Maisha na Huduma ya Yesu’
Safari Nyingine ya Kuhubiri Galilaya
AADA ya miaka miwili hivi ya kuhubiri kwa bidii nyingi, je! Yesu sasa ataanza kupunguza bidii yake na kustarehe? Tofauti na hilo, yeye anapanua utendaji wake wa kuhubiri kwa kuanza safari nyingine bado, safari ya tatu ya Galilaya. Yeye anazuru miji na vijiji vyote katika eneo hilo, akifundisha katika masinagogi na kuhubiri habari njema za Ufalme. Yale anayoona katika safari hii yanamsadikisha hata zaidi kuliko wakati mwingine wowote juu ya uhitaji wa kuzidisha kazi yake ya kuhubiri.
Kokote Yesu aendako, yeye anaona umati wenye uhitaji wa kuponywa kiroho na faraja. Wao ni kama kondoo wasio na mchungaji, waliochoka na kutawanyika, naye anawahurumia. Anawaambia wanafunzi wake: “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.“
Yesu ana mpango wa tendo. Yeye anaita wale mitume 12, ambao yeye alikuwa amewachagua karibu mwaka mmoja mapema. Yeye anawagawa wawili-wawili, akifanya timu sita za wahubiri, na kuwapa maagizo, akisema: “Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kwenenda kwenu, hubirini mkisema Ufalme wa mbinguni umekaribia.
Huo Ufalme ambao walipaswa kuhubiri juu yao ni ule ambao Yesu alikuwa amewafundisha kuomba katika ile sala ya kielelezo. Ufalme huo ulikuwa umekaribia katika maana ya kwamba Mfalme wa Mungu aliyekusudiwa, Yesu Kristo, alikuwapo. Ili kuthibitisha madai ya wanafunzi wake kuwa mawakili wa serikali hiyo yenye uwezo upitao wa kibinadamu, Yesu anawapa uwezo wa kuwaponya wagonjwa na hata kufufua wafu. Yeye anawaagiza kufanya mautumishi hayo bure.
Halafu yeye anawaambia wanafunzi wake wasifanye matayarisho ya mambo ya kimwili kwa ajiii ya safari yao ya kuhubiri. “Msichukue dhahabu, wala fedha wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbiii, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake.“ Wale wanaothamini ujumbe huo wataitikia na kuchanga chakula na makao. Kama asemavyo Yesu: “Na mji wo wote au kijui cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu [mwenye kustahili, NW]; mkae kwake hata mtakapotoka,“
Kisha Yesu anawapa maagizo jinsi ya kuwaendea wenye nyumba wakiwa na ujumbe wa Ufalme. “Nanyi mkiingia katika nyumba,“ yeye anaagiza, “isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kungʼuteni mavumbi ya miguuni mwenu.“
Kwa habari ya mji ambao ungekataa ujumbe wao, Yesu anasema hivi: “Itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.“ Hilo laonyesha kwamba angalau baadhi ya wasio waadilifu ambao wanafunzi wake wangehubiria watakuwapo wakati wa Siku ya Hukumu. Hata hivyo, hawa wafufuliwapo wakati wa Siku ya Hukumu, itakuwa vigumu hata zaidi wao kujinyenyekeza na kukubali Kristo kuwa mfalme kuliko itakavyokuwa kwa watu watakaofufuliwa kutoka ile miji ya kale yenye ufisadi ya Sodoma na Gomora. Mathayo 9:35-10:15; Marko 6:6-12; Luka 9:1-5.
◆ Ni wakati gani Yesu anaanza safari ya tatu ya kuhubiri Galilaya, nayo inamsadikisha juu ya nini?
◆ Anapowatuma mitume wake 12 kuhubiri, yeye anawapa maagizo gani?
◆ Kwa sababu gani ilikuwa sahihi kwa wanafunzi kufundisha kwamba Ufalme ulikuwa umekaribia?
◆ Itakuwaje rahisi zaidi kustahimili kwa Sodoma na Gomora kuliko kwa wale waliokataa wanafunzi wa Yesu?