Danieli
11 “Mimi, katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario+ Mmedi, nilisimama ili kumtia nguvu na kumwimarisha.* 2 Nitakayokwambia sasa ndiyo kweli:
“Tazama! Wafalme watatu zaidi watasimama* kwa ajili ya Uajemi, na wa nne atajikusanyia utajiri mwingi zaidi kuliko wengine wote. Na atakapokuwa na nguvu kupitia utajiri wake, atachochea kila kitu dhidi ya ufalme wa Ugiriki.+
3 “Na mfalme mwenye nguvu atasimama na kutawala kwa mamlaka kubwa sana+ na kufanya apendavyo. 4 Na atakapokuwa amesimama, ufalme wake utavunjwa na kugawanywa kuelekea pepo nne za mbinguni,+ lakini si kwa wazao wake* na si kwa mamlaka aliyotawala nayo; kwa maana ufalme wake utang’olewa na kuchukuliwa na wengine zaidi ya hao.
5 “Na mfalme wa kusini atakuwa na nguvu, yaani, mmoja wa wakuu wake; lakini kuna mmoja atakayemshinda na kutawala kwa mamlaka kubwa sana, kubwa kuliko mamlaka yake.
6 “Baada ya miaka kadhaa wataungana, na binti ya mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini ili kufanya makubaliano. Lakini nguvu za mkono wa binti huyo hazitadumu; na mfalme huyo hatasimama, wala mkono wake; na binti huyo atatiwa mikononi mwa wengine, yeye pamoja na wale wanaomleta, na yule aliyemzaa, na yule atakayemtia nguvu nyakati hizo. 7 Na mmoja kutoka katika chipukizi la mizizi yake atasimama katika cheo cha mfalme huyo, na mfalme huyo atalijia jeshi na kushambulia ngome ya mfalme wa kaskazini naye atachukua hatua dhidi yao na kushinda. 8 Mfalme huyo atakuja Misri pamoja na miungu yao, sanamu zao za chuma,* na vitu vyao vinavyotamanika* vya fedha na vya dhahabu, pamoja na mateka. Kwa miaka kadhaa hatamshambulia mfalme wa kaskazini, 9 ambaye ataushambulia ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi katika nchi yake mwenyewe.
10 “Na wanawe watajitayarisha kwa ajili ya vita na kukusanya jeshi kubwa sana. Naye hakika atasonga mbele na kupita kama mafuriko. Lakini atarudi, naye atapigana vita mpaka kwenye ngome yake.
11 “Na mfalme wa kusini atakasirika, naye atatoka na kwenda kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini, ambaye atakusanya umati mkubwa wa watu, lakini umati huo utatiwa mikononi mwa mfalme huyo.* 12 Na umati huo utachukuliwa. Moyo wake utajikweza, naye atasababisha makumi ya maelfu waanguke; lakini hatatumia nafasi aliyopata ya ushindi.
13 “Na mfalme wa kaskazini atarudi na kukusanya umati mkubwa zaidi kuliko ule wa kwanza; na mwishoni mwa zile nyakati, baada ya miaka kadhaa, kwa hakika atakuja na jeshi kubwa na mali nyingi. 14 Nyakati hizo wengi watampinga mfalme wa kusini.
“Na watu wakatili* miongoni mwa watu wako watashawishiwa kujaribu kutimiza maono; lakini watajikwaa.
15 “Na mfalme wa kaskazini atakuja na kujenga boma la kuzingira na kuteka jiji lenye ngome. Na majeshi ya kusini hayatasimama,* wala wanaume wake mashujaa; nao hawatakuwa na nguvu za kusimama. 16 Yule anayekuja kupigana naye atafanya apendavyo, na hakuna yeyote atakayesimama mbele yake. Atasimama katika nchi ya lile Pambo,*+ na uwezo wa kuangamiza utakuwa mikononi mwake. 17 Naye ataazimia kabisa* kuja na nguvu kamili za ufalme wake, atafanya makubaliano pamoja na mfalme huyo; naye atatenda kwa mafanikio. Na kumhusu yule binti wa wanawake, mfalme huyo atapewa ruhusa ya kumwangamiza. Na binti huyo hatasimama, wala hataendelea kuwa wake. 18 Mfalme huyo ataugeuza uso wake na kurudi kwenye nchi za pwani, naye atateka maeneo mengi. Na kamanda fulani atakomesha kwa faida yake mwenyewe ufidhuli kutoka kwa mfalme huyo, hivi kwamba ufidhuli huo hautakuwepo. Ataufanya umrudie mfalme huyo. 19 Kisha* ataugeuza uso wake kurudi kwenye ngome za nchi yake mwenyewe, naye atajikwaa na kuanguka, na hatapatikana.
20 “Na katika cheo chake atasimama mtu anayemfanya mtozaji* apite katika ufalme wenye fahari, lakini katika siku chache atavunjwa, ingawa si kwa hasira wala vitani.
21 “Na katika cheo chake atasimama mtu anayedharauliwa,* nao hawatampa fahari ya ufalme huo; naye atakuja wakati wa usalama* na kuchukua ufalme kwa ujanja.* 22 Na majeshi yaliyo kama mafuriko yatafagiliwa* mbali kwa sababu yake, nayo yataangamizwa; kama itakavyokuwa kwa Kiongozi+ wa lile agano.+ 23 Na kwa sababu ya muungano waliofanya naye, ataendeleza udanganyifu na kuinuka na kuwa mwenye nguvu kupitia taifa dogo. 24 Wakati wa usalama,* atavamia maeneo ya mkoa* yenye utajiri mwingi zaidi* na kufanya mambo ambayo baba zake na mababu zake hawakufanya. Atawagawia watu wake vitu alivyopora na nyara na mali; naye atapanga njama zake dhidi ya mahali penye ngome, lakini kwa muda tu.
25 “Akiwa na jeshi kubwa, atakusanya nguvu zake na moyo wake dhidi ya mfalme wa kusini, naye mfalme wa kusini atajitayarisha kwa ajili ya vita hivyo akiwa na jeshi kubwa kupita kiasi, tena lenye nguvu. Naye hatasimama, kwa sababu watapanga njama dhidi yake. 26 Na wale wanaokula vyakula vyake bora watasababisha aanguke.
“Na jeshi lake litafagiliwa mbali, na wengi watauawa.
27 “Kuhusu wafalme hawa wawili, moyo wao utakuwa na mwelekeo wa kufanya maovu, nao wataketi kwenye meza moja wakiambiana uwongo. Lakini hakuna lolote litakalofanikiwa, kwa maana mwisho utakuja kwa wakati uliowekwa.+
28 “Na mfalme wa kaskazini atarudi katika nchi yake akiwa na mali nyingi, na moyo wake utapinga lile agano takatifu. Atatenda kwa mafanikio na kurudi katika nchi yake.
29 “Kwa wakati uliowekwa atarudi na kushambulia kusini. Lakini wakati huo mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa mwanzoni, 30 kwa maana meli za Kitimu+ zitamshambulia, naye atanyenyekezwa.
“Atarudi na kumwaga shutuma* dhidi ya lile agano takatifu,+ naye atatenda kwa mafanikio; atarudi na kuwakazia fikira wale wanaoliacha agano takatifu. 31 Na majeshi yatasimama, kutoka kwake; nayo yatachafua patakatifu,+ ile ngome, na kuondoa ile dhabihu inayotolewa daima.*+
“Nao watasimamisha kile kitu chenye kuchukiza sana kinachosababisha ukiwa.+
32 “Na wale wanaotenda uovu dhidi ya lile agano, atawaongoza kwa maneno ya ujanja* waingie katika uasi imani. Lakini watu wanaomjua Mungu wao watakuwa imara na kutenda kwa mafanikio. 33 Na wale walio na ufahamu+ miongoni mwa watu watawasaidia wengi kupata uelewaji. Nao* watakwazwa kwa upanga na kwa mwali wa moto, kwa kutekwa na kwa kuporwa, kwa siku kadhaa. 34 Lakini watakapokwazwa, watapokea msaada kidogo; na wengi watajiunga nao kwa maneno ya ujanja.* 35 Na baadhi ya wale wenye ufahamu watakwazwa, ili kazi ya kuwasafisha watu ifanywe kwa sababu yao na kazi ya kuwatakasa na kuwafanya kuwa weupe+ mpaka wakati wa mwisho; kwa maana bado ni ya wakati uliowekwa.
36 “Mfalme huyo atafanya apendavyo, naye atajikweza na kujitukuza juu ya kila mungu; naye atasema mambo ya kushangaza dhidi ya Mungu wa miungu.+ Naye atafanikiwa mpaka shutuma itakapofikia mwisho; kwa sababu kilichoamuliwa lazima kitendeke. 37 Hatamjali Mungu wa baba zake; wala hatajali tamaa ya wanawake wala hatajali mungu mwingine yeyote, lakini atajitukuza mwenyewe juu ya kila mtu. 38 Badala ya Mungu wa baba zake atampa utukufu mungu wa ngome; na kwa kutumia dhahabu na fedha na mawe yenye thamani na vitu vinavyotamanika,* atampa utukufu mungu ambaye baba zake hawakumjua. 39 Naye atashinda ngome zilizoimarishwa kabisa akiwa pamoja na* mungu wa kigeni. Atawapa utukufu mwingi wale wanaomtambua,* naye atawafanya wawatawale watu wengi; na ataigawa ardhi kwa malipo.
40 “Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atasukumana* naye, na mfalme wa kaskazini atamshambulia vikali kwa kutumia magari ya vita na wapanda farasi na meli nyingi; naye ataingia katika nchi hizo na kupita humo kama mafuriko. 41 Ataingia pia katika nchi ya lile Pambo,*+ na nchi nyingi zitakwazwa. Lakini hizi ndizo nchi zitakazoponyoka mikononi mwake: Edomu na Moabu na sehemu kuu ya Waamoni. 42 Naye ataendelea kuunyoosha mkono wake kwa nguvu dhidi ya nchi hizo; na nchi ya Misri haitaponyoka. 43 Naye atatawala hazina zilizofichwa za dhahabu na fedha na vitu vyote vinavyotamanika* vya Misri. Na Walibya na Waethiopia watafuata nyayo zake.*
44 “Lakini habari kutoka mashariki* na kutoka kaskazini zitamhangaisha, naye atatoka kwa hasira kali ili kuwaangamiza na kuwaua wengi. 45 Naye atapiga mahema yake ya kifalme* kati ya bahari kuu na mlima mtakatifu wa lile Pambo;*+ naye atasonga kufikia mwisho wake, na hakuna atakayemsaidia.