Kitabu Cha Biblia 41—Marko
Mwandikaji: Marko
Mahali Kilipoandikiwa: Rumi
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 60–65 W.K.
Wakati Uliohusishwa: 29–33 W.K.
1. Ni nini kinachojulikana juu ya Marko na familia yake?
YESU alipokamatwa kule Gethsemane na mitume wakatoroka, “kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili mwake nguo ya kitani [juu ya mwili wake ulio uchi].” Wakati umati ulipojaribu kumkamata pia, ‘aliiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi.’ Kwa ujumla mwanamume huyo kijana huaminiwa kuwa Marko. Yeye aelezwa katika Matendo kuwa “Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko” na yaweza kuwa alikuwa ametoka katika familia yenye hali ya starehe katika Yerusalemu, kwa maana walikuwa na nyumba yao wenyewe na watumishi. Mama yake, Mariamu, alikuwa Mkristo pia, na kundi la mapema lilitumia nyumba yake kuwa mahali pa kukutania. Katika pindi moja alipokombolewa na malaika kutoka gerezani, Petro alienda kwenye nyumba hii na kukuta akina ndugu wamekusanyika humo.—Mk. 14:51, 52; Mdo. 12:12, 13.
2, 3. (a) Bila shaka ni nini kilichochea Marko aingie utumishi wa misionari? (b) Ni ushirika gani aliokuwa nao pamoja na wamisionari wengine, hasa pamoja na Petro na Paulo?
2 Misionari Barnaba, Mlawi kutoka Saiprasi, alikuwa binamu ya Marko. (Mdo. 4:36; Kol. 4:10) Wakati Barnaba alipokuja na Paulo Yerusalemu kuhusiana na msaada wa njaa, Marko pia alipata kumjua Paulo. Mashirika hayo katika kundi na pamoja na wahudumu wenye kutembelea wenye bidii bila shaka yalitia ndani ya Marko tamaa ya kuingia utumishi wa misionari. Kwa hiyo twaona akiwa mwandamani na mhudumu wa Paulo na Barnaba kwenye safari yao ya kwanza ya misionari. Hata hivyo, kwa sababu fulani Marko aliwaacha katika Perga, Pamfilia, na kurejea Yerusalemu. (Mdo. 11:29, 30; 12:25; 13:5, 13) Kwa sababu ya hilo, Paulo alikataa kuambatana na Marko kwenye safari ya pili ya misionari, na hilo likatokeza mwachano kati ya Paulo na Barnaba. Paulo alichukua Sila, naye Barnaba akachukua binamu yake Marko na kuabiri (kusafiri) naye kwenda Saiprasi (Kipro).—Mdo. 15:36-41.
3 Marko alijithibitisha katika huduma na akawa msaada wenye thamani si kwa Barnaba tu bali pia baadaye kwa mitume Petro na Paulo. Marko alikuwa na Paulo (karibu 60-61 W.K.) wakati wa kufungwa kwake gerezani kwa kwanza katika Rumi. (Fil. 1, 24) Kisha twaona Marko na Petro katika Babuloni kati ya miaka 62 na 64 W.K. (1 Pet. 5:13) Paulo ni mtumwa tena katika Rumi yawezekana katika mwaka 65 W.K., na katika barua moja amwuliza Timotheo aandamane na Marko, akisema, “maana anifaa kwa utumishi.” (2 Tim. 1:8; 4:11) Huo ndio mtajo wa karibuni zaidi wa Marko katika maandishi ya Biblia.
4-6. Marko aliwezaje kupata habari za kindani kwa ajili ya Gospeli yake? (b) Ni nini kinachoonyesha ushirika wake wa karibu pamoja na Petro? (c) Toa vielelezo vya sifa za Petro katika Gospeli hii.
4 Mtungo wa hii iliyo fupi zaidi kati ya Gospeli (Injili) wahesabiwa kuwa wa Marko. Yeye alikuwa mfanya kazi mwenzi wa mitume wa Yesu na mmoja ambaye alitia maisha yake katika utumishi wa habari njema. Lakini Marko hakuwa mmoja wa mitume 12, naye hakuwa mwandamani wa karibu wa Yesu. Yeye alipata wapi habari za kindani zinazofanya simulizi lake la huduma ya Yesu liwe hai kweli kweli tangu mwanzo mpaka mwisho? Kwa kulingana na mapokeo ya mapema zaidi ya Papias, Origen, na Tertullian, chanzo hicho kilikuwa ni Petro, ambaye Marko alishirikiana naye kwa ukaribu.a Je! Petro hakumwita “Marko mwanangu”? (1 Pet. 5:13) Petro alikuwa shahidi aliyejionea karibu yote ambayo Marko aliandika, kwa hiyo angaliweza kujifunza kutoka kwa Petro mambo mengi ya usimulizi usiopatikana katika Gospeli nyinginezo. Kwa kielelezo, Marko anena juu ya “watu wa mshahara” waliomfanyia kazi Zebedayo, yule mkoma mwenye kumsihi Yesu akiwa ‘amepiga magoti,’ yule mwanamume aliyepagawa na roho waovu mwenye “kujikata-kata kwa mawe,” na kutoa kwa Yesu unabii juu ya ‘kuja kwa Mwana wa Adamu kwa nguvu nyingi na utukufu’ alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni “kuelekea hekalu.”—Mk. 1:20, 40; 5:5; 13:3, 26.
5 Petro mwenyewe alikuwa jamaa mwenye hisia nyingi za moyoni na kwa hiyo angeweza kuthamini na kumweleza Marko kwa zile hisia na maono ya moyoni ya Yesu. Ndiyo sababu Marko mara nyingi aandika jinsi Yesu alivyohisi na kuwa na itikio-tendo; kwa kielelezo, kwamba alitazama “pande zote kwa hasira, akiona huzuni,” kwamba “akaugua,” na kwamba “akaugua rohoni.” (3:5; 7:34; 8:12) Marko ndiye atuambia juu ya hisia za Yesu kuelekea yule mtawala kijana tajiri, akisema kwamba “akampenda.” (10:21) Na jinsi tunavyopata uchangamshi katika simulizi la kwamba Yesu hakusimamisha tu mtoto mchanga katikati ya wanafunzi wake bali pia “akamkumbatia,” na katika pindi nyingine “akawakumbatia” watoto.—9:36; 10:13-16.
6 Baadhi ya sifa za Petro zaonekana katika mtindo wa kuandika wa Marko, ambao ni wa haraka-haraka, ulio hai, wenye nguvu, wa muhimu, na wenye kueleza wazi. Yaonekana ana haraka kubwa ya kusimulia matukio. Kwa kielelezo, neno “mara” latokea tena na tena, likiendeleza hadithi hiyo kwa mtindo wenye msisimuo.
7. Ni nini kinachotofautisha Gospeli ya Marko na ile ya Mathayo?
7 Ijapokuwa Marko angeweza kupata Gospeli ya Mathayo na maandishi yake yana asilimia 7 tu ya mambo ambayo hayamo katika Gospeli zile nyingine, lingekuwa kosa kuamini kwamba Marko alifupiza tu Gospeli ya Mathayo na kuongeza habari chache za kindani. Ingawa Mathayo alikuwa ameonyesha Yesu kuwa Mesiya na Mfalme aliyeahidiwa, Marko sasa afikiria uhai wake na kuendelea kutoka upande mwingine. Yeye aonyesha Yesu kuwa Mwana wa Mungu mwenye kufanya miujiza, Mwokozi mwenye kushinda. Marko akazia utendaji wa Kristo badala ya mahubiri na mafundisho yake. Ni kisehemu kidogo tu cha mifano na moja ya hotuba ndefu zaidi za Yesu inayoripotiwa, na Mahubiri ya Mlimani hayakutiwa ndani. Ndiyo sababu hiyo Gospeli ya Marko ni fupi zaidi, ingawa ni yenye msisimuo wa matendo sawa na zile nyingine. Angalau miujiza 19 yarejezewa kikamili.
8. Ni mambo gani yanayoonyesha Gospeli ya Marko kwa wazi iliandikiwa Warumi?
8 Ingawa Mathayo aliandika Gospeli yake kwa ajili ya Wayahudi, Marko kwa wazi aliandika hasa kwa ajili ya Warumi. Twajuaje hilo? Sheria ya Musa yatajwa wakati tu wa kuripoti mazungumzo yaliyoirejezea, na nasaba ya Yesu haikutiwa ndani. Gospeli ya Kristo yawakilishwa kuwa ni ya umaana wa ulimwengu wote. Yeye atoa maelezo yenye kufafanua desturi na mafundisho ya Kiyahudi ambayo wasomaji wasio Wayahudi huenda wasiyafahamu. (2:18; 7:3, 4; 14:12; 15:42) Semi za Kiaramu zimetafsiriwa. (3:17; 5:41; 7:11, 34; 14:36; 15:22, 34) Afafanua majina ya kijiografia ya Kipalestina na uhai wa mimea kwa maelezo. (1:5, 13; 11:13; 13:3) Thamani ya sarafu za Kiyahudi yatolewa katika pesa za Kirumi. (12:42, NW, kielezi-chini) Atumia maneno zaidi ya Kilatini kuliko wale waandikaji wengine wa Gospeli, vielelezo vikiwa ni speculator (mlinda mwili), praetorium (ikulu ya gavana), na centurio (ofisa wa jeshi).—6:27; 15:16, 39.
9. Kitabu cha Marko kiliandikiwa wapi na wakati gani, na nini kinachothibitisha uasilia wacho?
9 Kwa kuwa kwa wazi Marko aliandika hasa kwa ajili ya Warumi, yaelekea sana aliandika akiwa Rumi. Mapokeo ya mapema zaidi na yaliyomo katika kitabu hicho yaruhusu kukata shauri kwamba kilitungwa katika Rumi wakati wa ama kufungwa gerezani kwa kwanza au kwa pili kwa mtume Paulo, na kwa hiyo wakati wa miaka 60-65 W.K. Katika miaka hiyo Marko alikuwa katika Rumi angalau mara moja, na yaelekea mara mbili. Wajuzi wote wakubwa wa karne za pili na tatu wathibitisha kwamba Marko alikuwa ndiye mwandikaji. Gospeli hiyo tayari ilikuwa inazunguka miongoni mwa Wakristo kufikia katikati ya karne ya pili. Kuonekana kwayo katika orodha zote za mapema za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo kwathibitisha uasilia wa Gospeli ya Marko.
10. Umalizio mrefu na mfupi wa Marko wapasa kuonwaje, na kwa nini?
10 Hata hivyo, umalizio mrefu na mfupi ambao nyakati nyingine huongezwa baada ya sura ya 16, mstari wa 8, haupaswi kuonwa kuwa asilia. Hauonekani katika hati zilizo nyingi za kale, kama vile Sinaitic na Vatican No. 1209. Wanachuo wa karne ya nne Eusebio na Jerome wakubliana kwamba maandishi asilia yamalizika kwa neno “waliogopa.” Umalizio ule mwingine yawezekana uliongezwa kwa kusudi la kunyoosha ughafula ambao kwao Gospeli hiyo yamalizika.
11. (a) Ni nini kinachotoa uthibitisho kuwa Gospeli ya Marko ni sahihi, na ni mamlaka gani inayokaziwa? (b) Ni kwa nini hii ni ‘habari njema,’ na Gospeli ya Marko yahusisha kipindi gani?
11 Kwamba simulizi la Marko ni sahihi yaonyeshwa na upatano kamili wa Gospeli yake si na Gospeli zile nyingine tu bali pia na Maandiko Matakatifu yote tangu Mwanzo mpaka Ufunuo. Zaidi ya hayo, Yesu aonyeshwa tena na tena kuwa ndiye mwenye mamlaka si katika neno lake la kinywa tu bali pia juu ya nguvu za asili, juu ya Shetani na roho waovu, juu ya ugonjwa na maradhi, ndiyo, juu ya kifo chenyewe. Kwa hiyo Marko afungua usimulizi wake kwa utangulizi wenye kutazamisha: “Mwanzo wa Injili [habari njema, NW] ya Yesu Kristo.” Kuja kwake na huduma yake vilimaanisha ‘habari njema,’ na kwa hiyo funzo la Gospeli ya Marko lazima liwe lenye mafaa kwa wasomaji wote. Matukio yanayoelezwa na Marko yahusisha kipindi cha tangu masika ya 29 W.K. mpaka masika ya 33 W.K.
YALIYOMO KATIKA MARKO
12. Ni nini kimeshindiliwa katika mistari 13 ya kwanza ya Marko?
12 Ubatizo na kushawishwa kwa Yesu (1:1-13). Marko aanza habari njema kwa kutambulisha Yohana Mbatizaji. Yeye ndiye mjumbe aliyetabiriwa, aliyepelekwa atangaze hivi: “Itengenezeni njia ya Bwana [Yehova, NW], Yanyosheni mapito yake.” Juu ya yule ambaye angekuja karibuni, mbatizaji huyo alisema, ‘Ana nguvu kuliko mimi.’ Ndiyo, yeye atabatiza, si kwa maji, bali kwa roho takatifu. Yesu sasa aja kutoka Nazareti ya Galilaya, na Yohana ambatiza. Roho yashuka juu ya Yesu kama hua, na sauti yasikiwa kutoka mbinguni: “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” (1:3, 7, 11) Yesu ashawishwa na Shetani katika nyika, na malaika wamhudumia. Matukio hayo yote makubwa yameshindiliwa katika mistari 13 ya kwanza ya Marko.
13. Ni katika njia gani Yesu adhihirisha mapema mamlaka yake kuwa “Mtakatifu wa Mungu”?
13 Yesu aanza huduma katika Galilaya (1:14–6:6). Baada ya Yohana kukamatwa, Yesu aenda akihubiri habari njema ya Mungu katika Galilaya. Jinsi alivyo na ujumbe wenye kusisimua! “Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili [habari njema, NW].” (1:15) Aita Simoni na Andrea na Yakobo na Yohana kuacha nyavu zao za kuvua wawe wanafunzi wake. Siku ya Sabato aanza kufundisha katika sinagogi kule Kapernaumu. Watu wastaajabu, kwa maana afundisha “kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.” Yeye adhihirisha mamlaka yake kuwa “Mtakatifu wa Mungu” kwa kufukuza roho mchafu kutoka kwa mtu aliyepagawa na kwa kuponya mama-mkwe wa Simoni, ambaye alikuwa mgonjwa homa. Habari hizo zaenea kama moto wa pori, na kufikia usiku “mji wote” umekusanyika nje ya nyumba ya Simoni. Yesu aponya wengi walio wagonjwa na kufukuza roho waovu wengi.—1:22, 24, 33.
14. Yesu athibitishaje mamlaka yake ya kusamehe dhambi?
14 Yesu ajulisha rasmi utume wake: “Nipate kuhubiri.” (1:38) Katika Galilaya yote ahubiri. Kokote aendako, afukuza roho waovu na kuponya wagonjwa, kutia na mkoma na mtu aliyepooza ambaye asema kwake hivi: “Umesamehewa dhambi zako.” Baadhi ya waandishi wawaza mioyoni mwao, ‘Makufuru hayo. Nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu?’ Akifahamu mawazo yao, Yesu atoa uthibitisho kwamba “Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi” kwa kumwambia mtu huyo aliyepooza ainuke na kwenda nyumbani. Watu wamtukuza Mungu. Mtoza ushuru Lawi (Mathayo) awapo mfuasi wake, Yesu awaambia waandishi hivi: “Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.” Ajionyesha kuwa “Bwana wa sabato pia.”—2:5, 7, 10, 17, 28.
15. Yesu ajulisha rasmi nini juu ya wale wanaokanusha miujiza yake, naye asema nini juu ya vifungo vya familia?
15 Sasa Yesu afanyiza kikundi cha mitume 12. Watu wake wa ukoo watokeza upinzani fulani, na kisha waandishi fulani kutoka Yerusalemu wamshtaki kwa kufukuza roho waovu kupitia mtawala wa roho waovu. Yesu awauliza, “Awezaje Shetani kumtoa Shetani?” na awaonya hivi: ‘Mtu atakayekufuru roho takatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele.’ Wakati wa mazungumzo yake, mama na ndugu zake waja wakimtafuta, na Yesu asukumwa ajulishe rasmi hivi: “Ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.”—3:23, 29, 35.
16. kwa vielezi, Yesu afundisha nini juu ya “ufalme wa Mungu”?
16 Yesu aanza kufundisha “siri [takatifu, NW] ya ufalme wa Mungu” kwa vielezi. Anena juu ya mtu anayepanda mbegu inayoanguka juu ya aina mbalimbali za udongo (kutoa kielezi cha aina tofauti za wasikiaji wa lile neno) na kuhusu taa inayong’aa kutoka kwenye kinara cha taa chayo. Katika kielezi kingine, Yesu anena kwamba Ufalme wa Mungu ni kama wakati mwanamume anapotupa mbegu juu ya ardhi: “Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke.” (4:11, 28) Pia atoa kielezi cha punje ya haradali, ambayo, ingawa ndiyo mbegu ndogo zaidi, hukua ikawa kubwa yenye matawi makubwa ya kinga.
17. Miujiza ya Yesu yaonyesha wazi kadiri ya mamlaka yake?
17 Wanapovuka Bahari ya Galilaya, Yesu afanya kimwujiza upepo mkali utulie, na bahari yenye mchafuko yawa shwari atoapo amri: “Nyamaza, utulie.” (4:39) Ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, Yesu afukuza “Legioni” ya roho waovu kutoka kwa mtu mmoja na awaruhusu waingie ndani ya kundi la nguruwe wapatao 2,000, ambao, nao, watimua mbio na kuanguka penye genge (mtelemko) wakafa maji ndani ya bahari. (5:8-13) Baada ya hilo, Yesu avuka ng’ambo ile nyingine ya ukingo. Mwanamke mmoja aponywa mtiririko wa damu, usioponyeka kwa miaka 12, kwa kugusa tu vazi la nje la Yesu, akiwa njiani kwenda kufufua binti wa miaka 12 wa Yairo. Kweli kweli, Mwana wa mtu ana mamlaka juu ya uhai na kifo! Hata hivyo, watu katika eneo la nyumbani la Yesu wabisha juu ya mamlaka yake. Yeye astaajabu kwa ajili ya ukosefu wao wa imani lakini aendelea ‘kuzunguka-zunguka katika vile vijiji, akifundisha.’—6:6.
18. (a) Huduma ya Yesu yapanuliwaje? (b) Ni nini kinachochochea Yesu afundishe na kufanya miujiza?
18 Huduma ya Galilaya yapanuliwa (6:7–9:50). Wale 12 watumwa 2 kwa 2 wakiwa na maagizo na mamlaka ya kuhubiri na kufundisha, kuponya watu, na kufukuza roho waovu. Jina la Yesu lajulikana sana, wengine wakifikiri ni Yohana Mbatizaji aliyeinuliwa kutoka kwa wafu. Uwezekano huo wamtia Herode wasiwasi, ambaye wakati wa karamu yake ya siku ya kuzaliwa, Yohana alikatwa kichwa. Mitume warejea kutoka safari yao ya kuhubiri na kutoa ripoti ya utendaji wao kwa Yesu. Umati mkubwa wa watu wafuata Yesu kuzunguka Galilaya, naye ‘awahurumia; kwa sababu wao ni kama kondoo wasio na mchungaji.’ Kwa hiyo yeye aanza kuwafundisha mambo mengi. (6:34) Kwa upendo awaandalia chakula cha kimwili pia, akilisha wanaume 5,000 kwa boflo tano za mkate na samaki wawili. Muda mfupi baadaye, wanafunzi wanapokuwa taabani wakipambana na tufani wakielekea Bethsaida, yeye aja akitembea juu ya bahari kuwaelekea na kutuliza upepo. Haishangazi kwamba hata wanafunzi ‘washangaa sana’!—6:51.
19, 20. (a) Yesu atoaje karipio kwa waandishi na Mafarisayo? (b) Ni hali gani zinazoongoza kwenye kukaripiwa kwa Petro?
19 Katika wilaya ya Genesareti, Yesu aingia kwenye mazungumzo na waandishi na Mafarisayo kutoka Yerusalemu juu ya kula kwa mikono isiyooshwa, naye awakemea kwa ajili ya ‘kuacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.’ Asema kinachoingia kutoka nje sicho kinachochafua mtu, bali ni kile kinachotoka ndani, ndani ya moyo, yaani, “mawazo mabaya.” (7:8, 21) Akienda kaskazini katika maeneo ya Tiro na Sidoni, yeye afanya mwujiza kwa asiye Myahudi, akifukuza roho mwovu kutoka kwa binti ya mwanamke Mtiro-mfoinike.
20 Arudipo Galilaya, Yesu aonea huruma tena umati unaomfuata na alisha wanaume 4,000 kwa boflo (mikate) saba na samaki wachache wadogo. Yeye aonya wanafunzi wake juu ya chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode, lakini wakati huo washindwa kuelewa. Kisha, mwujiza mwingine—kuponywa kwa mwanamume kipofu kule Bethsaida. Katika mazungumzo wakiwa njiani kwenda vijiji vya Kaisaria Filipi, kwa usadikisho Petro atambulisha Yesu kuwa “Kristo” lakini akataa vikali Yesu anenapo juu ya mateso na kifo cha Mwana wa Adamu kinachokaribia. Kwa ajili ya hilo, Yesu amkaripia: “Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” (8:29, 33) Yesu ahimiza wanafunzi wake wamfuate daima kwa ajili ya habari njema; wakimwonea aibu, yeye atawaonea aibu awasilipo katika utukufu wa Baba yake.
21. (a) Nani wanaoona “ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu,” na jinsi gani? (b) Yesu akaziaje kuweka Ufalme kwanza?
21 Siku sita baadaye, akiwa juu ya mlima mrefu, Petro, Yakobo, na Yohana wapendelewa kuona “ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu” waonapo Yesu akigeuzwa sura katika utukufu. (9:1) Kwa mara nyingine Yesu adhihirisha mamlaka yake kwa kufukuza roho asiye na uneni kutoka kwa mvulana mmoja, na mara ya pili anena juu ya mateso na kifo chake kinachokuja. Yeye ashauri wanafunzi wake wasiruhusu chochote kiwazuie wasiingie katika uhai. Je! mkono wako wakufanya ukwazike? Ukate! Mguu wako? Ukate! Jicho lako? Litupe! Afadhali zaidi kuingia katika Ufalme wa Mungu umelemaa kuliko kutupwa ukiwa mzima ndani ya Gehena.
22. Ni shauri gani linalokaziwa na huduma ya Yesu katika Perea?
22 Huduma katika Perea (10:1-52). Yesu aja kwenye mipaka ya Yudea na “ng’ambo ya Yordani” (ndani ya Perea). Mafarisayo sasa wamwuliza juu ya talaka, naye atumia nafasi hiyo kueleza kanuni za kimungu juu ya ndoa. Mwanamume mmoja kijana aliye tajiri amwuliza juu ya kurithi uhai wa milele lakini ahuzunika asikiapo kwamba ili kupata hazina mbinguni, ni lazima auze mali zake na kuwa mfuasi wa Yesu. Yesu awaambia wanafunzi wake hivi: “Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Yeye atia moyo wale ambao wameacha vyote kwa ajili ya habari njema, akiwaahidi “mia sasa . . . na udhia; na katika ulimwengu [mfumo wa mambo, NW] ujao uzima wa milele.”—10:1, 25, 30.
23. Ni mazungumzo na mwujiza gani uliotokea safarini ya kwenda Yerusalemu?
23 Yesu na wale 12 wafunga safari wakielekea Yerusalemu. Yesu awaambia mara ya tatu juu ya mateso yaliyo mbele yake na pia juu ya ufufuo wake. Awauliza kama waweza kunywa kikombe kile kile anachokunywa, naye awaambia hivi: “Mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.” Wakiwa safarini ya kutoka Yeriko, mwombaji kipofu aita kutoka kando ya barabara: “Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu.” Yesu afanya mwanamume huyo kipofu aone—ponyo lake la mwisho la kimwujiza kama ilivyoandikwa na Marko.—10:44, 47, 48.
24, 25. (a) Yesu alishuhudia mamlaka yake kwa vitendo gani? (b) Yeye ajibu wapinzani wake kwa hoja gani? (c) Ni onyo gani ambalo Yesu atoa kwa umati, naye apendekeza nini kwa wanafunzi wake?
24 Yesu katika Yerusalemu na ujirani walo (11:1–15:47). Simulizi hilo lasonga mbele upesi! Yesu apanda juu ya mwana-punda kuingia katika jiji hilo, na watu wamshangilia kuwa Mfalme. Siku inayofuata asafisha hekalu. Makuhani wakuu na waandishi wamhofu na kumtafutia kifo. “Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya?” wauliza. (11:28) Kwa ustadi Yesu ageuza swali hilo liwaelekee na asema kielezi cha wapandaji shamba waliomwua mrithi wa shamba hilo la mizabibu. Waelewa na kumwacha.
25 Kisha watuma baadhi ya Mafarisayo wamnase juu ya swali la ushuru. Akiitisha dinari, yeye auliza: “Ni ya nani sanamu hii na anwani hii?” Wao wajibu: “Ni ya Kaisari.” Kisha Yesu asema: “Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu.” Haishangazi wamstaajabia! (12:16, 17) Sasa Masadukayo, ambao hawaamini ufufuo, wajaribu kumnasa na swali hili: ‘Ikiwa mwanamke alikuwa na waume saba kwa mfululizo, yeye atakuwa mke wa nani katika kiyama?’ Yesu ajibu mara moja kwamba wale wanaoinuka kutoka kwa wafu watakuwa “kama malaika walioko mbinguni,” kwa maana hawatafunga ndoa. (12:19-23, 25) “Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” auliza mmoja wa waandishi. Yesu ajibu hivi: “Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana [Yehova, NW] Mungu wetu ni Bwana [Yehova, NW] mmoja; nawe mpende Bwana [Yehova, NW] Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho [nafsi, NW] yako yote, na kwa akili zako zote, na nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.” (12:28-31) Baada ya hilo, hakuna mtu anayethubutu kumwuliza. Mamlaka ya Yesu akiwa mwalimu mkamilifu yathibitishwa. Umati mkubwa huo wasikiliza kwa upendezi, na Yesu awaonya juu ya waandishi wenye maringo. Kisha kwa wanafunzi wake apongeza yule mjane maskini aliyetia zaidi katika kasha (sanduku) la hazina ya hekalu kuliko wengine wote, kwa maana sarafu zake mbili ndogo ndizo “vyote alivyokuwa navyo, ndiyo rikizi yake yote pia.”—12:44.
26. Ni ipi hotuba ndefu pekee iliyoandikwa na Marko, nayo yamalizika kwa onyo gani?
26 Akiwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni kuelekea hekalu, Yesu awaambia wanne wa wanafunzi wake faraghani juu ya “dalili” ya umalizio wa mambo hayo. (Hii ndiyo hotuba ndefu pekee iliyoandikwa na Marko, na yalingana na ile ya Mathayo sura za 24 na 25.) Yamalizia kwa onyo hili la Yesu la upole: “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba. Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.”—13:4, 32, 37.
27. Eleza matukio yanayoongoza kwenye kusalitiwa kwa Yesu katika Gethsemane.
27 Katika Bethania iliyo karibu mwanamke ampaka Yesu mafuta yenye manukato ya bei kubwa. Wengine wapinga ya kuwa huo ni ufujaji (uharibifu) huo, lakini Yesu asema ni tendo jema, matayarisho kwa ajili ya maziko yake. Kwenye wakati uliowekwa, Yesu na wale 12 wakusanyika katika jiji kwa ajili ya Kupitwa. Yeye atambulisha msaliti wake na kuanzisha chakula cha jioni cha ukumbusho pamoja na wanafunzi wake waaminifu, nao waondoka kwenda kwenye Mlima wa Mizeituni. Wakiwa njiani Yesu awaambia kwamba watakwazika. “Siyo mimi,” atamka Petro. Lakini Yesu amwambia hivi: “Usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.” Wafikapo mahali paitwapo Gethsemane, Yesu ajitenga akasali, akiwauliza wanafunzi wake walinde. Sala yake yafikishwa kwenye upeo kwa maneno haya: “Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” Mara tatu Yesu arejea kwa wanafunzi wake, na mara tatu awakuta wamelala, hata “wakati kama huu!” (14:29, 30, 36, 41, NW) Lakini saa imefika! Tazama!—msaliti huyu!
28. Ni nini hali za kukamatwa kwa Yesu na kutokezwa mbele ya kuhani wa juu?
28 Yuda akaribia na kumbusu Yesu. Hiyo ndiyo ishara kwa wanaume wenye silaha wa makuhani wakuu wamkamate. Wamleta kwenye mahakama ya kuhani wa juu, ambako wengi watoa ushahidi bandia juu yake, lakini ushuhuda wao haupatani. Yesu mwenyewe aendelea kuwa kimya. Hatimaye, kuhani wa juu amwuliza hivi: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?” Yesu ajibu, “Mimi ndiye.” Kuhani wa juu apaaza sauti, “Kufuru!” na wote wamlaani vikali kuwa apaswa kufa. (14:61-64) Katika ua ulio chini, Petro amemkana Yesu mara tatu. Jogoo awika mara ya pili, na Petro, akikumbuka maneno ya Yesu, ahuzunika na kulia machozi.
29. Ni maandishi gani anayofanya Marko ya kujaribiwa kwa Yesu kwa mwisho na kuuawa, na Ufalme waonyeshwaje kuwa ndilo suala?
29 Bila kukawia penye mapambazuko Sanhedrini yashauriana na kupeleka Yesu kwa Pilato akiwa amefungwa. Upesi atambua kwamba Yesu si mvunja sheria na ajaribu kumfungua. Hata hivyo, kwa usisitizo wa umati uliochochewa na makuhani wakuu, hatimaye awakabidhi Yesu akatundikwe. Yesu aletwa Golgotha (maana yake, “Fuvu la Kichwa”) na atundikwa, shtaka kumhusu likiwa limeandikwa juu: “MFALME WA WAYAHUDI.” Wapita njiani wamsuta hivi: “Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe!” Saa sita giza lafunika bara lote mpaka saa tisa. Kisha Yesu apaaza sauti kubwa, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” na kukata roho. Aonapo mambo hayo, ofisa mmoja wa jeshi atamka hivi: “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” Yusufu wa Arimathaya, mmoja wa Sanhedrini lakini mwamini katika Ufalme wa Mungu, aomba Pilato mwili wa Yesu na kuulaza ndani ya kaburi lililochongwa katika mwamba.—15:22, 26, 31, 34, 39.
30. Siku ya kwanza ya juma, ni nini chatukia penye kaburi?
30 Matukio ya baada ya kifo cha Yesu (16:1-8). Mapema sana siku ya kwanza ya juma, wanawake watatu waenda kwenye kaburi. Kwa mshangao wao wakuta kwamba lile jiwe kubwa kwenye mwingilio limebingirishwa. “Kijana” aliyeketi ndani awaambia kwamba Yesu ameinuliwa. (16:5) Hayumo humo tena lakini ametangulia mbele yao kuingia Galilaya. Wakimbia kutoka kaburi hilo, wakitetemeka na katika hofu.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
31. (a) Marko ashuhudiaje Yesu kuwa ndiye Mesiya? (b) Ni nini kinachothibitisha mamlaka ya Yesu kuwa Mwana wa Mungu, naye alikazia nini?
31 Kupitia picha hii ya maandishi iliyo wazi ya Yesu Kristo, wasomaji wote wa Marko, tangu nyakati za kale za Kikristo mpaka sasa, wameweza kutambulisha utimizo wa unabii mwingi mbalimbali wa Maandiko ya Kiebrania kuhusu Mesiya. Tangu nukuu la ufunguzi, “Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako,” mpaka maneno yenye maumivu makali ya Yesu akiwa juu ya mti, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” simulizi lote la huduma yake yenye bidii, kama lilivyoandikwa na Marko, lapatana na yale ambayo Maandiko ya Kiebrania yalitabiri. (Mk. 1:2; 15:34; Mal. 3:1; Zab. 22:1) Zaidi ya hayo, miujiza na matendo yake ya ajabu, fundisho lake lenye afya, makanusho yake yasiyo na dosari (kosa), utegemeo wake kamili juu ya Neno na roho ya Yehova, na uchungaji wake mwororo wa kondoo—yote hayo yamtia alama kuwa Yule aliyekuja na amri akiwa Mwana wa Mungu. Yeye alifunza “kama mtu mwenye amri,” amri iliyopokewa kutoka kwa Yehova, naye alikazia ‘kuhubiri habari njema ya Mungu,’ yaani, kwamba “ufalme wa Mungu umekaribia,” kuwa kazi yake ya msingi hapa duniani. Fundisho lake limetoa uthibitisho kuwa lenye mafaa isiyokadirika kwa wote ambao wamelifuata.—Mk. 1:22, 14, 15.
32. Marko atumia usemi “ufalme wa Mungu” mara ngapi, na zipi baadhi ya kanuni zenye kuongoza anazoweka wazi kwa ajili ya kupata uhai kupitia Ufalme?
32 Yesu aliwaambia hivi wanafunzi wake: “Ninyi mmejaliwa kuijua siri [takatifu, NW] ya ufalme wa Mungu.” Marko atumia usemi huu “ufalme wa Mungu” mara 14 na aandika kanuni nyingi zenye kuongoza kwa ajili ya wale ambao wangepata uhai kupitia Ufalme huo. Yesu alieleza hivi: “Mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili [habari njema, NW], huyu ataisalimisha.” Kila kizuizi cha kupata uhai lazima kiondolewe: “Afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako Jehanum [Gehena, NW].” Yesu aliendelea kujulisha rasmi hivi: “Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa,” na, “Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!” Alisema kwamba yeye anayefahamu kwamba kushika zile amri mbili kubwa kuna thamani zaidi ya sadaka nzima za kuchomwa na dhabihu ‘hayuko mbali na ufalme wa Mungu.’ Hayo na mafundisho mengine mengi ya Ufalme ya Gospeli ya Marko yana maonyo mengi mazuri ambayo twaweza kutumia katika maisha zetu za kila siku.—4:11; 8:35; 9:43-48; 10:13-15, 23-25; 12:28-34.
33. (a) Twaweza kupataje mafaa kutokana na Gospeli ya Marko? (b) Marko chapasa kututia moyo kuelekea mwendo gani, na kwa nini?
33 Habari njema “kulingana na Marko” labda yaweza kusomwa yote kwa saa moja au mbili, hilo likimpa msomaji pitio lenye kusisimua, la haraka, na lenye nguvu la huduma ya Yesu. Usomaji huo wa moja kwa moja wa simulizi hilo lililopuliziwa na Mungu, na pia funzo la karibu zaidi na utafakari wayo, sikuzote litakuwa jambo lenye mafaa. Gospeli ya Marko ni yenye mafaa kwa Wakristo wenye kunyanyaswa leo kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza, kwa maana Wakristo wa kweli wakabili sasa “nyakati za hatari [ngumu kushughulika nazo, NW]” na wahitaji uongozi huo uliopuliziwa na Mungu kama unavyopatikana katika maandishi haya kuhusiana na Kielelezo chetu, Yesu Kristo. Yasome, sisimuliwa na matendo yenye kutazamisha yaliyomo, na upate kitia-moyo ufuate hatua za Wakili Mkuu na Mkamilishaji wa imani yetu, Yesu, kwa shangwe ile ile isiyoshindika aliyooynyesha. (2 Tim. 3:1; Ebr. 12:2) Ndiyo, mwone kuwa mtu wa kitendo, ingiwa na bidii yake, na ufuate ukamilifu wake usio na kigeu-geu na wenye moyo mkubwa katikati ya jaribu na upinzani. Pata faraja kutokana na kisehemu hiki chenye utajiri cha Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu. Acha yakunufaishe katika mfuatio wako wa uhai wa milele!
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 2, ukurasa 337.