Ezra 1:7-11.
13, 14. (a) Ingawa askari wa Umedi na Uajemi hawatamani nyara, wao watamani nini? (b) Koreshi ashindaje kinga za kujivunia za Babiloni?
13 Ingawa askari wa Umedi na Uajemi hawatamani sana nyara, wanatamani makuu hata hivyo. Hawataki wawe chini ya taifa jingine lolote ulimwenguni. Zaidi ya hayo, Yehova aweka “maangamizi” mioyoni mwao. (Isaya 13:6) Basi, kwa kutumia nyuta zao za chuma—ziwezazo kupiga mishale na vilevile kushambulia na kuwaponda wanajeshi adui, wazao wa akina mama wa Babiloni—wameazimia kushinda Babiloni.
14 Ngome za Babiloni hazimzuii Koreshi, kiongozi wa majeshi ya Umedi na Uajemi. Usiku wa Oktoba 5/6, 539 K.W.K., aagiza maji ya Mto Frati yaelekezwe kwingine. Maji yapungukapo, wavamizi waingia jijini kimya-kimya, wakitembea ndani ya bonde la mto katika maji yanayowafikia mapajani. Wakazi wa Babiloni wavamiwa ghafula, na Babiloni laanguka. (Danieli 5:30) Yehova Mungu ampulizia Isaya atabiri matukio hayo, hatua inayohakikisha kwamba Yeye ndiye anayeelekeza mambo.
15. Ni wakati ujao wa aina gani unaongojea Babiloni?
15 Babiloni litaharibiwa kadiri gani? Sikiliza tangazo la Yehova: “Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko. Na mbwa-mwitu watalia ndani ya ngome zake; na mbweha ndani ya majumba ya anasa; na wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka.” (Isaya 13:20-22) Jiji hilo litakuwa ukiwa kabisa.
16. Hali ya sasa ya Babiloni hutupa uhakika gani?
16 Jambo hilo halikutimia mara moja mwaka wa 539 K.W.K. Ingawa hivyo, leo ni wazi kabisa kwamba kila jambo alilotabiri Isaya kuhusu Babiloni limetimizwa. “Sasa na pia kwa karne nyingi, [Babiloni] limekuwa mahali penye ukiwa kabisa, nalo ni rundo la magofu,” asema mwelezaji mmoja wa Biblia. Kisha aongeza: “Haiwezekani kutazama mahali hapo kisha usikumbuke jinsi ambavyo matabiri ya Isaya na Yeremia yametimizwa kwa ukamili.” Kwa wazi, hakuna mwanadamu yeyote katika siku ya Isaya ambaye angeweza kutabiri kuanguka kwa Babiloni na ukiwa wake wa baadaye. Kwani, kuanguka kwa Babiloni mikononi mwa Wamedi na Waajemi kulitukia miaka ipatayo 200 baada ya Isaya kuandika kitabu chake! Kisha ukiwa wake wa mwisho ukaja karne kadhaa baadaye. Je, jambo hilo haliimarishi imani yetu katika Biblia kuwa ni Neno la Mungu lililopuliziwa? (2 Timotheo 3:16) Aidha, kwa kuwa Yehova alitimiza unabii mbalimbali wakati uliopita, twaweza kuwa na hakika kamili kwamba unabii mbalimbali wa Biblia ambao haujatimizwa utatimizwa kwa wakati ufaao wa Mungu.
“Raha Baada ya Huzuni Yako”
17, 18. Kushindwa kwa Babiloni kutaleta baraka gani kwa Israeli?
17 Anguko la Babiloni litakuwa kitulizo kwa Israeli. Anguko hilo litasababisha kuachiliwa kwao kutoka utekwani na kuwapa fursa ya kurudi katika Bara Lililoahidiwa. Basi, Isaya sasa asema: “BWANA atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, naye atawaweka katika nchi yao wenyewe; na mgeni atajiunga nao, nao wataambatana na nyumba ya Yakobo. Na hao mataifa watawatwaa na kuwaleta mpaka mahali pao wenyewe, na nyumba ya Israeli watawamiliki, na kuwafanya watumishi na wajakazi katika nchi ya BWANA; nao watawachukua hali ya kufungwa watu wale waliowafunga wao, nao watawamiliki watu wale waliowaonea.” (Isaya 14:1, 2) Hapo, neno “Yakobo” larejezea Israeli kwa jumla—makabila yote 12. Yehova atahurumia “Yakobo” kwa kuliruhusu taifa hilo lirudi nyumbani. Wataambatana na maelfu ya wageni, ambao wengi wao watakuwa watumishi wa hekaluni wa Waisraeli. Hata Waisraeli fulani watakuwa na mamlaka juu ya watekaji wao wa awali.c
18 Maumivu ya kuishi uhamishoni yatatokomea mbali. Badala yake, Yehova atawapa watu wake “raha baada ya huzuni ya[o], na baada ya taabu ya[o], na baada ya utumishi ule mgumu [wa]liotumikishwa.” (Isaya 14:3) Baada ya kuachiliwa kutoka katika utumwa wa kimwili, Israeli hatapatwa tena na huzuni na taabu ya kuishi miongoni mwa waabudu wa miungu isiyo ya kweli. (Ezra 3:1; Isaya 32:18) Kitabu cha Lands and Peoples of the Bible, kikielezea jambo hilo, chasema: “Miungu ya Babiloni ilifanana na Wababiloni, katika tabia yake mbaya sana. Hiyo ilikuwa yenye woga, ulevi na upumbavu.” Ni kitulizo kilichoje kuponyoka kutoka katika hali hiyo mbaya ya kidini!
19. Ni nini kinachohitajiwa ili Israeli ipate msamaha wa Yehova, nasi twaweza kujifunza nini kutokana na hilo?
19 Hata hivyo, rehema ya Yehova ina masharti. Lazima watu wake waonyeshe majuto kwa sababu ya uovu wao, uliomfanya Mungu awaadhibu vikali. (Yeremia 3:25) Ungamo la unyofu, litokalo moyoni, litafanya Yehova awasamehe. (Ona Nehemia 9:6-37; Danieli 9:5.) Kanuni hiyohiyo yatumika leo. Kwa maana “hakuna mtu asiyekosa,” sisi sote twahitaji rehema ya Yehova. (2 Mambo ya Nyakati 6:36) Yehova, Mungu mwenye rehema, hutuomba kwa upendo tuungame dhambi zetu kwake, tutubu, na tuache mwenendo wowote mbaya, ili tupate kuponywa. (Kumbukumbu la Torati 4:31; Isaya 1:18; Yakobo 5:16) Jambo hilo hutusaidia tupate upendeleo wake na pia hutufariji.—Zaburi 51:1; Mithali 28:13; 2 Wakorintho 2:7.
“Mithali” Dhidi ya Babiloni
20, 21. Jirani za Babiloni washangiliaje kuanguka kwake?
20 Zaidi ya miaka 100 kabla ya Babiloni kuinuka kuwa serikali kubwa ya ulimwengu, Isaya atabiri jinsi ulimwengu utakavyotenda Babiloni aangukapo. Kupitia unabii, awaamuru hivi Waisraeli ambao wameachiliwa kutoka utekwani Babiloni: “Utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri! BWANA amelivunja gongo la wabaya, fimbo ya enzi yao wenye kutawala. Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, kwa mapigo yasiyokoma; aliyewatawala mataifa kwa hasira, ameadhibiwa asizuie mtu.” (Isaya 14:4-6) Babiloni amejifanyia jina la kuwa mshindi mwenye kuonea, awafanyaye watu huru kuwa watumwa. Basi, yafaa kama nini kwamba kuanguka kwake kushangiliwe kwa “mithali” inayoelekezwa hasa kwa nasaba ya wafalme ya Babiloni—kuanzia kwa Nebukadreza na kuishia kwa Nabonido na Belshaza—iliyoongoza wakati wa siku za utukufu wa jiji hilo kubwa!
21 Kuanguka kwake kutaleta hali tofauti kama nini! “Dunia yote inastarehe na kutulia; hata huanzilisha kuimba. Naam, misunobari inakufurahia, na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, hapana mkata miti aliyetujia.” (Isaya 14:7, 8) Machoni pa watawala wa Babiloni, wafalme wa mataifa jirani walikuwa kama miti ya kukatwa na kutumiwa kwa malengo yao wenyewe. Lakini hayo yote yamekwisha. Mkata miti wa Babiloni amekata mti wake wa mwisho!
22. Kishairi, Sheoli yaathiriwaje na kuanguka kwa nasaba ya wafalme ya Babiloni?
22 Babiloni yaanguka kwa ajabu sana hivi kwamba kaburi lenyewe lajibu hivi: “Kuzimu [“Sheoli,” “NW”] chini kumetaharuki kwa ajili yako, ili kukulaki utakapokuja; huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, naam, walio wakuu wote wa dunia; huwainua wafalme wote wa mataifa, watoke katika viti vyao vya enzi. Hao wote watajibu na kukuambia, Je! wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, na sauti ya vinanda vyako; funza wametandazwa chini yako, na vidudu vinakufunika.” (Isaya 14:9-11) Huo ni mfano wa kishairi wenye nguvu kama nini! Ni kana kwamba kaburi la ujumla la wanadamu lapaswa kuwaamsha wafalme wote waliokufa kabla ya nasaba ya wafalme ya Babiloni ili wapate kumlaki mgeni huyo. Waidhihaki serikali inayotawala ya Babiloni, ambayo sasa haijiwezi, ikiwa imelala kwenye kitanda cha funza badala ya kitanda chenye bei ghali, ikiwa imefunikwa na vidudu badala ya vitani vyenye bei ghali.
“Kama Mzoga Uliokanyagwa Chini ya Miguu”
23, 24. Wafalme wa Babiloni waonyesha kiburi gani kikuu?
23 Isaya aendeleza mithali hiyo: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!” (Isaya 14:12) Kiburi chenye ubinafsi chawafanya wafalme wa Babiloni wajiinue juu ya jirani zao. Kama nyota ing’aayo sana katika anga la alfajiri, wao wadhihirisha uwezo na mamlaka yao kwa njia yenye kiburi. Jambo hasa linalosababisha kiburi ni ushindi wa Nebukadreza juu ya Yerusalemu, ambao Ashuru ilishindwa kutekeleza. Tamko la mithali laonyesha nasaba ya wafalme ya Babiloni yenye kiburi, ikisema: “Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na yeye Aliye juu.” (Isaya 14:13, 14) Je, kuna utovu mkubwa kushinda huo?
24 Katika Biblia, wafalme wa nasaba ya Daudi hufananishwa na nyota. (Hesabu 24:17) Kuanzia kwa Daudi na kuendelea, “nyota” hizo zilitawala huko Mlima Sayuni. Baada ya Solomoni kujenga hekalu katika Yerusalemu, jina Sayuni likaja kumaanisha jiji lote. Chini ya agano la Sheria, ilikuwa lazima kwa wanaume wote Waisraeli kusafiri hadi Sayuni mara tatu kwa mwaka. Basi, jiji hilo likawa “mlima wa mkutano.” Kwa kuazimia kushinda wafalme wa Yuda na kuwaondoa katika mlima huo, Nebukadreza atangaza lengo lake la kujiinua juu ya “nyota” hizo. Yeye hamsifu Yehova kwa sababu ya ushindi wake juu yao. Badala yake, ni kana kwamba ajiweka kwa kiburi mahali pa Yehova.
25, 26. Nasaba ya wafalme ya Babiloni yakumbwaje na mwisho wenye kufedhehesha?
25 Basi kuna mambo yaliyo kinyume kama nini yanayoingojea nasaba ya wafalme ya Babiloni! Babiloni kamwe haitainuliwa juu kuliko nyota za Mungu. Badala yake, Yehova asema: “Utashushwa mpaka kuzimu [“Sheoli,” “NW”]; mpaka pande za mwisho za shimo. Wao wakuonao watakukazia macho, watakuangalia sana, wakisema, Je! huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, huyu ndiye aliyetikisa falme; aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?” (Isaya 14:15-17) Nasaba hiyo ya wafalme yenye kutamani makuu itashuka ndani ya Hadesi (Sheoli), kama binadamu mwingine yeyote.
26 Basi, serikali iliyoshinda falme, ikaharibu nchi inayozaa, na kupindua majiji mengi itakuwa wapi? Serikali ya ulimwengu iliyochukua mateka na ikakataa kuwaruhusu kurudi nyumbani kwao itakuwa wapi? Kwani, nasaba ya wafalme ya Babiloni hata haitazikwa inavyofaa! Yehova asema: “Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe; bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, kama chipukizi lililochukiza kabisa; kama vazi la wale waliouawa, wale waliochomwa kwa upanga, wale washukao mpaka misingi ya shimo; kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu. Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, kwa maana umeiharibu nchi yako, umewaua watu wako; kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele.” (Isaya 14:18-20) Katika ulimwengu wa kale, ilikuwa aibu kwa mfalme kutozikwa kwa heshima. Basi, vipi kuhusu nasaba ya wafalme ya Babiloni? Ni kweli kwamba labda wafalme mmoja-mmoja wazikwa kwa heshima, lakini nasaba ya wafalme iliyotokana na Nebukadreza yatupwa ‘kama chipukizi linalochukiza kabisa.’ Ni kana kwamba nasaba hiyo ya wafalme imetupwa ndani ya kaburi lisilojulikana—kama mwanajeshi wa nchi kavu aliyeuawa vitani. Walitwezwa kama nini!
27. Vizazi vya baadaye vya Wababiloni vyatesekaje kwa sababu ya uovu wa baba zao?
27 Mwishoni mwa mithali hiyo, Wamedi na Waajemi wanaoshinda wapewa maagizo: “Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake. Kwa sababu ya uovu wa baba zao; wasije wakainuka na kuitamalaki nchi, na kuujaza miji uso wa ulimwengu.” (Isaya 14:21) Anguko la Babiloni litakuwa lenye kudumu. Nasaba ya wafalme ya Babiloni itang’olewa kabisa. Haitainuka tena. Vizazi vya baadaye vya Wababiloni vitateseka kwa sababu ya “uovu wa baba zao.”
28. Ni nini kilichosababisha dhambi ya wafalme wa Babiloni, nasi twajifunza nini kutokana na jambo hilo?
28 Hukumu iliyotolewa dhidi ya nasaba ya wafalme ya Babiloni inatupa fundisho muhimu. Tamaa ya makuu isiyo na kikomo ndiyo iliyosababisha dhambi ya wafalme wa Babiloni. (Danieli 5:23) Mioyo yao ilijaa tamaa ya kupata mamlaka. Walitaka kutawala wengine. (Isaya 47:5, 6) Nao walitamani utukufu wa wanadamu, ambao wafaa kupewa Mungu. (Ufunuo 4:11) Hilo ni onyo kwa yeyote aliye na mamlaka—hata katika kutaniko la Kikristo. Tamaa ya makuu na kiburi chenye ubinafsi ni tabia ambazo Yehova hatavumilia, katika watu mmoja-mmoja au katika mataifa.
29. Kiburi na tamaa ya makuu ya watawala wa Babiloni vilidhihirisha nini?
29 Kiburi cha watawala wa Babiloni kilidhihirisha roho ya “mungu wa huu mfumo wa mambo,” Shetani Ibilisi. (2 Wakorintho 4:4) Yeye pia ana hamu ya kupata mamlaka naye hutamani kujiinua juu ya Yehova Mungu. Kama ilivyokuwa kwa habari ya mfalme wa Babiloni na watu aliotiisha, tamaa ya Shetani isiyo takatifu imetokeza taabu na mateso kwa wanadamu wote.
30. Ni Babiloni gani mwingine anayetajwa katika Biblia, naye ameonyesha roho gani?
30 Zaidi ya hayo, twasoma juu ya Babiloni mwingine katika kitabu cha Ufunuo—“Babiloni Mkubwa.” (Ufunuo 18:2) Shirika hilo, milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli, pia limeonyesha roho yenye kiburi, yenye kuonea, na yenye ukatili. Basi, yeye pia lazima akabili ‘siku ya Yehova’ na aharibiwe wakati wa Mungu ufikapo. (Isaya 13:6) Tangu mwaka wa 1919 ujumbe huu umetangazwa kotekote duniani: “Babiloni Mkubwa ameanguka!” (Ufunuo 14:8) Aliposhindwa kuwazuia watu wa Mungu utekwani, alianguka. Karibuni ataangamizwa kabisa. Yehova aliamuru hivi kuhusu Babiloni la kale: “Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake; mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda; kwa sababu amefanya kiburi juu ya BWANA, juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.” (Yeremia 50:29; Yakobo 2:13) Babiloni Mkubwa atahukumiwa vivyo hivyo.
31. Ni nini kitakachompata Babiloni Mkubwa hivi karibuni?
31 Basi, taarifa ya mwisho ya Yehova kwenye unabii huu katika kitabu cha Isaya haihusu Babiloni ya kale peke yake, bali pia Babiloni Mkubwa: “Nitainuka, nishindane nao . . . na katika Babeli nitang’oa jina na mabaki, mwana na mjukuu . . . Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu.” (Isaya 14:22, 23) Magofu yaliyoachwa ukiwa ya Babiloni ya kale yaonyesha kile ambacho karibuni Yehova atautenda Babiloni Mkubwa. Ni faraja iliyoje kwa wapendao ibada ya kweli! Ni kitia-moyo kilichoje cha kujitahidi kutoruhusu kamwe tabia za Shetani za kiburi, dharau, au ukatili zisitawi ndani yetu!
[Maelezo ya Chini]
a Isaya ataja Wamedi peke yao kwa jina, ingawa mataifa kadhaa yataungana dhidi ya Babiloni—Umedi, Uajemi, Elamu, na mataifa mengine yaliyo madogo zaidi. (Yeremia 50:9; 51:24, 27, 28) Mataifa jirani huwaita Wamedi na pia Waajemi kuwa “Mmedi.” Isitoshe, katika siku ya Isaya, Umedi ndiyo serikali kubwa. Uajemi yaja tu kuwa kubwa Koreshi anapotawala.
b Hata hivyo, yaonekana kwamba baadaye Wamedi na Waajemi walipenda sana anasa.—Esta 1:1-7.
c Kwa kielelezo, Danieli aliteuliwa kuwa ofisa wa juu katika Babiloni chini ya Wamedi na Waajemi. Na karibu miaka 60 baadaye, Esta akawa malkia wa Mfalme Ahasuero wa Uajemi, naye Mordekai akawa waziri mkuu wa Milki yote ya Uajemi.
[Picha katika ukurasa wa 178]
Babiloni aliyeanguka atakuwa makao ya hayawani wakali wa nyikani
[Picha katika ukurasa wa 186]
Kama vile Babiloni la kale, Babiloni Mkubwa atakuwa rundo la magofu