Sura Ya Kumi Na Sita
Wafalme Washindani Wakaribia Mwisho Wao
1, 2. Mfalme wa kaskazini alibadilika akawa nani baada ya vita ya ulimwengu ya pili?
AKIZUNGUMZIA hali ya kisiasa ya Marekani na Urusi, mwanafalsafa Mfaransa aliye pia mwanahistoria Alexis de Tocqueville aliandika hivi mwaka wa 1835: “Mmoja ana uhuru akiwa njia kuu ya utendaji; yule mwingine ana utumwa. . . . Njia zao [ni] tofauti; hata hivyo, kila mmoja aonekana kuwa amepata mwito fulani wa siri wa Mungu wa kuongoza nusu ya ulimwengu siku moja.” Utabiri huo ulikuwa sahihi kadiri gani baada tu ya Vita ya Ulimwengu ya Pili? Mwanahistoria J. M. Roberts aandika hivi: “Mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu ya pili, ilionekana kana kwamba ulimwengu ungetawalwa na serikali mbili kubwa zenye mifumo tofauti kabisa ya kutawala, mmoja ukitegemea iliyokuwa Urusi, mwingine ukiwa Marekani.”
2 Wakati wa zile vita mbili za ulimwengu, Ujerumani ilikuwa adui mkuu wa mfalme wa kusini—Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani—nayo ilikuwa mfalme wa kaskazini. Hata hivyo, baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, taifa hilo liligawanyika. Ujerumani Magharibi ikajiunga na mfalme wa kusini, nayo Ujerumani Mashariki ikajiunga na serikali nyingine yenye nguvu—mataifa ya Kikomunisti yakiongozwa na Muungano wa Sovieti. Mataifa hayo, au utawala wa kisiasa, yakawa mfalme wa kaskazini, yakipingana vikali na Muungano wa Uingereza na Marekani. Nao ushindani kati ya wafalme hao wawili ukawa Vita Baridi, vita iliyodumu tangu 1948 hadi 1989. Awali, mfalme wa kaskazini wa Ujerumani alikuwa ‘kinyume cha agano takatifu.’ (Danieli 11:28, 30) Mataifa ya Kikomunisti yangetendaje kuhusiana na agano hilo?
WAKRISTO WA KWELI WAANGUKA LAKINI WAWA HODARI
3, 4. Ni nani “wafanyao maovu juu ya hilo agano,” nao wamekuwa na uhusiano gani na mfalme wa kaskazini?
3 “Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano,” akasema malaika wa Mungu, mfalme wa kaskazini “atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza.” Kisha malaika akasema hivi: “Lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu. Na hao walio wenye hekima katika watu watafundisha wengi; hata hivyo wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi.”—Danieli 11:32, 33.
4 Wale “wafanyao maovu juu ya hilo agano” waweza tu kuwa viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, wanaodai kuwa Wakristo lakini kulingana na matendo yao wanalichafua jina lenyewe la Ukristo. Katika kitabu chake Religion in the Soviet Union, Walter Kolarz asema hivi: “[Wakati wa vita ya ulimwengu ya pili] Serikali ya Sovieti ilijitahidi kuungwa mkono kihalisi na kiadili na Makanisa ili kulinda nchi yao.” Baada ya vita hiyo viongozi wa kanisa walijaribu kudumisha urafiki, ijapokuwa serikali ya mfalme wa kaskazini ilikuwa na sera za kutoamini kuwapo kwa Mungu. Kwa hiyo, Jumuiya ya Wakristo ikawa sehemu ya ulimwengu huu kuliko wakati mwingine wowote—uasi imani wenye kuchukiza machoni pa Yehova.—Yohana 17:16; Yakobo 4:4.
5, 6. “Watu wamjuao Mungu wao” walikuwa nani, na walipatwa na hali gani chini ya mfalme wa kaskazini?
5 Vipi juu ya Wakristo wa kweli—“watu wamjuao Mungu wao” na “wenye hekima”? Ingawa walikuwa “katika ujitiisho kwa mamlaka zilizo kubwa” ifaavyo, Wakristo walioishi chini ya utawala wa mfalme wa kaskazini hawakuwa sehemu ya ulimwengu. (Waroma 13:1; Yohana 18:36) Walikuwa waangalifu kumlipa “Kaisari vitu vya Kaisari,” na kumlimpa “Mungu vitu vya Mungu.” (Mathayo 22:21) Kwa sababu hiyo, uaminifu-maadili wao ulijaribiwa.—2 Timotheo 3:12.
6 Kwa sababu hiyo, Wakristo wa kweli ‘walianguka’ na ‘wakawa hodari.’ Walianguka katika maana ya kwamba walinyanyaswa vikali, hata wengine wakauawa. Lakini walikuwa hodari katika maana ya kwamba walio wengi waliendelea kuwa waaminifu. Waliushinda ulimwengu, kama alivyofanya Yesu. (Yohana 16:33) Isitoshe, hawakuacha kuhubiri, hata ikiwa walifungwa gerezani au kwenye kambi za mateso. Kwa kufanya hivyo, ‘waliwafundisha wengi.’ Licha ya mnyanyaso katika nchi nyingi zilizotawalwa na mfalme wa kaskazini, idadi ya Mashahidi wa Yehova iliongezeka. Kwa sababu ya uaminifu wa “wenye hekima,” “umati mkubwa” unaoongezeka daima umetokea katika nchi hizo.—Ufunuo 7:9-14.
WATU WA YEHOVA WATAKASWA
7. Ni “msaada kidogo” gani ambao Wakristo watiwa-mafuta waliokuwa wakiishi chini ya mfalme wa kaskazini walipokea?
7 Watu wa Mungu “watakapoanguka, watasaidiwa kwa msaada kidogo,” akasema malaika. (Danieli 11:34a) Ushindi wa mfalme wa kusini katika vita ya ulimwengu ya pili ulitokeza utulivu kidogo kwa Wakristo waliokuwa chini ya mfalme wa kaskazini. (Linganisha Ufunuo 12:15, 16.) Hali kadhalika, walionyanyaswa na mfalme aliyetawala baadaye, walipata utulivu pindi kwa pindi. Ile Vita Baridi ilipokuwa ikipungua, viongozi wengi walipata kutambua kwamba Wakristo waaminifu hawakuwa tisho lolote na hivyo wakawapa kibali cha kisheria. Pia, msaada ulitokana na idadi kubwa yenye kuongezeka ya umati mkubwa, walioitikia kuhubiri kwa uaminifu kulikofanywa na watiwa-mafuta na kuwasaidia.—Mathayo 25:34-40.
8. Watu fulani waliambatanaje na watu wa Mungu “kwa maneno ya kujipendekeza”?
8 Baadhi ya wale waliodai kwamba wanapenda kumtumikia Mungu wakati wa ile Vita Baridi hawakuwa na makusudi mazuri. Malaika alikuwa ameonya hivi: “Lakini wengi wataambatana nao kwa maneno ya kujipendekeza.” (Danieli 11:34b) Wengi walipendezwa na kweli lakini hawakutaka kujiweka wakfu kwa Mungu. Lakini wengine ambao walionekana kana kwamba waliikubali kweli, kwa kweli walikuwa wapelelezi wa wenye mamlaka. Ripoti moja kutoka nchi moja yataarifu hivi: “Baadhi ya watu hao wasio wanyoofu walikuwa Wakomunisti sugu na walikuwa wamepenya ndani ya tengenezo la Bwana, wakajionyesha kuwa na bidii nyingi, na hata walikuwa wamewekwa katika vyeo vya juu vya utumishi.”
9. Kwa nini Yehova aliruhusu baadhi ya Wakristo waaminifu ‘waanguke’ kwa sababu ya watu waliopenya ndani ya tengenezo lake?
9 Malaika huyo aliendelea kusema hivi: “Na baadhi yao wenye hekima wataanguka, ili kuwatakasa, na kuwasafisha, na kuwafanya weupe, hata wakati wa mwisho; kwa maana ni kwa wakati ulioamriwa, ambao haujaja.” (Danieli 11:35) Watu hao waliokuwa wamepenya ndani walisababisha waaminifu waanguke mikononi mwa wenye mamlaka. Yehova aliruhusu mambo hayo yatukie ili watu wake watakaswe na kusafishwa. Kama vile Yesu “ali[vyo]jifunza utii kutokana na mambo aliyoteseka,” ndivyo waaminifu hao wamejifunza uvumilivu kwa sababu imani yao imejaribiwa. (Waebrania 5:8; Yakobo 1:2, 3; linganisha Malaki 3:3.) Kwa hiyo, ‘wanatakaswa, kusafishwa, na kufanywa weupe.’
10. Ni nini kinachomaanishwa na maneno “hata wakati wa mwisho”?
10 Watu wa Yehova wangeanguka na kutakaswa “hata wakati wa mwisho.” Bila shaka, wanatarajia kunyanyaswa hadi mwisho wa mfumo huu mwovu wa mambo. Hata hivyo, uvamizi wa mfalme wa kaskazini unaosababisha watu wa mungu kusafishwa na kufanywa weupe ni “kwa wakati ulioamriwa.” Kwa hiyo, kwenye Danieli 11:35, “wakati wa mwisho” lazima uwe mwisho wa kipindi cha wakati kinachohitajiwa ili watu wa Mungu watakaswe huku wakivumilia mashambulio ya mfalme wa kaskazini. Yaonekana kule kuanguka kuliisha kwenye wakati ulioamriwa na Yehova mwenyewe.
MFALME AJITUKUZA
11. Malaika alisema nini juu ya mtazamo wa mfalme wa kaskazini kuelekea enzi kuu ya Yehova?
11 Kuhusu mfalme wa kaskazini, malaika aliongeza kusema hivi: “Mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye [akikataa kukiri enzi kuu ya Yehova] atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika. Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote.”—Danieli 11:36, 37.
12, 13. (a) Mfalme wa kaskazini alikataaje “miungu ya baba zake”? (b) “Wanawake” ambao mfalme wa kaskazini hakuijali ‘tamaa’ yao walikuwa nani? (c) Mfalme wa kaskazini alimtukuza “mungu” gani?
12 Akitimiza maneno hayo ya kiunabii, mfalme wa kaskazini alikataa “miungu ya baba zake,” kama vile mungu wa Utatu wa Jumuiya ya Wakristo. Mataifa ya Kikomunisti yaliendeleza moja kwa moja fundisho la kukataa kuwapo kwa Mungu. Kwa hiyo, mfalme wa kaskazini alijifanya kuwa mungu, ‘akijiadhimisha juu ya kila mungu.’ Bila kujali “aliyetamaniwa na wanawake”—nchi zilizo chini yake, kama vile Vietnam Kaskazini, ambazo zilikuwa kama vijakazi vya utawala wake—mfalme alitenda “kama apendavyo.”
13 Akiendelea na unabii huo, malaika alisema hivi: “Katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo.” (Danieli 11:38) Kwa hakika, mfalme wa kaskazini alitumaini silaha za kivita za kisayansi za kisasa, “mungu wa ngome.” Alitafuta wokovu kupitia “mungu” huyo, akitoa mali nyingi kwenye madhabahu yake.
14. Mfalme wa kaskazini ‘alitendaje kwa matokeo’?
14 “Ataziteka nyara [“Atatenda kwa matokeo dhidi ya,” NW] ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa.” (Danieli 11:39) Akimtegemea “mungu [wake] mgeni” wa kijeshi, mfalme wa kaskazini “alitenda kwa matokeo,” akijithibitisha kuwa serikali ya kijeshi yenye nguvu sana katika “siku za mwisho.” (2 Timotheo 3:1) Waliounga mkono dhana zake walitegemezwa kisiasa, kiuchumi, na nyakati nyingine kijeshi.
‘MSUKUMO’ WAKATI WA MWISHO
15. Mfalme wa kusini ‘alimsukumaje’ mfalme wa kaskazini?
15 “Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye [“atamsukuma,” NW],” malaika akamwambia Danieli. (Danieli 11:40a) Je, mfalme wa kusini ‘amemsukuma’ mfalme wa kaskazini katika “wakati wa mwisho”? (Danieli 12:4, 9) Ndiyo, bila shaka. Baada ya vita ya ulimwengu ya kwanza, ule mkataba wa amani wa kumwadhibu mfalme wa kaskazini—Ujerumani—kwa kweli ‘ulimsukuma,’ ukimchochea alipize kisasi. Baada ya ushindi wake katika vita ya ulimwengu ya pili, mfalme wa kusini alimlenga mpinzani wake kwa makombora ya nyuklia yenye kuhofisha na kupanga muungano wa kijeshi wenye nguvu dhidi yake, Shirika la Kujihami la North Atlantic Treaty Organization (NATO). Kuhusu utendaji wa NATO, mwanahistoria mmoja Mwingereza asema hivi: “Ndicho kilichokuwa chombo kikuu cha ‘kuudhibiti’ [Muungano wa Sovieti], ambao sasa ulionwa kuwa tisho kuu la amani ya Ulaya. Lengo lake lilidumu kwa miaka 40, nalo lilitimizwa kwa mafanikio sana.” Miaka ya Vita Baridi ilipoendelea, kule ‘kusukumwa’ na mfalme wa kusini kulitia ndani upelelezi wa hali ya juu na vilevile mashambulio ya kidiplomasia na ya kijeshi.
16. Mfalme wa kaskazini alitendaje aliposukumwa na mfalme wa kusini?
16 Mfalme wa kaskazini alitendaje? “Na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati.” (Danieli 11:40b) Historia ya siku za mwisho imeonyesha upanuzi wa mfalme wa kaskazini. Wakati wa vita ya ulimwengu ya pili “mfalme” wa Nazi alipanua mipaka yake na kuingia katika nchi jirani. Mwishoni mwa vita hiyo, “mfalme” aliyetawala baada yake alijenga milki yenye nguvu. Wakati wa ile Vita Baridi, mfalme wa kaskazini alipigana na mpinzani wake kwa kutegemeza pande tofauti katika vita na maasi katika Afrika, Amerika ya Latini, na Asia. Aliwanyanyasa Wakristo wa kweli, akizuia—wala si kusimamisha kamwe—utendaji wao. Nayo mashambulio yake ya kijeshi na ya kisiasa yalimwezesha kuongoza nchi nyingi. Hilo ndilo hasa jambo ambalo malaika alikuwa ametabiri: “Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri [makazi ya kiroho ya watu wa Yehova], na nchi nyingi zitapinduliwa.”—Danieli 11:41a.
17. Ni nini kilichozuia upanuzi wa mfalme wa kaskazini?
17 Hata hivyo, mfalme wa kaskazini hakuushinda ulimwengu wote. Malaika alitabiri hivi: “Lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni.” (Danieli 11:41b) Nyakati za kale, Edomu, Moabu, na Amoni zilikuwa katikati ya milki ya mfalme wa kusini wa Misri na milki ya mfalme wa kaskazini wa Siria. Leo zawakilisha mataifa na mashirika ambayo mfalme wa kaskazini alilenga lakini akashindwa kuyadhibiti.
MISRI HAIOKOKI
18, 19. Mfalme wa kusini alihisije uvutano wa mpinzani wake?
18 Malaika wa Yehova aendelea kusema hivi: “Naye [mfalme wa kaskazini] ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka. Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibia na Wakushi watafuata nyayo zake.” (Danieli 11:42, 43) Hata mfalme wa kusini, “Misri,” hakuokoka matokeo ya sera za upanuzi za mfalme wa kaskazini. Kwa kielelezo, mfalme wa kusini alishindwa vibaya huko Vietnam. Vipi juu ya “Walibia na Wakushi”? Huenda kwa kufaa majirani hao wa Misri ya kale wakawakilisha mataifa ambayo ni majirani wa “Misri” ya leo (mfalme wa kusini). Nyakati nyingine, yamekuwa ‘yakifuata nyayo za’ mfalme wa kaskazini.
19 Je, mfalme wa kaskazini amepata kutawala ‘hazina za Misri’? Kwa kweli, amekuwa na uvutano wenye nguvu juu ya jinsi mfalme wa kusini ametumia mali zake. Kwa sababu ya kumhofu mpinzani wake, mfalme wa kusini ametumia kiasi kikubwa cha fedha ili kudumisha jeshi la nchi kavu, la majini, na la angani lenye nguvu sana. Kwa hiyo, mfalme wa kaskazini ‘amekuwa na nguvu juu ya,’ au amedhibiti, matumizi ya mali za mfalme wa kusini.
VITA YA MWISHO
20. Malaika afafanuaje vita ya mwisho ya mfalme wa kaskazini?
20 Ushindani kati ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini—uwe wa kijeshi, kiuchumi, au mwingineo wowote—wakaribia kwisha. Akifunua kinaganaga juu ya pambano lililo mbele, malaika wa Yehova asema hivi: “Habari zitokazo mashariki [“macheo ya jua,” NW] na kaskazini zitamfadhaisha [mfalme wa kaskazini]; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi. Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikilia ajali yake [“atakuwa amefikia kikomo chake,” BHN], wala hakuna atakayemsaidia.”—Danieli 11:44, 45.
21. Kuna mambo gani bado ya kujifunza juu ya mfalme wa kaskazini?
21 Muungano wa Sovieti ulipovunjika Desemba 1991, mfalme wa kaskazini alipatwa na madhara makubwa. Ni nani atakayekuwa mfalme huyo wakati ambapo Danieli 11:44, 45 litakapotimizwa? Je, atakuwa mojawapo ya nchi zilizokuwa Muungano wa Sovieti? Au atabadilika kabisa, kama vile ambavyo amefanya mara kadhaa? Je, kutengenezwa kwa silaha za nyuklia kunakofanywa na mataifa mengine katika shindano jingine la silaha kutabadili utambulisho wa mfalme huyo? Wakati tu ndio utakaotoa majibu ya maswali hayo. Ni jambo la hekima kwamba tusikisie-kisie. Mfalme wa kaskazini arudiapo vita yake ya mwisho, wale wote wenye ufahamu wa kina unaotegemea Biblia watauona utimizo wa unabii huo waziwazi.—Ona “Wafalme Katika Danieli Sura ya 11,” kwenye ukurasa wa 284.
22. Ni maswali gani yanayozuka juu ya shambulio la mwisho la mfalme wa kaskazini?
22 Hata hivyo, twajua hatua ambayo mfalme wa kaskazini atachukua hivi karibuni. Akichochewa na ‘habari zitokazo macheo ya jua na kaskazini,’ atapanga vita ili “kuwaondolea mbali watu wengi.” Vita hiyo itapiganwa dhidi ya nani? Nazo ni “habari” gani zinazochochea shambulio hilo?
ASHTUSHWA NA HABARI ZENYE KUSUMBUA
23. (a) Ni tukio gani lenye kutokeza ambalo lazima litukie kabla ya Har–Magedoni? (b) “Wafalme watokao macheo ya jua” ni akina nani?
23 Fikiria jambo ambalo kitabu cha Ufunuo chasema juu ya mwisho wa Babiloni Mkubwa, milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli. Kabla ya “vita ya siku kubwa ya Mungu Mweza-Yote,” Har–Magedoni, adui huyo mkubwa wa ibada ya kweli “atachomwa kabisa kwa moto.” (Ufunuo 16:14, 16; 18:2-8) Kuharibiwa kwake kuliwakilishwa na kumwagwa kwa bakuli la sita la hasira ya kisasi ya Mungu kwenye mto wa ufananisho wa Eufrati. Mto huo wakauka ili “njia ipate kutayarishwa kwa ajili ya wafalme watokao macheo ya jua.” (Ufunuo 16:12) Wafalme hao ni nani? Si wengine ila Yehova Mungu na Yesu Kristo!—Linganisha Isaya 41:2; 46:10, 11.
24. Ni tendo gani la Yehova ambalo huenda likamsumbua mfalme wa kaskazini?
24 Kuharibiwa kwa Babiloni Mkubwa kwafafanuliwa kinaganaga kwenye kitabu cha Ufunuo, kinachotaarifu hivi: “Pembe kumi ulizoziona [wafalme wanaotawala katika wakati wa mwisho], na hayawani-mwitu [Umoja wa Mataifa], hawa watamchukia kahaba na watamfanya ukiwa na kuwa uchi, na watakula kabisa sehemu zake zenye nyama na watamchoma kabisa kwa moto.” (Ufunuo 17:16) Kwa nini wafalme watamharibu Babiloni Mkubwa? Kwa sababu ‘Mungu atia ndani ya mioyo yao ili watekeleze fikira yake.’ (Ufunuo 17:17) Mfalme wa kaskazini ni mmoja wa watawala hao. Huenda habari asikiazo kutoka “macheo ya jua” zarejezea tendo hilo la Yehova, atiapo ndani ya mioyo ya viongozi wa kibinadamu fikira ya kumwangamiza kahaba huyo mkubwa wa kidini.
25. (a) Lengo la pekee la mfalme wa kaskazini ni nini? (b) Mfalme wa kaskazini “ataweka hema zake za kifalme” wapi?
25 Lakini mfalme wa kaskazini ataelekeza hasira yake yenye kisasi mahali fulani pa pekee. “Ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari [“bahari kuu,” NW] na mlima mtakatifu wa uzuri,” asema malaika. Wakati wa Danieli bahari kuu ilikuwa Meditarenia nao mlima mtakatifu ulikuwa Zayoni, ambapo hekalu la Mungu lilikuwa wakati mmoja. Kwa hiyo, katika utimizo wa unabii huo, mfalme wa kaskazini aliyekasirishwa apanga vita dhidi ya watu wa Mungu. Katika maana ya kiroho, mahali palipo ‘kati ya bahari kuu na mlima mtakatifu’ pawakilisha makazi ya kiroho ya watumishi wa Yehova watiwa-mafuta. Wametoka kwenye “bahari” ya wanadamu waliotengwa na Mungu nao wana tumaini la kutawala kwenye Mlima Zayoni wa kimbingu pamoja na Yesu Kristo.—Isaya 57:20; Waebrania 12:22; Ufunuo 14:1.
26. Kama inavyoonyeshwa na unabii wa Ezekieli, huenda habari ‘itokayo kaskazini’ yatokana na nani?
26 Ezekieli, aliyeishi wakati mmoja na Danieli, alitabiri pia juu ya shambulio dhidi ya watu wa Mungu “katika siku za mwisho.” Alisema kwamba uhasama huo ungeanzishwa na Gogu wa Magogu, yaani, Shetani Ibilisi. (Ezekieli 38:14, 16) Kwa njia ya kitamathali, Gogu atokea upande gani? “Pande za mwisho za kaskazini,” asema Yehova, kupitia Ezekieli. (Ezekieli 38:15) Hata shambulio hilo liwe kali namna gani, halitawaharibu watu wa Yehova. Tukio hilo lenye kutokeza litamfanya Yehova achukue hatua ili kuyaangamiza majeshi ya Gogu. Kwa hiyo, Yehova amwambia Shetani hivi: ‘Nitakutia kulabu katika mataya yako, nami nitakutoa.’ “Nitakupandisha toka pande za mwisho za kaskazini; nami nitakuleta juu ya milima ya Israeli.” (Ezekieli 38:4; 39:2) Kwa hiyo, habari ‘itokayo kaskazini’ ambayo yamkasirisha mfalme wa kaskazini lazima iwe yatokana na Yehova. Lakini Mungu tu ndiye atakayeamua habari kamili zitokazo ‘macheo ya jua na kaskazini’ zitakuwa nini, nao wakati utafunua.
27. (a) Kwa nini Gogu atayachochea mataifa, kutia ndani mfalme wa kaskazini, yashambulie watu wa Yehova? (b) Matokeo ya shambulio la Gogu yatakuwa nini?
27 Gogu anapanga shambulio la kufa na kupona dhidi ya ufanisi wa “Israeli wa Mungu,” ambao, pamoja na “umati mkubwa” wa “kondoo wengine,” si sehemu ya ulimwengu wake. (Wagalatia 6:16; Ufunuo 7:9; Yohana 10:16; 17:15, 16; 1 Yohana 5:19) Gogu awatazama kichongochongo “watu waliokusanyika toka mataifa, waliopata ng’ombe na mali [za kiroho].” (Ezekieli 38:12) Akiyaona makazi ya kiroho ya Wakristo kuwa “nchi yenye vijiji visivyo na maboma” iliyo rahisi kuteka, Gogu ajitahidi sana kufagilia mbali kipingamizi hicho apate kudhibiti kabisa wanadamu. Lakini ashindwa. (Ezekieli 38:11, 18; 39:4) Wafalme wa dunia, kutia ndani mfalme wa kaskazini, washambuliapo watu wa Yehova, ‘watakuwa wamefikia kikomo chao.’
‘MFALME ATAKUWA AMEFIKIA KIKOMO CHAKE’
28. Twajua nini juu ya wakati ujao wa mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini?
28 Vita ya mwisho ya mfalme wa kaskazini haitakuwa dhidi ya mfalme wa kusini. Kwa hiyo, mfalme wa kaskazini hafikii kikomo chake mikononi mwa mpinzani wake mkuu. Hali kadhalika, mfalme wa kusini haharibiwi na mfalme wa kaskazini. Mfalme wa kusini aharibiwa, “bila kazi ya mikono” ya kibinadamu, bali na Ufalme wa Mungu.a (Danieli 8:25) Kwa hakika, kwenye vita ya Har–Magedoni, wafalme wote wa kidunia wataondolewa na Ufalme wa Mungu, na yaonekana hilo ndilo litakalompata mfalme wa kaskazini. (Danieli 2:44) Andiko la Danieli 11:44, 45 lafafanua matukio yanayoelekeza kwenye pigano la mwisho. Si ajabu basi kwamba “hakuna atakayemsaidia”!
[Maelezo ya Chini]
a Ona Sura ya 10 ya kitabu hiki.
UMEFAHAMU NINI?
• Mfalme wa kaskazini alibadilikaje baada ya vita ya ulimwengu ya pili?
• Ni nini kitakachompata mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini hatimaye?
• Umenufaikaje kwa kusikiliza unabii wa Danieli juu ya ushindani kati ya wafalme wawili?
[Chati/Picha katika ukurasa wa 284]
WAFALME KATIKA DANIELI SURA YA 11
Mfalme wa Mfalme wa
Kaskazini Kusini
Danieli 11:5 Niketa Seleuko wa I Ptolemy wa Kwanza
Danieli 11:6 Antiochus wa Pili Ptolemy wa Pili
(mke Laodice) (binti Berenice)
Danieli 11:7-9 Seleuko wa Pili Ptolemy wa Tatu
Danieli 11:10-12 Antiochus wa Tatu Ptolemy wa Nne
Danieli 11:13-19 Antiochus wa Tatu Ptolemy wa Tano
(binti Kleopatra wa I) Mwandamizi:
Waandamizi: Ptolemy wa Sita
Seleuko wa Nne na
Antiochus wa Nne
Danieli 11:20 Augusto
Danieli 11:21-24 Tiberio
Danieli 11:27-30a Milki ya Ujerumani Uingereza,
(Vita ya Ulimwengu ikifuatwa na
ya Kwanza) Serikali ya Ulimwengu ya
Uingereza na Marekani
Danieli 11:30b, 31 Milki ya Tatu ya Hitler Serikali ya (Vita ya Ulimwengu Ulimwengu ya
ya Pili) Uingereza na Marekani
Danieli 11:32-43 Mataifa ya Kikomunisti Serikali ya (Vita Baridi) Ulimwengu ya
Uingereza na Marekani
[Maelezo ya Chini]
b Unabii katika Danieli sura ya 11 hautaji majina ya tawala zinazofanyiza mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini wa nyakati mbalimbali. Wanajulikana baada tu ya mambo kuanza kutukia. Isitoshe, kwa kuwa mapambano yatukia pindi kwa pindi, kuna vipindi vya kutopambana—mfalme mmoja awa na mamlaka huku yule mwingine akiwa asiyetenda.
[Picha katika ukurasa wa 271]
[Picha katika ukurasa wa 279]
‘Kusukuma’ kunakofanywa na mfalme wa kusini kumetia ndani upelelezi wa hali ya juu na utendaji wa kijeshi