SURA YA 124
Kristo Asalitiwa na Kukamatwa
MATHAYO 26:47-56 MARKO 14:43-52 LUKA 22:47-53 YOHANA 18:2-12
YUDA AMSALITI YESU KATIKA BUSTANI
PETRO AMKATA MTU SIKIO
YESU AKAMATWA
Ni usiku wa manane. Makuhani wamekubali kumlipa Yuda vipande 30 vya fedha ili amsaliti Yesu. Basi Yuda anaongoza kundi kubwa la wakuu wa makuhani na Mafarisayo kwenda kumtafuta Yesu. Wako pamoja na kikundi cha wanajeshi Waroma walio na silaha na kamanda wa jeshi.
Inaonekana Yesu alipomwambia Yuda aondoke kwenye mlo wa Pasaka, alienda moja kwa moja kwa wakuu wa makuhani. (Yohana 13:27) Waliwakusanya maofisa wao na kikundi cha wanajeshi. Huenda Yuda aliwapeleka kwanza kwenye chumba ambacho Yesu na mitume wake walisherehekea Pasaka. Lakini sasa kundi hilo limevuka Bonde la Kidroni na wanaelekea kwenye bustani. Mbali na silaha, wamebeba mienge na taa, wakiwa wameazimia kumpata Yesu.
Yuda anapoongoza kundi hilo kupanda Mlima wa Mizeituni, ana uhakika kwamba anajua mahali atakapompata Yesu. Katika juma lililotangulia, Yesu na mitume wake walipokuwa wakienda Yerusalemu na kurudi Bethania, mara kwa mara walisimama katika bustani ya Gethsemane. Lakini sasa ni usiku, na huenda Yesu amefichwa na kivuli cha mizeituni iliyo katika bustani. Basi, wanajeshi ambao huenda hawajawahi kumwona Yesu, watamtambuaje? Yuda atawapa ishara ili kuwasaidia. Anasema hivi: “Yule nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni na kuondoka naye akiwa chini ya ulinzi.”—Marko 14:44.
Yuda anaongoza kundi hilo kuingia katika bustani, kisha anamwona Yesu na mitume wake naye anamwendea moja kwa moja. Yuda anasema: “Salamu, Rabi!” Kisha anambusu kwa wororo. Yesu anamuuliza: “Mwenzangu, umekuja kufanya nini?” (Mathayo 26:49, 50) Yesu anajibu swali alilouliza kwa kusema: “Yuda, unamsaliti Mwana wa binadamu kwa busu?” (Luka 22:48) Lakini Yesu haendelei na mazungumzo hayo!
Sasa Yesu anakuja kwenye mwangaza wa zile taa na mienge na kuuliza: “Mnamtafuta nani?” Umati unamjibu: “Yesu Mnazareti.” Kwa ujasiri Yesu anasema: “Ni mimi.” (Yohana 18:4, 5) Bila kujua jambo litakalotokea, wanaume hao wanaanguka chini.
Badala ya kutumia fursa hiyo kukimbilia gizani, Yesu anawauliza tena wanamtafuta nani. Wanaposema tena, “Yesu Mnazareti,” anasema hivi kwa utulivu: “Niliwaambia ni mimi. Basi, ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni wanaume hawa waende.” Hata katika kipindi hiki kigumu, Yesu anakumbuka jambo alilosema mapema, kwamba hatampoteza hata mmoja. (Yohana 6:39; 17:12) Yesu amekuwa pamoja na mitume wake waaminifu na hajampoteza hata mmoja, isipokuwa “mwana wa maangamizi”—Yuda. (Yohana 18:7-9) Basi, sasa anaomba wafuasi wake washikamanifu waachwe waende.
Wanajeshi wanaposimama na kumkaribia Yesu, mitume wanatambua jambo linaloendelea. Wanauliza: “Bwana, tuwashambulie kwa upanga?” (Luka 22:49) Kabla Yesu hajajibu, Petro anachukua upanga mmoja kati ya panga mbili walizo nazo mitume. Anamshambulia Malko, mtumwa wa kuhani mkuu, na kulikata sikio lake la kulia.
Yesu analigusa sikio la Malko, na kuponya kidonda hicho. Kisha anafundisha somo muhimu, anamwamuru hivi Petro: “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote wanaochukua upanga wataangamia kwa upanga.” Yesu yuko tayari kukamatwa, kwa kuwa anauliza hivi: “Maandiko yanayosema lazima itendeke hivi yatatimizwaje?” (Mathayo 26:52, 54) Kisha anaongezea hivi: “Je, sipaswi kukinywa kikombe ambacho Baba amenipa?” (Yohana 18:11) Yesu anakubaliana na mapenzi ya Mungu kwake, hata kufikia hatua ya kufa.
Yesu anauliza umati hivi: “Je, mmekuja kunikamata mkiwa na mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mwizi? Siku baada ya siku nilikuwa nikiketi hekaluni nikifundisha lakini hamkunikamata. Lakini yote haya yametokea ili kutimiza mambo yaliyoandikwa na manabii.”—Mathayo 26:55, 56.
Kikosi cha wanajeshi, kamanda wa jeshi, na maofisa wa Wayahudi wanamkamata Yesu na kumfunga. Mitume wanapoona hivyo, wanakimbia. Hata hivyo, “kijana fulani”—labda ni mwanafunzi Marko—anabaki katika umati ili kumfuata Yesu. (Marko 14:51) Umati unamtambua kijana huyo, nao wanajaribu kumkamata, analazimika kuacha vazi lake la kitani na kukimbia.