Endelea Kuutafuta Ufalme na Uadilifu wa Mungu
“Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki [uadilifu, NW] yake; na hayo yote mtazidishiwa.”—MATHAYO 6:33.
1, 2. Waandishi na Mafarisayo waliyageuza kuwa nini matendo ambayo yenyewe yalikuwa mema, na Yesu aliwapa wafuasi wake onyo gani?
WAANDISHI na Mafarisayo walitafuta uadilifu kwa njia yao wenyewe, ambayo haikuwa njia ya Mungu. Isitoshe, walipofanya matendo ambayo yenyewe yalikuwa mema, waliyageuza yakawa matendo ya kiunafiki ili yaonwe na wanadamu. Walikuwa wakitumikia, si Mungu, bali majivuno yao wenyewe. Yesu alionya wanafunzi wake dhidi ya kisingizio hicho: “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.”—Mathayo 6:1.
2 Yehova huwathamini wale wawapao maskini—lakini si wale wapao kama Mafarisayo walivyofanya. Yesu alionya wanafunzi wake dhidi ya kuwaiga: “Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao [wanapata thawabu yao kwa ukamili, NW].”—Mathayo 6:2.
3. (a) Waandishi na Mafarisayo walilipwaje kwa ukamili kwa sababu ya upaji wao? (b) Msimamo wa Yesu juu ya upaji ulikuwaje tofauti?
3 Neno la Kigiriki la kusema ‘wanapata kwa ukamili’ (a·peʹkho) lilikuwa neno lililoonekana mara nyingi katika risiti (stakabadhi) za kibiashara. Utumizi walo katika Mahubiri juu ya Mlima waonyesha kwamba “wamekwisha kupata thawabu yao,” yaani, “wametia sahihi risiti ya thawabu yao: haki yao ya kupokea thawabu yao imepatikana, sawasawa kabisa kana kwamba walikuwa tayari wametoa risiti ili waipate.” (An Expository Dictionary of New Testament Words, cha W. E. Vine) Zawadi kwa maskini ziliapizwa peupe katika barabara. Katika masinagogi majina ya wapaji yalitangazwa. Wale waliotoa kiasi kikubwa waliheshimiwa kwa njia maalumu kwa kupewa viti karibu na marabi wakati wa ibada. Walitoa ili waonwe na wanadamu; walionwa na kutukuzwa na wanadamu; kwa sababu hiyo, wangeweza kuipiga risiti hiyo muhuri wa kwamba “Imelipwa Kikamili” kwa sababu ya thawabu waliyopata kwa kutoa kwao. Msimamo wa Yesu ulikuwa tofauti kama nini! Toa “kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”—Mathayo 6:3, 4; Mithali 19:17.
Sala Ambazo Hupendeza Mungu
4. Kwa nini sala za Mafarisayo zilisababisha Yesu awaite wanaume hao wanafiki?
4 Yehova huthamini sala ambazo huelekezwa kwake—lakini si kama vile Mafarisayo walivyosali. Yesu alisema hivi kwa wafuasi wake: “Msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia [pana, NW], ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.” (Mathayo 6:5) Mafarisayo walikuwa na sala nyingi za kukaririwa kila siku, kwenye nyakati hususa, hata kama walikuwa wapi. Kikanuni, walipaswa kuzitoa faraghani. Ingawa hivyo, kwa mpango wa kimakusudi waliweza kuwa ‘katika pembe za njia pana,’ wakionekana na watu wenye kupita kutoka pande nne, wakati saa ya sala ilipofika.
5. (a) Ni mazoea gani zaidi yaliyosababisha sala za Mafarisayo zipite bila kusikiwa na Mungu? (b) Ni mambo gani ambayo Yesu aliweka kwanza katika sala yake ya kiolezo, na je! watu leo huafikiana na jambo hilo?
5 Kwa kuonyesha utakatifu bandia, walikuwa “wakisingizia kuwa wema kwa kusali sala ndefu.” (Luka 20:47, HNWW) Pokeo moja la mdomo lilisema hivi: “Watu wa zamani wenye kicho walikuwa wakingoja muda wa saa moja kabla hawajaisema Tefillah [sala].” (Mishnah) Kufikia muda huo ingekuwa hakika kwamba kila mtu angeona kicho chao na kukistaajabia! Sala hizo hazikufika umbali unaozidi vichwa vyao wenyewe. Yesu alisema sala itolewe faraghani, bila mrudiorudio wa ubatili, naye aliwapa kiolezo sahili. (Mathayo 6:6-8; Yohana 14:6, 14; 1 Petro 3:12) Sala ya Yesu ya kiolezo iliyaweka kwanza mambo yaliyo ya kwanza: “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe [litakaswe, NW], ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe.” (Mathayo 6:9-13) Ni watu wachache leo wajuao jina la Mungu, sembuse kutaka litakaswe. Hivyo wao wamfanya awe mungu mkosa jina. Eti Ufalme wa Mungu uje? Wengi hufikiri upo hapa tayari, ndani yao. Huenda wakasali mapenzi yake yafanywe, lakini walio wengi hufanya mapenzi yao wenyewe.—Mithali 14:12.
6. Kwa nini Yesu aliishutumu mifungo ya Kiyahudi kuwa isiyo na maana?
6 Mfungo wakubalika kwa Yehova—lakini si kama vile Mafarisayo walivyoufanya. Kama vile Yesu alivyofanya kwa habari ya kutoa sadaka za kusaidia maskini na kusali kwa waandishi na Mafarisayo, aliupuuza pia mfungo wao kuwa usio na maana: “Mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.” (Mathayo 6:16) Mapokeo yao ya mdomo yalionyesha kwamba wakati wa mifungo Mafarisayo hawakupaswa kuoga wala kujipaka mafuta bali kujipaka majivu juu ya vichwa vyao. Wasipokuwa wakifunga, kwa ukawaida Wayahudi walijiosha na kujisugua mwili kwa mafuta.
7. (a) Wafuasi wa Yesu walipaswa kujiendeshaje wakati wa kufunga? (b) Kwa habari ya kufunga, Yehova alitaka nini katika siku ya Isaya?
7 Kuhusu kufunga, Yesu aliwaambia wafuasi wake hivi: “Jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako.” (Mathayo 6:17, 18) Katika siku ya Isaya Wayahudi wenye kurudi nyuma waliona upendezo mwingi katika kufunga kwao, wakisumbua nafsi zao, wakiinamisha vichwa, na kuketi katika nguo za magunia na katika majivu. Lakini Yehova aliwataka waweke huru wenye kuonewa, wawalishe wenye njaa, wawape nyumba wasio na makao, na wawavike walio uchi.—Isaya 58:3-7.
Weka Hazina ya Kimbingu
8. Ni nini kilichosababisha waandishi na Mafarisayo wakose kuona jinsi ya kupata kibali cha Mungu, nao walisahau kanuni gani iliyoelezwa baadaye na Paulo?
8 Katika kufuatia uadilifu, waandishi na Mafarisayo walikosa kuona jinsi ya kupata kibali cha Mungu na wakakaza fikira juu ya kuvutia sifa ya wanadamu. Walijihusisha sana katika mapokeo ya wanadamu hivi kwamba wakaliweka kando Neno la Mungu lililoandikwa. Waliweka mioyo yao juu ya cheo cha kidunia badala ya hazina ya kimbingu. Walipuuza ukweli mmoja sahili ambao Farisayo-mgeukia-Ukristo aliandika miaka kadhaa baadaye: “Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana [Yehova, NW], wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana [Yehova, NW] ujira wa urithi.”—Wakolosai 3:23, 24.
9. Ni hatari zipi zaweza kutisha kuharibu hazina ya kidunia, lakini ni nini kitakachoweka hazina ya kweli ikiwa salama?
9 Yehova apendezwa na ujitoaji wako kwake, si na hesabu ya pesa ulizo nazo katika benki. Yeye ajua kwamba moyo wako upo ilipo hazina yako. Je! kutu na nondo vyaweza kula hazina yako? Je! wevi waweza kuchimba kuta za matope na kuiiba? Au katika nyakati za ki-siku-hizi zisizo na usalama wa kiuchumi, je! infleshoni yaweza kupunguza nguvu za pesa za ununuzi au mishuko mikubwa katika soko la thamani ya pesa yaweza kuifutilia mbali? Je! ongezeko kubwa la uhalifu litasababisha hazina yako iibwe? Sivyo ikiwa imewekwa mbinguni. Sivyo ikiwa jicho lako—taa iangazayo mwili wako mzima—ni sahili, likiwa limekazwa juu ya Ufalme wa Mungu na uadilifu wake. Mali zina njia ya kutoweka. “Usijitaabishe ili kupata utajiri; acha kuzitegemea akili zako mwenyewe. Je! utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, kama tai arukaye mbinguni.” (Mithali 23:4, 5) Hivyo basi kwa nini upoteze usingizi juu ya utajiri? “Kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi.” (Mhubiri 5:12) Kumbuka onyo la Yesu: “Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.”—Mathayo 6:19-24.
Imani Ambayo Huondolea Mbali Wasiwasi
10. Kwa nini ni jambo la maana sana kutia imani yako katika Mungu badala ya katika mali za kimwili, na Yesu alitoa shauri gani?
10 Yehova ataka imani yako iwe katika yeye, si katika mali za kimwili. “Pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” (Waebrania 11:6) Yesu alisema hivi: “Uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” (Luka 12:15) Mamilioni ya pesa katika benki hayatafanya mapafu magonjwa yaendelee kufanya kazi wala moyo uliochoka upigepige. “Ndiyo maana nawaambieni,” Yesu akaendelea kusema katika Mahubiri yake juu ya Mlima: “Msiwe [acheni kuwa, NW] na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji kwa kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi?”—Mathayo 6:25, HNWW.
11. Yesu alipata wapi vingi vya vielezi vyake, na hiyo yaonyeshwaje katika yale Mahubiri juu ya Mlima?
11 Yesu alikuwa stadi wa kutumia vielezi vya maneno. Alivifikiria popote alipotazama. Aliona mwanamke akiweka taa iliyowashwa juu ya kinara cha taa na kufanya hicho kiwe kielezi. Aliona mchungaji akitenga kondoo kutoka kwenye mbuzi; hicho kikawa kielezi. Aliona watoto wakicheza sokoni; hicho kikawa kielezi. Na ndivyo ilivyokuwa katika yale Mahubiri juu ya Mlima. Alipokuwa akiongea juu ya kufanya wasiwasi wa mahitaji ya kimwili, aliona vielezi katika nyuni wenye kupitapita hapo na katika maua yaliyotandaa kama zulia katika pande za kilima hicho. Je! nyuni hupanda mbegu na kuvuna? Sivyo. Je! maua husokota na kufuma? Sivyo. Mungu ndiye aliyefanyiza vitu hivyo; ndiye huvitunza. Nyinyi, hata hivyo, ni wa bei kuliko nyuni na maua. (Mathayo 6:26, 28-30) Yeye alitoa Mwana wake kwa ajili yenu, si kwa ajili yao.—Yohana 3:16.
12. (a) Je! vielezi juu ya nyuni na maua vilimaanisha kwamba haingekuwa lazima wanafunzi wa Yesu wafanye kazi? (b) Yesu alikuwa akikazia jambo gani kuhusu kazi na imani?
12 Hapa Yesu hakuwa akiambia wafuasi wake kwamba haikuwa lazima wafanye kazi ili wajilishe na kujivika. (Ona Mhubiri 2:24; Waefeso 4:28; 2 Wathesalonike 3:10-12.) Katika asubuhi hiyo ya masika, nyuni walikuwa wenye shughuli wakichakura chini wapate chakula, wakibembelezana kirafiki, wakijenga viota, wakikalia mayai, wakilisha makinda yao. Walikuwa wakifanya kazi lakini bila wasiwasi. Pia maua yalikuwa na shughuli yakisukuma mizizi yayo ndani ya udongo kutafuta maji na madini na kuelekeza majani yayo yafikilie nuru ya jua. Ilikuwa lazima yakomae na kuchanua na kuangua mbegu kabla hayajafa. Yalikuwa yakifanya kazi lakini bila wasiwasi. Mungu huandalia nyuni na maua riziki. ‘Je! hataona ni afadhali zaidi kuwaandalia nyinyi, nyinyi wenye imani kidogo?’—Mathayo 6:30, NW.
13. (a) Kwa nini ilifaa Yesu atumie dhiraa ili kupima alipokuwa akiongea juu ya kuongezea muda wa maisha ya mtu? (b) Wewe waweza kurefushaje maisha yako kana kwamba ni kwa mamilioni ya kilometa zisizo na mwisho?
13 Kwa hiyo iweni na imani. Msiwe na wasiwasi. Wasiwasi hautabadili chochote. “Ni nani miongoni mwenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuuongeza muda wa maisha yake hata kwa siku [dhiraa, NW] moja?” (Mathayo 6:27, HNWW) Lakini kwa nini Yesu ahusianisha kipimo halisi cha umbali, dhiraa moja, na kipimo cha wakati katika muda wa maisha? Labda ni kwa sababu mara nyingi Biblia hufananisha muda wa maisha ya wanadamu na safari, ikitumia semi kama “njia ya watenda dhambi,” “kijia cha waadilifu,” ‘njia pana iendayo upotevuni,’ na ‘njia ambayo imesonga iendayo uzimani.’ (Zaburi 1:1; Mithali 4:18, NW; Mathayo 7:13, 14, UV) Wasiwasi juu ya mahitaji ya kila siku hauwezi kurefusha maisha ya mtu hata kwa kijisehemu, kama kwa ‘dhiraa moja.’ Lakini kuna njia ya kurefusha maisha yako kana kwamba ni kwa mamilioni ya kilometa zisizo na mwisho. Si kwa kuwa na wasiwasi na kusema “Tule nini?” au “Tunywe nini?” au “Tuvae nini?” bali kwa kuwa na imani na kufanya Yesu atuambialo tufanye: “Bali utafuteni [endeleeni kutafuta, NW] kwanza ufalme wake, na haki yake [uadilifu wake, NW]; na hayo yote mtazidishiwa.”—Mathayo 6:31-33.
Kuufikia Ufalme wa Mungu
na Uadilifu Wake
14. (a) Ni nini kichwa cha yale Mahubiri juu ya Mlima? (b) Waandishi na Mafarisayo waliutafuta Ufalme na uadilifu kwa njia gani yenye makosa?
14 Katika sentensi yake ya ufunguzi ya Mahubiri yake juu ya Mlima, Yesu alisema Ufalme wa mbingu ni wa wale wajuao uhitaji wao wa kiroho. Katika sentensi ya nne, alisema kwamba wale wanaoona njaa na kiu ya uadilifu wangejazwa. Hapa Yesu aweka Ufalme na pia uadilifu wa Yehova mahali pa kwanza. Mambo hayo ndiyo kichwa cha yale Mahubiri juu ya Mlima. Ndiyo jibu kwa mahitaji ya ainabinadamu yote. Lakini Ufalme wa Mungu na uadilifu wa Mungu hufikiwaje? Sisi twaendeleaje kuyatafuta? Si jinsi waandishi na Mafarisayo walivyofanya. Wao waliutafuta Ufalme na uadilifu kwa njia ya Sheria ya Kimusa, waliyodai ilihusisha mapokeo ya mdomo, kwa kuwa waliamini kwamba Musa alipewa na Mungu Sheria iliyoandikwa na pia mapokeo ya mdomo kwenye Mlima Sinai.
15. (a) Kulingana na Wayahudi, mapokeo yao ya mdomo yalianza lini, nao waliyainuaje juu ya Sheria ya Kimusa iliyoandikwa? (b) Mapokeo haya yalianza lini hasa, na yakiwa na tokeo gani juu ya Sheria ya Kimusa?
15 Pokeo lao kuhusu hilo ilisema hivi: “Musa aliipokea Sheria [kielezi-chini, “‘Ile Sheria ya Mdomo’”] kutoka Sinai na kuikabidhi kwa Yoshua, naye Yoshua kwa wazee, nao wazee kwa Manabii; nao Manabii wakaikabidhi kwa wanaume wa lile Sinagogi Kubwa.” Baada ya muda sheria yao ya mdomo ilikwezwa juu hata kuliko Sheria iliyoandikwa: “[Ikiwa] yeye akiuka maneno ya Sheria [iliyoandikwa], hana hatia,” lakini ikiwa “yeye aongezea maneno ya Waandishi [ma-pokeo ya mdomo], ana hatia.” (Mishnah) Mapokeo yao ya mdomo hayakuanzia Sinai. Kwa uhakika, yalianza kurundikana upesi-upesi karne mbili hivi kabla ya Kristo. Wao waliiongezea, wakaipunguza, na kuibatilisha Sheria ya Kimusa iliyoandikwa.—Linganisha Kumbukumbu 4:2; 12:32.
16. Uadilifu wa Mungu waja jinsi gani kwa ajili ya ainabinadamu?
16 Uadilifu wa Mungu waja si kupitia ile Sheria bali bila hiyo: “Hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki [mwadilifu, NW] mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki [uadilifu, NW] ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki [uadilifu, NW] ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo.” (Warumi 3:20-22) Hivyo basi uadilifu wa Mungu waja kwa kuwa na imani katika Kristo Yesu—kwa wingi jambo hilo ‘lilishuhudiwa na torati na manabii.’ Unabii mbalimbali wa Kimesiya ulitimizwa katika Yesu. Yeye aliitimiza Sheria pia; iliondolewa njiani kwa kupigiliwa misumari kwenye mti wake wa mateso.—Luka 24:25-27, 44-46; Wakolosai 2:13, 14; Waebrania 10:1.
17. Kulingana na mtume Paulo, Wayahudi walikosaje kuujua uadilifu wa Mungu?
17 Kwa sababu hiyo, mtume Paulo aliandika juu ya kushindwa kwa Wayahudi kutafuta uadilifu: “Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa. Kwa maana, wakiwa hawaijui haki [uadilifu, NW] ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki [uadilifu, NW] yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki [uadilifu, NW].” (Warumi 10:2-4) Pia Paulo aliandika hivi juu ya Kristo Yesu: “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki [uadilifu, NW] ya Mungu katika Yeye.”—2 Wakorintho 5:21.
18. ‘Kristo aliyetundikwa’ alionwaje na wanamapokeo Wayahudi, wanafalsafa Wagiriki, na “kwao waitwao”?
18 Wayahudi walimwona Mesiya mwenye kufa kuwa goigoi asiyejiweza. Wanafalsafa Wagiriki walidhihaki Mesiya wa jinsi hiyo kuwa upumbavu. Hata hivyo, ni kama vile Paulo alivyopiga mbiu: “Kwa maana wote Wayahudi waziomba ishara na Wagiriki watafuta hekima; lakini sisi twamhubiri Kristo mtundikwa, kwa Wayahudi ni kisababishi cha kujikwaa lakini kwa mataifa ni upumbavu; hata hivyo, kwa wale ambao ni walioitwa, wote Wayahudi na Wagiriki, ni Kristo nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Kwa sababu kitu kipumbavu cha Mungu ni chenye hekima kuliko wanadamu, na kitu dhaifu cha Mungu ni imara kuliko wanadamu.” (1 Wakorintho 1:22-25, NW) Kristo Yesu ni udhihirisho wa nguvu na hekima ya Mungu na ni njia ya Mungu ya uadilifu na uhai wa milele kwa ainabinadamu iliyo tiifu. “Hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”—Matendo 4:12.
19. Makala inayofuata itaonyesha nini?
19 Makala inayofuata itaonyesha kwamba ili tuokoke uharibifu na kupata uhai wa milele, ni lazima tuendelee kuutafuta Ufalme wa Mungu na uadilifu wake. Ni lazima hilo lifanywe si kwa kusikiliza tu semi za Yesu bali pia kwa kuzifanya.
Maswali ya Kupitia
◻ Wanadini Wayahudi walizigeuza kuwa nini zawadi zao za rehema,
sala, na mifungo?
◻ Ni mahali gani salama pa kuiweka akiba hazina yako?
◻ Kwa nini twapaswa kuepuka kufanya wasiwasi juu ya mahitaji
yetu ya vitu vya kimwili?
◻ Ni dai gani bandia ambalo Wayahudi walifanya juu ya mwanzo wa
mapokeo yao ya mdomo?
◻ Ufalme wa Mungu na uadilifu wake vyaja kwa njia gani?
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mafarisayo walipenda kusali kwa kusimama katika pembe za barabara, ambapo wangeweza kuonwa na wanadamu