Sura 11
Uasi-Imani—Njia ya Kwenda Kwa Mungu Yazibwa
1, 2. (a) Ni kwa nini miaka 400 ya kwanza ya historia ya Jumuiya ya Wakristo ni ya maana? (b) Yesu alisema juu ya ukweli gani unaohusu uchaguzi?
NI KWA nini miaka 400 ya kwanza ya historia ya Jumuiya ya Wakristo ni ya maana sana? Kwa sababu ile ile ambayo miaka ya kwanza ya maisha ya mtoto ni ya maana—kwa sababu ndiyo miaka ya ukuzi ambapo msingi huwekwa kwa ajili ya utu wa mtu wa wakati ujao. Karne za mapema za Jumuiya ya Wakristo zafunua nini?
2 Kabla hatujajibu swali hilo, acheni tukumbuke ukweli fulani ambao Yesu alieleza: “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” Barabara ya starehe ni pana; ile ya kanuni zinazofaa ni nyembamba.—Mathayo 7:13, 14.
3. Ni miendo gani miwili iliyopatikana wakati wa kuanzishwa kwa Ukristo?
3 Wakati wa mwanzo wa Ukristo, kulikuwako njia mbili zilizopatikana kwa wale waliokubali imani hiyo isiyopendwa na wengi—kushikilia mafundisho na kanuni zisizoridhiana za Kikristo na Maandiko au kuvutwa kuelekea njia pana na ya kuchukua mambo kirahisi ya kuridhiana na ulimwengu wa wakati huo. Kama tutakavyoona, historia ya miaka 400 ya kwanza yaonyesha ni njia gani ambayo walio wengi hatimaye walichagua.
Utongozi wa Falsafa
4. Kulingana na mwanahistoria Durant, Roma ya kipagani iliathirije kanisa la mapema?
4 Mwanahistoria Will Durant aeleza hivi: “Kanisa lilitwaa desturi fulani za kidini na namna-namna zilizokuwa kawaida ya Roma [ya kipagani] ya kabla ya Ukristo—kanzu na mavazi mengine ya makuhani wapagani, matumizi ya ubani na maji matakatifu katika mitakaso, kuchomwa kwa mishumaa na nuru ya daima mbele ya altare, ibada ya watakatifu, muundo wa basilika, sheria ya Roma kuwa msingi wa sheria ya kanisa, jina Pontifex Maximus kwa ajili ya Askofu Mkuu Zaidi, na, katika karne ya nne, lugha ya Kilatini . . . Upesi maaskofu, badala ya maofisa wa Kiroma, wangekuja kuwa ndio chanzo cha agizo na makao ya mamlaka katika miji; makasisi wa majimbo, au maaskofu wakuu, wangekuja kuunga mkono, ikiwa si kung’oa, maliwali wa jimbo; na baraza la maaskofu wa jimbo lingekuja kuchukua mahali pa bunge la jimbo. Kanisa la Roma lilifuata hatua za serikali ya Kiroma.”—The Story of Civilization: Part III—Caesar and Christ.
5. Mtazamo wa kuridhiana na ulimwengu wa kipagani wa Kiroma ulitofautianaje na maandishi ya Kikristo ya mapema?
5 Mtazamo huu wa kuridhiana na ulimwengu wa Kiroma watofautiana waziwazi na mafundisho ya Kristo na mitume wake. (Ona kisanduku, ukurasa 262.) Mtume Petro alishauri hivi: “Wapenzi, . . . naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha, mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu, mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu.” Paulo alishauri waziwazi hivi: “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? . . . Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana [Yehova, NW], Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.”—2 Petro 3:1, 2, 17; 2 Wakorintho 6:14-17; Ufunuo 18:2-5.
6, 7. (a) “Mababa” wa mapema wa kanisa walivutwaje na falsafa ya Kigiriki? (b) Uvutano wa Kigiriki ulijionyesha katika mafundisho gani hasa? (b) Paulo alitoa onyo gani juu ya falsafa?
6 Ijapokuwa onyo hilo lililo wazi, Wakristo waasi-imani wa karne ya pili walitwaa sura ya dini ya kipagani ya Roma. Wakaacha vyanzo vyao vyenye kutakata vya Biblia na badala yake wakajivika majoho na majina ya Roma ya kipagani na kufyonza falsafa ya Kigiriki. Profesa Wolfson wa Chuo Kikuu cha Harvard aeleza katika The Crucible of Christianity kwamba katika karne ya pili, kulikuwako mwingio mkubwa katika Ukristo wa “watu wasio Wayahudi waliozoezwa kifalsafa.” Wao walistaajabia hekima ya Wagiriki na waliwaza kuwa waliona mifanano kati ya falsafa ya Kigiriki na mafundisho ya Maandiko. Wolfson aendelea hivi: “Nyakati nyingine wanajieleza kwa njia mbalimbali kwamba falsafa ni zawadi maalumu ya Mungu kwa Wagiriki kupitia kusababu kwa kibinadamu kama ambavyo Maandiko yalivyo kwa Wayahudi kupitia ufunuo wa moja kwa moja.” Yeye aendelea hivi: “Mababa wa Kanisa . . . walianza kazi yao ya hatua kwa hatua ili kuonyesha jinsi, katika lugha ya kupendeza ambayo kwayo Maandiko hupenda kujifafanua, kulivyo na mafundisho yaliyofichwa ya wanafalsafa yakiwa yamepenyezwa katika istilahi za kiufundi zisizokuwa wazi zilizobuniwa katika Chuo chao, Lyceum, na Porch [vitovu vya mazungumzo ya kifalsafa].”
7 Mtazamo huo uliacha njia wazi kwa ajili ya falsafa na matumizi ya maneno ya Kigiriki yapenye mafundisho ya Jumuiya ya Wakristo, hasa katika nyanja za fundisho la Utatu na imani katika nafsi isiyoweza kufa. Kama Wolfson anavyotoa taarifa hii: “Mababa wa [kanisa] walianza kuchunguza rundo la matumizi ya maneno ya kifalsafa ili wapate istilahi mbili za kiufundi, ambazo moja ingetumiwa kuwa mtajo wa uhalisi wa utofauti wa kila mshiriki wa Utatu akiwa mtu mmoja na ule mwingine ungetumiwa kuwa mtajo wa umoja wao wa pamoja wa msingi.” Hata hivyo, walilazimika kukubali kwamba “ile dhana ya Mungu wa nafsi tatu ni fumbo lisiloweza kutatuliwa kwa kusababu kwa kibinadamu.” Tofauti na hilo, Paulo alikuwa ametambua waziwazi hatari ya uchafu huo na ‘ugeuzaji wa Injili alipoandikia hivi Wakristo Wagalatia na Wakolosai: “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure [Kigiriki, phi·lo·so·phiʹas] na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”—Wagalatia 1:7-9; Wakolosai 2:8; 1 Wakorintho 1:22, 23.
Ufufuo Watanguliwa
8. Watu wameng’ang’ana na tatizo gani, na dini zilizo nyingi zimejaribuje kulitatua?
8 Kama tulivyokwisha kuona katika kitabu hiki chote, sikuzote binadamu ameng’ang’ana na tatizo la maisha yake mafupi na yenye ukomo ambayo mwisho wayo ni kifo. Ni kama Gerhard Herm mtungaji Mjerumani alivyotoa taarifa hii katika kitabu chake The Celts—The People Who Came Out of the Darkness: “Miongoni mwa vitu vingine dini ni njia ya kupatanisha watu na uhakika wa kwamba siku fulani lazima wafe, kwamba ni kwa njia ya ahadi ya maisha bora zaidi baada ya kufa, kuzaliwa upya, au yote mawili.” Karibu kila dini hutegemea imani ya kwamba nafsi ya kibinadamu haiwezi kufa na kwamba baada ya kifo hiyo husafiri kwenda kwenye maisha ya baadaye au huhama kuingia katika kiumbe kingine.
9. Miguel de Unamuno msomi Mhispania alikata maneno gani kuhusu imani ya Yesu juu ya ufufuo?
9 Karibu dini zote za Jumuiya ya Wakristo leo hufuata imani hiyo. Miguel de Unamuno, msomi Mhispania aliye maarufu wa karne ya 20, aliandika hivi juu ya Yesu: “Badala yake yeye aliamini ufufuo wa mnofu [kama katika kisa cha Lazaro (ona kurasa 249-52)], kulingana na namna ya Kiyahudi, si katika kutoweza kufa kwa nafsi, kulingana na namna ya Kiplato [ya Kigiriki]. . . . Vithibitisho vya hilo vyaweza kuonwa katika kitabu chochote chenye haki cha fasiri.” Yeye alikata maneno hivi: “Kutoweza kufa kwa nafsi . . . ni fundisho la kifalsafa la kipagani.” (La Agonía Del Cristianismo [Maumivu Makali ya Ukristo]) Hilo “fundisho la kifalsafa la kipagani” lilipenya ndani ya mafundisho ya Jumuiya ya Wakristo, hata ingawa Kristo kwa wazi hakuwa na wazo kama hilo.—Mathayo 10:28; Yohana 5:28, 29; 11:23, 24.
10. Ni nini yaliyokuwa baadhi ya matokeo ya imani katika nafsi isiyoweza kufa?
10 Uvutano wenye hila wa falsafa ya Kigiriki ulikuwa sababu kubwa ya uasi-imani uliofuata kifo cha mitume. Fundisho la Kigiriki la nafsi isiyoweza kufa lilidokeza kuwapo kwa vituo mbalimbali kwa ajili ya nafsi—mbinguni, moto wa helo, purgatori, paradiso, Limbo.a Kwa kutumia kwa werevu mafundisho hayo, ikawa rahisi kwa jamii ya kikasisi kutiisha makundi yao na kuwahofisha kuhusu Maisha ya baadaye na kuyatoza kwa nguvu zawadi na sadaka. Hilo latuongoza kwenye swali jingine: Jamii tofauti ya kikasisi ya Jumuiya ya Wakristo ilianzaje?—Yohana 8:44; 1 Timotheo 4:1, 2.
Jinsi Jamii ya Makasisi Ilivyoanzishwa
11, 12. (a) Ni ishara gani nyingine ya uasi-imani iliyotokea? (b) Mitume na wazee katika Yerusalemu walitimiza fungu gani?
11 Dalili nyingine ya uasi-imani ilikuwa kupa kisogo huduma ya ujumla ya Wakristo wote, kama ambavyo Yesu na mitume walikuwa wamefundisha, na kuingilia jamii ya kikasisi na viongozi wa kidini peke yao ambayo ilisitawi katika Jumuiya ya Wakristo. (Mathayo 5:14-16; Warumi 10:13-15; 1 Petro 3:15) Wakati wa karne ya kwanza, baada ya kifo cha Yesu, mitume wake, pamoja na wazee wengine Wakristo waliostahili kiroho katika Yerusalemu, walitumika kutoa shauri na kuelekeza kundi la Kikristo. Hakuna yeyote wao aliyepiga ubwana juu ya wale wengine—Wagalatia 2:9.
12 Katika mwaka 49 W.K., ikawa lazima kwao wakutane katika Yerusalemu ili watatue maswali yaliyohusu Wakristo kwa ujumla. Simulizi la Biblia hutuambia kwamba baada ya mazungumzo yaliyowahusisha wao wote, “ikawapendeza mitume na wazee [pre·sbyʹte·roi] na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; . . . Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao, Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu.” Kwa wazi mitume na wazee walitumika wakiwa wakala wa usimamizi wenye kuongoza kwa ajili ya makundi ya Kikristo yaliyotapakaa.—Matendo 15:22, 23.
13. (a) Ni mpango gani uliokuwako kwa ajili ya uangalizi wa mahali katika makundi ya kwanza ya Kikristo? (b) Sifa za wazee wa kundi zilikuwa nini?
13 Sasa kwa kuwa kikundi hicho chenye kuongoza katika Yerusalemu kilikuwa ndicho mpango wa mapema wa Kikristo kwa ajili ya usimamizi wa ujumla wa Wakristo wote, kilikuwa na mfumo gani wa mwelekezo katika kila kundi, mahali palo? Barua ya Paulo kwa Timotheo yaonyesha wazi kwamba makundi yalikuwa na waangalizi (Kigiriki, e·piʹsko·pos) ambao walikuwa wazee wa kiroho (pre·.sbyʹte·.roi), wanaume waliokuwa wamestahili kwa mwenendo wao na hali yao ya kiroho ya kufundisha Wakristo wenzao. (1 Timotheo 3:1-7; 5:17) Katika karne ya kwanza, wanaume hao hawakuwa jamii ya kikasisi iliyo tofauti. Hawakuvaa kanzu yoyote ya kuwatofautisha. Kitofautisho chao kilikuwa ni hali yao ya kiroho. Kwa kweli, kila kundi lilikuwa na baraza la wazee (waangalizi), wala si utawala wa bwana-mkubwa mmoja.—Matendo 20:17; Wafilipi 1:1.
14. (a) Maaskofu wa Jumuiya ya Wakristo waliingiaje hatimaye mahali pa waangalizi Wakristo? (b) Ni nani aliyeng’ang’ania daraja la kwanza kati ya maaskofu?
14 Ilikuwa tu baada ya wakati kupita kwamba neno e·piʹsko·posb (mwangalizi, msimamizi) likaja kubadilishwa kuwa “askofu,” kumaanisha kasisi mwenye mamlaka juu ya washiriki wa kikasisi katika dayosisi yake. Ni kama anavyoeleza Myesuiti Mhispania Bernardino Llorca: “Kwanza, hakukuwako tofauti kubwa iliyofanywa kati ya maaskofu na wazee (Kiingereza, presbyters), na fikira zilikazwa tu juu ya maana ya maneno: askofu ni sawa na msimamizi; presbyter ni mwanamume mzee. . . . Lakini kidogo kidogo tofauti hiyo ikawa wazi zaidi, kwa kuwapa mtajo askofu wasimamizi walio mashuhuri zaidi, ambao walikuwa na mamlaka kuu zaidi ya kikasisi na uwezo wa kuwekelea mikono na kukabidhi ukasisi.” (Historia de la Iglesia Católica [Historia ya Kanisa Katoliki]) Kwa kweli, maaskofu wakaanza kutenda katika aina fulani ya mfumo wa utawala wa mtu mmoja, hasa kuanzia karne ya nne. Viongozi wa dini, au baraza la makasisi lenye kutawala, likaanzishwa, na punde si punde askofu wa Roma, akidai kuwa mwandamizi wa Petro, alikiriwa na wengi kuwa askofu mkuu zaidi na papa.
15. Ni pengo gani lililoko kati ya uongozi wa mapema wa Kikristo na ule wa Jumuiya ya Wakristo?
15 Leo cheo cha askofu katika makanisa tofauti-tofauti ya Jumuiya ya Wakristo ni cheo cha umashuhuri na nguvu, kwa kawaida kikiwa na malipo makubwa, na mara nyingi chahusishwa na jamii ya watawala maalumu wa kila taifa. Lakini katikati ya hali yao ya kiburi na kukwezwa na usahili wa tengenezo chini ya Kristo na wazee, au waangalizi, wa makundi ya mapema ya Kikristo, kuna tofauti kubwa mno. Nasi tuseme nini juu ya pengo kubwa mno lililo kati ya Petro na waitwao waandamizi wake, ambao wametawala katika maskani yenye anasa ya Vatican?—Luka 9:58; 1 Petro 5:1-3.
Mamlaka ya Kipapa na Umashuhuri
16, 17. (a) Twajuaje kwamba kundi la Kiroma la mapema halikuwa chini ya uongozi wa askofu au papa? (b) Matumizi ya jina la cheo “papa” yalisitawije?
16 Miongoni mwa makundi ya kwanza yaliyokubali mwelekezo kutoka kwa mitume na wazee katika Yerusalemu ni lile lililokuwa katika Roma, ambako ukweli wa Kikristo yaelekea uliwasili wakati fulani baada ya Pentekoste 33 W.K. (Matendo 2:10) Kama vile kundi jingine lolote la Kikristo la wakati huo, lilikuwa na wazee, waliotumikia wakiwa baraza la waangalizi bila ya yeyote wao kuwa mkuu zaidi. Hakika hakuna wowote wa waangalizi wa mapema zaidi katika kundi la Roma walionwa na wenzao kuwa maaskofu au kuwa papa, kwa kuwa utawala wa kiaskofu wa mtu mmoja kule Roma ulikuwa ungali haujasitawi. Ni vigumu kutaja mwanzo barabara wa utawala wa askofu mmoja. Uthibitisho watoa dalili kwamba ulianza kusitawi katika karne ya pili.—Warumi 16:3-16; Wafilipi 1:1.
17 Jina “papa” (kutoka kwa paʹpas la Kigiriki, baba) halikutumiwa wakati wa karne mbili za kwanza. Aliyekuwa Myesuiti Michael Walsh aeleza hivi: “Mara ya kwanza Askofu wa Roma kuitwa ‘Papa’ yaelekea ni karne ya tatu, na jina hilo alipewa Papa Kalisto . . . Kufikia mwisho wa karne ya tano ‘Papa’ kwa kawaida lilimaanisha Askofu wa Roma na si mwingine. Hata hivyo, haikuwa mpaka karne ya saba, kwamba Papa akawa aweza kusisitiza kwamba jina hilo litumiwe kumhusu yeye pekee.”—An Illustrated History of the Popes.
18. (a) Ni nani aliyekuwa mmoja wa maaskofu wa kwanza wa Roma kupiga ubwana wake? (b) Dai la kipapa la daraja la kwanza limetegemezwa juu ya nini? (c) Mathayo 16:18, 19 yapasa kuelewekaje kwa kufaa?
18 Mojawapo maaskofu wa kwanza wa Roma kupiga ubwana wake alikuwa Papa Leo I (papa, 440-461 W.K.). Michael Walsh aendelea kueleza: “Leo alijitwalia lile ambalo wakati mmoja lilikuwa jina la cheo cha kipagani la Pontifex Maximus, ambalo lingali latumiwa na mapapa leo, na ambalo, mpaka kuelekea mwisho wa karne ya nne, lilitumiwa na Wamaliki Waroma.” Msingi wa vitendo vya Leo I ulikuwa ni fasiri ya Katoliki ya maneno ya Yesu yanayopatikana katika Mathayo 16:18, 19. (Ona kisanduku, ukurasa 268.) Yeye “alijulisha rasmi kwamba kwa sababu Mt. Petro alikuwa wa kwanza miongoni mwa Mitume, kanisa la Mt. Petro lapasa kupewa daraja la kwanza miongoni mwa makanisa.” (Man’s Religions) Kwa hatua hii, Leo I akaonyesha wazi kwamba ijapokuwa maliki alikuwa na mamlaka ya kiserikali katika Konstantinopo katika Mashariki, yeye alikuwa na mamlaka ya kiroho kutoka Roma katika Magharibi. Mamlaka hiyo ilionyeshwa zaidi wakati Papa Leo III alipomvika taji Charlemagne maliki wa Milki Takatifu ya Kiroma katika 800 W.K.
19, 20. (a) Papa ameonwaje katika nyakati za kisasa? (b) Ni yapi baadhi ya majina rasmi mbalimbali ya cheo cha papa? (c) Twaweza kuona utofautiano gani kati ya mwenendo wa mapapa na ule wa Petro?
19 Tangu 1929 papa wa Roma ameonwa na serikali za nchi kuwa mtawala wa serikali yenye enzi yayo tofauti, Jiji la Vatican. Kwa hiyo, Kanisa Roma Katoliki, tofauti na matengenezo mengine ya kidini, laweza kupeleka wajumbe wa kibalozi, wanunsio, kwenye serikali za ulimwengu. (Yohana 18:36) Papa huheshimiwa kwa kupewa majina mengi ya cheo, baadhi yayo yakiwa ni Vikari wa Yesu Kristo, Mwandamizi wa Mkuu wa Mitume, Askofu Mkuu Zaidi wa Kanisa la Ulimwengu Wote Mzima, Mzee wa Magharibi, Mkuu wa Italia, Mwenye Enzi Kuu wa Jiji la Vatican. Yeye huchukuliwa kwa fahari na sherehe. Yeye hupewa heshima anazopewa kiongozi wa Serikali. Tofauti na hilo, angalia jinsi Petro, ambaye hudhaniwa kuwa papa wa kwanza na askofu wa Roma, alivyoitikia kwa tendo wakati akida Mroma Kornelio alipoanguka miguuni pake ili amsujudie: “Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.”—Matendo 10:25, 26; Mathayo 23:8-12.
20 Sasa swali ni hili, Mamlaka na umashuhuri mwingi hivi ulipataje kuwa wa kanisa lenye kuasi imani la karne hizo za mapema? Usahili na unyenyekevu wa Kristo na Wakristo wa mapema viligeuzwaje kuwa fahari na umashuhuri wa Jumuiya ya Wakristo?
Msingi wa Jumuiya ya Wakristo
21, 22. Ni badiliko gani kubwa linalodhaniwa lilitukia katika maisha ya Konstantino, na alilitumiaje kwa faida yake?
21 Upeo wa dini mpya hii katika Milki ya Kiroma ulikuwa ni 313 W.K., tarehe ya kunakoitwa kuongoka kwa Maliki Konstantino kuingia “Ukristo.” Kuongoka huko kulitukiaje? Katika 306 W.K., Konstantino alirithi baba yake na hatimaye, pamoja na Lisinio, akawa mtawala-mwenzi wa Milki ya Kiroma. Yeye alivutiwa na jinsi mama yake alivyojitoa kwenye Ukristo na jinsi yeye mwenyewe alivyokuwa na imani katika himaya ya kimungu. Kabla hajaenda kupigana karibu na Roma kwenye Daraja Milvian katika 312 W.K., alidai kwamba aliambiwa katika ndoto aandike herufi za kwanza za “Kikristo”—herufi za Kigiriki khi na rho, herufi mbili za jina la Kristo katika Kigiriki—kwenye ngao za askari-jeshi wake.c Wakiwa na ‘talasimu takatifu’ hiyo, majeshi ya Konstantino yalishinda adui yake Maksentio.
22 Muda mfupi baada ya kushinda pigano hilo, Konstantino alidai kwamba yeye alikuwa amekuwa mwumini, ijapokuwa yeye hakubatizwa mpaka tu kabla ya kifo chake miaka 24 hivi baadaye. Yeye alikuja kuungwa mkono na waliodai kuwa Wakristo katika milki yake kwa “yeye kukubali [herufi za Kigiriki] Chi-Rho kuwa kifananishi chake . . . Hata hivyo, Chi-Rho tayari zilikuwa zimetumiwa kuwa muunganisho wa herufi katika maandishi ya kipagani na ya Kikristo.”—The Crucible of Christianity, kilichohaririwa na Arnold Toynbee.
23. (a) Kulingana na mfafanuzi mmoja, ni wakati gani Jumuiya ya Wakristo ilipoanza? (b) Ni kwa nini twaweza kusema kwamba Kristo hakuanzisha Jumuiya ya Wakristo?
23 Kama tokeo, msingi wa Jumuiya ya Wakristo ukawa umewekwa. Ni kama alivyoandika mtangazaji-habari wa Uingereza Malcolm Muggeridge katika kitabu chake The End of Christendom: “Jumuiya ya Wakristo ilianza na Maliki Konstantino.” Hata hivyo, pia alitoa maelezo haya ya ufahamu: “Waweza hata kusema kwamba Kristo mwenyewe alikomesha Jumuiya ya Wakristo kabla haijaanza kwa kutoa taarifa kwamba ufalme wake haukuwa wa ulimwengu huu—mojawapo taarifa zake zenye matokeo makubwa na zenye maana.” Nayo ni mojawapo taarifa zinazopuuzwa sana na watawala wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo na wa kisiasa.—Yohana 18:36.
24. Ni badiliko gani lililotokea katika kanisa wakati Konstantino ‘alipoongoka’?
24 Kwa kuungwa mkono na Konstantino, dini ya Jumuiya ya Wakristo ikawa dini rasmi ya Serikali ya Roma. Elaine Pagels, profesa fulani wa dini, aeleza hivi: “Maaskofu Wakristo, ambao wakati fulani walikuwa shabaha ya kukamatwa, kuteswa, na kuuawa, sasa wakasamehewa kutozwa kodi, wakapewa zawadi kutoka hazina ya kimaliki, umashuhuri, na hata mamlaka barazani; makanisa yao yakapata utajiri mpya, mamlaka, na umaarufu.” Wao walikuwa wamekuwa marafiki wa maliki, marafiki wa ulimwengu wa Kiroma.—Yakobo 4:4.
Konstantino, Uzushi, na Fundisho
25. (a) Kufikia wakati wake Konstantino ni mjadala gani wa kitheolojia uliokuwa umepamba moto? (b) Kabla ya karne ya nne, ni hali gani iliyokuwako kwa habari ya kuelewa uhusiano wa Kristo na Baba yake?
25 Ni kwa nini “kuongoka” kwa Konstantino kulikuwa kwa maana sana? Kwa sababu yeye akiwa maliki alikuwa na uvutano mkubwa sana katika mambo ya kanisa la “Kikristo” lililogawanyika kimafundisho, na yeye alitaka umoja katika milki yake. Wakati huo mjadala ulikuwa umepamba moto kati ya maaskofu wenye kuongea Kigiriki na wale wenye kuongea Kilatini juu ya “uhusiano kati ya ‘Neno’ au ‘Mwana’ wa ‘Mungu’ aliyechukua umbo la Yesu, na ‘Mungu’ mwenyewe, sasa akiitwa ‘Baba’—jina lake, Yahweh, limesahauliwa kwa ujumla.” (The Columbia History of the World) Baadhi yao walipendelea maoni yenye kuungwa mkono na Biblia kwamba Kristo, yule Loʹgos, aliumbwa na kwa hiyo ni mdogo kwa Baba yake. (Mathayo 24:36; Yohana 14:28; 1 Wakorintho 15:25-28) Kati yao alikuwa Ariasi, kasisi fulani katika Aleksandria, Misri. Kwa kweli, R. P. C. Hanson, profesa fulani wa elimu ya kidini, atoa taarifa hii: “Hakuna mwanatheolojia yeyote katika Kanisa la Mashariki au Magharibi kabla ya kulipuka kwa ubishi wa Kiaria [karne ya nne], ambaye kwa maana fulani hamwoni Mwana kuwa mdogo kwa Baba.”—The Search for the Christian Doctrine of God.
26. Kufikia mapema mwa karne ya nne, hali ilikuwa nini kuhusu fundisho la Utatu?
26 Wengine walichukua maoni hayo ya udogo wa Kristo kuwa uzushi na wakakengeuka zaidi kuelekea ibada ya Yesu kuwa “Mungu Aliyechukua Umbo Jingine.” Hata hivyo, Profesa Hanson atoa taarifa kwamba kipindi kinachozungumzwa (karne ya nne) “hakikuwa historia ya kutetea fundisho [la Utatu] lililoafikiwa na kusuluhishwa dhidi ya mashambulizi ya uzushi [wa Kiaria] ulio wazi. Kuhusu habari ambayo hasa ilikuwa inazungumzwa bado hakukuwako fundisho lolote halali.” Yeye aendelea hivi: “Pande zote ziliamini kwamba zilikuwa na mamlaka ya Maandiko ikiziunga mkono. Kila mmoja ulieleza ule mwingine kuwa huo sio wa halali, haufuati mapokeo na si wa Kimaandiko.” Hesabu za kidini zilikuwa zimegawanywa kabisa juu ya suala hilo la kitheolojia.—Yohana 20:17.
27. (a) Konstantino alifanya nini ili kujaribu kutatua mjadala juu ya asili ya Yesu? (b) Baraza la Nisea liliwakilisha kanisa kwa kadiri gani? (c) Je! Kanuni ya Imani ya Nisea ilitatua ubishi juu ya fundisho la Utatu lenye kusitawi?
27 Konstantino alitaka umoja katika milki yake, na katika 325 W.K. aliitisha baraza la maaskofu wake katika Nisea, eneo la upande wa Mashariki, lenye kuongea Kigiriki la milki yake, ng’ambo nyingine ya Bosporasi kutoka jiji jipya la Konstantinopo. Husemekana kwamba maaskofu kati ya 250 mpaka 318 walihudhuria, wakiwa ni wachache tu kati ya jumla ya idadi, na wengi wa wale waliohudhuria walitoka eneo hilo lenye kuongea Kigiriki. Hata Papa Sylvester I hakuwapo.d Baada ya mjadala mkali, kutoka kwa baraza hilo lisilowakilishwa vilivyo ikatokea Kanuni ya Imani ya Nisea yenye kupendelea mno wazo la Kiutatu. Hata hivyo ilishindwa kumaliza ubishi wa kimafundisho. Haikuonyesha wazi daraka la roho takatifu ya Mungu katika theolojia ya Kiutatu. Mjadala ulipamba moto kwa makumi mengi ya miaka, na ilihitaji mabaraza na mamlaka zaidi ya wamaliki tofauti-tofauti na kupeleka watu uhamishoni ili kufikia upatano hatimaye. Ulikuwa ushindi wa theolojia na kushindwa kwa wale walioshikilia Maandiko.—Warumi 3:3, 4.
28. (a) Baadhi ya matokeo ya fundisho la Utatu yamekuwa nini? (b) Kwa nini hakuna msingi wa Kibiblia wa kuheshimu mno Mariamu kuwa “Mama ya Mungu”?
28 Kwa kupita kwa karne nyingi, tokeo moja la fundisho la Utatu limekuwa kwamba Mungu wa kweli mmoja, Yehova amezamishwa katika tope la theolojia ya Mungu-Kristo ya Jumuiya ya Wakristo.e Kulingana na kusababu kuzuri, tokeo likawa kwamba kama ni kweli Yesu alikuwa Mungu Akiwa na Umbo Jingine, basi Mariamu, mama yake Yesu, kwa wazi alikuwa “Mama ya Mungu.” Miaka ilivyopita, hilo limeongoza kwenye kuheshimu mno Mariamu katika namna tofauti-tofauti, ingawa hakuna kabisa maandiko yanayomsema Mariamu kuwa ana daraka lolote la umaana isipokuwa kuwa mama mzazi mnyenyekevu wa Yesu.f (Luka 1:26-38, 46-56) Kwa muda wa karne nyingi fundisho la Mama ya Mungu limesitawishwa na kukaziwa sana na Kanisa Roma Katoliki, tokeo limekuwa kwamba Wakatoliki wengi huheshimu mno Mariamu kwa juhudi nyingi zaidi ya wanavyomwabudu Mungu.
Faraka za Jumuiya ya Wakristo
29. Paulo alionya juu ya kusitawi kwa kitu gani?
29 Tabia nyingine ya uasi-imani ni kwamba unaongoza kwenye mgawanyiko na mivunjiko. Mtume Paulo alikuwa ametabiri hivi: “Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.” Paulo alikuwa ametoa shauri lililo wazi kwa Wakorintho alipotoa taarifa hii: “Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja.” Ijapokuwa kitia moyo chake Paulo, uasi-imani na migawanyiko upesi ikatia mzizi.—Matendo 20:29, 30; 1 Wakorintho 1:10.
30. Ni hali gani ambayo upesi ikasitawi katika kanisa la mapema?
30 Makumi machache ya miaka baada ya kifo cha mitume, faraka zilikuwa tayari zimedhihirika miongoni mwa Wakristo. Will Durant atoa taarifa hii: “Selso [mpinzani wa Ukristo wa karne ya pili] mwenyewe alikuwa amesema kwa kukejeli kwamba Wakristo ‘walikuwa wamegawanyika kuwa vikundi vingi sana, kila mtu mmoja mmoja akitaka kuwa na chama chake mwenyewe.’ Karibu 187 [W.K.] Irenaeus aliorodhesha aina-aina ishirini za Ukristo; karibu 384 [W.K.] Epifanio alihesabu themanini.”—The Story of Civilization: Part III—Caesar and Christ.
31. Mtengano mkubwa ulisitawije katika Kanisa Katoliki?
31 Konstantino alipendelea upande wa Mashariki, wa Kigiriki, wa milki yake kwa kujenga jiji kuu jipya katika iliyo Uturuki leo. Aliliita Konstantinopo (Istanbul ya kisasa). Tokeo likawa kwamba kwa muda wa karne nyingi Kanisa Katoliki liligawanyika na kutenganishwa na lugha na mahali pia—Roma yenye kunena Kilatini katika Magharibi dhidi ya Konstantinopo katika Mashariki yenye kunena Kigiriki.
32, 33. (a) Visababishi zaidi vya migawanyiko katika Jumuiya ya Wakristo vilikuwa nini? (b) Biblia yasema nini juu ya matumizi ya mifano katika ibada?
32 Mijadala ya kugawanya juu ya sehemu za fundisho la Utatu lililokuwa lingali lasitawi iliendelea kusababisha mchafuko katika Jumuiya ya Wakristo. Baraza jingine lilifanywa katika 451 W.K. kule Chalcedon ili kufafanua tabia ya “asili” za Kristo. Ingawa Magharibi ilikubali imani iliyotolewa na baraza hilo, makanisa ya Mashariki hayakuafiki, hilo likaongoza kwenye kuundwa kwa Kanisa Koptiki katika Misri na Abisinia (Ethiopia) na makanisa ya “Kiyakobo” ya Shamu na Armenia. Umoja wa Kanisa Katoliki daima ulitishwa na migawanyiko juu ya mambo ya kitheolojia yasiyoeleweka, hasa kuhusu ufafanuzi wa fundisho la Utatu.
33 Kisababishi kingine cha mgawanyiko kilikuwa ni kuheshimiwa mno kwa mifano. Wakati wa karne ya nane, maaskofu wa Mashariki waliiasi ibada hiyo ya sanamu na kuingia katika kiitwacho kipindi cha kuangamiza mifano. Baada ya muda walirejea kwenye matumizi ya sanamu.—Kutoka 20:4-6; Isaya 44:14-18.
34. (a) Ni nini kilichoongoza kwenye ufa mkubwa katika Kanisa Katoliki? (b) Tokeo la mwisho la ufa huo lilikuwa nini?
34 Mtihani mwingine mkubwa ulikuja wakati kanisa la Mashariki lilipoongeza neno la Kilatini filioque (“na kutoka kwa Mwana”) kwenye Kanuni ya Imani ya Nisea ili kuonyesha kwamba Roho Takatifu ilitoka kwa Baba na Mwana pia. Tokeo la mwisho la mgeuzo huo wa karne ya sita lilikuwa ni ufa wakati “katika 876 sinodi [ya maaskofu] kule Konstantinopo ililaani vikali papa kwa ajili ya utendaji wake wa kisiasa na kwa sababu yeye hakusahihisha uzushi wa kifungu cha maneno cha filioque. Kitendo hicho kilikuwa sehemu ya Mashariki kukataa kabisa dai la papa la kuwa mwenye mamlaka ya ulimwenguni kote juu ya Kanisa.” (Man’s Religions) Katika mwaka 1054, mwakilishi wa papa alifukuza kwenye ushirika mzee wa Konstantinopo, ambaye naye akaweka laana juu ya papa. Hatimaye mtengano huo uliongoza kwenye kuundwa kwa Makanisa ya Orthodox ya Mashariki—Kigiriki, Kirusi, Kiromania, Kipoland, Kibulgaria, Kiserbia, na makanisa mengine yenye kujiongoza.
35. Wawaldo walikuwa nani, na imani zao zilitofautianaje na zile za Kanisa Katoliki?
35 Chama kingine kilikuwa pia kimeanza kusababisha mchafuko katika kanisa. Katika karne ya 12, Peter Waldo, kutoka Lyons, Ufaransa, “alihusisha wasomi fulani watafsiri Biblia katika langue d’oc [lugha ya kimkoa] ya Ufaransa kusini. Yeye alichunguza tafsiri hiyo kwa bidii, na akakata maneno kwamba Wakristo wapaswa kuishi kama mitume—bila mali ya kibinafsi.” (The Age of Faith, cha Will Durant) Yeye alianzisha chama cha kuhubiri kilichokuja kujulikana kuwa Wawaldo. Wao walikataa ukasisi wa Ukatoliki, hati za rehema, purgatori, kugeuka kwa mkate na divai kuwa mnofu na damu ya Yesu halisi, na mazoea na imani nyingine za kimapokeo za Ukatoliki. Walisambaa katika nchi nyingine. Baraza la Toulouse lilijaribu kuwazuia katika 1229 kwa kupiga marufuku kuwa na vitabu vya Kimaandiko. Vitabu vya liturjia tu ndivyo vilivyoruhusiwa na tena katika lugha ya Kilatini iliyokuwa imeachwa kunenwa. Lakini mgawanyiko zaidi wa kidini na mnyanyaso vilikuwa njiani.
Mnyanyaso wa Waalbigense
36, 37. (a) Waalbigense walikuwa nani, nao waliamini nini? (b) Waalbigense waligandamizwaje?
36 Bado chama kingine kilianzishwa katika karne ya 12 katika kusini mwa Ufaransa—Waalbigense (wanaoitwa pia Kathari), waliopewa jina kufuatia mji wa Albi, ambako walikuwa na wafuasi wengi. Walikuwa na jamii yao wenyewe ya makasisi wasiofunga ndoa, ambao walitazamia wasalimiwe kwa heshima sana. Wao waliamini kwamba Yesu alinena kitamathali wakati wa kijio chake cha mwisho aliposema kuhusu mkate, “Huu ni mwili wangu.” (Mathayo 26:26, NAB) Wao walikataa mafundisho ya Utatu, Uzawa wa Bikira, helo yenye moto, na purgatori (toharani). Ndivyo kwa matendo walivyotilia shaka mafundisho ya Roma. Papa Innocent III aliagiza kwamba Waalbigense wanyanyaswe. “Ikiwa lazima,” akasema, “wagandamizeni kwa upanga.”
37 Krusedi ilifanywa juu ya “wazushi” hao, na wafanya krusedi Wakatoliki wakachinja-chinja wanaume, wanawake, na watoto 20,000 katika Béziers, Ufaransa. Baada ya umwagaji mwingi wa damu, ikaja amani katika 1229, Waalbigense waliposhindwa. Baraza la Narbonne “lilikataza mtu wa kawaida kuwa na sehemu yoyote ya Biblia.” Kiini cha tatizo la Kanisa Katoliki kwa wazi kilikuwa ni kuwapo kwa Biblia katika lugha ya watu.
38. Mahakama ya Kuhukumia Wazushi wa Kidini ilikuwa nini, nayo ilitendaje kazi?
38 Hatua iliyofuata kuchukuliwa na kanisa ilikuwa ni kusimamisha Mahakama ya Kuhukumia Wazushi wa Kidini, mahakama iliyoundwa ili kugandamiza uzushi. Tayari watu walikuwa na roho ya kutovumiliana, wakiwa washirikina na wenye nia kubwa ya kushambulia bila sababu na kuua “wazushi.” Hali katika karne ya 13 zilifaa ili zitumiwe vibaya na mamlaka ya kanisa. Hata hivyo, “wazushi waliolaaniwa vikali na Kanisa wangekabidhiwa ‘mkono wa nchi’—mamlaka za mahali—na kuteketezwa mpaka kifo.” (The Age of Faith) Kwa kuachia mamlaka za nchi unyongaji wenyewe, kanisa lingeonekana halina hatia ya damu. Mahakama ya Kuhukumia Wazushi wa Kidini ilianzisha muhula wa mnyanyaso wa kidini uliotokeza matusi, mashutumu bandia na yasiyojulikana, mauaji yaliyopangwa, unyang’anyi, kuteswa-teswa, na kifo cha polepole cha maelfu waliothubutu kuamini tofauti na kanisa. Uhuru wa dini wa kusema ulizuiwa. Je! kulikuwako tumaini lolote kwa watu waliokuwa wakijitahidi kutafuta Mungu wa kweli? Sura ya 13 itajibu hilo.
39. Ni chama gani cha kidini kilichoanza katika karne ya sita, na jinsi gani?
39 Yote hayo yalipokuwa yakitukia katika Jumuiya ya Wakristo, Mwarabu mmoja katika Mashariki ya Kati alichukua msimamo wa kupinga ubaridi wa dini na ibada ya sanamu ya watu wake mwenyewe. Yeye alianzisha chama cha kidini katika karne ya saba ambacho leo chavuta utii na unyenyekeo wa watu karibu milioni elfu moja. Chama hicho ni Uislamu. Sura yetu ifuatayo itazungumza juu ya historia ya nabii-mwanzilishi wacho kisha kufafanua baadhi ya mafundisho yake na chanzo chayo.
[Maelezo ya Chini]
a Semi “nafsi isiyoweza kufa,” “moto wa helo,” “purgatori,” na “Limbo” hazipatikani popote ndani ya Biblia ya awali ya Kiebrania na Kigiriki. Kinyume cha hayo, neno la Kigiriki kwa “ufufuo” (a·naʹsta·sis) hutokea mara 42.
b Neno la Kigiriki e·piʹsko·pos kwa uhalisi humaanisha ‘mmoja anayetazama juu ya.’ Katika Kilatini likawa episcopus, na katika Kiingereza cha Kale likageuzwa kuwa “biscop” na baadaye, katika Kiingereza cha Enzi ya Katikati, kuwa “bishop.”
c Hekaya fulani yenye kupendwa na wengi husema kwamba Konstantino aliona njozi ya msalaba wenye maneno ya Kilatini “In hoc signo vinces” (Katika ishara hii shinda). Wanahistoria fulani husema yaelekea zaidi ilikuwa katika Kigiriki, ‘En toutoi nika” (Katika huu shinda). Hekaya hii inatiliwa shaka na wasomi fulani kwa sababu haipatani na wakati.
d The Oxford Dictionary of Popes chatoa taarifa hii kuhusu Sylvester I: “Ijapokuwa alikuwa papa kwa karibu miaka ishirini na miwili ya utawala wa Konstantino Mkuu (306-37), uliokuwa muhula wa matukio makubwa ya kanisa, yaelekea yeye alitimiza sehemu ndogo katika matukio makubwa yaliyokuwa yakitendeka. . . . Hakika kulikuwako maaskofu ambao Konstantino alifanya kuwa wasiri wake, na ambao alielekezea sera zake za kikanisa; lakini [Sylvester] hakuwa mmoja wao.”
e Ili kupata mazungumzo ya kirefu ya mjadala wa Utatu, ona broshua yenye kurasa 32 Je! Uamini Utatu? iliyotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1990.
f Mariamu, mama ya Yesu, anatajwa kwa jina au kuwa mama yake katika maandiko 24 tofauti-tofauti katika zile Gospeli nne na mara moja katika Matendo. Yeye hatajwi katika barua yoyote ya kimitume.
[Sanduku katika ukurasa wa 262]
Wakristo wa Mapema na Roma ya Kipagani
“Chama cha Kikristo kilipojitokeza ndani ya Milki ya Kiroma, kiliwataka waongofu wapagani, pia, wabadili mitazamo na tabia zao. Wapagani wengi ambao walikuwa wamelelewa kuona ndoa kwa lazima kuwa mpango wa kijamii na kiuchumi, ngono za watu wa jinsia moja kuwa kitu cha kutazamiwa cha elimu ya kiume, umalaya, wa kiume na kike, kuwa ni kawaida na halali, na talaka, kutoa mimba, kuzuia mimba, na kuponza [kwenye kifo] watoto wachanga wasiotakwa kuwa mambo yenye manufaa halisi, waliuitikia, kwa mshangao wa familia zao, ujumbe wa Kikristo, ambao ulipinga mazoea hayo.”—Adam, Eve, and the Serpent, cha Elaine Pagels.
[Sanduku katika ukurasa wa 266]
Ukristo Dhidi ya Jumuiya ya Wakristo
Porfiri, mwanafalsafa wa karne ya tatu kutoka Tiro na mpinga Ukristo, alitokeza swali juu ya “kama wafuasi wa Yesu, badala ya Yesu mwenyewe, ndio waliokuwa na daraka la namna yenye kutofautisha dini ya Kikristo. Porfiri (na Julian [maliki wa Kiroma wa karne ya nne na mpinga Ukristo]) alionyesha, kwa msingi wa Agano Jipya, kwamba Yesu hakujiita mwenyewe Mungu na kwamba yeye alihubiri, si juu yake mwenyewe, bali juu ya yule Mungu mmoja, aliye Mungu wa wote. Wafuasi wake ndio walioacha fundisho lake na kuanzisha njia mpya yao wenyewe ambayo katika hiyo Yesu (wala si yule Mungu mmoja) ndiye aliyekuwa kitu cha kupewa ibada na uchaji. . . . [Porfiri] alielekeza kwenye suala lenye kusumbua Wakristo wanaofikiri: je! imani ya Kikristo yategemea kuhubiri kwa Yesu au juu ya mawazo yaliyobuniwa na wanafunzi wake katika vizazi vingi baada ya kifo chake?”—The Christians as the Romans Saw Them.
[Sanduku katika ukurasa wa 268]
Petro na Upapa
Kwenye Mathayo 16:18, Yesu alimwambia mtume Petro hivi: “Na mimi nakuambia wewe, wewe ndiwe Petro [Kigiriki, Pe’tros], na juu ya mwamba huu [Kigiriki, peʹtra] mimi nitajenga kanisa langu, na nguvu za kifo hazitafua dafu dhidi yalo.” (RS) Kwa kutegemea hilo, Kanisa Katoliki hudai kwamba Yesu alijenga kanisa lake juu ya Petro, ambaye, wao husema, ndiye aliyekuwa wa kwanza wa mstari wa maaskofu wa Roma, na waandamizi wa Petro.
Mwamba ambao Yesu alidokeza kwenye Mathayo 16:18 ulikuwa nani, Petro au Yesu? Muktadha waonyesha kwamba kichwa cha mazungumzo kilikuwa ni utambulisho wa Yesu kuwa “Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” kama alivyokiri Petro mwenyewe. (Mathayo 16:16, RS) Kwa hiyo, ni kufikiri kuzuri kwamba Yesu mwenyewe angekuwa ndiye mwamba huo imara ulio msingi wa kanisa, wala si Petro, ambaye baadaye angemkana Kristo mara tatu.—Mathayo 26:33-35, 69-75.
Twajuaje kwamba Kristo ndiye jiwe la msingi? Kwa ushuhuda wa Petro mwenyewe, alipoandika: “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima . . . Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko, Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, na kila amwaminiye hatatahayarika.” Paulo pia alieleza hivi: “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.”—1 Petro 2:4-8; Waefeso 2:20.
Hakuna uthibitisho wowote katika Maandiko wala historia ya kwamba Petro alionwa kuwa na daraja la kwanza miongoni mwa wenziye. Yeye hataji hilo katika barua zake mwenyewe, na zile Gospeli tatu nyingine—kutia ile ya Marko (ambayo yaelekea Petro alimsimulia Marko)—hazitaji hata taarifa ya Yesu kwa Petro.—Luka 22:24-26; Matendo 15:6-22; Wagalatia 2:11-14.
Hakuna hata uthibitisho wowote kamili kwamba Petro alipata kuwa katika Roma. (1 Petro 5:13) Wakati Paulo alipozuru Yerusalemu, “Yakobo, na Kefa [Petro], na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo,” walimwunga mkono. Kwa hiyo wakati huo Petro alikuwa mmoja wa angalau nguzo tatu katika kundi. Yeye hakuwa “papa,” wala hakujulikana hivyo au kuwa “askofu” mkubwa katika Yerusalemu.—Wagalatia 2:7-9; Matendo 28:16, 30, 31.
[Picha katika ukurasa wa 264]
Umbo la Pembetatu la Fumbo la Utatu la Jumuiya ya Wakristo
[Picha katika ukurasa wa 269]
Vatican (bendera yaonyeshwa chini) hupeleka wajumbe wa kibalozi kwenye serikali za ulimwengu
[Picha katika ukurasa wa 275]
Baraza la Nisea liliweka msingi wa lile ambalo baadaye lingekuwa fundisho la Utatu
[Picha katika ukurasa wa 277]
Kumheshimu mno Mariamu akiwa na mtoto, katikati, hurudisha kwenye ibada ya kale zaidi ya vijimungu-vike vipagani—kushoto, Isisi na Horasi vya Misri; kulia, Mater Matuta cha Roma
[Picha katika ukurasa wa 278]
Makanisa ya Orthodox ya Mashariki—Sveti Nikolaj, Sofia, Bulgaria, na, chini, la Mt. Vladimir, New Jersey, U.S.A.
[Picha katika ukurasa wa 281]
Wafanya krusedi “Wakristo” walijipanga si kukomboa tu Yerusalemu kutokana na Uislamu bali pia ili kuchinja-chinja “wazushi,” kama vile Wawaldo na Waalbigense
[Picha katika ukurasa wa 283]
Tomás de Torquemada, mtawa wa Dominika, aliongoza Mahakama ya Kuhukumia Wazushi wa Kidini yenye ukatili ya Kihispania, iliyotumia zana za mateso kufanya watu waungame makosa