Ushindi wa Mwisho wa Mikaeli, Yule Mwana-Mfalme Mkuu
“Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari [mwana-mfalme, NW] mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako.”—DANIELI 12:1.
1. Watawala wengi wa ulimwengu wamedhihirisha mtazamo upi kuelekea enzi kuu ya Yehova, na mfalme wa kaskazini hajawa tofauti kwa njia gani?
“BWANA [Yehova, NW] ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao?” (Kutoka 5:2) Hayo yalikuwa maneno ya Farao yenye kudhihaki kuelekea Musa. Akikataa kukiri Uungu mkuu zaidi wa Yehova, Farao alikuwa ameazimia kuweka Israeli katika utumwa. Watawala wengine wamemdharau Yehova jinsi iyo hiyo, na wale wafalme wa unabii wa Danieli hawako tofauti hata kidogo. (Isaya 36:13-20) Kwa kweli, mfalme wa kaskazini amefanya zaidi ya hayo. Yule malaika asema hivi: “Atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu. . . . Wala hataijali miungu ya [Mungu wa, NW] baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote.”—Danieli 11:36, 37.
2, 3. Mfalme wa kaskazini alikataliaje mbali “Mungu wa baba zake” akipendelea kumwabudu “mungu” mwingine?
2 Akitimiza maneno hayo ya kiunabii, mfalme wa kaskazini alikatalia mbali “Mungu wa baba zake” (NW) (au, “miungu ya baba zake” UV), iwe ni ile miungu ya kipagani ya Waroma au ule Utatu wa kimungu wa Jumuiya ya Wakristo. Hitler alitumia Jumuiya ya Wakristo kwa makusudi yake mwenyewe lakini kwa wazi alipanga kuweka kanisa jipya la Kijerumani mahali payo. Mfalme wa kaskazini aliyemfuata aliendeleza imani ya kutokuamini kabisa kuwako kwa Mungu. Hivyo, mfalme wa kaskazini amejifanya mwenyewe mungu, ‘akijitukuza mwenyewe juu ya wote.’
3 Unabii huo waendelea hivi: “Katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo.” (Danieli 11:38) Kwa kweli, mfalme wa kaskazini aliweka tumaini lake katika hatua za kijeshi zinazotegemea sayansi ya ki-siku-hizi, “mungu wa ngome.” Katika muda wote wa siku za mwisho, amejaribu kupata wokovu kupitia “mungu” huyo, akidhabihu utajiri mwingi mno juu ya madhabahu yake.
4. Mfalme wa kaskazini amekuwa na mafanikio gani?
4 “Ataziteka nyara [atatenda kwa matokeo dhidi ya, NW] ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa.” (Danieli 11:39) Akitumaini “mungu [wake] mgeni” wa kijeshi, mfalme wa kaskazini ametenda “kwa matokeo” sana, akithibitika kuwa serikali ya kijeshi yenye kutisha katika “siku za mwisho.” (2 Timotheo 3:1) Wale waliounga mkono itikadi yake walipewa thawabu ya utegemezo wa kisiasa, wa kifedha, na wa kijeshi nyakati nyingi.
“Wakati wa Mwisho”
5, 6. Mfalme wa kusini ‘ameshindanaje,’ na mfalme wa kaskazini ameitikiaje?
5 Danieli 11:40a lasomwa hivi: “Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye.” Mstari huo na ile inayofuata imeonwa kuwa na utimizo katika wakati wetu ujao. Hata hivyo, ikiwa “wakati wa mwisho” hapa wamaanisha sawasawa na vile umaanishavyo kwenye Danieli 12:4, 9, twapaswa kutafuta utimizo wa maneno hayo muda wote wa siku za mwisho. Je! mfalme wa kusini ‘ameshindana na’ mfalme wa kaskazini katika wakati huu? Kwa kweli, ndiyo. Baada ya vita ya ulimwengu ya kwanza, ule mkataba wa amani wenye kuadhibu ulikuwa ni ‘kushindana’ kwa hakika, uchochezi wa kulipa kisasi. Baada ya ushindi wake katika vita ya ulimwengu ya pili, mfalme wa kusini alilenga silaha za nyukilia zenye kuhofisha kuelekea mshindani wake na kupanga dhidi yake muungano wa kijeshi wenye nguvu, NATO. Miaka ilipopita, ‘kushindana’ kwake kulitia ndani upelelezi wenye ufundi wa hali ya juu pamoja na mashambulio ya kibalozi na ya kijeshi.
6 Mfalme wa kaskazini aliitikiaje? “Mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati.” (Danieli 11:40b) Historia ya siku za mwisho imetokeza upanuzi wa mfalme wa kaskazini. Katika vita ya ulimwengu ya pili, “mfalme” wa Nazi alifurika kupita mipaka yake akaingia mabara yaliyokuwa kandokando. Mwishoni mwa vita hiyo, “mfalme” aliyefuata alijenga milki yenye nguvu nje ya mipaka yake mwenyewe. Katika ile Vita Baridi, mfalme wa kaskazini alipigana na mshindani wake katika vita vidogo-vidogo kati ya nchi walizounga mkono na katika maasi mbalimbali katika Afrika, Asia, na Amerika ya Latini. Aliwanyanyasa Wakristo wa kweli, akiuwekea mipaka utendaji wao (lakini bila kuukomesha hata kidogo). Na mashambulio yake ya kijeshi na ya kisiasa yalifanya mabara kadhaa yawe chini ya udhibiti wake. Ilikuwa barabara kama vile yule malaika alivyotoa unabii: “Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri [hali ya kiroho ya watu wa Mungu], na nchi nyingi zitapinduliwa.”—Danieli 11:41a.
7. Kulikuwa na mipaka gani kwa upanuzi wa mfalme wa kaskazini?
7 Hata hivyo, ingawa—kwa maoni ya mshindani wake—mfalme wa kaskazini ameonekana kuwa tisho, yeye hajatimiza ushindi wa ulimwengu. “Nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni.” (Danieli 11:41b) Katika nyakati za kale, Edomu, Moabu, na Amoni kwa ujumla zilikuwa katikati ya Misri na Siria. Leo zaweza kuonwa kuwa zawakilisha yale mataifa na mashirika ambayo mfalme wa kaskazini alikusudia kuleta chini ya uvutano wake lakini akashindwa.
“Misri Haitaokoka”
8, 9. Uvutano wa mfalme wa kaskazini umehisiwaje, hata na mshindani wake mkuu?
8 Yule malaika aendelea kusema hivi: “Ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka. Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibia na Wakushi watafuata nyayo zake.” (Danieli 11:42, 43) Hata mfalme wa kusini, “Misri,” hakuokoka matokeo ya sera za upanuzi za mfalme wa kaskazini. Kwa kielelezo, yeye alishindwa vibaya katika Vietnam. Na namna gani “Walibia na Wakushi”? Majirani hao wa Misri ya kale waweza sana kufananisha mataifa yaliyo majirani wa “Misri” ya ki-siku-hizi, kwa kusema kijiografia, na ambayo nyakati nyingine yamekuwa wafuasi wa, ‘kufuata nyayo za,’ mfalme wa kaskazini.
9 Je! mfalme wa kaskazini amekuwa na nguvu juu ya ‘hazina za Misri zilizofichika’? Bila shaka, yeye hajashinda mfalme wa kusini, na kufikia 1993 hali ya ulimwengu ilifanya ionekane haielekei kwamba atafanya hivyo. Lakini amekuwa na uvutano wenye nguvu juu ya njia ambayo mfalme wa kusini alitumia nyenzo zake za kifedha. Kwa sababu ya kumhofu mshindani wake, mfalme wa kusini ametumia fedha nyingi sana kila mwaka ili kudumisha jeshi, jeshi la baharini, na jeshi la wanahewa, lenye kutisha. Kwa kadiri hiyo mfalme wa kaskazini angeweza kusemwa kuwa ‘alikuwa na nguvu,’ akadhibiti, matumizi ya utajiri wa mfalme wa kusini.
Kampeni ya Mwisho ya Mfalme wa Kaskazini
10. Yule malaika asimulia kwa njia gani mwisho wa ule ushindani kati ya wale wafalme wawili?
10 Je! ule ushindani kati ya wafalme hao wawili waendelea hadi wakati usiojulikana? La. Yule malaika alimwambia Danieli hivi: “Habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha [mfalme wa kaskazini]; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi. Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikilia ajali yake [mwisho wake, NW], wala hakuna atakayemsaidia.”—Danieli 11:44, 45.
11, 12. Ni matukio gani ya kisiasa ya hivi karibuni yanayohusiana na ule ushindani kati ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini, na twahitaji kujifunza nini bado?
11 Matukio hayo ni ya wakati ujao bado, kwa hiyo hatuwezi kusema kwa urefu jinsi unabii huo utakavyotimizwa. Hivi karibuni hali ya kisiasa kuhusu wafalme hao wawili imebadilika. Ule ushindani mkali kati ya United States na nchi za Ulaya ya Mashariki umepoa. Zaidi ya hayo, ule Muungano wa Sovieti ulivunjwa katika 1991 na haupo tena.—Ona Mnara wa Mlinzi la Machi 1, 1992, kurasa 4, 5.
12 Kwa hiyo ni nani aliye mfalme wa kaskazini sasa? Je! atambulishwe kuwa ni moja kati ya nchi zilizokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti wa zamani? Au anaubadili kabisa utambulisho wake, kama vile amefanya mara kadha kabla ya hapo? Hatuwezi kusema. Ni nani atakayekuwa mfalme wa kaskazini wakati Danieli 11:44, 45 litimizwapo? Je! ushindani kati ya wafalme hao wawili utalipuka tena? Na namna gani juu ya zile akiba kubwa mno za silaha za nyukilia zilizoko bado katika mabara kadhaa? Ni wakati tu utakaoandaa majibu kwa maswali hayo.
13, 14. Twajua nini juu ya wakati ujao wa wale wafalme wawili?
13 Twajua jambo moja. Hivi karibuni, mfalme wa kaskazini ataongoza kampeni ya kushambulia itakayochochewa na ‘habari itokayo mashariki na kaskazini itakayomfadhaisha.’ Kampeni hiyo itafanywa kabla tu ya “mwisho” wake. Twaweza kujifunza zaidi juu ya “habari” hiyo tukichunguza unabii mwingine wa Biblia.
14 Lakini, kwanza ona kwamba matendo hayo ya mfalme wa kaskazini hayasemwi kuwa ni dhidi ya mfalme wa kusini. Yeye hafikilii mwisho wake mikononi mwa mshindani wake mkubwa. Vivyo hivyo, mfalme wa kusini haharibiwi na mfalme wa kaskazini. Mfalme wa kusini (anayewakilishwa katika unabii mwingine mwingi kuwa ile pembe ya mwisho kutokea kwenye hayawani-mwitu) aharibiwa “bila kazi ya mikono [ya kibinadamu]” na Ufalme wa Mungu. (Danieli 7:26; 8:25) Kwa kweli, wafalme wote wa kidunia wanaharibiwa hatimaye na Ufalme wa Mungu kwenye pigano la Har–Magedoni, na hilo kwa wazi ndilo jambo limpatalo mfalme wa kaskazini. (Danieli 2:44; 12:1; Ufunuo 16:14, 16) Danieli 11:44, 45 yasimulia matukio yanayoongoza kwenye pigano hilo la mwisho. Haishangazi kwamba “hakuna atakayemsaidia” wakati mfalme wa kaskazini akabilipo mwisho wake!
15. Ni maswali gani ya maana yanayobaki kuzungumziwa?
15 Basi, ni upi ule unabii mwingine mwingi unaoangazia nuru ile “habari” inayomsukuma mfalme wa kaskazini kuanza “kuwaondolea mbali watu wengi”? Na ni nani wale “wengi” ambao atataka kuharibu?
Habari Kutoka Mashariki
16. (a) Ni lazima jambo jipi la kutokeza litukie kabla ya Har–Magedoni? (b) Ni nani wale “wafalme watokao katika maawio ya jua”?
16 Kabla ya pigano la mwisho, Har–Magedoni, ni lazima adui mmoja mkuu wa ibada ya kweli aharibiwe—Babuloni Mkuu aliye kama kahaba, milki ya ulimwenguni pote ya dini bandia. (Ufunuo 18:3-8) Kuharibiwa kwake kwafananishwa na kule kumwagwa kwa bakuli la sita la ghadhabu ya Mungu juu ya mto Frati wa ufananisho. Mto huo wakauka “ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua.” (Ufunuo 16:12) Wafalme hao ni nani? Si wengine ila Yehova Mungu na Yesu Kristo!a
17. (a) Biblia hutuambia nini juu ya uharibifu wa Babuloni Mkubwa? (b) Zile habari “zitokazo mashariki” zaweza kuthibitika kuwa nini?
17 Uharibifu wa Babuloni Mkubwa unasimuliwa waziwazi katika kitabu cha Ufunuo: “Zile pembe kumi ulizoziona [‘wafalme’ wanaotawala katika wakati wa mwisho], na huyo mnyama [yule hayawani-mwitu mwenye rangi-nyekundu-nyangavu, akiwakilisha shirika la Umoja wa Mataifa], hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto.” (Ufunuo 17:16) Kwa kweli, mataifa ‘yala nyama tele’! (Danieli 7:5) Lakini kwa nini watawala, kutia na mfalme wa kaskazini, wataharibu Babuloni Mkubwa? Kwa sababu ‘Mungu atia mioyoni mwao kufanya shauri lake.’ (Ufunuo 17:17) Ile habari ‘itokayo mashariki’ yaweza kuwa yarejezea tendo hilo la Yehova, atiapo mioyoni mwa viongozi wa kibinadamu shauri la kuangamiza yule kahaba mkubwa wa kidini, kwa njia achaguaye.—Danieli 11:44.
Habari Kutoka Kaskazini
18. Mfalme wa kaskazini anamlenga nani mwingine, na awa wapi afikiliapo mwisho wake?
18 Lakini ghadhabu ya mfalme wa kaskazini inamlenga mwingine. Yule malaika asema kwamba “ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri.” (Danieli 11:45) Katika wakati wa Danieli, bahari tukufu ilikuwa Mediterania, na mlima mtakatifu ulikuwa Sayuni, ambao wakati mmoja ulikuwa mahali pa hekalu la Mungu. Kwa hiyo, katika utimizo wa unabii huo, mfalme wa kaskazini mwenye ghadhabu aongoza kampeni ya kijeshi dhidi ya watu wa Mungu! Kwa maana ya kiroho leo, “kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri” kwamweka katika makao ya kiroho ya watumishi wa Mungu wapakwa, ambao wametoka katika “bahari” ya ainabinadamu iliyotengwa na wana tumaini la kutawala juu ya Mlima Sayuni wa kimbingu pamoja na Yesu Kristo.—Isaya 57:20; Waebrania 12:22; Ufunuo 14:1.
19. Kama ionyeshwavyo katika unabii wa Ezekieli, twaweza kutambulishaje ile habari ichocheayo shambulio la Gogu? (Ona kielezi-chini.)
19 Ezekieli, aliyeishi wakati wa Danieli, alitoa unabii pia wa shambulio juu ya watu wa Mungu “katika siku za mwisho.” Alisema kwamba uhasama huo ungeanzishwa na Gogu wa Magogu, akiwakilisha Shetani Ibilisi. (Ezekieli 38:16) Gogu atokea wapi, kwa ufananisho? Yehova, kupitia Ezekieli, asema hivi: “Utakuja kutoka mahali pako, kutoka pande za mwisho za kaskazini.” (Ezekieli 38:15) Kwa hiyo, habari ‘itokayo kaskazini’ yaweza kuwa ni propaganda ya Shetani ikimchochea mfalme wa kaskazini na wale wafalme wengine wote washambulie watu wa Yehova.b—Linganisha Ufunuo 16:13, 14; 17:14.
20, 21. (a) Kwa nini Gogu atachochea mataifa, kutia na mfalme wa kaskazini, ili kushambulia watu wa Mungu? (b) Je! shambulio lake litafanikiwa?
20 Gogu apanga shambulio hilo la kufa na kupona kwa sababu ya ufanisi wa “Israeli wa Mungu,” ambao, pamoja na ule mkutano mkubwa wa kondoo wengine, si sehemu ya ulimwengu wake tena. (Wagalatia 6:16; Yohana 10:16; 17:15, 16; 1 Yohana 5:19) Gogu atazama kwa chuki kuelekea “watu waliokusanyika toka mataifa, waliopata ng’ombe na mali [za kiroho].” (Ezekieli 38:12; Ufunuo 5:9; 7:9) Katika utimizo wa maneno hayo, watu wa Yehova wanafanikiwa leo kuliko wakati mwingine wowote. Katika mabara mengi katika Ulaya, Afrika, na Asia walikopigwa marufuku wakati mmoja, wao huabudu kwa uhuru sasa. Kati ya 1987 na 1992, “vitu vinavyotamaniwa” zaidi ya milioni moja vilitoka katika mataifa kwenda kwenye nyumba ya Yehova ya ibada ya kweli. Kiroho, wao ni matajiri na wenye amani.—Hagai 2:7; Isaya 2:2-4; 2 Wakorintho 8:9.
21 Akiona hali ya kiroho ya Kikristo kuwa “nchi yenye vijiji visivyo na maboma,” iliyo rahisi kutekwa, Gogu afanya jitihada kubwa zaidi ya kufutilia mbali kizuizi hiki dhidi ya udhibiti wake kamili juu ya ainabinadamu. (Ezekieli 38:11) Lakini ashindwa. Wafalme wa dunia washambuliapo watu wa Yehova, ‘wataufikilia mwisho wao.’ Jinsi gani?
Mfalme wa Tatu
22, 23. Gogu ashambuliapo, ni nani asimamaye upande wa watu wa Mungu, na kukiwa na matokeo gani?
22 Ezekieli asema kwamba shambulio la Gogu ndiyo ishara kwa Yehova Mungu ya kuinuka kwa niaba ya watu wake na kuharibu majeshi ya Gogu “juu ya milima ya Israeli.” (Ezekieli 38:18; 39:4) Hilo latukumbusha juu ya yale ambayo yule malaika amwambia Danieli: “Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari [mwana-mfalme, NW] mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.”—Danieli 12:1.
23 Katika 1914, Yesu—Mikaeli yule mwanavita wa kimbingu—alikuwa Mfalme wa Ufalme wa Mungu wa kimbingu. (Ufunuo 11:15; 12:7-9) Tangu wakati huo, amekuwa akisimama ‘upande wa wana wa watu wa Danieli.’ Lakini, hivi karibuni, yeye “atasimama” katika jina la Yehova akiwa Mfalme-Mwanavita asiyeshindika, “akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu.” (2 Wathesalonike 1:8) Mataifa yote ya dunia, kutia na wale wafalme wa unabii wa Danieli, ‘wataomboleza.’ (Mathayo 24:30) Wakiwa bado na mawazo maovu mioyoni mwao kuelekea ‘watu wa Danieli,’ wataangamia milele mikononi mwa ‘Mikaeli, yule mwana-mfalme mkuu.’—Ufunuo 19:11-21.
24. Funzo hili juu ya unabii wa Danieli lapasa lituathirije?
24 Je! hatutamani kuona ushindi huo mtukufu wa Mikaeli na wa Mungu wake, Yehova? Maana ushindi huo utamaanisha ‘kuokolewa,’ wokovu, kwa Wakristo wa kweli. (Linganisha Malaki 4:1-3) Kwa hiyo, tukitazama wakati ujao tukiwa na matazamio yenye hamu, twakumbuka maneno ya mtume Paulo: “Lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa.” (2 Timotheo 4:2) Acheni tuendelee kulishika sana Neno la uhai na kutafuta kondoo wa Yehova kwa bidii-nyendelevu hali wakati ufaao uendeleapo. Tumo katika sehemu ya mwisho katika lile shindano la mbio la kupata uhai. Thawabu yaonekana. Na tuazimie kuvumilia hadi mwisho na hivyo tuwe miongoni mwa wale watakaookolewa.—Mathayo 24:13; Waebrania 12:1.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu! kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., kurasa 229-30.
b Kwa njia nyingine, ile habari ‘itokayo kaskazini’ ingeweza kuthibitika kuwa yatokana na Yehova, kwa kupatana na maneno yake kwa Gogu: “Nami nitakugeuza na kutia kulabu katika mataya yako, nami nitakutoa.” “Nami . . . nitakupandisha toka pande za mwisho za kaskazini; nami nitakuleta juu ya milima ya Israeli.”—Ezekieli 38:4; 39:2; linganisha Zaburi 48:2.
Je! Wewe Waelewa?
◻ Mfalme wa kusini ameshindanaje na mfalme wa kaskazini muda wote wa wakati wa mwisho?
◻ Twahitaji kujifunza nini bado kuhusu tokeo la ule ushindani kati ya hao wafalme wawili?
◻ Ni matukio gani mawili kabla ya Har–Magedoni ambayo kwa hakika yatahusisha mfalme wa kaskazini?
◻ ‘Mikaeli, yule mwana-mfalme mkuu,’ atawalindaje watu wa Mungu?
◻ Twapaswa kuitikiaje funzo letu juu ya unabii wa Danieli?
[Picha katika ukurasa wa 19]
Mfalme wa kaskazini ameabudu mungu aliye tofauti na miungu ya watangulizi wake
[Hisani]
Kushoto juu na katikati: UPI/Bettmann; kushoto chini: Reuters/Bettmann; kulia chini: Jasmin/Gamma Liaison