SILAHA, MAVAZI YA SILAHA
Silaha na mavazi ya silaha vinatajwa mara nyingi katika Biblia, lakini haitaji habari za kina kuhusu jinsi zilivyotengenezwa na jinsi zilivyotumiwa.
Ingawa Maandiko ya Kiebrania yanataja tena na tena kuhusu matumizi ya upanga, mkuki, ngao, na silaha nyingine, yanakazia mara nyingi umuhimu na faida za kumtegemea Yehova. (Mwa 15:1; Zb 76:1-3; 115:9-11; 119:114; 144:2) Uhakika wa kwamba Daudi alimtegemea Yehova unaonekana katika maneno aliyomwambia Goliathi: “Unakuja kupigana nami kwa upanga, mkuki, na fumo, lakini mimi naja kupigana nawe kwa jina la Yehova wa majeshi, Mungu wa vikosi vya Israeli, ambaye umemtukana. Siku hii ya leo Yehova atakutia wewe mikononi mwangu . . . Na watu wote waliokusanyika hapa watajua kwamba Yehova haokoi kwa upanga wala kwa mkuki, kwa sababu vita ni vya Yehova.” (1Sa 17:45-47) Kutegemea roho ya Yehova na si nguvu za kijeshi kunaonyeshwa kuwa jambo la msingi na lenye matokeo mazuri. (Zek 4:6) Yehova alipokuwa akimthibitishia upendo wake Sayuni, mke wake wa mfano, alimhakikishia hivi: “Hakuna silaha yoyote itakayotokezwa dhidi yako itakayofanikiwa, . . . Huu ndio urithi wa watumishi wa Yehova.”— Isa 54:17.
Neno la Kiebrania keliʹ linaweza kumaanisha “silaha,” lakini linaweza pia kurejelea “kitu,” “chombo,” au “kifaa.” (Amu 9:54; Law 13:49; Eze 4:9; Hes 35:16) Katika hali ya wingi linaweza kurejelea “silaha,” na pia “mizigo,” “vitu,” na “vifaa.” (1Sa 31:9; 10:22; Mwa 31:37; Hes 4:32) Neno lingine la Kiebrania kwa ajili ya “silaha” (neʹsheq) linatokana na na·shaqʹ mzizi wa maneno, unaomaanisha “kujihami; kuwa tayari.” (1Fa 10:25; 1Nya 12:2; 2Nya 17:18) Neno la Kigiriki hoʹplon (silaha) linahusiana na pa·no·pliʹa, linalomaanisha “silaha zote; mavazi kamili ya silaha.”—Yoh 18:3; Lu 11:22; Efe 6:11.
Silaha (za Vita). Upanga na kisu. Mara nyingi neno la Kiebrania cheʹrev hutajwa kuwa “upanga,” lakini linaweza pia kumaanisha ‘kisu,’ na “tindo.” (Mwa 3:24; 1Fa 18:28; Yos 5:2; Kut 20:25) Upanga unatajwa mara nyingi zaidi katika Maandiko ya Kiebrania kama silaha ya kupigana na ya kujilinda. Ulikuwa na mshikio na kichwa cha chuma, ambacho kingeweza kutengenezwa kwa chuma au shaba. Mapanga yalitumiwa kwa ajili ya kukata (1Sa 17:51; 1Fa 3:24, 25) na kuchoma. (1Sa 31:4) Baadhi ya mapanga yalikuwa mafupi, na mengine marefu, yakiwa na makali upande mmoja au pande zote mbili. Wavumbuzi wa vitu vya kale wanatofautisha mapanga na visu kwa kutegemea urefu wavyo, vikiwa na tofauti ya sentimita 40 hivi (inchi 16.).
Kwa kawaida, upanga ungening’inizwa upande wa kushoto kwenye mshipi (1Sa 25:13) na ulivaliwa ukiwa ndani ya ala, kifuko cha ngozi au kifuniko cha upanga au kisu. Kitabu cha Pili cha Samweli 20:8 kinaonyesha kwamba huenda Yoabu alilegeza kimakusudi upanga wake ili uanguke kutoka katika ala yake na hivyo kushika kwa urahisi silaha yake mkononi badala ya kuirudisha katika ala yake. Bila kushuku chochote, inaelekea Amasa alifikiri kwamba ulianguka kimakosa, na hakujali. Hilo lilisababisha kifo chake.
Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, neno la Kigiriki maʹkhai·ra linatumiwa kwa ukawaida kumaanisha upanga (Mt 26:47), ilhali neno rhom·phaiʹa, linatumiwa kumaanisha “upanga mrefu.” (Ufu 6:8) Kuwepo kwa mapanga mawili kati ya wanafunzi wa Yesu katika usiku ambao alisalitiwa hakukuwa jambo la kushangaza siku hizo (Lu 22:38), na kuna ushahidi kwamba kubeba silaha kulikuwa jambo la kawaida, hasa kwa Wagalilaya. (Ona The Jewish War, kilichotungwa na F. Josephus, III, 42 [iii, 2].) Maneno haya ya Yesu kwenye Luka 22:36, “yule asiye na upanga, auze vazi lake la nje anunue upanga,” hayakudokeza kwamba punde si punde wanafunzi wake wangeingia kwenye maisha hatari. Badala yake, alitaka wanafunzi wake wawe na upanga katika usiku huo ili kuonyesha waziwazi kwamba, ingawa wangejikuta katika hali ambazo zingechochea mapambano ya silaha, hakukusudia kuutegemea upanga badala yake angejisalimisha kwa hiari kupatana na mapenzi ya Mungu. Hivyo, Petro alipotenda kwa kujaribu kupambana kwa silaha na kulikata sikio la Malko, Yesu alimwamuru hivi: “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote wanaochukua upanga wataangamia kwa upanga.” (Mt 26:52; Yoh 18:10, 11) Ni wazi kwamba, upanga wa Petro na yale mapanga mengine waliyokuwa nayo yangewalinda kwa njia ndogo dhidi ya kundi hilo kubwa la wanaume wenye silaha, na kwa kujaribu kuyatumia, bila shaka ‘wangeangamia kwa upanga.’ (Mt 26:47) Zaidi ya hayo, jaribio la namna hiyo la kumuua Yesu lisingefanikiwa, kwani lingekuwa kinyume kabisa na kusudi la Yehova Mungu. (Mt 26:53, 54) Kama ilivyokuwa, baadaye siku hiyohiyo Yesu angeweza kumwambia hivi Pilato kwa uhuru: “Kama Ufalme wangu ungekuwa sehemu ya ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini, kama ilivyo, Ufalme wangu hautoki katika chanzo hiki.”—Yoh 18:36.
Mkuki na fumo. Silaha zilizotumiwa kwa ajili ya kuchoma au kurusha, zikiwa na mpini uliounganishwa na kichwa kilichochongoka. (1Sa 17:45; 18:11) Aina mbalimbali za mikuki na fumo zilitumiwa na mataifa yote ya kale. Haijulikani waziwazi kulikuwa na tofauti zipi hasa kati yazo, kama zinavyotambulishwa kwa maneno tofauti-tofauti ya Kiebrania.
Inaonekana, katika Maandiko ya Kiebrania mkuki (Kiebr., chanithʹ) ulikuwa mkubwa zaidi ya fumo, ukiwa na mpini mrefu wa mbao na kwa kawaida jiwe lililochongoka au kichwa cha chuma. Zikipangwa kulingana na umuhimu mkuki ulichukua nafasi ya pili kwa upanga. Yule jitu Goliathi alibeba mkuki uliokuwa na kichwa cha chuma kikiwa na uzito wa “shekeli 600” (kilogramu 6.8) na ulikuwa na mpini wa mbao “kama mti wa wafumaji wa nguo.” (1Sa 17:7) Baadhi ya mikuki ilikuwa na ncha ya chuma kwenye kitako ambayo ingewezesha kuchomeka mkuki ardhini. Hivyo, ncha hiyo, na si mkuki peke yake, ingeweza kutumiwa vizuri na shujaa. (2Sa 2:19-23) Kudungwa kwa mkuki ardhini kunaweza kuashiria makazi ya muda mfupi ya mfalme.—1Sa 26:7.
Katika maandiko ya Kigiriki ya Kikristo mkuki (Kgr., logʹkhe) unatajwa kwenye andiko la Yohana 19:34, linalosema kwamba baada ya Yesu Kristo kufa, “mwanajeshi mmoja [aliuchoma] ubavu wa Yesu kwa mkuki.” Kwa kuwa mwanajeshi huyo alikuwa Mroma, inaelekea fumo la Kiroma lilitumiwa. Silaha hiyo ilikuwa na urefu wa mita 1.8, ikiwa na kichwa cha chuma kilichorefushwa hadi nusu ya urefu wa mpini wa mbao.
Mkuki wenye ncha kali (Kiebr., roʹmach), silaha yenye mpini mrefu na ncha iliyochongoka, ilitumiwa kwa ajili ya kuchoma. (Hes 25:7, 8) Ilikuwa silaha ya kawaida ya Waebrania.
Fumo (Kiebr., ki·dhohnʹ) lilikuwa na ncha ya kichwa cha chuma na kwa kawaida lilirushwa. Inaonekana lilikuwa dogo na jepesi kuliko mkuki, na hilo lilifanya iwezekane kulishika kwa mkono ulionyooshwa. (Yos 8:18-26) Kwa kawaida fumo lilibebwa si na mkono bali mgongoni.
Ni wazi kwamba kishale (Kiebr., mas·saʽʹ) kilikuwa kombora mfupi lenye ncha linalofanana na mshale. (Ayu 41:26) Sheʹlach, neno la Kiebrania kwa ajili ya kombora, linatokana na mzizi wa kitenzi sha·lachʹ, kinachomaanisha “tuma; toa nje; futilia mbali.” (2Nya 23:10; Mwa 8:8, 9; Kut 9:15) Neno la Kiebrania ziq·qimʹ linadokeza “vishale vinavyowaka moto” na linahusiana na neno zi·qohthʹ, linalomaanisha “cheche.”—Met 26:18; Isa 50:11.
Neno la Kigiriki beʹlos (kombora) linatokana na mzizi balʹlo, unaomaanisha “tupa.” Mtume Paulo alitumia neno hilo la Kigiriki alipoandika kuhusu “makombora” ambayo mtu anaweza kuyazima kwa kutumia ngao kubwa ya imani. (Efe 6:16, maelezo ya chini) Kwa Waroma, vishale vilitengenezwa kwa matete, na kwenye sehemu ya chini, chini ya ncha, kulikuwa na chombo cha chuma ambacho kingeweza kujazwa mafuta mepesi yanayowaka. Hivyo, kishale kilirushwa kwa upinde uliolegea, kwa kuwa kukirusha kwa kutumia upinde uliokazwa kungetokeza moto. Kujaribu kuzima kombora kama hilo kwa maji kungeongeza tu moto, na njia pekee ya kulizima ilikuwa ni kwa kulifunika na udongo.
Upinde na mshale. Kuanzia nyakati za kale upinde (Kiebr., qeʹsheth; Kigr., toʹxon) ulitumiwa katika kuwinda na kwenye vita. (Mwa 21:20; 27:3; 48:22; Ufu 6:2) Ilikuwa ni silaha ya kawaida kwa Waisraeli (2Nya 26:14, 15), wale waliopigana kwa ajili ya Wamisri (Yer 46:8, 9), Waashuru (Isa 37:33), na Wamedi na Waajemi.—Yer 50:14; 51:11; pia ona MPIGA MISHALE.
Inaelekea mtajo “upinde wa shaba” ulieleweka kwamba unamaanisha upinde wa mbao uliofunikwa na shaba. (2Sa 22:35) Msemo ‘kupinda upinde’ (kihalisi, ‘kukanyaga upinde’) unarejelea kuukunja upinde. (Zb 7:12; 37:14; Yer 50:14, 29) Hilo lingeweza kufanyika kwa kuweka mguu kwa nguvu kwenye sehemu ya katikati ya upinde; au ukingo mmoja wa upinde wenye kamba ungeweza kushikiliwa ardhini kwa mguu wakati ule ukingo mwingine ukipindwa ili kupokea ukingo ulio huru wenye kamba.
Mishale (Kiebr., chits·tsimʹ) ilitengenezwa kwa matete au mbao nyepesi, kwa kawaida vitako vyayo vikiwa na manyoya. Mwanzoni, ncha za mishale zilitengenezwa kwa jiwe gumu lenye makali au mfupa na baadaye kwa chuma. Wakati mwingine mishale ilikuwa na ncha kali, ilichovywa kwenye sumu (Ayu 6:4), au iliwekewa vitu vinavyoweza kuwaka moto. (Zb 7:13) Ilipohusu mshale unawaka moto, kitani kilichochovywa kwenye mafuta kiliwekwa kwenye mashimo kuzunguka kingo za kichwa cha chuma cha mshale huo, ili kitani kishike moto mshale ulipotumiwa.
Kwa kawaida, mishale thelathini iliwekwa kwenye kifuko cha ngozi au podo. Picha zilizochorwa na Waashuru zinaonyesha kwamba podo iliyobebwa kwenye gari la kivita ilichukua mishale 50.—Linganisha Isa 22:6.
Kombeo. Tokea nyakati za kale, kombeo (Kiebr., qeʹlaʽ) limekuwa silaha ya wachungaji (1Sa 17:40) na mashujaa wa vita. (2Nya 26:14) Ilikuwa ngozi laini au mkanda uliosokotwa kwa vitu kama vile kano za wanyama, matete, au manyoya ya wanyama. Sehemu pana ya katikati, yaani “tundu la kombeo,” ilitumika kuwekea kitu kilichopaswa kurushwa. (1Sa 25:29 NW) Mwisho mmoja wa kombeo ungeweza kufungwa mkononi au kwenye kitanga cha mkono, na mwisho wa pili ulishikwa na ili uachiliwe kombeo lilipozungushwa. Kombeo lenye kitu cha kurushwa lilizungushwa juu ya kichwa, huenda mara kadhaa, halafu mwisho mmoja uliachiliwa kwa ghafla, likitupa kombora mbele kwa nguvu na kasi kubwa. Mawe laini na ya mviringo yatumiwa zaidi kwa ajili ya kurushwa kwa kombeo. Ingawa hivyo, vitu vingine pia vilitumiwa kwa ajili ya kurushwa. (1Sa 17:40) Wanajeshi waliorusha mawe kwa kombeo walikuwa sehemu ya kawaida ya jeshi la Yuda (2Nya 26:14) na Israeli.—2Fa 3:25.
Rungu la vita na shoka la vita. Ni wazi kwamba “rungu la vita” lilikuwa rungu zito au rungu lenye vyuma vinavyochomoza, wakati mwingine likifunikwa kwa chuma. (Met 25:18; Eze 39:9) Shoka la vita lilikuwa silaha yenye mshikio wa mbao au wa chuma na kichwa cha jiwe au chuma kikiwa na wembe mkali. Zaburi 35:3 inataja tamathali ya semi kuhusiana na shoka la vita wakati Daudi alipomwomba Yehova ‘ainue mkuki wake na shoka lake la vita dhidi ya wale waliomfuatia.’
Mavazi ya Silaha (ya Kujilinda). Ili kuulinda mwili wake kutokana na silaha zenye kudhuru za adui, mwanajeshi alivalia aina kadhaa za ngao na mavazi ya silaha ya kujilinda.
Ngao. Kipande kipana cha mavazi ya silaha ya kujilinda yaliyotumiwa na mataifa yote ya kale. Ilikuwa na mshikio kwa ndani na ilibebwa na shujaa wa vita wakati wa pigano, hasa kwenye mkono wa kushoto, ingawa wakati wa mazoezi huenda ilining’inizwa kwenye mkanda wa begani. Andiko la Isaya 22:6 linadokeza kwamba pengine baadhi ya ngao zilikuwa na mifuniko ambayo iliondolewa wakati wa pigano. Mara nyingi, wakati wa amani ngao ziliwekwa ghalani.—Wim 4:4.
Kwa kawaida, ngao zilizotumiwa nyakati za kale zilitengenezwa kwa mbao na kufunikwa kwa ngozi, na ngao kama hizo zingeweza kuchomwa moto. (Eze 39:9) Ingawa ngao za mbao na za ngozi zilitumiwa kwa ukawaida, inaonekana kwamba ngao za chuma hazikutumiwa sana, zilitumiwa hasa na viongozi, walinzi wa mfalme, au labda kwa ajili ya matumizi ya kisherehe. (2Sa 8:7; 1Fa 14:27, 28) Ngao ziliwekwa mafuta ili kuzifanya ziwe sawa na zisiharibiwe na unyevu, kutunza chuma kisipate kutu, au kuzifanya ziwe laini na nyororo. (2Sa 1:21) Kwa kawaida, ngao ya ngozi ilipambwa kwa chuma kigumu sehemu ya katikati (kirungu au stud), ambacho kiliongeza ulinzi zaidi.—Ayu 15:26.
“Ngao kubwa” (Kiebr., tsin·nahʹ) zilibebwa na wanajeshi wenye nguvu waliojihami kwa silaha (2Nya 14:8) na wakati mwingine na mbeba silaha. (1Sa 17:7, 41) Zilikuwa ama za duara au za mstatili kama mlango. Kwa kufaa, “ngao kubwa” sawa na hizo zimetajwa katika Waefeso 6:16 kwa kutumia neno la Kigiriki thy·re·osʹ (linalotokana na thyʹra, linalomaanisha “mlango”). Tsin·nahʹ ilikuwa na ukubwa unaoweza kufunika mwili wote. (Zb 5:12) Pindi fulani ilitumiwa kutengeneza mistari ya mbele ya vita iliyo imara huku fumo zikizochomoza. Pindi fulani ngao kubwa inatajwa pamoja na fumo na mkuki kama njia ya kurejelea silaha za vita kwa ujumla.—1Nya 12:8, 34; 2Nya 11:12.
“Ngao” au “ngao ndogo” (Kiebr., ma·ghenʹ) ilibebwa na wapiga mishale na kwa kawaida inahusianishwa na silaha nyepesi kama vile upinde. Kwa mfano, ilibebwa na wapiga upinde Wabenjamini wa kikosi cha jeshi la Mfalme Asa wa Yuda. (2Nya 14:8) Kwa kawaida ngao ndogo zilikuwa za mviringo na zilitumiwa zaidi kuliko ngao kubwa, na huenda zilitumiwa hasa katika mapigano ya uso kwa uso. Ukweli wa kwamba tsin·nahʹ na ma·ghenʹ za Kiebrania zilitofautiana hasa kwa ukubwa unaonekana katika ngao za dhahabu ambazo Sulemani alitengeneza, ngao kubwa ikitumia kiasi cha dhahabu mara nne ya ngao ndogo. (1Fa 10:16, 17; 2Nya 9:15, 16) Inaonekana ma·ghenʹ, kama tu tsin·nahʹ, ilitumiwa kama sehemu ya kawaida ya silaha za vita.—2Nya 14:8; 17:17; 32:5.
Neno la Kiebrania sheʹlet, linalotafsiriwa kuwa ‘ngao za mviringo’ linaonekana mara saba katika Maandiko ya Kiebrania na ni wazi kwamba linafanana na neno linalijulikana zaidi ma·ghenʹ (ngao), kwa kuwa linatumiwa pamoja na ma·ghenʹ katika kitabu cha Wimbo wa Sulemani 4:4.
Kofia ya chuma. Kofia ya mwanajeshi iliyotengenezwa ili kumlinda mpiganaji wakati wa pigano na ni sehemu ya msingi sana ya mavazi ya silaha za kujilinda. Neno la Kiebrania kwa ajili ya “kofia ya chuma” ni koh·vaʽʹ (au qoh·vaʽʹ), wakati neno la Kigiriki ni pe·ri·ke·pha·laiʹa, kihalisi linamaanisha “kuzunguka kichwa.”—1Sa 17:5, 38; Efe 6:17.
Mwanzoni, inaelekea kofia za wanajeshi Waisraeli zilitengenezwa kwa ngozi. Baadaye kofia hizo zilifunikwa kwa shaba au chuma na zilivaliwa juu ya kofia za sufu, kitambaa kigumu, au ngozi. Kofia za shaba zilitumiwa katika Israeli mapema tangu siku za Mfalme Sauli. (1Sa 17:38) Ingawa mwanzoni kofia hizo zilitumiwa na wafalme na viongozi wengine peke yao, baadaye zilitumiwa kwa ukawaida, Mfalme Uzia akilihami jeshi lake lote kwa kofia hizo.—2Nya 26:14.
Wafilisti walimiliki kofia za chuma; Goliathi alivaa kofia ya shaba. (1Sa 17:5) Ezekieli alitaja kofia hizo alipozungumza kuhusu Waajemi, Waethiopia, na wengine.—Eze 27:10; 38:5.
Koti la vita. Koti lililovaliwa kwa ajili ya kujilinda wakati wa vita. Koti la vita (Kiebr., shir·yohnʹ au shir·yanʹ) lilitia ndani joho la kitambaa au ngozi ambalo lilikuwa na mamia ya vipande vidogo vya chuma (pengine kama magamba ya samaki) vilivyoshikiliwa juu yake. Kwa kawaida lilifunika kifua, mgongo na mabega, ingawa wakati mwingine lilifika magotini au hata miguuni.—1Sa 17:5.
Mara nyingi, koti la vita la Waebrania lilitengenezwa kwa ngozi iliyofunikwa kwa magamba au vipande vidogo vya chuma. Mvaaji alifurahia kiasi fulani cha ulinzi, ingawa, hata hivyo, kuna sehemu zingemweka hatarini hasa sehemu ambazo vipande vya chuma viliunganishwa au pale koti hilo lilipoungana na sehemu nyingine za mavazi ya silaha. Hivyo, Mfalme Ahabu alijeruhiwa vibaya na mpiga upinde ambaye “[alimpiga] mfalme wa Israeli katikati ya sehemu ambazo koti lake la vita linaungana.”—1Fa 22:34-37.
Mshipi. Mshipi wa kijeshi wa nyakati za kale ulikuwa mkanda wa ngozi uliovaliwa kiunoni au kuzunguka nyonga. Ilitofautiana katika upana kuanzia sentimita 5 hadi 15 na kwa kawaida ilifunikwa kwa vipande vya chuma, fedha au dhahabu. Upanga wa shujaa ulining’inizwa katika mshipi, na wakati mwingine mkanda huo ulisaidiwa na ukanda uliopita mabegani. (1Sa 18:4; 2Sa 20:8) Ingawa mshipi uliolegezwa ulimaanisha starehe (1Fa 20:11), kukaza mshipi kiunoni au kwenye nyonga kuliashiria utayari kwa ajili ya kuchukua hatua au kwa ajili ya pigano.—Kut 12:11; 1Fa 18:46; 1Pe 1:13.
Mabamba ya miguuni. Mavazi ya silaha yaliyotia ndani vipande vyembamba vya chuma, vilivyofunika miguu kati ya kifundo cha mguu na goti. Mahali pekee yanapotajwa katika Biblia ni kwenye 1 Samweli 17:6, ambapo inaonyeshwa kwamba jitu Mfilisti Goliathi kutoka Gathi alikuwa na “mabamba ya shaba yaliyokinga miguu yake [Kiebr., mits·chathʹ] .” Huenda Waisraeli pia walitumia mabamba ya miguuni kwa kiasi fulani.
Mavazi ya Silaha ya Kiroho. Ingawa Wakristo wa kweli hawashiriki katika vita vya kimwili, wanashiriki katika pigano na wanafananishwa na wanajeshi. (Flp 2:25; 2Ti 2:3; Flm 2) Mkristo anapambana “dhidi ya serikali [zisiyofanyizwa na wanadamu wenye mwili wa nyama], dhidi ya mamlaka, dhidi ya watawala wa ulimwengu wa giza hili, dhidi ya majeshi ya roho waovu katika mahali pa kimbingu.” (Efe 6:12) Kwa kuwa silaha na mavazi ya silaha halisi hayangekuwa na thamani yoyote katika pigano dhidi ya viumbe wa roho wenye nguvu kuliko wanadamu, ni lazima Wakristo wachukue “mavazi kamili ya silaha kutoka kwa Mungu.”—Efe 6:13.
Mtume Paulo aliwashauri Wakristo ‘wajifunge kiunoni mshipi wa ile kweli.’ (Efe 6:14) Kama tu mshipi unavyoweza kutoa msaada na ulinzi kwa ajili ya kiuno, kushikamana kikiki na kweli za Mungu kunaweza kumwimarisha Mkristo katika azimio lake la kubaki imara licha ya majaribu.
Kisha, ni lazima Mkristo avae “bamba la kifuani la uadilifu.” (Efe 6:14) Bamba halisi la kifuani lilitumiwa kulinda viungo muhimu sana, hasa moyo. Ni muhimu sana kuwa na uadilifu kama bamba la kifuani linalotoa ulinzi kwa ajili ya moyo wetu wa mfano, kwa sababu moyo una mwelekeo wa kufanya dhambi.—Mwa 8:21; Yer 17:9.
Sehemu ya mavazi ya silaha ya kiroho ni “[kuvaa] viatu miguuni tayari kutangaza habari njema ya amani.” (Efe 6:15) Neno la Kigiriki he·toi·ma·siʹa, linalotafsiriwa kuwa “equipment,” has the basic meaning “readiness.” (See Int; NIV; TEV.) Sikuzote Mkristo anapaswa kuwa tayari kutangaza “habari njema” kwa wengine, na kufanya hivyo licha ya matatizo, kunaweza kumsaidia kuvumilia kwa uaminifu.
Sehemu yenye kutokeza ya mavazi ya silaha ya kiroho ni “ngao kubwa ya imani.” Kama ngao kubwa inayofunika karibu mwili wote, imani katika Yehova Mungu na katika uwezo wake wa kutimiza ahadi zake itamsaidia Mkristo “[kuizima] mishale yote inayowaka moto ya yule mwovu.” (Efe 6:16; linganisha Zb 91:4.) Imani itamsaidia Mkristo kushinda mashambulizi ya roho waovu, kupinga vishawishi vya ukosefu wa maadili, kuepuka kutamani vitu vya kimwili, na kutoshindwa na woga, shaka, au huzuni iliyopita kiasi.—Mwa 39:7-12; Ebr 11:15; 13:6; Yak 1:6; 1Th 4:13.
Kama vile kofia inavyolinda kichwa cha mwanajeshi, ndivyo na “kofia ya chuma ya wokovu” inavyolinda nguvu za akili za Mkristo kutokana na uvutano wa ulimwengu. (Efe 6:17) Kuvaa “tumaini la wokovu kama kofia ya chuma” kunamaanisha ‘kukaza macho kwenye malipo ya thawabu’ kama Musa alivyofanya.— 1Th 5:8; Ebr 11:26.
“Upanga wa roho, yaani, neno la Mungu” ni wa muhimu kwa Mkristo ili kukata mafundisho ya uongo na desturi za wanadamu na katika kufundisha kweli na “kuzipindua ngome zenye nguvu.”—Efe 6:17; 2Ko 10:4, 5.
[Picha katika ukurasa wa 171]
Mwanajeshi Mroma akiwa na ngao