Kitabu Cha Biblia Namba 7—Waamuzi
Mwandikaji: Samweli
Mahali Kilipoandikiwa: Israeli
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 1100 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: c. (karibu) 1450—c. (karibu) 1120 K.W.K.
1. Kipindi cha waamuzi kilikuwa chenye kutokeza katika njia zipi?
HII ni sehemu ya historia ya Israeli iliyojawa na vitendo, yenye visa vya kujiingiza katika dini ya roho waovu yenye kuleta msiba na ukombozi wa Yehova wenye rehema wa watu wake wenye kutubu kupitia waamuzi waliowekwa kimungu. Ni yenye kutia nguvu imani matendo makuu ya Othnieli, Ehudi, Shamgari, na waamuzi wengine waliofuata. Ni kama alivyosema mwandikaji wa Waebrania: “Wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha . . . ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki . . . walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.” (Ebr. 11:32-34) Ili kukamilisha hesabu hiyo ya waamuzi waaminifu 12 wa kipindi hicho, pia kuna Tola, Yairi, Ibzani, Eloni, na Abdoni. (Kwa kawaida Samweli hahesabiwi kati ya waamuzi.) Yehova alipigana mapigano ya waamuzi hao kwa ajili yao, na roho iliwafunika walipokuwa wakifanya matendo yao ya ushujaa. Walimpa Mungu wao sifa na utukufu wote.
2. Jina la Kiebrania la kitabu cha Waamuzi lafaa katika njia gani?
2 Katika Septuagint kitabu hicho chaitwa Kri·taiʹ, na katika Biblia ya Kiebrania, ni Sho·phetimʹ, ambacho hutafsiriwa “Waamuzi.” Sho·phetimʹ hutokana na kitenzi sha·phatʹ, maana yake “amua, tetea, adhibu, ongoza,” yanayoonyesha vizuri cheo cha hawa wawekwa kitheokrasi wa “Mungu mwamuzi wa watu wote.” (Ebr. 12:23) Wao walikuwa wanaume walioinuliwa na Yehova katika pindi fulani hasa, ili kukomboa watu wake kutoka utumwa wa kigeni.
3. Waamuzi kiliandikwa lini?
3 Waamuzi kiliandikwa lini? Semi mbili katika kitabu hicho hutusaidia kupata jibu. Wa kwanza ni: “Bali Wayebusi walikaa . . . ndani ya Yerusalemu hata hivi leo.” (Amu. 1:21) Kwa kuwa Mfalme Daudi aliteka “ngome ya Sayuni” kutoka kwa Wayebusi katika mwaka wa nane wa utawala wake, au katika 1070 K.W.K., lazima Waamuzi kiwe kiliandikwa kabla ya tarehe hiyo. (2 Sam. 5:4-7) Usemi wa pili hutukia mara nne: “Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli.” (Amu. 17:6; 18:1; 19:1; 21:25) Kwa hiyo, maandishi hayo yaliandikwa wakati ambao kulikuwako “mfalme katika Israeli,” yaani, baada ya Sauli kuwa mfalme katika 1117 K.W.K. Kwa hiyo lazima kiwe cha tarehe ya katikati ya 1117 na 1070 K.W.K.
4. Ni nani aliyekuwa mwandikaji wa Waamuzi?
4 Mwandikaji alikuwa nani? Bila shaka, alikuwa mtumishi aliyejitoa wa Yehova. Samweli ndiye anayesimama peke yake kuwa mteteaji mkuu wa ibada ya Yehova katika wakati huu wa badiliko kutoka waamuzi hadi kwenye wafalme, na yeye pia ndiye wa kwanza wa mstari wa manabii waaminifu. Kwa hiyo, lingekuwa jambo la akili kwamba Samweli ndiye aliyeandika historia ya waamuzi.
5. Kipindi cha Waamuzi chaweza kuhesabiwa?
5 Waamuzi kinahusisha kipindi kirefu jinsi gani? Hilo laweza kuhesabiwa kutokana na 1 Wafalme 6:1, panapoonyesha kwamba Sulemani alianza kujenga nyumba ya Yehova katika mwaka wa nne wa utawala wake, ambao pia ulikuwa ni “katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya kutoka wana wa Israeli katika nchi ya Misri.” (“wa mia nne na themanini” ikiwa ni namba mpango, yawakilisha miaka 479 kamili.) Vipindi vijulikanavyo vinavyotiwa katika hiyo miaka 479 ni miaka 40 chini ya Musa katika jangwa (Kum. 8:2), miaka 40 ya utawala wa Sauli (Mdo. 13:21), miaka 40 ya utawala wa Daudi (2 Sam. 5:4, 5), na miaka mitatu kamili ya kwanza ya utawala wa Sulemani. Kuondoa jumla hii ya miaka 123 kutoka miaka 479 ya 1 Wafalme 6:1, kwabaki miaka 356 ya kipindi cha katikati ya kuingia kwa Israeli katika Kanaani na mwanzo wa utawala wa Sauli.a Matukio yaliyoandikwa katika kitabu cha Waamuzi, kuanzia hasa kifo cha Yoshua hadi wakati wa Sauli, yahusisha miaka kama 330 ya kipindi hiki cha miaka 356.
6. Ni nini kinachothibitisha uasilia wa Waamuzi?
6 Uasilia wa Waamuzi hautiliki shaka. Sikuzote Wayahudi wamekitambua kuwa sehemu ya Maandiko ya Biblia. Waandikaji wa Maandiko ya Kiebrania na ya Kigiriki ya Kikristo walitumia maandishi yacho, kama katika Zaburi 83:9-18; Isaya 9:4; 10:26; na Waebrania 11:32-34. Kuhusu kweli, hakifichi chochote katika kupungukiwa na kurudi nyuma kwa Israeli, wakati uo huo kikikuza fadhili za upendo za Yehova zisizo na kipimo. Yehova, na wala si mwamuzi mnyonge wa kibinadamu, ndiye anayepokea utukufu kuwa Mkombozi katika Israeli.
7. (a) Akiolojia yaungaje mkono maandishi katika Waamuzi? (b) Ni kwa nini kwa kufaa Yehova aliamuru waabudu wa Baali wafutiliwe mbali?
7 Na zaidi, vitu vya akiolojia vilivyopatikana vyaunga mkono uhalisi wa Waamuzi. Vyenye kutokeza zaidi ni vile vinavyohusu asili ya dini ya Baali ya Wakanaani. Kando ya marejezo ya Biblia, ni machache yaliyojulikana juu ya Ubaali mpaka jiji la kale la Kikanaani la Ugariti (Ras Shamra wa kisasa kwenye pwani ya Shamu mkabala (kuangaliana) wa ncha ya kaskazini mashariki ya kisiwa cha Saiprasi) lilipochimbuliwa, kuanzia 1929. Hapa, dini ya Baali ilifunuliwa kuwa yenye kufuatia mali, uzalendo wa kishabiki, na ibada ya ngono. Kwa wazi kila jiji la Kikanaani lilikuwa na patakatifu pa Baali na pia vihekalu vijulikanavyo kuwa mahali pa juu. Ndani ya vihekalu hivyo, huenda ikawa ilikuwako mifano ya Baali, na karibu na madhabahu nje kukawako nguzo za mawe—labda ishara za viungo vya uzazi vya Baali. Dhabihu za kibinadamu zenye kuchukiza zilitia madoa ya damu kwenye vihekalu hivyo. Waisraeli walipotiwa unajisi na Ubaali, wao pia walitoa sadaka wana na mabinti wao. (Yer. 32:35) Kulikuwako kigingi kitakatifu kilichowakilisha mama ya Baali, Ashera. Mungu-mke wa mrutubisho, Ashtorethi, mke wa Baali, aliabudiwa kwa sherehe za ngono zilizopotoka, wanaume na wanawake wakiwekwa kuwa makahaba wa hekalu “waliowekwa wakfu.” Si ajabu kwamba Yehova alikuwa ameamuru kumalizwa kwa Ubaali na wafuasi wao wenye unyama. “Jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao.”—Kum. 7:16.b
YALIYOMO KATIKA WAAMUZI
8. Waamuzi chajigawanya kwa kufaa katika visehemu gani?
8 Kitabu hiki chajigawanya kwa kufaa katika sehemu tatu. Sura mbili za kwanza zaeleza hali za wakati huo katika Israeli. Sura za 3 hadi 16 zaeleza ukombozi mbalimbali wa wale waamuzi 12. Kisha Sura za 17 hadi 21 zaeleza matukio fulani yaliyohusu mzozo wa kindani katika Israeli.
9. Ni habari gani ya msingi inayotolewa na sura mbili za ufunguzi za Waamuzi?
9 Hali katika Israeli wakati wa waamuzi (1:1–2:23). Makabila ya Israeli yaelezwa yanaposambaa kukalia maeneo yaliyogawiwa. Hata hivyo, badala ya kuwaondosha kabisa Wakanaani, wanawatia wengi wao katika kazi ngumu ya lazima, wakiwaruhusu wakae miongoni mwa Waisraeli. Kwa hiyo malaika wa Yehova ajulisha rasmi hivi, “Watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.” (2:3) Kwa hiyo, kizazi kipya kinapotokea kisichojua Yehova wala kazi zake, upesi watu wamwacha ili watumikie Mabaali na miungu mingine. Kwa sababu mkono wa Yehova uko juu yao kuleta msiba, ‘wafadhaika sana.’ Kwa sababu ya vichwa vigumu na kukataa kusikiliza hata waamuzi, Yehova haondoshi hata taifa mojawapo la mataifa aliyoacha yatie Israeli kwenye mtihani. Habari hiyo ya msingi ni msaada wa kuelewa matukio yanayofuata.—2:15.
10. Othnieli aamua kwa nguvu gani, na tokeo lawa nini?
10 Mwamuzi Othnieli (3:1-11). Wakisononeka kwa sababu ya utumwa wao kwa Wakanaani, wana wa Israeli waanza kumwitia Yehova kwa ajili ya msaada. Kwanza ainua Othnieli kuwa mwamuzi. Je! Othnieli ahukumu kwa nguvu na hekima ya kibinadamu? La, kwa maana twasoma: “Roho ya BWANA [Yehova, NW] ikamjilia juu yake” ili atiishe maadui wa Israeli. “Nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini.”—3:10, 11.
11. Yehova amtumiaje Ehudi katika kuleta ukombozi kwa Israeli?
11 Mwamuzi Ehudi (3:12-30). Wana wa Israeli wakiisha kutiishwa chini ya mfalme Egloni wa Moabu kwa miaka 18, Yehova asikia kwa mara nyingine miito yao ya msaada, naye ainua Mwamuzi Ehudi. Akiwa na mashauriano ya sirini pamoja na mfalme, Ehudi mwenye kutumia mkono wa kushoto anyakua upanga wake uliotengezewa nyumbani kutoka chini ya joho lake na kumwua Egloni kwa kuingiza upanga huo ndani kabisa ya tumbo la Egloni aliye mnono. Israeli wajiunga upesi upande wa Ehudi katika pigano juu ya Moabu, na bara kwa mara nyingine laonea shangwe pumziko lililotolewa na Mungu, kwa miaka 80.
12. Ni nini kinachoonyesha kwamba ushindi wa Shamgari ni kupitia nguvu za Mungu?
12 Mwamuzi Shamgari (3:31). Shamgari aokoa Israeli kwa kupiga dharuba Wafilisti 600. Kwamba ushindi huo umetolewa kwa nguvu za Yehova yadokezwa na silaha anayotumia—mchokoo wa ng’ombe tu.
13. Ni matukio gani yenye kutokeza yanayofikia upeo kwa wimbo wa ushindi wa Baraka na Debora?
13 Mwamuzi Baraka (4:1–5:31). Kisha Israeli watiishwa kwa mfalme Yabini Mkanaani na amiri jeshi wake, Sisera, anayejivunia magari-farasi ya vita 900 yenye panga za chuma. Kwa mara nyingine Israeli waanzapo kulilia Yehova, Yeye ainua Mwamuzi Baraka, akiungwa mkono vizuri na nabii-mke Debora. Ili Baraka na jeshi lake wasiwe na sababu ya kujivuna, Debora ajulisha kwamba pigano litafanywa kwa mwelekezo wa Yehova, naye atabiri hivi: “BWANA [Yehova, NW] atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke.” (4:9) Baraka akusanya wanaume wa Naftali na Zabuloni kwenye Mlima Tabori. Jeshi lake la 10,000 ndipo latelemka kupigana. Imani yenye nguvu yashinda siku hiyo. ‘Yehova afadhaisha Sisera na magari yake yote, na jeshi lake lote,’ akiwalemea kwa furiko la ghafula katika bonde la Kishoni. “Hakusalia hata mtu mmoja.” (4:15, 16), Yaeli, mke wa Heberi Mkeni, ambaye Sisera akimbilia hema lake, afikisha tamati ya machinjo hayo kwa kugongomelea kichwa chake Sisera kwenye ardhi kwa kigingi cha hema. “Hivyo Mungu akamshinda Yabini.” (4:23) Debora na Baraka washangilia katika wimbo, wakiadhimisha uwezo usioshindika wa Yehova, aliyesababisha nyota zipigane kutoka kwenye buruji zazo juu ya Sisera. Kweli kweli, ni wakati wa ‘kuhimidi Yehova’! (5:2) Miaka arobaini ya amani yafuata.
14, 15. Gideoni apokea ishara gani ya kutegemezwa na Yehova, na utegemezo huo unakaziwaje zaidi katika kushindwa kwa mwisho kwa Wamidiani?
14 Mwamuzi Gideoni (6:1–9:57). Wana wa Israeli wafanya tena yaliyo mabaya, na bara laharibiwa na Wamidiani wenye kuvamia. Yehova, kupitia malaika wake, ampa Gideoni utume kuwa mwamuzi, na Yehova mwenyewe aongeza uhakikisho kwa maneno haya, “Hakika nitakuwa pamoja nawe.” (6:16) Tendo la kwanza la Gideoni la moyo mkuu ni kuvunja-vunja madhabahu ya Baali katika jiji la nyumbani kwake. Majeshi ya adui yaliyoungana sasa yavuka na kuingia Yezreeli, na ‘roho ya Yehova ikaja juu yake Gideoni’ aitapo Israeli wapigane. (6:34) Kwa lile jaribu la kuacha ngozi ya kondoo kwenye umande katika kiwanja cha kupuria, Gideoni apokea ishara yenye kujumlisha mbili kwamba Mungu yu pamoja naye.
15 Yehova amwambia Gideoni kwamba jeshi lake la 32,000 ni kubwa mno na kwamba ukubwa huo huenda ukasababisha wajivunie ushindi. Wenye kuhofu warudishwa nyumbani kwanza, wakiachwa 10,000 peke yao. (Amu. 7:3; Kum. 20:8) Kisha, kwa mtihani wa kunywa maji, wote isipokuwa 300 walio chonjo na wenye kulinda, waondolewa. Gideoni apeleleza kambi ya Kimidiani usiku na ahakikishwa asikiapo mwanamume mmoja akifasiri ndoto moja kumaanisha kwamba “habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni . . . Mungu [wa kweli, NW] amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake.” (Amu. 7:14) Gideoni aabudu Mungu na kisha aweka wanaume wake katika vikundi vitatu kuzunguka kambi ya Kimidiani. Utulivu wa usiku unaondolewa ghafula na mlio wa tarumbeta, na kuvunja-vunja vipande mitungi mikubwa ya maji, na mmweko wa mienge, na wale 300 wa Gideoni wenye kupiga kelele, “upanga wa BWANA [Yehova, NW] na wa Gideoni”! (Amu. 7:20) Kambi ya adui yawa na kizaazaa (machafuko). Wanaume hao wapigana wao kwa wao na kukimbia. Israeli wawafukuza, wakiwachinja na kuwaua wakuu wao. Watu wa Israeli sasa wamwuliza Gideoni awatawale, lakini akataa, akisema, “BWANA [Yehova, NW] atatawala juu yenu.” (8:23) Hata hivyo, afanyiza naivera (efodi) kutokana na nyara za pigano, ambayo baadaye yaja kustahiwa mno na kwa hiyo yawa mtego kwa Gideoni na nyumba yake. Bara lapumzika kwa miaka 40 wakati wa uamuzi wa Gideoni.
16. Ni maangamizi gani yanayompata Abimeleki mnyakuzi wa utawala?
16 Abimeleki, mmoja wa wana wa Gideoni kupitia kwa suria fulani, anyakua mamlaka baada ya kifo cha Gideoni, na kuua nduguze-nusu 70. Yothamu, mwana mchanga zaidi wa Gideoni, ndiye pekee anayeponyoka, naye akiwa juu ya Mlima Gerizimu apiga mbiu ya kuangamizwa kwa Abimeleki. Katika mfano unaohusu miti, yeye afananisha ‘ufalme’ wa Abimeleki na ule wa “mti wa miiba” ulio mnyonge. Upesi Abimeleki aingia katika mzozo wa kindani katika Shekemu na aaibishwa katika kifo, akiuawa na mwanamke apigapo shabaha kwa jiwe la kusagia lililotupwa kutoka juu ya mnara wa Thebesi, na kuponda-ponda fuvu la kichwa chake.—Amu. 9:53; 2 Sam. 11:21.
17. Maandishi yaeleza nini juu ya Waamuzi Tola na Yairi?
17 Waamuzi Tola na Yairi (10:1-5). Hao ndio wanaofuata kutokeza ukombozi kwa nguvu za Yehova, Tola akiwa mwamuzi kwa miaka 23 naye Yairi 22.
18. (a) Yeftha aleta ukombozi gani? (b) Ni nadhiri gani kwa Yehova anayotimiza Yeftha kwa uaminifu? Jinsi gani?
18 Mwamuzi Yeftha (10:6–12:7). Israeli wadumupo katika kugeukia ibada ya sanamu, kasirani ya Yehova yawaka tena juu ya taifa hilo. Watu sasa wadhulumiwa na Waamoni na Wafilisti. Yeftha aitwa tena kutoka uhamishoni aongoze Israeli kwenye pigano. Lakini ni nani mwamuzi halisi katika ubishi huu? Maneno ya Yeftha mwenyewe yatoa jibu: “Yeye BWANA [Yehova, NW], yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni.” (11:27) Roho ya Yehova ijapo juu yake sasa, yeye atoa nadhiri kwamba arejeapo kutoka Amoni katika amani, atatoa kwa Yehova yule atakayetoka kwanza katika nyumba yake amlaki. Yeftha atiisha Amoni kwa machinjo makubwa. Arejeapo kwenye nyumba yake katika Mispa, binti yake mwenyewe ndiye wa kwanza kuja akikimbia kumlaki kwa shangwe kwa ajili ya ushindi wa Yehova. Yeftha atimiza nadhiri yake—la, si kwa dhabihu ya kibinadamu ya kipagani kulingana na sherehe za Baali, bali kwa kumtoa binti yake wa pekee kwenye utumishi kamili katika nyumba ya Yehova iwe kwa sifa Yake.
19. Ni matukio gani yanayoongoza kwenye mtihani wa “Shibolethi”?
19 Wanaume wa Efraimu sasa wapinga kwamba hawakuitwa wakapigane na Amoni, na watisha Yeftha, ambaye alazimika kuwasukuma nyuma. Kwa ujumla, Waefraimu 42,000 wachinjwa, wengi wao kwenye vivushio vya Yordani, ambako wanatambulikana kwa kushindwa kutamka kisahihi neno la kutambulisha “Shibolethi.” Yeftha aendelea kuwa mwamuzi katika Israeli kwa miaka sita.—12:6.
20. Kisha ni waamuzi gani watatu wanaotajwa?
20 Waamuzi Ibzani, Eloni, na Abdoni (12:8-15). Ingawa ni machache yanayotajwa kuhusu hao, vipindi vyao vya kuwa waamuzi vyaelezwa kuwa miaka saba, kumi, na nane.
21, 22. (a) Ni matendo gani ya ushujaa anayofanya Samsoni, na kwa nguvu za nani? (b) Samsoni ashindwaje na Wafilisti? (c) Ni matukio gani yanayofikisha kwenye upeo wa tendo kuu zaidi la Samsoni, na ni nani anayemkumbuka wakati huu?
21 Mwamuzi Samsoni (13:1–16:31). Kwa mara nyingine Israeli watekwa na Wafilisti. Safari hii Samsoni ndiye anayeinuliwa na Yehova kuwa mwamuzi. Wazazi wake wamtoa awe Mnadhiri tangu kuzaliwa, na hilo lataka kwamba wembe wowote usipite kwenye nywele zake kamwe. Akuapo, Yehova ambariki, na baada ya muda ‘roho ya Yehova ikaanza kumtaharakisha.’ (13:25) Siri ya nguvu zake, si misuli ya kibinadamu, bali ni uwezo uliotolewa na Yehova. ‘Roho ya Yehova inapomjilia kwa nguvu’ ndipo anapotiwa nguvu za kumwua simba kwa mikono mitupu na baadaye kulipa kisasi njama ya Kifilisti kwa kupiga dharuba 30 kati yao. (14:6, 19) Wafilisti wanapoendelea kufanya hila kuhusiana na Samsoni kumposa msichana Mfilisti, Samsoni atwaa mbweha 300 na, akiwageuza mikia yao ielekeane, awasha moto katikati ya mikia yao na kuwaachilia wakateketeze mashamba ya nafaka, ya mizabibu, na ya mizeituni ya Wafilisti. Kisha achinja hesabu kubwa ya Wafilisti, akiwapiga “mapigo makuu.” (15:8) Wafilisti washawishi Waisraeli wenzake, wanaume wa Yuda, wamfunge Samsoni na kumpokeza kwao, lakini tena ‘roho ya Yehova yamjia kwa nguvu,’ na pingu zake ni kama zayeyuka kwenye mikono yake. Samsoni apiga dharuba Wafilisti elfu moja—“chungu juu ya chungu”! (15:14-16) Silaha yake ya uharibifu ni nini? Mfupa mbichi wa taya ya punda. Yehova aburudisha mtumishi wake aliyechoka sana kwa kusababisha kwa kimwujiza chemchemi ya maji itokee kwenye uwanja wa pigano.
22 Kisha Samsoni apata malazi kwenye nyumba ya kahaba katika Gaza, ambako Wafilisti wamzingira kimya-kimya. Hata hivyo, roho ya Yehova kwa mara nyingine yathibitisha kuwa pamoja naye ainukapo usiku wa manane, kung’oa milango ya lango la jiji na vigingi vya kando, na kuvibeba hadi kwenye kilele cha mlima unaoelekea Hebroni. Baada ya hilo ampenda Delila mwenye hila. Akiwa chombo chenye nia cha Wafilisti, amfanyia chokochoko mpaka afunua kwamba ujitoaji wake wa Kinadhiri kwa Yehova, kama unavyofananishwa na nywele zake ndefu, ndio chanzo halisi cha nguvu zake kuu. Huku akiwa amelala, Delila apanga nywele zake zikatwe. Safari hii aamkapo apigane yawa kazi bure, kwa maana ‘Yehova amemwacha.’ (16:20) Wafilisti wamkamata, wang’oa macho yake, na kumlazimisha asage akiwa mtumwa katika nyumba yao ya gereza. Ufikapo wakati wa sikukuu kubwa ya kuheshimu mungu wao Dagoni, Wafilisti wamtoa Samsoni nje ili awachekeshe. Kwa kushindwa kuona umaana wa uhakika wa kwamba nywele zake zimekuwa sana tena, wamruhusu asimamishwe katikati ya nguzo mbili kubwa za nyumba inayotumiwa kwa ajili ya ibada ya Dagoni. Samsoni amwitia Yehova: “Ee Bwana MUNGU [Yehova, NW], unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu.” Yehova amkumbuka kweli kweli. Samsoni ashika kwa nguvu nguzo hizo na ‘kuinama kwa nguvu’—nguvu za Yehova—‘nyumba yaanguka, hata wale watu anaoua wakati wa kufa kwake ni wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.’—16:28-30.
23. Ni matukio gani yanayosimuliwa katika sura za 17 hadi 21, nayo yalitukia wakati gani?
23 Sasa twaja kwenye sura za 17 hadi 21, zinazoeleza baadhi ya mizozo ya kindani ambayo kwa huzuni yapiga Israeli wakati huu. Matukio hayo yatokea mapema sana katika kipindi cha waamuzi, kama inavyodokezwa na kutajwa kuwa Yonathani na Fineasi, wajukuu wa Musa na Haruni, kuwa walikuwa wangali hai.
24. Wadani fulani wanasimamishaje dini yenye kujitegemea?
24 Mika na Wadani (17:1–18:31). Mika, mwanamume wa Efraimu, asimamisha makao yake mwenyewe ya kidini yenye kujitegemea, “nyumba ya miungu” ya ibada ya sanamu, ikiwa kamili na mfano uliochongwa na kuhani Mlawi. (17:5) Watu wa kabila la Dani wapitia kwa Mika wakiwa safarini kwenda kutafuta urithi kaskazini. Wateka nyara vinyago vya Mika vya kidini na kuhani wake, nao wapiga hatua kuelekea mbali kaskazini wakaangamize jiji lisilokuwa na habari la Laishi. Badala yalo wajenga jiji lao wenyewe la Dani na kusimamisha mfano wa kuchonga wa Mika. Kwa njia hiyo, wafuata dini ya uchaguzi wao wenyewe wa kujitegemea siku zote ambazo nyumba ya Yehova ya ibada ya kweli yaendelea katika Shilo.
25. Mzozo wa kindani katika Israeli unafikiaje upeo kule Gibea?
25 Dhambi ya Benyamini kule Gibea (19:1–21:25). Tukio lifuatalo kuandikwa latokeza maneno ya baadaye ya Hosea: “Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea.” (Hos. 10:9) Akirudi nyumbani pamoja na suria wake, Mlawi fulani kutoka Efraimu apata malazi usiku kucha kwa mwanamume mzee katika Gibea wa Benyamini. Mabaradhuli (wanaume ovyo) wa jiji wazingira nyumba hiyo, wakidai wataka kufanya ngono na Mlawi huyo. Hata hivyo, badala yake wakubali suria wa Mlawi huyo na kumnajisi usiku kucha. Apatikana amekufa mlangoni asubuhi. Mlawi huyo apeleka maiti yake nyumbani, aikatakata kuwa vipande 12, na kuvipeleka hivi katika Israeli yote. Kwa njia hiyo yale makabila 12 yatiwa kwenye mtihani. Je! wataadhibu Gibea na hivyo kuondosha hali ya ukosefu wa adili katika Israeli. Benyamini waruhusu uhalifu huo mbaya. Yale makabila mengine yakusanyika mbele za Yehova kule Mispa, ambako waazimia kwa kura kwenda kupigana na Benyamini kule Gibea. Baada ya kushindwa kwa umwagaji mkubwa wa damu mara mbili, yale makabila mengine yafanikiwa kwa kuvizia na wakaribia sana kuangamiza kabisa kabila la Benyamini, wakiokoka wanaume 600 peke yao kwenye jabali la Rimoni. Baadaye, Israeli waghairi kwamba kabila moja limekatiliwa mbali. Pindi yatwaliwa ya kuwapa wake Wabenyamini waliopona kutoka kati ya mabinti wa Yabeshi-gileadi na wa Shilo. Huo ndio umalizio wa maandishi yenye mzozano na kutatanika katika Israeli. Kama ambavyo maneno ya umalizio ya Waamuzi yanavyorudia, “Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe.”—Amu. 21:25.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
26. Ni maonyo gani yenye nguvu katika Waamuzi yanayotumika katika siku hii pia?
26 Kuliko kuwa maandishi ya mzozano na umwagaji wa damu tu, kitabu cha Waamuzi chatukuza Yehova kuwa Mkombozi mkuu wa watu wake. Chaonyesha jinsi rehema na ustahimilivu wake ambavyo havilinganiki huonyeshwa kwa watu wa jina lake wanapomjia kwa mioyo yenye kutubu. Waamuzi ni chenye mafaa zaidi katika kutetea moja kwa moja ibada ya Yehova na maonyo yacho yenye nguvu kuhusu upumbavu wa dini ya roho waovu, kuchanganya imani, na mashirika ya ukosefu wa adili. Laana kali ya Yehova ya ibada ya Baali yapasa kutusukuma tujiepushe kabisa na vilinganisho vya kisasa vya kufuatia mali, uzalendo, na ukosefu wa adili za kingono.—2:11-18.
27. Sisi leo twawezaje kufaidika na kielelezo kizuri cha waamuzi?
27 Uchunguzi wa imani isiyo na hofu na moyo mkuu wa waamuzi wapasa kuchochea mioyoni mwetu imani kama hiyo. Si ajabu kwamba wanatajwa kwa kibali sana kwenye Waebrania 11:32-34! Wao walikuwa wapiganaji katika utakaso wa jina la Yehova, lakini si kwa nguvu zao wenyewe. Wao walijua chanzo cha nguvu zao, roho ya Yehova, na kwa unyenyekevu walikiri hivyo. Vivyo hivyo, sisi leo twaweza kutwaa ‘upanga wa roho,’ Neno la Mungu, tukiwa na uhakika kwamba Mungu atatutia nguvu kama alivyowatia Baraka, Gideoni, Yeftha, Samsoni, na wengine. Ndiyo, katika kushinda vipingamizi vikubwa, kwa msaada wa roho ya Yehova, twaweza kuwa wenye nguvu kiroho kama Samsoni alivyokuwa kimwili tukisali kwa Yehova na kumwegemea.—Efe. 6:17, 18; Amu. 16:28.
28. Kitabu cha Waamuzi chaelekezaje kwenye utakaso wa jina la Yehova kupitia Mbegu ya Ufalme?
28 Nabii Isaya arejezea Waamuzi katika sehemu mbili ili kuonyesha jinsi Yehova, bila kushindwa, atavunja-vunja kongwa ambalo maadui Wake huweka juu ya watu wake, kama alivyofanya katika siku za Midiani. (Isa. 9:4; 10:26) Hilo latukumbusha sisi pia wimbo wa Debora na Baraka, ambao wamalizika kwa sala hii ya bidii: “Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee BWANA [Yehova, NW]. Bali wao wampendao na wawe kama jua hapo litokapo kwa nguvu zake.” (Amu. 5:31) Na hao wampendao ni nani? Akionyesha kuwa wao ni warithi wa Ufalme, Yesu Kristo mwenyewe alitumia usemi kama huo kwenye Mathayo 13:43: “Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao.” Kwa hiyo, kitabu cha Waamuzi chaelekeza mbele kwenye wakati ambao Mwamuzi mwadilifu na Mbegu ya Ufalme, Yesu, atakapotumia mamlaka. Kupitia kwake, Yehova ataleta utukufu na utakaso kwa jina Lake, kwa kupatana na sala ya mtunga zaburi kuhusu maadui wa Mungu: “Uwatende kama Midiani, kama Sisera, Kama Yabini, penye kijito Kishoni . . . wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.”—Zab. 83:9, 18; Amu. 5:20, 21.
[Maelezo ya Chini]
a Tafsiri nyingi za kisasa hushuhudia kwamba “miaka kama mia nne na hamsini” ya Matendo 13:19 hailingani na kipindi cha waamuzi bali ni kabla yacho; yaelekea kuhusisha kipindi cha tangu kuzaliwa kwa Isaka katika 1918 K.W.K. hadi kugawanywa kwa Bara la Ahadi katika 1467 K.W.K. (Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 462) Utaratibu ambao waamuzi watajwa katika Waebrania 11:32 ni tofauti na ule katika kitabu cha Waamuzi, lakini uhakika huo haudokezi kwa lazima kwamba matukio katika Waamuzi hayafuati utaratibu wa kronolojia (tarehe za matukio), kwa maana bila shaka Samweli hakufuata Daudi.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 228-9, 948.