Sura ya 30
“Kutetea na Kuthibitisha Kisheria Habari Njema”
MNYANYASO mkali dhidi ya Mashahidi wa Yehova umewafanya wapelekwe mbele ya maofisa wa polisi, mahakimu, na watawala duniani pote. Kesi za kisheria zinazohusu Mashahidi zimefikia hesabu ya maelfu mengi, na mamia yazo zimekatwa rufani katika mahakama za juu zaidi. Hilo limekuwa na tokeo kubwa juu ya sheria yenyewe na mara nyingi limeimarisha uhakikisho wa sheria juu ya uhuru wa msingi kwa watu kwa ujumla. Lakini hilo halijawa kusudi kuu la Mashahidi wa Yehova.
Tamaa yao kuu ni kupiga mbiu ya habari njema za Ufalme wa Mungu. Hatua za kisheria wanazochukua si kwa sababu wao ni wachochezi wa kijamii au warekebishaji wa sheria. Lengo lao ni “kutetea na kuthibitisha kisheria habari njema,” kama alivyofanya mtume Paulo. (Flp. 1:7, NW) Kusikizwa kwa kesi mbele ya maofisa wa serikali, iwe kumeombwa na Mashahidi au kwa sababu ya kukamatwa kwa ajili ya utendaji wao wa Kikristo, huonwa pia kuwa fursa za kutoa ushahidi. Yesu Kristo aliwaambia wafuasi wake: “Mtaburutwa mbele ya magavana na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushahidi kwao na kwa mataifa.”—Mt. 10:18, NW.
Furiko la Kimataifa la Hatua za Kisheria
Muda mrefu kabla ya vita ya ulimwengu ya kwanza, makasisi walijitahidi kuzuia kugawanywa kwa fasihi na Wanafunzi wa Biblia katika maeneo yao kwa kuwakaza maofisa wenyeji. Hata hivyo, kufuatia Vita ya Ulimwengu 1, upinzani uliongezeka. Katika nchi moja baada ya nyingine, vizuizi vya kisheria vya kila aina vinavyoweza kuwaziwa viliwekwa mbele ya wale waliokuwa wakijaribu kutii amri ya kiunabii ya Kristo ya kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu kwa kusudi la kutoa ushahidi.—Mt. 24:14.
Wakichochewa na ithibati ya kutimizwa kwa unabii wa Biblia, Wanafunzi wa Biblia waliondoka kwenye mkusanyiko Cedar Point, Ohio, katika 1922, wakiazimia kujulisha ulimwengu kwamba Nyakati za Mataifa zilikuwa zimekwisha na kwamba Bwana alikuwa amechukua uwezo wake mkuu na alikuwa akitawala kutoka mbinguni akiwa Mfalme. Shime ilikuwa ni “Mtangazeni, mtangazeni, mtangazeni, Mfalme na ufalme wake.” Mwaka uo huo, makasisi katika Ujerumani walichochea polisi wawakamate baadhi ya Wanafunzi wa Biblia walipokuwa wakigawanya fasihi za Biblia. Hilo halikuwa tukio la peke yalo. Kufikia 1926, kulikuwa na visa kama hivyo 897 vikingojea kuamuliwa katika mahakama za Ujerumani. Uchochezi mwingi sana ulihusika hivi kwamba katika 1926 ilikuwa lazima Watch Tower Society ianzishe idara ya sheria katika ofisi yayo ya tawi katika Magdeburg. Wakati wa 1928, katika Ujerumani pekee kulikuwa na mashtaka 1,660 dhidi ya Wanafunzi wa Biblia, na mkazo ukazidi kuongezeka mwaka baada ya mwaka. Makasisi waliazimia kukomesha kazi ya Wanafunzi wa Biblia, na walishangilia wakati uamuzi wowote wa mahakama ulipoonyesha kwamba walikuwa wakifanikiwa kwa kadiri fulani.
Katika Marekani, Wanafunzi wa Biblia walikamatwa kwa ajili ya kuhubiri nyumba hadi nyumba katika 1928, katika South Amboy, New Jersey. Katika muda wa mwongo mmoja idadi ya kila mwaka ya waliokamatwa kuhusiana na huduma yao katika Marekani ilizidi 500. Wakati wa 1936 idadi hiyo ilipanda sana—hadi 1,149. Ili kuandaa msaada wa kisheria uliohitajika, ikawa lazima kuwa na idara ya sheria kwenye makao makuu ya Sosaiti pia.
Vilevile utendaji mwingi wa kuhubiri nchini Rumania ulikabili upinzani mkali kutoka kwa wenye mamlaka waliokuwa uongozini. Mashahidi wa Yehova waliogawanya fasihi za Biblia walikamatwakamatwa na kupigwa kikatili. Kuanzia 1933 hadi 1939, Mashahidi huko walikabiliwa na mashtaka 530. Hata hivyo, sheria za nchi hiyo zilihakikisha kwamba kuna uhuru, kwa hiyo kukatwa rufani katika Mahakama Kuu ya Rumania kulileta maamuzi mengi mazuri. Wakati polisi walipoanza kung’amua jambo hilo, wao wangetwaa fasihi na kuwatenda vibaya Mashahidi lakini wangejaribu kuepuka kuchukua hatua za kisheria. Baada ya Sosaiti hatimaye kuruhusiwa usajili ikiwa shirika katika Rumania, wapinzani walijitahidi kuzuia kusudi la usajili huo halali kwa kupata agizo la mahakama la kukataza kugawanywa kwa fasihi za Watch Tower. Uamuzi huo ulibatilishwa na mahakama ya juu zaidi, lakini makasisi walimshawishi waziri wa madhehebu achukue hatua ili kukinza uamuzi huo.
Nchini Italia na Hungaria, kama vile nchini Rumania, fasihi za Biblia zilizotumiwa na Mashahidi zilitwaliwa na polisi chini ya serikali zilizokuwa zikitawala wakati huo. Jambo hilohilo lilifanywa katika Japani, Korea, na Gold Coast (sasa inayoitwa Ghana). Mashahidi wa Yehova waliokuwa wametoka ng’ambo waliamriwa waondoke Ufaransa. Kwa miaka mingi hakuna yeyote wa Mashahidi wa Yehova aliyeruhusiwa kuingia katika Muungano wa Sovieti ili kuhubiri juu ya Ufalme wa Mungu.
Huku harara ya utukuzo wa taifa ikikumba ulimwengu wote kuanzia 1933 hadi miaka ya 1940, Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku na serikali katika nchi moja baada ya nyingine. Maelfu ya Mashahidi waliletwa mbele ya mahakama wakati wa kipindi hicho kwa sababu ya kukataa kwao kwa kudhamiria kusalimu bendera na kusisitiza kwao juu ya kutokuwamo kwa Kikristo. Katika 1950 iliripotiwa kwamba wakati wa miaka 15 iliyotangulia, Mashahidi wa Yehova zaidi ya 10,000 walikuwa wamekamatwa katika Marekani pekee.
Wakati zaidi ya Mashahidi 400 walipoletwa mbele ya mahakama ya Ugiriki katika muda mfupi mwaka 1946, huo haukuwa mwanzo wa kushtakiwa kwao huko. Kulikuwa kumeendelea kwa miaka mingi. Zaidi ya vifungo, faini kubwa zilitozwa, zikifilisisha akina ndugu kifedha. Lakini kama walivyoona hali yao, walisema: “Bwana alifungua njia ili kazi ya kutoa ushahidi ifikie maofisa wa Ugiriki, waliosikia kuhusu kusimamishwa kwa ufalme wa uadilifu; pia mahakimu katika mahakama walikuwa na fursa ileile.” Mashahidi wa Yehova waliliona jambo hilo waziwazi katika ile njia ambayo Yesu alisema wafuasi wake wapaswa kuliona.—Luka 21:12, 13.
Vita Iliyoonekana Kuwa Haiwezekani Kushinda
Wakati wa miaka ya 1940 na 1950, mkoa wa Quebec wa Kanada ulikuwa uwanja wa vita kihalisi. Kukamatwa kwa ajili ya kuhubiri habari njema kulikuwa kumekuwa kukiendelea huko tangu 1924. Kufikia kipupwe cha 1931, Mashahidi fulani mmoja-mmoja walikuwa wakichukuliwa na polisi kila siku, nyakati nyingine mara mbili kwa siku. Gharama za kisheria za Mashahidi katika Kanada zikawa kubwa. Kisha, mapema katika 1947, jumla ya idadi ya kesi zilizohusisha Mashahidi zilizokuwa zikisubiri mahakamani katika Mkoa wa Quebec zikaongezeka kufikia 1,300; na bado, kulikuwa na kikundi kidogo tu cha Mashahidi wa Yehova huko.
Hicho kilikuwa kipindi ambacho Kanisa la Katoliki ya Roma lilikuwa na uvutano mwingi ambao kila mwanasiasa na kila hakimu katika mkoa huo asingepuuza. Katika Quebec makasisi kwa kawaida walionwa kwa heshima kuu, na watu wengine walitii kwa utayari maneno ya padri mwenyeji. Kama vile kitabu State and Salvation (1989) kilivyoeleza hali hiyo: “Kadinali wa Quebec alikuwa na kiti kikuu Bungeni kando tu ya kile cha mkuu wa serikali. Kwa njia moja au nyingine sehemu kubwa ya Quebec ilikuwa chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa kanisa . . . Kwa kweli, lengo la kanisa lilikuwa ni kufanya hali ya kisiasa ya Quebec ipatane na wazo la Katoliki ya Roma ambalo kwalo kweli ni Ukatoliki, kosa ni chochote kisicho cha Ukatoliki, na uhuru ni kutozuiwa kusema na kuishi kulingana na kweli ya Katoliki ya Roma.”
Kusema kibinadamu, magumu yaliyokabili Mashahidi katika Quebec na ulimwenguni pote yalionekana kuwa yasiyoshindika.
Mashtaka ya Kila Aina Yanayoweza Kuwaziwa
Wapinzani wa Mashahidi walichunguza kabisa vitabu vya sheria ili kupata udhuru wowote unaowezekana ili kukomesha utendaji wao. Mara nyingi hao waliwashtaki kwa kuchuuza bila leseni, hivyo wakidai kwamba kazi hiyo ilikuwa biashara. Katika kupinga hilo, kwingineko baadhi ya mapainia walishtakiwa kwa kuzururazurura kwa sababu ilisemekana kwamba hawakuajiriwa kwa njia ya faida.
Kwa miongo mingi, maofisa katika mikoa fulani ya Uswisi walijaribu tena na tena kuainisha ugawanyaji wa fasihi za Biblia wa Mashahidi wa Yehova na uchuuzi wa kibiashara. Wakili wa serikali katika Mkoa wa Vaud unaosema Kifaransa, hasa aliazimia kutoruhusu maamuzi yoyote kutoka kwa mahakama za chini yaliyopendelea Mashahidi yaendelee kutumika.
Katika sehemu moja baada ya nyingine, Mashahidi wa Yehova waliambiwa kwamba wangelazimika kupata ruhusa ili kugawanya fasihi zao au kufanya mikutano yao ya Biblia. Lakini je, ruhusa ilihitajiwa kweli? Mashahidi walijibu “La!” Kwa msingi gani?
Walieleza: ‘Yehova Mungu huamuru mashahidi wake wahubiri gospeli ya ufalme wake, na amri za Mungu ni za juu zaidi na lazima mashahidi wake wazitii. Hakuna baraza lolote la kidunia linalofanyiza sheria au linalohakikisha kwamba sheria inafuatwa ambalo kwa kufaa linaweza kuingilia sheria ya Yehova. Kwa kuwa hakuna uwezo wowote wenye kutawala duniani unaoweza kwa kufaa kukataza kuhubiriwa kwa gospeli, hakuna mamlaka ya ulimwengu au uwezo kama huo unaoweza kutoa ruhusa ya kuhubiri gospeli. Kwa njia moja au nyingine serikali za ulimwengu hazina mamlaka katika jambo hilo. Kuwaomba wanadamu ruhusa ya kufanya jambo fulani ambalo Mungu ameamuru kungekuwa ni kumdhihaki Mungu.’
Mashtaka yaliyowekwa dhidi ya Mashahidi mara nyingi yalitoa ithibati yenye nguvu juu ya uhasama wa kidini. Hivyo, wakati vijitabu Face the Facts (Yakabili Mambo ya Hakika) na Cure vilipogawanywa, mwangalizi wa tawi la Sosaiti katika Uholanzi alipewa samansi na mahakama katika Haarlem, mwaka 1939, ili kujibu shtaka la kudhihaki kikundi cha watu wa Uholanzi. Kwa kielelezo, kiongozi wa mashtaka alitoa hoja kwamba, fasihi za Watch Tower zilisema kwamba viongozi wa Katoliki ya Roma walipata pesa kutoka kwa watu kwa njia ya udanganyifu kwa kudai kuwaweka huru wafu kutoka mahali ambapo hao wafu hawapo—kutoka purgatori, ambayo kulingana na fasihi hizo, Kanisa halingeweza kuthibitisha juu ya kuwapo kwayo.
Kwenye kizimba shahidi mkuu wa viongozi hao wa kidini, “Baba” Henri de Greeve, aliomboleza: “Sikitiko langu kuu ni kwamba mtu wa nje angeweza kuwa na maoni kwamba sisi mapadri ni kikundi cha walaghai na wadhalimu tu.” Alipoombwa ajitetee, mwangalizi wa tawi la Sosaiti alifungua Biblia ya Katoliki na kuonyesha mahakama kwamba yale ambayo kijitabu kilisema kuhusu mafundisho ya Katoliki yalipatana na Biblia yao. Wakati wakili wa Sosaiti alipomuuliza de Greeve ikiwa angeweza kuthibitisha mafundisho ya moto wa mateso na purgatori, yeye alijibu: “Siwezi kuyathibitisha; mimi ninayaamini tu.” Upesi hakimu aling’amua kwamba hayo ndiyo hasa kijitabu hicho kilikuwa kimedai. Kesi ilifungwa, na padri huyo akaondoka mahakamani kwa ghadhabu!
Wakighadhibishwa na utendaji ulioongezeka wa Mashahidi wa Yehova katika sehemu ya mashariki mwa ile iliyokuwa wakati huo Chekoslovakia, makasisi huko waliwashtaki Mashahidi kwa ujasusi. Hali ilikuwa kama ile ambayo mtume Paulo alipata wakati viongozi wa kidini wa Kiyahudi wa karne ya kwanza walipomshtaki kwa uhaini. (Mdo. 24:5) Mamia ya kesi yalienda mahakamani katika 1933-1934, hadi serikali iliposadikishwa kwamba hakukuwa na msingi unaofaa wa mashtaka hayo. Katika mkoa wa Quebec wa Kanada, katika miaka ya 1930 na 1940, Mashahidi pia walipelekwa mahakamani kwa mashtaka ya kufanya uhaini wenye hila. Makasisi wenyewe—wa Katoliki na Protestanti pia, lakini hasa wa Katoliki ya Roma—hata walienda mahakamani wakiwa mashahidi dhidi yao. Mashahidi wa Yehova walikuwa wamefanya nini? Makasisi walitoa hoja kwamba walikuwa wamehatarisha umoja wa taifa kwa kuchapa mambo ambayo yangeweza kusababisha chuki dhidi ya Kanisa la Katoliki ya Roma. Hata hivyo, Mashahidi walijibu kwamba, kwa uhalisi, walikuwa wamegawanya fasihi zilizoletea watu wanyenyekevu faraja kutoka kwa Neno la Mungu lakini kwamba hilo liliwaghadhibisha makasisi kwa sababu mafundisho na mazoea yasiyo ya Kimaandiko yalikuwa yakifunuliwa.
Ni nini kilichowezesha Mashahidi wa Yehova waendelee kusonga mbele wajapokabiliwa na upinzani mwingi hivyo? Ilikuwa imani yao katika Mungu na Neno lake lililopuliziwa, ujitoaji wao usio na ubinafsi kwa Yehova na Ufalme wake, na nguvu inayotokana na utendaji wa roho ya Mungu. Kama vile Maandiko yasemavyo, “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida [ni] ya Mungu na si ile ya kutoka katika sisi wenyewe.”—2 Kor. 4:7, NW.
Mashahidi wa Yehova Wachukua Hatua Kubwa Katika Uwanja wa Sheria
Kwa miongo mingi kabla ya Vita ya Ulimwengu 1, Wanafunzi wa Biblia walikuwa wameshiriki katika kugawanya bure kwa kiwango kikubwa fasihi za Biblia kwenye barabara karibu na makanisa na kutoka nyumba hadi nyumba. Lakini miji na majiji mengi katika Marekani yalipitisha sheria zilizozuia sana “kazi ya kujitolea” kama hiyo. Ni nini kingeweza kufanywa?
The Watch Tower la Desemba 15, 1919 lilieleza: “Tukiamini kuwa ni jukumu letu kutia kila jitihada iwezekanayo ili kutoa ushahidi kuhusu ufalme wa Bwana na bila kuwa wazembe kwa sababu tunaona mlango ukifungwa, na kwa sababu kulikuwa na jitihada nyingi za kupinga kazi ya kujitolea, mipango ilifanywa ili gazeti litumiwe, . . . THE GOLDEN AGE.”a
Hata hivyo, kadiri ambavyo kazi ya kutoa ushahidi nyumba hadi nyumba ilivyoongezeka, ndivyo majaribio ya kutumia sheria za kuizuia au kuikataza yalivyoongezeka. Si nchi zote zilizo na maandalizi ya kisheria yanayofanya iwezekane kupata uhuru wa walio wachache wanapokabiliwa na upinzani wa serikali. Lakini Mashahidi wa Yehova walijua kwamba Katiba ya Marekani ilihakikisha uhuru wa dini, uhuru wa usemi, na uhuru wa uandishi. Kwa hiyo, wakati mahakimu walipotumia vibaya sheria za mahali kwa njia ya kuzuia kuhubiriwa kwa Neno la Mungu, Mashahidi walikata rufani ya kesi zao kwa mahakama za juu zaidi.b
Katika kupitia yale yaliyotukia, Hayden C. Covington, aliyekuwa na daraka kuu katika mambo ya kisheria kwa ajili ya Watch Tower Society, alieleza hivi baadaye: “Ikiwa yale maelfu ya mashtaka yaliyorekodiwa na mahakimu, mahakama za polisi na mahakama za chini hayangalikatiwa rufani, mlima wa maamuzi hayo ya awali ungalirundamana na kuwa kizuizi kikuu katika uwanja wa ibada. Kwa kukata rufani tumezuia kuwapo kwa kizuizi kama hicho. Njia yetu ya ibada imetiwa ndani katika sheria za nchi ya Marekani na nchi nyinginezo kwa sababu ya kufuliza kukata rufani baada ya maamuzi yasiyopendeleka.” Katika Marekani, kesi kadhaa zilifikia Mahakama Kuu Zaidi.
Kuimarisha Uhakikisho wa Uhuru
Mojawapo ya kesi za kwanza zinazohusiana na huduma ya Mashahidi wa Yehova kufikia Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani ilitoka katika Georgia na ilijadiliwa mbele ya Mahakama hiyo mnamo Februari 4, 1938. Alma Lovell alikuwa ameshtakiwa katika mahakama ya Griffin, Georgia, juu ya kukiuka sheria iliyokataza kugawanywa kwa fasihi za aina yoyote bila kibali cha mkuu wa jiji. Miongoni mwa mambo mengine, Dada Lovell alikuwa amewatolea watu gazeti The Golden Age. Mnamo Machi 28, 1938, Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani iliamua kwamba sheria hiyo haikufaa kwa sababu ilizuia uhuru wa uandishi na kuleta ukaguzi.c
Mwaka uliofuata J. F. Rutherford, akiwa wakili wa mlalamishi, alitoa hoja katika Mahakama Kuu Zaidi katika kesi ya Clara Schneider v. State of New Jersey.d Hiyo ilifuatwa, katika 1940 na Cantwell v. State of Connecticut,e ambayo J. F. Rutherford aliandika hoja za kisheria naye Hayden Covington akatoa hoja kwa maneno mbele ya Mahakama. Matokeo yenye kufaa ya kesi hizo yaliegemeza uhakikisho wa kikatiba wa uhuru wa dini, uhuru wa usemi, na uhuru wa uandishi. Lakini kulikuwa na vizuizi.
Vizuizi Vikali Mikononi mwa Mahakama
Suala la kusalimu bendera kama lilivyohusu watoto wa shule wa Mashahidi wa Yehova lilifika kwa mara ya kwanza kwenye mahakama za Amerika mwaka wa 1935 katika kesi ya Carlton B. Nicholls v. Mayor and School Committee of Lynn (Massachusetts).f Kesi hiyo ilipelekwa kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Massachusetts. Katika 1937, mahakama iliamua, kwamba hata iwe ni nini ambayo Carleton Nichols, Jr., na wazazi wake walisema waliamini, imani ya kidini haikuhusika, kwa sababu ilisema, “salamu ya bendera na kiapo cha ushikamanifu yanayozungumziwa hapa hayahusu dini katika njia yoyote ifaayo. . . . Hayahusu maoni ya mtu yeyote kwa Muumba wake. Hayahusu uhusiano wake na Mfanyi wake.” Wakati suala la kusalimu bendera kwa lazima lilipokatiwa rufani kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani katika kesi ya Leoles v. Landersg katika 1937, na tena katika Hering v. State Board of Educationh katika 1938, Mahakama ilitupilia mbali kesi hizo kwa sababu kwa maoni yayo, hilo halikuwa suala la maana la kitaifa kuweza kujadiliwa. Katika 1939 Mahakama tena ilitupilia mbali rufani iliyohusu suala lilo hilo, katika kesi ya Gabrielli v. Knickerbocker.i Siku iyo hiyo, bila kusikiza hoja za maneno, walikubali uamuzi usiopendeleka wa mahakama ya chini katika kesi ya Johnson v. Town of Deerfield.j
Hatimaye, katika 1940, Mahakama ilisikiliza kikamili kesi iliyoitwa Minersville School District v. Gobitis.k Kundi kubwa la mawakili mashuhuri walitoa hoja katika kesi hiyo kwa pande zote. J. F. Rutherford alitoa hoja ya maneno kwa niaba ya Walter Gobitas na watoto wake. Mshiriki wa idara ya sheria ya Chuo Kikuu cha Harvard aliwakilisha Shirika la Mawakili wa Marekani na Chama cha Kutetea Uhuru wa Raia katika kutoa hoja dhidi ya kusalimu bendera kwa lazima. Hata hivyo, hoja zao zilikataliwa, na kukiwa na mmoja tu aliyekuwa na maoni tofauti, Mahakama Kuu Zaidi iliamua mnamo Juni 3, kwamba watoto ambao hawangesalimu bendera wangefukuzwa kutoka shule za umma.
Wakati wa miaka mitatu iliyofuata, Mahakama Kuu Zaidi iliamua dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika kesi 19. Wenye kutokeza zaidi ulikuwa ni uamuzi usiopendeleka, wa mwaka 1942, katika kesi ya Jones v. City of Opelika.l Rosco Jones alikuwa ameshtakiwa kwa kushiriki katika kugawanya fasihi katika barabara za jiji la Opelika, Alabama, bila kulipa kodi ya leseni. Mahakama Kuu Zaidi iliunga mkono hukumu hiyo na kusema kwamba serikali zina haki ya kutoza kiasi kinachofaa cha ada kwa ajili ya kuombaomba na kwamba sheria kama hizo hazingeweza kupingwa hata ikiwa wenye mamlaka wenyeji huenda wakabatilisha ile leseni. Hilo lilikuwa pigo kubwa, kwa sababu sasa jumuiya yoyote, ikichochewa na makasisi au mtu mwingine yeyote aliyepinga Mashahidi, ingeweza kuwapuuza kisheria na hivyo wapinzani huenda wakawaza kwamba hilo lingekomesha utendaji wa kuhubiri wa Mashahidi wa Yehova. Lakini jambo lisilo la kawaida likatukia.
Hali Yabadilika
Katika kesi ya Jones v. Opelika, ule uamuzi ambao ulikuwa pigo kubwa kwa huduma ya hadharani ya Mashahidi wa Yehova, mahakimu watatu kati ya wengine walisema kwamba, wao hawakukubaliana na uamuzi wa walio wengi Mahakamani juu ya kesi hiyo na pia walihisi kwamba walikuwa wamesaidia kuweka msingi wayo katika kesi ya Gobitis. “Kwa kuwa tuliungana katika maoni katika kesi ya Gobitis,” wakaongeza, “tunafikiri hii ni pindi inayofaa kusema kwamba sasa tunaamini kwamba hiyo pia iliamuliwa vibaya.” Mashahidi wa Yehova waliona hiyo kuwa ishara ya kupeleka masuala hayo upya Mahakamani.
Maombi ya Kusikizwa Tena kwa kesi yalipelekwa katika kesi ya Jones v. Opelika. Katika maombi hayo, hoja za kisheria zenye nguvu zilitolewa. Pia yalijulisha hivi kwa imara: “Mahakama hii yapasa ifahamu jambo kuu la hakika, kwamba inashughulika kisheria na watumishi wa Mungu Mweza Yote.” Mifano ya Kibiblia iliyotangulia ikionyesha maana ya hayo ilipitiwa. Uangalifu ulielekezwa kwenye shauri lililotolewa na mwalimu wa torati Gamalieli kwa mahakama kuu ya Kiyahudi ya karne ya kwanza, yaani: “Msijiingize katika mambo ya watu hawa, bali waacheni; . . . ama sivyo, huenda [labda] mkaonwa kuwa wapiganaji dhidi ya Mungu kwa kweli.”—Mdo. 5:34-39, NW.
Hatimaye, katika Mei 3, 1943, katika kesi ya maana sana ya Murdock v. Commonwealth of Pennsylvania,a Mahakama Kuu Zaidi ilibatilisha uamuzi wayo wa kwanza katika kesi ya Jones v. Opelika. Ilijulisha kwamba kodi yoyote ya leseni inayoitishwa kwanza ili mtu aweze kuwa na uhuru wa dini wa kugawanya fasihi za kidini ni jambo lisilo la kikatiba. Kesi hiyo iliandaa fursa kwa Mashahidi wa Yehova katika Marekani na imerejezewa kuwa kiolezo katika mamia ya kesi tangu wakati huo. Mei 3, 1943, ilikuwa siku ya kukumbukwa kikweli kwa Mashahidi wa Yehova kuhusiana na mashtaka mbele ya Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani. Katika siku hiyo moja, kesi 12 kati ya 13 (zote zikiwa zimejumlishwa ziweze kusikizwa na kuamuliwa katika maamuzi manne), Mahakama iliamua kwa kuwapendelea.b
Karibu mwezi mmoja baadaye—mnamo Juni 14, Siku ya Bendera ya kila mwaka ya taifa—Mahakama Kuu Zaidi tena ilibadili uamuzi wayo, wakati huu kuhusiana na uamuzi katika kesi ya Gobitis, wakifanya hivyo katika kesi iliyoitwa West Virginia State Board of Education v. Barnette.c Iliamua kwamba “hakuna ofisa, wa juu au wa chini, awezaye kuonyesha yale yanayokubalika na ya kweli katika siasa, utukuzo wa taifa, dini, au mambo mengineyo au kuwalazimisha raia waungame kwa maneno au watende kupatana na imani yao.” Hoja nyingi zilizotolewa katika uamuzi huo zilitumiwa baadaye nchini Kanada na Mahakama ya Rufani ya Ontario katika kesi ya Donald v. Hamilton Board of Education, na Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada ilikataa kubatilisha uamuzi huo.
Kupatana na uamuzi wayo katika kesi ya Barnette, na katika siku hiyohiyo, katika kesi ya Taylor v. State of Mississippi,d Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani iliamua kwamba Mashahidi wa Yehova hawangeweza kwa kufaa kushtakiwa uhaini kwa kueleza sababu zao za kutosalimu bendera na kwa kufundisha kwamba mataifa yote yako upande wa ushinde kwa sababu yanapinga Ufalme wa Mungu. Maamuzi hayo pia yalitayarisha njia kwa maamuzi yaliyofuata yenye kupendeleka katika mahakama nyinginezo katika kesi zilizohusu wazazi Mashahidi ambao watoto wao walikuwa wamekataa kusalimu bendera shuleni, pamoja na katika masuala yaliyohusu uajiri na utunzi wa watoto. Hali ilikuwa imebadilika kabisa.e
Kufungua Kipindi Kipya cha Uhuru Katika Quebec
Mashahidi wa Yehova walikuwa wakishughulikia suala la uhuru wa ibada katika Kanada. Kuanzia 1944 hadi 1946, mamia ya Mashahidi walikamatwa katika Quebec waliposhiriki katika huduma yao ya hadharani. Sheria ya Kanada iliruhusu uhuru wa ibada, lakini wafanyaghasia walivunja mikutano mahali ambapo Biblia ilikuwa ikijadiliwa. Polisi walitii matakwa ya makasisi Wakatoliki kwamba Mashahidi wa Yehova wakomeshwe. Mahakimu wa mahakama za chini walirundika dhihaka juu ya Mashahidi, ingawa hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya washiriki wa magenge. Ni nini kingeweza kufanywa?
Sosaiti ilipanga kuwe na kusanyiko la pekee katika Montreal mnamo Novemba 2 na 3, 1946. Wasemaji walizungumzia msimamo wa Mashahidi wa Yehova Kimaandiko na kutoka msimamo wa sheria za nchi hiyo. Kisha mipango ilitangazwa kwa ajili ya ugawanyaji wenye mfululizo wa siku 16, kutoka pwani moja hadi ile nyingine—katika Kiingereza, Kifaransa, na Kiukrainia—wa trakti Quebec’s Burning Hate for God and Christ and Freedom Is the Shame of All Canada. Iliripoti kwa kirefu jeuri ya magenge na ukatili mwingineo ambao Mashahidi wa Yehova walikuwa wakitendwa katika Quebec. Hiyo ilifuatwa na trakti ya pili, Quebec, You Have Failed Your People!
Waliokamatwa katika Quebec waliongezeka sana. Ili kukabiliana na hali hiyo, tawi la Kanada la Watch Tower Society lilianzisha idara ya sheria na wawakilishi wakawekwa katika Toronto na Montreal pia. Wakati habari zilipofikia magazeti ya habari kwamba Maurice Duplessis, waziri mkuu wa Quebec, alikuwa ameharibu kimakusudi biashara ya mkahawa ya Frank Roncarelli, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, kwa sababu tu alitoa dhamana kwa ajili ya Mashahidi wenzake, watu wa Kanada walilalamika vikali. Kisha, mnamo Machi 2, 1947, Mashahidi wa Yehova walianzisha kampeni ya taifa lote wakiwaalika watu wa Kanada waombe serikali Taarifa ya Haki za Msingi za Kibinadamu. Sahihi zaidi ya 500,000 zilipatikana—hayo yakiwa maombi mengi zaidi yaliyopata kupelekwa katika Bunge la Kanada! Mwaka uliofuata, hilo lilifuatwa na maombi mengi hata zaidi ili kuegemeza yale ya awali.
Wakati uo huo, Sosaiti iliteua kesi mbili za kujaribia ziweze kukatiwa rufani kwa Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada. Mojawapo ya hizo, Aimé Boucher v. His Majesty The King, ilishughulika na mashtaka ya uhaini yaliyokuwa yamefanywa mara kwa mara dhidi ya Mashahidi.
Msingi wa kesi ya Boucher ulikuwa ile sehemu ambayo mkulima mpole aitwaye Aimé Boucher, alishiriki katika kugawanya trakti Quebec’s Burning Hate. Je, ulikuwa uhaini kujulisha juu ya jeuri ya magenge iliyoelekezwa dhidi ya Mashahidi katika Quebec, juu ya kutokujali sheria upande wa maofisa walioshughulika nao, na ithibati kwamba askofu Mkatoliki na wengine miongoni mwa makasisi Wakatoliki walikuwa wakichochea jeuri hiyo?
Katika kuchanganua trakti iliyogawanywa, mmojawapo mahakimu wa Mahakama Kuu Zaidi alisema: “Hati hiyo ilikuwa na kichwa ‘Chuki Kuu ya Quebec kwa Mungu na Kristo na Uhuru Ni Jambo Linaloaibisha Kanada Yote;’ kwanza ilikuwa na maombi ya utulivu na kutoa sababu katika kukadiria mambo yanayoshughulikiwa katika kuunga mkono kichwa hicho; pili ilikuwa na marejezo ya ujumla kwa mnyanyaso wa kulipa kisasi uliofanywa katika Quebec juu ya Mashahidi wakiwa ndugu za Kristo; masimulizi yenye mambo mengi kuhusu visa hususa vya mnyanyaso; na mwishowe maombi kwa watu wa mkoa huo, katika kulalamika dhidi ya utawala wa magenge na mbinu za gestapo, ili kwamba, kupitia funzo la Neno la Mungu na utii kwa amri zalo, kuwe na ‘mazao mengi ya matunda mema ya upendo kwa ajili Yake na Kristo na uhuru wa kibinadamu.’”
Uamuzi wa Mahakama ulibatilisha mashtaka ya Aimé Boucher, lakini mahakimu watatu kati ya watano waliagiza tu kesi isikizwe tena. Je, hilo lingetokeza uamuzi usio na upendeleo katika mahakama za chini? Maombi yalifanywa kupitia wakili wa Mashahidi wa Yehova ili Mahakama Kuu Zaidi yenyewe isikilize kesi hiyo tena. Kwa kushangaza, hilo lilikubaliwa. Huku maombi yakisubiri majibu, idadi ya mahakimu wa Mahakama iliongezeka, na mmojawapo mahakimu wa awali akabadili maoni yake. Tokeo katika Desemba 1950 lilikuwa ni uamuzi wa 5 dhidi ya 4, Ndugu Boucher akiondolewa mashtaka kabisa.
Mwanzoni, uamuzi huo ulipuuzwa na katibu wa mkuu wa sheria na waziri mkuu pia (aliyekuwa pia mkuu wa sheria) wa mkoa wa Quebec, lakini hatua kwa hatua uliimarishwa katika mahakama. Hivyo mashtaka ya uhaini yaliyokuwa yamezushwa mara kwa mara dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika Kanada yalifutiliwa mbali.
Kesi nyingine ya kujaribia ilikatiwa rufani katika Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada—Laurier Saumur v. The City of Quebec. Hiyo ilikabiliana na sheria za majiji zilizohusika katika hesabu kubwa ya mashtaka katika mahakama za chini. Katika kesi ya Saumur, Sosaiti ilikuwa ikitafuta amri ya kudumu dhidi ya jiji la Quebec ya kuzuia wenye mamlaka wasiingilie kugawanywa kwa fasihi za kidini na Mashahidi wa Yehova. Mnamo Oktoba 6, 1953, Mahakama Kuu Zaidi ilitoa uamuzi wayo. Jibu lilikuwa “Ndiyo” kwa Mashahidi wa Yehova, “La” kwa mkoa wa Quebec. Uamuzi huo pia ulileta ushindi katika kesi nyingine elfu moja ambamo kanuni iyo hiyo ya uhuru wa kidini ilikuwa jambo la msingi. Hiyo ilifungua kipindi kipya cha kazi ya Mashahidi wa Yehova katika Quebec.
Kuelimishwa juu ya Haki na Utaratibu wa Kisheria
Kadiri ambavyo hesabu ya kesi za mahakama iliongezeka katika miaka ya mwisho ya 1920 na baada ya hapo, ikawa lazima Mashahidi wa Yehova wafunzwe juu ya taratibu za kisheria. Kwa kuwa J. F. Rutherford alikuwa wakili na yeye mwenyewe alikuwa ametumikia akiwa hakimu, yeye alifahamu uhitaji wa Mashahidi kupata mwelekezo katika mambo hayo. Hasa tangu 1926 Mashahidi walikuwa wamekuwa wakikazia kuhubiri nyumba hadi nyumba siku za Jumapili, kwa kutumia vitabu vinavyoeleza juu ya Biblia. Kwa sababu ya upinzani dhidi ya kugawanya kwao fasihi za Biblia siku ya Jumapili, Ndugu Rutherford alitayarisha kijitabu Liberty to Preach ili kusaidia wale walioko Marekani waelewe haki zao chini ya sheria. Hata hivyo, yeye binafsi hangeweza kufanya kazi yote ya kisheria, kwa hiyo alipanga ili mawakili wengine watumike wakiwa sehemu ya wafanya kazi wa makao makuu ya Sosaiti. Kwa kuongezea, mawakili wengine waliokuwa sehemu mbalimbali nchini, walishirikiana kwa ukaribu.
Mawakili hawangeweza kuwapo kwa ajili ya kusikizwa kwa maelfu ya kesi zilizohusu utendaji wa kuhubiri wa Mashahidi wa Yehova, lakini wangeweza kutoa shauri lenye thamani. Kwa kusudi hilo, mipango ilifanywa ili kuzoeza Mashahidi wa Yehova wote taratibu za sheria za msingi. Hilo lilifanywa kwenye makusanyiko ya pekee katika Marekani katika 1932 na baadaye, kwenye programu za kawaida za Mikutano ya Utumishi makutanikoni. Sehemu ya “Utaratibu wa Mashtaka” yenye kutia mambo mengi ilichapwa katika Kitabu-Mwaka cha 1933 cha Mashahidi wa Yehova (baadaye ikiwa karatasi iliyotenganishwa). Maagizo hayo yalirekebishwa kulingana na hali. Katika toleo la Consolation la Novemba 3, 1937, shauri zaidi la kisheria lilitolewa kuhusu hali hususa zilizokuwa zikikabiliwa.
Kwa kutumia habari hiyo, mara nyingi Mashahidi walishughulikia utetezi wao wenyewe katika mahakama za kwao, badala ya kupata utumishi wa wakili. Walipata kwamba kwa njia hiyo mara nyingi wangeweza kutoa ushahidi mahakamani na kutoa masuala ifaavyo kwa hakimu, badala ya kesi zao kuamuliwa kwa kutegemea utaratibu wa kisheria tu. Wakati kesi ilipoamuliwa isivyopendeleka, mara nyingi rufani ilikatwa, ingawa baadhi ya Mashahidi walifungwa badala ya kumtumia wakili, ambaye utumishi wake ungehitajiwa katika mahakama ya rufani.
Kadiri ambavyo hali mpya zilitokea na vigezo vikawekwa kwa maamuzi katika mahakama, habari zaidi iliandaliwa ili kuwaweka Mashahidi wakiwa na habari za kisasa. Hivyo, katika 1939 kijitabu Advice for Kingdom Publishers kilichapwa ili kusaidia akina ndugu katika vita vya mahakamani. Miaka miwili baadaye mazungumzo yenye kutia mambo mengi zaidi yaliandaliwa katika kijitabu Jehovah’s Servants Defended. Kilinukuu au kuzungumzia maamuzi 50 tofauti ya mahakama ya Amerika yaliyohusu Mashahidi wa Yehova, pamoja na kesi nyinginezo nyingi, na kikaeleza jinsi vigezo hivyo vya kisheria vingeweza kutumiwa kwa manufaa. Kisha katika 1943, nakala ya Freedom of Worship ilitolewa kwa kila Shahidi na ikasomwa kwa bidii kwenye Mikutano ya Utumishi makutanikoni. Zaidi ya kuandaa muhtasari wa thamani wa kesi za kisheria, kijitabu hicho kilionyesha kikamili sababu za Kimaandiko za kushughulikia mambo kwa njia fulani hususa. Hicho kilifuatwa, katika 1950, na kijitabu chenye habari za wakati huo Defending and Legally Establishing the Good News.
Hiyo yote ilikuwa elimu ya kisheria yenye kuendelea. Hata hivyo, kusudi halikuwa kuwafanya Mashahidi wawe mawakili bali ni kufungua njia ya kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu hadharani na nyumba hadi nyumba.
Kama Kundi la Nzige
Mahali ambako maofisa walijiona kuwa hawako chini ya sheria, nyakati nyingine waliwatenda Mashahidi kikatili sana. Hata hivyo, hata iwe ni njia gani iliyotumiwa na wapinzani wao, Mashahidi wa Yehova walijua kwamba Neno la Mungu hushauri: “Wapendwa, msijilipizie kisasi wenyewe bali iachieni nafasi hasira ya kisasi; kwa maana imeandikwa: “Kisasi ni changu; hakika mimi nitalipa, asema Yehova.” (Rum. 12:19, NW) Hata hivyo, walihisi wakiwa na jukumu kubwa la kutoa ushahidi. Walifanyaje hivyo walipokabiliwa na upinzani wa wakuu?
Ingawa mara nyingi wakati wa miaka ya 1930 makutaniko mbalimbali ya Mashahidi wa Yehova yalikuwa madogo, walikuwa na kifungo chenye nguvu miongoni mwao. Kulipokuwa tatizo kubwa katika sehemu yoyote, Mashahidi kutoka maeneo yanayozunguka walikuwa na hamu ya kusaidia. Kwa kielelezo, katika 1933 katika Marekani, Mashahidi 12,600 walipangwa katika vikundi 78. Walipokamatwa-kamatwa katika sehemu fulani, au wakati wapinzani walipofaulu kukaza stesheni za redio zifute maafikiano ya kutangaza programu zilizotayarishwa na Mashahidi wa Yehova, ofisi ya Sosaiti katika Brooklyn ilijulishwa. Katika muda wa juma moja, msaada wa ndugu ulipelekwa kwenye eneo hilo ili kutoa ushahidi mwingi.
Ikitegemea uhitaji, Mashahidi kuanzia 50 hadi 1,000 wangekutana mahali katika wakati uliopangwa, mara nyingi katika eneo la mashambani karibu na eneo litakalofanyiwa kazi. Wote walikuwa wenye kujitolea; wengine wakija umbali upatao kilometa 320. Vikundi mbalimbali vilipewa eneo ambalo lingeweza kuenezwa kwa labda dakika 30 au hata karibu saa mbili. Kila kikundi cha gari kilipoanza kufanyia kazi sehemu waliyogawiwa, halmashauri ya ndugu waliwasiliana na polisi ili kuwajulisha juu ya kazi iliyokuwa ikifanywa na kuwaandalia orodha ya Mashahidi wote waliokuwa wakifanya kazi katika jumuiya hiyo asubuhi hiyo. Waking’amua kwamba askari wao wenyewe walizidiwa sana na idadi kubwa ya Mashahidi, katika mahali pengi, maofisa waliruhusu kazi iendelee bila kuzuiwa. Katika maeneo mengine walijaza Mashahidi katika magereza yao lakini hawangeweza kufanya zaidi ya hayo. Kwa wowote waliokamatwa, Mashahidi walikuwa na mawakili papo hapo wakiwa na dhamana. Matokeo yalikuwa kama yale ya kundi la nzige wa ufananisho linalorejezewa katika Maandiko kwenye Yoeli 2:7-11 na Ufunuo 9:1-11. Kwa njia hiyo iliwezekana kuendelea kuhubiri habari njema hata walipokabiliwa na upinzani mwingi.
Kufunulia Umma Matendo ya Maofisa Wadhalimu
Lilionwa kuwa jambo la kunufaisha kuwajulisha watu katika maeneo fulani juu ya yale ambayo maofisa wa huko walikuwa wakifanya. Katika Quebec, wakati mahakama zilipowatenda Mashahidi kwa njia iliyofanana na ile ya Mabaraza ya Kuwahukumu Wazushi wa Kidini, barua ilipelekwa kwa washiriki wote wa bunge la Quebec ikieleza mambo ya hakika. Hatua ilipokosa kuchukuliwa, Sosaiti ilipeleka nakala ya barua hiyo kwa wafanya-biashara 14,000 kotekote mkoani. Kisha habari hiyo ikapelekwa kwa wahariri wa magazeti ya habari ili ichapwe.
Katika mashariki mwa Marekani, umma ulifahamishwa kwa matangazo ya redio. Kwenye Betheli ya Brooklyn idadi fulani ya waigizaji waliozoezwa, walio hodari katika mchezo wa kuigiza, walifanyiza yale yaliyoitwa The King’s Theater (Maonyesho ya Mfalme). Wakati maofisa wadhalimu walipowashtaki Mashahidi wa Yehova, utaratibu wote wa mahakama ulirekodiwa kwa maandishi ya ufupizo. Waigizaji walikuwako mahakamani ili kufahamu vema namna ya sauti na njia ya usemi wa polisi, kiongozi wa mashtaka, na hakimu. Baada ya utangazaji mwingi ili kuhakikisha kwamba kungekuwa na wasikilizaji wengi wa redio, Maonyesho ya Mfalme yangeigiza mandhari ya mahakamani kwa njia halisi sana ili kwamba umma ujue hakika yale ambayo maofisa wao walikuwa wakifanya. Baadaye, kwa sababu ya wao kufunuliwa sana kwa umma, baadhi ya maofisa wakawa waangalifu zaidi katika namna walivyoshughulikia kesi zilizohusu Mashahidi.
Hatua ya Pamoja ya Kukabiliana na Uonevu wa Kinazi
Wakati serikali ya Ujerumani ya Nazi ilipoanzisha kampeni ya kukomesha utendaji wa Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani, jitihada za mara kwa mara zilifanywa ili kupata kusikilizwa na wenye mamlaka wa Ujerumani. Lakini hakuna kitulizo chochote kilichopatikana. Kufikia kiangazi cha 1933, kazi yao ilikuwa imepigwa marufuku katika majimbo mengi ya Ujerumani. Kwa hiyo, mnamo Juni 25, 1933, azimio kuhusu huduma yao na makusudi yayo lilipitishwa na Mashahidi wa Yehova kwenye kusanyiko katika Berlin. Nakala zilipelekwa kwa maofisa wakuu wa serikali, na mamilioni zaidi zikagawanywa kwa umma. Hata hivyo, katika Julai 1933 mahakama ilikataa kuruhusu kusikizwa kwa kesi hiyo. Mapema mwaka uliofuata, barua ya kibinafsi kuhusu hali hiyo iliandikwa na J. F. Rutherford kwa Adolf Hitler na kupelekwa kwake na mjumbe wa pekee. Kisha udugu wa ulimwenguni pote ukachukua hatua.
Siku ya Jumapili asubuhi, Oktoba 7, 1934, saa tatu, kila kikundi cha Mashahidi katika Ujerumani kilikusanyika. Walisali ili kupata mwongozo na baraka za Yehova. Kisha kila kikundi kikapeleka barua kwa maofisa wa serikali ya Ujerumani wakijulisha azimio lao imara la kuendelea kumtumikia Yehova. Kabla ya kutawanyika, walizungumzia pamoja maneno ya Bwana wao, Yesu Kristo, kwenye Mathayo 10:16-24. Baada ya hayo walienda kutoa ushahidi kwa majirani wao kuhusu Yehova na Ufalme wake chini ya Kristo.
Siku iyo hiyo, Mashahidi wa Yehova walikutana kotekote duniani na baada ya sala ya pamoja kwa Yehova, wakapeleka barua ya kebo ikionya serikali ya Hitler: “Kuwatenda vibaya kwako Mashahidi wa Yehova kunashangaza watu wema wote duniani na kunavunjia heshima jina la Mungu. Usiendelee kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova; ama sivyo Mungu atakuharibu wewe na chama chako cha kitaifa.” Lakini huo haukuwa ndio mwisho.
Gestapo waliongeza jitihada zao za kukomesha utendaji wa Mashahidi wa Yehova. Baada ya wengi kukamatwa katika 1936, walifikiri kwamba labda walikuwa wamefanikiwa. Lakini mnamo Desemba 12, 1936, Mashahidi kama 3,450 ambao bado walikuwa huru katika Ujerumani waligawanya upesi nchini kote azimio lililochapwa lililoonyesha wazi kusudi la Yehova na likaonyesha uamuzi wa Mashahidi wa Yehova wa kumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu. Wapinzani hawangeweza kuelewa ni kwa njia gani ugawanyaji huo uliwezekana. Miezi michache baadaye, wakati Gestapo walipopuuza mashtaka yaliyofanywa katika azimio hilo, Mashahidi wa Yehova walitayarisha barua ya wazi ambamo kwayo walitaja waziwazi majina ya maofisa wa Nazi waliokuwa wamewatenda kikatili Mashahidi wa Yehova. Katika 1937, barua hiyo pia iligawanywa sana katika Ujerumani. Hivyo matendo ya watu waovu yalifunuliwa ili watu wote waone. Hilo liliwapa umma fursa ya kuamua ni mwendo gani ambao wao binafsi wangefuata kuhusu watumishi hao wa Aliye Juu Zaidi.—Linganisha Mathayo 25:31-46.
Utangazaji wa Duniani Pote Waleta Kitulizo Kidogo
Serikali nyingine pia zimewatendea kikatili Mashahidi wa Yehova, zikikataza mikutano yao na mahubiri ya hadharani. Katika visa fulani serikali hizo zimefanya Mashahidi wakafukuzwa kazini kwa nguvu na watoto wao wakazuiwa kwenda shuleni. Idadi fulani ya serikali pia zimetumia ukatili wa kimwili. Na bado, mara nyingi nchi hizohizo zina katiba inayohakikishia uhuru wa ibada. Kwa kusudi la kuleta kitulizo kwa ndugu zao wanaonyanyaswa, mara nyingi Watch Tower Society imejulisha waziwazi ulimwenguni pote mambo mengi kuhusu mnyanyaso huo. Hayo hufanywa kupitia magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! na nyakati nyingine ripoti hizo hutumiwa na waandishi wa magazeti. Kisha maelfu mengi ya barua za kutoa maombi kwa niaba ya Mashahidi hufurika ndani ya ofisi za maofisa wa serikali kutoka kotekote ulimwenguni.
Kama tokeo la kampeni kama hiyo katika 1937, gavana wa Georgia, katika Marekani alipokea barua zipatazo 7,000 kutoka nchi nne katika kipindi cha siku mbili, na meya wa La Grange, Georgia, pia aligharikishwa na maelfu ya barua. Kampeni kama hizo zilifanywa vilevile kwa niaba ya Mashahidi wa Yehova nchini Argentina katika 1978 na 1979, Benin katika 1976, Burundi katika 1989, Ethiopia katika 1957, Gabon katika 1971, Hispania katika 1961 na tena katika 1962, Jamhuri ya Dominika katika 1950 na 1957, Kamerun katika 1970, Malawi katika 1968, 1972, 1975, na tena katika 1976, Maleya katika 1952, Msumbiji katika 1976, Singapore katika 1972, Swaziland katika 1983, Ugiriki katika 1963 na 1966, Ureno katika 1964 na 1966, pia Yordani katika 1959.
Kielelezo cha hivi karibuni cha yale yanayofanywa na Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote ili kuleta kitulizo kwa ndugu zao wanaoonewa, ni hali katika Ugiriki. Kwa sababu ya mnyanyaso mwingi wa Mashahidi wa Yehova wenye kuchochewa na makasisi wa Orthodoksi ya Ugiriki huko, magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! pia (ambayo yana mwenezo wa ujumla wa kimataifa zaidi ya nakala 22,000,000) yaliripoti mambo mengi kuhusu mnyanyaso huo katika 1986. Mashahidi katika nchi nyinginezo waliombwa wawaandikie maofisa wa serikali ya Ugiriki kwa niaba ya ndugu zao. Wao walifanya hivyo; na kama ilivyoripotiwa katika gazeti la habari la Athens Vradyni, waziri wa sheria aligharikishwa na barua zaidi ya 200,000 kutoka nchi zaidi ya 200 na katika lugha 106.
Mwaka uliofuata, wakati kesi iliyohusu Mashahidi iliposikizwa katika mahakama ya rufani katika Hania, Crete, wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova walikuwapo kutoka nchi nyingine saba (Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japani, Hispania, na Marekani) wakiwa washiriki katika kesi hiyo na kwa kuwaunga mkono ndugu zao Wakristo. Kisha, katika 1988 kufuatia uamuzi usiopendeleka katika Mahakama Kuu Zaidi ya Ugiriki katika kesi nyingine iliyohusu Mashahidi, rufani ilikatwa kwa Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu ya Ulaya. Huko, mnamo Desemba 7, 1990, mahakimu 16 kutoka sehemu zote za Ulaya walipewa orodha ya watu waliokamatwa kama 2,000 na mamia ya kesi za mahakama ambazo kwazo Mashahidi wa Yehova katika Ugiriki walikuwa wamehukumiwa kwa sababu walizungumza juu ya Biblia. (Kwa kweli, watu 19,147 walikuwa wamekamatwa katika Ugiriki kuanzia 1938 hadi 1992.) Tume hiyo iliamua kwa umoja kwamba kesi hiyo yapaswa isikizwe na Mahakama ya Haki za Kibinadamu ya Ulaya.
Katika visa fulani kufunuliwa huko kwa kuvunjwa kwa haki za kibinadamu huleta kiasi fulani cha kitulizo. Hata hivyo, bila kujali hatua inayochukuliwa na mahakimu au watawala, Mashahidi wa Yehova huendelea kumtii Mungu akiwa Mtawala wao Mkuu Zaidi.
Kupata Utambulisho wa Kisheria
Bila shaka idhini ya kuendelea na ibada ya kweli haitokani na mwanadamu yeyote au serikali yoyote ya kibinadamu. Hiyo hutoka kwa Yehova Mungu mwenyewe. Hata hivyo, katika nchi nyingi, ili kupata ulinzi unaotolewa na sheria ya ulimwengu, imethibitika kuwa yenye mafaa kwa Mashahidi wa Yehova kusajiliwa na serikali kuwa shirika la kidini. Mipango ya kununua mali kwa ajili ya ofisi ya tawi au kufanya uchapaji mwingi wa fasihi za Biblia yawezekana kwa kufanyiza mashirika ya kisheria ya mahali. Kwa kupatana na kigezo kilichowekwa na mtume Paulo katika Filipi ya kale katika “kutetea na kuthibitisha kisheria habari njema,” Mashahidi wa Yehova huchukua hatua zifaazo ili kutimiza hayo.—Flp. 1:7, NW.
Nyakati nyingine, imekuwa vigumu sana kufanya hivyo. Kwa kielelezo, katika Austria, ambako mkataba pamoja na Vatikani huhakikishia Kanisa Katoliki kupokea msaada wa kifedha kutoka kwa serikali, jitihada za hapo awali za Mashahidi wa Yehova zilikatizwa na maofisa, waliosema: ‘Kusudi lenu ni kufanyiza shirika la kidini, na shirika la aina hiyo haliwezi kukatibiwa chini ya sheria ya Austria.’ Hata hivyo, katika 1930, waliweza kusajilisha shirika la kugawanya Biblia na fasihi za Biblia.
Katika Hispania, utendaji wa karne ya 20 wa Mashahidi wa Yehova hurudi nyuma kwenye wakati wa Vita ya Ulimwengu 1. Lakini tangu miaka ya mapema ya Baraza la Kuwahukumu Wazushi wa Kidini katika karne ya 15, Kanisa la Katoliki ya Roma na Serikali ya Hispania zilikuwa zimefanya kazi kwa ukaribu sana, isipokuwa katika pindi chache tu. Mabadiliko ya hali ya kisiasa na kidini yalifanya watu mmoja-mmoja waruhusiwe kwa kadiri fulani wafuatie dini nyingine, lakini madhihirisho ya hadharani ya imani yao yalikatazwa. Kujapokuwa hali hizo, Mashahidi wa Yehova walitafuta kupata utambulisho wa kisheria katika Hispania katika 1956 na tena katika 1965. Na bado, haikuwa hadi Bunge la Hispania lilipopitisha Sheria ya Uhuru wa Kidini katika 1967 kwamba maendeleo yoyote halisi yaliwezekana. Hatimaye, mnamo Julai 10, 1970, wakati ambapo Mashahidi walikuwa na idadi iliyozidi 11,000 katika Hispania, wao walipewa utambulisho wa kisheria.
Maombi kwa ajili ya kutambuliwa kisheria kwa Watch Tower Society yalifanywa kwa gavana wa koloni la Ufaransa la Dahomey (sasa iitwayo Benin) mwaka 1948. Lakini haikuwa hadi 1966, miaka sita baada ya nchi hiyo kuwa jamhuri huru, kwamba utambulisho huo wa kisheria ulitolewa. Na bado, utambulisho huo wa kisheria uliondolewa katika 1976 na kisha kurudishwa tena katika 1990 wakati mabadiliko yalipotukia katika hali za kisiasa na katika mtazamo wa serikali kuelekea uhuru wa kidini.
Ingawa Mashahidi wa Yehova walikuwa wameonea shangwe kutambuliwa kisheria katika Kanada kwa miaka mingi, Vita ya Ulimwengu 2 iliandaa kisababu cha wapinzani kusadikisha gavana-jenerali mpya awatangaze Mashahidi kuwa wasio halali. Hilo lilifanywa mnamo Julai 4, 1940. Miaka miwili baadaye, wakati Mashahidi walipopewa fursa ya kujitetea mbele ya halmashauri teule ya Bunge, halmashauri hiyo ilipendekeza kwa dhati kwamba marufuku juu ya Mashahidi wa Yehova na mashirika yao halali iondolewe. Hata hivyo, haikuwa hadi kulipokuwa na mijadala ya mara kwa mara na ya muda mrefu katika Bunge na kazi nyingi ya kupata sahihi za maombi mawili ya taifa lote ikafanywa, ndipo waziri wa sheria, ambaye alikuwa ni Mkatoliki wa Roma, alihisi ameshurutishwa kuondoa marufuku kabisa.
Mabadiliko ya msingi katika mitazamo ya serikali za Ulaya Mashariki yalihitajika kabla Mashahidi wa Yehova hawajaweza kupata utambulisho wa kisheria huko. Hatimaye, baada ya miongo ya kuomba uhuru wa kidini, Mashahidi walitambuliwa kisheria nchini Poland na Hungaria katika 1989, nchini Rumania na Ujerumani Mashariki (kabla ya muungano wayo na Jamhuri ya Muungano wa Ujerumani Magharibi) katika 1990, nchini Bulgaria na ile iliyokuwa wakati huo Muungano wa Sovieti katika 1991, na nchini Albania katika 1992.
Mashahidi wa Yehova hujitahidi kujipatanisha na sheria za taifa lolote. Kwa msingi wa Biblia, wao huunga mkono kwa dhati, kuonyesha heshima maofisa wa serikali. Lakini wakati sheria za wanadamu zinapohitilafiana na amri za Mungu zilizosemwa waziwazi, wao hujibu: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.”—Mdo. 5:29, NW.
Wakati Woga Ufanyapo Watu Wasahau Uhuru wa Msingi
Kwa sababu ya ongezeko la utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa watu wengi na infleshoni ambayo mara nyingi imelazimisha waume na wake pia wafanye kazi za kimwili, Mashahidi wa Yehova katika Marekani wamejipata wakikabiliwa na hali mpya katika huduma yao. Wakati wa mchana, ujirani mwingi uko karibu kuwa tupu, na uvunjaji nyumba umezidi. Watu wanaogopa. Mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1970 na mapema miaka ya 1980, sheria nyingi za kupata leseni ya kuombaomba zilipitishwa ili kujua mahali wageni walipo katika jumuiya mbalimbali. Miji mingine ilitisha kuwakamata Mashahidi wa Yehova iwapo hawangepata idhini. Lakini msingi ufaao wa kisheria ulikuwa tayari umewekwa, kwa hiyo jitihada zingeweza kufanywa ili kushughulikia matatizo hayo nje ya mahakama.
Wakati magumu yanapozuka, wazee wenyeji wanaweza kukutana na maofisa wa mji ili kupata utatuzi. Mashahidi wa Yehova hukataa kwa uthabiti kuomba ruhusa ya kufanya kazi ambayo Mungu ameamuru, na Katiba ya Marekani, ikitegemezwa na maamuzi ya Mahakama Kuu Zaidi, inahakikishia uhuru wa ibada na wa uandishi ambao hautozwi ada yoyote kwanza. Lakini Mashahidi wa Yehova huelewa kwamba watu huogopa, na ikiwa lazima, huenda wakakubali kuwajulisha polisi kabla ya wao kuanza kutoa ushahidi katika eneo fulani. Hata hivyo, ikiwa hakuna mapatano yoyote yanayofikiwa, wakili kutoka makao makuu ya Sosaiti atawasiliana na maofisa wenyeji akieleza juu ya kazi ya Mashahidi wa Yehova, sheria ya katiba inayounga mkono haki yao ya kuhubiri, na uwezo wao wa kuhakikisha kwamba kuna haki hiyo kupitia mashtaka ya kulipwa ridhaa dhidi ya mji huo na maofisa wayo.f
Katika nchi nyingine huthibitika kuwa lazima kwenda mahakamani ili kuimarisha tena uhuru wa msingi ambao kwa muda mrefu umechukuliwa vivi-hivi. Mambo yalikuwa hivyo nchini Finland mwaka 1976 na tena katika 1983. Ili eti kuweka amani kwa ajili ya wenye nyumba, sheria nyingi za huko zilikataza kazi ya kidini iliyohusu kwenda nyumba hadi nyumba. Hata hivyo, ilionyeshwa mahakamani jijini Loviisa na Rauma kwamba kuhubiri nyumba hadi nyumba ni sehemu ya dini ya Mashahidi wa Yehova na kwamba serikali ilikuwa imekubali njia hiyo ya kueneza evanjeli ilipoidhinisha kukatibiwa kwa shirika la kidini la Mashahidi wa Yehova. Pia ilionyeshwa kwamba watu wengi hukaribisha ziara za Mashahidi na kwamba kungekuwa ni kuzuia uhuru kupiga marufuku utendaji huo kwa sababu tu si kila mtu anayeithamini. Kufuatia umalizio wenye mafanikio wa kesi hizo, miji na majiji mengi yalibatilisha sheria zayo.
Kurekebisha Sheria ya Kikatiba
Katika nchi nyingine, utendaji wa Mashahidi wa Yehova umekuwa jambo kuu katika kurekebisha sheria. Kila mwanafunzi wa sheria wa Amerika ajua vema sehemu waliyoshiriki Mashahidi wa Yehova katika kutetea haki za raia katika Marekani. Makala zilizoonyesha kadiri ya ushiriki huo ni kama zifuatazo: “Deni la Sheria ya Kikatiba kwa Mashahidi wa Yehova,” iliyotokea katika Minnesota Law Review, la Machi 1944, na, “Kisababishi cha Marekebisho ya Sheria ya Kikatiba: Mashahidi wa Yehova Katika Mahakama Kuu Zaidi,” iliyochapwa katika University of Cincinnati Law Review, katika 1987.
Kesi zao za mahakamani hufanyiza sehemu kubwa ya sheria za Marekani zinazohusu uhuru wa dini, uhuru wa usemi, na uhuru wa uandishi. Kesi hizo zimeshiriki sehemu kubwa katika kudumisha uhuru si wa Mashahidi wa Yehova tu bali pia wa watu wote. Katika hotuba kwenye Chuo Kikuu cha Drake, mwandishi na mhariri mashuhuri, Irving Dilliard, alisema: “Upende usipende, Mashahidi wa Yehova wamefanya mengi katika kusaidia kudumisha uhuru wetu kuliko kikundi kingine chochote cha kidini.”
Na kuhusu hali katika Kanada, utangulizi wa kitabu State and Salvation—The Jehovah’s Witnesses and Their Fight for Civil Rights unajulisha hivi: “Mashahidi wa Yehova walifunza serikali, na watu wa Kanada, kile kinachomaanishwa na ulinzi wa sheria wa vikundi vinavyofarakana. Zaidi ya hayo, ule . . . mnyanyaso [wa Mashahidi katika mkoa wa Quebec] uliongoza kwenye mfululizo wa kesi ambazo, katika miaka ya 1940 na 1950, ulifikia Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada. Wao pia walishiriki sehemu ya maana katika kubadili mitazamo ya Wakanada kuhusu haki za raia, na wanafanyiza msingi wa sheria za uhuru wa raia katika Kanada leo.” “Mojawapo ya matokeo” ya vita vya kisheria vya Mashahidi kwa ajili ya uhuru wa ibada, kitabu hicho chaeleza, “ni ule utaratibu wa muda mrefu wa mazungumzo na mijadala iliyoongoza kwenye Katiba ya Haki,” ambayo sasa ni sehemu ya sheria za msingi za Kanada.
Ukuu wa Sheria ya Mungu
Hata hivyo, kimsingi, rekodi ya sheria ya Mashahidi wa Yehova imekuwa ushuhuda juu ya usadikisho wao kwamba sheria ya kimungu ndiyo kuu zaidi. Kwenye shina la msimamo ambao wamechukua ni ufahamu wao wa suala la enzi kuu ya ulimwengu wote mzima. Wao hutambua Yehova kuwa Mungu wa pekee wa kweli na Mwenye Enzi Kuu ya ulimwengu wote mzima kwa haki. Kwa hiyo wao huchukua msimamo imara kwamba sheria au maamuzi yoyote ya mahakama ambayo yangekataza kufanya yale ambayo Yehova huamuru si halali na kwamba chombo cha kibinadamu ambacho kimeweka vizuizi hivyo kimepita mamlaka yacho. Msimamo wao ni kama ule wa mitume wa Yesu Kristo, waliojulisha hivi: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.”—Mdo. 5:29, NW.
Kwa msaada wa Mungu, Mashahidi wa Yehova wameazimia kuhubiri habari njema hizi za Ufalme wa Mungu katika dunia yote inayokaliwa kwa ajili ya ushahidi kwa mataifa yote kabla ya mwisho kuja.—Mt. 24:14.
[Maelezo ya Chini]
a Toleo la kwanza lilikuwa na tarehe ya Oktoba 1, 1919. Kugawanywa kwa gazeti hilo na waandamizi walo, Consolation na Amkeni!, kumekuwa kusiko kwa kawaida. Kufikia 1992, mwenezo wa kawaida wa Amkeni! ulikuwa 13,110,000 katika lugha 67.
b Ukiwa mwongozo wa ujumla, walipopelekwa mahakamani kwa sababu ya kutoa ushahidi, Mashahidi wa Yehova walikata rufani ya kesi zao badala ya kulipa faini. Ikiwa walishindwa kesi baada ya rufani kusikizwa, basi badala ya kulipa faini, walienda gerezani, iwapo waliruhusiwa kufanya hivyo na sheria. Kukataakataa kwa Mashahidi kulipa faini kulisaidia kuvunja moyo maofisa fulani wasiendelee kuingilia utendaji wao wa kutoa ushahidi. Ingawa mwongozo huo ungali waweza kufuatwa katika hali fulani, Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) la Aprili 1, 1975, lilionyesha kwamba katika visa vingi faini ingeweza kuonwa kwa kufaa kuwa adhabu ya kisheria, kwa hiyo kuilipa hakungekuwa ni kukubali hatia, kama vile kwenda gerezani hakungemthibitisha mtu kuwa mwenye hatia.
c Lovell v. City of Griffin, 303 U.S. 444 (1938).
d Schneider v. State of New Jersey (Town of Irvington), 308 U.S. 147 (1939).
e 310 U.S. 296 (1940).
f 297 Mass. 65 (1935). Kesi iliyohusu mvulana wa shule mwenye miaka minane, ambaye jina lake huendelezwa kwa usahihi kuwa Carleton Nichols.
g 302 U.S. 656 (1937) (kutoka Georgia).
h 303 U.S. 624 (1938) (kutoka New Jersey).
i 306 U.S. 621 (1939) (kutoka California).
j 306 U.S. 621 (1939) (kutoka Massachusetts).
k 310 U.S. 586 (1940). Walter Gobitas (mwendelezo sahihi), aliyekuwa baba, pamoja na watoto wake William na Lillian, walikuwa wameenda mahakamani ili kuzuia baraza la shule lisiwakataze watoto hao wawili kuhudhuria shule ya umma ya Minersville kwa sababu watoto hao hawangeisalimu bendera ya taifa. Mahakama ya wilaya ya taifa na mahakama ya mzunguko ya rufani pia ziliamua kwa kuwapendelea Mashahidi wa Yehova. Kisha baraza la shule likakata rufani ya kesi hiyo kwa Mahakama Kuu Zaidi.
l 316 U.S. 584 (1942)
a 319 U.S. 105 (1943).
b Wakati wa mwaka wa kalenda wa 1943, maombi na rufani katika kesi za kisheria 24 zilizohusu Mashahidi wa Yehova yalipelekwa kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani.
c 319 U.S. 624 (1943).
d 319 U.S. 583 (1943).
e Kuanzia 1919 hadi 1988, maombi na rufani katika jumla ya kesi 138 zilizohusu Mashahidi wa Yehova yalifanywa katika Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani. Kesi 130 kati yazo zilipelekwa mahakamani na Mashahidi wa Yehova; 8, na washindani wao wa kisheria. Katika kesi 67 Mahakama Kuu Zaidi ilikataa kusikiliza tena kesi hizo kwa sababu, kama vile Mahakama ilivyoona jambo hilo wakati huo, hakukuwa na masuala ya maana ya kikatiba au kisheria ya taifa yaliyozushwa. Katika kesi 47 ambazo Mahakama ilisikiliza, maamuzi yaliwapendelea Mashahidi wa Yehova.
f Kesi ya Jane Monell v. Department of Social Services of the City of New York, 436 U.S. 658 (1978).
[Blabu katika ukurasa wa 680]
Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku na serikali katika nchi moja baada ya nyingine
[Blabu katika ukurasa wa 682]
Kesi ilifungwa, na padri huyo akaondoka mahakamani kwa ghadhabu!
[Blabu katika ukurasa wa 693]
Baadhi ya maofisa wakawa waangalifu zaidi katika namna walivyoshu- ghulikia kesi zilizohusu Mashahidi
[Sanduku katika ukurasa wa 684]
Ushahidi kwa Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani
Alipotokea mbele ya Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani akiwa mshauri wa kisheria katika kesi ya “Gobitis,” Joseph F. Rutherford, mshiriki wa Shirika la Mawakili wa New York na msimamizi wa Watch Tower Society, alikazia fikira waziwazi juu ya umaana wa kujinyenyekeza kwa utawala wa Yehova Mungu. Yeye alisema:
“Mashahidi wa Yehova ni wale wanaotoa ushuhuda kwa jina la Mungu Mweza Yote, ambaye jina lake pekee ni YEHOVA. . . .
“Ninaelekeza fikira kwenye uhakika wa kwamba Yehova Mungu, aliahidi miaka zaidi ya elfu sita iliyopita, juu ya kusimamisha serikali ya uadilifu kupitia Mesiya. Atatimiza ahadi hiyo kwa wakati wake. Mambo ya hakika ya siku za leo kulingana na unabii yanaonyesha kwamba wakati huo u karibu. . . .
“Mungu, Yehova, ndiye chanzo pekee cha uhai. Hakuna mtu mwingine anayeweza kutoa uhai. Jimbo la Pennsylvania haliwezi kutoa uhai. Serikali ya Amerika haiwezi. Mungu alifanya sheria hii [kukataza ibada ya sanamu], kama vile Paulo anavyosema, ili kulinda salama watu Wake na ibada ya sanamu. Mnasema hilo ni jambo dogo. Na ndivyo lilivyokuwa lile tendo la Adamu la kula tunda lililokatazwa. Si lile tofaa alilokula Adamu, bali ni lile tendo lake la kutomtii Mungu. Suala ni ikiwa mwanadamu atamtii Mungu au atatii mfumo fulani wa kibinadamu. . . .
“Ninakumbusha Mahakama hii (si lazima nifanye hivyo) kwamba katika kesi ya ‘Church v. United States’ Mahakama hii ilisema kwamba Amerika ni taifa la Kikristo; na hiyo inamaanisha kwamba ni lazima Amerika itii sheria ya Kimungu. Pia inamaanisha kwamba Mahakama hii inatambua kisheria uhakika wa kwamba sheria ya Mungu ndiyo kuu zaidi. Na ikiwa mtu anaamini kwa kudhamiria kwamba sheria ya Mungu ni kuu zaidi na anajiendesha mwenyewe kwa kudhamiria kulingana nayo, hakuna mamlaka ya kibinadamu inayoweza kudhibiti au kuingilia dhamiri yake. . . .
“Naomba nikubaliwe kuelekeza fikira kwenye jambo hili: kwamba mwanzoni mwa kila kikao cha Mahakama hii mtangazaji hutangaza maneno haya: ‘Mungu okoa Marekani na Mahakama hii inayoheshimika.’ Na sasa ninasema, Mungu okoa Mahakama hii inayostahika isitende kosa litakaloongoza watu hawa wa Marekani kuwa jamii yenye mamlaka kamili na kuharibu uhuru wote unaohakikishiwa na Katiba. Hili ni jambo lililo takatifu kwa kila Mwamerika anayempenda Mungu na Neno Lake.”
[Sanduku katika ukurasa wa 687]
Matukio Yaliyotangulia Kubadilishwa kwa Uamuzi
Katika 1940, wakati Mahakama Kuu Zaidi ya Amerika ilipoamua, katika kesi ya “Minersville School District v. Gobitis,” kwamba watoto wa shule wangetakiwa kusalimu bendera, mahakimu wanane kati ya tisa waliunga mkono uamuzi huo. Ni Hakimu Stone pekee aliyepinga. Lakini miaka miwili baadaye, walipokuwa wakiandikisha tofauti zao katika kesi ya “Jones v. Opelika,” mahakimu wengine watatu (Black, Douglas, na Murphy) walitumia pindi hiyo kusema kwamba waliamini kwamba kesi ya “Gobitis” ilikuwa imeamuliwa vibaya kwa sababu ilikuwa imeshusha uhuru wa kidini. Hiyo ilimaanisha kwamba mahakimu wanne kati ya tisa waliunga mkono kubadilishwa kwa uamuzi katika kesi ya “Gobitis.” Mawakili wawili kati ya wale watano waliokuwa wamepuuza uhuru wa kidini walistaafu. Kulikuwa na wengine wawili wapya (Rutledge na Jackson) wakati kesi iliyofuata ya kusalimu bendera ilipopelekwa kwenye Mahakama Kuu Zaidi. Katika 1943, katika kesi ya “West Virginia State Board of Education v. Barnette,” wote wawili waliunga mkono uhuru wa kidini badala ya jambo la kushurutishwa kusalimu bendera. Hivyo, huku mahakimu 6 dhidi ya 3 zikiunga mkono, mahakama ilibadilisha msimamo iliyokuwa imechukua katika kesi tano za mapema (“Gobitis,” “Leoles,” “Hering,” “Gabrielli,” na “Johnson”) zilizokuwa zimekatwa rufani katika Mahakama hiyo.
Kwa kupendeza, katika kupinga uamuzi wa kesi ya “Barnette,” Hakimu Frankfurter alisema hivi: “Kama vile imekuwa katika nyakati zilizopita, Mahakama itabadilisha msimamo wayo mara kwa mara. Lakini ninaamini kwamba Mahakama hii haijapata kamwe kubatilisha maamuzi yayo ili kupunguza uwezo wa serikali ya kidemokrasia, kabla ya kesi hizi za Mashahidi wa Yehova (isipokuwa mabadiliko madogomadogo yaliyopatikana baadaye).”
[Sanduku katika ukurasa wa 688]
“Aina ya Uenezaji-Evanjeli wa Wamishonari Ulio wa Kikale”
Katika 1943, katika kesi ya “Murdock v. Pennsylvania,” Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani ilisema hivi, miongoni mwa mambo mengine:
“Kugawanywa kwa trakti za kidini kwa mkono ni aina ya uenezaji-evanjeli wa wamishonari ulio wa kikale—wa kale kama historia ya matbaa ya uchapaji. Kumekuwa kani yenye nguvu katika mashirika mbalimbali ya kidini kwa muda wa miaka mingi. Aina hiyo ya uenezaji-evanjeli inatumiwa leo kwa kiwango kikubwa na mafarakano mbalimbali ya kidini ambayo makolpota wayo hupeleka Gospeli kwa maelfu na maelfu ya makao na hutafuta kupata wenye kushikamana na imani yao kupitia ziara za kibinafsi. Ni zaidi ya kuhubiri; ni zaidi ya kugawanya fasihi za kidini. Ni jumla ya hayo yote mawili. Kusudi layo ni kueneza evanjeli kama lile la mkutano wa kuhuisha. Aina hiyo ya utendaji wa kidini ni ya cheo kilekile cha juu chini ya Rekebisho la Kwanza kama vile ibada katika makanisa na mahubiri kutoka kwa mimbari. Hudai ulinzi uleule ambao utendaji mwingineo wa kidini unaokubalika na ulio wa kawaida hupewa. Pia hudai uhakikisho wa uhuru wa usemi na uhuru wa uandishi kama ule mwingineo.”
[Sanduku katika ukurasa wa 690]
“Haki Sawa kwa Wote”
Katika 1953, chini ya kichwa kilichoko juu, mwandikaji safu za magazeti Mkanada aliyejulikana sana wakati huo aliandika hivi: “Moto mkubwa wa sherehe wapaswa kuwashwa kwenye Parliament Hill ili kusherehekea uamuzi wa Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada katika kesi ya Saumur [iliyoletwa mbele ya Mahakama na Mashahidi wa Yehova]; moto wa sherehe unaostahili tukio la maana sana. Ni maamuzi machache katika historia ya kutoa hukumu ya Kanada yanayoweza kuwa yalikuwa yenye umaana zaidi. Mahakama Kuu Zaidi imenufaisha Kanada zaidi ya mahakama nyinginezo. Hakuna mahakama nyingine inayostahili shukrani zaidi kutoka kwa Wakanada. . . . Uhuru huo wastahili sherehe kubwa kuliko ile inayoweza kufanywa.”
[Sanduku katika ukurasa wa 694]
Taarifa Madhubuti kwa Serikali ya Nazi
Mnamo Oktoba 7, 1934, barua ifuatayo ilipelekwa kwa serikali ya Ujerumani na kila kutaniko la Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani:
“KWA MAOFISA WA SERIKALI:
“Neno la Yehova Mungu, kama lilivyoandikwa katika Biblia Takatifu, ndiyo sheria kuu zaidi, na kwetu sisi hilo ndilo mwongozo wetu pekee kwa sababu ya kujitoa kwetu kwa Mungu na sisi ni wafuasi wa kweli na wenye moyo mweupe wa Kristo Yesu.
“Wakati wa mwaka uliopita, na kinyume cha sheria ya Mungu na kwa kuvunja haki zetu, mmetukataza sisi tukiwa Mashahidi wa Yehova kukutana pamoja ili kujifunza Neno la Mungu na kumwabudu na kumtumikia. Katika Neno lake yeye hutuamuru sisi kwamba tusiache kukusanyika pamoja. (Waebrania 10:25) Kwetu sisi Yehova aamuru: ‘Nyinyi ni mashahidi wangu kwamba mimi ni Mungu. Nendeni mkawaambie watu ujumbe wangu.’ (Isaya 43:10, 12; Isaya 6:9; Mathayo 24:14) Kuna hitilafiano la moja kwa moja kati ya sheria yenu na sheria ya Mungu, na kwa kufuata mwongozo wa mitume waaminifu, ‘twapaswa kumtii Mungu badala ya watu,’ na hilo tutafanya. (Matendo 5:29) Kwa hiyo hii ni kuwajulisha kwamba hata iweje tutatii amri za Mungu, tutakutana pamoja kwa ajili ya funzo la Neno lake, na tutaabudu na kumtumikia kama alivyoamuru. Ikiwa serikali yenu au maofisa wenu watufanyia jeuri kwa sababu tunamtii Mungu, basi damu yetu itakuwa juu yenu na mtatoa jibu kwa Mungu Mweza Yote.
“Hatuhusiki na mambo ya kisiasa, bali tumejitoa kikamili kwa ufalme wa Mungu chini ya Kristo Mfalme wake. Hatutamjeruhi au kumuumiza yeyote. Tungefurahi kukaa kwa amani na kufanya mema kwa watu wote kwa kadiri tupatavyo nafasi, lakini, kwa kuwa serikali yenu na maofisa wayo yaendelea katika jitihada zenu za kutulazimisha tusitii sheria ya juu zaidi ya ulimwenguni pote, tunashurutika kuwajulisha sasa kwamba, kwa fadhili yake, tutamtii Yehova Mungu na kumtumaini Yeye kabisa aweze kutuokoa kutoka uonevu wote na wenye kuonea.”
[Sanduku katika ukurasa wa 697]
Mashahidi Waliopigwa Marufuku Waeleza Msimamo Wao Waziwazi
Tengenezo la Mashahidi wa Yehova lilipigwa marufuku na serikali katika Kanada mwaka 1940. Baada ya hapo kulikuwa na mashtaka zaidi ya 500. Mashahidi wangeweza kutoa utetezi gani? Kwa heshima lakini kwa uthabiti, walitolea Mahakama taarifa inayokaribiana na haya yafuatayo:
‘Sitaomba radhi kwa sababu ya vitabu hivi. Vinafunza njia ya kwenda kwenye uhai wa milele. Ninaviamini kikweli kwamba vinaeleza kusudi la Mungu Mweza Yote la kusimamisha Ufalme wa uadilifu duniani. Kwangu mimi, vimekuwa baraka kubwa sana maishani mwangu. Kwa maoni yangu kuviharibu vitabu hivi na ujumbe wa Mungu uliomo kungekuwa ni kufanya dhambi dhidi ya Mweza Yote, kwa njia ileile ambayo ingekuwa dhambi kuchoma Biblia yenyewe. Kila mtu ni lazima achague kama atajasiria kupoteza kibali cha wanadamu au kupoteza kibali cha Mungu Mweza Yote. Kwangu mimi nimechukua msimamo upande wa Bwana na Ufalme Wake, na ninajitahidi kuheshimu jina la Aliye Juu Zaidi, ambalo ni Yehova, na ikiwa nitaadhibiwa kwa ajili ya hilo, basi wale wanaotoa adhabu hiyo watatwaa daraka mbele za Mungu.’
[Sanduku katika ukurasa wa 698]
Maoni ya Wabunge wa Serikali ya Kanada juu ya Jambo Hilo
Hapa pana taarifa zilizotolewa na baadhi ya washiriki wa Bunge la Kanada katika 1943 walipohimiza waziri wa sheria kuondoa marufuku juu ya Mashahidi wa Yehova na mashirika yao ya kisheria:
“Hakuna ithibati iliyotolewa mbele ya halmashauri na idara ya sheria iliyoonyesha kwamba mashahidi wa Yehova wangepaswa kutangazwa kuwa shirika lisilo halali wakati wowote . . . Ni jambo la kufedhehesha kwa Serikali ya Kanada kwamba watu wapaswa kuhukumiwa kwa ajili ya masadikisho yao ya kidini katika njia ile ambayo watu hawa wanaoonewa wamehukumiwa.” “Kwa maoni yangu ni chuki ya kidini ya wazi kabisa inayodumisha marufuku hiyo.”—Bw. Angus MacInnis.
“Maoni ya wengi wetu yamekuwa kwamba hao ni watu wasio na dhara, wasio na kusudi lolote la kukosea serikali. . . . Kwa nini marufuku haijaondolewa? Haiwezi kuwa kwa sababu ya hofu yoyote kwamba shirika hili ni hatari kwa hali njema ya serikali, au kwamba utendaji walo unapinga jitihada ya vita. Hakujapata kamwe kuwa na ithibati hata iliyo ndogo zaidi kwamba hivyo ndivyo mambo yalivyo.”—Bw. John G. Diefenbaker.
“Inafanya mtu afikiri kama hatua dhidi ya Mashahidi wa Yehova ilikuwa hasa kwa sababu ya mtazamo wao kuelekea Wakatoliki wa Roma, badala ya kwamba wana mtazamo unaopotoa.”—Bw. Victor Quelch.
[Sanduku katika ukurasa wa 699]
“Utumishi kwa Lengo la Kupata Uhuru wa Kidini”
“Isingekuwa haki kupuuza pitio hili fupi la matatizo ya Mashahidi wa Yehova na Serikali bila kurejezea utumishi kwa lengo la kupata uhuru wa kidini chini ya Katiba yetu ambao umetolewa kwa sababu ya kusisitiza kwao. Katika miaka ya karibuni wamechukua wakati mwingi wa mahakama kuliko kikundi kinginecho cha kidini, na kwa umma wameonekana kuwa wasio na akili, lakini wameshikamana na masadikisho yao ya kudhamiria, na kama tokeo mahakama za Taifa zimetoa mfululizo wa maamuzi ambayo yameleta na yakapanua uhakikisho wa uhuru wa kidini kwa raia wa Amerika, na yamelinda na kuongeza uhuru wao wa kiraia. Kesi zipatazo thelathini na moja ambazo walihusika zililetwa mbele ya Mahakama Kuu Zaidi katika miaka mitano kuanzia 1938 hadi 1943, na maamuzi ya kesi hizo na nyinginezo za baadaye yamesitawisha sana lengo la uhuru wa Haki za Msingi za Kibinadamu kwa ujumla, na kulindwa kwa uhuru wa kidini hasa.”—“Church and State in the United States,” cha Anson Phelps Stokes, Buku 3, 1950, ukurasa 546.
[Picha katika ukurasa wa 700, 701]
Washangilia Katika Uhuru Wao wa Kuabudu
Katika nchi nyingi ambako zamani Mashahidi wa Yehova hawakuwa na uhuru kamili wa kidini, sasa wao hukutana waziwazi kwa ajili ya ibada na hushiriki na wengine habari njema za Ufalme wa Mungu bila kuzuiwa.
Quebec, Kanada
Wakati wa miaka ya 1940, Mashahidi wachache hapa katika Châteauguay walishambuliwa na wafanyaghasia. Katika 1992, Mashahidi zaidi ya 21,000 katika wilaya ya Quebec walikuwa wakikutana kwa uhuru katika Majumba ya Ufalme yao
St. Petersburg, Urusi
Katika 1992, watu 3,256 walijitoa kwa ajili ya ubatizo kwenye mkusanyiko wa kwanza wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova katika Urusi
Palma, Hispania
Baada ya Mashahidi wa Yehova katika Hispania kutambuliwa kihalali katika 1970, ishara kubwa kwenye mahali pa kukutania zilionyesha shangwe yao kwa kuweza kukusanyika waziwazi
Tartu, Estonia
Mashahidi katika Estonia wamekuwa wakishukuru kwa kupokea fasihi za Biblia bila kizuizi tangu 1990
Maputo, Msumbiji
Katika muda wa mwaka mmoja baada ya Mashahidi wa Yehova kutambuliwa kihalali huku katika 1991, makutaniko zaidi ya 50 ya Mashahidi wenye idili yalikuwa yakiendesha huduma yayo jijini na viungani vyalo
Cotonou, Benin
Walipowasili kwenye mkutano katika 1990, wengi walishangaa kuona kitambaa kikubwa chenye maandishi ya kuwakaribisha Mashahidi wa Yehova. Huku walifahamu kwamba marufuku juu ya ibada yao ilikuwa imeondolewa
Prague, Chekoslovakia
Wanaoonyeshwa chini ni wachache waliomtumikia Yehova chini ya marufuku ya serikali kwa miaka 40. Katika 1991, walishangilia kuwa pamoja kwenye mkusanyiko wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova katika Prague
Luanda, Angola
Marufuku ilipoondolewa katika 1992, watu mmoja-mmoja na familia zaidi ya 50,000 walikaribisha Mashahidi wajifunze Biblia pamoja nao
Kiev, Ukrainia
Katika nchi hii, wengi huhudhuria mikutano (mara nyingi katika majumba yaliyokodiwa), hasa tangu Mashahidi wa Yehova watambuliwe
kihalali katika 1991
[Picha katika ukurasa wa 679]
Katika kesi 138 zilizohusu Mashahidi wa Yehova, rufani na maombi yamepelekwa kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani. Katika kesi 111 kati ya hizo, Hayden Covington (anayeonyeshwa hapa) alitumikia akiwa wakili wa sheria, kuanzia 1939 hadi 1963
[Picha katika ukurasa wa 681]
Maurice Duplessis, waziri mkuu wa Quebec, akipiga magoti hadharani mbele ya Kadinali Villeneuve mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1930 na kuweka pete kwenye kidole chake ukiwa uthibitisho wa uhusiano wa karibu kati ya Kanisa na Serikali. Katika Quebec, mnyanyaso wa Mashahidi wa Yehova ulikuwa mwingi hasa
[Picha katika ukurasa wa 683]
W. K. Jackson, aliyekuwa mmoja wa wafanyakazi wa sheria katika makao makuu ya Sosaiti, alitumikia miaka kumi akiwa mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 685]
Rosco Jones, ambaye kesi yake iliyohusu huduma ya Mashahidi wa Yehova ilipelekwa mara mbili kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani
[Picha katika ukurasa wa 686]
Mahakimu wa Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani ambao, 6 dhidi ya 3 walikataa jambo la kushurutishwa kusalimu bendera katika kesi ya “Barnette,” wakiunga mkono uhuru wa ibada. Hiyo ilibatilisha uamuzi wa mapema wa Mahakama iyo hiyo katika kesi ya “Gobitis”
Watoto walio- husika katika kesi hizo
Lillian na William Gobitas
Marie na Gathie Barnette
[Picha katika ukurasa wa 689]
Aimé Boucher, aachiliwa huru na Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada katika uamuzi ambao ulifutilia mbali mashtaka ya uhaini dhidi ya Mashahidi wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 691]
Trakti hii, katika lugha tatu, ilijulisha Kanada yote juu ya ukatili waliotendwa Mashahidi wa Yehova katika Quebec
[Picha katika ukurasa wa 692]
Ikawa lazima kufundisha Mashahidi wa Yehova taratibu za kisheria ili waweze kushughulika na upinzani katika huduma yao; hivi ni baadhi ya vichapo vya kisheria walivyotumia